‘Huyu jamaa hutaamini, ni msomi, na alijiweza kwani alifikia
kumuoa mke wa kizungu., na alimuolea huyo mwanamke huko huko nje....’akaanza
kuongea mzee mmoja.
Mzee huyo tulimkuta akiwa amekaa nje ya nyumba ambayo inasemakana ni mali ya jamaa
ambaye tulimkuta mitaani, mara akihubiri dini, mara anageuka kuwa mkufunzi,
mwalimu, dakitari, lakini ghafla akabadilika na kuanza kushusha matusi , matusi
mabaya tena ya nguoni.
Mimi na marafiki zangu ambao tulikuwa mitaani katika
harakati zetu, za kusaidia wale ambao wana matatizo mbali mbali, tukakutana na
huyu jamaa akiwa kazungukwa na watu. Sisi kwa nia njema, tukisaidiwa na
wafadhili, tulianzisha kundi maalumu la kuwasaidia wenzetu walioharibikiwa
kutokana na madawa ya kulevya, kuumwa, au kuharibikiwa na akili kwa hili au
lile.
Kundi hili bado changa, kwani lilihitajia ufadhili, na
tulipofika eneo hilo na sisi tukavutika kuona kinachoendelea, tukakaribia,
japokuwa tulikuwa tunahitajika kukutana na baadhi ya wafadhili wetu, lakini
hisi zikatuvuta tufike hapo tuone kinachoendelea
‘Tutachelewa jamani, huo unawezekana ni ugomvi, au ni hawa
watu wanahubiri mabarabarani...’akasema mmoja wetu
‘Tuone kidogo, maana moja ya kazi zetu ni kuangalia shida za
watu, huenda hapa tukakutana na mojawapo,...’nikasema
‘Shida hizo zipo nyingi muhimu ni wafadhili, na unakumbuka
tuliambiwa tufike saa ngapi....’akasema mwenzetu, na mara tukasikia watu
wakipiga makofi, mimi sikuwaangalai wenzanu nikajongea hadi kwenye ilo kundi la
watu kuona kuna nini. Kilichotokea hapo baadaye kilitufanya tujikute tunaamulia
ugomvi, na tukajikuta tukimbeba jamaa aliyeumizwa hadi kituo cha afya.
‘Huyu mtu wenu hajaumia sana....’akasema docta
‘Sasa ndugu tunaomba utupeleke nyumbani kwake....’tukamuambia
jamaa aliyetusaidia kuamua huo ugomvi akisema anamfahamu huyo mtu
‘Nyumbani kwake sio mbali na hapa, twendeni niwapaleke...’akasema
huyo mtu na tukaongzana na huyu jamaa aliyemizwa, kwa muda huo alikuwa katulia
tu, hangei, na mguu kwa mguu hadi tukafka nyumbani kwa huyo jamaa aliyeumizwa.
**********
‘Ina maana jamaa huyu kachanganyikiwa, na ana matatizo ya
akili...?’ nikamuuliza mwenyeji tuliyemkuta baada ya kujitamblisha na kusalimiana
naye.
‘Ndivyo ilivyo,
kachanganyikiwa, ... ana matatizo ya akili.....kavurugukiwa...kwani kumetokea
nini, maana kanitroka hata sijui katoka saa ngapi,....mmh sasa hata mimi
yatanishinda,....’akasema huyo mzee tuliyemkuta hapo nyumbani.
‘Mliwahi kumpeleka hospitalini?’ nikamuuliza
‘Hahaha, ...matatizo hayo hayatibiki hospitalini, hata
muende kwa bingwa gani huwezi kuyatibia matatizo kama hayo..’akasema huyo mzee
akionyeshea kwa kichwa kumuelekezea huyo jamaa aliyepigwa huko mitaani
‘Kwanini, .....maana kama ni matatizo ya akili yana tiba
yake au sio,....mzee labda tukumpe mfano hai, sisi kuna watu kama huyu ambao tumewasaidia na
sasa ni wazima kabisa, tatizo ni kuwa watu hawalichukulii maanani hilo tatizo,
na wanachelewa hadi inafikia hatua mbaya,...’akasema mwenzangu
‘Na wengine wakiona ndugu yao anaumwa kama hivyo wanamficha,
wanamzarau, badala ya kufuatilia na kuona jinsi gani ya kumsaidia,..wanamuacha
tu anazidi kuathiria...’akazidi kuongea huyo mwenztu.
‘Sasa mlitaka mimi nifanye nini...?’ akauliza akionyesha
kukerekwa.
‘Ujue mzee, tatizo kama hili ni sawa na magonjwa mengine tu,
ukimuwahisha mgonjwa yoyote kwenye tiba
sahihi, ukafika kwa wataalamu sahihi, madocta bingwa, mbona wanapona tu,
wapo wataalamu bingwa wa magonjwa ya akili, na wengine inabidi kufanyiwa
upasuaji ikibidi...kutegemea na chanzo cha hilo tatizo...kuna wengine
wanatakiwa kufika hadi India ambapo kuna wataalamu wanafanya upasuaji wa
ubongo....lakini, ikibidi.....’akaendelea kuongea mwenzetu.
‘Hivi nyinyi mnanielewa lakini, mnafikiri mimi sina huruma
na huyu mtoto, nimekwenda hadi kwa docta bingwa wa pale Muhimbili, kahangaika wee
mpaka akanyosha mkono....India, india,...huyo acha ya huko India, huyu alipelekwa hadi huko Ulaya, lakini haikusaidia
kitu...acheni bwana...huyo, ana matatizo makubwa ya kiasili....’akasema
‘Amelogwa...?’akasema mwenzangu na akatufanya tucheke
‘Aheri angelogwa, ningelijua moja, maana nawafahamu waganga
wa kienyeji waaliobobea kwa watu waliofanyiwa hivyo..., mimi mwenyewe ni mganga
wa kienyeji, lakini hapo nimenyosha mkono...ila nilichowaambia ni hicho
hicho....’akasema akikatiza hayo maneno na kujinyosha kwenye kiti chake cha
kunesa.
‘Kama sio kulogwa, kama sio ....basi tatizo nini, au
anatumia, madawa ya kulevya...?’ nikauliza
‘Hata sigara hajawahi kuvuta huyo, niwaambie kitu, mkewe
alikuwa hapendi harufu ya sigara kabisa, sasa hayo madawa ya kuleya angliwezaje
kuyatumia, sana sana ni unywaji wa pombe zao za kizungu.....na hiyo sio sababu
ya matatizo yake....’akasema
‘Kwahiyo ni ugonjwa wa akili wa kawaida, au sio..huenda basi
hukufika kwa mtaalamu mwenyewe, hebu tuambie pale Muhimbili ulionana na docta
gani...?’ tukamuuliza
‘Vijana naona hamunielewi...kwanza hapa nina njaa
sijala...nimekuwa nikihangaika kumtafuta huu chizi..mpaka nimeshau kula chips
zangu zimepoa,...karibuni....’akasema sasa kwa sauti ya kama kakasirika huku
akifungua chips zake kwenye mfuko na kuanza kula.
‘Hapa nataka soda baridiiii...mmmh, alikuja jamaa mmoja ana
matatizo yake nimemuagua kanipatia viseneti, ndio nimenunua hiki chakula, na
huyo chizi nimemuwekea chake, akijisikia atakwenda kula, anajua kipo
wapi,..lakini wageni..si unajua tena nyumba hii tunaishi kizungu....’akasema
akiendelea kula.
‘Mzee sikiliza kama tulivyokuambia nia yetu ni kutaka
kumsaidia huyu jamaa, maana anaonekana ni mtaalamu, ..mwalimu, msomi, kama
tukimsaidia, tutakuwa tumesaidia taifa, nia yetu ni njema kabisa....’nikasema
‘Mhh mumeoana eeh, ni chizi msomi, ...lakini hivi niwaulize,
kuna docta bingwa wa maradhi ya radhi ya wazazi ...’akasema huyo mzee sasa akijifuta mdomoni, nasote tukashituka na
tukajikuta tukisema
‘Radhi ya wazazi...??’
tukasema sote kwa pamoja
‘Mhh, hamjui eeh, niwaambie kitu nyie vijana , hasa nyie mnajiona
mumekulia kwenye hii zama ya utandawazi, mnaona mambo yapo tu, ...mnasaahu hata
asili yenu...hata kijiji mlipozaliwa hamtaki kufika, kisa nini mumesoma...’akatulia
‘Haya na hata huo utandawazi hamjaufahamu vyema mnaiuingia
kichwa kichwa..., hamjui wenzenu wamewatengenezea nini, hamjui lengo lao ni
nini, ...mnafahamu wenzenu ni wajanja sana...’akasema
‘Akina nani....?’ nikamuuliza
‘Hao waligundua huo utandawazi,..nia yao kubwa ni kuwaharibu
akili zenu,, kuwapotezea maadili yenu mema...mnaiga tu, kila mkiona jambo
kafanya mzungu basi ni sahihi, mnafikia hata kutembea uchi, kuangalia mapicha
mabaya ya kuwaharibu ubongo, wengine ndio hao wanabwia unga...’akasema na
kunyosha mkono mbele,
‘Ina maana huyu anatumia madawa ya kulevya...?’ nikamuuliza
‘Hapana huyu hajawahi kufanya hivyo nina uhakika....’akasema
na kumuangalia huyo jamaa akiwa bado kalala pale sakafunii ambapo alijilaza
tulipofika naye hapo nyumbani.
‘Tatizo sugu ni kuwa nyie vijana, mumefikia kubaya, mnafikia
kuwadharau hata wazazi wenuu waliowazaa eti kwa vile mumesoma, eti kwa vile mna
kazi, eti kwa vile...mna cheo, mnawaona wazazi wenu wananuka, hawafai, hawana
hadhi, .....nawaambia ukweli, hamna lolote mbele ya wazazi wenu...’akasema
‘Ni kweli mzee, mtu akisoma vyema, hawezi kufanya hivyo,
ukiona mtu anafanya hivyo, hakusoma alikwenda kukariri tu shuleni, ili tu apate
pesa, elimu humuongoza mtu atende mambo mema.na sahihi...’akasema jamaa yangu.
‘Hahaha, mema na sahihi,...hao wanaiba serikalini, haoo
mafisadi..hawajasoma, hayo wanayofanya ni sahihi, ni mema....msitudanganye
hapa...’akasema mzee, na tukaona kama anapoteza lengo letu.
‘Mzee tunataka kujua huyu ana tatizo gani....’akasema
mwenzangu
‘Sasa mwenzenu huyo alisoma,alisoma kweli...na sio kukariri
kama munavyodai nyie...watu wabaya duniani ni wasomi, niwaambie ukweli...hao
ndio wanaiharibu dunia...hicha cha kusema kusoma ndio unatenda mema na ukweli
sio sahihi...sasa huyo mwenzenu ni msomi kweli kweli..., uliza wasomi
wanaomfahamu...hata mkewe alisema huyu alitakiwa kubakia huko majuu, kufundisha....’akasema
‘Kama mumewahi kumsikia huko mitaani, mtajua kuwa kweli
alisoma...hajakariri kama mnavyodai..., lakini kisomo chake hakikuwa na maana,
...akashindwa kujua kuwa alizaliwa, ...namsikitikia sana, maana nimehangaika
nimeshindwa, imefikia sasa ni kumuangalia tu..’akasema huyo mzee
‘Mhh, mzee, labda ungetusimulia maisha ya huyu jamaa
tungejua nini kilimtokea ili kama yawezekana tuweze kumsaidia....’akasema
mwenzangu mimi bado nikiwa nimeduwaa
‘Mhh jamani, hilo tatizo alilo nalo, watu wamehangaika,
wameshindwa, mimi mweyewe nilihangaika nikamfikisha hadi muhimbili,
ikashindikana, akapelekwa sijui wapi ikashindikana, hata mkewe ambaye sasa
karudi kwao, alimpeleka kwao uzunguni ikashindikana akamrejesha hapa
nyumbani... ndio huyo hapo....nimekwenda zaidi ya hapo, waganga wote wa
kienyeji nimemaliza, nikaenda kwenye maombi, wakaomba mpaka wakaukwa na koo,
hakuna kilichosaidia.......’akatulia huyo mzee
‘Samani kwanza, nikuulize, ina maana huyu jamaa mkewe
alikuwa ni mzungu...?’ nikauliza
‘Ndio mkewe alikuwa ni mzungu, na walizaa naye watoto
wawili, watoto wamechukuliwa na mkewe, maana angekaa nao angeliwaua, si mnaona
kawa chizi...’akasema huyo mzee
‘Kwanini nyie ndugu zake msingeliwachukua hao watoto, hasa
wewe baba yake mdogo...mnaacha watoto wanachukuliwa na wazungu?’ akauliza
rafiki yangu
‘Baba zake wadogo...! hahaha, huyu hana baba wadogo, huyu
hana mama, huyu hana baba,, na hakuwahi kuwa na ndugu..’akasema mzee, na kuzidi
kutufanya tuingiwe na hamasa ya kukisikia kisa cha ‘kichaa msomi...’
‘Wamekufa au....?’ nikauliza
‘Huyu ni kichaa msomi, docta wa miondoka, msomi aliyekubuhu,
anayejua kucheza mitindo yote ya muziki, hujasikia wakimuita, ‘kichaa midundo,..’ au ‘kichaa style..’ kichaa miondoko....ana majina mengi
kutegemeana na mazingiza.
‘Hahaha , msione nacheka, moyoni naumia sana, huyu ukikutana
naye akiwa katulia hutaweza kuamini kuwa humu hazimo,...ni msomi kweli....lakini
akishavurugikiwa masikini mwanangu....’akasema sasa akishika shavu..
‘Huyu, ukikutana naye akitembea, ukamwambia kichaa style,...kichaa miondoko...basi anabadili
mwendo, ana miondoka ya kila aina, anajua kucheza mziki mtindo wa kila aina,
anajua kiingereza kuliko waingereza wenyewe....anajua mambo mengi, lakini...kikimcharukia,
ni matusi, matusi makubwa makubwa tena ya nguoni.
‘Wasio mfahamu wanakimbilia kumpiga..nimekuwa nikitembea
naye, nikimfuatilia kila anapokwenda, ili kumsaidia, watu wasimuumize.,
inafikia muda na mimi nachoka,.....tatizo hataki kukaa, hataki kutulia hapa
nyumbani...unajua, anakwenda hata vyuoni kutaka kufundisha.....lakini
kisimcharukie....’akatuliza huyo mzee
Ni kweli aliyosema
huyo mzee, maana siku tulipomkuta mitaani akiwa kavalia vizuri tu, alianza
kuongea kiingereza safi kabisa, na akawa anatoa darasa kwa kiingereza na
kutafsiri kwa Kiswahili akawa anaongelea mambo mengi, mambo ya uchumi, mara
akamaliza, akaingia mambo ya vita baridi, jinsi Warusi na Marekani walivyokuwa
wakipambana, akamaliza, akaanza kuongelea mambo ya sayansi ugunduzi mbali mbali
jinsi ndege ilivyoguduliwa, au meli, au uguduzi wa madawa...mmh, wengi hasa
wasomi wakamsogelea wakijua kuwa huyu ana PHD, na wengine waakaanza kunukuu
Haikupita muda, akapita mama mmoja,..mara yule jamaa akamgeukia
yule mama, na kuanza kumporomoshea matusi, matusi mabaya mabaya ya nguoni, ....akiyaelekeza
kwa akina mama, yule mama alikuwa hamjui, akaanza kujibishana naye, akimtukana
pia,..oooh, akawa kajichongea, maana ilibidi mume wa yule mama kuingilia
kati...akaaza kusaidiwa na wenzake na kuanza kumpiga huyo jamaa, wakati huo
yule mama akiwa analia..., na sisi tukabakia tumeduwaa
‘Mhh, huyu jamaa vipi,....’mmoja akauliza
‘Hata sielewi, uliona jinsi alivyokuwa akishusha shule ya
historia, shule ambayo, sijawahi kuisikia,...’akasema jamaa aliyekuwa karibu
yangu
‘Acha hiyo historia, huenda kaogeza chumvi, lakii hiyo
sayansi aliyoiogelea hapo, utafikiri
alikuwepo kwenye huo ugunduzi wa mitambo, madawa....hizo fomula zake...ooh,
nimezimia, hajakosea kabisa...’akasema jamaa mwingine
‘Lakini mengine huenda anabuni tu, mimi sijwahi kusikia hayo
aliyoyaongelea, ...ila mambp ya uchumi nayakubali, hapo aliifikisha kweyewe.....’akasema
mwingine
‘Hiyo historia aliyoogolea hapo sio uwongo, hayo aliyoongea
ni ukweli mtupu....yalitokea, na ukienda kwenye vitabu vya kumbukumbu kama eclospidia, utayakuta, ndivyo, ilivyo,
mimi nafundisha masomo hayo chuo kikuu, nilipomsikia nilijua ni mmoja wa walimu
wangu walionifundisha,...’akasema jamaa mmoja aliyevalia suti alikuwa ni
mwalimu wa chuo kikuu.
‘Mhh, sasa mbona kabadilika ghafla tena, mumegudua kitu
kabadilika ghafla pale alipomuona huyo mama, ...ulimuona alivyofanya, kwanza
kaaza kuita , mama....mama, halafu yule mama alipokaa kimia,jamaa sijui kaoaa
kazarauliwa, akaanza kutukana....hivi kweli mtu kama huyu hawezi kusaidiwa?’
nikauliza
‘Hapo ndio hata mimi nimeshangaa...huyu kweli aahitajia
msaada....’akasema huyo mwalimu wa chuo kikikuu
‘Kuna tatizo....ni lazima tulichunguze hili tatizo, hili ni
jembe jamani...’nikasema
‘Ni kweli hebu tufuatilie tulijue ni tatizo gani tuone kama
tunaweza kumsaidia...’akasema mwenzangu ambaye tuliamua kuanzisha kampuni binafsi
ya kujitolea kuwasaidia vijana na watu wazima waliotindikiwa au kuwa na
matatizo ya akili, na kujaribu kuona kama wanaweza kusaidiwa.
Basi safari yetu ikatupeleka hadi sehemu ambapo tulikuja
kuambiwa huyu jamaa ndipo anapoishi na hiyo nyumba tuliyoiona hapo ni nyumba
yake mwenyewe.
Ilikuwa nyumba nzuri tu, nyumba ya kisasa yenye kila kitu, ni
kwa uwani kulikuwa na bwawa la kuogelea la kisasa kabisa, wenyewe wanasema
nyumba hiyo ilijengwa kizungu.
Tulipofika hapo tukatafuta mtu wa karibu ndipo tukakutana na
huyo mzee, akajitambulisha kuwa yeye ni
baba yake mdogo, baba ambaye aliamua kumsaidia, zaidi ya huyo baba hakukuwa na mtu mwingine.
‘Kwahiyo wewe ni nani kwake..?’ nikamuuliza
‘Mimi ni baba yake mdogo,...’akasema
‘Ehe, hebu tuambie, ilikuwaje, je huyu jamaa hana wazazi
kweli, kama ulivyodai, kuwa hana baba, hana mama ,...na hana ndugu kweli, sasa
wewe imekujaje kuitwa baba yake mdogo wake....’tukamuuliza na mzee huyo
akatulia kama anawaza jambo, huku akimuangalia jamaa yetu aliyekuwa kalala,
baada ya kupokea kipigo cha watu, watu ambao walikuwa hawamfahamu, .
Bado hatujafanikiwa kupata wafadhili,na sehemu ya kujishikiza ili tuweze kumudu gharama... lakini nimeona nisikae tu, nitajitahidi hivi hivi kutoa visa vyetu, na mungu yupo pamoja nasi tutakuja kufanikiwa .
WAZO LA LEO:
Watiini wazazi wenu, waheshimuni wazazi wenu, na wasaidieni wanapofikia utu
uzima, na hata kama hawajiwezi kwasababu hii na ile, msiwanyanyapae, mkawatenga, mkawakataa, maana
hamjui jinsi gani walivyoteseka kwa ajili yenu, ogopeni radhi ya wazazi, kwani
akifikia hatua ya kuitoa, ujue radhi hiyo haina dawa, na si lazima atamke,
.....hala hala, vijana, halahala wapendwa, ogopeni radhi ya wazazi.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment