Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, June 29, 2015

RADHI YA WAZAZI-12


‘Kiukweli kama nilikuwa sijasikia sifa za huyu mama kutoka kwa huyo mlinzi mkusanya mizigo nisingeliogopa vitisho kama hivyo, vitisho kama hivyo kwenye hizo kazi nilishavizoea, ....’

Tuendelee na kisa chetu...

*********

Mwanzoni nilipoanza kujiunga na tabia hizo chafu, nilikuja kusimuliwa habari za makundi hayo haramu,....

‘Kulikuwa na makundi ya kijambazi, maharamia, wanyang’anyi ,wabakaji, wenye kila kila aina za hila....’ wenyeji wakawa wanasema

‘Watu hao hao wabaya waliwatumia vijana, masharubaru, wenye nguvu, wakawaingiza kwenye magenge, na kuanza kupora watu njiani kwa kutumia pikipiki, na wengine wakajiingiza kwenye ujambazi wa  silaha, na zaidi wakaanziaha wizi wa mitandao, utekaji nyara , ubakaji, na kula milungula(blackmail) ....’wakaendelea kusema.

‘Kiukweli ilikuwa ni zama  ya majinamizi,maana ulikuwa huna amani, huwezi kutembea peke yako,na hata mkiwa kundi,badohuna amani,kwani hujui wanavyoweza kukuingilia....’ walisema .

‘Mmm,kwahiyo wengi wao walikuwa vijana?’ nikauliza

‘Si ndio,si ndio wenye nguvu, na pupa ya maisha,lakini pia walikuwepo watu wazima, ambao walikubuhi kwenye hizo kazi....wanaume na wanawake....’akasema  mtu mzima mmoja

‘Hata wanawake....?’ nikauliza kwamshangao

‘Haaah,yah, hata wanawake,...tena wanawake ndio walikuwa hatari zaidi,maana akikujia huwezi kumdhania vibaya,...’akasema huyo mtu mzima , sikuwa nimewahi kuambiwa kuhusu huyu mama kabla, ila nilisikia tu kuwa kulikuwa na mama mmoja aliyekua jasiri, lakini sikutegemea kuwa atakuwa huyo mama...

‘Hata waamke , walikuwa mstari wa mbele hadi kupewa uongozi wa kuongoza makundi hayo,haiwezekani...!?’ nikasema kwa dharau, na sikutaka kusikiliza zaidi kuhusu huyo mwanamke aliyekuwa kiongozi wao,mimi nilikuwa na kasumba ya kuzarau wanawake....sasa kumbe ningelisikia mapema, huenda ingenipa tahadhari fulani...

‘Lakini mkono waserikali mrefu, wengi wao walikuja kukamatwa...baada ya msako wa nyumba hadi nyumba...’akasema mama mmoja mtu mzima

‘Lakini sio wote...’akasema mume wake

‘Ndio kwa muda ule hawakukamatwa wote, ....walibakia viongozi wao, wakajificha, wakawa wanafanya mambo yao kwa siri....’akasema huyo mama

‘Walipoona kuwa kuna bado mabaki,na hayo mabaki ndio hatari zaidi, ndio wakabuni mbinu ya kuweka mitambo ya mitandao kila kona kuoana mizunguko ya watu, mitandao hiyo iliwekwa kwa siri, ilichukua muda sana....na ndipo wakaja kuwanasa hao wakubwa zao, na mmoja wa hao alikuwa ni mwana mama aliyekuwa tishio...’akasema huyo mama mtu mzima.

‘Mwanamke  gani huyo alikuwa jasiri kihivyo...?’ niliuliza japokuwa sikuwa makini sana, kwani niliona kama hadithi tu...

‘Usiombe ukutane naye...’jamaa mmoja akasema na mimi nikazarau tu.

‘Cha kutisha zaidi wengi wao bado wapo jela,...’wakaniambia  hawakuniambia kuwa huyo mama alikuwa kaweza kumaliza kifungo,au kuachiwa kwa msamaha,...kwani ndivyo ilivyokuwa kwa huyo mama, kumbe baadaye alikuja kuachiwa kwamsamaha,baada ya kuonyesha mwenendo mzuri huko jela,lakini baada ya kusota jela miaka mingi, ...

‘Kwa kipindi kile sikuwa na hamasa ya kumfahamu sana huyo mama, ningelijua ningelijua cha kufanya, huenda ningemchunguza na kumfahamu kuwa ni mama gani..., ila waliposema alifungwa na huko jela alikuwa kiongozi wa wafungwa,..na jela ni kama nyumbani kwake.,...

Moja ya sifa kubwa ya huyu mama ni kuwa haogopi, ana uwezo wa kupigana kwa kutumia mikono yake bila silaha, lakini silaha pia anaimudu vyema,..yeye akikosana na mtu anapanga pambano, na anakuambia kabisa ukimshinda basi umfanye utakavyo, ila akikushinda cha moto utakiona, ole wako....damu yako ni halali yake, na hakuna aliyewahi kumshinda....’ nikakumbuka maneno ya yule mlinzi.

Sasa kumbe huyo mama ndio aliyekuwa bosi wangu,ndiye huyo nilimuingilia na kuanza kufanya mambo yale aliyokuwa ameyaacha yeye...nikachokoza nyoka aliyekuwa kajificha shomoni....

*********

Wazo la kwanza lilikuwa kutafuta usaidizi, kwani kulikuwa na watu kazi yao ndio hiyo, kutoa ulinzi, muhimu uwe na pesa za kuwalipa, au wanakwenda kupambana na huyo mtu, nikaona nifanye hivyo haraka iwezekanavyo....maana nimeshatishiwa amani...., nikampigia jamaa mmoja mwenye kumiliki kundi la walinzi kama hao;

‘Rafiki yangu kuna mtu kanitishia amani, nataka msaada wako...si unajua zangu ni za mdomoni,..... sasa huyu haongei anatenda kwa kipigo....’profesa akamwambia huyo mkuu wa walinzi

‘Hamna shida ni pesa yako tu...’akaambiwa

‘Si unanijua tena mkuu, kwasasa sina kianzio, ila nakuahidi kuwa nitakulipa haraka iwezekanavyo...na ahadi kwangu kwako ni deni...kwa hivi sasa sijapata pesa yangu, ....’profesa akasema

‘Hapana wewe siku hizi umebadilika kabisa, ...sifa zako zimekuwa za maneno tu, siwezi kutoa watu wangu halafu niwaambie wasubirie, hata mimi nipo katika hali mbaya kibiashara....’akasema

‘Mkuu je nilishawahi kukubabaisha kwa ahadi hewa,...?’ akauliza profesa

‘Kwangu hujawahi, ...najua ukifanya hivyo kwangu hutaishi, huwa sibabaishwagi, ujue kabisa,...sitaki usumbufu, sasa hivi serikali ipo makini sana na watu kama sisi...usije nikaja kunyang’anywa leseni yangu....’akasema

‘Kwahiyo...?’ profesa akauliza akijifanya anazo,

‘Nimekupa angalizo tu, kuwa sitaki kazi ya ubabaishaji, kwanza nataka kianzio,...’akasema

‘Aaaa kianzio ndio hicho,.... huyu mtu hataki kunilipa nahitaji watu wakunisaidia, ili nizipate pesa zangu......’akasema

‘Ok,...kama ni kwenda kuchukua pesa yako tu,  nambie ni nani ili watu wangu waanza kumfanyia kazi,kama kweli kuna malipo sahihi...ni nani na anaishii wapi?’ akauliza

Madame Africa..yule ni bosi wangu namdai pesa zangu nyingi tu hataki kunilipa nataka niende na walinzi wawili....najua atanilipa tu, na baada ya hapo wawe wananilinda, ..si unajua tena....’akasema profesa akijua sasa mambo yatakuwa safi,

Akilini alishaliwazia hilo, kuwa akienda kwa huyo mama, akiwa na hao walinzi,kuwa anadai pesa zaidi, kwa kumzalilisha,na anamstishia kuwa ukizidi kumfuata fuata atazitangaza  siri zake zote, na keshaajiri hao walinzi..

Japokuwa historia zake za nyuma zilitisha, lakini niliona siwezi kuziachia pesa alizokuwa tayari azipate, na akizipata anahama kabisa..

‘Nilipoongea hivyo, nikatulia kimia, sasa kusikia jamaa huyo anayemiliki hao walinzi atasemaje,nilijua ataulizia namdai huyo mama shilingi ngapi,  maana huyo mama kwa muda huo ni tajiri, ana uwezo,...’

Basi profesa akiwa kashikilia simu kwa madaha,akatulia, akasikilizia majibu kutoka kwa huyo mkuu wa mabaunsa..., lakini hakupata hayo majibu, kumbe simu ilishakatwa

‘Halooh, vipi....’simu haikuweo hewani,..akajaribu kupiga tena, kwanza ikaita halafu ikakatwa, ilionyesha kuwa jamaa hataki kupokea tena simu yake..., na baadaye ikawa akipiga hiyo namba anaambiwa haipatikani.

‘Mhh,huyu jamaa vipi....’profesa akabaki  akijiuliza huku nywele zikimsisimuka  kwa woga.

******
Siku hiyo ikapita profesa akawa kama mgonjwa, ....

‘Hapo sina pesa, nina madeni lukuki, mimi nitazipatia wapi hizo pesa, na kiukweli nilikuwa nadaiwa pesa nyingi, kuacha hizo za huyo mama, ...

Unajua kuna kule kujidanganya kwa kujipa moyo, sikukata tamaa, unajua tabia ya maisha hayo yalivyo, na mimi yalishanikaa mwilini,unaweza ukasota kweli, huna pesa, maisha magumu, lakini ukiibuka wewe ni tajiri, japo ni kwa muda...nikajipa moyo kuwa huo ni muda wa kusota, lakini nitakuja kuibuka tu....

Nikachukua karatasi na kupiga mahesabu, pesa anazonidai huyo mama peke yake, ooh, nilijikuta mwenyewe siamini kuwa nilikuwa nimetumia pesa nyingi sana kwa huyo mama.

‘ Pesa haramu , pesa za dhuluma za huyo mama zilikuwa nyingi, achilia za hao wengine na kutokana na huyo mama alivyosema, keshawapanga watu wengine, niliowahi kuwafanyia hivyo,sijui aliwezaje kuwafahamu....akidai kuwa yeye sasa keshajiunga na kundi la kusafisha wabaya mitaani....hasa watu kama mimi...’

Ujue mimi sasa hivi ni kiongozi wa kufuta watu wote wabaya wameniamini kwa vile nawafahamu wote, ...sasa wewe kinyamkera sijui umatokea wapi...nakuhakikishia utazilipa hizo pesa zao..’nikakumbuka maneno ya huyo mama

Kiukweli siku hiyo nikaona nisitoke kabisa...nikalala..lakini usingizi ungetoka wapi,nikajikuta namuota huyo mama akinijia na kisu mkononi,mara akiwa na sura ya shetani....

 Siku ya pili, ikapita, siku ya tatu,..wiki ikapita nikajua huyo mama keshasahau. Huenda alikuja kunitishia tu, hana uhakika kuwa ni mimi...Nikaona nitoke niingie kwenye mishe mishe zangu maana nitakufa njaa, sasa niende wapi, nikajiuliza.

Mara nyingi mtu ukikwama kuna sehemu tunakwenda kwa mtaalamu wa kupanga dili,...nikaona ngoja niende kwake nikajaribu bahati yangu..., huenda nikapewa dili ya kuingiza pesa, japokuwa kwake napo kuna ushuru wa kumlipia, kwanza kwa ajili ya kukupangia hiyo dili,

‘Hakupangii mipangilio hiyo bure...unamlipa,ni kama madalali walivyo huku...’akasema profesa

‘Kwanza unamlipa pesa ya kukupangia mikakati, halafu ukifanikiwa unamlipa ushuru wake mwingine...ni wajanja wajanja fulani hivi...’akaongeza kuongea

‘Basi nikaona nipitie kwake,...’ akasema

‘Kiukweli bro,huyu jamaa ni kichwa, yeye hafanyi kazi zaidi ya kupanga mikakati, ..mikakati ya wizi,...., na hakosei...ana mitandao ya aina yake, anaweza akafanya vitu vyake, akazima mashine ya kuona matukio sehemu fulani unapokwenda kufanyia hujuma, ikibidi...., lakini hapo unatakiwa umlipe pesa nyingi...’akaendelea kuongea.

Japokuwa sikuwa na pesa, nikaona nimuone tu, nitamkopa,..pamoja na ubabaishaji wangu, lakini watu walikuwa wakiniamini kwa kazi za mdomoni, kukiwa na kazi ya kwenda kuongea, aaah,nimo sana,siunajua wabongo kwa kuongea....’akakuna kuchwa

‘Ila kazi za kupigana ngumi,kutumia bastola....simo,..naweza kutumia silaha ndio,lakini ilikuwa sio fani yangu....mimi ni kupepeta  mdomo, weee, walikuwa wakinijulia kwa hilo...hasa hii kazi ya mlingula, kule wanaiita blackmail..hiyo ni kazi nyeti kule...

********
‘Ndugu umekuja,ulikuwa wapi,sijakuona karibu wiki....’akaniambia huyo jamaa

‘Nipoo nipo tu....’nikasema

‘Sasa kulikuwa na kazi moja,...nataka wewe uifanyie....’akaniambia kama vile alifahamu kuwa nimekuja kwa kwa hilo.

‘Mhh, kwa hivi sasa nipo mtegoni, siwezi,...’nikasema

‘Sasa umekuja kufuata nini...?’ akaniuliza akionyesha kutotaka kuongea na mimi tena.

‘Mhh,....kiukweli nimekuja kwa hilo, ila iwe kazi ya chapu chapu....’nikasema huku moyoni natamanii anipe dili yenye unafuu, sikutaka shari kwa muda huo.

‘Unajua kazi yenyewe ni kazi gani....?’ akaniuliza

‘Sijui nambie wewe....’profesa akasema

‘Hiyo kazi, nilishaifanyia kazi, ...unajua na mimi nahitajia pesa kidogo, nataka kununua chombo fulani, ni gharama sana....na nikikipata hicho, dunia nitaiweka hapa....sasa nikaitafiti hiyo dili,nikaona wewe unafaa....’akasema akionyeshea mkononi kuwa dunia ataiweka hapa(unakumbuka kisa cha dunia yangu)

‘Mhh, lakini kwanini mimi..?’ profesa akauliza

‘Aaah, sio lazima wewe, ila ulivyokuja nikajua una njaa..au..kama hutaki basi...’akasema akigeukia komputa yake maana masaa yote yupo kwenye komputa.

My friend, mtu akija kwako, ujue hajafika kuongea au sio, ila..sitaki kazi ya kunichukulia muda mrefu..., nataka kupata na kuachia, na kutoweka, nipo kwenye kamba nyembamba, naweza kudondoka...’nikamwambia tukitumia lugha zetu

‘Kuna kazi moja, ikifanikiwa utaingiza ,dola laki moja na elifu hamsini,kama kianzio unazipata bila ubishi, na hapo ushanilipa ushuru wangu....,’akasema huku akitabasamu

‘Na kila mwezi kama kawaida utapata elifu hamsini, kwa miezi kama mitatu,...au hata thelathini, ukimuhurumia,...na hushuki zaidi ya hapo,...mimi unanipa zangu kumi kumi kila mwezi kwa miezi hiyo mwili,sitaki zaidi....’akasema akijizungusha kwenye kiti chake.

‘Unaona ilivyo,...baada ya mikupuo mitatu, wakati bado anahaha,....unampa unafuu, mimi naachana na wewe, unabakia wewe na mwenye kisima,maana si umeshamfahamu, nazimamitamb yangu, unafanya vitu vyako,ukitaka....mpaka utakapohakikisha kisima kimekauka, ni wewe tu na njaa zako...’akasema huyo mtaalamu.

‘Mhh, dola laki moja na elifu hamsini, tasilimu!...na bado kila mwezi naingiza hamsini,au thelathini!...halafu unasema wewe nitakuwa nakulipa kumi kumi kila mwezi, kwa miezi miwili....mmh hapo bado nitabakia na ...ooh, usinitanie...?’ nikasema nikitabasamu.

‘Kwanini niendelee kukulipa kidogo kidogo kidogo,wakati wewe tunakulipa kianzia na ushuru tu,...?’ nikauliza nikianza kuingiwa na tamaa na ubinafsi hata kazi sijaifanya.

‘Maana tukienda kwenye ushuru wangu utaona pesa ni nyingi,  ndio nikaona unilipe kwa mikupuo..uonavyo,vinginevyo tutaingia kwenye asilimia ya pato,..ni wewe tu...’akasema
Kiukweli moyoni hamasa na tamaa vikajijenga, sikuwa na matarajio kama hayo, na huyu ni mtaalamu kweli akikuambia kitu ni kweli kinafanyika, na hana ubabaishaji.

‘Hii kazi nimeshaifanyia utaratibu wote, kinachohitajika ni mtu wa kuongea, mtaalamu wa kuongea lugha tofauti..maana kuna maeneo saba ya kucheza nayo,...huyu ni kuku mgeni ,...hana hiana, ni muoga,..ni tajiri bahili,...’akasema

‘Tajiri bahili dawa yake ni moja tu...hahaha,...huyu jamaa bwana kaibukia toka huko kwao,..huko naona alikuwa hapati nafasi..., lakini ana upele kila sehemu, japo anajifunika, tunahtajika tuukune huko upele...natumai unanielewa....hana ujanja, ila ana pesa anayo,nimeshapata akaunti zake zote....’akasema kwa kutumia lugha wanazozijua...

 Jamaa alipofika hapo akajinyosha kuonyesha kachoka kuongea na kaka mtu mwenyewe akasimama na kuchukua kopo la maji akampa ndugu yake anywe, hamasa ya kusikia zaidi ilishamuingia, na ndugu yake alipomaliza kunywa maji akasema;

‘Bro,hapa ungenipa kinywaji...mmh, nakumbukia enzi zangu....’akasema

‘Achana na ulevi,afya yako yenyewe migogoro,..hebu nikuulize swali...’akasema kaka mtu

‘Maswali utanipotezea mpangilia uliopo kichwani,..kwani unataka kuuliza nini bro,kuhusu kijana wako...?’ akasema jamaa

‘Ina maana mlikuwa mkilipwa pesa zote hizo, hizo si dola ukibadilisha kwa pesa ya kwetu ni shilingi ngapi....mbona pesa nyingi sana...halafu ina maana hata kijana ulimlea katika mazigira hayo hayo,maana hapo hujamtaja kabisa..?’ akauliza kaka mtu akiwa na mshangao machoni

‘Hahaha, bro, tatizo pesa hizo ni chafu, unazipata leo, kesho hakuna kitu...ukizipata unakimbilia kulipia madeni, kulewa na starehe, ...zinapukutika kama vumbi hafifu jangwani linavyopeperushwa na upepo...

‘Bro ya kijana wako utakuja kuyasikia, kwanza uone maisha yangu, na utakuja kuona chanzo cha kijana wako kuja kupata mke,....ilianzia mbali....’akasema akijiegemeza kwenye kiti.

‘Haya endelea.....’akasema kaka mtu

‘Basi huyo mtaalamu aliponitajia kiwango hicho cha pesa, nikajua nitaweza kupunguza pesa za huyo mama, na nitamuahidi kuwa nitamrejeshea kila mwezi, elifu kumi kumi yake, na huku nabakiwa na pesa za kujitanua mitaani, sina shida nikiwa na pesa,....’akasema akionyesha kwa vidole

‘Bro,unajua  maisha ni mafupi tumia pesa ukipata ukikosa unajutia unabakia kuota ndoto za Alinacha kwenye vitabu vya zamani, kama ninavyoota sasa hivi...

‘Niliwazia kuwa huyo mama, pamoja na mengine ana udhaifu mmoja,anapenda sana pesa, ukamtajia kuwa ataingiza pesa nzuri, mhhh, wewe utakuwa rafiki yake..’ aakatabasamu.

Basi nikaendelea kuongea na mtaalamu,nikamwambia;

‘Kama una uhakika,....kuwa nitazipata hizo pesa...nitajaribu..’nikasema huku tamaa ya kuingiza hizo pesa ikinitawala akilini,akaniangalia kwa jicho la haraka halafu akakunja sura, akasema;

‘Hakuna kujaribu hapa, kama huwezi useme si-we-zi....na mimi nitamchukua mtu mwingine anayefaa....siwezi kupoteza taaluma yangu kwa mtu wa majaribio.....unanifahamu nilivyo....’akasema huku akikagua kitu kwenye komputa yake.

‘Unasikia profesa, nataka mtendaji na sio mtu wa kujaribu, na swala la kuwa mimi nina uhakika, nashangaa kwanini unaniuliza hivyo,na umekuwa mtu wa kwanza kunitilia mashaka kwenye dili zangu, haijatokea,...mimi sipendi kabisa...’akasema akinitupia jicho la udadisi.

‘Sijatilia mashaka dili zako...,najua wewe ni mtalaamu wa dili....nilikuwa nasemea tu...kama umeshaifanyia kazi, isije nikaingia kichwa kichwa...’akasema profesa

‘Sikiliza nimechanganua, nikaona wewe unafaa, kuna kazi nyingi tu, lakini hizo nyingine zinahitaji mtu mwenye nguvu, wewe huna nguvu, nguvu zako zipo mdomoni tu.. .nitakuelekeza utaratibu..’akasema huku akiendelea kuangalia kwenye komputa yake.

‘Muhimu,ukifanya nitakavyokuelekeza, haina shaka utafanikiwa, ila ukijifanya una akili zako nyingine,ukafanya uonavyo wewe,ukivuruga mimi sipo, ninachohitaji kwanza ni kianzio cha kukupa hii dili na sio mtu mwingine na ushuru wangu ukishafanikisha....’akaniambia huku akionyesha uso wa kunidadisi.

‘Ok,...ok...lakini hapo nina shida....’akasema profesa

‘Shida gani tena, usisema umechacha....kwanza nikuulize ile dili yako binafsi ulishaimaliza...?’ akaniuliza

‘Dili ipi...?’ nikamuuliza nikionyesha uso wa mshangao,maana dili binafsi ninayoijua mimi ni hiyo ya huyo mama,...nyingine ni za kuchangia, na hakuna mtu niliyemuhusisha, sikutaka kumuhusisha mtu yoyote, sasa huyu mtu kafahamu vipi hiyo dili binafsi...,nilipotaka kumdadisi haraka akasema;

‘Tuyaache hayo...hayanihusu,...,nakuuliza tena, upo tayari kwa hiyo kazi,...utaiweza hiyo kazi,asilimia kubwa ya hiyo kazi, ni mdomo tu, kuongea halafu ikifika kwenye kuchota pesa ni lugha ya vitisho kwa mdomo tu,lugha ya hadaa kwa mdomo tu...,na wewe ni mkali kwahilo...sasa usinipotezee muda,nahitajia kumuita mtu mwingine...’akasema

‘Aaa, sijasema siwezi kuifanya,...nipe hiyo kazi...nitaifanya.....’nikakubali, lakini moyoni nilikuwa na mashaka, nilishaingiwa na uwoga fulani, ambao nilikuwa sinao kabla, baada ya kujiunga na mambo haya nilijifunza kutokuwamuoga,kutokuwa na huruma hasa unapoona jambo hilo ni la pesa...

‘Lakini pamoja na wasiwasi, mashaka, kiasi hicho cha fedha kilichotajwa kutoka kwa huyu mtaalamu kilivutia sana...tamaa,...ubinafsi,ukanitawala, na kutokana na njaa , na shida niliyokuwa nayo, nikajipamoyokuwa nitaiweza hiyokazi,japokuwa nilikuwasijaambiwa ni kazi gani.

‘Utaifanya hiyo kazi sio.....?’ akaniuliza akiniangalia kwa macho ya udadisiakitaka uhakika tena wa kauli yangu,maana mamboyetu unaulizwa mara mbiliya tatu inakuwa nimkataba...

 Nikatabasamu huku akilini nikianza kuzihesabu pesa kimawazo, nikiwazia kuwa muda huo nipo nimesima mbele ya huyo mama, huku namuhesibia pesa zake na huyo mama akitabasamu kwa tamaa, lakini cha ajabu alipotabasamuu niliona meno ya kishetani ya kijitokeza...

NB : Habari ndio hiyo, na hayo ndiyo mambo ya ulaya  na profesa, je ilikuwaje


WAZO LA LEO: Tamaa ni mbaya, mtu usipotosheka na pato lako halali ukataka zaidi ya halali yako, ukadumu kwenye dhuluma, ukajenga, ukajijenga, ukachuma kwa mtindo huo, usitarajie amani katika maisha yako,dhuluma hiyo itakuandama hadi unaingia kaburini, achana kabisa na tabia hiyo, rizika na pato lako halali. 
Ni mimi: emu-three

No comments :