Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, May 18, 2015

NANI KAMA MAMA-78 Docta aliponiambia kuwa mama yangu ana uvimbe ndani ya ubongo, uvimbe ambao nilijua kabisa umetokana na madhila ya watu, mama kupigwa kichwani na hata pale aliposukumwa na mke wangu akadondokea kichwa, vinaweza kuwa ni sababu ya uvimbe huo lakini sikuwa na ushahidi wa kumnyoshea mtu kidole.

‘Docta Sasa tutafanyaje kuhusu huo uvimbe..?’ nikamuuliza dakitari nikitaka kujua kuwa huenda kuna dawa inayoweza kumtibia, lakini jibu nilipopewa lilinikatisha tamaa,

‘Uvimbe huo huondolewa kwa kufanyiwa upasuaji, na tatizo ni kuwa upasuaji kama huo, hauwezekani hapa kwetu,..’akasema docta akiangalia faili la mama kama vile anasoma kitu ili anielezee nilipoona yupo kimia nikamuuliza.

‘Una maana gani,  …sasa kwahiyo docta mama atatibiwaje…?’ nikauliza

‘Kama nilivyokuambia uvimbe kama huo unahitajika kufanyiwa upasuaji, ni bahati mbaya kuwa sisi hapa nchini hatuna upasuaji wa namna hiyo…’akasema

‘Upasuaji huo unafanyiwa wapi….?’ Nikauliza

‘Upasuaji huo unafanyiwa India..lakini kwanza hebu subiria vipimo vingine maana bado kuna vipimo hapa havijakamilika, vikikamilika..utakuja kuambiwa kila kitu …’akasema na kuanza kuondoka, nilitaka kumsimamisha lakini hata nikimsimamisha nitamuambia nini….

Basi siku ile nikabakiwa kuwaza na kuwazua, nikalia na kulia, …lakini yote hiyo haikusaidia kitu..

Tuendelee na kisa chetu

*********

‘Mnakumbuka pale nilipowahdithia, kuwa mimi na mama tulikwenda kuomba kwenye nyumba moja kwa mama mmoja ambaye alikuwa na asili ya mtu kutoka India,…na akaingia ndani, baadaye kukaja gari la landrover ndani yake kulikuwa na askari mgambo na polisi..?’ akatuuliza rafiki yangu

‘Ndio tunakumbuka, kwani ilikuwaje…?’ nikauliza

‘Tukio hilo siku hiyo ndio tukio lililonitenganisha mimi na mama yangu…’akasema

‘Mhh, ina maana huyo mama mwenye asili ya kihindi, aliwapigia simu polisi…?’ nikauliza

‘Ndio…kwasababu taarifa zilishasambazwa kuwa kuna mama mmoja jambazi, gaidi, anatafutwa na polisi, mama huyo huwa anajifunika uso wake, yeyote atakayemuona atoe taarifa polisi, kwani mama huyo ni hatari…’akasema

‘Mhh..yaani ilifikia hapo, mkaitwa magaidi….?’ Akauliza jamaa mwingine.

‘Kuna usemi wa wenzetu kuwa ukitaka kumuua mbwa, cha kwanza mchukia yule mbwa, halafu umuite majina mabaya…na ndivyo ilivyotokea kwetu, hatukutakiwa kabisa maeneo hayo, tulionekana ni uchafu…kwahiyo ili zoezi hilo likamlike, tukapakaziwa ubaya, kuwa sisi ni wezi, sisi ni mjambazi, sisi ni magaidi…’akasema

‘Mhh, kweli dunia haina wema..’akasema mmojawapo

‘Ndivyo ilivyo…mnyonge hata siku moja hana haki, hasa anaposhindana na mwenye uwezo, mwenye mali….wewe una nini, utafanya nini mwenzako ana pesa ataajiri wanasheria wa kumtetea, wewe atakutetea nani…na ndivyo ilivyotokea kwetu, ...'akatulia

'Kuna raia walilalamika kuwa wanamiliki maeneo kuzunguka eneo hilo toka mababu zao, lakini hawakusikilizwa, kwa vile hawakuwa na hati miliki, ..muwekazaji akafuata sheria zote, akapata haki miliki...utashindana na yeye.....na sisi tukatumbukizwa kwenye mkumbo, kwani tulikuwa tukitumia eneo hilo kujihifadhia...


'Basi tukio hilo ndilo lililonitenganisha mimi na mama yangu , linanikumbusha mbali na ni tukio nisiloweza kulisahau, na nikiwa hapo hospitalini nikakumbuka maneno ya mama akiniambia….

Mwanangu hapa naona hakuna usalama, na kama kutatokea fujo kimbia moja kwa moja hadi mfichoni kwetu usijali litakalo tokea….mungu atakulinda…

Nililikumbuka sana tukio hilo siku hiyo wakati nipo nasubiria vipimo vya mama ambavyo niliambiwa havijakamilika,…nililikumbuka kwani ni tukio lililonifanya nitengane na mama yangu, na sasa tena naambiwa mama yangu ili apone anatakiwa apelekwe India,…sina pesa, sina chochote,hali yatu ni dhalili…nani atatusaidia..ni tukio ambalo sitaweza kulisahau…

‘Kwani ilikuwaje walipofika hao mgambo…?’ nikamuuliza

Siku ile walipofika hao mgambo, utafikiri walimpania mama, kwani kwa pamoja walimkimbilia mama, wakaanza kumpiga, wakati huo mimi nimekamatwa, askari mmoja alikuwa kanishika mkono kuhakikisha sitoroki. Wao walishaniona kuwa eti mimi ni tishio, ni mkorofi, ni mtoto wa nyoka…yaani kama alivyo mama, basi hata mimi  mbaya naweza kuleta maangamizi.

‘Nyie ndio wakaidi eeh, mnadiriki kuwaumiza walinzi, …..mumewaumiza askari mgambo wawili….mnajifanya magaidi eeh….’akasema askari huku akiangalia jinsi gani mgambo wale wanavumpiga mama..kipigo cha hasira kipigo cha kulipiza kisasi,…mama hakuwa na la kufanya alitulia kimia huku virungu mabuti yakitua mwili mwake, bila kujali wanapiga wapi, na mimi nilibakia kulia tu nikiita

‘Mama..mama..mnamuua mama yangu…’lakini kilio changu hakikuwa na maana kwao.

‘Lazimz iwe fundisho kwenu…mnavuruga amani,..hamtaki kutii sheria…mama yako atakuwa fundisho kwa wengine…’akasema huyo askari

‘Mama…msimuue mama yangu…jamani mama mnamuua mama yangu…’nikawa nalia na huyo askari akawa anatabasamu tu.

‘Muache afe kwani ana faida gani,…san asana ni kutuletea shida, sisi tunahitajia mendeleo, wawekezaji wanataka kujenga kiwanda hapa, kitakacho waajiri watu wengi, nyie mnaleta ukaidi mnawaumiza watu wa usalama….hamuoni kuwa nyie ni wakorofi…’akasema

‘Sisi hatujafanya hivyo….sisi ni omba omba tu afande..’nikasema

‘Omba omba…kwani muombe, kwani nyie hamuna mikono ya kufanyia kazi, mama yako ana mapungufu gani, kwanini asiende kulima,….’akasema

‘Mama haan shamba, ..shamba kanyang’anywa..’nikasema

‘Acha uwongo…funga domo lako…’akasema na kuminya mkono mpaka nikawa nasikia maumivu.

Jinsi walivyokuwa wakimpiga mama bila huruma, moyoni nilijawa na chuki , nikajisemea mwenyewe hivi kwanini binadamu tunakuwa hatuoneani huruma, watu wazima na akili zao hawaoni kuwa kitendo kama kile kinamuumiza binadamu mwenzao, na hawajui kwanini mama anaishi mazingira kama yale, hawajui na hawataki kujua, sana sana tunaonekana ni uchafu…nikakumbuka yanatokea huko dunia nyingine ambapo mtoto anashuhudia mateso hayo kwa wazazi wake, unafikiri mtoto kama huyo akiwa mkubwa atafanay nini…ni chuki zisizoisha na matokea yake mtoto anabadilika na kuwa gaidi wa ukweli.

Wakati mgambo wamehakikisha kuwa maa hajiwezi tena, mara likatokea lori jingine likiwa limebeba watu, nikagundua ni wale ombe omba, na watoto wasio na wazazi, wakiwa wamebebwa kwenye hilo lori, na nikajua huo ni mpango maalumu wa kuhakikisha sote tunaondolewa eneo hilo ili muwekezaji aweze kuweka vitega uchumi vyake, wazawa tukawa hatuna haki,..na hata kama tungekuwa na haki, sis tungewekeza nini, san asana tulionekana ni udhia wa mji…


Lile lori lilipofika mama akabebwa kama gunia na kutupiwa ndani ya hilo lori na baadaye kuondoka likiongozwa na landrove mbili za polisi moja mbele na nyingine nyuma,…

Hapo sikujua wanapeleka wapi mama, mimi nikiwa nimeshikwa mkono na mgambo mmoja aliyebakia nyuma, yeye hakuondoka na wenzake, labda alibakizwa kwa ajili yangu. Baadaye ikakaja gari aina ya pick-up, yule mgambo akaniongoza kwenye hilo gari akanipandisha nyuma, na ndani yake nikakutana na watoto kama mimi na wengi wao nilikuwa nikiwajua. Wote walikuwa watoto wa mitaani na omba omba kama mimi!

‘Sasa tunapelekwa wapi…’ mmoja wa watoto akauliza, na yule mgambo akasikia na kutuangalia kwa jicho baya. Mimi nilikuwa nawaza wapi wamempeleka mama yangu, na hali kama ile, maana alivyopigwa ni lazima atakuwa na hali mbaya. Nilililia sana kisirisiri, na kila mgambo akiniangalia nilijifanya najikuna machoni, niliogopa nikilia sana atanipa adhabu kwani sura yake naikumbuka vyema, ni yule yule mgambo niliyempiga kigogo kichwani siku ile …, wakati akimkanyaga mama yangu.

Tulisafirishwa hadi mbali kidogo na mji, gari lilikatisha katikati ya mji na kutokea sehemu nyingine nje ya mji, na kuingia eneo la msitu halafu tukatokea eneo lenye miti mingi, halafu kwa mbele yetu tukaona jengo kubwa kama shule, na majengo mengine madogo madogo yaliyokaribu yake, na eneo la pembeni kidogo kulikuwa na uwanja wa michezo mbalimbali.

‘Hapo mnapopaona mbele yenu kutakuwa ndio nyumbani kwenu, kuanzia leo, na ole wenu mmoja atoroke ,…narudia tena kusema ole wenu..mtu ajifanya anajua kutoroka, atakuja kupambana na kifo…’akasema huyo askari.

‘Unaona huu msitu….kuna wanyama waakli , kuna simba, chui…mkijifanya wajuaji kutoroka mtaenda kuliwa na wanyama wakali…, cha muhimu ni kukaa shuleni, kwani hapa ni shule, ni kambi itakayokulea ili baadaye uwe na maisha mazuri kuliko kuzurura mitaani….’ Akasema jamaa mmoja, ambaye tulikuja kujua kuwa ndiye mkuu wa kambi.

Tulifika hapo kambini , na kuwakuta watoto wengine wakiwa wanafanya kazi mbalimbali, wengine wananyweshea bustani, wengine wanaweka mbolea, ..na kazi nyingine nyingine, na wote wamevaa sare moja, nilivutiwa kidogo na manthari hiyo, …lakini kila mara mawazo yangu yalikuwa yakimuwaza mama yangu.

Ilipofika usiku tulionyeshwa sehemu ya kulala, na usiku kulikuwa na vibweka vyake maana wapo wale waliotangulia ,wenyeji wa siku nyingi, wao walikuwa watukutu, sisi wageni tulianza kuteswa, eti tunakaribishwa kambini, tulilazimishwa kuimba, kuruka kichura…

Ilikuwa ni kero nyingine, sikujua kuwa hata sie watoto tuna roho mbaya, kwani walichotufanyia hakikustahiki, lakini wao walijiona wanajua zaidi,…vitendo hivyo viliendelea hadi saa nne, …na hapo ghafla, tukaona wale wote waliokuwa wakitutesa wakirukia vitanda mwao na kujifunika gubigubi , na kuifanya wamelala…

Mara akaingia mbaba mmoja na kirungu, huyu alikuwa mmoja wa walezi, au mwalimu wa zamu wa kambi , akawa anazunguka huku na kule bila kusema neno, alifanya hivyo kwa muda na sisi wageni tulikuwa tumekaa sakafuni, hatukujua tufanye nini…

‘Mlikuwa mnafanya nini, siliwaambia kuwa kila mtu kitandani kwake hapa mnafanya nini..?’ akauliza yule mlezi

‘Walikuwa wanatutesa, wanatuimbisha, wanaturusha vichura…na…’ akasema mmmoja wetu

‘Eti nini ni nani anafanya hivyo, silishawakataza hii tabia, …kesho mutanionyesha ni nani anayewanyanyasa wenzake…tabia hii siitaki kabisa, huyu aliyefanya hivyo namtaka kesho ofisini. Wewe na wewe kesho utanitajia ni nani, … atakiona cha mtema kuni…’alikagua vitanda na kuita majina , halafu taa ikazimwa akaondoka.

Alivyoondoka wale watoto watukutu wakainuka, kama vile hawajali, wakawa wanatupitia vitandani na maji, wanatumwagia na huku wakitoa onyo kuwa atakayemtaja yoyote kati yao kesho kuwa alikuwa akiwanyanyasa atatoa macho ya yoyote atakayefungua domo lake.

‘Ulizeni wenzenu hapa, mimi ndio nani, nitawatoa macho wote mbakie vipofu, na nitawafanyizia kitu mbaya ambacho hamtakisaahu maishani mwenu…oooh, …’ akatamba mmojawapo…na, baadaye tukalala.

Utukutu huu haukuishia hapa vijana hawa walikuwa wanatumwagia maji kitandani ili tuonekane tumekojoa vitandani, na asubuhi yake tunaishia kuadhibiwa kwa kudeki na kufua, na adhabu nyingine, …kwakweli ikawa ni shida juu ya shida na hali kama hii ikawa inanikumbusha sana mama yangu, nikiwa peke yangu ninalia sana, lakini hata nilie ingesaidia nini. Tuliogopa kabisa kuwashitaki hawa watoto watukutu, kwani walikuwa wakubwa na inavyoonekana walikuwa wakiogopwa na watoto wengine!

Siku zikaenda, miezi miaka, umri ukawa mkubwa, lakini siku moja wakaja wale mgambo na askari polisi, walipokuja nikaitwa, nikijua kuwa labda kuna taarifa nzuri kuwa mama atakuja kunitembelea au kunichukua, lakini maswali niliyoulizwa yalinikatisha tamaa;

‘Wewe mtoto mama yako mara nyingi anaishi wapi na jamaa zake ni nani?’ nikaulizwa

‘Mimi sijui jamaa za mama , mama hana jamaa zake … sisi hatukuwa na nyumba, kwani mama yupo wapi…?’ nikauliza

‘Mama yako siku anapelekwa mahakamani kwa kumjeruhi askari akiwa kazini,… aliruka kwenye gari, na sehemu aliyoruka ni karibu na daraja, akazaam majini, ..tulimtafuta bila mafanikio…’akasema

‘Mama yangu…ina maana mumemuua mama yangu..’nikalia

‘Mama yako ni mkaidi,a liruka mwenyewe..hakuna aliyemuua, tunahisi atakuwa katokea upande mwingine wa mto…, ndio maana tulikuwa tunakuulizia kama unajua wapi mama yako huwa anapenda kwenda au kama kuna jamaa au ndugu utuambie, ili tuwe na uhakika kuwa yupo salama au …?’ akasema yule mmoja wa askari.

‘Mimi sijui jamaaa yoyote..’nikasema

‘Na ule mto ni balaa umejaa mamba, viboko, sasa yeye alijifanya mjuaji akaruka, akijua katoroka mkono wa sheria kumbe anakwenda kuliwa na mamba…sasa wewe hapa utulie kabisa….’akasema askari.

‘Namataka mama yangu..’nikasema kwa hasira.

‘Mama yako, kwa ukadi wake atakuwa kaliwa na mamba, na wewe ukijifamnya mkaidi utaliwa na simba, ole wako ujaribu kutoroka, ..humo msituni kuna simab, chui, mamba…’akasema askari mmoja.

‘Sisi bado tunamtafuta mama yako, maana mama yakoa naonekana ni gaidi, kwanza tuambe kwanini anajifunika uso wake,..huoni kuwa ni mkosaji, alifanya makosa sasa anaficha sura yake….’akasema na mimi nikawa kimia moyoni nikiwa hasira

‘Sasa, kama kweli unajua wapi jamaa zako wanaishi na hutaki kutaja, tutakuja kukuchukua ukafungwe gerezani, unasikia…?’ akasema yule askari mwingine hata bila huruma.

Alipofika kusema hivyo mimi sijua kabisa nini kilinipata, nilishikwa na kitu kama kwikwi, mfulululizo, huku natingishwa mapaka nakosa pumzi. Ikabidi nipelekwe kwa dakitari, lakini hali yangu ikawa mbaya, ikabidi nisafirishwe kupelekwa mjini. Na nilipofikishwa hospitali nikalazwa kwa siku tatu.

Nikiwa hapo nilikiwa kila mara nikiwaza sana, na usiku naota ndoto nikiwa na mama, tukipambana na mgambo, basi naamuka kwa kupiga kelele, na hali hii iliniandama sana, lakini baadaye ikatulia, na usiku mmoja nikaona ni bora nitoroke, lakini kabla sijapata njia ya kutoroka, jamaa wakaja wakanichukua na kunirudisha kambini.

Kule kambini jamaa watukutu wakazidi kutuandama , sisi kundi lililokuja mwishoni kuwa eti tumewachongea na sasa hawana kazi ya uongozi, na mmmojawapo alikuwa kaka mkuu akaachishwa kazi ya ukaka mkuu, kwahiyo kisasi chake kikawa dhidi yetu…hasa mimi.

Kwakweli hali hii ya mateso nikaona haivumiliki na niliambiwa kuwa huyo jamaa anasema kweli alishamtoa mtoto mmoja macho na hakuna aliyemsema kwa wakubwa, kwani ukisema anakutoa macho na wewe au anakuumiza sehemu ambayo utapata shida sana, kwahiyo wanamuogopa sana. Basi nikpata wazo la kutoroka.

Huwa mara kwa mara kuna gari la kubeba bidhaa , vyakula na vifaa vingine , lori hili huja mara mbili au mara tatu kwa wiki, na kila likija, baadhi ya watoto wanapewa kazi ya kuliosha,basi katika kulichunguza sana, nikagundua kuwa kwa chini kuna nafasi ambayo ukiweka maboksi vizuri na ukafunga kitu kama kamba unaweza ukalala, ukasafiri bila shida,..

Nikikumbuka baadhi ya filamu nilizowahi kuona, nikakumbuka makomandoo walivyokuwa wakifanya, basi kila gari likika nafanya zoezi la kuweka maboksi na kufunga vyema, nikafanya hivi mara mbili, kuweka boksi wakati linasafishwa , halafu nalala pale wakati linasogezwa kuweka karibu na stoo, nikagundua kuwa inawezekana kusafiri …

Kitu kilichoniogepesha ni kuwa barabara tulizopitishwa wakati nakuja ni mbaya sana, na sehemu nyingine kuna vumbi, lakini nikasema kwasababu mara nyingi magari hayo kama nilivyoambiwa huwa yanasafiri usiku, mimi nitaweza kujifunika na vile vifaa tunavyotumia wakati tunafagia kwenye mavumbi. Nikatafuta kifaa kimoha ambacho unaweza kukivaa vyema kabisa nikakificha.

Jamaa yule aliyefukuzwa ukiranja mkuu, akawa ni adui wangu mkubwa, tulikorofishana naye , kwani wakati mwingine na mimi sikukubali kuonewa, kuna siku nilimshitakia, ..basia kajua mimi ndiye chanzo cha yote hayo, japokuwa nilikuwa mdogo, lakini sikukubali kuonewa, kuna muda na mimi nilikuwa najitutumua hivyo hivyo,…kama alivyokuwa mama, huyo jamaa  akaahidi kuwa usiku atakuja na kuhakikishaa ananitoa macho yangu..niliogopa sana.

Basi siku ambapo jamaa huyo alipanga kunivamia …kama nilivyodokezwa na wenzangu , nikaona ndio siku nitoroke, kwani marafiki zangu waliniambia kuwa wamesikia jamaa huyo akipanga na wenzake kuwa atakuja kunivamia usiku na atahakikisha amenitoa macho yangu kiukweli.

‘Yule jamaa huwa hatanii, na anajuana na wakubwa wa hapa, hata ukimshitakia huwezi kuaminika,..si umeona tumemshtakia, lakini amefanywa nini..kafukuzwa ukiranja mkuu baada ya watu wengi kulalamika….’akaambiwa

‘Nitajua la kufanya…’nikasema na sikuwahi kumwambia mtu mpango wangu huo, nilikumbuka mama aliwahi kuaniambia kwa ukiwa na jambo la siri usimuamini yoyote yule, kwani huyo unayemuamini anaweza akawa ndiye adui wako..

Ilipofika usiku wa saa sita…nikawaona wale jamaa watukutu wakiongea, na baadaye wakalala, niliujua kabisa wameshapanga kunivamia, basi kulipokuwa kimya, nikatoka nje, kama nakwenda kujisaidia, nilijua kabisa kuwa bado mapema, lakini niliwaogopa sana wale watukutu, wanaweza wakaja kunivamia nikiwa nimelele, nikaona heri nikalale pale kwenye gari, …, nikafika pale , nikiwa nimevaa sweta la baridi na vifaa vyangu vingine nilishaviweka kwenye ile sehemu, matunda kidogo na maji ya kunywa.

Bahati nzuri mlinzi alikuwa kalala, basi nikajisokomeza ile sehemu na kujilaza vizuri kabisa na kulala, nilikaa kwa muda mpaka nikafikiri labda gari halitaondoka, ila baadaye nikashikwa na usingizi, na ndani ya usingizi, niliota napaishwa juu, huko juu nikakautana na upepo mkali wenye vumbi, ngurumo kama ya simba nikawa nakohoa sana, nilipaa wee, baadaye nikadondoka kwenye shina la mti…baadaye nikazinduka, nilipoangalia nikasikia mngurumo wa gari , mara nikawa natingishwa sana.

Nilipokumbuka kuwa nipo nyuma ya lile gari , nikajiweka vizuri, kusubiri gari liondoke, kumbe ndio lilikuwa linakatisha nyika, na sijui wapi nilipo. Kumbe muda wote niliokuwa nikiota nilikuwa nipo ndani ya lile gari, na kuota kukohoa ni kwasababu ya vumbi, na kumbe gari limeshaondoka muda na lipo mbali kabisa na ile kambi.

Nikajiweka vizuri ili nisije nikaonekana. Na ilikuwa dhahiri kuwa tumeshamaliza barabra ya vumbi, tunaingia barabara ya lami. Nikachukua kile chombo changu nikakivaa puani,, lakini ilikuwa haina haja tena kwani barabara ya lami vumbi lake ni kidogo.

‘Ni heri kufa kuliko kurudi kambini….’ Nikasema na kuapa moyoni

Tulisafiri, mpaka kukapamabuzuka, sasa ikawa joto, …ilibidi nifungue yale maboksi ili nipate hewa, na katika pilika pilika hizi nikajikuta naharibu ile kamba niliyoifunga kama kinga ya kunifanya nisidondoke, na nikagundua kuwa nyuma kuna msururu wa magari ina maana watu waliopo kwenye magari ya nyuma wanaweza hata kuniona. Nilijishikilia kwa shida sana, na mara usingizi ukanishika. Ndoto zikaniandama tena na ile ndoto mbaya ya kutisha iliponitokea nikazindukana kwa wasiwasi, nikipiga kelele na kutaka kukimbia, na hapo nilikuwa nimejisahau kuwa nipo wapi.

Nilishituka nimeachia ile sehemu niliyoishika na ghafla nikabwagwa chini kwenye lami, …nilisikia maumivu makali, nikaserereka barabarani na huku nyuma magari yalikuwa yakija kwa kwa kasi, nilichosikia na mlio wa gari likifunga breki, nikahisi kama napigwa kikumbo kikubwa, …hapo nikaona giza nene likatanda usoni, sikujielewa kabiasa kuwa kumetokea nini, nikapoteza fahamu


WAZO LA LEO: Utalawa bora ni pamoja na kutoa haki sawa kwa kila mtu  bila kujali hali za watu, utofauti wao wa kipato, rangi, jinsia au kabila, na kuwe na taratibu nzuri za kuwahudumia watu kutokana na uwezo wao, wale wenye uwezo wawe ni chanzo cha kuwawezesha wale wasio na uwezo ili ifikie hatua kuwa kila mmoja anaweza kujimudu. Hii itasaidia kuondoa utofauti mkubwa wa kipato.


Ni mimi: emu-three

No comments :