‘Hivi kweli mimi nina mke, mke wangu yupoje, anafananaje, je
ananipenda…naona atafurahi sana akiniona nimepona, au…oh nahis huenda tulikuwa
na furaha sana,’ yalikuwa maswali mengi kichwani, na sijui kwanini nilikuwa
nikiwaza hili la mke sana, kuliko mambo
mengine.
Nilifikia kuwaza jinsi tulivyokutana tukapendana,….tukafikia
kuoana..nikajenga taswira nyingi za huyo mwanamke kuwa ni mrembo sana….nikajaribu
kufikiria sura nzuri zaidi,…na mimi mwenyewe kujiona kijana mtanashati…yaani
mawazo mawazo….
‘Sijui sasa mke wangu atakuwaje…kakonda, hapana, ni ….mmmh….’nikajikuta
naongea peke yangu.
Nikawa nasubiri kuwaona hao
jamaa zangu ambao niliambiwa wanakuja kila siku, nakumbuka kuna watu huwa
wanakuja, tunasalimiana na wanandoka, lakini sijui ni akina nani, labda ndio
hao jamaa zangu sikuwa na uhakika kwa kweli.
Siku hiyo niliwaza sana, nikiwa na matumaini ya kuwaona hao ndugu
zangu, nikiwa na matumaini ya kwenda kupaona hapo nyumbani kwangu, sikuwa najua
ni wapi, na kama nina nyumba au nimepanga,…
Wakati nawaza haya nikashikwa na usingizi, na ndani ya usingizi
nikamuona mwanamke mmoja akiwa, kavaa nguo zinazomeremeta, alikuwa kakaa kwenye
kiti, halafu anakunywa kinywaji kweny gilasi, alikuwa mwanamke mrembo wa
kuvutia, na alionekana hataki kuguswa na takataka, kwani kila mara alikuwa
akijiangalia na kila akiona kitu tofauti anakifuta,…alikuwa anameta meta
Baadaye nikaona hali inabdilika, ile sura yake ikawa inabadilika
taratibu, na ilna akawa anaingiwa na madoa ya uchafu , na kila kiona hivyo
anahangaika kuyaondoa hayo madoa lakini yakwa yanamjia kwa aksi, akawa anabadilika
hata sura, na baadaye ile rangi ikawa sura ya kutisha ajabu, mdomoni akawa
anatoa uchafu, ….ulikuwa unatoa harufu mbaya ajabu. Na alipofunua meno yake
yakawa ya kutisha kama ya shetani…
Nikawa sitaki kumtizama yule mwanamke, naye anakazania nimtizame
kile anachotoa mdomoni, na mara akatokea mwanamke mwingine akiwa kajifunika
usoni, alikuwa akimtizama yule mwanamke kwa macho ya huruma, halafu akanitizama
mimi, na akawa kama ananionya kuwa huyo mwanamke atanilisha uchafu wake nisogee
pembeni, nikawa najaribu kusogea lakini sikuweza kuinua hata mkono.
Yule mwanamke anayetoa uchafu mdomoni, akacheka kicheko cha
dharau, huyo mwanamke mwingine ambaye kajifunika, akatikisa kichwa na kunyosha
mkono wake kuniweka kichwani, lakini kila akijaribu kunisogelea yule mwanamke
anayetoa uchafu anamzuia, ikawa kama wanashindana, na mimi siwezi kuinuka, wala
kufanya lolote….
Na katika juhudi hizo ,yule mwanamke aliyejifunika uso, akaweza
kunifikia na mkono wake akanifikia kichwani, ilikuwa kama ubaridi fulani, au kitu ambacho
huamusha hisia mwilini, …kwani nilihisi mwili ambao ulikuwa joto unapoa, mwili
ambao ulikuwa hauna hisia unahisi kitu fulani.
Mara yule mwanamke anayetoa uchafu akaanza kubadilika sura, na
kama vile anaoza, na kuanza kumomonyoka, na baadaye akawa anapotoea
kidogokidogo huku anapiga ukulele. Huyu mwanamke aliyenishika kichwani akawa
ananitizama usoni, lakini nilikuwa simuoni vyema sura yake kwani alikuwa
amejifunika usoni kwa nguo.
Baadaye yule mwanamke aliyebadilika akapotoea kabisa nikabakia na
huyo mwanamke aliyejifunika usoni, akaniuliza,. ..
‘Unajisikiaje kwa sasa,….?’ Akaniuliza nikajaribu kupanua mdomo
niongee sikuweza, basi nikawa namjibu kwa hisia
‘Naona nimepona…’nikasema kwa hisia, halafu akaniuliza;
‘Unajua mimi ni nani?’ akauliza yeye alikuwa anatoa sauti, mimi
nikamjibu kwa hisia tu.
‘Nitajuaje we ni nani wakati umejifunika uso wako….’ Na nikijibu
kwa hisia anaelewa, nikaongezea kumuuliza kwa hisia;
‘Naomba ujifunue uso wako maana naona wewe ni mtu mwema sana ….kwani
wewe unanifahamu kuwa mimi ni nani….?’ Akanitizama, alitoa sauti kama ya
kicheko, halafu akasema;
‘Mimi nakufahamu sana, hata kama wewe ungejifunika kama mimi
ningekufahamu pia,…’akasema
‘Kwa vipi, kwani wewe ni nani mpaka unifahamu kihivyo,..?’
nikauliza kwa hisia nikionyesha mshangao
‘Mimi nakujua ,a kukufahamu hata kabla wewe hujajiua wewe ni nani…’akasema
‘Mhh, basi wewe sio binadamu wa kawaida…naomba nikufahamu wewe ni
nani…kwani kuna ubaya….naomba pia nikuone sura yako….’nikasema kwa hisia
‘Ipo siku utaniona vyema kwani kwasasa siwezi kutizimika,….nilivyo
watu, hata wewe hutatamani kunitizama, ….’akasema
‘Kwanini huwezi kutizamika, kwani sura yako ipoje, inatisha, au
imefanyaje au wewe sio binadamu wa kawaida? …mimi kwa vyovyote uwavyo
nitafurahi kukuona sura yako…’nikasema kwa hisia, na yeye akasema.
‘Yote ni mapenzi ya mungu, na yote yametokea ili mapenzi ya kweli
ya mama na mtoto wake yaonekane…’akasema
‘Mama na mtoto wake…?’ nikauliza
‘Nikuulize wewe je unamfahamu mama yako ni nani, mama yako wa
kweli, aliyekuzaa, akakulea, …?’
Nikijaribu kufunua mdomo ili nitamke neno mama, lakini haukuweza,
nikasema kwa hisa ile ile,
‘Mama, mama yangu, yupo wapi…mimi simjui mama yangu….’nikasema
‘Unaona..wewe humjui mama, je kweli mtoto anaweza kuzaliwa bila
mama yake..?’ akaniuliza
‘Hapana….najua kuwa nina mama, lakini sijawahi kumuona..’nikasema
kwa hisia
‘Lakini mama yako anakujua na anajua ana mtoto kama wewe hata kama
kumbukumbu zake hazipo, …unajua ni kwanini?’ akauliza
‘Mhh…sijui…’nikasema hivyo hivyo kwa hisia, nikashngaa kwanini
kaniuliz vile, na kabla sijasema neno kwa hisia akasema ,
`Nikuonyesha kuwa hakuna kama mama, kwani mama anakujua wewe kabla
hujajiua, alikuhisi ukiwa tumboni mwake, ukacheza huko ndani ukampiga mateke,
akakuzaa kwa shida, wewe hujui na wala hujijui, je atawezaje kukusahau baada ya
kukuzaa…’akasema.
‘Lakini ….wewe ni nani, basi niambie mama yangu ni nani na yupo
wapi…’ nikauliza swali na akasema
‘Usiwe na haraka, utamfahamu kwa wakati muafaka…kwani ukimfahamu
sasa hivi huenda, kwa hali ya kibinadamu ukaweza kuingiwa na huzuni, na hata
kuchukia, na mwisho wake utakosa radhi,,,vuta subira kwani kila jambop la heri
huja kwa amani na kwa wakati muafaka...’huyo mama akasema na akawa kama
anapotoea
‘Mama…mama yangu yupo wapi…’sasa kilichotamka ni mdomo, na
nilipoweza kutamka hivyo, mara nikazindukana kutoka kwenye ile ndoto.
Nilipogundua kuwa ilikuwa
ndoto nikapapasa macho na kutizam huku na kule, nilijikuta nimezungukwa na
baadhi ya watu akiwemo dakitari na wanaume wawili na mwanamke mmoja…akili
ilianza kufanya kazi kuwa hawa watu sio mara ya kwanza kuwaona, nikajaribu
kukumbuka wapi niliwaona lakini ikawa vigumu.
‘Hawa ndio jamaa zako niliokuambia, …inaonekana ulikuwa kwenye
ndoto kali , na hatukutaka kukuamusha maana ilionekana ni ndoto njema, mwanzoni
uliweweseka na kupiga ukelele, lakini baadaye ukaonyesha furaha, unaweza
kutuambia ulikuwa unaota nini..?’ docta akauliza.
‘Mhh, hata sikumbuki…mmh, ngoja nikumbuke, nilikuwa naongea na
mtu, na wanawake wawili, na wote wamepotoea, .’ nikasema
‘Hukuweza kuwakumbuka sura zao, na je unawafahamu ni akina nani..?’
akauliza dakitari.
‘Kwa kweli siwajui, ila mmoja anatisha, sitaki hata kukumbuka
alikuwa anatoa harufu mbaya mdomoni na kila neno analoongea linanuka…aah, sijui
ni kwanini…’nikasema
‘Na huyo mwingine…?’ akauliza docta
‘Mhh huyu wa mwisho alikuwa mwema sana, alinishika kichwani,
nikajiona nimepona, aliniambia maneno matamu ambayo nilitamani kuyasikiliza
wakati wote, ila aliniuliza swali moja kabla sijamjibu akawa mumeniamusha,
….huyu mwanamke amejifunika uso mzima, …sijui kwanini…’ nikawaangalia kama vile
walikuwepo kwenye ndoto , na wao wakabakia kushangaa.
‘Hebu tuambie sasa unajisikiaje sasa, maana umesharuhusiwa, na
hawa ndio jamaa zako….’akasema docta na wale watu wakanisogelea
‘Haya inuka tuondoke…maana umesharuhusiwa , docta kasema huhitajiki
kuendelea kukaa hapa kwani hali yako inaendelea vyema, ni swala la kurudisha
kumbukumbu tu ndilo limebakia…na tumekuja na kigari utakuwa unakitumia hadi
hapo utakapoweza kutembea vyema’ akasema mwanaume mmojawapo na yule mwanamke
alikuwa akikusanya vitu nilivyokuwa nikitumia, nikajiuliza ndio mke wangu nini,
mbona ni mkarimu sana kwangu.
Nilikiangalia kile kigari nikawa najissikia vibaya, kwani kutokuweza
kutembea vyema ndio tatizo jingine lililokuwa likinikera docta alisema hayo
yanatokana na tatizo kwenye ubongo, kumbukumbu zikikaa vyema na hata kutembea
kutarudi,…
‘Inaoenekana unawaza sana, hujakumbuka lolote..?’ aliyeuliza hivyo
alikuwa ni yule dakitari wangu wa kila siku.
‘Kukumbuka, …hapana, nakumbuka ulisema mke wangu yupo, ndio yupi,
nilitarajia angekuja kuniona leo, au…’ nikamgeukia yule mwanamke aliyekuwa
akikusanya vitu , yeye hakuwa akituskiliza kwani alikuwa akihangaika kukusanya
vitu, na alipogeuka akakuta ninamtizama, akashangaa na kutuangalia.
‘Vipi mbona wote mnanitizama mimi..’ akauliza huyo mwanamke
‘Mgonjwa anahisi wewe ni mkewe…’ akasema mwanaume mmoja
‘Hahaha kweli….unafikiria hivyo, …basi usiwe na wasiwasi mimi ni
mke mwema sana, nikipata bahati ya kuwa na wewe hutapata shida, utapona
kabisa..’ akasema huku anaweka vifaa kwenye kapu.
Na mimi nikawa nashangaa, kuwa mbona kanijibu kama vila utani,
mimi nilizania kuwa yeye ndiye mke wangu halafu anajibu kinyume na matarajio
yangu.
Tuliondoka hapo hospitalini hadi kwenye nyumba moja nzuri, hapo
nikaambiwa kuwa patakuwa nyumbani kwangu,…nikashangaa kwa akuli hiyo
`Patakuwa nyumbani kwangu,
kwani kwangu ni wapi..nikajiuliza lakini sikutaka kuuliza sana, nikawa mara
nyingi namwangalia yule mwanamke kwa kujiiba, na alikuwa mkarimu kwangu kupita
kiasi, wakati mwingine ananikanda akisema kufanya vile kunasaidia kurudisha
hisia za mwilini na kunipa mazoezi hasa ya miguu ili iweze kuwa na nguvu ya
kutembea.
Hali yangu ilikuwa ikirudi kidogokidogo sana, mwili ukaanza
kuingiwa na nguvu, na kuongezeka kidogo kidogo, maana nilikonda sana,…na
nilionekana kama mzee, lakini sasa sura ikaanza kutakaka, lakini tatizo likawa
ni kumbukumbu na kuweza kutembea vyema,
nikawa natumia kigari cha kukaa…..ilinikera sana hiyo hali.
Miezi ikapita mingi tu na mwaka sasa unaingia….sijaweza kukumbuka
au kuweza kutembea bila kutumia kigari, san asana nikisimama natumia fimbo, na
napaat shida na husihia kudondoka chini.
Siku moja tulibakia mimi na
huyo mwanamke, akawa nanifanyia `masaji’ na alipomaliza nilihisi
msisimuko mwilini, msisimuko ambao sikuwahi kuuhisi kabla, kwani mara
nyingi mwili wangu ulikuwa kama una ganzi fulani, lakini kila mara alipokuwa
akinishika huyu mwanamke, nilikuwa nahisi kuwa kweli ananishika tofauti na
awali.
‘Nahisi msisimuko, leo umenipaka nini mwilini..?’ nikauliza, na
yule mwanamke akacheka na kutabasamu, akasema ni mafuta yale, yale ya kawaida.
Nilimtizama machoni mpaka akaona aibu, akaniuliza kuwa nawaza nini, nikamwambia
nahisi kuwa yeye ni mke wangu,
Nilipoatamka hivyo akacheka sana ,hakusema kitu akamaliza kazi
zake na baaadaye akaja akakaa karibu name, akaniuliza
‘Kwanini unahisi kuwa mimi ni mke wako..?’ akaniuliza
‘Maana docta aliniambia yupo mke wangu, na tangu nifike hapa
sijamuona nakuona wewe, sasa kwanini nisikubali kuwa wewe ni mke wangu.
‘Unamfahamu vyema huyo mke wangu..?’ nikamuuliza.
‘Mhh,..si unajua tatizo langu, sina kumbukumbu za nyuma, sikumbuki
kitu, simkumbuki hata nikimuona..hata sura siikumbuki…’nikasema
‘Mhh, sasa kwanini unifikirie kuwa mimi ni mkeo ….?’ Akaniuliza
‘Ni kama nilivyokuambia, wewe ndiye upo karibu nami, na kama kweli
nina mke kwanini hajafika kuniona..zaidi yako wewe….au wewe unamfahamu mke
wangu…?’nikasema na kumuuliza
‘Nitamjua wapi wako, wakati tangu tuanze kukuuguza , ukatoka
hospitalini, tumekuleta hapa tumekaa wote, tumeulizia jamaa zako, lakini hakuna
aliyejitokeza, kwa kweli hatujawahi kumuona ndugu yako yoyote aliyewahi kuja
kukuona….! ..’akasema na hapo nikahisi mwili ukinyong’onyea, ina maana kumbe
hawa sio ndugu zangu ni wasamaria wema tu.
‘Mhh, ina maana nyie sio ndugu zangu…?’ nikauliza
‘Kiukweli sisi sio ndugu zako, tunasubiri upone labda utatuambia
ndugu zako ni nani, maana hatuna njia nyingine ya kuwajua, tumejitahdi
tuwezavyo, tumefikia hatua tumekata tamaa..’ akasema yule mwanamke.
‘Wewe umeolewa…?’ nikamuuliza, na yule mwanamke akacheka sana.
‘Hahaha…swali gani hilo mpendwa, kama sijaolewa unataka kunioa
wewe…utaniweza lakini?’ akaniuliza
‘Kwanini nisikuweze, niambia ukweli kama hujaolewa….’nikasema
‘Mimi ndio nimeolewa….sasa nikuambia ukweli’akasema na hapo mwili
ukazidi kuisha nguvu sijui ni wivu sijui ni-nini
‘Umeolewa na nani…nilijua tu ni huyo mwanamue unayekuja naye mara
kwa mara…na siku hizi simuoni tena, yupo wapi, ndiye mume wako…, lakini mbona
sijasikia mkiitana mke wangu, mume wangu…sioni dalili kama hiyo..?’ nikauliza na
yeye akanitizama usoni, akasema,
‘Ndio…si umateka nikuambie ukweli, mimi- nimeolewa- na –wewe, umefurahi sasa… hebu
kumbuka vyema , yaani wewe unamsahau hata mke wako, mmh wewe ni mume gani , ….’
akasema na kunitizama usoni, alinitizama hivyo kwa muda mpaka nikawa anjiuliza kwanini
alikuwa akinitizama hivyo, nami nilihisi kitu fulani moyoni, nilimuona kama
mwanamke mwema, mrembo , na nilitamani awe kweli ni mke wangu.
‘Mhh, sasa hapo unanichanganya,…mwanzoni ulisema wewe sio mke
wangu,…sasa tena unasema wewe ni mke wangu, hebu niambie ukweli ili nisichanganyikiwe
zaidi..’nikasema
‘Kwani wewe ulitakaje..hebu nambie ukweli wako, wewe ulitaka iwe
vipi?’ akaniuliza
‘Mimi eeh, ..nataka hivi kama hujaolewa…eeh, unajua nikuambie
ukweli wewe ni mwanamke mwema sana, wanaume wanatafuta mke kama wewe, wewe
unaonekana ni mke mwema sana…na kama kweli sina mke …au mke wangu
hanitaki,…maana naanza kuamini kuwa wewe kweli sio mke wangu, ..’nikatulia
kidogo na yeye alipoona nimetulia akaniangalia akasema
‘Kwanini sasa uaamini hivyo, kuwa mimi sio mke wako…?’ akaniuliza
‘Mhh, kama wewe kweli ni mke wangu, mbona hujawahi kuja kulala na
mimi..’nikasema na yeye akasimama, maana muda wote alikuwa kaka karibu yangu ,
alianza kukusanya vitu, akawa kimia kwa muda.
‘Kama kweli nina mke kwanini huyo mke wangu haji kuniona, unajua
siamini,…siamini kama kweli nina mke…., sizani, mimi nahisi sina mke, eti hata
wewe huwezi kuliona hilo….! Kusema ukweli natamani wewe uwe mke wangu…’ nikasema
nay eye akageuka kuniangalia huku akitabasamu akasema.
‘Usijali, najua ukipona utabadili mawazo, …hiyo ni kawaida
kwasababu nipo karibu nawe muda wote, kwahiyo unahisi kuwa mimi ni wa pekee
sana, akili ikichanganya na kuwaona wanawake wengine, au akija mke wako,
utagundua kuwa mimi si chochote mbele yao….’ Akasema huku ananimiminia gilasi
ya juice ya matunda.
Nilipomaliza kunywa huyo mwanamke akaondoka, nikabakia peke yangu,
nami niliendelea kutawaliwa na hisia ambazo sio za kawaida, hisia hizi
zilinitawala akilini, na akili ikawa kama inawanga vile…na ingawaje yule
mwanamke alishaondoka, lakini nilikuwa bado namuwaza yeye, nikawa natamani
kumuita arudi lakini alishaondoka na akiondoka kurudi kwake hapo ni muda wa
chakula cha mchana.
Siku zikaenda na hali ilikuwa ni ile ile…na siku moja nikiwa
nimepumzika, nikitafakari dunia ilivyo, nilishajiona mwenye mapungufu mwili,
maana kama siwezi kutembea vyema mpaka kutumia kigari, na kama siwezi kukumbuka
vyema basi mimi ni nani..
Niliwaza sana na kitu kikanijia kichwani, kikiniambia mimi ni bora
nife tu, nitafute sumu nijiue,…sijui kwanini wazo hilo lilinijia muda kaam huo,
kujiua, kwanini nijiue, kwasababu sina faida, kwasababu mimi ni mtu wa
kuhudumiwa tu, sina ndugu, sina thamani yoyote duniani
Wazo lilianza kama mzaha, nikajikuta natafuta njia za kujiua, kwa
sumu au kwa kujinyonga…nikawa nawazia kila njia, akili sasa ikaganda kwenye
hilo wazo, nikaenda mlangoni nikaufunga kwa ndani, sikutaka watu waje
kunikatiza nilitaka nife kimia kimia…
Na wakati napanga njia rahisi ya kutenda tendo hilo, mara nikasikia
hodi mlangoni…
Kwa muda huo nilikuwa nimekaa kwenye hicho kigari cha kukokotwa na
kusukumwa kwa mikono, nilikuwa najaribu kuangalia njia ya kutenda hilo wazo
lililonijia akilini, hodi ndio iliyolipoteza hilo wazo..nikageuka kuangalia
mlangoni, sikutarajia hodi kwa muda huo..nikawa najiuliza ni nani huyo..
Sikupoteza muda nikasukuma magudumu ya kile kigari change cha
kusukuma hadi mlangoni.. nilikuwa nimefunga mlango kwa ndani,…ili nikifanya
nikaufungua
Aliyekuwa kasimama mlangoni alikuwa alikuwa ni mwanamke mmoja
akiwa kashika begi dogo, na nyuma yake yupo docta. Nilipomuangalai yule
mwanamke nikajikuta kama nashikwa na kitu kama kizunguzungu na mara sura nyingi
zikawa zinakua kichwani, na sauti nyingi sana, ilikuwa kama mtu kawekwa kwenye
chumba cha giza ambacho kinakuja mwanga wa sura za watu, halafu makelele mengi…
Hi ile ikanitesa sana na kichwa kikawa kinauma kweli, nikashika
kichwa na kuhangaika nikawa kama
nachanganyikiwa, nikashika kichwa na kuanza kulalamika kichwa changu , kichwa
changu, huku nahangaika sana , na docta akaja karibu yangu na kuniambia nimeze
dawa ya maumivu ya kichwa, lakini sikumuuelewa. Na sikutaka kumsikiliza..kwani
sauti yake ilikuwa kama kero fulani inapaa kama mwangi, nikawa nimeshikilia
kichwa nalia…
Yule mwanamke aliyeshika begi mkononi akawa anashangaa na kunionea
huruma, akanisogelea, na kumuomba docta asogee pembeni, akanitizama usoni, na
nikaona machozi yakimtoka …akatikisa kichwa na mara akainua mkono wake, na
kunishika kichwani.
Ajabu ilioje, nilihisi ubaridi ukiniingia mwilini, nilihisi kitu
fulani kikisafaisha yale mahangaiko na makelele kwenye ubongo wangu , maumivu
yote yakapotea…na mwili ukawa kama unaingiwa na ubaridi na hisia kutoka
kichwani taratbu ukashuka hadi miguuni..
Ilikuwa ni maajabu, nikainua kichwa kumtizama yule mwanamke na
mkono wake ukiwa bado kichwani mwangu…na mara kumbukumbu zikaanza kunijia
kwa mbali, nikawa nakumbuka kitu,…nikawa nayaona maisha yaliyopita kama
vile mtu anajitizama kitu kwenye runinga….
NB: Mhh, kidole kinauma tusihie hapa kwa leo
WAZO LA LEO: Ugumu wa maisha ,mawazo, matatizo, shida fedheha, vinaweza kumtuma mtu
kufanya jambo ambalo hata hakulikusudia,…wengine hukimbilia kulewa, lakini je
itasaidia,…. muhimu ukijiona upo kwenye hali hii mkumbuke mola wako, kumbuka
kuwa kuna watu walipata matatizo zaidi yako kumbuke wale waliopo chini yako,…kuna
watu wasio na uwezo kabisa,..lakini bado wanaishi, wana furaha, na wanafanya
hayo kwa sababu gani,kwasababu wamemuweka mungu mbele wakijua kuwa mungu ndiye
mjuzi wa hayo yote,kwake yeye yote yanawezekana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment