Kaka wa
profesa alikuwa ndio keshafika mlangoni na muda huo kijana naye alikuwa
ameshaingia akiwa katokea kwenye masomo ya ziada, au kama ijulikanavyo `tuition’ na alipofika tu haraka haraka akawa
anaelekea kwenye jokofu, na ndipo wakakutana na baba na mtoto, na wote
wakasimama, wakiangaliana.
Baba
hakuamini jinsi mtoto wake alivyovaa, na masikioni kaweka vitufe vya
kusikilizia mziki, kutoka kwenye simu, na jinsi alivyovaa huwezi kufikiria ni mwanafunzi,...
‘Ni nini
hiki....’akasema baba mtu, na kijana akatoa zile waya masikioni akamwangalia
huyo mtu aliyesimama mbele yake, kwa muda ule kwanza hakufahamu ni nani, ndipo akauliza
‘Who are you....?’ akauliza japo sasa
alishamkumbuka
‘Hiyo ndio
salamu yako kijana kwa baba yako,...hiyo ndio adabu uliyofundishwa na baba yako
mdogo, au ndiye amekuharibu kiasi hiki..., hebu angalia ulivyovaa, ni kama
muhuni gani sijui,....hivi kweli huyu ni mwanafunzi au ni mtu gani, wewe bwana
mdogo ni nini kavaa huyu mtoto,...?’ akauliza kaka mtu
‘Bro....huo
ni utandawazi bro, ni wakati wa huo..., sasa hivi wapo likizo, sio lazima kuvaa
sare za shule, wanajifurahisha vijana,...’ilikuwa sauti ya profesa akija,
akijua asipofika hap kunaweza kutokea sintofahamu.
‘Sasa ndio
hata salamu hakuna wakiwa likizo hawasalimii, ndivyo walivyofundishwa huk
shuleni kwao...?’ akauliza
‘Wewe
kijana,...hamfundishwi kusalamia wakubwa....?’ akauliza
‘How are you
sir....?’ akasema
‘Sema
shikamoo baba...hawayuu, hawayuu..wewe ni mtanzania unatakiwa usalimie kwa
lugha yako yenye kuonyesha adabu....’akasema na kijana akasimama akiwa anataka
kupita.
‘Hutaki
kusalamia sio, nikufundishe kusalamia.....?’ akamuuliza
‘But,
nimeshakusalamia, unataka zaidi...’akasema kijana
‘Mimi ni
nani kwako?’ akauliza
‘Sijui....sikujui....’akasema
‘Hujaambiwa
kuwa mimi ni baba yako...?’ akaulizwa
‘Kiukweli,
...hata kama nimeambiwa, lakini huwezi kunilazimisha kuwa wewe ni baba
yangu...mimi hadi nimefikia umri huu, najua kuwa mimi ni mtoto yatima, sina
baba wala mama...’akasema
‘Lakini sasa
umeshaambiwa kuwa una baba na mama yako, na mimi ndio baba yako,..’akasema
‘Siwezi kuwa
na baba kama wewe...’akasema
‘Eti
nini....?’ akauliza kwa hasira, na kijana akageuka kutaka kuondoka, na baba
yake akawa anamjia kutaka kumshika
‘Dad, is this man again, I told you before...’akaanza
kuongea kijana sasa akimpita baba yake akielekea kule aliposimama profesa bila
kujali..., lakini hakuweza kumpita baba yake, baba yake akamdaka na kumshika
mkono.
‘Wewe mtoto,
ujue mimi ni baba yako, na kama hujafundishwa adabu leo mimi nitakufundisha
adabu, ...’akasema sasa akimvuta tayari kumzaba kibao, na isingelikuwa profesa
kuja kuwahi kuwatengenisha, kijana angelishaonja kibao kipigo.
‘What....unataka
kunipigia nini,.... I am not your son, sikutaki...sikujui,...wewe sio mzazi
wangu, kwanini unanifuatilia maisha
yangu....’kijana akasema sasa akiwa huru pembeni kwa profesa.
‘Mimi sio
mzazi wako,...? ‘akauliza jamaa kwa hasira sasa akimfuata kijana kutaka
kumshika, na kijana akakimbia
‘Bro,
kwanini unataka kulazimisha mambo, nimeshakuambia huyu kijana bado hajaelewa,
ndio ni mkubwa, miaka kumi na sita ni miezi kadhaa, lakini kwa vile hakuwahi
kuishi na nyie, bado hajawaelewa, na ....ni kutokana na ile hali ya kusoma na
kuambiwa kuwa yeye ni mtoto yatima....’akasema profesa
‘Sasa hilo
ni kosa la nani...wewe ndiye umefanya haya yote, ...kwahiyo lawama zote
zitakuendea wewe...na ole wako, ....nakuambia hii sio mara yangu ya mwisho kuja
hapa, nikija safari nyingine namchukua huyo kijana, sitaki aende popote, nataka
nikaishi naye kijijini, unanielewa, nikitoka hapa kurudi kijijini nitahakikisha
shera zote zinafuatwa,..sitaki nije kueleweka vibaya...’akasema kaka mtu.
‘Aaaah kaka,
tulishaongea hilo, kwanini utake kuharibu,....unataka kuniharibia na mimi, huyu
ana wafadhili, na kila mwezi kuna pesa tunapata kwa ajili ya kumlea, kwa vile
ni yatima, hana baba wala mama, ukifanya hivyo misaada yote itakatika, na
huenda nikaingia matatani....’akasema.
‘Ohooo,
kumbeee,ndio maana, ina maana utajiri wote huo unapata kwa kupitia mgongo wa
mwanangu, unapata mipesa, na sisi wazazi wake hatujui,....sasa hilo
nitahakikisha nimelikomesha...mimi naondoka, na nikirudi tena hapa nakuja na
watu wa usalama, waliokuwa wakimtafuta...’akasema.
‘Kaka ukija
kufanya hivyo, udugu utakufa,.....nikuambie ukweli, unajua jinsi gani
nilivyohangaika a huyu mtoto, ndio shukurani yenu hiyo....nenda kashitaki, na
hapo hutampata tena huyu mtoto...’akasema na kaka mtu akageuka akamuangalia kwa
makini halafu akasema.
‘Kama mimi
sio kaka yako tutaona, si unataka kushindana na mimi, kwa vile unajiona
umesoma, kumbe kusoma kwenyewe ni kwa utapeli, wizi na ulaghai,...sasaa wewe
utaishia kifungoni...sijali cha udugu...’akasema na kuondoka.
*********
‘Kwanini
umefanya hivyo...?’ profesa alimuendea kijana akiwa kajiinamia pale alipokaa
kitandani kwake.
‘I told you
before dad, mimi simtaki huyo mtu...unaona alivyotaka kunipiga, kama ingelikuwa
ulaya ningemshitaki....na kesho nakwenda polisi kumshitaki, ...’akasema
‘Sikiliza
hapa sio sawa na ulaya, ..hapa kuna utaartibu wake, ..mtoto anatakiwa kumtii
baba yake na baba ana weza kukuchapa ukikosea,...na alichotaka kukuelekeza ni
kuwa wewe umuheshimu kama baba yake, ...’akasema profesa
‘Lakini yeye
sio baba yangu...’akasema kijana
‘Sasa baba
yako ni nani...?’ akauliza profesa
‘Baba yangu
ni nani, kila kitu kipo kwenye maandishi mimi ni mtoto yatima, sina baba wala
mama, ...’akasema
‘Tulishaongea
hilo , kwanini hutaki kunielewa, tatiz lako umerithi ubishi wa baba yako, yeye
akiamua kitu hataki kurudi nyuma,..sasa sikiliza, kwa hali inavyokwenda, mimi
naweza kukamatwa kwa kosa la kukuchukua kutoka kwa wazazi wako...na sitaki hilo
litokee...’akasema
‘Kukamatwa
kwa kosa gani....?’akauliza
‘Hukusikia
yule kaka yangua alivyosema anakwenda kuchukua polisi, na polisi wakiambiwa
kila kitu kitaharibika, ...kwahiyo sasa tujiandae, hapa tunaondoka,...nataka
ikiwezekana kesh tuwe safarini, tutapitia Kenya,...kule Kenya nina jamaa yangu,
...na tukitoka huko unarudi shuleni kwako...’akasema
‘That’s is a
god news dad, ..ndio maana nakupeda Dad, wewe ndiye baba yangu, ...hao sijui baba,
sijui mama, ...halafu yule mama,...mmh,sitaki kabisa kuwa naye karibu, anaumwa
nini....?’ akaulizwa
‘Yule ni
mama yako, chunga ulimi wako...utakuja haribikiwa,....nilishakuambia chezea
baba yako, lakini usije kuchezea mama yako,....utaiona dunia ngumu....’akasema
‘I don’t
care...unasikia dad, mimi ni yatima, simjui baba au mama....kama wewe wawataka
sawa, lakini mimi msimamo wangu ndio huo..siwezi kabisa kuishi na mama kama
yule,...’akasema na profesa akatulia kwa
muda, akiwaza kichwani alikuwa hataki hiyo kauli ya huyo mtoto, lakini
alishindwa asema nini kwa muda huo.
*******
Siku ya pili
yake, alihakikisha kijana ametangulia kuondoka, akiwa kaongozana na jamaa yake
anayefahamiana naye wakiekea Kenya kama walivyopanga, yeye alibakia nyuma akihakikisha
shughuli zake zipo salama, na wakati anataka kuondoka mara gari la watu wa
usalama likasimama nje ya nyumba yake...
‘Niwasaidie
nini....?’ akauliza akiwa keshajipanga kuongea nao, hakuonyesha wasiwasi.
‘Sisi ni
watu wa usalama,....’wakaonyesha vitambulisho vyao,
‘Tumekuja
hapa kwako.., kuna malalamiko kuwa wewe unaishi na mtoto ambaye sio mtoto
wako....’akaambiwa
‘Ni nani
kawaambia hivyo?’ akauliza akijifanya kushangaa, anajua jinsi gani ya kuigiza
kihali hiyo.
‘Ni mama wa
huyo mtoto...’akaambiwa
‘Mama wa
huyo mtoto, ina maana ni mke wangu, mlionana naye wapi, maana mke wangu
tuliachana naye muda sasa...imekuwaje amuache mume wake aje kudai tena huyu
mtoto, niwaulize kitu, yeye huyo mke wangu ana uhakika gani kuwa huyo mtoto anayemdai
ni mtoto wake....?’ akauliza
‘Yeye sio
mke wako bwana....ila yeye ni mama wa huy mtoto, kwahiyo kama ni maam wa huyo
mtoto, atakuwa na uhakika huo, kwa vile yeye ndiye aliyemzaa huyo mtoto...’wakasema
‘Ndugu
zanguni, nyie ni watu wa usalama...si ndio, mimi hapa nilikuwa naishi na kijana
wangu, mtoto wangu niliyezaa na mke ambaye tuliishi naye tu, hatukuwahi kufunga
ndoa, ..na ikawa bahati mbaya, akaolewa, na tulikaa tukakubaliana kuwa mtoto
huyo nimlee mwenyewe, huo ndio ukweli wenyewe....’akasema
‘Sasa kama
ni yeye kanigauka tena, akaja kwenu kudai huyo mtoto, basi kamwambieni aje
tuongee, ...’akasema
‘Tumekuambia
kuwa huyo anayedai mtoto sio mke wako, ni mama mwingine tu, naye alikuwa na
mume wakaachana,....’akasema
‘Ohooo,
umenikumbusha kitu, siku moja, nilikutana na mama mmoja anaumwa hivi, unajua
lile tatizo la kifafa, linaweza kumharibu mtu akili,.....mimi ni profesa, na ni
mtaalamu sana wa matatizo hayo...sasa nilikwenda kumtibia huyo mama, nikiwa na
huyo kijana wangu, huyo mama sijui kwanini, ...mara akaonyesha dalili za kusema
huyo mtoto wangu ni mtoto wake...niliona ajabu kabisa, hata mtoto wangu
akaogopa na kukimbia...’akasema
‘Hayo yote
tumeambiwa,....lakini huyo mama anadai kuwa huyo mtoto ni wa kwake.....kwahiyo
tulikuwa tunahitajia tumuone huyo mtoto...’akasema
‘Nyie ni
watu wa usalama, najua mnatimiza wajibu wenu siwakatazi,..ila huyo mama
anashuku tu,...hivi huyo mama ana akili nzuri, mumemchunguza vyema...hebu
wekeni akili, mtu aje akute mtu ana mtoto wake, halafu aanza kudai kuwa ni
mtoto wake....mbona haiji akilini...je mumefanya utafiti gai hadi mkaona kuwa
hayo madai ya huyo mama yana ukweli?’ akauliza
‘Kwanini
unasema hivyo?’ akaulizwa
‘Mliwahi
kumuuliza huyo mtoto anayemdai alikuwa wapi...ana umri gani, maana kijana
aliyenikuta naye ni kijana wangu mkubwa tu....’akasema
‘Yupo wapi
huyo kijana....tunataka tumuone?’ akauliza huyo askari
‘Kijana
wangu kesharudi shuleni...shule zimeshafunguliwa, kwahiyo nimempeleka mtoto
wangu shuleni....’akasema
‘Kwahiyo ni
mtoto wako..?’ akauliza askari sasa akiwa anakagua kwa macho hiyo nyumba na
vilivyomo humo ndani
‘Ndio hivyo
waheshimiwa,...nashangaa mnakuja kudai kuwa ninaishi na mtoto asiye wa mtoto wangu,
nimewauliza je mliwahi kufanya uchunguzi gani, au mnakuja kuvamia nyumba za
watu tu,hebu fuateni utaratibu wa kazi zenu...’akasema
‘Una
ushahidi gani kuwa huyo mtoto unayeishi nawe ni mtoto wako....?’ akaulizwa
‘Hahaha....hivi
nyie niwaulize na huyo mama ana ushahidi gani kuwa huyo mtoto anayedai kuwa ni mtotowake
ni mtoto wake kweli, anao ushahidi wowote....?’ akauliza
‘Tusitake
kusumbuana, ...sisi ni askari polisi, na huyo mama miaka kumi sita iliyopita
alipotelewa na mtoto wake, kuna kumbukumbu za hayo madai,.....kwahiyo
alivyomuona huyo mtoto akamtambua....’akasema
‘Miaka kumi
na sita nyuma..leo hii mnakuja kudai mtoto..huyo mama hebu mkamchunguze
vyema,...mimi nahisi ana matatizo ya akili...kama ni yule niliyemtibia, nahisi
yale matatiz yamemletea athari akilini, lakini zile dawa nilizompa zitamsaidia
sana...yupo wapi huyo mama...?’ akasema na kuuliza
‘Wewe ndio
unasema hivyo, lakini sisi tunajua huyo mama ana akili sawasawa,...usitake
kugeuza geuza maneno.’akasema huyo askari mwingine aliyeonyesha kuwa na uhakika
lakini mwenzake alionekana ameshakurizika kuwa huyo mtoto sio wa huyo mama.
‘Sasa
tusipotezeane muda, mimi nina ushahidi kuwa huyo ni mtoto wangu, nataka na nyie
mnipe huo ushahid kuwa huyo ni mtoto wa huyo mama....’akasema akifungua mkoba
wake na kutoa cheti cha kuzaliwa
Polisi
wakaangaliana, na mmojawapo akataka kukiona hicho cheti, na profesa,akasema;
‘Aaah,
...nionyesheni na nyie ushahidi wenu, vinginevyo hili swala tutalifikisha
mahakamani, kwani mnanivunjia heshima yangu..maana nyie badala ya kufanya kazi
zenu kwa sahihi, mnaingilia nyumba za watu na kuleta madai yasiyosahihi,..huko
ni kukiuka haki za raia,.....’akasema,
‘Tunataka
tuone huo ushahidi wako,.....’akasema yule askari na profesa akaona isiwe
shida, akachukua kile cheti cha kuzaliwa cha mtoto akamkabidhi huyo askari, na
yule askari akakifungua na kuanza kukisoma....
*********
Siku
iliyofuata waliokuja hapo nyumbani kwa profesa ni kaka mtu, akiwa kaongozana na wale watu wa usalama, na
walipofika wakitarajia kuwa watamkuta, lakini walipofika waliambiwa profesa hayupo
‘Hayupo
kaenda wapi ?’ akauliza kaka mtu kwa hasira
‘Amesafiri
...’akaambiwa,
‘Kasafiri kwenda
wapi, na mtoto je , kwanini hajaniaga, siku zote akisafiri huwa ananiaga,...ananipigia
simu kuwa anasafari ?’ akauliza akionyesha kutokuamini
‘Kwakweli
sisi hatujui,..yeye jana aliondoka na ndege ya usiku, kwenda ulaya..na mtoto
aliondoka mapema tu kurudi shuleni huko alipokuwa akisoma.....’akaambiwa
‘Haiwezekani..huyu
bwana mdogo anataka kunipanda kichwa,..kwaninis asioe akazaa mtoto wake
mwenyewe, kwanini anataka kuharibu watoto wa wenzake...’akasema kaka mtu kwa
hasira
‘Ina maana huyo
mdogo wako hana mke?’ akauliza mtu wa usalama
‘Hana mke
yule, ...hajawahi kuoa, na ataishi na mke yule....mtu hajatulia, tulimshauri
siku nyingi aoe, lakini anasema wake yupo, na ni huyo huyo...mara akasema huyo
mchumba wake kaolewa, na kama kaolewa, yeye hataoa tena....ni muhuni fulani
hivi....’akasema kaka mtu kwa hasira
‘Lakini
katuonyesha cheti halali cha kuzaliwa cha mtoto, inaonyesha kweli yeye ni baba
wa huyo mtoto kisheria...na alisema alikuwa na mwanamke aliyezaa naye huyo
mtoto, japokuwa hawakuwahi kufunga naye ndoa...’akasema huyo mtu wa usalama
‘Mhh,....muongo,
ndio zake hizo, anaweza akatunga uwongo, mpaka wote mkaamini,.... huyu mdogo
wangu ananitafuta ubaya...bora ningekiona hicho cheti,na nikaonana na yeye
mwenyewe,mbona hakuwahi kunionyesha hichoo cheti,...kitakuwa ni cheti ni cha
bandia ili kufanikisha mambo yake...lakini yeye sio kweli kuwa ni baba wa huyo
mtoto, ..’akasema
‘Kwanini
afanye hivyo....?’ akauliza mtu wa usalama, hapo kaka mtu hakuwa tayari kuongea
kila kitu, akasema;
‘Sijui, yule
ndivyo maisha yale yalivyo, kujifanya mjanja mjanja, kamuharibu hata mtoto
wangu,...ila ninachowaambia yule mtoto
ni mtoto wangu nilizaa na mke niliyeachana naye....na angekuwepo hapa angesema
ukweli wote, lakini kwa vile kuna mambo yake anataka yafanikiwe kwanza ndio
maana akawaambia hivyo....’akasema
‘Sawa lakini
kisheria anaweza kuwashinda, je nyie mnacho cheti cha huyo mtoto cha kuzaliwa
kinachoonyesha kuwa nyie ni wazazi wake halali, ...?’ akauliza huyo mtu wa
usalama
‘Cheti ..cha
nini...sawa, kwa ajili ya mtoto sio, ...unajua huyo mtoto alikuwa mikononi mwa
mama yake,...sasa huko kwa mama yake, sina uhakika kama walifuatilia hicho
cheti,.., labda nikifuatilie mimi mwenyewe,...hata hivyo, unajua mimi kama baba
yake, sihitaji kuthibitisha hilo,...kwanini nithibitishe, wakati kweli nafahamu
kuwa mimi ni baba yake halali...’akasema
‘Lakini kama
mtoto keshasema yule ni baba yake, na huyo baba yake ana cheti cha kuthibitisha
hilo, mtakuwa hamna haki ya kumdai kuwa ni mtoto huyo ni wa kwenu....’akasema
mtu wa sheria
‘Huyu mtoto
kajazwa ujinga na huyo mdogo wangu, ...yeye bado mdogo, ...siwezi kumlaumu
sana, ila kama ataendelea hivyo, wakati keshaujua ukweli, akaja kunikataa,
oooh,...sijui...unajua mzazi ni mzazi tu,..hata aweje ukimkataa, oh, sijui,
dunia itamfunzam na mwenyewe atakuja kunitafuta, kama bado nipo hai...akisubiria
nikifa atapata shida....’akasema
‘Mhh, hapo
mwenzenu kawazidi ujanja...na kweli kuna anachokitafuta sio bure tu...huwezi
kung’ang’ania mtoto wa mtu hivi hivi...na kwa vile anasoma huko ulaya, basi
atarudi....ila ni nani anamdhamini kusomea huko, ni huyo baba yake mdogo ndiye
anayemlipia gharama, au...?.’akauliza mtu wa usalama
‘Unasema
kanizid ujanja, hahaha, ujanja gani huo,
damu ya mtu hata siku moja haiibiwi bwana,..sema tatizo ni kuwa anamuharibia
mtoto maisha yake, ....na sijui ni nani anaye mlipia hizo gharama, ...’akasema
kaka mtu akijaribu kuficha ukweli.
‘Na....vipi
huyo mama yake, maana hali yake kwa sasa sio nzuri, anataka ampate mtoto wake,
...na anasema ni njama zetu watu wa familia yenu, mlimuiba mtoto ni kweli mlifaya
hivyo?’ akaulizwa
‘Mimi
nigefaya hivyo ningehangaika hivi....huyu bwana mdogo, sijui alimpataje.. wale
wananinyoshea kidole bure, najua ni kwasababu ya yaliyopita, kuwa
tumeachaa...lakini hayo yalishapita, ....’akasema
‘Ulimuacha
eti kwa vile alikuwa anaumwa, ana matatizo kama hayo ya kudondoka dondoka...?’
akauliza mtu wa usalama
‘Hayo
yalishapita....., na ni kati yangu mimi na yeye, hayana mahusiano na mtoto,...na
mimi ninawalaumu sana wao..., kwanini hawakuwa makini na kumlea huyo mtoto,
alifikaje kwa huyu bwana mdogo,...wao ndio wa kulaumiwa, sio mimi kumuacha
yeye..., na kama kweli wangelikuwa makini na ulezi kwanini mtoto anawakana,
mtoto hataki hata kumuona mama yake..kwanini ....’akawa kama kauliza
‘Nasikia huyo
mama alidondoka na kupoteza fahamu, alipoambiwa huyo mtoto hamtambui yeye kama
mama yake,...mmmh,huyo kijana hajui kiasi gani anavyomuumiza huyo mama...lakini
je ni kosa lake...na kwanini ilifikia hapo, nahisi kuna tatizo....na wewe
ulikuwa unawasiliana na huyo mtoto?’akauliza huyo mtu wa usalama.
‘Kuwasiliana
kwa vipi...? Usiniuliza swali la ujanja ujanja, la kunitega...nimeshakuambia
mimi sijui huyu bwana mdogo alimpataje huyu mtoto, nilikuja kugundua siku za
hivi karibuni, ndio nikaja kuongea na nyie,...na..na nikaona kwa vile hili
swala lilikuwa mikononi mwa sheria, basi ngoja niwaone nyie ...sikujali kuwa
huyo ni ndugu yangu,...si mnajua mimi ni mjumbe, najua sheria, ...ndio
nikawaambia....’akasema
‘Basi hilo
tuachieni, tutapambana na huyu mtu, huyu
ni tapeli tutana mwisho wake ni wapi,...na mtoto mwenyewe atafikia umri wa
kujua baya na zuri, sasa hivi hatuwezi kumlaumu sana huyo mtoto na nyie kama
wazazi mnatakiwa kutumia hekima, mbaya ni huyo mdogo wako,...’akasema mtu wa
usalama.
‘Sawa hata
huyo mtoto akifikia umri wa kujua ukweli na bado akaendelea kuleta hiyo tabia,
akaendelea kuwakana wazazi wake,...ataiona dunia chungu..mimi si nipo hapa,
mtakuja kuniambia, ..’akasema
‘Usiseme
hivyo mzazi.....’akasema mtu wa usalama
‘Aaaah, mimi
sina tatizo, maana nina watoto wengine, tatizo ni kwa huyo mama yake...si
mumeona hali aliyo nayo...’akasema na kutikisha kichwa akionyesha huzuni.
‘Ila sisi
sasa tutapambana na na huyo anayejifanya ni profesa wa ulaghai, wenzake
wanaumiza vichwa madarasani kuupata huo uprofesa, yeye wa kwake anaupatia
mitaani kwa kulaghai watu, watu kama hao wapo mpaka maofisini, wenzao wameumiza
vichwa kusomea fani fulani, wao wanatumia ujanja kujifanya wanajua...’akasema
jamaa mwingine aliyekuwepo
‘Hata
maofisini pia,..mmh, mimi huko sijui maana sijawahi kuajiriwa,...lakini ni
ujinga tu..kwanini wasitafute chao, kama ni kusoma , wakasomee hiyo fani, ni
ujinga na sio ujanja..hata kama atapata utajiri, lakini utajiri huo utakuwa
unanuka dhuluma....’akasema
‘Ok tutaona
nani zaidi, uprofesa wake wa ulaghai au sheria...tutampata tu...’akasema mtu wa
usalama, huku akiandika kumbukumbu kwenye makabrasha yao..
Profesa
akawa keshaondoka nchini, na hakuonekana mpaka miaka kumi na kitu mingine,...na
alirejea akiwa mikononi mwa polisi, akiwa na hali mbaya kweli, kakonda, yupo kama mgonjwa, na isitoshe zaidi alikuwa anadaiwa, na alipofika tu nyumba yake ikapigwa mnada kulipia madeni,...
‘Kwanini...?’
tukauliza tulipoona msimuliaji akitulia,..
WAZO LA LEO: Binadamu huwa tunakosea, na wengi
tunafahamu kuwa tumekosea, tumemkosea huyu na yule kwasababu hii na ile, ubora
wa imani thabiti, ni kutubu, na kukirini moyoni kuwa nimekosa, na muhimu
kumuendea yule uliyemkosea na kumuomba msamaha, au kumrejeshea kile ulichomdhulumu,
hapo utafanikiwa kuwa na imani thabiti, katika maisha yako ya hapa duniani na
kesho ahera. Tutubu toba ya kweli, kwani mwezi mtukufu, mwezi wa toba, na
kusamehewa umeshafika, RAMADHANI KAREEM.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment