Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, June 22, 2015

RADHI YA WAZAZI-8


Profesa alichukuliwa na kaka yake hadi kijijini, huko akagiza dawa anazojua yeye mwenyewe aletewe maana hata kutembea hadi huko maporini ilikuwa ni shida, kiukweli mtu huyu alishakuwa mtaalamu wa dawa za mitishamba, lakini kilichokuwa kikimuharibu ni tamaa, na tamaa yake hiyo ikampelekea kuwa muwongo, akawa sasa anaongeza chumvi, ili kupata zaidi.

‘Kaka naomba ukanitafutie huu mti, na mizizi yake,...na huu mti na majani yake, ukinieletea nitatengeneza dawa yangu mwenyewe ...sihitaji kwenda kutibiwa hospitalini....’akasema

‘Kwanini usiende kupimwa kwanza ukajulikana unaumwa nini?’ akashauriwa.

‘Najua watakuja kutaja maradhi makubwa..na nyie mtakata tamaa...mimi najua dawa za maradhi haya, dawa hizi huongeza CD4, mnajua CD4 nyie...hamjui kwahiyo niachieni mwenyewe,..’akasema

‘Hali uliyo ayo si yakuuguliwa nyumbani, ....’akazidi kuambiwa

‘Nyie msijali, najua nina maradhi makubwa, lakini nitapambana nayo, nyie nileteeni, hivyo nilivyowaagiza, nikitengeneza hizo  dawa , nitapata nguvu na huenda maradhi hayo mengine hayatakuwa na nguvu sana....’akasema huku akijaribu kujiinua kwa shida

‘Kwahiyo wewe unafahamu unaumwa maradhi gani, kwanini hutuambii,....?’ akaulizwa

‘Kaka nyie fanyeni hivyo....ili nisje kuwakatisha tamaa,mnavyozidi kuniuliza mnapoteza muda,au mnataka nife....’akasema na kaka yake akafanya hivyo, akaenda kumtafutia hiyo miti shamba

Na kweli dawa alizotengeneza alipozitumia, akaanza kubadilika, afya iliyozorota, ikaanza kutengamana, akaanza kuingiwa na siha, na mwili wake ukarejea katika hali inayorizisha, japokuwa sio kama awali, ila akaweza kuanza maisha ya kijijini, na kuanza shughuli zake za madawa, japokuwa baadhi ya watu walishaanza kutokumuamini

‘Huyu ndugi yako katumia dawa gani maana ulisema sio mtu wa kuishi, ...?’ watu wakaanza kuhoji

‘Mhh, mungu mwenyewe ndiye anajua, si mlishasikia ni mtaalamu wa miti shamba, kajitengenezea mwenyewe, .....’akasema na hilo likasaidia kuwavuta watu kuja kununua dawa kwake.

Siku moja akiwa katulia, kaka yake akamjia na kumuuliza maswali

‘Je unakumbuka ahadi yako?’ akaulizwa

‘Ahadi gani tena kaka yangu, maana niliyoahidi kwa watu ni mengi, na niliyowahi kutelekeza ni machache, na hilo linaniuma sana....nilikuwa mtu wa kuahidi hata yasiyotekelezeka,...ili tu niweze kupata chochote....’akasema huku akitikisa kichwa kwa masikitiko.

‘Kwanini ulifanya hivyo, hukujua kuwa ahadi ni deni?’ akaulizwa

‘Nilijua hilo, lakini tamaa ya kupata, hata kama najua ni ulaghai ilikuwa mbele yangu, nilikuwa kama mafundi ambao hupenda kupokea kazi mpya kila siku, bila kujali ahadi ya kazi za awali, ambazo hajazitekelezeka, na ndio maana mafundi wengi sio waaminifu, hata sisi waganga, hasa wakienyeji tunafanya hivyo, wengi wetu ni waongo...’akasema

‘Na wewe ulikuwa fundii wa hadaa, fundi wa kuwarubuni watu, ukitumia ulimi wako na taaluma ndogo aliyokuruzuku mungu ya ulimi, ukautumia ulimi kwa masilahi yako binafsi,hujui ulimi unaweza kukuingiza motoni ...’akasema kaka mtu

‘Nimekuelewa kaka, na najitahidi kujirekebisha, ila najua unalo jambo, ulitaka kunikumbusha ahadi gani niliyowahi kuiahidi...?’ akauliza huku akijikuna kichwa kwa mashaka akihisi labda kuna deni anadaiwa.

‘Ulisema utatuhadithia, maisha yako ya huko Ulaya, na kijana wetu ili watu wapate kuelemika, hebu tuambie ilikuwaje hadi ukaingia jela,.je kijana wetu huko yupoje, na atarudi lini...?’ akaulizwa

Tuendelee na kisa chetu

**************

‘Kaka wengi wetu tunaamini kuwa ulaya na marekani ni kama sehemu yenye asali na maziwa, kuwa ukifika huko utachota na kunywa,...kiukweli maisha ya huko ni magumu, hasa ukiwa huna kipato cha kuaminika....hata wale wenye kipato huishi kwa kubana matumizi kweli kweli...wanaishi kwa bajeti...’akatulia.

‘Kwanza ujue kama nchi, kama eneo husika, kuna namna ya kuhakikisha kila mtu analipa kodi,...’akashika simu yake na kuiinua juu

‘Wenzetu wana mitandao ya kukusanya kodi, hii simu usiione ivi unatumia tu, lakini kule inakuwa kielelezo cha kukujua wewe upo, wapi..na kwa vile umeshajiandikisha kama raia, au mgeni, popote utakapokuwep utajulikana tu.....’akawa anafunga funga dawa zake

‘Kwahiyo wewe kama raia huna ujanja wa kukwepa kodi, ...kule hakuna muda wa kupoteza, kila mmoja yupo mbio mbio, kutafuta pato la siku maana usipolipata ujue una deni la kodi ya serikali, una deni la sehemu unapoishi, na wewe unatakiwa ule, na kule hakuna mjomba au shangazi kuwa utakwenda kudowea, kwake kuwa usibiri kiive ule huko hakuna ukikuta mwenye anakula ujue utameza mate tu..hata akibakisha hakupi, anakwenda kutupa, maana sio bajeti yako....’akasema

‘Hata ukiwa umekwama, huna hela ya kula, huwezi kwenda kuomba...kwa jirani, au kwa ndugu labda ukakope tena kwa riba, kwasababu gani yeye keshapanga bajeti yake ya siku, kutokana na kipato chake anachopata...’akatulia

‘Mimi nilipofika awali, dawa zangu zilipendwa,..unajua tena kipya kinyemi, zikawa zinasaidia watu, laikini siku zilivyokwenda wenye dawa kama hizo wakawa wengi, ukawa ni ushindani tena wa biashara, na mimi nikaanza kuyumba,...’akatulia

‘Na kilichonisaidia sana awali, ambachoo kilinidanganya ni zile pesa za misaada niliyokuwa nikipata kwa ajili ya kuwa mlezi wa huyo kijana, niliaminika kama mlezi wake, kwahiyo nikapewa dhamana ya kupokea pesa zake, lakini hilo lilikuwa na mwisho wake, maana yule kijana naye alifikia umri wa kufanya kazi, na kweli akapata kazi na kuanza kujitegemea..hapo ule mrija wa ruzuku ukaziba,...’akatulia

‘Hao wadhamini ni wale ambao wanazalisha kwa wingi, wapo watu wa namna hiyo wenye ubiandamu, lakini sio wote...’akatulia kidogo

‘Bashara ya dawa ikawa haina mauzo..., siku inaweza kupita bila kuuza chochote, na njaa ikaanza kuninyemelea, nikaona sasa naumbuka, mwanzoni, ikabidi nimuendee kijana, nimuombe msaada, na yeye kama walivyo wengine wa daraja hilo, alikuwa na bajeti yake ya maisha,..mwanzoni alinisaidia,kidogo,lakini alipoona nazidi kuja kumuomba, akaanza kunikatalia

‘Kijana, unajua mimi ni baba yako..?’ nikamwambia

‘Ni baba mlezi ndio natambua hilo, lakini maisha kama unavyoona, siwezi kukubeba zaidi,.....’akasema

‘Hicho unachopata tugawane, la sivyo nitakuja kusema wewe hukuwa yatima..unakumbuka ulipotoka, bila mimi usingelikuwepo hapo ulipo....’ikafikia muda nikamtishia hivyo

‘Hahaha, dad, ...usinitishe kwa hilo, na kwa vile umelitamka hilo, kuanzia sasa ujua maisha yako mwenyewe, na kama unataka kunipakazia, hivyo, nenda kasema,....mimi siogopi...’akasema kwa hasira, na toka siku hiyo akawa hataki hata kuniona

‘Basi siku ya siku, nikaibiwa vitu vyangu vyote, nikamuhisi kuwa ni yeye  kijana alifanya njama hizo kwa kutuma watu kuiba vitu vyangu ili akipate hicho cheti cha kuzaliwa, nilichokuwa nikimtishia nacho kuwa nitakionyesha na itajulikana kuwa yeye hakuwa ni mtoto yatima....’akasema

‘Na kweli ulipanga kufanya hivyo kwa kijana wako mwenyewe kama hakukusaidia...?’ akaulizwa

‘Maisha ya Ulaya ni ushindani, na kila nafasi unatakiwa uitumie, kwa jinsi alivyonifanyia, ...sijui, hata wewe huoni mbona mimi hajanionea huruma, mimi nilimpenda sana kama mtoto wangu lakini yeye hakunijali...’akasema

‘Sasa kwanini ulipoona hali ni mbaya kwanini usingelirejea nyumbani kwenu mapema, una nyumba yako, una biashara zako na ulishajenga jina huku...ungalifanya hivyo mapema yote haya yasingekupata...?’ akaulizwa

‘Ukionja asali, huwezi kuonja mara moja,akili ilikuwa na hamu ...nilijua ninaweza kufanikiwa,tamaa ilikuwa mbele, na pia aibu, si unajua tena ...hata hivyo ningeondakaje kirahisi hivyo, sina nauli, nadaiwa....’ akasema huku akitabasamu kwa aibu.

‘Balaa halikuishia hapo, mimi kwa kukosa soko, nikawa nafanya biashara zingine haramu, huku nauza dawa, huku nauza madawa ya kulevya, nikaja kugundulikana, nikashitakiwa, nikafungwa, ...’hapo akatulia kidogo kama anakumbuka jambo.

‘Japokuwa kifungu hicho cha mwanzo kilikuwa ni kidogo tu, kwasababu hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja, nilitakiwa kulipa faini, na sikuwa na pesa,...niliomba wamuone kijana wangu ili anilipie, lakini hakupatikana, nahisi alikataa, japokuwa sikuweza kuonana naye kwa kesi hiyo, basi  ikabidi nifungwe tu..nikaja kuachiwa, hata kabla muda haujaisha.

Nikaendelea na biashara zangu, lakini hakukuwa na masilahi, siku moja wakaja watu wa vibali vya kuishi huko, nikakamatwa tena, kwani waligundua kuwa hata kibali changu cha kuishi huko kilikuwa kimekwisha, ...’akatulia

‘Ikabidi nifanya mipango ya kuongeza muda,...ilihitajika pesa tu, tatizo sikuwa na pesa, nikaona sasa nitarudi nyumbani, lakini nitarudije na mimi sina kitu.. nikakopa kopa pesa kwa washikaji..., nikafanyiwa mipango nikapata hicho kibali cha muda, lakini kibali hicho kilikuwa na masharti,...aina za biashara na kazi..kwahiyo hapo nikawa nafanya kazi zile za muda muda tu, hutaamini nilifikia kufanya kazi za kufagia barabarani, kuomba kazi hata za kusafisha vyoo kwa wazungu,....’akatulia

‘Nikakutana na matepeli wa huko, wakaniingiza kwenye biashara nyingine haramu,..mbaya hata siwezi kuzihadithia,...hizo zikanifanya niwe mbaya wa watu, maana nikajikuta nafitinisha watu kwa kutafuta machafu yao na kuyauza ili watoe pesa...maisha magumu ajabu...ilikuwa nikipewa kazi ya kusafisha vyoo, au kazi yoyote ndani naweka vifaa vingine kuchunguza watu wanavyoishi, na kuwafanyia utapeli,..nikaja kugundulikana...

‘Haikupita muda, kukatokea mauaji, na ikaonekana mimi nami kwa namna moja au nyingine nilihusika,..lakini haiuwa ni kweli, lakini sikuwa na jinsi ya kujitetea, wakiangalia kumbukumbu zangu za nyuma, nikaonekena na mimi nilikuwa ni chanzo, ..na kesi hii ikawa ni mbaya kwangu, wenzangu wakaniruka, nikabakia peke yangu, na hukumu ikatolewa kufungwa miaka mingi tu...’akatulia

‘Ilitakiwa nipate wadhamini ili nitoke kwa dhamana, kwani nilikata rufaa, lakini nani atanidhamini, nikaomba aitwe kijana wetu aje kunidhamini, kijana akakana kuwa hanijui,....niliomba angalau aje tuongee, na siku alipokuja akanipa makavu makavu, kuwa yeye hana baba tapeli, mwizi, muuza madawa ya kelevya, hanijui na wala nisimjue,....’

‘Kijana naomba unidhamini, maana kesi hii nimebambikiwa tu, nitashinda, nikishinda nitakulipa gharama zako...?’ nikamuomba hadi kumpigia magoti, lakini aliondoka huku akisema;

Its too much, nimekukopesha pesa nyingi tu ambazo hata huwezi kunilipa ..siwezi kabisa kukubeba tena, na kwa jinsi ulivyo utanifanya hata mimi niingie kwenye matatizo...., siwezi...sikujui na usinijue...’akasema na kuondoka, nililia sana siku  hiyo maana ndani ya jela nilikuwa na maadui wengi, na walishapanga kunifanyia ubaya

‘Kiukweli jela niliyofungwa kipindi hiki cha mwisho ilikuwa ile ya watu wabaya,..huko nikageuzwa mtumwa wa machafu...sijawahi kuteseka kama nilivyoteseka hapo, nikaanza kuumwa...na hukoo kuumwa ndiko kuliniokoa, kwani nililazwa hospitalini, ikabidi niombe niendelee kuumwa....’ akasema

‘Ina maana jela huko ni kubaya sana, mbona kuna vijana wanataka wafike huko hata kama ni kufungwa wafungwe, wanavyodai huko jela,  ni bora  kuliko maisha wanayoishi huku, ..ndivyo wanavyodai wao...?’ akaulizwa

‘Asikudanganye mtu, ukumbuke jela, kuna watukutu, wengine ni wabaya kweli,...wasiotosheka, wenye tabia mbovu,...hata kama wangepewa nini bado kuna ubabe,...kuna dhuluma, kuna tabia chafu...huna uhuru,...jela ni jela tu hata kama kungekuwaje,...hakuna jela nzuri...sijawahi kufungwa hapa nchini, lakini usiombe kwenda jela...sipendi kuwaficha, jela ni mateso,...’akasema

‘Wakati nafungwa nilikuwa na madeni mengi, ya kodi za serikali, ya watu, na wengine nilikutaa nao huko jela, wakanigeukia....kwahiyo sikuwa na amani, nilijua hata nikitoka bado nitajikuta kwenye maisha magumu, ...ndipo nikakumbuka kuwa nyumbani ni nyumba yenye thamani kubwa, nikatafuta wakili, akanisaidia, nikiwa nimemuahidi kumlipa kutokana na mauzo hayo ya nyumba..

‘Kwa vile ile kesi niliyofungwa ilikuwa ya kutengenezwa, ili maadui zangu wanikomoe, wakili wangu akaenda kuongea na hao watu, kuwa nitawalipa kiasi fulani, na wao  wakaona hakitaharibika kitu.., basi mambo yakawekwa sawa, ikakubalika hivyo...

‘Huyu wakili ulimpataje na wewe huna pesa...?’ akaulizwa

‘Yupo jamaa anatokea huku ananifahamu, na anajua kuwa kweli nina nyumba yenye thamani kubwa, huyo ndiye aliyefanikisha hilo.....akijua kuwa kweli ikiuzwa atarejesha gharama zake pia, maisha ya sasa ni ushindani, ukiona sehemu ina masilahi unabahatisha, na huyo wakili ndio maisha yake, akabahatisha hivyo, na kweli kafanikiwa....’akasema

‘Mhh, ...kwahiyo kesi ikaisha tu kihivyo...ina maana hata huko rushwa ipo?’akaulizwa

‘Hakuna sehemu kusipokuwa na rushwa, hata hivyo yangu haikuwa ni rushwa, ni kitu kipo moja kwa moja, walionishitakia walihitaji fidia kubwa ili esi hiyo ifutwe..., mimi nikawa sina na kiukweli sikupatikana moja kwa moja kama muuaji, basi tu , ni kutokana na tabia yangu, na jinsi nilivyokuwa nikichukua machafu ya watu na kuyatumia kuwatishia, wasiponipa pesa nawatangaza, nikaonekana mimi ni mchochezi, unaona hapo....’akasema

‘Hutaamini, ...nikaachiwa hivyo kuwa nirejeshwe nyumbani na mali yangu iuzwe madeni ya watu yalipwe, na nisionekane tena huko ulaya..na hiyo ikawa ndio salama yangu...na kwa muda huo nilikuwa naumwa kweli, hali yangu ilikuwa mbaya sana... waliniona kama mzigo tu wakaona bora nirejeshwe nchini kwangu....’akatulia

‘Ndio nikasaidiwa hivyo,na huyo wakili akafanya taratibu zote, nikarejeshwa nyumbani na mali zangu zikapigwa mnada,wakili akachukua kilich chake nyingine zikalipia madeni ya watu ....na ikawa mwisho wa maisha yangu , sasa sina kitu nipo nipo tu....’akasema

‘Pole sana..lakini vipi maisha ya kijana wako, maana sitaki hata kumuita kijana wangu, huyo ni kijana wako uliyemtengeneza wewe mwenyewe maana kaharibikia mikononi  mwako, hebu tuambie,unasema ameshaoa mwanamke, tena mwanamke  wa kizungu..., je maisha yake yapoje...na vipi anatarajia kurudi huku kwao tena..?’ akaulizwa

‘Mhh...maisha yake ni ya kawaida tu, kwa vile ana kazi, na aliyemuoa ni binti anayetoka kwenye familia ya kawaida tu,japo, haikuwa rahisi hivyo kumpata ...unajua huyo binti nilimfanyia mimi mipango,.. ..lakini yeye hilo halikumbuki, keshasahau...’akasema

 ‘Ulimfanyia  wewe mipango kwa vipi....?’ akaulizwa

NB, Tutaliona hilo sehemu ijayo.


WAZO LA LEO: Unapoamua kubeba majukumu, ujue kuwa mzigo huo ni wako, na utawajibika nao, na unatakiwa kuufikisha sehemu husika salama. Unapoamua kulea mtoto wa mwenzako ujue huyo ni mtoto wako umtendee vyema, kwa kumlea vyema, kama vile ambavyo ungelimtendea, au kumlea mtoto wako, na ujua akiharibika wewe ndiye mwenye kulaumiwa, kwani ilivyo kila mmoja atakuja kuulizwa kila kilichokuwa mikononi mwake, jinsi gani alivyowajibika nacho.
Ni mimi: emu-three

No comments :