Wanasema kawaida mwizi huwa hatoki ,mbali, kwahiyo mimi nikajenga
ukaribu na hiyo familia, nikichunguza nyendo, tabia....na nilipohakikisha
nimefanikiwa, nikaanza kazi
Tuendelee na kisa
chetu
************
Jamaa huyo
alikuwa na familia, ya mke na watoto wawili, binti mkubwa akisoma kidato cha sita, na kijana wa kiume akiwa
kidato cha nne, na mke alikuwa akifanya kazi mbali tofauti na mume wake.
Mume yeye alikuwa akifanya kazi karibu sana na nyumbani
wanaposihi, ukilinganisha na mkewe , lakini mke alikuwa wakati wote wa kwanza
kufika nyumbani.
Mume alikuwa
na tabia ya kupitia kwenye bar moja na
kupata kinywaji, na alikuwa na muda wake maalumu wa kuondoka, huwa haupitlizi....ukishafika
muda huo wa kuondoka, haraka analipia bili yake na kuelekea kwenye gari lake ,
na akifika kwenye gari lake huchukua muda kidogo, haijulikani anafanya nini
kwenye gari, baadaye huondoka.
Basi mimi nilipohakikisha
nimekusanya zile habari muhimu nilizozihitajia ndani ya hiyo familia, nikaona
sasa niingie hatua nyingine,..hatua hiyo ilihitajia msaidizi, na nilishajua ni
nani atanifaa ili kuweza kukamilisha hiyo kazi ya pesa nyingi.
Kwahiyo nilikwenda
kwenye hiyo bar,ambayo huyo jamaa huwa anakwenda kupata kinywaji, sio mbali na
hapo nyumbani kwao, ni mtaa wa pili yake, nilishapata habari za juu kwa juu
kutoka kwa mtaalamu, kuwa huyo jamaa huwa halewi sana, anakunywa kiasi, kwahiyo
isingelikuwa ni rahisi sana kupitiliza na kupoteza utashi wa kujichunga.
‘Kwa namna
hiyo ni lazima upate binti mcheshi anayejua kumpagawisha mwanaume, ahakikisha
anamzoea , halafu ahakikishe anamfanya amuone tofauti, na ikibidi uongeze
makali kwenye kinywaji chake....’alikumbuka alivyoelekezwa na mtaalamu.
‘Mhh, hilo
la kuongeza makali, ni hatari...naliogopa sana, sitaki kufanya kosa hilo
tena...’akasema profesa
‘Siseme umuwekee madawa, usininakili.... hapana, siku hizi kinywaji kinaweza kuongezwa makali kutokana na
mnywaji mwenyewe, niongezee sijui gongo, au nini,....au sio...wauzaji wanalifahamu hilo..’akasema
‘Inabidi
kujihami, maana ni lazima akija kuzindukana atajua kuna kitu kilifanyika na
kama ni mjanja anaweza kwenda kupima, akigundua aliwekewa kitu, unahisi itakuwaje, binti
aliyehusika atakuwa matatani, na binti akiingia matatani,mini sitaaminika tena,...mimi naona nikumweka sawa huyo binti yeye atajua ni nini cha kufanya, wao ni wazoefu wa hizo kazi,
sizani kama atashindwa....’akasema profesa
‘Hiyo ni kazi
yako, muhimu ni kucheza na muda,...tunataka tuliwahi tui, likiwa bado...ok, mimi siwezi kukuingilia huko, muhimu uwe makini na huyo binti utakayemchagua..., awe kweli anaweza
kumpagawisha huyu mtu, ..na msiri...kazi hii pamoja na yote inahitajia usiri...'akasema mtaalamu
'Huyu jamaa bado hajafahamu mazingira na tabia za hapa kwetu, na anavyoonekana, kahamanika na vimwana wa hapa, anafikiri vyote ving'aavyo ni dhahabu, anaonekana ana kihoro, ana pupa, na nahisi mkewe
sio mlishaji mnzuri, ...na watu kama hawa wakipata mwanya...si unajua ...’akasema
mtaalamu akitikisa kichwa na tabasamu mdomoni.
‘Mhh, hilo nitalijua
nikiongea na huyo binti, wapo wanajua hiyo kazi muhimu ni pesa tu...na kama
anakunywa mahali hapo....ameingia mkenge....’akakumbuka alivyomwambia mtaalamu.
Basi mimi baada
ya kuifahamu hiyo familia na udhaifu wa huyo jamaa hatua ya pili ikawa sasa
kumtafuta mwenza, ambaye atacheza picha na jamaa,huyu ni muhimu sana, na
anatakiwa mtu unayemfahamu vinginevyo anaweza kukuuza,ukainga hatiani, au
akakusaliti na ukajikuta mnanyang’anyana tonge.
Nilishakuwa
mtaalamu wa mambo hayo, kwahiyo nilijua nimuendee nani, na muda gani,siku hiyo
nilimaliza kazi zangu mapema za vibarua vya hapa na pale nikapata pesa ya kukaa
kiti kirefu,....sina shida, utafikiri ninazo,kumbe nanuka ukata...
Nikafika kwenye
hiyo bar, muda ambao najua huyo jamaa anakuwa bado hajafika, nikaagiza kinywaji
rahisi, na wakati nakata kiu, nikamuita dada mmoja ninayemfahamu, aliponiona tu
akajua kuna jambo.
‘Mhh,nambie
maana weweukija hapa najua kuna jambo,na sizani kamaumekuja kunilipa pesa yangu....’akasema
‘Una muda
kidogo nataka tuongee dili...’nikasema
‘Si unaona
mwenyewe,...muda kama huu wateja bado kabisa, wewe nambie....’akasema
‘Nikaongea
naye moja kwa moja bila kuficha maana ni mdada tunayefahamiana, na alishakuwa karibu
nami sana,na kutokana na maelezo ya
mtaalamu,huyo mdada alishakuwa na ukaribu na huyo jamaa,binti huyo nilishamzoea
kabla,na kuna kazi nyingine nilishawahi kufanya naye.
Sikupoteza
muda nikamwambia lengo langu, ...
‘Mhh,tatizo
lako wewe unaniona nina maana pale ukinipa kazi zako, lakini ukishazishika pesa
mkononi waniona sina maana tena...,unanipa shida kuzifuatilia pesa zangu, sasa
sitaki tena kazi zako,kwanza zinaniweka kwenye wakati mgumu, naishi kwa mashaka
mashaka wakati mshahara wangu unanitosha...’akasema
‘Lakini wewe
wahitajia kutoka, kujijenga, na hutegemei kupata pesa nyingi kama hizi za
safari hii, safari hii kuna kazi nzuri yenye masilahi zaidi ukizipata unaweza
kufanya jambo la maana,...’akasema
‘Nimekuambia
sitaki,kazi zako,...kwanza nilipe lile deni langu, usifikiri nimesahau, ...’akasema.
‘Sikiliza
kazi hii ndio itanifanya nikulipe deni lako,....ni kazi rahisi sana,lakini ina
pesa nyingi ajabu..wewe hutaki pesa nyingi...?.’profesa akasema na huyo binti
ukimtajia pesa nyingi,uso unameta meta kwa furaha
‘Unajua,mimi
sikuamini,..ila kama kuna pesa nyingi kama ulivyodai,nataka ukipata kwanza
unilipe deni langu, na nakuonya, safari hii,nahitajia pesa yangu mapema,la
sivyo,nitakuumbua...’akasema huyo binti.
‘Wewe
usijali, ...kama unataka tuandikishane,hakuna shida,nina uhakika wa pesa
nyingi...’profesa akasema.
‘Inamuhusu nani,na
isije ikawa kama zile kazi nyingine ambazo zitanifanya nikimbizane na polisi,
sitaki matatizo na polisi....’akasema binti
‘Hiyo kazi rahisi
sana,...nina uhakika polisi hawatahusika
kamwe....’akasema profesa
‘Mhh, ngoja
nifikirie...’akasema
‘Hakuna muda
wa kufikiria, tukichelewa, itakuwa vigumu kuzipata hizo pesa...’akasema profesa
‘Ina muhusu
nani,au unataka mimi nifanya nini...?’ akauliza binti
‘Kuna yule jamaa
mmoja anakuja hapa na akija hupenda kukaa pale pembeni na wewe ndiye
unayemuhudumia sana....anakuja muda wa jioni....,ni mgeni mgeni sana...’profesa
akasema.
‘Nilijua
tu,....nyie watu,...mhh, ehe wataka nifanya nini na yule mbaba...?’akasema na
kuuliza.
‘Ni lazima
hawa wau tuwakaribishe mjini,...,si umemuona jamaa mwenyewe alivyo
lakini...nimgeni kweli,na kuku mgeni hakosi nini,...kamba au sio,umeona kamba
yake ilivyoning’inia
mguuni...haijifichi...sasa kazi zaidi nitakuelezea....’profesa akasema
‘Mhh,hapana,..unajua
nyie mnamuangalia mtu kwa nje,mimi nilishamuona na nilifikiria hivyo , nikajua
hata mimi mwenyewe naweza kumtoa pesa, lakini ni mumu, bakhili..sijawahi
kuoana...’akasema.
‘Huyu ni
rahisi sana...tumeshamchunguza kila kona,...tunachohitajia, ni wewe kucheza
naye, afike kitandani....sio lazima ufikie hatua ya.....tunahitajia picha zile
za kumfanya mkewe, azimie...najua hilo unalifahamu...’akasema.
‘Mhhh,.hapo
pagumu, unajua halewi sana...na anajua kutumia muda, ukifika muda wake wa
kuondoka, haraka anasimama, hata kama mlishafikia mazungumzo gani, hataki tena
kuendelea kuongea, utafikiri kafinywa...sasa sijui...’akasema mdada.
‘Tafuta
mbinu, wewe hujawahi kushindwa jambo, wewe unawajulia wanaume, sizani kama huyo
atakushindwa, hata ikibidi,...tunahitaji alewe , apitilize, asijitambue, sizani
kama akilewa anaweza kujimudu, hakuna anayeweza kuzitawala hisia zake kipindi
kama hicho, ...’akasema
‘Si mpaka
alewe, umenielewa hapo,maana siwezi kumnunulia pombe, pombe ananunua
mwenyewe,...siwezi kumgharamia mimi,...nikifanya hivyo
atanishitukia,...’akasema mdada.
‘Hiyo hiyo
anayonunua yeye,...badala ya kuchanganya kipimo anachotaka yeye, ongeza ukali,
lakini usije kuweka madawa ambayo yakipimwa, inaweza kuleta matatizo,...kwani
ni lazima tuchukue tahadhari zote....najua hilo unalielewa,...na mhh,kwani
hawezi kwenda kunywea vyumba maalumu vya juu, ...huwezi kufanya mpango huo...?’
akaulizwa
‘Hilo
linawezekana, lakini si pesa ya mtu bhana..., jamaa huyo ni bakahili pesa yake
anaitolea kwapani,wewe ukimuona akitoa pesa yake utacheka...hahaha....lakini sijui...nahitajia
muda wa kumjaribisha...’akasema
‘Hatuhitaji
muda wa kupoteza, sikiza, ...tayarisha pombe yake mapema, ongeza makali kabla
hajafika,...akija tu, usipoteze,muda,....ongea naye, kimapenzi, nilimsikia
akilalamika,lalamika ..kuna kitu wanasigishana na mkewe, na hapo ndipo pa
kupenyeza sumu,...halafu unamualika juu kuwa unamuhitaji akupe company, na siku
hizi za mwezi si huwa mnafanya vijisherehe vyenu, hakuna anayesherehekea siku
ya kuzaliwa, sasa hapo hapo unaweza kuchezea karata yako...’akasema
‘Mhh nakuelewa
sana, hayo yote lishayafikiria, ....si unajua zangu, natafuta pesa, kwa mbinu
....najua huyu jamaa ana pesa, natafuta sana jinsi ya kumtoa, lakini sikutaka
kuingia kwenye mambomabaya....’akasema.
‘Haya sio
mambo mabaya, ni yeye mwenyewe atajiingiza huko...yeye mwenyewe ndiye
atajilengesha...’akasema.
‘Ndio maana
nakuambia nahitajia mazoezi, huwezi ukamchukua mtu kwa haraka hivyo, hilo
niachie nitalifanyia kazi, na kama kuna pesa nzuri una uhakika huo, haitachukua
siku mbili,mimi nitatimiza nafasii yangu ...mambo mengine ni juu
yako,...’akasema.
‘Haya ya juu
yangu usijali, nimeshajiandaa kabisa...’akasema profesa.
‘Lakini
mbaba wa watu namuonea huruma sana...nilishamuona, anajionyesha kama ananipenda
sana, na wengi humu wameshaniambia mbaba, yupo hoi juu yako, hajui kuwa
anapenda nyoka mwenye sumu,....hahaha, ...kiukweli,...ila simuamini...’akasema
‘Kwa vipi?’
akauliza profesa akionyesha mashaka
‘Ipo siku mkewe
aliwahi kufika, alikuja kumtafuta,...sijui kwanini, haijatokea... akanikuta nipo
naye, aliniangalia kwa jicho la chuki, akamshika mumewe mkono,wakaondoka
naye....’akasema.
‘Kama
waliondoka naye kuna ubaya gani, wewe si muhudumu tu...’akasema profesa
‘Ni wakati
wanaondoka naye,...yule mkewe akawa akigeuka kunitizama mara mbili
tatu,sikupenda,alihisi kitu...keshaijua sura yangu kwahiyo naogopa sana kuja
kufanya makosa....sitaki uhasama na wake za watu....’akasema
‘Mkewe huna
haja ya kukutana naye...eti hutaki uhasama na waume za watu, wewe, mbele ya pesa, hoo, umwambie mwingine sio mimi,..'akasema profesa na huyo binti akacheka tu
'Sikiliza, sisi tunachohitajia ni kuhakikisha muda wa tendo, unakuwa sio wewe, kisura ....hutakuwa ni wewe...si unajua zile zako, tayarisha vifaa, , ....sina haja ya kukufundisha, maana unatakiwa hiyo pesa uifanyie
kazi...pesa nzuri lazima ina gharama zake....’akasema profesa
‘Kujiweka tofauti, ni gharama, vifaa hivyo ni vya kukodi, kwahiyo hapo uanifanya nitumie pesa yangu , hata sijapata hiyo pesa, je isipopatikana, ...’akasema
‘Hiyo ni
gharama yako...kwenye mahesabu yako, sihitaji kulipia mimi, unajua utaratibu
ulivyo...kama vipi nikate kwenye mahesabu yako’akasema profesa
‘Sawa, ...hahaha,
umeshanitamanisha...kiukweli kama kuna pesa nyingi, mimi siwezi kuipotezea...utaona
vumbi langu, ila nahitaji pesa zangu za nyuma kwanza, hilo utaniona mbaya,
siwezi kutumiwa kama malaya, wakati mimi sio malaya...’akasema binti.
‘Umeshaanza,..pesa
yako nitakulipa,...pesa itakuja kwa kazi hiyo,nilikabanwa kidogo,na yule bosi
wangu, lakini sasa nimeachana naye,...’akasema
‘Sasa
unaishije,...?’ akauliza
‘Ndio
hivyo,mtoto wa mji mimi,...nalala siku moja na njaa, siku ya pili akili
inafanya kazi, ukinipa leo kidogo ya kula sio mbaya, tutakatana mbele kwa mbele...,'akasema
'Eti nini...hahaha, usiongee kitu kama hicho,kwangu hupati hata senti moja.....'akasema mdada
'Sikiliza, wewe fuata nitakavyo kuambia...sasa ni saa
eeh,...’nikaangalia saa kwa mbwembwe, nilishajiona tajiri hapo
‘Muda wake
wa kufika bado kabisa.....’akasema mdada
‘Hebu kwanza
nikuuliza wewe na yeye mlishafikia wapi...mumekwenda mbali kiasi gani,
alishawahi kukuomba urafiki, upenzi,kuacha yale ya utani,...maana nijue wapi pa
kuanzia...?’ akauliza
‘Sana sana
ni porojo tu na miadi ya hapa na pale, kutongoza ndio zake, na ahadi
kibao,ukifikia kwenye kutoa pochi, anashikwa na kiguumizi...akitoka ananiachia
kiasi kidogo tu, ni bahili kweli...si unanijua nilivyo na mimi, wanaume bakhili
ni takataka kwangu, sina muda nao kabisa, lakini huyu mmh, nilishahisi kuna
pesa inakuja...’akasema
‘Nakufahamu
unajua kunusa pesa...sasa tufanye kazi....nataka wewe uache umalaya kabisa,
ukipata pesa hiyo unafungua salooni yako, au sio...’akasema
‘Nafahamu
wanaume wengi mnanifikiria hivyo kuwa mimi ni malaya, kumbe ni maneno
tu,mwisho wa siku wanakung’uta mifuko yao,mimi huyooo..lakini huyu kiukweli
nina usongo naye, maana sijawahi kuachiwa pesa ndogo kiasi hicho...ananishushia
hadhi yangu, nilitaka nimtumpie usoni, siku ya kwanza, lakini ....’akakunja uso
kwa hasira
‘Mteja ni
mfalme au sio....usisahau kunipa pesa ya kula leo,...pesa inakuja usijali kabisa....’akasema profesa
‘Usinichefue...tuongee kuhusu huyo jamaa,mimi huyo jamaa nimemlia
chachandu...nitamuhangaikia,nitamfanya ajisikie yupo nyumbani, na ataingia
kwenye anga zangu, atamsahau mkewe, atajikuta anafungua pochi lake hadharani....’akasema
na kutoa kicheko chake cha mahaba.
‘Nakuaminia mdada,sio pochi
tu...atahudhuria ATM yake na account yake kama inamdai,...wewe utaona tu...kila
kitu kimeshawekwa sawa,ni wewe tu...’akasema profesa
‘Hahahaha, ni mimi tu eeh, acha wee...mimi eeh, wewe utaona mshindwe nyie...mimi ukiongelea pesa,ushaniloga,naweza kufanya lisilofanyika,..ila ....ohoo...’akasema na kuendelea kujichekesha,
...
Huyu binti
akicheka, na kutabasamu, utafikiria ni mrembo wa kutoka mlimbwende wa kimataifa
ni mnzuri, sio utani, tatizo ni hiyo tabia aliyo nayo, tamaa na kupenda sana
pesa
‘Ulishawahi
kuwa na urafiki naye wa kimpenzi...?’ kaka mtu akauliza akimuangalia ndugu yake
kama anaangalia mtoto mpotevu
‘Bro, ...dau
lake kubwa, simuwezi, urafiki wetu sana sana ni wa kikazi tu alishaniambia mimi
ananijali kwa vile najua mbinu za kupata pesa, vinginevyo, hana habari na mimi
kabisa....’akasema
‘Nilipomuona
mara ya kwanza nilijiuliza kwanini mrembo kamahuyu haolewi,akawa na mume
wake wakatulia..maana ni mrembo
kweli,lakini ukimgusia maswala ya kuolewa,anakuambia,hawezi kuwa mtumwa wa
ndoa, na akihitajia kuolewa,ataolewa na tajiri wa kiukweli huko kwao...
‘We
jiendekeze tu,uzuri wenu mungu kaujalia,lakini una muda maalumu, ni kama ua
linavyochanua kwenye kikonyo, haliwezi kuchanua milele,linafikia muda
linanyauka na uzuri unapotea...sasa wewe jipotezee muda wako tu...’nikamwambia
‘Kwahiyo
unataka unioe wewe, kapuku, usiye na mbele wala nyuma....sitembeagi na mtu
asiye na pesa....hata siku moja,ni nuksi kwangu...’akasema
‘Sio lazima
mimi, nakushauri kama dada yangu, unajua nimekuzoea sana ni mtu ambaye
tunafanya kazi pamoja nikipata dili, tunalindana, nikikwama unaniinua,japo kwa
masimango...’akasema profesa
‘Usijali,hata
mimi najijua,...najua lini na wakati gani nifanye nini,sasa hivi ni muda wa
kutumia...muda wa kutulia na kupata mume ukifika hutaamini...’akaniambia siku
nilipoanza kuzoeana naye
‘Basi,tuongee
biashara...’nikamwambia,na kweli kila nikihitajia pesa za haraka kwa kumtumia
huyo binti sizikosi, ila tatizo langu kama anavyosema,mimi nikishika pesa ni
zangu, kuzitoa ....mmh,labda nikununulie kinywaji, nikiwa kwenye matumizi,
natanua kweli, nanunulia watu najitangaza, ...lakini sio kutoa pesa taslimu,
pesa ikiwa mkoni mwangu ni yangu...
‘Kwahiyo
tuanze lini...?’ akauliza binti
‘Leo, leo
hii akija wewe muanze, na hata kama leo ataingia kwenye kingi, ..mimi nipo
tayari, kila kitu nimeshatayarisha, si unajua siku hizi, simu inakuwa na kila
kitu...ni wewe tu, unajua zile ishara zetu...sichezi mbali...’akasema profesa
‘Sawa,
muhimu tu, tusije kuonana wabaya,...ngoja namalizie hizi kazi ili nije tukae
unipe mikakati yote, na kiasi changu kitakuwa shilingi ngapi....na nataka kwa
maandishi...’akasema binti
‘Maandishi,
ya nini , unataka kuharibu sasa...’akasema profesa
‘Na safari
hii kaka yangu atakuwepo, kuhakikisha hunidhulumu...’akasema
‘Aaah, kaka
wako wa nini...’akasema profesa
‘Yeye
hatashiriki, na wala hatajua, ila
hatacheza mbali, nilishamwambia ikifika jioni aje, awe bodyguard , siku hizi hana kazi,...namlipa kitu kidogo, kwa siku
ili asilale njaaa, sasa wewe ukinidhulumu tu, nitampa ishara na yatakayotokea
mimi sipo...’akasema binti
‘Hapana hilo
siwezi kukubaliana nalo...sihitaji mtu mwingine hususani kaka yako, kaka yako
mimi simuamini kabisa, ni mshari, na
anapenda uchimbi, simuamini kabisa...’akasema profesa
‘Nimekuambia
yeye hatashiriki, yeye anakuwa nje, kunisubiria wakati wanguu wa kuondoka, ni
mimi na yeye, siwezi kumuambia leo usije wakatii tumeshapangana
hivyo,....’akasema
‘Yule
ananusa..anajua hapa kuna jambo, simuamini kabisa,....’akasema
‘Kama hutaki
basi mimi hata hiyo kazi yako siitaki,sio lazima niifanye mimi , tafuta mtu
mwingine...nimeshakuambia safari hii sitaki kudhulumiwa, nimeshafanya kazi zako
nyingi, na mwisho wa siku naishia kudhulumiwa, ....sasa uamuzi ni wako...’akasema
binti
NB: Habari ndio hiyo, lakini usiige, ni hatari,ni mbaya..utaona mwisho wake...
WAZO LA LEO: Penye dhuluma, hakuna kuaminiana
kila mmoja anataka zaidi, kwani mwenye tabia ya kudhuluma huwa hatosheki,
kajawa na roho mbaya, na kwa vile ni dhuluma, mwisho wake watu haohao
walioshiriki kwenye kudhulumu wenzio huja kuumbuana wenyewe kwa wenyewe.
Dhuluma ni
mbaya, dhuluma ni laana, na kama usipojirekebisha mapema, dhuluma hiyo hutafuna
baraka ya riziki kama kansa inavyotafuna uhai wa mtu, kama asipowahiwa haraka kutibiwa.
Tuache dhuluma, na tutosheke na riziki ya halali ya jasho letu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment