Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, June 2, 2015

NANI KAMA MAMA-85



Mtoto huyo hakuwahi kupatikana …au huyo mama wa mitaani hakuwahi kurejea tena hapo hospitalini, wote wakatoweka kwa namna ambayo hakuna aliyefahamu, na ikabakia ni historia kwenye hiyo hospitali, hata leo ukienda hapo hospitalini ukawakuta waliokuwepo kipindi hicho watakuhadithia hicho kisa  cha mama wa ajabu . Na huko kijijini ambapo mama huyo aliwahi kufika, wengi bado wanaamini kuwa huyo mama alikuja kutoka mbinguni na alipofika akamchukua mtoto wake, akatoweka naye….

Je ni kweli alikuwa mama wa mbinguni,

Tuendelee na kisa chetu

                                                  *****************
 Haya yote yakiendelea huko mjini na huko kijijini, kwenye bonde moja ambalo lilijulikana kama bonde la takataka, kulikuwa na banda bovu ambalo mchana huwa  halina dalili ya kuishi watu, lakini ikifika muda wa saa mbili hivi za usiku utakuta moto ukiwaka na kundi la watoto huonekana wakija hapo mmoja baada ya mwingine. 

Mchana kunakuwahakuna watu maana hakuna usalama , wakazi wa banda hilo huwa wanafukuzwa na mgambo, lakini usiku ndio sehemu nafuu ya kujisitiri…!

‘Mama leo hatukupata kitu, mgambo wametufukuza, na hata hatujala chochote..’ ilikuwa muda wa saa mbili na muda huo kila mmoja huleta chochote alichojaliwa nacho na humkabidhi mama yao ambaye baadaye kwa usawa hugawa hicho kilichopatikana na kama ni chakula, kinapashwa moto.

'Msijali hii ndio riziki yenu ya leo...mimi nilibahatika kupata hiki kidogo..'akasema mama huyo na kuwagaia hicho alichopata, hayo ndio maisha yao...

Katika hiyo hali watoto hawa walikuja kumkubali huyu mama kama mama yao mlezi, na walimpenda sana, na kujiona na wao wana mzazi katika dunia hii. Ikifika muda kama huo kila mmoja hupata nafasi ya kusimulia habari zake na kwanini alifika maeneo kama hayo.

Kwa leo, mmoja akahadithia jinsi mama yake alivyopigwa na baba yake hadi kupooza viungo, na hatimaye akafariki dunia, na baba akaona mke mwingine ambaye alimnyanyasa sana na akaona ni heri akimbie, ndio maana anaishi maisha ya majalalani na kuombaomba.

'Pole sana mwanangu hayo ndio maisha na wala usikate tamaa, muhimu tuwe na malengo maisha haya ya kuomba omba sio maisha, kwahiyo tumuombe mungu itokee neema, atokee mtu atuone kwa jicho la huruma, ili msome...mtafanikiwa tu watoto wangu, na wewe ilikuwaje, hebu tuambie kidogo...'akasema mama akimuangalia mtoto mwingine.

 Mwingine akasema yeye hajui hata huyo mama au baba yupoje, alikuwa akilelewa na bibi yake ambaye alifariki akabakia mwenyewe kwenye nyumba, nyumba ikaja kuchukuliwa na watu waliodai kuwa ni mali yao ya kifamilia na wale walioichukuwa wakawa wanapanga mbinu ya kumuua yeye , eti kwasababu akiachwa akikua atadai mali hiyo ni mali ya baba yake, basi akaona bora akimbie…

'Mhh, unapakumbuka hapo nyumbani?' akaulizwa

'Napakumbuka ndio, lakini naogopa kurudi tena..'akasema

'Siku utakuwa mkubwa utakwenda kudai haki yako, lakini kwa sasa tuhangaike hivi hivi...nina imani ipo siku mtapata, na muhimu ni kusoma..'akasema mama

Kila siku hupewa nafasi ya watoto wawili kusimulia kisa cha maisha yao, na wengine huchangia ni nini cha kufanya, ...visa vingi vilikuwa vya huzuni, na wakati mwingine hutia majonzi na mtoto muhadithiaji hushia kulia,  …mama ikawa kazi yake kuwapa moyo kuwa wasijali sasa kwani yeye yupo kwa ajili yao, …wasiwe na waswasi kwasababu wamepata mama wa kweli ambaye atawalinda na kuwalea, hata kama ni kwa shida.

Ndio ikafikia watoto hao kumkubali mama huyo  kama mama yao na kuishi naye kwenye banda hilo la maboksi na mabati waliolitengeneza wenyewe, na vitanda vilikuwa mifuko laini laini ya sulphate na matambara mabovu. Na walikuwa kila siku wanaamrishwa kuoga, hata kama wanaishi sehemu ya majalalani…!

‘Mnajua hata kama unavaa matambara usafi wa mwili ni muhimu sana…na usafi wa moyoni, usafi wa moyoni ndio muhimu sana, mnapokwenda huko msiibe, msiseme uwongo, muwe na adabu huo ndio usafi wa moyoni, ukiwa na mbaya, roho mbaya, mwizi, wewe ni mchafu wa moyoni....’ akawaambia mama yao huyo.

‘Lakini mama mbona siku zote unaficha sura yako, tutakuwa hatukujui siku ukijifunua, au likitokea tatizo,tutakuelezaje.. tunaomba tukuangalie sura yako, kwani sisi ni watoto wako…’ watoto wadadisi wakaanza kuhoji.

‘Wanangu niliwasimulia siku moja yule baba mkatili alivyo mpiga mkewe akishirikiana na mke wake mdogo, wakamtupa yule mama kwenye miiba, akachomwa na miba , na kuharibika usoni, kwani ile miba ilikuwa mikali, ilivuta ngozi ya uso…mnakumbuka hiyo hadithi..?' akawauliza

'Ndio tunakumbuka...'wakasema kwa pamoja

'Niliwaambia kuwa sura ya yule mama iliharibika sana na madonda yale yakawa kama yanaoza kwasababu hayakupatiwa matibabu, sura yake ikawa ya kustisha,..halafu aakpotewa na kumbukumbu, akawa hajui wapi alipotoka, halafu niliwaambia alifanya nini yule mama..?’ akawauliza watoto.

‘Alifunika nguo usoni, ili wasione sura yake…’ wakasema watoto.

‘Basi nikiwaambia kuwa yule mama wa hadithi ile yupo nanyi wakati wote mtasadiki..?’ akauliza yule mama.

‘Hatusaidiki, kwasababu ile ni hadithi tu…na hakuna mtu mnyama kama huyo ampige mkewe mjamzito, amtupe kwenye miiba…’akasema mtoto mmojawapo mkubwa, waliemuita Chokoraa.

 ‘Mumeonaeeh, hamuwezi kusadiki na kwahiyo hata mkija kumuona huyo mama, alivyo, mtamuogopa...kwa vile mimi nawapenda sana watoto wangu nataka muishi kwa amani,…sipendi mje mnikimbie, sipendi mniogope…’ akasema yule mama.

'Kwanini mama unasema hivyo, una maanisha huyo mama ndio wewe, ndio maana unajifunika uso wako?' wakamuuliza

'Naona mumechoka, nataka mlale mapema, kuna sehemu nimeipata tunaweza kuanzisha mradi wa mchicha...'akasema

'Khaa, na jembe tutapata wapi..?' mmoja akauliza

'Tutatumia hata mabati...mnakumbuka tuliokota majembe...yale yale yatafaa..'akasema mama

Lakini hata baada ya kusema vile, watoto wakawa kila siku wanadai wamuone mama huyo uso, watoto ni wadadisi sana,..japokuwa huyo mtoto wa huyo mama alipinga hilo sana, lakini wenzake wakamgeuka, wakataka kujua huyo mama yao wa kuwalea yupoje. Walipoona wameshindwa kumshawishi huyo mama kuwaonyesha uso kwa matakwa yake, wakapanga njama kuwa wamvizie akiwa amelala usiku wamfunue.

 Siku moja asubuhi, yule mama akiwa amelala,watoto watundu wakamvizia yule mama, na kwa haraka wakamvuta yule mama kile kitambaa kichwani, na kwa vile yule mama alikuwa kachoka na pilika pilika za mchana za kutafuta riziki alishindwa kujizua haraka na akabakia uso wazi. 

Hutaamini hata yule mtoto wake ambaye alikuja naye hapo, alijikuta akitimua mbio, hadi walipofika mahali wakakaa na kutulia kwa muda, halafu wakashauriana, wakaona wamefanya kosa,... ndipo wakarudi, waliporudi walikuta yule mama keshajifuniika, lakini walimuangalia mama huyo kwa mashaka…

‘Kumbe nyie hamunipendi watoto wangu, yaani mumeamua kunifanyia hivyo…’ akasema yule mama huku akiwa amekaa, watoto wale wote kwa pamoja wakamsogelea na kukaa pembeni mwake, wakimkumbatia na wakisema

‘Mama tunakupenda sana ila tulitishika,..na huyu ndiye aliyetushawishi tufanye ivyo ili tusaidiki hadithi yako…tulishaanza kuhisi umetuhadithia hadithi ya uwongo,..kumbe yule mama wa hadithi ndio wewe...’akasema mtoto mmojawapo mdogo alikuwa karibu sawa na mtoto wake.

Yule mtoto wake wa kumzaa akaja na kupiga magoti mbele yake akasema;

‘Mama nisamehe sana, nilishindwa kuwazuia, sikujua kuwa wamepanga mpango huu, mimi sikuwepo wakipanga kukufanyia hivyo... niliporudi nikakuta wameshakufunua, niliangalia kdogo..sikuona vyema nilipoona wenzangu wnakimbia na mimi nikakimbia...’akajitetea.

'Usijali....ila kamwe msiwe wakaidi, mzazi akikuambia jambo fulani usifanye, utii, maana yeye kaona lima madhara yake..'akasema huyo mama

 Watoto wakanywea na kuanza kumuonea huruma mama yao, wakikumbuka hiyo hadithi aliyowasimulia, kumbe kweli yule mama wa hadithi ndio huyo huyo aliyekuwepo mbele yao, na badala ya kumuogopa sasa wakazidi kumpenda na wakaahidi kuwa wakijaliwa kupata kazi watamsaidia na hata kumtafutia dakitari wa kumtengeneza sura yake.

‘Mimi mama kama nitajaliwa kusoma, ipo siku nitahakikisha uso wako unarudi kama zamani…’ akasema yule mtoto aliyemvua kile kitambaa yule mama usoni, yeye alikuwa na utundu wa udakitari.

                                    **************

‘Mwanangu hicho ndicho kisa , na natumai kuwa mengine unayajua kwani  kinaendelea wakati wewe ulishakuwa mkubwa wa kujua nini kilitokea, kwani maisha yetu pamoja yalikuwa kule shimo la takataka, na maadui wetu wakubwa walikuwa wale mgambo.

 Siku tulipoachana na wewe walitupeleka na kutufunga jela, na siku ya kunipeleka mahakamini nikaruka nje ya gari, ilikuwa karibu na mto, nikaponea chupuchupu kuliwa na mamba. Nikawa naishi maisha ya kujificha, hadi ile hali ikaisha.

Niliwaza sana wapi pa kumpata mtoto wangu, sikukuta tamaa, nikarudi mjini, na nikawa nafanya vibarua hapa na pale, …maisha yalikuwa magumu sana, kwani wakati mwingine mabosi wangu walinishurutisha kuvua kitambaa changu usoni, na hata kunilazimisha…wakiniona sura yangu wananifukuza kazi..ndivyo maisha yalivyokwenda, siku unapata siku unakosa, nikawa nalia kila mara nikimkumbuka mtoto wangu…

‘Miaka ikaenda, nikawa nakata tamaa, lakini kila  mara naota kuwa wewe bado upo hai, lakini wapi nitakupata ikawa ni shida. Na siku moja nikakutana na yule nesi wa hospitali, akanikumbuka na kunichukua kwake, …niliishi naye kwa muda mrefu. Yule nesi alikuwa keshaolewa na dakiatari mmoja, nikawaomba wanisaidie kumtafuta mwanangu, na wao wakaahidi kufanya hivyo.

 Siku moja ikaja taarifa kuwa umeonekana huku Dar-es-salaam na una kazi , halafu umeoa, nilifurahi sana siku hiyo, ndio tukamtuma mtu  aliywahi kukuona, kuwa akutafute mpaka akuone, na baadaye ndio ukaja ile mara ya kwanza kuniona,…unakumbuka uliponiona ilikuwaje,…na mara ya pili ukaja kunichukua na kunileta kwako. Hivyo ndivyo ilivyokuwa….

‘Ila mwanangu ninachotaka kukuelezea ni kuwa, katika dunia hii tenda wema sana, bila kujali ni nani unayemtendea wema, na watendee wema sana watoto, hasa watoto mayatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu,  kwani huwezi kujua nini bahati waliyopangiwa na mola wao. …’akasema mama.

Nilipokuwa India nilikutana na dakitari ambaye ni miongoni mwa walionisaidia, akaniambia yeye ni Mtanzania, ….na nilipoongea naye sana akanikumbuka kuwa yeye ndiye aliyenifanyia ule upasuaji wa kujifungua kwako,…na aliniambia huko kwenye hiyo  hospitali, walikuwa wakimuita dakitari kijana...nikakumbuka nesi jinsi alivyonisimulia kuhusu huyo dakitari, nilikutana naye wakati nimeshafanyiwa upasuaji, kwahiyo hakuwa na la kufanya ...kesheoa ana watoto.

‘Na jingine ambalo linasadikisha maneno niliyowatabiria watoto wale niliosihi nao majalalani ni kuwa mmoja wao ....alifanikiwa ndoto yake..'akasema

'Yupi huyo mama..?' nikamuuliza

'Huyu aliyenileta hapa ni miongoni mwa wale mliokuwa nao kule shimoni, tukiomba omba pamoja,..'akasema mama.

'Mbona mimi sikuweza kumkumbuka...?' nikamuuliza mama

‘Kwasababu kabadilika kweli...ila mimi sisahau wato ovyo, nilisahau kipindi akili yangu ilipopoteza kumbkumbu, lakini kumbukumbu ziliporejea nimekuwa nikikumbuka kila kitu, mimi nilimkumbuka ndio maana nikamwambia wewe na mimi mguu kwa mguu hadi hapa kwako, sikutaka akukumbushe yeye ni nani ila ipo siku mtakutana naye na tutaongea kwa kirefu mkumbuke maisha yenu ya kule shimoni;

'Ina maana hakukumbuka, mama kiukweli hata mimi kama ungekuja tu, bila kujitambuslisha vyema sijui…ila macho yako mama, …hahaha macho yako mama niliyakumbuka ....’nikasema na mama akacheka.

‘Yeye hakunikumbuka, kwani tulipokuwa tumefika hapa nilimuangalia na kumuuliza;

‘Hivi wewe hunikumbuku, akasema

‘Mhh, Mama mimi simkumbuki kabisa…’ akasema

'Nikamwambia anitizame vyema, lakini hata aliponitizama hakuweza kunikimubuka. Ni kweli sio rahisi maana tulipoachana pale shimono sikuwahi kukutana naye, na siku ile aliponifunua, aliniona kwa kipindi kifupi, aheri ya wewe mwanagu tumeishi nawe, umeniona sura yangu, ...'akasema.

'Sasa akakaufahamuje, na kukuamini kuwa ni wewe...?' nikamuuliza

'Baada ya kumuelezea mimi ni nani, aliniangalia na kujikuta akitoa machozi ya furaha, akanikumbatia na watu waliokuwepo hapo nje walishangaa, maana mtu tumefika naye, halafu tunasubiri mara wanaona hicho kitendo, walijikuta wakijiuliza maswali mengi.

Unajua yule dakitari aliniambia hivi, `mimi mungu kanijalia sana kukumbuka sura za watu, nawakumbuka wengi tulioishi nao tangu utoto, na hata nikukutana na watu mia kwenye mkusanyiko ninaweza kuwakumbuka wote…lakini cha ajabu wewe sura yako ilinitoka, …sikuweza kuikariri siku ile...’akaniambia

‘Ina maana alipofika hapa alinikumbuka mimi…?’ nikauliza

‘Ajabu ya mungu hakuweza kukumbuka na wewe, yeye anakufahamu tu kama mgonjwa wake, wewe hukuona jinsi alivyokuwa akikuangalia kwa mashaka, ila nilimueleza kuwa asikuambie kwanza kuwa yeye ni nani.... 'akasema mama

Leo atakuja...na nilitaka tukakutanie kule nyumbani kwangu, kwani kuna mtu mwingine naye atakuja,...mmh mwanangu kwa jinsi ulivyokonda wengi hawataweza kukumbuka ..unajua mwanangu unaonekana mzee kweli...nilivyokuacha na sasa umezidi kuzeeka, tofauti na umri wako....’akasema mama.

‘Najua hilo mama, ....ni matatizo haya yaliyonikumba, na wala sio ugonjwa kama watu wanavyodai,na mitihani, mitihani imekuwa mingi kwangu, nikawa kama mgonjwa, …nimekonda kama mgonjwa wa magonjwa mabaya, angalau sasa natazamika, nafikiri kama ungenikuta miezi kadhaa nyuma, hivi…hata sikumbuki lini nilipoanza kuumwa, na kupoteza kumbukumbu, lakini sasa sijambo, na nahisi nguvu zikinirudia mwilini…na kwa vile mama yupo nitanenepa haraka sana…’ nikasema huku namkumbatia mama yangu.

Mara ikapigwa hodi na aliyeingia ni yule docta sasa akiwa kavalia kiraia, akasalimia kwa adabu halafu akageuka kuniangalia mimi, akatabsamu, akasema

‘Ohh,... mshirika kumbe ndio wewe..ajabu kabisa…haaa, hata sijui niseme nini nisameheni sana....unajua sikukumbuka kabisa, nimekutibia, lakini sikuweza kukutambua, amebadilika sana.....’akasema huku akimuangalia mama halafu mimi.

'Ni kweli ni matatizo ...'akasema mama akionyesha uso wa huzuni.

Docta akatulia na kusema, `kweli mama ni mtu muhimu sana katika maisha, mimi sina mama kabisa, na…hata baba simjui, lakini mama huyu ndiye mama yangu , na hata katika kumbukumbu zangu za wazazi nimeandika jina la mama huyu, na nilikuwa kila mara namuwaza, wapi nitamuona, ili ile ahadi yangu niliyoiweka siku ile itimie…, na namshukuru mungu kuwa ile ahadi imetimia japo sio kwa moja kwa moja....’akasema

‘Ilitimiaje..?’ mama akauliza kwa mshangao

‘Katika watu waliosaidia kufanikisha safari yako mimi nilikuwa mmojawapo, na wakati huo nilikuwa sijajua ni wewe, ila niliposikia kuna mama mmoja yupo hivi na vile akili yangu ikanituma kuwa unaweza kuwa ni wewe, nikaanza kuhangaika,…nikawatafuta wafadhili,…na kumbe na nimefanya kile nilichoahidi…

'Ina maana ni wewe uliyewatafuta wale wafadhili...mimi nilikuwa sijijui, hayo nimeambiwa nilipofika huko...'akasema mama

'Ndio, niliongea na dakitari wa hapo, akaniambia kuna mama mmoja hajiwezi, na anahitajia kupelekwa India...nikamuuliza yupoje akaniambia,..mimi haraka nikakumbuka kampuni moja ya kuwasaidia watu wasiojiweza, kuna rafiki yangu moja yupo hapo, nikampigia simu, ....ndio wakafika, wakaja kuniambia wamafenikisha...'akasema

'Mimi tulipotoka pale, ..nilibahatika kusoma walikuja wafadhili wakatuchukua, na kutusomesha, nikaweza kufika hadi Ulaya.. hadi India nimefika,..ndio niliwasiliana na dakitari huyo aliyakufanyia upasuaji wa kichwa..lakini ajabu uliporudi sikuweza kukumbuka kuwa ni wewe...umebadilika mama...’akatulia akimuangalia mama

‘Siku walipokufanyia upasuaji nilimuuliza huyo dakitari kama kafanikiwa akaniambia kafanikiwa, na nikatingwa na shughuli nikawa sina mawasiliano na huyo dakitari, simu yangu ikapotea, iliyokuwa na namba yake basi ikawa mwisho wa kufuatilia kujua kinachoendelea. Muhimu tu .... tatizo lilitatuliwa kwangu ikawa ni faraja.. japokuwa sikuwa na uhakika kuwa ni wewe....’akasema huyo dakitari.

‘Rafiki yangu hunikumbuki…’akaniuliza lakini mimi kiukweli nilikuwa simkumbuki vyema

 ‘Ngoja nikukumbushe kidogo..unakumbuka siku ile kule jalalani yule ,… yule  mtoto uliyemfunua mama kitambaa alichokuwa kajifunga mama yako…yule mtoto aliyekuwa mtukutu kupita wote, yule ambaye mtu akiumia anakuwa tabibu wenu…humkumbuki vyema…’ docta akasema na kutabasamu..

‘Oh, mungu wangu, …ndio wewe docta mtukutu, na tabasamu lako la dharau nimelikumbuka, ina maana ndio wewe..mtoto mtukutu…’ nikasema na kuinuka pale nilipokuwa nimekaa na kumsogelea yule dakitari na kweli kumbukumbu za nyuma zikanijia na kumbkumbuka vyema, …oh nilimshika mkono halafu tukakumbatiana, na kujikuta sote tukilengwa lengwa na machozi, halafu wote tukamsogelea mama tukakumbatiana kwa furaha, na  badala ya kucheka kwa furaha kikapita kipind kifupi machozi yakitutoka.

                          **************

`Ndugu zanguni mnaokifuatilia na kukisikiliza hiki kisa, ni kisa chenye masikitiko, mitihani mingi, lakini mwisho wa siku neema ilituandama' akasema rafiki yangu akishika begi lake kutaka kuondoka, akaendelea kusema,

`Kwakweli  hutaamini, docta aliyekuja kumsaidia mama kufika India kwenda kuondolewa huo ule uvimbe ni mmoja wa watoto waliokulia majalalani, alipotoka pale jalalani siku ile ya kusombwa-sombwa na wanamgambo, alipata wafadhili , akasoma na akiwa darasani akaonekana ni kijana mwenye akili za ziada akawa mmoja wa vijana waliopelekwa nje kupata masomo ya utibabu na akawa dakitari bingwa.

Akiwa katika kazi ya hiyo akapata nafasi ya kwenda India kwa mkataba maalumu na hospitali moja huko, lengo lake likiwa ni kuendeleza kipaji chake. Baadaye akarudi nchini kulitumikia taifa, na moja ya malengo yake kichwani ikawa kuwasaidia akina mama , watoto mayatima, na wasiojiweza.

Kwahiyo aliposikia kuna mama mmoja, anahitajia msaada, haraka akaongea na watu wenye kazi hiyo na safari hiyo ikafanikiwa..na huko akawasiliana na madocta kutafuta bingwa wa kumrekebisha huyo mama sura, kilichogomba ikawa ni pesa, akawa anahangaika kutafuta wafadhili kabla mama huyo hajarudi, lakini ikawa ngumu kweli, na simu ikapotea na kupoteza namba ya dakitari anayemfahamu kwa kazi hiyo, lakini hakukata tamaa!

Alipopata wafadhili wa humu humu nchini ili huyo mama asirudi bila kurekebishwa sura yake, akaja kuambiwa huyo mama keshafanyiwa, kwahiyo haina haja tena, basi akashukuru, hakujua kuwa atakuja kukutana na huyo mama kwa njia hiyo... na hakuwa na uhakika kuwa huyo mama anayemsaidia ndio yule yule, kwa hisia tu alihisi kuwa ndio yeye...

‘Basi mwanangu ya mungu mengi wakati nimereeja kutoka India, nikiwa kwenye nyumba ndogo, ..sikuwa naishi kwenye nyumba hiyo kubwa ninayoishi sasa…hii ya sasa ilikuja kwa miujiza yake mingine..’akasema mama

‘Ipi tena..’?’ nikauliza

Siku hiyo nilikuwa nimechoka sana, nikaamua kulala, mara nikaamushwa, na huyo docta aliyekuwaa akinisaidia, akaniambia kuna mtu mmoja kamleta baba yake kashikwa na kichwa kibaya na anaogopa kuwa isije ikamfikisha kwenye kiharusi.

Nikatoka, nikasalimiana naye, mimi nikamkumbuka, lakini sikutaka kumuelezea mimi ni nani kwa muda ule, nikamsaidia baba yake, na bahati nzuri baba yake akapona yale matatizo ya kichwa..., yule baba alipoambiwa ataje anachokitaka akasema..mtoto wangu atakupa nyumba yake moja... anipe mimi…mtoto akabakia mdomo wazi.

'Baba....mbona...'akawa analalamika

‘Mwanangu unanipenda baba yako…?’ baba akauliza na yule mtoto ambaye nilishamfahamu nakumbuka kwenye kisa chake, alisema aliishi na mama yake maisha yakawa magumu akakimbia kutafuta maisha ila aliahidi kuwa siku akimpata baba yake, hataweza kumtelekeza, kwani baba yake alikamatwa kwa kesi ya uwongo akafungwa na kosa alifanya yeye mtoto....ni kisa kirefu tu, siwezi kuwahadithia , ipo siku atawahadithia mwenyewe.

Na alipojaliwa kupata utajiri akamtafuta baba yake hadi akampata…’akasema mama
 Basi walipofika hapo walikuja na gari aina la landcruser, wengi wanamfahamu nikasikia mmoja akisema;

‘Huyu jamaa ni tajiri sana, anamiliki kampuni ya madini, na ameingia ubia na wazungu,…mimi nilipomtupia jicho tu, nikamgundua..’akasema mama

‘Ni nani huyo..?’ nikamuuliza

‘Ni yule aliyekuwa kiongozi wenu kule mjalalani, …ukimuona sasa hivi alivyobadilika huwezi kumtabua vyema…’akasema mama

‘Alikuwa akiitwa nani…?’ nikamuuliza mama

‘Chokoraa’ akasema mama…aliposema mama mara nje tukasikia gari likisimama, na haikuchukua muda akaingia jamaa mmoja kavalia suti safi na kitambi juu, akasogea pale alipokaa mama akafanya kama anapiga magoti, akasema;

‘Mama nimefika ofisini kwako nikakukosa, na nimekuja na habari nzuri, tunaweza kumpata mtoto wako haraka iwezekanavyo…’akasema

‘Mtoto wangu..?’ mama akauliza kwa mshangao

‘Ndio...ulisema bado unamtafuta  yule mdogo wetu, nimekutana na docta mmoja hivi anafanyia kazi muhimbili wakati naongea naye nikamuulizia kama aliwahi kufika jamaa mmoja nikamuelezea jinsi ulivyosema ndugu yetu huyo yupo hivyo, akasema mbona huyo jamaa anamfahamu..’akasema

‘Ukaambiwa yupo wapi?’ mama akamuuliza sasa akionyesha uso wa kutabasamu

‘Aaah, kasema, jamaa aliumwa sana akawa kama kapotewa na kumbukumbu kwahiyo hawezi hata kukumbuka wewe mwenyewe, maana hata yeye mwenyewe hajikumbuki, kwahiyo, mama, nimepanga nije nikuchukue,twende kwa huyo dakitari atupeleke hapo alipo tutampata mama…ni lazima leo au kesho apatikane..’akasema huyo jamaa, na mama akageuka na kuniangalia, akasema

‘Huyu ndiye Chokoraa…’akasema na huyo jamaa akageuka na kuniangalia mimi, hakuonyesha dalili ya kunikumbuka

Docta aliyekuwa kakaa pembeni akasimama na kumuelekea huyo chokoraa akasema ;

 ‘Mhhh, ndio nyie mnaopata utajiri na kuwasahau wenzenu, nilitaraja baada ya kufanikiwa ungewatafutwa wenzeko na kuwawezesha...'akasema

'Mhh, kwani wewe ni ....?' akauliza akimgeukia mama

'Umemsahau, kichwa chako kigumu kukumbuka.....'akasema mama

‘Mhh, kidogo naanza kuikumbua hii sura…’akasema.

‘Mtundu, cha utundu….’akasema docta na Chokoraa akageuka kumuangalia mama, halafu akageuka kuniangalia mimi, akaniangalia kwa makini halafu akamgeukia docta na kusema

'Yaani ndio wewe....'akamshika mkono docta na kuutingisha kwa nguvu, halafu akanigeukia mimi, akaniangalia kwa makini

‘Hayo macho,…mama huyo…hebu niambie ukweli…’akasema akimuangalia mama

‘Huyu ndiye ndugu yako tunayemtafuta…’akasema mama, na Chokaraa akabakia kaduwaa…akaniangalia kwa muda halafu akatikisa kichwa akionyesha kusikitika, akasema

‘Pole sana..usijali, siku hizi kuna ushauri nasaha..utabadilika, na mimi nitahakikisha unakuwa kama mimi hata watu hawatajua kuwa unaumwa..’akasema

‘Haumwi bwana,..ni kukonda huko…ni shida tu…huyu ni mzima, shida zikiisha atakuwa kama wewe…’akasema mama

‘Una uhakika..mama..kwani siku hizi huu ugonjwa ni siri, ilikuwa zamani!...’ akasema Chokoraa

‘Muulize docta huyu hapa…’akasema mama akimuangalia `cha utundu…’ na chokoraa akageuka kumuangalia ‘cha utundu’

‘Ina maana wewe ni docta umetimiza dhamira yako,maana kule wewe ndiye ulikuwa docta wangu…maana nilikuwa sikosi kuumia,..hahaha…'akacheka na kukumbatiana kwa furaha.

'Na huyu mziwanda...ooh, kwanini ukonde hivi, wakati sisi tupo, ..unajua utajiri hauna maana mtu anakufa anauacha, lakini matendo mema, hubakia milele na ni akiba ya baadaye, mimi sasa ni tajiri, lakini najiona sina maana, ...furaha yangu ni kusaidia wenzangu..mimi nilijua mziwanda kaukwaa..’akasema na wote wakaishia kucheka kwa furaha na kukumbatiana.

 Chokoraa kama alivyoahidi naye akatimiza ile ahadi yake yakutuwezesha, akaniingiza kwenye kampuni yake, nikawajibika kwa muda, na nikiwa humo nikafanikiwa kuanzisha kampuni yangu mwenyewe, na sasa namshukuru mungu, kuwa na mimi ninaitwa mkurugenzi, nikiwa na wafanyakazi wanaonitegemea, na jambo la furaha ni kuwa nilimpata mke ambaye ndiye aliyejali kipindi cha dhiki.

‘Ni huyo nesi aliyekuwa akikuuguza ulipokuwa hujijui..?’ tukamuuliza

‘Ndio huyo huyo….’akasema msimuliaji.
           
‘ Mke wangu wa zamani, alionekana mara moja, na alikuja kunikabidhi mtoto wangu akidai kashindwa kumlea, alikuwa katika hali mbaya sana, ingawaje alidai kuwa kaolewa na anaishi kwa raha, sikutaka kumfuatilia maisha yake tena! Nilifanya juhudi ya ziada kumbadili mwanangu mpaka akaelekea, sasa yupo sekondari kidato cha sita…hicho ndicho kisa changu ambacho nakimalizia kwa kujibu lile swali nililowauliza mwanzoni kuwa;

`Nani kama mama…?’ nami ninawajibu hivi `hakuna kama mama..’ mama ni mtu wa pekee katika maisha yetu, ukibahatika kuwa naye hadi ukapata kazi ushukuru sana, katu usimsau, kwani wao ni watu wa pekee katika maisha na makuzi yetu…, mama ni mama yako tu, baba unaweza ukabambikiwa lakini sio mama. Ahsanteni sana ,

Huu ndio Mwisho wa kisa chetu, kama kuna maoni shukurani tuma kwa e-maili hii hapa: miram3.com@gmail.com


WAZO LA LEO: Ukipata ukala ukashiba na kusanza kumbuka kuwa kuna ambaye anakitafuta hajapata, ana njaa hana cha kula,..hajui akalale wapi…masikini, mayatima, wasiojiweza, wagonjwa wote wanakuhitaji. Na pengine umasikini wao umetokana na ubadhirifu wako,..ulipewa cheo ukafisidi, ukajijenga kwa jasho lao, leo wanataabika wewe unawasuta, unawadharau,…tukumbuke kuwa dunia hii ni mapito tu, ipo siku tutarejea kwa mola na dhuluma uliyotenda, utakuja kuulizwa, hujachelewa, toa ulicho nacho uwasaidie wasiojiweza,..usidhulumu, na watendee haki waliopo kwenye dhamana yako.

Ni mimi: emu-three

No comments :