‘Mimi niliwahi kusoma,
enzi hizo,...usinione hivi, nikafika hadi
nje, watu wakiniona natangaza madawa ya kienyeji basi wanafikiria mimi ni
mwenzao,.. na hilo ndilo lililonifanya niwe karibu sana na huyu kijana, namuita
kijana msomi mwenye mazarau,alifikia hata kunizarau hata mimi, nikamwambia wee,
wee ...kumbuka ulipotoka...lakini bwana sikio la kufa halisikii dawa...’akasema
‘Kwahiyo wewe ni mtoto
wake kivipi?’ akaulizwa
‘Huyu ...chizi, eeeh ni
mtoto wangu, baba yake na baba yangu wamezaliwa tumbo moja, ...unasikia
japokuwa kulitokea namna yao, wakaachana, lakini ni damu yetu .....’akaanza
kutuelezea.
‘Huyu ni mtoto pekee
kwa mama yake, mama yake alichika mapema tu, na kipindi hicho alikuwa na
ujazito wa huyu kijana,...unasikia sana...sasa hebu tulieni, nahisi mnata kujua
hasa ilianzaanzaje ili msije mkapoteza muda wenu bure.....’akatulia, halafu
ndio akaanza kuhadithia kisa hicho kwa marefu akiturudisha miaka 32
iliyopita...
*****
‘Huyu si mama Totoo...?’
mama mmoja akiwa na mwenzake akasema na mwezake akasema
‘Ndio yeye, jamani kadondekea
mtoni, hebu njoo tumsaidie kumtoa ...’akasema huyo mama akitangulia bondoni
kwenye eneo wanapochotea maji,...na mwenzake kwanza alisita, akiogopa kuwa
huenda huyo mama ni maiti, lakini alipoona mwenzake akielekea hapo alipolala
huyo mama bila kuogopa na yeye akamfuata nyuma, na wote wawili walipofika hapo
mtoni, wakaaza kazi ya kumtoa huyo mama hapo
mtoni na bahati nzuri sehemu ya kichwa ilikuwa nje ya maji japo ilikuwa ni kwenye
matope.
‘Mhh, bado
anahema,....jamani huu ugojwa sio wa kumuachia mwenyewe, kwanini wanafanya hivi
hawa watu...bahati hakuyanywa maji, maana angekuwa maiti....’ akasema huyo mama
‘Lakini ni bahati mbaya
tu, kwani walijua itamtokea....., maana hiyo hali haitokei mara kwa mara, wakati wote, mbona anaweza hata
kukaa miezi bila kusikia tukio kama hili....’akasema mama mwenzake.
‘Mhh, lakini ni hatari,
halafu hebu angalia, mbona yaonekana
kama alikuwa kabeba kitu nyuma huoni hii hicho kitenge aliyojifunga nyuma,
hakuwa amebeba kitu kama mtoto....’akasema mwenzake
‘Mtoto ! Haiwezekani,
kama angelikuwa kabeba mtoto tungelimuona, ...na hiki kisima nilisikia wakisema
kina chatu na mamba, mungu wangu, kama alibeba mtoto mmmh,..... hebu tutoe
taarifa nyumbani kwao haraka...’wakasema na mmoja akabakia na mgonjwa, huku
mwingine akipanda juu huku akipiga yowe la kuomba msaada.
Kwanza akafika mzee
mmoja, na kabla hajamchunguza huyo mama, ambaye wakati huo alikuwa akibabaika,
hajajijua vyema na mara ndugu wa huyo mama wakafika, na wakati huo huyo mama
akawa sasa keshazindukana, na akawa anaulizia,;
‘Mtoto wangu yupo
wapi...mtoto wangu yupo wapi jamani....?’ akawa anauliza akijishika huku na
kule
‘Ulikuja mtoni na
mtoto...?’ akauliza yule mama aliyemsaidia
‘Jamani mtoto wangu
yupo wapi...nani kamchukua mtoto wangu?’ akauliza na ndugu sasa wakawa
wanaangalia huku na kule kama kuna dalili yoyote ya mtoto.
‘Tulikuambia ukija
mtoni usije na mtoto, sasa unaona.....mtoto yupo wapi...?’alikuwa mama yake
‘Huu sio muda wa
kulaumiana, cha muhimu ni kutafuta mtoto yupo wapi....’akasema baba mtu, na
watu wakaitwa na kuanza msako, lakini hakukuwa na dalili ya mtoto.
‘Tatizo mto huu una
mamba na kenge na chatu..., lakini hapa hakuna dalili ya kuonyesha mtoto
kachukuliwa na hao wadudu wabaya..., tungeliona damu au alama yoyote...’akasema
mzee mmoja anayefahamu sana tabia za hao wanyama
‘Sasa mtoto atauwa kaenda
wapi...au alipoona mama yake kapoteza fahamu alianza kutembea ovyo...?’ ndugu
wakaulizana bila jibu. Baadaye, taarifa zikafika kwa vyombo vya usalama, lakini
hakukuonekana cha mtoto wala dalili ya mtoto.
Mama wa mtoto akawa
analia, hakubali kuondoka eneo hilo la tukio, akasema hawezi kuondoka hapo
mpaka mtoto wake apatikane, na baadaye watu wa usalama wakafika na kuanza
kumhoji huyo mama;
Kwani ulipojisikia
vibaya mtoto alikuwa wapi...?’ akauliza
‘Nilimbeba mgongoni na
kitenge, sikutaka kumuachia ...’akasema mama yake
‘Ehe, hebu tueleze
ikawaje, ...’akaambiwa
‘Mimi nilifika kuchota
maji, mara nikasikia kitu kama mchakato, nikawa naogopa, nikajua ni wanyama
wabaya...nikatulia hadi mchakato huo ukaisha nikachota maji, mara nikaanza
kuhisi vibaya, nikaanza kuvutwa kama inavyotokea, na sikukumbuka kitu hadi
nilipozindukana na kumuona huyu mama akiwa pembeni yangu...’akasema
‘Ulianzaje kujisikia
vibaya...?’ akaulizwa
‘Mhh, ni .....nahisi
kama harufu, ...sia uhakika, nilichokumbuka ni kuwa nilianza kutikisika, na
mwili ukawa unavutwa.....pumzi ikaniishia na....’akatulia, na yule mtu wa
usalama akamgeukia huyo mama aliyeambiwa alikuwepo wakati huyo mgonjwa
alipozidukana.
‘Mhh na wewe mama
ulimkutaje huyu mama....?’ akaulizwa huyo mama na yeye akaelezea ilivyotokea na
huyo mama aliyekuwa naye akatoa ushahidi kuwa walikuwa wanapita ndio wakamuona
huyo mama akiwa kalala kwenye tope nusu ya mwili ukiwa majini, lakini kichwa
kilikuwa nje ya maji, wakasaidiana na kumtoa nje
‘Je wakati mnamtoa mliona
nini mwilini kwake...?’ akauliza mtu wa usalama
‘Tuliona hicho kitenge
kikionekana kuwa alikuwa kabeba kitu mgongoni, ndio tukahisi alikuwa kabeba
kitu, lakini sisi hatukuwa na mawazo ya mtoto, maana tujuavyo familia yake
isingelikubalii huyu mama aje huku kisimani na mtoto wakijua kuwa ana
matatizo..’akasema huyo mama.
‘Ana matatizo!,
matatizo gani?’ akaulizwa na huyo mama akawageukia wazazi wa huyo mama mgonjwa,
ili wao wajielezee, lakini kabla hawajasema kitu huyo mama mgonjwa akaaza kulia
tena akisema;
‘Mtoto wangu
jamani....nirudishieni mtoto wangu...’akasema huyo mama
‘Unahisi ni nani
anaweza kumchukua mtoto wako?’ akaulizwa huyo mama
‘Mimi sijui jamani,...na
kwanini wamchukue mtoto wangu,nimewakosea nini...hivi hawanionei huruma, pamoja
na mitihani huu wa ugonjwa, nimeachika kwasababu ya huu ugonjwa, mungu
kanijalia mtoto bado tu binadamu hawanitaki, basi na mimi waniue...’akawa
analalamika.
‘Hebu tuambieni mume wa
huyu mama yupo wapi?’ mtu wa usalama akamgeukia mzazi wa huyo mama na kumuuliza
maswali
‘Aliachika...’akasema
baba mtu
‘Kwanini aliachika,
waligombana au kulikuwa na tatizo gani...?’ akaulizwa
‘Ni kutokana na
matatizo aliyokuwa nayo mwanangu,...’akasema mama wa binti
‘Matatizo gani?’
akaulizwa
‘Ana tatizo la
kudondoka, dondoka, na kupoteza fahamu...’akasema mama akioyesha kusita
‘Ana tatizo la
kifafa...’akaongezea baba wa mtoto alipoona mkewe anasita kufafanua
‘Ina maana wakati
aanolewa haikujulikana kuwa ana tatizo hilo?’ akauliza mtu mwingine
‘Mwanangu hakuwa na
tatizo hilo kabisa, tatizo hilo limetokea huko huko kwa mwanaume, wamampachika
mtoto wangu gonjwa, halafu wakampa talaka, ...’akasema mama wa binti
‘Kwahiyo aliachika
akiwa na mimba...?’ akaulizwa
‘Wakati wanamuacha
hawakujua kuwa ana mimba, mimba hii tumeigundua wakati tupo naye, ...’akasema
mama
‘Je baba yake anafahamu
kuwa mtaliki wake ana mtoto...?’ akauliza
‘Ndio waafahamu, ,...kumekuwa
na mvutano sana kuhusu huyo mtoto, kwanza huyo baba yake alikataa kuwa sio
mimba yake tulipomweleza mwanzoi..., lakini mtoto alipozaliwa akaonekana ni
dume, na anafanana na huyo mwanaume, basi wakabadilika, na kuanza kuja kudai
mtoto...’akasema baba wa binti
‘Mkaelewana au
ilikuwaje?’ wakaulizwa
‘Kuna cha kuelewana
hapo, hebu fikiria mwenyewe, walimuacha, kwa dharau kuwa eti mtoto wetu aa huo
ugonjwa, ataharibu familia yao, tukasema sawa, kama hawamtaki basi binti yetu
ana kwao, hatua shida, baadaye tukagundua kuwa binti ana mimba, na binti
akasema ni mimba ya huyo mwanaume aliyemuacha,..ikabidi twende huko kutoa
taarifa, wakakana kuwa mimba hiyo sio ya mtoto wao, na mtoto wao akakana mbele
yetu...’akatulia
‘Sasa kazaliwa
dume...na sura sawa kabisa na baba mtu...wakaanza kueleta vurugu, nikawaambia
wasisogee kabisa kwenye eneo langu, la sivyo tutatafutana ubaya, ....wakaenda
kushitaki, lakini sheria ikawabana, kwani kauli ya kukataa mimba ilitolewa
mbele ya wazee wenye hekima zao...’akatulia
‘Kwahiyo wakakubali
kushindwa..?’ wakaulizwa
‘Sasa wangefanyaje...?’
naye akawa kama anauliza
‘Je kwa hali hiyo
mnaweza kuhisi kuwa huenda wao ndio wamemchukua huyo mtoto?’ wakaulizwa
‘Hilo hatuna uhakika
nalo, kwasababu hao watu wanaishi kijiji cha mbali, na kama wangelionekana huku
tungelipata taarifa....’akasema mzee mmoja.
‘Wanaweza kutuma mtu
kuja kuifanya hiyo kazi...’akasema mzee mwingine
‘Haiwezekani, maana
mimi nalima hapo jirani, sikuwahi kuona mtu yoyote akipita eneo hili, na unaona
pale shambani kwangu kulivyo ni juu, mtu akija eneo hili namuona
kabisa...’akasema mzee mmoja
‘Je huyu mama wakati
anapita kuja kisimani wewe ulimuona?’ akaulizwa huyo mzee, na huyo mzee bila
kusita akasema;
‘Ndio nilimuona kwani
alisimama tukasalimiana, ...’akasema huyo mzee
‘Na alikuwa na mtoto
mgongoni...?’ akaulizwa
‘Ndio alikuwa na mtoto
mgongoni...’akasema huyo mzee
‘Na kama ulivyosema mtu
akija au kutoka kisimani, unamuona ina maana huyo mtoto kama alimtoroka mama
yake akiwa kazimia, ungelimuona, au sio...?’ akaulizwa
‘Ndio
ningelimuona...huyo mtoto hajatoka humu, ....sizani, angelipita wapi...’akasema
huyo mzee
‘Je wakati hawa akina
mama wanapiga ukelele wa msaada uliwasikia?’ akaulizwa
‘Ndio niliwasikia, na
nilikuwa wa kwanza kuja eneo hili la tukio, ndio nikamkuta huyu mama akiwa na
huyo mama mwenye mtoto, na wakati huo alikuwa hajajitambua vyema, na baadaye
ndugu zake wakafika....’akasema huyo mzee
‘Sasa kiutaratbu wa
kuisaidia polisi, nyie mama wawili na wewe mzee uliyemuona huyo mama
tutaongozana hadi kituo cha polisi mkaandikishe maelezo yenu, na tutawahoji
kidogo, ili kupata ukweli,...’akasema huyo mtu wa usalama
‘Lakini sisi tulikuwa
tunapita tu...’wakalalamika hao akina mama wawili
‘Na mimi nilikuwa
nalima tu....’akasema huyo mzee
‘Ni utaratibu, tunataka
kupata uhakika, na sio hawa tu, tutawahoji watu wote tutakaowahisi, maana
hatuna uhakika bado...kama huyo mtoto apotea kivipi, na tumewaita watu wa
wanyama pori wajaribu kutafiti eneo lote ili tuwe na uhakika zaidi...’akasema
huyo mtu wa usalama
‘Kwahiyo mnaweza
kutawanyika, na sisi tutaendelea kufanya uchunguzi...’wakasema watu wa usalama
‘Mimi siondoki, mpaka
nimpate mtoto wangu...’mama wa mtoto akagoma kuondoka
***********
‘Hivyo ndivyo ilivyotokea
awali....’akasema huyo mzee na kutulia, na tulipoona haendelei, tukaanza
kumuuliza maswali
‘Ina maana huyo mama
alikuwa na ugojwa wa kifafa...?’ nikauliza
‘Ndio huyo mama yake
alikuwa na tatizo la kifafa...unajua tatizo hili enzi za mababu zetu ukionekana
nalo, kama ni mwanamke aghalabu kuolewa, basi mama yake alipogundulikana ana
tatizo hilo, baba yake akaamua kumuacha...’akasema
‘Kwanini walikuwa
wakifanya hivyo....?’ akauliza mwenzangu
‘Sijui, ila mimi kama
mganga wa kienyeji, nina tiba za kusaidia, ila ukichunguza sana, kwa vile
ilishafikia hali wanaona ugonjwa huo hauna tiba hasa ikiwa tatizo hilo
limetokana na kurithiwa, ina maana ukiwa nao unaweza kuzaa watoto wenye
matatizo hayo,....’akatulia
‘Hivi ndivyo ilivyo, ina
maana kifafa hakina dawa...?’ mwenzangu mmoja akauliza
‘Dawa ni za kutuliza
tu, mababu zetu wao waliona Ili kukwepa kuuendeleza hilo tatizo, wakaamua kuwa
kama mke ana hilo tatizo haolewi na akiolewa na akagundulikana anao
anaachika...’akasema huyo mzee
‘Na kama mwanaume ndiye
mwenye tatizo hilo, ina maana haoii...?’ nikauliza
‘Wazazi wa mke
wakigundua hilo, hawatamruhusu binti yao kuolewa huko....japokuwa kwa kujitetea
wanasema ugonjwa huo ukitokea kwa mama ndio unaendelea lakini kama ni kwa baba,
unakuwa hauna nguvu sana ya kuendelea...hilo ni kwa wazee wetu...’akasema
‘Mhh, huo sio
ubinadamu...’akasema mwenzangu.
‘Ndio hivyo hayo ni ya
kizamani na wao walikuwa na mfumo wao, na kwa vile utaalamu ulikuwa haujakwenda
mbali zaidi, basi ilibidi wafanye hivyo, huwezi kuwalaumu,....’akasema huyo
mzee
‘Lakini kwa umri wa
huyu mwenzetu sio zamani kihivyo, eti....madawa yapo, tiba zipo, ...na
unyanyasaji tu..’akalalamika mwenzangu
‘Hivi unajua kuna
sehemu bado watu wanafuata mila za zamani kabisa, kwa karne hii...wengine hata
dawa za hospitalini hawaziamini...nchi hii kubwa,...’akasema mwigine na yule
mzee, akakohoa kama atalazimisha tunyamaze akaendelea kusema;
‘Sasa mama yake huyu
alikuwa na tatizo hilo, na aliweza kudondoka popote na hata akiwa
jikoni anaweza
kudondoka hata kuungua...kwahiyo ni ugonjwa fulani unaotesa, na unamuadhiri
sana muathirika, mtu una...hamjana mtu mwenye tatizo hilo anavyokuwa, ....ni hatari
kidogo...’akasema huyo mzee
‘Kwahiyo watu wenye
tatizo hilo hawana haki ya kuoana..si ndivyo hivyo?’ akauliza mwenzagu
‘Mimi sijasema hivyo,
maana mimi nina tiba zake, ....unasikia sana...ila wao, walifikia maamuzi
hayo,....mimi muda huo nilikuwa sipo ningelikuwepo ningewashauri vinginevyo....’akasema
‘Baba yake huyo kuona
hivyo akaamua kumuacha kutokana na ushauri wa familia yao, wakiogopa kuwa
akizaa mtoto atakuwa na huo ugonjwa, na kizazi hicho kitaendeleza huo ugonjwa
...na hawakutaka kizazi au familia hiyo iwe na tatizo kama hilo...’akasema huyo
mzee
‘Kwahiyo huyo mama na
mume wake hawakukaa wakajadili na kufikia makubaliano , maana nijuavyo mimi, wawili
hao walioana wakiwa wanapendana, hawakulazimishiwa kuoana..au sio?.’akauliza
mwenzangu.
‘Unajua, pamoja na
mapenzi waliyokuwa nayo, lakini ilifika waati mume akashauriwa na wanandugu, si
unafahamu wanadugu walivyo, ikabidi akubali, na kusimamia upande wa ndugu,
hakumjali tena mkewe, na hakutaka hata kukaa na mkewe kushauriana lolote..,japokuwa
walipendana, hata kuoana kwao, kulikuwa ni kwa ubishi, ...hayo nikipata muda
nitawasimulia...ila mjue tu kuwa walioana bila kufuata ushauri wa wazazi wao,
na ilipotokea hili, wakamwambia unaonaeeh, usemi wenu hua....basi kukawa hakuna
jinsi.’akasema
‘Mzee hebu tueleze
maisha hayo ya wanandoa hao ili tujue chimbuko la huyu , huyu eeh, jina lake
nani, nimesikia wakimuita Kejeli miondoko,...na hivi kweli mzee ugonjwa, ndio
usababishe watu kuachana , waliopendana wakatiliana kiapo cha shida na raha, mimi naona kama ni uonevu fulani...?’ akauliza
mwenzangu na huyo mzee akakaa kimia, na haikuonyesha dalili kuwa anaendelea na
simulizi hilo, na mimi nikamuuliza...
‘Sasa baaadaye
ikawaje...?’ nikamuuliza huyo mzee, na huyo mzee akaoyesha ishara kuwa koo
limekauka...
NB, Tukutane sehemu
ijayo...
WAZO LA LEO:
Mnapofikia hatua mbaya ya mfarakano,kati ya wanandoa, ni muhimu mkakaa na
kutafuta njia sahihi za kusuluhisha hilo tatizo lenu, na kama itafikia hatua
mbaya ya kuachana, ni vyema mkajadiliana msitakabali wa watoto, ...mjue
matatizo yenu yatawaathiri sana watoto, kwahiyo kunahitajika hekima ya hali ya
juu kuhakikisha kuwa watoto hawaumii au kuteseka.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment