Baada ya kama
miaka kumi na miwili hivi mingine wakati watu wameshaanza kusahau, na hata watu
wa usalama wakawa wamekata tamaa kufuatilia hiyo kesi, mara siku moja ikaja
taarifa kuwa Profesa karudi, na yupo kituo cha polisi, na karudi akiwa kasindikizwa
na watu wa usalama wa kimataifa...
Aliyepewa
taarifa hiyo alikuwa kaka mtu, akaambiwa ndugu yake yupo polisi anatakiwa
kwenda kumdhamini la sivyo ataishia jela
‘Mimi siwezi
kupoteza muda wangu na mtu kama huyo...’akasema kaka mtu akiwa kajichokea, na
mkewe akamwambia;
‘Usifanye
hivyo huyo ni ndugu yako, na huenda kaja na mtoto wako....’mkewe akamwambia
‘Na hata
kama kaja na huyo mtoto, mimi atanisaidia, ...?’ akauliza
‘Swala sio
la wewe kusaidiwa, lakini ni muhimu kama baba kwenda kujua ukweli, na ikibidi
utoe msaada...’akaambiwa
‘Mimi
nitatoa msaada gani, maisha yetu tunajua wenyewe, niharibu nauli yagu hadi
huko, haya nikifika huko nikatakiwa kudhamini, au kuna kitu cha kulipa
nitapatia wapi hizo pesa, ....’akasema akiwa hataki hata kusikiliza
‘Lakini
fanya juhudi, hata ikibid kuuza mbuzi, ..’akaambiwa
‘Hivi wewe
hujakutana na hao watu, eeh,..mfani haya nikienda huko, nikakutana na huyo
mtoto,na huyo mtoto akija kunikana mbele za watu nitasema nimekwenda kutafuta
nini, si kwenda kujisononesha na kujiletea magonjwa ya moyo kwa hasira, niache,
waache kama wapo jela, dunia iwafunze....’akasema
‘Lakini ujue
hapo labda yupo mtoto wako, na huyo ni ndugu yako ni muhimu uende tu ukajue ni
nini kinachoendelea, unafikiri ukiamua kuchukulia hasira dunia
itakuwaelewaje...mfano wazazi wako wangelikuwa hai ungelifanya hivyo, ujue huko
walipo wanakuona..na wewe ndiye kaka yao mkubwa ....’akaambiwa
Baada ya
ubishani wa muda, kaka mtu akakubali kufunga safari kwenda hadi kituo
alichoshikiliwa ndugu yake, alipofika, akakutana na wahusika ndipo akaanza
kupewa taarifa kamili.
‘Huyu ndugu
yako karudishwa kutoka huko alipokuwa anaishi....’akaambiwa
‘Najua
alikuwa huko Ulaya sio, kwanini sasa arudishwe yeye si alishaukana utaifa wake,
na huyo mtoto naye yupo wapi...?’ akauliza
‘Sisi
tumempokea ndugu yako kwa taarifa ndefu ya makosa yake, kwanza huko alipokuwa
akiishi kibali chake kilishaisha muda wake, akawa anaishi kwa kujiiba iba...hata
hivyo, pamoja na hayo, aligeuka kuwa tapeli, na muuza madawa yasiyokubalika...na
makosa meng mengi.....’akaambiwa
‘Nilijua tu
mwisho wake utakuwa huo, huwezi kuishi kwa maisha ya kuhadaa, sasa ikawaje..kwanini
mnamshikilia....hapa nchini aliondoka akiwa kaacha nyumba yake,...na pia
alikuwa na biashara zake, kwanini asiende kwenye nyumba yake, na biashara zake?’
akaulizwa
‘Huko
alipokuwa akiishi, ilifikia muda hana kazi, si unajua maisha ya huko, kuna
kulipia kodi ya serikali, pia kulipia pango alipokuwa amepanga, ...watu wakaja
kumgundua kuwa ni tapeli wa dawa zake..., na muda huo alikuwa na madeni mengi
ya watu, ...akashitakiwa, na kuswekwa, ndani, huku akitakiwa kulipa madeni ya
watu....’akaambiwa
‘Kifungo cha
utapeli kilipoisha, akatakiwa kulipa madeni ya watu, akawa hana pesa, kwahiyo
alitakiwa kuendelea kufungwa, ...lakini akawa ameahidi kuwa huku nyumbani ana
nyumba na miradi ambayo inaweza kulipa hilo deni....akadhaminiwa na watu
wanaomfahamu....’.
‘Basi ndio
akarejeshwa huku, akiwa kaambatana na watu wa usalama, na hao walimdhamini, na
wakaja huku kupiga mnada hiyo nyumba, na duka lake la dawa, ...kwahiyo amerudi
hapa akiwa hana mbele wala nyuma, ukizingatia kuwa huko katokea kifungoni kwa
makosa ya utapeli, na wizi wa hadaa....’
‘Sasa hivi haruhisiwi
kusafiri nchi yoyote, atakuwa hapa hapa nchini kwa kifungo cha nje...na
tulihitajia mtu wa kumdhamini, kama wewe ni kaka yake basi ubebe hilo jukumu...’akaambiwa
kaka mtu,na kama mtu kwanza alikataa, lakini alipoambiwa kama hakuna mdhamini
ndugu yake anakwenda kufungwa jela ya ndani, udugu ukamjia, akakumbuka kuwa
wazazi wake walimuachia majukumu ya kulea ndugu zake, akasema;
‘Na mtoto
aliyekuwa naye?’ akauliza
‘Hana cha
mtoto, tumemuuliza,anasema mtoto alimkana, na kwa vile mtoto alikuwa na cheti
cha kuonyesha kuwa yeye ni yatima, na ndivyo alivyoandikishwa huko, ikawa haina
nguvu,....sisi tumempokea yeye, mengine yatafuta baadaye, kama waliomshitakia
watafufua kesi iendelee haya....’akaambiwa
‘Kwahiyo
hata yeye kakanwa na mtoto, kuwa yeye sio baba yake, si mlisema alikuwa na
cheti cha kuonyesha kuwa yeye ni baba yake...?’ akauliza
‘Tulimuuliza,
lakini huko nje cheti hiko hakikutambulikana, hakuweza hata kukionyesha, na
hakutaka hata kukitoa, anasema vitu vyake vyote viliibiwa, kwahiyo hajui wapi
kilipo, hata hivyo, mtoto mwenyewe hamtambui....’akasema mtu wa usalama
‘Basi naomba
niongee naye kwanza kabla sijakubali hiyo dhamana, maana anaweza kunikana, ....’akasema
kaka mtu
‘Kwa hali
aliyo nayo hawezi kufaya hivyo, alishakutaja kuwa wewe ndiye ndugu unayeweza
kumsaidia,....sasa kama wewe utakataa, kubeba hiyo dhamana, sis hatuna jinsi
inabidi tukamfunge jela ya ndani...’akaambiwa
Basi kaka
mtu ikabidi akaongee na mdogo wake, na alimkuta mdogo wake kalazwa kwenye
kitanda cha wagonjwa, kwa hali aliyomkuta nayo, alivyoisha, kakonda, mgonjwa, na
kawa mzee hata kuliko yeye, akajikuta machozi yanamlenga lenga, ...na mdogo mtu
alipomuona kaka yake, akaishia kupiga magoti huku akilia
‘Kaka
nisamehe sana..najua nimewakosea, lakini nilichofanya wakati huo ilitakiwa kiwe
hivyo, nikiwa na nia ya kumsaidia mtoto, ..japokuwa pia niliona ndio nafasi
yangu ya kujipatia maisha mazuri...’akasema
‘Kwa kupitia
mtoto wa watu, utapeli na dhuluma au sio, ukamuharibu huyo mtoto, ili
asiwatambue wazazi wake....si ndio hivyo?’ akaulizwa
‘Mimi
sikumuharibu kihivyo, sikuwahi kumuambia asiwatambue wazazi wake, siku zote
nimekuwa nikimsihi kuwa mimi sio baba yake hasa, nilimwambia wazazi wake wapo,
ndio maana kipindi kile nilikuja naye, lakini hakukubali...’akatulia
‘Huko Ulaya aliandikishwa
kama yatima ili aweze kusoma, na nilifanya hivyo ili apate hiyo nafasi,....na
kiukweli nilijitahidi sana ili awatambue wazazi, wake..hasa tukiwa huku, lakini
mtoto mwenyewe ndiye alikataa,ningefanya nini, na mimi pia nilihitajia hiyo
misaada, ili maisha yaendelee..hilo nawathibitishia..kuna mengi mengi sana....’akasema
‘Lakini
chanzo cha kuharibika mtoto ni wewe, kama usingelifanya hayo yote haya yasingelitokea...ukajifanya
unajua zaidi, ukitaka kuchuma kwa kutumia migongo ya wenzenu...’akaambiwa
‘Ndio hivyo..hil
nakiri kuwa nimefanya kosa, naombeni mnisamehe..maana hapa naumwa, sijui mbele
wala nyuma, kila nilichokuwa nacho kimechukuliwa, na huko ulaya nadaiwa, hayo
madeni ni baadhi tu, kuna watu walishaapa kuwa wakiniona wataniua kwahayo
niliyowafanyia, najuta kabisa...na sizani kama nina muda mrefu wa
kuishi....nisamehe kaka yangu...’akasema
‘Leo
umefikia hivyo, kujiamini kote kumeishia hapa, siamini, wewe tulikuwa tukifika
kwako unatuona kama wachafu, watu wa kijijini, tusiojua maisha,...hahaha, kweli
ishi uone...sasa hali yetu unaifahamu mimi nitakusaidia nini...?’ akauliza kaka
mtu
‘Yaani hapa
nilipo, japo maisha nayatamani, lakini sina halii ni bora ya mfu, nimeshakuwa
zaidi ya masikini...kaka wewe ni dhamini tu nisiende jela, najua kabisa
nikienda huko sitaishi, nitakufa tu....’akawa analalamika
‘Hiyo ndio
adhabu ya mtu kama wewe, mali yote uliipata kwa ujanja ujanja, kuwatapeli watu,ukajiona
umesoma sana, unajua kila kitu sheria wewe, kila kitu wewe, sisi wazee wako
ukatuona hatuna maana ...na adhabu za watu kama nyie zinaanzia hapa hapa
duniani...sasa sijui kama utaweza kuishi maisha ya huko kwetu kijijini....’akaambiwa
‘Na ukumbuke
kuwa huko bado una kesi, unatafutwa kwa kuiba mtoto wa watu,, ukamtumia kwa
mambo yako...kule nilipokuwa nimeoa, wameahidi kuwa ukionekana tu kesi ipo pale
pale....umefanya mama wa watu hajitambui....’akaambiwa
‘Lakini mimi
sikumuiba huyo mtoto, nilimuokoa na ushahidi nilikuwa nao, ukienda kwenye
mtandao utaona...hilo ni kweli kabisa.., na kama wenyewe mnamuhitaji, huyo
mtoto muende huko alipo, mkamchukue, mimi kazi yangu ya kumsomesha,
ilishakwisha, kwanza sasa hivi sio mtoto
ataweza kujieleza mwenyewe, ...’akasema
‘Sasa
kwanini hukurudi naye...?’ akaulizwa
‘Aaah, mimi sitaki
hata kuonana naye tena, kaniharibia kila kitu, kanikana kuwa hanijui, wakati
mimi ndiye niliyemfikisha hapo alipo...’akalalamika
‘Ina maana
hata wewe amekukana...kuwa wewe sio baba yake, wewe si ulikuwa na cheti cha
kuzaliwa cha huyo mtoto...ukadai kuwa wewe ndiye baba yake halali....?’ kaka
mtu akamuuliza
‘Nimeshawaambia
vitu vyote niliibiwa, ..cheti cha kuzaliwa kilinisaidia hapa nchini tu, huko
ulaya hakikutakiwa kuonekana kabisa....na ilifika mahali sikuwa na cha
kujitetea, na ambaye angeniokoa kwenye hilo tatizo na huyo mtoto, lakini
akajifanya hanitambui, baada ya kuambiwa nina madeni mengi, na hasa alipotajiwa
kuwa nina kesi inayonikabili....’akasema
‘Ulikuwa na
kesi gani?’ akaulizwa
‘Aaah, kesi
ya ...tuyaache hayo, ilibidi nianza maisha hayo, sikuwa na ujanja ningeliishije
huko ulaya. Ujue kazi ya wafadhili kwa walishamaliza na ikafikia kijana ana
kazi yao, na kuweza kujimudu, nikawa sipati kitu tena...nilitegemea yeye
atanitetea, anisaidie lakini ndio hivyo...kanikana...kuna mambo ya ajabu sana
alinifanyia huko,sikuamini,....’akawa anaonyesha huzuni
‘Sasa huyo
mtoto yupo wapi, maana sasa sio mtoto tena si umesema ana kazi au sio ana kazi
gani sijui, ...au ndio kaandikishwa uraia wa huko nje...tunajua sasa sio mtoto
ana maisha yake, na hatutaki kumuingilia, keshakuwa mkubwa msomi au sio..lakini
sisi bado tunataka kujua yupo wapi na huko anafanya nini...na muhimu ni mama
yake ambaye hajiwezi, haachi kumtaja mtotowake hadi hii leo...?’ akaulizwa
‘Nitawaambia
kila kitu ili watu wajifunze, ..lakini kwanza kaka naomba unitoe humu, nikapate
dawa...kuna dawa zangu nikizipata najua tatizo hili litakwisha, na dawa hizo zipo
huko kijijini.....’akasema, na kaka mtu akacheka, kichwani alikuwa keshakata
tamaa, alijua huyo mtu anapeleka maiti, kwa hali aliyo nayo alijua hatamaliza
mwezi..
‘Kaka nina
mengi ya kuwahadithia ili watu wajifunze...maisha ya ulaya mmh, hapana...ni
bora huku kwetu kijijini...’akasema
‘Leo unaona
kijijini ni bora ehe....haya ukawahadithie wenzako huko kijijini, ili
wakuelewe...wenzako wanasema heri wakafungwe huko ulaya kuliko maisha
wanayoishi nayo sasa ...’akasema kaka mtu akigeuka kuondoka
‘Hawajui
tu....nitawasimulia ...kule hakuna ujanja, kama huna kazi, umekwisha, kama huna
kibali cha kuishi huko...kaka nitoe humu...tafdahali nipo kwenye miguu yako...’akawa
anaendelea kupiga magoti
NB: Tutaona
hayo kwenye sehemu ijayo
WAZO LA LEO: Mwisho wa dhuluma, ni fedheha tu,
mungu atakuachia utambe, ujione unacho, ujione wewe mjanja, ujione wewe umefika
...lakini muda utafika, utabakia kujuta, na majuto ni mjukuu huja baadaye,
ukiwa huna mbele wala nyuma. Acha dhuluma, tafuta riziki ya halali, hata kama
ni kwa shida, kwani riziki ya halali ina baraka.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment