Siku ya pili mama alifika akamalizana na
mfadhili wangu na hatukuruhusiwa kuondoka moja kwa moja, mfadhili alikuwa na
hamu ya kusikia mengi kutoka kwa mama wapi alitokea, na mama akasema;
‘Mengi ya maisha yangu ni ya kawaida japokuwa
yamejaa mitihani mingi, na maisha yangu mengine nisingelipenda kuyaongea kwa
kila mtu, ila kwa vile mtoto wangu kaniuliza swali akitaka kujua pale
nilipoishia wakati nilipomhadithia kuhusu maisha yangu…nitaongea kidogo kabla
hatujaondoka…’akasema mama na kutulia akijinyosha kwenye kiti.
‘Kiukweli historia za maisha yangu, zilizopita zinaweza kufufua vidonda vilivyoanza
kupona, lakini wakati mwingine ni ibra , ni
taswira ya kukuonyesha wapi ulipotoka, na wapi unapokwenda…kiukweli
maisha yangu ya nyuma yamejaa sana simanzi , na ukiyawaza sana mwishowe
unakaribisha hasira za visasi, mwanangu unaonaje tukiyasahau yaliyopita tukaganga
yajayo…?’Mama akasema
‘Ni kweli mama, lakini mimi natamani
niyasikie, kwani ulishanianzishia maelezo na ukafika sehemu ambayo ulishindwa
kuendelea pale ulipo-poteza fahamu, naomba mama uendelee tu kuanzia pale kama
hutojali..’
nikamsisitizia mama. Na mama akaniangalia
tena , halafu akaanza kunihadithia pale tulipoishia.
Tuendelee na kisa chetu…
***********
‘Mwanangu, siku ile nesi na dada yake walijikuta wakifurahia
ujauzito ambao kwao ulikuwa kama mgumba kupata mtoto, kiasi kwamba walijikuta
wanasahau kile kilichokuwa kimewaleta
pale, na docta bosi wa nesi alipoangalia saa, akashituka na kusema;
‘Mhh, muda umekwenda, mimi natakiwa kurudi mjini….’akasema
‘Docta, kwanini usilale ukaondoka kesho….’akaambiwa na mama mwenye
nyumba
‘Hapana, ni lazima niondoke, ila nesi anaweza kubakia na mtoto, na
anaweza kukaa hapa akarudi kazini jumatatu, kwa vile leo ni Ijumaa..’akasema
docta.
‘Mhh, nashukuru sana docta, maana furaha niliyo nayo sitaki
kuondoka hapa haraka..’akasema nesi
‘Lakini sasa wasiwasi wangu ni huyo mama, anaweza kufika hapa
naomba akifika hapa msimkabidhi huyo mtoto kwanza, tunahitajia mambo yaende
kisheria, mtoto atakabidhiwa kwake, baada ya kuhakiki mambo yote muhimu, na
hilo litafanyika kule kule hospitalini..’akasema docta.
‘Mhh, jamani ina maana bado kang’ang’ania kwanini sije tukaongea,
mtoto tukaishi naye hadi hapo atakapokuwa mkubwa, na mimi mbona sijamini kuwa
mtoto huyu ni wake..’akasema mama mwenye nyumba.
‘Ni wa kwake bwana…’akasema baba mwenye nyumba kwa sauti kali.
‘Una uhakika gani…?’ akauliza mkewe
‘Nimeshakuambia hivyo na unielewe hivyo, huyu mtoto arudishwe kwa
wazazi wake, ..’akasema baba mwenye nyuma kwa ukali.
‘Haya jamani mimi naondoka ila kama nilivyowaambia, muhakikishe
huyo mtoto anakuwa salama na anarudi kule kwa ajili ya taratibu za kisheria,
mengine tutaongea huko na huyo mama, kama atakubali, basi tutaona jinsi gani ya
kufanya..’akasema docta
‘Mtajua wenyewe la kufanya, ila mimi kama nilivyowaambia sitaki
kujiingiza na maswala ya hao watu, kwangu hapa wapaone kituo cha polisi, …’akasema
baba mwenye nyumba na nesi akabakia akimuangalia kwa mshangao, docta kwa vile
walishaongea na mtu huyo hakuonyesha kusangaa sana.
Basi docta na mlinzi wake wakaondoka kurudi mjini, wakitarajia
kuwa watakutana na huyo mama huyo hospitalini, na walipanga wakikikutana naye
watamshauri afanye subira ili taratibu za kisheria zifanyike ikiwemo vipimo
vingine, na hata watu wa sheria wawepo ili kulimaliza hilo tatizo kabisa.
Huku nyuma nesi akabakia na ndugu zake wakifurahi na mtoto naye
akifurahia kuwaona wazazi wake wa kufikia yeye alijua hao ndio wazazi wake.
***********
Docta wakafika mjini hospitalini, na walipofika hospitali wakakuta
taarifa kuwa yule mama alirudi hapo hospitalini, na alipofika hakuonyesha ule
ukali aliokuwa nao mwanzoni, alikuwa mpole na mstaarabu sana, akauliza mtoto
wake yupo wapi, jibu alilopewa ndilo lilimbadili hiyo hali na kuanza kucharuka
tena
‘Na nesi na mwenzake wapo wapi?’ akauliza kwa hasira
‘Wamekwenda huko kijijini kwao…’akaambiwa
‘Na mtoto wangu sio…wanataak kumrudisha huko, sikubali…’akasema na
hakuna aliyetaka kuongea naye sana, yeye akageuka kutaka kuondoka, na docta
aliyekutana naye akamwambia
‘Mama unajua hujaruhusiwa kuondoka, hujapona, …..’akaambiwa
‘Hivi mnafikiri kama ingelikuwa ni nyie, mngefurahia hili
mnalonifanyia mimi, au kwa vile ni mimi, au kwa vile mnaniona
nimechanganyikiwa, …’akasema
‘Sio hivyo mama..’akasema docta
‘Hivi kweli mnapenda mama atengane na mtoto wake hivihivi,
kirahisi tu…sikubali, nitampata mtoto wangu mpende msipende…subirini…mtaona
kitakachotokea, sitaki ubaya na mtu, na sitaki mtu aumie tena,….’ Akasema na
kuanza kuondoka, na docta hakutaak kusumbuka na huyo mama tena, na jinsi
alivyoondoka, wengi walijua anaelekea tena huko kijijini.
‘Kwahiyo mkamuacha akaondoka..?’ akauliza docta huyu aliyetokea
kijijini
‘Ndio tungefanyaje…unajua huyo mama keshapona, keshajijua, na hali
aliyo nayo, sio ya kumlazimisha, ni bora tumuache tuone anachotaka kukifanya ni
nini..’akasema docta mwenzake.
‘Ok, sawa kwa vile nilishaongea na nesi na ndugu zake, sizani kama
akifika huko kijijini ataleta fujo, muhimu n kuwaatarifu tu wajiandae kwa ujio
huo…’akasema docta
Siku ya Jumamosi kukawa na mawasiliano kati ya docta bosi na
nesi, akitaka kujua kama huyo mama kawasili huko kijijini, na nini kinaendelea
huko ! Cha kushangaza taarifa zilizofika ni kuwa yule mama hajaonekana huko
kijijini, na wao walijua labda huyo mama amekubali kusubiri huko hospitali …!
Taarifa hiyo ikawaacha mdomo wazi madocta na watendaji wa hiyo
hospitalini, na kuwaacha kwenye mashaka wakijiuliza huyo mama atakuwa kaenda
wapi maana bado alikuwa ni mgonjwa wao!
‘Au kagundua kuwa sio yeye na mtoto sio wa kwake, na kaamua
kuishia!..mimi bado nina mashaka sana na huyo mama , mimi simuamini bado…?’
akasema nesi
‘Lakini dalili na vielelezo vyote kama alivyotupa docta kijana vinaendana
na yeye, sasa sidhani kama kuna mama mwingine zaidi yake labda…kama yupo mama
mwingine mwenye sura kama hiyo…labda, …mimi naona tungoje, kama ndio yeye
lazima atarudi tu, kama sio yeye basi tutakuwa na kazi ya ziada, maana
tumemuachia mgonjwa kuondoka bila ruhusa na pili ni kumtafuta huyo mama halali
wa mtoto, vinginevyo, inabidi uwaombe ndugu zako waendelee kumkubali huyo mtoto
kama mtoto wao..’ akasema docta bosi wa nesi.
