Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, May 12, 2015

NANI KAMA MAMA-75



Kama ulivyoona sehemu iliyopita rafiki yangu ilifikia muda alishindwa kuendelea kunihadithia kisa chake,...kina machungu mengi, ... na akaondoka, niliwasiliana naye baadaye akapanga kuja na tulikutana sehemu ile ile..nikiwa na maswali mengi kichwani, kwani kuna sehemu kubwa kama kaicha, ni kwanini..tutakuja kufahamu huko mbele, ..na je ni kwanini alishinwa kuendelea kuhadithia kisa akawa kama analia, hebu tuone sehemu hii ndogo ambayo inamtoa machozi...

*****

 ‘Maisha yangu na mama yakawa ni ya kuomba omba, kuzunguka majalalani, tutakachopata ndio riziki yetu….mama aliniambia tutanatafutwa na polisi kwahiyo hatuwezi kukaa sehemu moja, tukawa tunabadilisha maeneo leo hapa kesho kule.., na usiku ukifika tunatafuta sehemu salama tunalala. Kuna matukio mengi tulikutana nayo, siwezi kuwaelezea kila kitu, ila nitawahadithia baadhi yake…’ alianza kusimulia rafiki yangu siku alipofika tena eneo hilo.

‘Siku moja wakati tupo majalalani tukiokota makombo na masalio ya vyakula waliyotupa matajiri, mara ghafla tukazungukwa na mgambo wa jiji. Unajua mgombo wa jiji wapo kila mkoa, mimi kwa vile nilishazoea hizo hangarihangari kwa kipindi hicho nikatimua mbio, na tulijua wapi pa kukutana na mama yangu zikitokea vurugu kama hizo.

Mama yeye mara nyingi alikuwa mbishi na aliweza kupambana na watu kama hawo, au vibaka. Ujue hata sisi tulikuwa tukipambana na vibaka,..vibaka hao walikuwa wakija kwenye maficho yetu na kutunyan’ganya hata kile kidogo tulichobahatika kukipata. Ndio maisha yalivyo…

Mama yangu alikuwa mlezi wa watoto watano kama mimi, kwani hutoamini eneo hilo tuliwakuta watoto wengine wadogo , ingawaje walikuwa na umri mkubwa kidogo ukilinganisha na mimi, lakini walikuwa watoto wadogo , na hawakustahili kuwa mbali na wazazi wao hasa mama!

 Basi mama kwa upendo wa watoto akawa ndio mlezi wao, atakachopata kidogo tunagawana, ingawaje mama alihakikisha kuwa mimi kwasababu ni mdogo kuliko wenzangu Napata kipa-umbele.

Ilikuwa tukiamuka asubuhi, wengine wanakwenda mabarabarani kuomba, wengine wanazunguka kwenye majalala na mama anahakikisha usalama wetu kwa kuwa karibu nasi na kidogo tulichopata tunakaa pamoja tunakula, kama ni pesa, mama anapanga nini tununue. Na watoto wakawa wamemheshimu mama na kumtii kila analosema. Mama alikuwa mkali kwa watoto watukutu, na kwahiyo adabu ilifuatwa.

Ilibidi ikifika jioni lazima maji ya kuoga, na kuhakikisha nguo zetu zipo safi, na usafi wa jalalani unaujua, zitafuliwa na maji machafu angalau sizipate chawa, wakati mwingine ilikuwa ni matambara tu yakusitiri aibu, na mama ikifika jioni anayashona-shona, ili kesho tusiadhirike.

Usiku wakati mwingine unakuwa wakati wa kupigia stori, kila mmoja anaelezea maisha yake, wapi alipotoka kitu gani alipambana nacho, hutaamini, watoto hawa wanakumbuka walipotoka, mmoja alisema alikimbia mteso ya mama wa kambo, baada ya mama yake kuachika, akawa anaishi na mama huyo wa kufikia.

Mwingine akasema alikimbia mateso ya baba yake mkubwa aliywakuwa akimlea, wazazi wake walifariki akiwa mdogo akawa analelewa na baba yake mkubwa, baba yake huyo alikuwa mkali kupita kiasi basi akaamua kukimbia…mwingine alipotea, wakiwa safarini na wazazi wake, ilikuwa kituoni gari limesimama, yeye akatoka nje, akajisahau, alipogeuka pale basi lilipokuwa limesimama akakuta halipo, akawatafuta wazazi wake mpaka leo hajawaona…ilikuwa ni visa vya kusikitisha tu. Mimi sikuwa na cha kusimulia.

Tulibahatika kupata eneo nzuri la kulala, na tulifanya hivyo baada ya kufukuzwa maeneo ya mjini, Kwani ingawaje sikumbuki vizuri, maisha ya mjini, ila kumbukumbu zinanijia kuwa tulikuwa tukiishi mjini kwa mara ya kwanza, lakini maeneo ya mjini yalikuwa ya mateso, na wahuni , watu wazima omba omba kaam sisi walikuwa wengi , kwahiyo mchana mnahangaika, lakini usiku ulikuwa mbaya sana,kwani usiku hupambani tu na wezi bali wauza unga, wabakaji …balaa mtindo mmoja.

Basi siku hiyo naikumbuka sana, kuliko siku zote ndio siku tulipovamiwa na mgambo, ….nilikimbia hadi juu kidogo ambapo niliweza kuona nini kinatokea kule chini, nikawaona wale mgombo wakitembeza kichapo, hutaamini kuwa binadamu wale hawakuwaonea huruma binadamu wenzao, badala ya kupambana na vibaka na wezi mitaani walikuja pale kupambana na masikini wanaotegemea makombo na masalia ya vyakula vilivyotupwa na matajiri.

Tuliwahi kuambiwa kuwa eneo hilo linahitajika kuchukuliwa na muwekezaji kutoka nje, kwahiyo lilitakiwa kusafishwa, kwahiyo ilitakiwa akija hapo asione hiyo aibu ya watu kama sisi…tukaanza kufukuzwa kwa njia hiyo.

Wakazi wengi wa eneo hilo hawakukubaliana na hilo, kwani wengine walikuwa wamejenga biashara zao pembezoni mwa barabara na wao pia walitakiwa kuondoka, sisi tulikuwa chini kwa bondeni ambapo taka taka hutupwa bila mpangilio, halikuwa jalala maalumu, ila watu wa maeneo hayo walikosa sehemu ya kutupa taka wakawa wanakuja kutupa hapo.

Kumbe eneo hilo sasa linahitajika kumilikiwa …

Nikiwa sehemu ya juu, nilimuona mama kwa mbali akipambana na mgambo mmoja, na baadaye yule mgambo alipomshindwa akawaita wenzake, wakaanza kumpiga mama kwa kushirikiana, utafikiri wanapiga mwizi, na baadaye nikasikia kwa mbali, wakisema kuwa mama yangu anaonekana ni mwizi kwasababu sura yake ambayo alikuwa akiificha ilikuwa imeharibikwa kwa kupigwa kama kibaka.

‘Huyu mama kumbe anaficha sura yake iliyoharibiwa..kumbe..anaogopa kutambulikana, ..ni kibaka huyu..piga…’nikasikia wakisema.

Wakaanza kumpiga,niliona kiatu cha mgambo kikitua kichwani kwa mama, baada ay kupigwa mtama na kudondoka chini..kwakweli niliumia, ..nikashindwa kuvumilia, …nikatafuta jiwe, nilikuwa na manati yangu ya kuwindia ndege shingoni, nikaitoa,..nikatafuta sehemu yenye nafasi,..nikachukua manati yangu nikaweka jiwe,..nikamlenga yule mgambo aliyekuwa akimkanyaga mama kwa buti..mimi nina shabaha sana, simukosea, nilisikia kilio tu, akawa kashika kichwa kinatoa damu.

Wenzake wakawa wanamuuliza kafanya nini, akawa kashikilia kichwa damu zinavuja.., akawaambia kpigwa na jiwe,..sasa wakawa wanahangaika kutafuta wapi jiwe lilipotokea, mimi nilikuwa mjanja nilishahama hapo na kuelekea sehemu nyingine ambapo hawanioni….nikakaa hapo kwa muda, halafu nikasimama kuangalia kinachoendelea., nilimuona mama akiwa chini, nahisi alikuwa kapoteza fahamu.

Nilipomuona kwenye ile hali, nikakumbuka kipindi tulipowasili maeneo ya hapo kutoka mjini, … nikiwa bado bado sijazoea hangari hangar hizo za kukimbizana na mgambo, au vibaaka…nilikuwa mchanga wa tabia hiyo…unajua eneo hilo tulikaa kama mwaka hivi.

Ilikuwa ni usiku ambao sitaweza kuusahau kwenye akili yangu..tulikuwa tumejibanza sehemu ambayo tunalala, kwenye chumba cha pembeni kabisa kwenye jengo ambalo halijakamilak kujengwa,  mara mlinzi wa nyumba ile ambayo ilikuwa ndio inajengwa akaja na vijana wanne, akasema;

‘Ndio hawa…’akasema na kuondoka, hatujua ana maana gani, mara wale mijaa wakatavumaia , mama akaanza kupambana nao. Mama alikuwa na nguvu, …

Lakini ile mijitu nayo ilikuwa na nguvu sana, walipigana na mama, sikujua nini wanataka kutoka kwa mama, kwani kwa walivyoonekana waliweza kutafuta mahitaji yao bila kuja kutuuibia, kwani vijisenti mama alivyopata siku hiyo vilikuwa vya kuuza mchicha na mboga mboga. Mboga mboga hizo zilitoka kwenye bustani mama aliyotengeneza kipindi cha mwanzoni mwa utoto wangu kabla hatujafukuzwa hapo.

Mama mwanzoni alimua kujituma kwa kulima bustani, kabla hajajiingiza kwenye kuomba omba..mama akawa analima na tunamwagilia mboga kwa  pamoja, lakini mavuno yanachukua muda, tunahitajika kula..kwahiyo ilibidi kufanya kazi nyingine, ..mama akawa anaomba vijikazi vya hapa na pale..ndivyo alivyokuwa akifanya mama mwanzoni kabla hatujafukuza kwenye hilo bonde eti lina mtu na huyo mtu analihitaji kwa kilimo cha kisasa….na pia tulikimbia hapo baada ya tukio baya ambalo sipendi kulihadithia…’akasema

‘Tukio gani,..tuhadithie tu bwana..’jamaaa mmoja akasema

‘Unajua maisha niliyopitia ni mabaya ..yana taabu, huzini na matukio mengine yanaumiza sana..sikupenda kumuhadithia mtu,..nitawahadithia hili moja tu…’akasema

‘ Basi kipindi hicho tulizoea hiyo kazi, mama analima mboga,. Kama mchicha ukikua,  tunauza mitaani tunapata hela ya kula , na kuipikia kidogo, baadaye tunakuja kulala kwenye hilo jumba.Jumba hilo lilikuwa na mlinzi, kilichotakiwa kufanywa ni kumlipa huyo mlinzi kiasi fulani kwa siku ili tupate kijisitiri hapo, na kama huna kitu huruhusiwi kulala hapo. Kwasababu nilikuwa mdogo, ikifika usiku mimi nalala fofo, na wala sijui kinachoendelea, mama ndiye mlinzi wangu, hakiwezi kupita kitu asiwepo macho…ole wako uniguse….

Siku moja, nilikuwa naumwa,mama akahangaika ili apate pesa ya kuniitibia, alihangaika huko alipohangaika,….mchicha ulikuwa umekwisha na kipindi hicho ndio tumepigwa marufuku ya kulima hilo bonde….mama akapata pesa kidogo, akanipeleka hospitalini, nikapata dawa, tukarudi mapema kwenye lile jengo na mlinzi yule muda kama huo haruhusu watu kama sisi kuwepo, kwani atagombezwa na muajiri wake, na usiku anafanya kama msaada tu, kwa posho kidogo tunayompa….

Kwa siku ile kwa vile nilikuwa naumwa, hali yangu ilihitaji kutulizwa mahali, basii mama akaongea na yule mlizi kuwa atalipa hela ya ziada mimi nipate shemu nilale…yule mlinzi akakubali kwa ahdi ya kulipwa pesa zaidi…, kumbe yule mlinzi  alikuwa na lengo lake kutukomoa. Hakupenda sisi tuendelee kukaa hapo.

Basi mimi nikalala pale na kwa vile nilikuwa naumwa nilishikwa na usingizi nilipoamuka nikakuta mama amesharudi, anahangaika kutengeneza malazi ya usiku. Na akanilisha chakula alichokuwa nacho akanipa dawa tukalala…

Ilikuwa usiku sasa, ndio hiyo mijamaa ikafika na mlinzi akasema `ndio hawa..’ akaondoka zake, na wale mijamaa ikatuvamia…nikajua wanataka hivyo vijisenti vya mama, nikatamani kumwambia mama awape tu, wasije wakamuua. Wakamshika mama kwa nguvu, wakampiga, na mmoja akamkaba mama shingo nikajua mama sasa anakufa na , mwingine akamshika miguu….’akatulia kidogo

Unajua kama nitaweza kukutana na watu wale, nikiwa na bastola sizani kama nitaweza kuvumilia, nita….oh…’akatulia kidogo

Wale mibaba, hawakujali kuwa mama kazimia..maana walihakikisha wamempiga, hadi kupoteza fahamu…na baadaye wakafanya walichokitaka huku nashuhudia kwa macho yangu, na baadaye wakachukua vile vijisenti vya mama wakaondoka navyo, na wakati wanaondoka wakaniona nimekaa pembeni nalia, waliponiona nalia hivyo wakanizaba kibao cha nguvu nikapoteza fahamu.

Tulihama eneo hilo usiku ule ule….

************

‘Ukumbuke kumbukumbu hizo zilinijia wakati nipo pale kilimani walipofika mgambo,….wakati nachungulia, nikihakikisha mgambo hawanioni, nia ni kuona kama mama yupo salama…nilimuona mama akiwa kalala chini, na wakati huo mgambo wanafukuzana na watu wengine.

Nilijua mama atakuwa kaumia sana, maana alikuwa kalala na hatikisiki..mara nikamuona mgambo mwingine sio yule ya kwanza niliyempiga jiwe, yule sikimuona maeneo hayo tena, huenda alikuwa kaondoka kujitibia jeraha..huyu sasa alikuwa mgambo mwingine .

Nikawa cha kufanya kama atampiga mama…nikawa nasubiria, sikujua nichukue hatua gani kumsaidia mama, ..yule mgambo akawa anamsogelea mama, pale alipolala, akamkanga mama mgongoni, maana mama alilala kifudi fudi..alipoona mama hainuki, akawa anamvuta mama juu akiwa kashikilia nguo za mama…nguo za mama zilikuwa ni kuuu kuu..zikawa zinachanika.

Mama akawa kabakia wazi mgoni, ..yule mgambao akainama na kumgeuza mama, nahisi alijua kafariki, …akawa anazidi kuzivta nguo za mama…mama akawa sasa karibu nusu uchi…wakati ule watu wengi walikuwa upande mwingine. Nikasikia akimuita mgambo mwenzake.

Yule mgamabo..akawa anamkokota mama sehemu ya chini kidogo, asipoonekana, nikajua ni yale yale ya wale mibaba..sikuvumilia, haraka nikatafuta kigogo…, nikashuka mbio nikiwa nimeshika kigogo, kwasababu nilikuwa mtoto, mgambo wengine hawakuweza kunijali, wakijua nakimbia tu huku na kule…

Nikafika karibu na pale aliposimama mgambo, yule mgambo bado alikuwa akihangaiak na mama, … akimburuza mama kama mzoga, na nikajua huenda mama ameshafariki,…alipofika ufichoni nikaona akimvuta mama nguo zilizobakia, sikuweza kuvumilia, mimi nilitumia nguvu zangu zote nikakirusha kile kigogo nilichokuwa nacho…, nilitumia  nguvu zangu zote, na kweli kilikwenda na kutua kwenye kichwa cha yule mgambo.

Kwa wakati ule gari la jiji la kuwasomba wote waliokamatwa pale lilishawasili kwahiyo ilie vuruguvurugu na watu kupambana na mgambo, huyu mgambo hakuona hicho kigogo kimetoka wapi. Kilimgonga yule mgambo bara bara kichwani, na kweli kilifanya kazi yake, yule mgambo akadondoka chini..nahisi alipoteza fahamu, kwani lidondoka chini akawa kimia..mimi nikakimbia hadi pale alipolala mama, nikamtiskisa

‘Mama amuka tukimbie…mama..mama…’nikaona mama yupo kimia, nikakumbuka kitu nikageuka huku na kule nikaona chupa yenye maji, sikujali ni chupa ya nini, nikasogea hadi pale alipo mama nikamwagia yale maji kichwani na mara maam akazindukana

Mama alipofumbua macho tu na kuniona mimi, na alipogeuka na kuona yule mgambo kalala chini nay eye yupo kwenye ile hali, haraka akanishika mkono tukaanza kukimbia..tulikimbia, hadi pumzi zikatuishia, tukawa tupo mbali kabisa na eneo hilo, na mama akasema tupumzike….

Ikabidi tuhame eneo hilo mama tulipata taarifa kuwa polisi na mgambo wanatutafuta kwa kuwaumiza walinzi …

NB:  Haya tumeona tukio hilo kidogo, tutaona tukio jingine kabla ya kuhitimisha kisa chetu, au mnasemaje..?


WAZO LA LEO: Binadamu ana stara yake hata kama hajitambui tunahitajika kuiheshimu stara hiyo, kuna watu wana majukumu ya kikazi kama vile walinzi, mgambo hata polisi, ni kweli tunapowajibika hatutakiwi kuangalai huyu ni nani, amri ikitolewa ni amri moja…piga ua, kama tunavyoona. Lakini sio lazima kufanya hivyo wakati wote, tukipewa amri tunatakiwa pia tujue jinsi gani ya kuitekeleza, tuheshimu sheria, kwani sisi ndio walinzi wa sheria, kuna walinzi hawajui hilo, na wanafanya kazi hizo kama kukomoa, au kwa matakwa na utashi wao,…huu sio uungwana kabisa.

Ni mimi: emu-three

No comments :