Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 10, 2015

RADHI YA WAZAZI-17

  

Huyu mume mtu, alifika nyumbani baada ya kutoka benki ,nia mojawapo ni kuangalia jinsi gani ataweza kuongezea kiasi alichotakiwa na wanaodai mlungula,(blackmailer) lakini pia kutafuta muda zaidi kama anaweza kuwakwepa, au kujadiliana nao,hata hivyo,hayo hayakuwezekana.

Na mbaya zaidi alikutana na mtu asiyemtarajia kabisa,...haa,kweli siku ya kufa nyani miti yote huteleza,..kwani alishaharibu mambo, lakini hata hivyo hana ujanja,kwani hao watu wa mlungula wameshamkalia kubaya, hawezi kufurukuta, huku nako ....

Tuendelee na kisa chetu

Mume mtu alipigwa na bumbuwazi, akabakia mdomo wazi, hakuratajia kabisa kukutana na huyu mtu ,na sio kawaida yake, yeye kuna muda aarudi nyumbani kwa dharura hii na ile kwa vile yeye anafanyia karibu na nyumbani, sasa alipomuona huyo mtu akajua kuna jambo ...akabakia akijiuliza, na kuweka fikira za labda,labda...ni sekunde chache za kuangaliana, hata hivyo,mwenzake, hakuonyesha kushangaa, na ndilo lilimfaya mume mtu kupata ahueni

‘Oh,vipi mume wangu, mbona upo nyumbani...’akauliza mkewe mtu huku akimpita mumewe kuingia ndani.

‘Nilikuja mara moja, kuna yaraka nilizifuatilia, jana kuna kazi nilifanyia nyumbani nikasahau kuchukua hizi kumbukumbu...’akasema huku akionyesha mkoba aliokuwa nao.

‘Mhh, sikukuona ukifanya kazi yoyote jana, Oh,....hata hivyo hata mimi kuna kitu nimesahau.. nina haraka kweli, niwahi kurudi ...’akasema mkewe mtu akimpita mumewe na kukimbilia ndani, ni kweli kuna kitu alikisahau na alihitajika kazini kwa haraka na hizi kumbukumbu za kazi aliyokuwa ameifanya jana usiku.

Mumemtu,akahisi labda mkewe kaja kuzichukua hizo pesa akazitume, hapo akasimama akitaka kurudi, lakini akilini akakumbuka vitisho vya hao watu....akaomba mkewe asije tu kuligundua hilo mapema.

Mumemtu kwanza akavuta subira, lakini moyoni pia, aliona kuwa mkewe ana haraka na uharaka ule, hautamfanya kuhesabu pesa, kama ni kuchukua pesa atazichukua na kuondoka, na akigundua atakuwa keshazirejesha zile pesa alizochukua na muda huo hatakosa uwogo wa kusema

Yeye,kwa haraka akatoka akapiga tambona kuelekea kwenye gari lake,...akaanzisha gari lake, na kwa haraka akaendesha kutoke eneo la nyumba, kuelekea sehemu aliyoahidiwa kuupeleka huo mzigo,...ilikuwa ni kule kule kwa yule mlinzi,yule mlinzi anaaminika kihivyo,na wengi wanamuamini, ...hakipotei kitu.

Hakusimama hadi alipofika kwenye hiyo hoteli, ambapo huyo mlinzi yupo na ofisi yake ya dharura kama hizo, akaingia, na kuelekea sehemu aliyoagizwa,akafika kwa huyo mlinzi, na kumsogelea huyo mlinzi.

‘Nina mzigo wangu wa haraka unatakiwa ufike kwa huyu mtu.....’akasema.

‘Atakuja mwenyewe au unapelekwa kwake,mbona hakuna anuani ya huyo mtu...?’ akauliza.

‘Atakuja mwenyewe...’akasema.

‘Unavyofanya hivi ni hatari, je kama mzigo huu usipofika kwa mlengwa mtakuja kunilaumu, ...halafu nikuulize kuna kitu gani ndani..?’ akauliza

‘Kwani unahitajika kufahamu ni kitu gani kipo ndani...?’ akauliza

‘Poa, haya nipe utambulisho wake...na gharama zangu?’ akauliza

Bwana mzee,akatoa kikaratasi na kumpa huyo mlinzi ,kulikuwa na maneno ya siri, ambayo mlinzi ataambiwa kabla ya kukabidhi huo mzigo na akatoa ushuru aliotajiwa..

‘Sawa, lakini tusilaumiane,....muhimu kwenye hii bahasha ni lazima kuwe na anuani ya mpokeaji, ili akija na kitambulisho inakuwa rahisi kumtambua..haya mzigo umefika,...’akasema na mumemtu huyu akabakia kaduwaa,alitaka kuongea na huyo mlinzi, hakuwa na uhakika jinsi gai huo mzigo utafika kwamlengwa, lakini wenyewe wamedai afanye hivyo, na asiwe na wasiwasi kwa hilo

Na wakati bado kaduwaa yule mlinzi akawa anaendelea na kupokea mizigo ya watu wengine, lakini akawa anasita, na kabla hajatulia vyema simu yake ya mkononi ikaita
Akapokea kwa haraka, na kabla hajasema neno akasikia sauti ile inaomnyimaraha ikisema;

‘Unaweza kuondoka,  mzigo umeshafika...’akaambiwa,hapo akageuka huku na kule kama anaweza kumuona huyo mtu, kwanza akamtilia mashaka huyo mlinzi, mlinzi alikuwa haongei ni simu, alikuwa akiwa anaongea na watu wanaompa mizigo yao

Akageuka huku na kule kama ataona mtu atakayemtilia mashaka, akiwa kashikilia simu,..lakini walikuwa watu wengi, wanaingia na kutoka, na wengine wanafika kwa huyo mlinzi na mizigo yao.

‘Umesikia ondoka eneo hilo,...toka kabisa hadi kwenye gari lako..sisi tunakuona, uavyoshangaa hapo...na usizime simu yakohadi tutakapokuambia, ’akaambiwa.

Hapo akawa hana ujanja, akatoka nje, huku simu ipo sikioni, alipofika kwenye gari lake akaambiwa.

‘Sasa rudi nyumbani kwako,...’akaambiwa

‘Na-na enda kazini...’akasema

‘Fuata tunavyokuambia....’akaambiwa, na hapo akaendesha gari kuelekea nyumbani kwake, a kabla hajafika akaambiwa;
,
‘Simamisha gari...’akasimamisha gari, na kutulia, ikisubiria amri nyingine, ikapita nusu saa hasiki kitu, akaitoa simu sikioni, kuoa kama simu ipo hewani, akakuta mpigaji hayupo hewani

Akatulia kwanza,kwani hajaambiwa afanye nini,...na mara simu yake ikaita akijua ni hao watu akaweka sikioni, alikuwamfanyakazi mwenzake akimuarifu kuwa aje kazini,anahitajika.

Kuona hivyo,akageuza gari lake na kuingia barabara ya kurudi kuelekea kazini, huku akisubiria kama hao watu watampigia simu tena kuwa kakiuka maagizo yao kuwa arudi nyumbani.

*********

Huku nyuma mkewe akaingia ndani,akachukua kitu alichokifuata, hakuwa na wasiwasi,akili yake ilikuwa kazi aliyokuwa anaihitajia, kwahiyo alipoiona, hakupoteza muda, akageuka kutoka, akijua atamkuta mumewe nje, ..

Ni wakati anatoka ndipo ndipo, akaona kitu, macho hayana pazia,akahisi mumewe kadondosha nyaraka za ofisini, akainama na kuikota,ili  amkimbilie mumewe nje labda ni nyaraka muhimu,..., lakini alipotoka nje hakumkuta mumewe ,kwani alishaondoka.

‘Mhh,sijui ni kitu gani hiki, labda wala sio kitu muhimu kwake....’akasema akikagua ile karatasi, ili kuwa karatasi nyepesi tu

‘Kama ni ya muhimu,nitampitishia kazini kwake...’akasema akiikunjua vyema,akagundua kuwa ni bank slip, ya kutolea pesa...

‘Mhh,mumewangu naye, kadondosha hii bank slip,huenda ni ya kazini,hajui kuwa ataulizwa...’akasema sasa akikagua maandishi yake.

Kwa haraka akaangalia kiwango cha pesa

‘Mhh, pesa yote hii,...itakuwa ni ya kazini kwake...’akasema, huku akiendelea kukagua, cha ajabu anaona jina la mtoaji,ni mumewe, jina la mwenye dhamana,ni mumewe....hapo akashituka

‘Inakuwaje kazini kwake,watumie jina la mumewe,...haiwezekani, au ndio kama alivyosema kuwa akaunti yake ilikuwa inatumika kuweka pesa za kazini, lakini hapana, sio kwa kiasi hiki, ....akaona sasa kuna kitu, akikumbuka jinsi alivyomuona mume wake wakati anaingia...Huwa anamfahamu mume wake,akiwa na wasiwasi,akiwa na huzuni,....ile hali aliyomkuta nayo,ilionyesha waziwazi mume wake alikua na wasiwasi, kama mtu aliyefumaniwa

‘Hapa kuna jambo...’akasema akizidi kuikagua ile nyaraka ya bank (bank slip), na kwa vile alikuwa na haraka, akaona akimbilie kazini,hayo mengine atayashughulikia badaye,akaondoka na ile nyaraka hadi kazini kwake.

Huyu mke mtu ofisi yake na kazi anazofanya zinafanana na za benki, ni kamuni inayojishughulisha na kutoa mikopo na dhamana mbali mbali mbali,na kwahiyo  mara kwa mara wanakuwa wakiwasiliana na watu wa benki  kupata uhakiki wa watu wanaotaka kukopa kwao,...,

Kampuni hii pia wakitaka taarifa fulani kwa waajiri ili kuhakiki baadhi ya mambo, huwa wanauliza waajiri hasa pale mkopaji anapoaisnisha kuwa muajiri wake ndiye  mdhamini wake,....na kwa vile wanaaminiana, huwa wanapewa taarifa hizo bila kufichwa.

Basi mkemtu huyu alipofika kazini na kuhakikisha kuwa keshamaliza kazi zake alizohitajiwa nazo, na kuzikabidhi kwa bosi wake, akarudi mezani kwake,na kuichukua ile nyaraka ya bank,( bank slip),  akatafuta namba ya mtu kwenye ile bank na ikawa vizuri kuwa huyo aliyemtafuta wameshawahi kuwasiliana naye mara kwa mara, akampigia;,
‘Tafadhali,kuna mtu kaleta hundi ya malipo hapa...nataka kuhakiki tu,kama ana pesa za kutosha...’akauliza akijitambulisha yeye ni nani

‘Mbona hujafuata utaratibu...kama kawaida yakompendwa...’akasema huyo mtu wa bank.

‘Ni malipo ya haraka, na kama unavyojua, hundi hii ikipita mnaweza mkapata hasara na ni hundi ya benki yenu,..’akasema

‘Unaweza kunitajia ni nani...?’ akauliza na mke mtu akamtajia akaunti namba,na jina la mwenye akaunti, na hapo akaambiwa asubiri, baadaye akaambiwa

‘Huyu mtu akaunti yake ina matatizo kuna nyaraka tunasubiria, ila kama ni malipo yanaweza kuingizwa tu,je hiyo hundi ni kiasi gani?’ akauliza na mkemtu akijua nini anachokifanya, akataja kiwango kikubwa zaidi

‘Mhh, haiwezi kupita hiyo hundi, yeye ana salio dogo,ni dola ....’akataja kiasi

‘Lakini kama maandishi hapa,alikuwa na dola za kutosha....’akasema lakini hakutaja kiasi

 ‘Ni kweli alikuwa na kiwango, cha kutosha, kabla hajachukua pesa leo,katoka kutoa pesa kiasi,...na kupunguza salio lake, inabidi tusubirie mwisho wa mwezi huu,sio mbali, akiweka pesa nyingine, huenda ikafikia hicho kiasi...’akasema

‘Je akiweka kiwango hicho anachoweka kitatosha...?’ akauliza huyo mke

‘Ndio kitatosha maana kila mwezi anaweka dola kama..eeh,...’akataja kiwango

‘Na pia kilamwezi kuna pesa kutoka kazini kwake, mshahara wake unapitia kwenye hii akaunti yake, na ukiingia huwa anakuja kuchukua nusu ya mshahara kila mwezi,...pesa tasilimu...’akasema na maelezo hayo yalimtosha mke mtu kujua ukweli alioutaka,

‘Mhh, huyu mwanamume ananizunguka, kumbe ana akaunti yake binafsi,na pesa anazodai kila mwezi kumbe anakuja kuzihifadhi kwenye hii akaunti, na mshahara wake kumbe mkubwa mara mbili ya huo anaoufahamu yeye,...na zaidi, ..hizi pesa nyingi alizotoa anapeleka wapi...’akawa anajiuliza, huku akiwa kashikilia ile karatasi ya kutolea pesa, hakuna maelezo kuwa anamlipa mtu.

‘Kwanza inabidi niongee naye kabla sijawasiliana na wazazi wangu,najua nikiongea na wazazi wangu watakimbilia kubaya,...nilishawaambia wazazi wangu mume huyu waniachie mwenyewe, japo walishasema sio mwaminifu...’akawa anaongea peke

‘Kwanza hizi simu za usiku zilikuwa za nini...?’ akawa anajiuliza kwani kuna muda usiku alisikia simu ya mezani na mumewe akatoka na kwenda kuongelea varandani, na akarudi na baadaye simu ikapigwa tena...akatoka, na alitoka karibu mara nne...

Usiku ule alipoona simu zimezidi kwa mume akashindwa kuvumilia, akainuka kitandani na kumfuatilia nyuma.., na ndipo akasikia mume akisema

‘Kwahiyo mnataka nini..?’ akauliza

‘Nilishawaambia pesa ni nyingi sana, ni mpaka niende benki....’akasema na akageuka na kuona mkewe akiwa kasimama mlangoni, akajibaragua na kusema

‘Sawa lakini sio kosa langu ni tatizo la umeme, nikienda benki nitawalipa....’akasema
Kwa vile mkewe anafahamu kuwa mumewe ni fundi wa umeme,akajua ni maswala ya kikazi, huenda kuna tatizo la umeme mahali,na huwa inatokea,..basi akapitiliza, na kujifanya anakwenda jikoni, baadaye akarudi, na kumkuta mumewe amelala

Sasa leo akiunganisha haya matukio,...akahisi kuna jambo..huenda linatokana na ile simu,huenda,kuna jambo mume wake hataki yeye kulifahamu, na kiwango cha pesa kwenye hiyo akaunti yake kikamtia mashaka,

*********

‘Sasa nifanyeje..ili niweze kuupata ukweli wote....’akawa anajiuliza,

‘Kwanza ni kuhakikisha mwenendo mzima wa hiyo akaunti...’akasema na kumigia tena huyo jamaa aliyempigia mwanzoni, alijua cha kusema, na taarifa aliyoipata ikwamka uhakika kuwa akaunti hiyo kweli ni ya mume wake,na pesa zilizopo sio kweli kuwa ni za kazini,ni pesa mume wake, alikwua akiweka.

‘Akaunti hii imekuwa ya kuweka tu, ...kila mwezi anaeka pesa bila kuhukua kitu, hadi alipotaka kutoa karibu pesa yote, lakini kutokana na kutokukamilisha baadhi ya nyaraka, ikabidi apewe pesa kidogo tu....’akaambiwa

‘Pesa kidogo...! ‘akasema na alipokumbuka kuwa anachohitaji ni kutaka uhakiki, sio kuelezea, hisia zake, akasema

‘Basi nashukuru sana, hiyo itanisaidia kuona kama kweli anastahiki kupewa huo mkopo alioomba.....’akasema na kukata simu, huku akitizama ile nyaraka ya benki ya kutoa pesa, akijiuliza wapi pesa hiyo mume waka kaipeleka, na mara akakumbuka kitu, akainua simu na kuongea na mtu anayemfahamu;

‘Habari yako mhasibu...mimi ni mfanyakazi wa benki binafsi ya kukopesha, nilikuwa nataka kupata taarifa za mmoja wa wafanyakazi wenu aliyekuja kutaka mkopo hapa kwetu, naomba msaada wako tafadhali na iwe ni siri....’akasema

‘Hamna shida , nitakusaidia tu, naweza kujua jina la huyo mfanyakazi....?’ akauliza na akataja jina la mume wake

‘Mhh, hatuna barua yoyote ya huyo mfanyakazi ya kutaka uthibitisho, au kudhaminiwa na kampuni kwa ajili ya kuchukua mkopo kwenye kampuni yenu..labda ni mkopo binafsi tu.’akasema

‘Nilitaka kujua kama kampuni inamdai, ..au ana deni lolote ili tuweze kutathimini kiasi alichotaka kukopa, kwani hapa kaelezea kuwa anahitaji pesa kwa ajili ya kulipia deni analodaiwa na kampuni...’akasema

‘Deni, .....Mhh, kwakweli sijui, ..huyu mtu hana deni lolote kwetu, huenda ana maana yake, unaonaje ukiwapigia simu utawala...’akasema

‘Unauhakika hajaandikiwa deni kwa sababu ya uharibifu wa vifaa vya kazi kutokana na uzembe alioufanya yeye, na kusababisha uharibifu mkubwa ...kutokana na  umeme...?’ akauliza.

‘Kutokana na umeme,....mmh, sijui..lakini hapa kwetu hana deni kabisa ....hajawahi kukopa au kuandikiwa deni, na kampuni haiwezi kumuandikia mtu deni kwasababu ya uharibifu wa kikazi. Mhh mimi hapo sielewi...’akasema huyo mhasibu

‘Na huo uharibifu ulitokea lini, haijawahi kutokea tatizo lolote la umeme,...na sijawahi kuona kitu kama hicho, hata hivyo huyu mfanyakazi ni mtaalamu sana wa umeme, hawezi kufanya uzembe wa kusababisha hasara, ndio maana nakushauri uongee na utawala....’akasema mhasibu

‘Pia kwenye barua hpa naona kaainisha kuwa alikuwa anapokea pesa za kampuni kwa niaba, na kuziweka kwa jina lake, na wakati anakuja kuziweka benki akaibiwa pesa nyingi tu, ina maana nyie mna utaratibu wa wafanyakazi kupokea pesa na kuweka kwenye akaunti zao binafsi...?’ akauliza

‘Haijawahi kutokea, hakuna kitu kama hicho, pesa ya kampuni inapitia moja kwa moja kwenye akaunti za kampuni, na malipo yote yapitia idara ya uhasibu, mtu kama huyu hana mamlaka ya kupokea pesa ya kampuni...labda kasema hivyo kwa minajili ya kupata mkopo, lakini kampuni haijawahi kupokea pesa kupitia kwa mtu, hususani yeye....’akasema

‘Basi hamna shida, ...kama ni lazima nitaongea na utawala, nimekuuliza tu kupata uhakika, sio kwamba hatutaki kumpa mkopo, nashukuru kwa msaada wako...’akasema na kukata simu.

Mke mtu huyu akawa haamini, ina maana mume wake amefiki hatua ya kumdanganya kiasi hicho, akasimama, ....akakaa...akaangalia muda ,muda wa kutoka kazini bado.

‘Mume wangu ananidanganya, ...kwa hili, sizani kama nitavumilia, ina maana ni kweli...walivyosema wazazi wangu kuwa huyu mtu sio mwaminifu, ina maana tabia za kifamilia zinaweza kurithiwa, kuwa wazazi wake sio waaminifu hata mtoto atakuwa hivyo hivyo..hapana...sikubali...’akajikuta akiongea peke yake

‘Kwanza lazima nimbane nijue ukweli....nataka ukweli wote, na ikibidi kama atanificha, nitamtumia mchunguzi....'akasema

'Nahisi kuna kitu.., ni lazima hii akaunti yake idhibitiwe kama zilivyo akaunti nyingine....'akawa anazidi kuwaza

'Na naona sasa ni wakati muafaka wakupitia makubaliano yetu ya ndoa na vitega uchumi vyetu, huyu mtu siwezi kumuamini tena kihivyo..., yaani namtetea nambeba, lakini habebeki, hapana....’akasema na kuinua simu yake

‘Halloh,nataka kuongea na wakili,..ndio wakili wa familia yangu....’akasema akijitambulisha kuwa yeye ni nani.....

Siku hiyo hakuchelewa kuondoka kama ilivyokuwa kawaida yake, akaondoka mapema kabisa kuwahi nyumbani,.


WAZO LA LEO: Tukumbuke kuwa wanandoa ni kitu kimoja, ni vyema kama wanandoa mkawa mnaaminiana, mnapanga mambo yenu kwa pamoja hasa wale mnaofanya kazi, na hata kama mmoja anafanya kazi na mwingine hafanyi, lakini inapendeza mara kwa mara mkifanya hivyo. Tabia ya kufichanafichana baadhi ya mambo, inachangia kuyumbisha ndoa yenu, na hilo linaonyesha kuwa kuaminiana kwenu ni kudogo,,...na kwa hali kama hiyo mnamkaribisha ibilisi kuvuruga ndoa yenu. 
Ni mimi: emu-three

No comments :