‘Hilo la ndugu zangu kumchukua huyu mtoto kama wao, sidhani kama
litawezekana kwasababu shemeji yangu anasema akimwangali huyo mtoto anamkumbuka
mbaya wake, kwsababau wanafanana sana..si unaona hiyo nimejaribu kuongea naye
kwa marafu na mapana, kiukweli shemeji yangu hataki kusikia lolote kuhusu huyo
mwanamke na familia yake’ akasema nesi.
‘Sasa kwa vile shemeji yako anamjua baba wa huyo mtoto na kijiji
kwao, kwanini asifanye mipango ili baba halali wa mtoto akapatikana..tuje hapo
na watu wa uslama mgu kwa mguu hadi kwa huyo baba halali?’akauliza docta.
‘Docta hawa watu wawili hawawezi kuelewana abadani, na kama kuna
kitu ambacho shemeji yangu hakitaki, ni kukutana na huyo mwanaume,….anasema
huenda wakikutana kutazuka fujo ambayo haijawahi kutokea,…tumeongea naye na
amaesema ili kuwe na amani, basi tusiongee maswala ya hao watu…kiufupi hilo la
huyu mtoto kubakia hapa halitawezekana aliniambia alishakuelezea msimao wake…’
akaseme nesi.
‘Aliniambia lakini mimi naona ni jaziba tu, kama tutamkalisha
chini na busara zikatumika, yeye anaweza kuwa msaada mkubwa kwetu, hasa kuipata
familia ya huyo mama, mume wake….’akasema docta
‘Je huyo mama ameshamkumbuka mume wake?’ akauliza nesi
‘Hajataka kutuambia, …na nahisi hataki kuliongelea hilo, japo
anadai hakumbuki…’akasema docta
‘Anadai mna uhakika kuwa sasa amaeshakumbuka kila kitu..?’
akauliza nesi
‘Kwa hali aliyofikia tunahisi hivyo, ila hatuwezi kumlazimisha,
sisi tulitaka kwanza tulimalize hili la mtoto, yeye akutane na mtoto wake tuone
athari zake, …..ni lazima kutakuwa na mabadiliko makubwa watu wawili hawa
wakikutana mama na mtoto wake..’akasema docta
‘Basi mimi nitajaribu kuongea tena na shemeji na dada tuone
watasaidiaje kabla sijarudi huko, lakini nijuavyo msimamo wa shemeji hauwezi
kubadilika…’akasema nesi
‘Ongea nao kwanza tuone, na jingine ni jinsi ya kumtoa mtoto hapo
nyumbani yeye anafahamu kuwa hao ndio wazazi wake, ni muhimu umueleze shemeji
yake atumie hekima, asija akaonyesha chuki za wazi kwa huyo mtoto,…natumai
ataelewa..’akasema docta
‘Haya baadaye…kama huyo mama ataonekana nitakupigia…’akasema nesi
na kukata simu
**************
Mazungumzo ya docta na nesi kwenye simu yaliishia bila kupata
ufumbuzi wa maana, iliyobakia ni kusubiri tu nini kitatokea , kama huyo mama
atatokea tena au kuna mama mwingine atakuja kujitambulisha yote kwao itakuwa
heri, lakini lazima utaratibu ufuatwe ili, isije ikaleta mgongano baadaye…!
Siku ya Jumamosi ikapita, na siku ya Jumapili ikaingia.
Ilikuwa siku ambayo wanafamilia walipanga kukutana na siku
hiyo waliipangia kuwa iwe siku muhimu sana kwao, waliamua kufanya tafrija ndogo
ambayo walikuwa wameipanga awali wakawa wanaiahirisha kwasababu hizi na zile,
na hata kuna muda waliona labda tafrija hiyo ifanyike baada ya kujifungua,
lakini wakaona siku hiyo ya Jumapili inafaa kwao kwa vile wanafamilia
wamekamilika, basi wakaitayarisha kwa harakaharaka.
Pamoja na hayo, waliona ni muhimu kama wanafamilia kukutana na
kubadilishana mawazo, wakaitana wanafamilia wote waliopo karibu, na bahati
nzuri , wanafamilia wengi walikuja , na ikaandaliwa tafrija fupi ya kumshukuru
mungu kwa mama aliyekuwa hakutarajiwa kupata mtoto , sasa ni mja mzito, na
mambo mengine ya kifamilia yakafanyiak kutoka na taratibu na mila zao, na nesi
akawa anawaza kichwani, hapo ni mimba tu, jei siku akizaliwa huyo mtoto sijui itakuwaje…
Pilika pilika zikaanza, majirani wengine wakajumuika na muongeaji mkuu
akaelezea ni nini hasa dhumuni la ile tafrija fupi, hakuelezea kwa undani zaidi
, alisema ni tafrijaya kumshukuru mungu kwa kumwezesha mwanafamilia kupata kile
alichokiomba kwa muda mrefu, na pia ni tafrija ya kuwakumbuka waliotangulia, na
zaidi ya hayo ni kukutana kama wanafamilia kujadili mambo yao…
‘Lakini mbona hawajatuweka wazi , kuwa walichokitaka wamekipata ni
kitu gani au ni uja uzito wa huyo mama, lakini mbona huyo mama ana mtoto tayari
kwanini waseme walikuwa wakitafuta na wamepata, …’watu wakaanza kunong’ona
‘Labda aliataka mtoto wa pili…’mwingine akasema
‘Lakini kuna kitu mimi nilisikia…’akasema mwingine
‘Mumesikia nini…?’ wakaulizana
‘Kuwa huyo mtoto sio wao, na mama yake huenda ni yule mama
aliyekuja kudai mtoto …’wakasema
‘Una maana yule mama aliyechanganyikiwa,….’wakasema
‘Ndio yeye….yawezekana kweli..’wakazidi kuongea
‘Lakini yule mama alikuwa akidai kwa wengi kuwa mtoto huyu mara
yule ni wake…’wakasema
‘Sijui kwanini tusiwaulize wenyewe….’wakasema lakini hakuna
aliyekuwa na sababu za kwenda kuuliza, wakawa wanaendelea na shereeh na kile
aliyeulizwa hakuwa na jibu zaidi ya wahusika wenyewe ambao ni mume na mke na
nesi.
Wakati watu wamejimwaga na vyakula vinaliwa, hakuna aliyekuwa na
wazo lolote zaidi ya ile sherehe, dada wa nesi na nesi walikuwa wamevalia sare,
na mume mtu alikuwa kavalia suri yake safi wakawa wamekaa pale mbele kama
wahusika wakuu, picha za kumbukumbu zikapigwa.
‘Mwiteni mtoto wetu naye apate picha ya kumbukumbu…’ akasema
dada wa nesi, akiwa na dada yake na hata nesi akasema hivyo. Hoja hii aliipingwa
na shemeji mtu, na shemeji mtu alipoona wenzake wanasisistiza, akaona isiwe
taabu yeye akaondoka pale walipokuwa wamekaa na kujitenga.
‘Mnaona niliwaambia… huyo mtoto sio wa hiyo familia kwanini yulebaba
hataki kupiga picha pamoja na yule mtoto, mtoto kaitwa yeye kajitenga..’watetesi
wakazidi kuongea
Kiukweli katika hizo siku tatu baba wa hiyo familia alikuwa na
wakati mgumu, hakupenda kabisa kushinda humo nyumbani, akawa anarudi usiku sana
akiwa na uhakika yule mtoto kalala, na yule mtoto alikuwa akilala na nesi na
ikitokea wakakutana na huyo mtoto hutafuta visingizio vya kumtoroka, licha ya
kuwa mtoto kila mara alikuwa akimlilia na kumuita `baba, baba…’
Siku hiyo ya jumapili hakuweza kumkwepa huyo mtoto, na alipoona
mtoto anamtaka sana wakae pamoja moyo wa
huruma ulimuingia, basi kwa kujibaragua akamchukua mtoto na kujifanya
anamjali,…lakini alipomtizama usoni ,…mmh, alijikuta akimweka chini …na akatafuta
mwanya wa kutoka hapo nyumbani , na kwenda zake nje kukutana na marafiki zake.
Mkewe alimshauri sana kuwa anachofanya siyo jambo la kiungwana,
kwani yule mtoto hana kosa kabisa, yeye kama mtoto hajui kabisa nini
kilitokea…mumewe anamjibu kuwa yeye hajui machungu gani aliyoyapitia , na mtoto
huyo humtonesha donda ambalo lilishaanza kupona! Na mazungumzo hayo hayaishii
vyema, mume mtu anaamua kundoka na kutembea tembea akisubiria muda huo wa
sherehe.
Basi mtoto akaambiwa aitwe ili picha ya pamoja ipigwe
‘Mtoto haonekani…’ akasema dada mmoja ambaye alitumwa kwenda
kumchukua huyo mtoto nje alipokuwa akicheza.
‘Umemwangalia huko alikokuwa akicheza na wenzake..’ akauliza nesi
‘Kote nimeangalia na nimewauliza wenzake wanasema hawajui wapi
ameenda..’akasema
‘Atakuwa kaenda wapi naye hata tabia ya kutembea mbali na hapa
nyumbani..’akasema mama wa kufikia alipopewa hiyo taarifa.
‘Alisema anakuja kunywa maji, na alipoondoka hajarudi…’akasema
mtoto mwingine.
‘Mimi nilimuona akiangalia ng’ombe aliokuwa wakipigana kule..’akasema
mtoto mwingine …’ ilimradi kila mtoto alisema lake. Ikawa shughuli kumtafuta mtoto
kaenda wapi. Mtoto hakuonekana, shughuli ikaingia mtafaruku.
.
‘Sasa tutafanyaje maana hii sasa ni kesi akija mama wa mtoto
tutamwambia nini…na wakuu wangu walishanikabidhi hili jukumu, si ndio kufukuzwa
kazi, ..hili ni balaa gani tena…’ akaanza kulalamika nesi.
‘Bwanae, naona unataka kutuharibia tafrija yetu, niliwaambia huyo
mtoto sio damu yetu atatuletea mabalaa hamtaki kusikia, angalieni sasa, mimi hili nilishaliona kabla, tangu huyo
mtoto aletewe hapa, kila mara linazuka jambo la utata..mnaona sasa..’akasema
baba mtu
‘Usiseme hivyo baba mtarajiwa, hapa cha muhimu ni kuhakikisha huyo
mtoto anapatikana hiyo ni dhamana tulikabidhiwa, …’akasema mke wake.
‘Mimi simo kabisa, na wala msinishirikishe, maana huyo mwanamke
balaa akija hapa atanizukia mimi na kuniletea mambo nisiyo yataka…’ akasema shemeji
mtu.
‘Hili ni letu sote kwasababu mtoto huyu aliachwa hapa kwenye
nyumba yako, huwezi kulikwepa cha muhimu ni kusaidiana jinsi ya kumtafuta , na
bora tuwape taarifa polisi…’ akasema mke mtu.
‘Nani aende polisi, yaani nipoteze muda wangu kwa ajili ya…mtoto
ambaye katelekezwa kwangu wakati wazazi wapo…hivi mnamjua baba yake, ni tajiri
wa ng’ombe….’ Aksema mume mtu na kabla hajamaliza simu ikaiita, na nesi
alipoitizama simu yake akakuta anayeiita ni docta, akasogea pembeni huku akiwa
na wasiwasi atamwambiaje huyo docta bosi wake ambaye alishachukua dhamana ya
usalama wa huyo mtoto!
NB: Kwa leo naishia hapa maana nahangaika kutafuta wadhamini wa
kuweka matangazo ili tuweze kwenda sawa
WAZO LA LEO: Ulimi ni kitu cha kuchunga sana, kauli
tunazozitoa kwa watu tujaribu kuwa makini nazo, sio kwa vile unajiweza , au
wewe ni kiongozi bosi, unaona sawa vyovyote utakavyoongea, hapana ukubwa wako ,
utajiri wako, ubosi wako hauna maana kama utakuwa na kauli chafu, roho mbaya na
dharau.Tukumbuke kuwa hekima busara ndiyo inamjenga mtu aoanekana wa maana
mbele ya wengine.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment