Kwa hali niliyoiona kwa wale wafadhili
wangu nikajua nikiendelea kukaa nao nitawazidshia mzigo, na isitoshe nimezembea
na kufanya vibaya kwenye mitihani ya kidato cha nne, nikaona aibu na hata waliponisisitizia
kuwa niendelee kukaa nao sikuweza kukubali kusema;
‘Hapana nitazidi kuwapa mzigo..mimi
niacheni, nitajua cha kufanya….’ nilikataa na kuingia mitaani kutafuta maisha.
*******
Maisha ya mitaani ndio jadi yangu, sikuchagua kazi, lakini
nilishajijua kuwa fani yangu ni ya ufundi, kwahiyo moja kwa moja nikaenda kwa
jamaa, niliowafahamu nikawaomba nijifunze ufundi wa kutengeza magari, wakanikubalia,
…
Kwasababu nilikuwa na kipaji cha ufundi, haikuchukua muda sana
kujua mambo mengi na jamaa yangu akaniamini sana, akajitahidi kunifundisha
kadri alivyoweza, hata hivyo sikubwetekea na fani hiyo peke yake, nikawa
najichanganya kwenye kila shughuli ilimradi iniingizie kipato cha siku
Mwanzoni nilikuwa narudi kwa wale wafadhili wangu kulala, lakini
baadaye nikaona nitafuta sehemu ya kuishi peke yangu ili niweze kupambana na
maisha kivyangu, nikatafuta chumba na bahati nikapata chumba cha banda la uani kwa
bei nafuu. Kutokana na ufundi magari nikajifunza kuendesha magari ya kila aina,
nikaamua nipate leseni kabisa ya udreva.
Kwa vile kiingereza kilikuwa kinapanda, japokuwa nilifeli kidato
cha nne, nikaona kwanini nisitafute kazi ya kuajiriwa, nikajaribu, ..unajua waajiri
wengi wanababaika na lugha, basi nilipoitwa kwenye usahili,…oh, jamaa
wakanikubali, nikapata kazi kwenye kampuni moja, ambayo nilifanya kazi hadi
siku ile nilipoona jina langu kuwa mimi ni miongoni mwa waliopunguzwa kazi.
***
Hayo yote yalikuwa ni mawazo, na mawazo hayo yalikuwa kichwani,
wakati natembea, sikujua kuwa nimefika kati kati ya barabara..muda huo ukumbuke
nilikuwa natokea hospitalini, naelekea kuchukua majibu ya vipimo vyangu, akili
ilikuwa sio yangu tena hapo…, kumbe nimeshafika kati kati ya mataa ya trafiki,
sikujali kuangalia kuwa tumerhusiwa watembea kwa miguu, sijui, sijijui.
Kumbe wakati huo magari yalisharuhusiwa, muda wa watembea kwa
miguu umepita mimi nikawa nimeshaingia barabarani, magari kutoka upande wa pili
yanakuja kwa kasi, …mara ya pili inanitokea hivyo.
Nilishituka magari haya yapo mbele yangu,…nikatoka kwenye njozi ya
kuwaza na kuiona hali halisi,…siunajua unapokuwa kati kati ya magari, magari
yanakuja, unajikuta unababaika nikaanza
kubabaika, mara niende mbele au nirudi nyuma, na kabla sijafanya lolote
nikajikuta naelea hewani na kabla sijatua chini nikajikuta nimedondokea kwenye
kiyoo cha mbele cha gari..
Ilikuwa ni ajali mbali, maana watu waliokuwepo hapo, waliniambia
walikuwa kimia kila mmoja akishikilia kichwa,akijua mimi ni maiti….gari
lilinigonga na kunirusha juu nikaja kudondokea kwenye kiyoo, halafu
nikaserereka na kudondokea mbele ya hilo gari-chini mbele ya lile gari
lilonigonga,na bahati nzuri lile gari likafunga breki haraka, vinginevyo
ningelikuwa chapati kwani magurudumu yalikuwa yanakuja kichwani mwangu.
‘Yallah,… mnaniua ili nisimsaidie mama yangu…..’ nikajikuta nasema
maneno haya na sikukumbuka kilichofuata baadaye.
‘Docta huyu mtu …anaonekana kabisa anaumwa…na ajali hii imetokana
na athari za huko kuumwa,…na huenda ni mmoja wa watu tunaowahitajia…, mnaona
jinsi alivyo, nahisi anaweza kuwa ni miongoni mwa waathirika na huu ugonjwa
tunaojaribu kupambana nao …’nilisikia sauti ya mtu akiongea kwa sauti yenye
mawimbi,masikio yangu yalikuwa kama mtu aliyezama kwenye maji.
‘Mhh, kwanza tulikuwa tunahangaikia majereha na kuona kama
hajavunjika mahali, tumechukua x-ray, na pia tutachukua vipimo vya damu, lakini
cha muhimu kwa sasa ni vipimo vya x-ray…hilo jingine linafuatiliwa baadaye,
…’sauti ikasema
‘Mhh, maana kwa uzoefu wangu …watu kama hawa, huwa wanakuwa kama
wamechanganyikiwa hasa kama hawajapata ushauri nasaha,…wakipitia sehemu za
ushauri nasaha wanabadilika, maana wengi hawajajua kuwa ugonjwa huu ni sawa na
ugonjwa mwingine, muhimu ni masharti tu….’sauti ikasema
‘Ni kweli…’sauti nyingine ikasema
‘Na huyu mtu amekonda sana, ….mmh docta tumesikitika kuwa
tumemgonga, lakini sio kusudio letu, unamuonaje docta, nahisi atakuwa na hilo
tatizo au sio docta?…’ nikasikia sauti ile ya kwanza ikisema, na wakawa kimya,
halafu nikasikia sautii nyingine, ikikohoa, ilikuwa karibu yangu sana
‘Mhh tusubiri vipimo tu….siwezi kusema lolote kwa sasa, sisi kazi
yetu ni kushughulikia ajali, tuone kama kuna atahri kwenye mifupa nk..sasa
ikifikia huko kwenye tiba nyingine mtaongea na docta muhusika….’sauti ikasema
na kukawa na ukimia fulani, nikajaribu kufungua macho, lakini yalikuwa mazito
sana, na baadaye kwa mbali nilimuona huyu aliyepo karibu nami akiwa na mavazi
meupe, akinikagua kagua akafunua macho yangu, mimi nilikuwa nimeyafumba,
sikutaka wajue kuwa nasikia wanachokiongea
Huyu aliyekuwa karibu yangu nikagunduaa kuwa ni dakitari.Kulikuwa
na ukimia, na nikasikia wale watu wakiongea lakini kwa sauti ndogo, nahisi
walikuwa wakiongea wenyewe wakati dakitari ananikagua na kuona nipoje.
Baadaye nikasikia watu wakisalimiana na maongezi yakaendelea
‘Aheri umekuja docta, maana huyu mtu akitoka hapa atakuwa mgonjwa
wako..’sauti ikasema
‘Kwani vipi ana matatizo gani zaidi..?’ sauti ikauliza
‘Nahisi atakuwa na matatizo mengine nah ii ajali huenda imetokana
na matatizo hayo,kama unavyomuona amekonda sana..na mwili wake ni mzaifu, sasa
ngoja tumalize shughuli yetu, halafu,…’akakatisha
‘Ok, hamna shida, naweza kumkagua kidogo…’sauti ikauliza
‘Endelea tu docta, ….tupo pamoja…’sauti ikasema na kukapita muda,
nilihis huyo docta mwingine akinikagua na kunishiak shika,akafunua mboni za
macho yangu, nilijitahidi kuyafumba, ….baadaye akasema;
‘Nahisi keshazindukana , lakini hajakuwa sawa..’sauti ikasema
‘Ok, kwahiyo umemuonaje…?’ sauti ikauliza
‘Nahisi huyu mtu nimeshawahi kukutana naye, sijawa na uhakika
kabisa..’akasema
‘Wapi..?’ sauti ikauliza
‘Mhh nimeshamkumbuka huyu
jamaa na hii itakuwa mara ya pili kukutaa naye, alikuja kule Lugalo, akiomba
apimwe vipimo vyote kikiwemo kipimo cha kujua kuwa kaathirika na ugonjwa wa
ukimwi au vipi, na tulimpima tukawambia arudi kesho yake, …hakutokea siku hiyo
na tukajua kaamua kutokurudi.
‘Alikuja mwenyewe akitaka kupimwa ukimwi..?’ akaulizwa
‘Mhh ndio, nilikutana naye hospitali ya lugalo, huwa nakwenda kule
mara kwa mara kutokana na kazi yangu hii,…na akaja akitaka kupimwa….’ huyu
dakitari akawa anaongea.
‘Kuna kitu muelewe, kukonda sana sio lazima uwe ni muathirika,
inawezekana kukawa an sababu nyingine, …na ili kujua hilo anahitajika kupitia
vipimo vingi, …na vipimo peke yake ndivyo vinaweza kuthibitisha kuwa ana…eeh
tatizo gani...’akasema docta mwingine.
‘Ndivyo nilivyowaambia hawa jamaa maana wao wanatokea kwenye
shirika la wafadhili wa walioathirika….na bahati mbaya wakamgonga kwa bahati
mbaya, akiwa katikati ya barabara….na kwa jinsi walivyomuona wakahisi ni
miongoni mwa waathirika wa huo ugonjwa…’akasema
‘Unajua kule Lugalo nakwenda kwa matatizo kama haya ya kupima
walioathirika na kutoa ushauri nasaha…na huyo jamaa nimemkumbuka alikuja
nikakutana naye,… alipofika, alishakata tamaa, nikajaribu kuongea naye, lakini
alikuwa yupo kama hayupo, nilihitajia muda wa kuongea naye zaidi….lakini muda
niliokuwa nao pale ulishakwisha, nikamwambia akija kuchukua vipimo tutaongea
naye zaidi….’akasema docta.
‘Kwahiyo vipimo vinasemaje….najua hutakiwi kutuambia lakini kwa
ajili ya hawa watu ambao lengo lao ni kuwasaidia watu walioathirika…..ingewasaidia
sana…’ sauti ikasema
‘Majibu yake yalishatoka, na hutaamini, hana tatizo la ukimwi
kabisa ...., nilitaka akija nimuombe tumpime tena…na kwa vile yupo hapa
tutampima tena tuhakikishe hilo, lakini tuna uhakika asilimia mia kuwa
hajaathirika, na vipimo vingine halikadhalika havionyeshi kuwa ana matatizo
makubwa…ni matatizo madogo madogo tu ….’akasema yule dakiatari.
Mara ikasikika sauti ya kike,
‘Docta vipimo vya huyu mgonjwa hivi hapa,…..’ kukapita ukimia
fulani halafu sauti ya docta ikasikika ikisema
‘Ok,….x-ray, inaonyesha kuwa hajavunjika mahali popote , hana
matatizo makubwa zaidi ni hiyo michubuko tu…labda nesi, chukua vipimo vya damu
na docta hapa atakuandikia ni nini zaidi kinahitajika, kwa upande wangu mimi
nimemalizana naye….’akasema docta
‘Ok, nipe hiyo karatasi….’sauti ikasema na kukapita muda kidogo,
halafu sauti nyingine ikauliza
‘Kwahiyo sasa docta sisi tunaweza kuondoka maana sisi tuna safari, itakuwa haina haja kwetu
tena kuendeela kusubiria, kwa sababau tulimgonga kwa bahati mbaya akiwa
katikati ya barabara, sio kosa letu…sijui ana mawazo gani… na kama atakuwa
muathirika, tunaomba tupate taarifa, tutajitahidi kurudi lakini hatuna uhakika
ni lini….’ nikasikia sauti ya mtu mwingine ikisema
‘Mimi naona bado tunahitajika kumsaidia huyu mtu, hata kama sio muathirika, nahis atakuwa na tatizo jingine kubwa, kuna
kitengo chetui kingine cha kusaidia watu wasiojiweza, kwahiyo tutalifikisha kwa
wenzetu…’sauti ikasema
‘Mimi nitakuja kulishughulikia,….mimi nipo kwenye kitengo hicho,’sauti
nyingine ikasema
‘Mhh, lakini hatuwezi kusubiria, tunakwenda na muda, tutakuja
kurudi, au wewe unasemaje, maana ni lazima tuongezane na wewe…’sauti nyingine
ikasema
‘Mimi nahisi huyu mtu ana matatizo ambayo yamemzonga, huenda ana
ugonjwa haujagundulikana au kuna jambo…’ sauti ikasema na kukawa na ukimia
fulani, muda huo nilijaribu kufungua macho tena
Docta ambaye alikuwa karibu nami nikamuona akinishika mkono, na
nilihisi kuwa wamehisi kuwa nimezindukana. Macho sasa yaliweza kufunguka, yalikuwa
yanaona vyema, na niliweza kuwaona wote waliokuwepo mle ndani. Kulikuwa na
madakitari wawili, na watu wengine ….kama waaa-nne hivi, mwanamke mmoja.
Mmmoja wa wale madakitari
akanisogelea zaidi na huku akiangalia mashine iliyopo ukutani ambayo inaonyesha
mienendo ya mwilini akatikisa kichwa, na kuwaambia wale watu;
‘Huyu mgonjwa keshazindukana, ila bado akili haijakaa sawa. ..’akasema
huyo docta
Akanisogelea na kunifunua mboni za macho, akashangaa namwangalia.
‘Vipi upo safi, …’ akaniliuliza
‘Nipo safi kwaaa-ni ooh, kichwa,..ooh, kwani vipi,nimefanya nini….docta,
kwani nina nini, na hapa ni-ni-po wapi…oooh’ nikakumbuka kitu kichwani,
nilikumbuka neno moja nikajikuta nikisema ;
`Mama yangu…docta mama anahitaji msaada wangu, na…aanhitajika
kupelekwa India.’nikasema
‘Mama yako…yupi huyo…, hebu
subiri kwanza , bado unahitajika kupumzika…wewe tulia kwanza…’ akasema docta.
‘Docta..kwani nimefanyaje..?’ nikauliza
‘Wewe umesema mama yako, …anahitajia msaada ni mama gani huyo na
yupo wapi?’ akaniuliza
‘Mama…..mimi nimesema mama….mmh, docta mbona sikumbuki kitu….’nikasema
nikijaribu kukumbuka
‘Basi tulia usiwe na wasiwasi….’docta akasema na akasogea akawa
anaongea na mwenzake kwa sauti nisiyoisikia vyema.
Nikabakia najiuliza kwanini nimesema mama, anahitajia msaada wangu
ni mama gani huyo inawezekana ni mama yangu, kwani mama yangu ni nani….’nikawa
najiuliza maswali mengi lakini sikuweza kukumbuka vyema.
‘Ina maana kumbukumbu zilipotea..?’ nikamuuliza rafiki yangu
‘Kwa muda huo sikuwa najua kitu, kuwa labda nimepotewa na
kumbukumbu, na sikuwa najifahamu…’akasema, wakati wale madocta wanaongea wale
jamaa wengine mmoja akanisogelea na kusema name;
‘Sikiliza ndugu, sisi ndio
tuliokugonga kwa bahati mbaya…samahani sana, na docta kasema hujaumia ni
mshituko tu uliokupata, lakini tunaona kuwa huenda una matatizo mengine ambayo
tungependa kuyajua ili kama inawezekana tukakusaidia kwani sisi p
tunashughulika na kampuni ya kusaidia wenye matatizo mbali mbali, hasa waathirika,
na …’ akasita kuongea.
‘Kwani mimi nimeathirika…?’ nikauliza
‘Hapana..hujaathirika, ..ila tunakuambia tu kuwa sisi ni shirika
binafasi linashughulikia matatizo mbali mbali, mojawapo ni kuwasaidia wale
walioathirika, wewe kwa mujibu wa dakitari, sio muathirika, lakini kutokana na
hali uliyo nayo, tunahisi una tatizo kubwa, unaweza kutuambia ni tatizo gani..?’
wakaniuliza
‘Tatizo…mmh mimi sijui kama nina tatizo, kwani ….mimi ni
nani..ooh, samahani …docta kwani nimefanyaje,….kwanini nipo hivi?’ nikawa
namuuliza docta na wale watu wakawa wananiangalia kwa mashaka.
‘Lakini wewe umesema sasa hivi kuwa mama yako anahitajia msaada
wako, mama yako yupo wapi na ana matatizo gani..?’ wakaniuliza
‘Nani, mama yangu, mama yangu ndio nani…yupo wapi, kwani ….mama
anahitajia msaada wangu nimesema hivyo…docta kwani mama yangu yupo wapi,..?’
nikauliza nikijaribu kukumbuka.
‘Usihangaike, wewe tulizana tu, ni kawaida ..’akasema docta na
wale jamaa mmojawapo aaknisogelea na kuniambia
‘Hebu tuambie mama yako ana tatizo gani la kuhitajika hadi apelekwe
India…?’
akasema mwanaume mmoja na kabla sijamwambia lolote, mara simu ya
huyo mtu ikaita, ikabidi awaangalie wenzake halafu akaniomba msamaha na
kuipokea ile simu.
‘Docta niambie naona nina bahati kubwa kupigiwa simu na mtu
mashuhuri kama wewe, …ndio , ndio kazi yetu docta, pesa zipo bwana, lakini
tunahitajia zaidi kutoka kwa wadau, wasamaria mwema wenye kujitolea,… hapa
nchini wapo wafadhili wengi wamechanga,..lakini bado, unajua wengi
hawajatufahamu lengo letu ni nini….’akatulia
‘Na unajua wapo watu wanahitaji kusaidia wenzao lakini nani wa
kusaidia ndio tatizo, ndio maana sisi tukaanzisha hili shirika, kuwa mtu kati,
wanaotaka kusaidia na wale wanaotaka kusaidiwa,….ndio, uaminifu, na kuaminiana
ndio lengo letu, sisi ni waumini,…kwahiyo hatuwezi kuwatapeli watu….’akasema
‘Mpaka sasa hatujajitangaza zaidi ya kupita mahospitalini,…tutakuja
kufanya hivyo, ila kwa sasa tuliona tuhakikishe tumejipanga vyema, kwa maana
tukiamua kujitangaza kwa sasa wanaweza wakaja hata wale wasiostahili hii
misaada…binadamu sio watu wema..’akasema akiongea na simu
‘Sasa hebu niambie una watu wangapi hapo hospitalini kwako,
wanaohitaji misaada,…?’ akauliza
‘Mhh, kuna wanaohitajika kwenda India kwa upasuaji, wapo wangapi…wanaume
wanne, na mwanamke mmoja, ….mmh, kwanini wanawake…ni wachache ina maana kweli
hakuna wanawake wanahitika kwenda huko..?’ akauliza
‘Ok, basi mimi nitakuja hapo kumuona huyo mwanamke… …yupoje…?,
ok…basi tukitoka hapa tunakuja huko.., na hao wanaume wapo hapo hapo au
kwingine,…ok, …haina tatizo ngoja kuna tatizo naliweka sawa hapa, nipo na
wenzangu wa kitengo cha kusaidia walioathirika kuna sehemu tunakwenda, mimi
naweza kuachana nao, nikaja huko..ok tunakuja.. ok, bye’ akakata simu.
Akawaangalia wenzake na kuonyesha saa mkononi …akanisogelea
na kuniambia kuwa wamepata dharura, lakini wakirudi watakuja kuona kama
wanaweza kusaidia hilo tatizo la mama yangu …kwani ni moja ya kazi yake
…nisiwe na wasiwasi watanisaidia…wapo kwa ajili ya kusaidia watu kama hawo
wasio na uwezo wa matibabu, nisitie shaka.
‘Mama, nina mama ..mbona sikumbuki, anahitajika kwenda India…mmmh,
mbona sikumbuki…’nikawa nababaika sikumbuki kitu.
‘Wewe usijali, tutarudi , huenda tukirudi utakumbuka vyema…’wakasema.
‘Muda gani mtarudi maana hapa sijui nini kinaendelea….’nikasema
nikijaribu kukumbuka lakini akili ilikuwa butu haikumbuki kitu, ni kama akili
isiyo na jambo, umetoka usingizini, hukumbuki hata kuota na hujui upo wapi na
kitu gani kimetokea.
‘Docta kwani mimi nina tatizo gani,na kwanini nimefungwa hivi…docta
nipo wapi…’nikawa naongea ovyo.
Na docta akahisi kitu na
akaongeza dawa fulani kwenye yale maji ya drip niliyotundukiwa, na …haikuchukua
muda nikajikuta kwenye usingizi mzito!
Hali yangu kiafya ikabadilika ghafla, nikawa mgonjwa kwelikweli, na
kumbukumbu zikapotea kabisa…na nikawa na hali mbaya, joto likawa kali,,na mara
kwa mara nikawa napoteza fahamu,…, nikizinduka, hali ni ile, ile..joto linakuwa
kali, mara mapigo ya moyo yanakuwa na kasi ya ajabu…, hali ikawa sio shwari,
wakagundua kuwa nina upungufu wa damu, shinikizo la damu, hata sukari…nikajua
sasa siku za kuishi duniani zimekwisha.
Katika hali hii ya kuumwa, kupoteza kumbukumbu, kwahiyo sikujua
nipo wapi, ila nilisahjua kuwa nimepatwa na ajali, ilikuwaje sikumbuki,
nimetokea wapi sikumbuki, na mara kwa mara wakawa wananiuliza kuhusu mama,
wanasema huwa nikilala naongea kuwa nina mama, anahitajika kwenda India,
anahitajia misaada ya watu, na wanasema nongea hayo nikiwa kwenye ndoto.
Hali ilizidi kuwa mbaya , wakaona nihamishiwe kwenye hospitali
kubwa zaidi
Nilihamishiwa hospitali ya Muhimbili, na huko nikakutana na
wataalamu ambao walinisaidia sana, mpaka hali ikaanza kurejea vyema, lakini
kumbukumbu ikawa ni tatizo kwangu, wakati mwingine naweza kuongea na mtu
akirudi namuuliza kuwa yeye ni nani na tuliongea nini…
‘Tatizo hili ni la muda tu, litaisha , kwasababu ubongo wako
umepitia mambo mengi, na ule mshituko wa kugongwa na gari ulileta athari ambayo
haikugundulika mapema, una bahati sana, kwani athari ile haikugusa
ubongo,…lakini hali inatengamaa usijali..’ docta akaniambia, nami sikuwa na
wasiwasi sana, niwe na wasiwasi na kitu gani…sielewi, na kwanini
nililetwa pale sijui kabisa!
Na kweli siku zilivyozidi kwenda ndivyo hali ilivyokuwa na
matumaini, nikiwa naona mabadiliko , na nilianza kukumbuka kumbuka kidogo
kidogo, na kumbukumbu nyingi zilikuwa za muda mfupi, kumbukumbu za zamani
nilikuwa sizikumbuki kabisa. Mpaka nikawa naona kero, mtu hujui umetoka wapi
wewe ni nani
‘Hili tatizo ni la muda, litakwisha usitarajie kuisha kwa haraka,
lakini sio tatizo la kukuumiza kichwa, na usijichoshe kwa kuwaza
sana….’akaniambia docta
‘Docta unajua nashangaa, kwanini nisikumbuke, hivi ina maana sina
ndugu, mbona….ooh,..na huyo mama mnayemtaja mbona haji kuniona au..’nikawa
nashika kichwa kujaribu kukumbuka.
‘Ndugu zako wapo usijali, ….na mama wewe ndiye unayemtaja mara kwa
mara kwenye njozi inaonekana kweli utakuwa na mama anayehitajia msaada,
tumejaribu kuwasiliana na hospitali mbali mbali lakin hatujaweza kugundua mama
kama huyo…’akasema docta na kuniacha nikiwa najaribu kuwaza ni kitu gani
kilitokea,….na mimi nimetokea wapi, na huyo mama ni nani , na atakuwa wapi…sikuweza
kukumbuka.
Mwezi ukapita, nikaonekana sijambo jambo…ila kumbukumbu bado zilikuwa
hazijakaa sawa, na madakitari wakaona haina haja ya kuendelea kulazwa, ila
natakiwa niwe nafika hapo hospitalini kila baada ya wiki moja, …
‘Sasa tunaoan tukuruhusu uende ukatulie nyumbani kwako, na utakuwa
ukirudi hapa kila baada ya wiki,..na tutaona huko mbele….kiafya huna tatizo
sana, ila kumbukumbu bado hazijaa sawa, zitarudi tu usijali..’akasema docta
‘Nyumbani kwangu ni wapi?
‘nikauliza na docta akajifanya kama ananishangaa…
‘Ndugu yangu ina maana hujui kwako ni wapi…!’ Akaniangalia kwa
makini halafu akatabasamu ni kuniambia;
‘Kama hujui kwako ni wapi inabidi ukalale polisi..’akasema kwa
utani
‘Kweli docta mimi sijui kwangu ni wapi, niende wapi
sasa..’nikasema
‘Mhh, usijali, kuna ndugu zako kila siku wanakuja kukuangalia,
naona siku mbili hizi sijawaona, …ngoja wakija nitaongea nao, usijali,
utapelekwa kwako..’akasema
‘Ndugu zangu, wale wanaosaidia watu au ni nani….ni wale waliofika
siku ile..hao nawakumbuka lakini wao sio ndugu zangu, walisema wao kazi yao ni
kusaidia watu, nakumbuka hilo sana..docta mimi sikumbuki kuwa na ndugu kama
wale..’nikasema
‘Mhh, yah, utakumbuka tu, na muhimu akija mke wako nataka nikae naye nimpe maelekezo jinsi gani ya
kuishi na wewe, hadi hapo hali yako itakaporejea kama kawaida..’ akasema docta.
‘Mke wangu!? Ni nani huyo?…mke wangu alishawahi kuja hapa…?, mbona
simkumbuki…hivi mimi nina mke kweli….?!’ nikawa nashangaa, kwani sikuwa na
kumbukumbu zozote za kuwa na mke.
‘Atakuwepo tu, sidhani kuwa huna mke,…huwa anafika na hao jamaa
zako mara kwa mara, ngoja jamaa zako
wakija tutaongea nao, wewe tulia hapo kitandani, usiwe na wasiwasi…’akasema
docta
‘Mke wangu….!?’ Nikabakia nikijiuliza
NB: Tatizo lileee kama la mama yake mnakumbuka mama yake alipoteza
kumbukumbu, kumbe ni kizalia, sasa mama yake imekuwaje..Jamani leo nimeona
nitoe sehemu hiyo ndogo, maana akili haijatulia kidogo, tukutane sehemu ijayo
tuone jamaa atakumbuka vipi na huyo mke wake ni nani
WAZO LA LEO: Tuheshimu na kujali rasilimali watu
kutokana na nguvu kazi yao, wewe kama muajiri, wewe kama una bahati ya kuwa na
watendaji wako unaowalipa,. Hakikisha unajali sana jasho lao, usitumie ujanja
kuwanyonya, usiwanyanyapae, au kuwanyanyasa , maana wanatoa jasho kwa ajili ya
kipato chako, hata kama wapo vipi, ilimradi ni watu wako na una dhamana nao, ni
muhimu sana kuweka mbele `utu’…kuliko ‘masilahi’ utu utalinda mali yako na
familia yako, utu utakuongezea baraka na huo utu, utakuongezea kipato.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment