Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, June 24, 2015

RADHI YA WAZAZI-9


Pole sana profesa hayo ndiyo malipo ya mtu kama wewe,

‘Lakini vipi maisha ya kijana wako,  uliyemtengeneza wewe mwenyewe maana kaharibikia mikononi  mwako, hebu tuambie,unasema ameshaoa mwanamke, tena mwanamke  wa kizungu..., je maisha yake yapoje...na vipi anatarajia kurudi huku kwao tena..?’ akaulizwa

Maisha ya kijana hadi kuoa kwake, au jinsi alivyokutana na huyo bibiye chanzo ilikuwa ni mimi..undani wake alivyokubaliana naye yeye mwenyewe akiwa hapa mtakuja kumuuliza....’akasema

‘Kwahiyo atarudi nchini, ...?’ akaulizwa

‘Ndio ni lazima arudi maana huko sio kwake, japokuwa keshapata kazi,...’akasema

‘Haya hebu tuambie ilikuwaje, maana unasema wewe ndiye uliyemfanyia mpango wa kumpata huyo binti wa kizungu....’akaambiwa

Tuendelee na kisa chetu

**********

‘Tuliandoka hapa kwa shinikizo kama mnakumbuka, ilikuwa sina jinsi, na ...ilibidi ili niwahi kupata mafao kutoka kwa wafadhili, kwani kama ningelimuachie aende peke yake, ile dhamana ya kuwa mimi ni mlezi wake ingeliondoka...’akaanza kusimuliza profesa

‘Tulipofika  huko kijana aliendelea na masomo yake kama kawaida, kidarasani alikuwa akijitahidi kwa kweli...na ilikuwa kila mwisho wa wiki anakuja hapo ninapokaa, na sikuacha kmshauri sana kuwa analofanya la kuwakataa wazazi sio jambo jema, ...’

‘Unajua hata mimi sikupenda hilo, ndio maana ilifika muda nikajaribu hata kumuelewesha jisi gani nilivyompata akiwa katikati ya msitu akitaka kuliwa na wanyama wakali, lakini sikupenda kumuonyesha huo ushahidi nilijua unaweza kumfanya akawachukua wazazi wake kabisa.

This is not true I will nevet believe this ...’ akasema na kweli hakuamini hayo, yeye alishikilia hivyo, kuwa yeye ni yatima na hana wazazi...

‘Basi nikasema ngoja nione mwisho wake huenda akabadilika, lakini kiukweli kila siku ilivyokwenda ndio alizidi kujiona kuwa yeye ni mtoto asiye wahi kuwa na wazazi..,na hata mimi ni kama mpita njia tu niliyejitolea kwake, ...

‘Nilipoona ananikasirikia na mimi, ikabidi sasa niachane naye katika ushauri maana niliona anaweza hata kukataa kuja kwangu, na hapo nitaonekana kuwa mimi sio mlezi wake kama nilivyoahidi, na tulikwenda hivyo hivyo mpaka akafikia muda wa yeye kuanza kazi na alipewa kipaumbele na wale wale wafadhili katika kutafutiwa kazi

‘Tutamchukua huyu kijana afanye kazi kwenye moja ya kampuni zetu....’siku hiyo nikaambiwa na mmoja wa wafadhili nilipoona hakuna kinachoingia kwenye akaunti yangu ya benki

‘Kwahiyo hakuna fedha yoyote ya kusaidia, maana nilikuwa na mambo yake mengi nafuatilia..’nikajaribu kujitetea

‘Mambo kama yapi, maana matibabu, na jinsi ya kuishi atakuwa sasa analipwa kutokana na mshahara wake, ...sisi tunaona hahitaji mtu wa kumsaidia tena, tumeshaongea naye na amesema anajimudu..na zaidi alisema hakuwa anapata hivyo unavyodai kuwa wewe ulikuwa ukimfanyia...’wakasema

‘Sio kweli, unajua huyo ni mtoto, na watoto wanataka kila kitu uwape, nilijitahidi kama mzazi kuhakikisha anapata kile kinachostahiki....’nikajitetea hivyo

‘Sisi kama wafadhili wake  tutalifanyia uchunguzi, na tukiona kuwa kweli wewe ulikuwa ukimtendea kinyume na makubaliano, tutahakikisha sheria inachukua mondo wake...’wakasema na hapo nikaanza kushituka, maana kiukweli nilikuwa nikitumia pesa zake kwa kiasi kikubwa kwa mambo yangu, na sikuwa namfahamisha huyo kijana kuwa kuna pesa nazipata kwa ajili yake.

Siku hiyo nikamtafuta kijana wetu ili nimuweke sawa, akubali kuwa nilikuwa nikimsaidia, lakini pia nilitumia muda huo kumshauri, kuwa sasa hivi sipati pesa zake kwa ajili ya mahitajio yake, kwahiyo akipata kazi asinisahau maana biashara zangu hazilipi tena....

Dad, siamini kuwa ulikuwa ukipata pesa kwa ajili yangu, mbona nimekuwa nikiishia maisha ya shida, kila nikikuambia nahitajia hiki au kile unasema huna pesa, ...na kumbe ulikuwa ukipewa pesa kwa ajili yangu...’akasema akionyesha kunikasirikia

‘Unasikia mimi kama mzazi nilitakiwa nihakikishe sikupi pesa ovyo , nilijua kwa tabia yako itaharibika nilikulea kama mtoto wa nyumbani, ili ujue maisha jinsi yalivyo...’nikamwambia hivyo

‘Kwa vile mimi ni yatima au sio , ...sina baba , na sina mama, hata walezi ndio nyie mnapewa pesa zangu mnazitumia wenyewe, sitakuamini kamwe, na sasa nitajitegemea mwenyewe, sihitaji msaada wako, nimeongea nao nimewaambia nitaweza kujimudu, haina haja ya wao kukutumia pesa tena kwa ajili yangu, labda wakupe tu kama kukusaidia wewe....’akaniambia

‘Sikiliza kijana wewe bado ni mdogo sana...., usijione kuwa umepata kazi ndio ujione kuwa unaweza kujimudu, unahitaji mtu mzima kama mimi wa kukuongoza, ..unajua wewe ni muafrika, hata kama unaishi huku, unatakiwa ujue maisha ya kikwenu, huko nyumbani maisha ni magumu, unatakiwa uwakumbuke wazazi wako,..ndio maana nilitaka nikujenge kihivyo....’nikamwambia

‘Sina uhakika na hilo... sizani kama ulikuwa ukiwatumia ndigu zako pesa yangu...ila kwa mahesabu niliyopewa na hao waliokuwa wakinifadhili, ningeliweza kuishi maisha mazuri tu....lakini hakuna shida, ulichotumia kinatosha, na sihitaji chochote kutoka kwako zaidi, na kwahiyo hatudaiani, nitawaambia ulikuwa ukinisaidia haina shida, ila kuanzia sasa mimi na wewe basi...kwaheri...’akasema na kutaka kuondoka

‘Mimi na wewe basi kivipi, ....Kwaheri kivipi, huoni nahitajika kulipia pesa ya kodi ya nyumba,  nitapatia wapi pesa, usiponisadia..umesikia nimekuambia hao wafadhili hawaingizi pesa tena kwenye akaunti yako, sina pesa, nitaishije...na mimi nimefanya haya yote kwa ajili yako...’nikamwambia na yeye akaniangalia kwa dharau.

‘Kijana ana dharau...hata sijui kama utaweza kuishi naye bila kukwaruzana, anajiona na uafrika kwake ni kama bahati mbaya...’akasema

‘Lakini yote si umeyafanya wewe kumuharibu...’akasema kaka mtu

‘Mhh, hapana...nilifanaya kile nilichoona ni sahihi kwa muda huo,sikujua kuwa atakuja kubadilika hivyo...’akasema

‘Mhh, sasa mkamalizana na yeye vipi, alikubalia kukusaidia, kulipia kodi ya nyumba?’ akaulizwa

‘Hakunisaidia,a lichosema kilikatisha tamaa, akasema;

‘Wewe rudi nyumbani kwenu..kama ulikuwa unaishi kwa mgongo wangu, ujue sasa mimi naishi kwa kujitegemea,ninaweza kujimudu mwenyewe, sihitaji msaada wako, nina mshahara wangu na maisha yangu, nimeshapata sehemu ya kuishi, nzuri tu....’akaniambia

‘Basi nitakuja tuishi sote maana hapa napo wananizingua, ni wapi nije ..nitamwambia huyu mwenye nyumba siishi tea hapa natoa notice ya kuondoka..kwanza alishanipa notice ...’nikasema na yeye akaniangalia kwa madharau akasema

‘Ninaishi kwenye sehemu yangu mwenyewe, sihitajii kuishia na mtu, labda nikioa nitaweza kuishi na mke wangu, na nikioa siwezi kuishi hapo nipoishi sasa hivi nitatafuta sehemu yenye nafasi, nina mahesau yangu, ya kunitosha mwenyewe....’akasema

‘Mhh, kijana usisahau kuwa mimi ndiye niliyekufikisha hapa, hutakiwi kunitupa hivyo...’nikamwambia

But, ...umeshatumia pesa yangu nyingi, ...na ukumbuke  hatukuwa na mkataba wowote kuwa nikipata kazi nikusaidie..au kuna mkataba kama huo, nikawaulize hao wafadhil...?’ akaniuliza akijua kuwa hakuna kitu kama hicho, na kabla sijajbu akasema

‘Kiukweli hakuna mkataba kama huo,.. wewe ulitumia ujanja ujanja tu...dad, whoever you are...nakushauri utafute njia nyingine ya kuishi, usitegemee tena kupitia mgongo wangu,  maana hao watu wamesema hawatakuingizia pesa tena, na ...mimi siwezi kukusaidia, nitakachokukusaidia ni kuwaambia kuwa kweli ulikuwa ukinisaidia, basi yaishe mengine, ..samahani sana....’akasema na hakupotea muza akaondoka.

You...son...a....’nikataka kumtukana lakini alishaondoka.

‘Ulitaka kumtukanaje wakati kosa ni lako, cha mjanja huliwa na mwerevu zaidi yake,...umeonaeeh, na maisha hayo ya ujanja ujanja matokeo ndio hayo...’akasema kaka mtu

‘Sawa kaka, ...kuna mengi yalitokea hapo....ila katika kuhangaika nikafanikiwa kufanya kazi kwa majumba ya watu kama niivyosema kazi za ovyo weli, na siku moja nikapata kazi kwa mama mmoja wa kiafrika aliyeolewa na mzungu, mama huyo tukaivana, akaniamini kupitiliza...

Wao walibahatika kumpata binti mkubwa tu, lakini ukimuangalia huyo binti , sura yake na wao haviendani kabisa,...nikajua hapa kuna namna..kawaida kila nikipata sehemu kazi yangu kubwa nikuchunguza maisha yao,...nilitafiti familia hiyo nikagundua kuna kitu kisicho sahihi....

‘Sasa maisha ya watu yanakuhusu nini...?’ kaka yake akauliza

‘Hahaha, bro....maisha hayo, niliishi nayo sana, hasa nilipokuwa sina kazi, nilikuja kufundishwa na washikaji fulani, ambao huishi kwa maisha hayo....’akasema

‘Mhh,....tabia mbaya sana hiyo...’akasema kaka mtu

‘Kwa vile hiyo familai waliniamini sana, niliweza hadi kuingia ndani, na kama hawapo natafuta kila kona, kuona kama kuna kitu kitanisaidia, hawakujua kuwa wameingiza nyoka ndani...’akasema

‘Maisha hayo nilifundishwa bro, ukiwa ulaya usipokuwa mjanja unaweza kufa njaa huku watu wanakuangalia tu, kial mtu na bajeti yake...watu wanakula wanasaza lakini hawawezi kumkumbuka mwenye njaa,....

‘Nilishakutana na kundi la mitaani,ambao huishi kwa utapeli, nilishapanga mipango nao mingi mmojawapo ni huo ..kuwa kila nipofanya kazi kwa watu nachunguza zile tabia ambazo zinaweza kuwaumbua, ...kama wanandoa kusalitiana, mambo ya siri ambayo hawataki yagundulikane....

Nilikuja kugundua kuwa binti yao huyo hawakuwa wamezaa pamoja, huyo mwanamke hakuwa na kizazi, wakapandikiza mbegu , na kumpata huyo binti, niligundua hilo kwenye kumbukumbu zao...nikaona sasa hapa ninaweza kufanya jambo

‘Jambo gani, kwani hayo yanakuhusu nini...?’ akasema kaka yake

‘Bro, wewe sikiliza, ...nikuonyeshe maisha niliyopitia, usinione ivi bro, nimeteseka sana, hadi kufikia kufanya hivyo, niliwahi kukaa siku mbili, sina kitu cha kula....hebu fikiria njaa inavyouma, nikafika kwa kijana akanifukuza kama mwizi....’

‘Ndio nikaanza kuhangaika, ...nilipoligundua hilo, kuwa familia hiyo ina mtoto wa bandia, na wakati wao walishaniambia walimzaa kihalali, nikajua kuna jambo..

‘Hilo nilologundua sikuwaambia kundi langu, nilichofanya ni kutafuta simu za mitaani , siku hiyo nikiwa nimejipanga nikabadili sauti, ..najua kubadili sauti za kila namna,....nikawapigia hawa watu wenye mtoto wa kupandikiza,

‘Haloh,,....mimi ni mchunguzi  huru wa magaeziti ya udaku, katika kufuatilia kumbukumbu zangu nimegundua kuwa nyie hamna mtoto halali ...’nikawaambia

‘Nani kakuambia hatuna mtoto halali na una maana gai kusema mtoto halali..?’ akaniuliza huyo mama, nilifurahia kuwa aliyepokea hiyo simu ni huyo mama mwenyewe, maana nilipiga simu ya ndani

‘Nyie huyo mtoto mumempata kwa kupandikiza uzazi....,’nikamwambia

‘Eti nini,....ok, sasa hata kama ni kweli, japokuwa  sio kweli inakuhusu nini....?’ akaniuliza

‘Kwasababu kwenye kumbukumbu zenu inanyesha mumezaa kihalali, na kunamambo ambayo mumeficha ukweli....’nikasema

‘Hata kama ni hivyo inakuhusu nini..kuna kosa gani tumefanya?’ wakauliza

‘Je binti yenu analifahamu hilo...?’ nikauliza nilishapanga kuwa huo uwe ndio mtego wangu, na niliposema hivyo, nikasikia mama akihema kwa mshituko.

‘Hata kama hafahamu inakuhusu nini wewe,...?’ akauliza...mwanzoni mama huyo 
alijifanya hajali, lakini kwa uzoefu wangu nikagundua hilo la kumuambia binti ya limemusa kwani niliwahi kuongea naye alisema kama kuna kitu ambachoo hataki kukifanya ..ni kumuuzi binti yake anampenda sana..kwahiyo aliposikia kauli hiyo, alihisi vibaya sana.

‘Basi mimi nitamwambia binti yenu tuone kama hatawachukia nyie kwa kitendo hicho...unakumbuka watoto kama hao wanavyokuwa wengine huweza hata kujiua...na wengine wanaachana na wazazi wao kabisa...’nikawaambia

‘Kwahiyo unahitajia nini kwetu...ni nini lengo lako?’ akaniuliza

‘Ili nihakikishe kuwa siri hiyo haivuji, na binti haipati hiyo taarifa, inabidi mlipe gharama fulani...kama dola elifu kumi tu...sitaki pesa nyingi....’nikasema

‘Wewe unaota hizo pesa sisi tutazipatia wapi, wakati kipato chetu ni shida....’akasema

‘Nataka hizo elifu kumi haraka...zingine nitajua jinsi gani ya kuwapunguzia...vinginevyo nitamwambia huyo binti yenu kila kitu kuwa nyie mlimpataje huyo binti.....’nikawaambia, na kukata simu

Watu kama hao hutakiwi kuwapa muda, mengine yanakuja yenyewe, nikakaa siku mbili, ukumbuke kuwa mimi nafanya kazi humo,na nilishaweka mitego yangu, kila kinachoendelea humo ndani nakifahamu, mama alionekana hana raha kabisa, na niliona kuwa hakuwahi kumuambia mume wake,

‘Mbona huna raha...?’ nikamuuliza

‘Nani,mimi...aah, ni mamb yangu tu..ni mambo ya kimaisha, ni..maisha magumu tu..’akaniambia

‘Kama kuna tatizo niambie, mimi kuishi mitaani ninajuana na watu wengi tu, ....najua mambo mengi tu....’nikamwambia

‘Hakuna tatizo, na kama lipo nitalimaliza mwenyewe sihitaji msaada wako...’akaniambia, na niliposikia hivyo nikajua kuwa kunahitajika shinikizo, ndio siku hiyo nikatafuta sehemu nyingine nikampigia simu

‘Nataka hizo pesa umpelekee yule jamaa wa kasino jirani yako, mlinzi wewe umkabidhi na bahasha, mimi nitajua jinsi gani ya kuzipata, vinginevyo, leo nitakutana na binti yako, ni siani kama utafurahia nikimwambia yote nina kumbkumbu zako sote....’nikamwambia

‘Sina hizo pesa...sijazipata bado nazitafuta....’akasema, nilishajua kuwa ana pesa alishakusanya, japokuwa hazikufikia hivyo, hakujua anayempigia simu ni nani,..

‘Wewe una kiasi gani?’ nikamuuliza

‘Nusu yake...’akasema

‘Nataka kumi, fanya haraka usinitanie...kwanza kuna mashindani  ya watoto kuwaonyesha wazazi wao vipaji vyao, hapo hapo nikimwambia najua atawachukia sana nyie wazazi wake...,sizani kama atafurahia kuwaona nyie kama sio wazazi wake...’nikamwambia na mama huyoo alioekana hana raha, hata nilipofika kazini, nilimuona kanyong’onyea

‘Kuna mzigo nataka umpelekee yule mtu wa kasino, yule mlinzi wao anayefanya kazi ya kupokea mizigo ya watu na kuifikisha anapoelekezwa..., lakini nataka iwe siri, nataka uchunguze baadaye ni nani atakuja kuzichukua kwa huyo mlinzi...’akaniambia

‘Mhh, mama naona kumbe kuna tatizo kwanini usiniambie ni tatizo gani ili niweze kukusaidia,...’nikasema

‘Sikiliza hakuna tatizo, nataka hiyo bahasha usije kuifungua, nitakufuatilia kwa nyuma, hakikisha inafika kwa huyo mtu...’akaniambia, basi mimi nikaongea na huyo mlinzi, namfahamu sana, kazi yake mojawapo ni hiyo kupokea mizigo ya watuu kwa ajili ya kuwapa watu wengine...anatambulikana na huwezi kumshitakia,,...

‘Basi mimi nikafanya kama nilivyoambiwa, nikamkabidhi huo mzigo, na nikarudi kwa huyo mama, nilikuta hayupo, nikajua anachunguza ni nanii atakuja kwa huyo mlinzi, na huyo mlinzi nilishapanga naye wapi nikachukue huo mzigo,...haikuwa shida kwake kwani ni kazi yake..., nikaupokea,..hahaha nikajua sasa huyu mama kaingia kwenye anga zangu....

Kesho yake nikafika kwa huyo mama, nilimkuta hana raha kama kawaida yake, nikamuuliza majibu yakawa ni yale yale, mwisho akaniuliza

‘Hivi yule mlinzi nikiongea naye hawezi kuniambia ni nani aliyempelekea  huo mzigo, hata nikimpa kitu kidogo...?’ akaniuliza

‘Mhh, mimi sijui,...lakini kama kazi yake ni hiyo ya kupokea mizigo kwa mtu fulani na kupeleka kwa mtu mwingine sijui kama atakuwa na kumbukumbu ya watu wote,...’nikasema

‘Nilikuambia ufuatilie ujue wapi kaupeleka huo mzigo...’akaniambia

‘Mimi nilijaribu kumfuatilia, nikakuta ana watu wengi wamempa mizigo na akizitoa inakuwa kwa siri kubwa,...sasa ungeniambia ni nani unamshuku au kuna tatizo gani ingelikuwa ni rahisi kwangu kuweza kusaidia...’nikamwambia

‘Mimi ni mtoto wa mjini, ....nimetokea huko huko, hanijui huyo mtu, utakuja kuona jinsi gani nitakavyo mnasa, si amekula pesa yangu hiyo, lakini atakuja kuirejesha...tena kwa malipo makubwa sana, ya maumivu...’akasema

Mimi sikujali maana ukiwa katika shughuli kama hizo, moyo unaota sugu, na kwa vile nilikuwa naye sambamba, sikuwa na wasiwasi, basi tukakaa hadi mwezi ukaisha , kulikuwa na tukio fulani shuleni kwa mtoto wake, la wazazi kukutana shuleni, na hapo tena nikaona kuna haja ya kupata pesa, nikampigia simu

‘Ni wewe tena, unajua unanitafuta ubaya, nitakuja kukuumiza ...’akasema

‘Kwani kuna tatizo, nilisema ili niweze kulimaliza hilo nahitajia kumi kumi kila mwezi,kwa miezi mitatu, ulitoa nane badala ya kumi, unadaiwa mbili, na kumi za mwezi huu, mimi nitajua jinsi gani ya kulifuta hilo, maana sipo peke yangu nitawanyamazishaje wenzangu...’akasema

‘Sikiliza hupati pesa yangu yoyote safari hii, nenda kokote,...’akasema

‘Leo ni siku ya wazazi, muulize binti yako aliongea na nani, na alihidiwa kupewa siri gani....?’ nikamwambia, nilishampigia huyo binti kwa siri, na kumwambia nina siri kubwa kutoka kwa wazazi, sikutaka kumuambia zaidi, nikasema

‘Ni nani wewe mbona sikujui....?’ akasema huyo binti kwenye simu

‘Wazazi wako wananifahamu sana,...’nikasema

‘Siri gani wataka kuniambia?’ akaniuliza

‘Nitakupa siri hiyo siku ya sherehe ya wazazi...’nikasema na kukata simu, nilijua ni lazima huyo binti atamwambia mama yake kwani walikuwa karibu sana..na kweli nilipoongea na huyo mama akaonyesha kuogopa zaidi akajua kumbe kweli niliongea na binti yake, akasema

I will kill you....ipo siku nitakunasa, utalia machozi ya damu...utanijua mimi nilitokea wapi...’akasema na kweli siku ile akapeleka elifu tisa, nikaona sio haba...

‘Unajua maisha yangu yalikuwa hivyo, kwangu mimi sikuwa nataka mapesa mengi,..hizo hizo elifu tisa, nane, kuna siku alitoa hadi elifu kumi na tano, nilimtega kubaya, nilijua ana pesa, nikampigia na hapo hapo nilishaongea na binti kwa siri..siku hiyo alijua kabisa siri itajulikaa akatoa kumi tano..

‘Kuna namna nyingi nilitumia kumtoa pesa huyo mama, hakujua kuwa ,mimi nilikuwa nafuatilia, nyendo zake, lini ana pesa, na lini naweza kumtoa, na inakuwa vigumu kwake kushindwa kunikatalia,..akawa ni mteja wangu, pamoja na wengine, na maisha yakawa yanakwenda.....

Baadaye huyo mama akamshirikisha mume wake, mume wake alikuwa mjanja sana,...wakaanza uchunguzi wakatafuta mpelelezi wa kujitegemea kunisaka mimi, lakini hawakujua kuwa nyoka wao yumo humo humo ndani...

Mwanzoni walishindwa,, lakni walipotafuta mpelelezi, mpelelezi akaja kuwashitua kuwa inawezakana mbaya wao atakuwa humo humo ndani kwani kwanini kila wanachopanga kinajulikana,....ghafla wakaamua kunisimamisha kazi

‘Ndugu sisi tuna matatizo makubwa,...hatutaweza kukulipa tena, kwahiyo tunakuomba utafute kazi sehemu nyingine...’siku hiyo wakaniambia, nikajua huenda wameshanihisi ..lakini sikuwa na njia ya kujitetea nikaachana nao,....

Nikawa nina shida ya pesa, na hapo ilikuwa ni sehemu yangu ya kunikoa, nikashindwa nifanye nini,...nikaona nitafute njia nyingine,  nikaona labda nipitie kwa binti yao, ili kupata taarifa za hapo nyumbani, kwahiyo kila mara nikajitahidi kukutana na binti yao, na weli alinizoea sana kwa vile nilikuwa karibu naye nikiwa hapo nyumbani, hakuweza kugundua lengo langu....

‘Kwahiyo huyo binti yao, ukataka akupe siri za hapo nyumbani kwao, wewe weli ni shetani...’akauliza kaka mtu

‘Bro wewe tulia, nikuonyeshe nilivyoishi ulaya kipindi hichoo cha shida...maisha yana fundisha mengi,...hapo ndipo nikagundua kuwa kijana wako alikuwa akimtamani huyo binti, kumbe alishaniona nikiwa sambamba na huyo binti, na kuna siku alikutana nami nikiwa na huyo binti baadaye akaja kunipigia simu

Dad, nimekuona na binti mmoja unamafahamu anapotokea?’ akaniuliza

‘Leo unaniita dad, si ulisema hunitambui tena mimi kama baba yako...’nikasema

‘Ninakuuliza tu...hamna shida, akakata simu, na nikajua sasa hapa naweza kufanya jambo, nikamtafuta kijana na kumueleza kuwa kama anamtaka huyo binti mimi nitamfanyia mipango, muhimu tu anijali..haikuwa shida, kijana alishazimia kwa huyo binti, akakiri kuwa kweli angelifurahi kuwa na urafiki na huyo binti

So how much...utanilipa mimi...?’ nikamuuliza

‘Kukulipa nini dad, hiyo inahitajia mimi nikulipe,...wewe unatakiwa kunielekeza wapi nionane naye, na ....’akasema

‘Oooh, hujui kuwa mimi nipo karibu sana na huyo binti, na naweza kukurahisishia hiyo kazi.....’nikasema

‘Nitakupa kiasi,....sina pesa kwa sasa...’akasema

‘Wewe ni kijana wangu, hata kama hunitaki, nipe kiasi tu,...lakini ujue kuwa nahitajia kumhonga huyo binti ili aweze kuachana na wazazi  wake,wazazi wake ni wakali sana, wanamlinda sana binti yao...’nikamwambia, kwahiyo nikapata mwanya wa kupata vijisenti, kutoka kwa kijana, akawa ananipa pesa, na zawadi, ili nimpelekee huyo binti

Yule binti yao nilishazoeana naye, nikawa nimefanya mipango ya kuwakutanisha na kijana wetu,na kweli wakaja kukutana na wakaivana, na kuwa wapenzi wa kweli, nikaona hapo hapo pia naweza kutumia mbinu zangu na kuzidi  kupata chochote kutoka kwa wazazi wake...,

Nikawa namdadisi huyo binti kuhusu familia yao sasa wapoje, wazazi wana matatizo gani , naongea naye kama mtu wa karibu, na binti akawa ananielezea yale yanayoendelea ndani ya familia kama mtu aliyekuwa anawajali...

Nilipojaribu kupiga simu na kuwataka wanilipe kama ilivyokuwa awali, nikakuta wananijibu kwa dhihaka;

You again, ...sasa tukumekufahamu kuwa wewe ni nani, utajuta kuzaliwa...’akasema huyo mama

‘Hata mkinijua haisaidii kitu, muhimu ni kunipa hiyo pesa haraka iwezekanavyo...kwani binti yenu nipo naye kila siku naongea naye na nimeshamuahidi kumuelezea kila kitu kuhusu wazazi wake...’nikawaambia, lakini pesa haikuletwa na kesho yake, nikajikuta nipo uso kwa uso na huyo mama, akaniambia;

‘Nina maongezi na wewe....’akasema

‘Kuhusu kazi, kama ni kazi msubiri hadi wiki ijayo...sasa hivi sina nafasi...’ nikajifanya kuringa, kumbe moyoni nilikuwa na wasiwasi kweli

‘Ni kuhusu malipo yako ya kila mwezi ya elifu kumi....’akasema huku akiniangalia usoni, na aliposema hivyo nikajua sasa nimeshapatikana, lakini nikajifanya sielewi anachoongea nikasema

‘Malipo gani ya elifu kumi....?’ nikamuuliza kwa wasiwasi

‘Unafikiri wewe ni mjanja sana, ..unajiona wewe una akili sana, umekuwa ukiishi nasi huku ukituchunguza,...na kuanza kutuibia, hizo elifu kumi kumi, utazilipa kwa maumivu makali sana, utajua kuwa mimi ni nani....’akasema akiniangalia kwa macho ambayo sijawahi kuyaona, yalionyesha ukatili ndani yake.

Nilikuja kugundua kuwa mama huyu alikuwa mmoja wa watu wakatili sana, katika usichana wake, alipitia uhuni wote, na ndipo alipoharibikiwa na kizazi, aliwahi kuwa mitaani na kujiunga na vikundi vya kijambazi, na katika kundi lake alikuwa mmoja wa watesaji, alikuwa na nguvu zaidi ya midume,...kwahiyo alikuwa akijulikana na wahuni wahuni, baadaye akatulia na kuingia kwenye ndoa...

‘Mbona sijui unaongea nini...’nikasema nikifanya nashangaa kwa maneno yake

‘Nimeshagundua kuwa wewe ndiye uliyekuwa ukitu-blackmail....’akaniambia akiniangalia kwa uso wa chuki.

What...! Mimi..hapana, siwezi kuwafanyia kitu kama hicho..’nikajitetea

NB:Naishia hapa kwa leo....tuzidi kuombeana heri

WAZO LA LEO: Wakati mwingine wenye makosa wanahitajia muda, na namna ya kuwarekebisha, wakati mwingine makosa hayo yanatokana  na uelewi na malezi waliyoyapitia,  au kutokana tu na ushawishi wa makundi rika, ulevi, nk...na sababu nyingine za kijamii  a wakipata mongozo wanaweza kubadilika na kuwa watu wema kabisa.


Sasa ni, muhimu kwa mzazi, mlezi na yule mwenye dhamana ni kuchukua muda, na kutafuta mbinu za kuwaelimisha hawa watu na sio tu kukikimbilia kuwaadhibu kwa kifungo, au kufukuza kazi, au kuwalaani kuwa hawafai katika jamii,...au wengine hukimbilia kuwatesa, au hata kuwaua, tutakuwa hatujatenda haki, ni muhimu kuwe na hatua za kurekebisha hawa watu, kwani tunaweza kuharibu kabisa badala ya kutengeneza. 

Ni mimi: emu-three

No comments :