`Baba…’ ilikuwa sauti ya mtoto akiwa anatokea chumba alichokuwa
amelazwa, chumba ambacho mara nyingi hukitumia nesi akiwepo hapo nyumbani….
kumbe mtoto huyo alishaamuka kutoka usingizini, na alipoona yupo peke yake
kitandani akateremka kutoka kitandani na kuja chumba cha maongezi.
Akili yake alianza kujiuliza yupo wapi, lakini alipochunguza kwa
makini akagundua yupo sehemu anayoifahamu, akaingiwa na furaha akijua sasa
atamuona mama yake na baadaye baba yake atakuja na zawaidi,…akatoka mle chumbani
na kuingia chumba cha maongezi,..alipofika chumba cha maongezi wa kwanza
kumuona alikuwa ni baba yake,…
‘Baba….’akaita kwa furaha
Kwa muda alipoingia, baba yake yeye alikuwa akiangalia mlango ule
wa jikoni, ni kwa muda ule nesi na dada yake walikuwa wakitokea jikoni wakiwa
na sinia lililokuwa na maandalizi ya wageni..na baba mwenye nyumba alikuwa
akiwaangalia wao, hakuwa ameangalia upande
ule wa mlango aliotokea mtoto, sauti ndiyo ilimshitua,…..na kugeuka kuangalia
huko
Baba mwenye nyumba aliposikia sauti ya huyo mtoto moyo ulimlipuka
phaaa.., kwanza alijishitukia akitaka kusimama kwenda kumpakata yule mtoto kama
kawaida yake, maana ilikuwa kawaida kila akitoka kazini mtoto huja kumpokea na
baba huwa anakuja na zawadi, basi hapo humuinua juu akazunguka naye halafu
anamweka chini anamwambia nisalimie.
Na mtoto huinua mkono na kushika kichwa cha baba yake na mwanzoni
ilikuwa hivyo na baadaye alivyoanza kuongea maneno mawili matatu, akawa anasema
`si-kamoo..’
Baba mwenye nyumba akajikuta kainuka kidogo,. Halafu kama vile kakumbuka
jambo… kuwa huyo mtoto ni wa nani, akarudi na kukaa akainamisha kichwa ,
hakupenda kuinua kichwa kumtizama yule mtoto, na alikaa hivyo kwa muda kidogo
Mtoto alitarajia tendo alilolizoea kutoka kwa baba yake huyo..lakini
haikutokea hivyo…, alishangaa kumuoana baba yake akiwa kainama chini na
kujifanya hakusikia, yeye hakujali akawa anamsogelea baba yake, moyoni alihis
huenda baba yake anaumwa… , mara akajikuta yupo kati kati ya watu, kumbe
hakujua,..kumbe kuna watu wengine, akageuka huku na kule, sasa akiwa na aibu,
au uwoga,…akawageukiwa hao watu, mmoja akamtambua
‘Si-kamoo….’akasalimia docta, na akamuona mlinzi akamsalimia pia.
‘Marahaba, haujambo, umeamuka eeh..?’ akauliza docta na mtoto
hakumjali yeye akageuka upande ule alipo baba yake.
Hakumjibu docta, yeye kwa haraka akageuka kumuangalia baba yake,
baba yake alikuwa bado kainama chini, kiakili za kitoto, hakujua afanye nini ,
lakini hakukata tamaa akawa sasa anamwendea baba yake pale alipokaa, baba yake
kuona hivyo,..japokuwa moyo ulikuwa umeshatanda huruma, lakini kwa upande
mwingine hasira na chuki zikamtawala…kwa haraka akasimama
‘Samahani natoka kidogo…nakuja..’akasema na kusimama na kwa haraka akatoka kuelekea
nje na wakati huo mtoto alishasogea karibu yake akitarajia lile tendo kutoka
kwa baba yake..na alivyoona baba yake anasimama akajua atapakatwa na kuinuliwa juu kwa juu kama
kawaida yake, na mtoto alipoona baba yake anatoka nje akasema
‘Si-sikamoo….baba….’
Lakini baba yake alishatoka nje, na hapo akabakia kasimama na
alipogeuka upande ule wa mlango wa kutokea jikoni, ndio akawaona nesi na mama
yake wakiwa wamesimama na vyakula kwenye sinia kubwa…mama yake huyu alimuangalai kwa jicho la huruma, na mtoto kwa haraka akamkimbilia, mama yake akisema;
‘Mama..baba..mama taka baba….’akasema
‘Ohh, mwanangu,…umekuja…ohh nimekumis kweli..haujambo mwanangu…’mama
mwenye nyumba akamuinua mtoto na kufanya afanyavyo baba yake, na baadaye
akampakata na kuanza kumuangalia machoni.
‘Si-sikamoo, mama..’akasalimia mtoto sasa akiwa anafuraha maana
yupo mikononi mwa mama yake na nesi hakuweza kujizuia akaona machozi yakimtoka.
‘Marahaba…haujambo, una njaa eeh, ngoja nikupe chakula chako
unachokipenda,…’akasema na kumchukua mtoto wakaelekea jikoni, huku nyuma nesi
akawa anawaandalia wageni na baadaye baba mwenye nyumba akaingia, na
kulionekana kama kuna kitu kimepita maana ukimiya ulitanda zaidi..
********
‘Rafiki yangu naona muda umepita sana…’alisema rafiki yangu
akisimama kutaka kuondoka
‘Hapana huwezi kuachia hapo, niambie kwanza ilikuwaje, yule mama
kaenda wapi,. Na huyo mtoto alibakia hapo…au ilikuwaje?’ nikamuuliza rafiki
yangu
Mkumbuke kuwa kisa hiki anayenisimulia ni rafiki yangu, lakini
maelezo hayo aliyokuwa akisimulia hadi hapo ni maelezo aliyoyapata kutoka kwa
mama yake..
`Kwahiyo baada ya hapo mtoto akapelekwa kwa mama yake, au
ilikuwaje?’ Nikamuuliza rafiki yangu ambaye alikuwa akitaka kuondoka , na
mimi na jamaa wengine waliokuwepo hapo ambao ilibidi waje na wao
wasikilize..baada ya kuona umuhimu wa kisa hicho..na wao walikuwa na hamu ya
kujua nini kilitokea baadaye. Nilijua kama nitamruhusu aondoke itakuwa sio
rahisi kumpata tena. Nikamganda kwa maswali!
‘Bwana wee, naona nia yako unataka nikuhadithie kila kitu,..kuna
sehemu siwezi kuzisimulia hapa tena…na sikutaka mtu ajue hayo yaliyotokea…,
kwani kiujumla kumbukumbu zake zinanitia machungu sana…’akasema
‘Lakini umeshaanza kunisimulia,…na ukiachia hapo utanifanya
nibakie na dukuduku moyoni…tafadhali endelea umalizie tu….’nikasema.
‘Hapo nilipofikia ndio mwisho wa sehemu aliyonisimulia mama, kutoka
hapo hakuweza kusema tena….’akasema
‘Hakuweza kusema tena…kwanini?’ nikamuuliza
‘Mama alikuwa katika hali mbaya, muda wote ananisimulia kisa hicho
alikuwa kumbe anaumai ndani kwa ndani..alikuwa akijikaza tu kunisimulia,
ikafika sehemu hajiwezi tena,hawezi kuongea…’akasema
‘Oh….’nikaguna.
‘Lakini ngoja nikuanzie maisha yangu na mama, ingawaje niliishi
naye kwa muda mfupi kabla ya kutengana naye katika mzingira ya kutatanisha…kumbukumbu
zangu zilianza kujua ni nini kinaendelea wakati nipo na mama yangu huyo…’akasema
‘Mama yupi?’ nikamuuliza
‘Mama aliyenizaa..’akasema
‘Ulifikaje kwake…?’ nikamuuliza
‘Hadi hapo, sehemu hiyo, sikukumbuka ilikuwaje…’akasema
‘Mama hakukusimulia..?’ nikamuuliza
‘Hadi hapo,…hapana…kama unataka nikuhadithie kimtiririko
ilivyokuwa …hadi hapo sikumbuki kilichotokea,..’akasema
‘Mhh, sasa…eeh..’nikabakia kutaka kujua, maana sehemu hiyo ni
muhimu sana, akaniangalia halafu akatabsamu…akasema
‘Sasa nitakuhadithia maisha yangu na mama mzazi…kipindi hicho nipo
naye, ukumbuke mama alikuwa hana kitu, hajui wapi pa kuishi,..hajui atakula
nini…lakini pamoja na hayo, mama alinipenda sana, na hakutaka kabisa niachane
naye, nilikuwa kama mboni yake ya jicho, lakini ilivyotokea, tukajikuta
tumetenganishwa tena…’akasema
‘Sijakuelewa…’nikasema.
‘Sehemu hiyo ya kwanza ya simulizi la mama iliishia hapo, ..’akasema
na mimi sikuwa na la kufanya ikabidi nimsikilize anavyokwenda na simulizi yake
…
*********
‘Nakumbuka maisha yangu na mama yalikuwa ya kutangatanga, mara leo
tupo hapa mara kesho tupo kule …na sehemu kubwa ya maisha ya mama yalikuwa ya
kuomba-omba, ili angalau mimi nipate chakula…’akaanza kuongea na machozi hapo
yalikuwa yakimlengalenga.
‘Ni…huzuni kwa kweli…ndio maana sitaki kusimilia sehemu hii…’akasema
‘Jikaze kiume bwana….’akasema jamaa mmoja aliyekuwa akifuatilia,
alikuwa na hamasa ya kutaka kujua,na mimi nilitaka hivyo hivyo, lakini
nilishaanza kumuonea huruma rafiki yangu kwani naona inampa uchungu zaidi.
‘Mhh…katika kuhangaika kwa mama, akagundua kuwa kwenye jalala moja
kuna vyakula huwa vinatupwa sana hapo, kwahiyo tukahamia hapo..sikuwa peke
yangu, kulikuwa na watoto wengine ambao hawakuwa na wazazi…’akatulia
‘Jalala….ina maana ilifikia hapo…?’ nikauliza
‘Kuna kitu niwaambie , ndio maana mimi nikiwaona akina mama
wanaomba omba mitaani,wakiwa na watoto …siwachukii, najua kabisa sio dhamira
yao..’akatulia
‘Hawajapenda iwe hivyo…ni ukweli usiopingika kuwa wengi wao
hawapendi hiyo hali..ona kama ilivyokuwa kwa mama..alitamani kabisa apate
kazi..ili alipwe, lakini ni nani atamkubali kumuajiri…kwanza ile hali yake ya
kujifunika, ikawa ni kero kwa wengine,….’akatulia
‘Kuna wakati alikwenda kwa mama Ntilia ili awasaidie kazi, ili
angalua nipate chakula…au aoshe vyombo wamlipe, lakini wanamkata, wanamuambia
ajifunue kwanza wamuone sura yake…, wanasema watamjuaje, kama ni mwizi…mama
hakutaka kabisa kujifunua..
‘Wewe uliwahi kumuona mama yako usoni kipindi hicho..?’
nikamuuliza
‘Kwa muda ule nilioishi naye hapana..sikuwahi kumuona mma yangu
akijifunua…, na sikuwa na haja ya kufanya hivyo, mimi nilijua ni mama yangu, na
kwanini anafanya hivyo haikuniingia akilini kumuuliza, nakumbuka watoto wengine
walikuwa wakiniuliza lakini mimi sikuwa na la kuwajibu..’akasema
‘Muhimu kwangu, ukilinganisha na wenzangu ni kuwa mimi nilikuwa na
ufahari maana nilikuwa na mama yangu…wenzangu walikuwa hawana wazazi…kwahiyo
kwa namna moja au nyingine walikuwa wakinione wivu…’akasema
‘Hebu kwanza nikuulize uliwezaje kumkubali huyo kuwa ni mama
yako..?’ nikamuuliza
‘Kumbukumbu hasa sijui, …unajua nilikuwa bado mdogo…nakumbuka
machache sana kutoka kwa mama mlezi hadi kwa mama huyo,..sikumbuki vyema
ilikuwaje hapo..ninachokumbuka ni kuwa nilikuwa mikononi mwa mama yangu huyo,
na nilishampenda..’akasema
‘Oh, hapo unatuacha kwenye mataa..’akasema jamaa aliyekuwa pembeni
yangu akimsikiliza rafiki yangu huyu.
‘Unakumbuka yeye ndiye aliyekuwa akinilea nikiwa na mama wa
kunilea…kama alivyonisimulia mama yangu, na nilikuwa nampenda sana..kama
alivyokuwa akinipenda mimi, kwahiyo ..hata sikumbuki..ila nilimuona na nikamtambua
kama mama yangu..kumbukumbu zangu ndivyo zinavyokumbuka, hadi hapo….’akasema
‘Hukuwa unamkumbuka mama yako wa kukulea..ukataka kurudi kwake..?’
nikamuuliza
‘Kuna muda nilikuwa nakumbuka na nilikuwa nikimuuliza mama yangu
huyo, lakini hakukuwa na muda wa maongezi, unajua utoto tena,..tunakutana na
watoto wengine tunakimbizana , tunapigana,..njaa inakushika, mama anahangaika
kunitafutia chakula…usiku unakuwa umechoka…unajikuta umelala tu…’akatulia
‘Sasa mlikuwa mnapataje chakula,..na kulala mlikuwa mnalala
wapi..?’ nikamuuliza
‘Kuna muda tulikuwa tunakosa chakula kabisa…majalala yamechomwa
moto, watupaji nao kwa roho mbaya wanakiharibu kile chakula…, mimi naishia
kulia..hapo ndio ninakuja kumkumbuka mama wa kunilea, hapo mama mzazi..atahangaika
huku na kule,…hata kwenda kupiga hodi majumbani mwa watu, kuniombea angalau
mimi nipate chochote, basi kwingine akifika mama anafukuzwa, ..lakini hakati
tamaa, mpaka apate kitu cha kunilisha…na wakati mwingine anarudi
nimeshalala..lakini atahangaika angalau niingize kitu tumboni…’akatulia
akionyesha uso wenye huzuni.
‘Na mlikuwa mnaishi wapi, …ni hapo hapo mjini, au mlirudi huko
kijijini..?’ akaulizwa
‘Ilikuwa maeneo ya hapo hapo mjini..na mama alijitahidi kubadili
maeneo ili asije akanyang’anywa mtoto wake, kwani kuna muda alikuwa akitafutwa
ili nichukuliwe na ustawi wa jamii….hospitali walifanya juhudi hizo, baada ya
kuona kuwa mama yangu hataweza kunilea…mama akatoroka mbali, na akawa anabadili
maeneo….’akasema
‘Kwahiyo ikawaje..?’ nikaulizwa
‘Kiukweli mama sikuishi naye kwa muda mrefu…kuna tukio lilitokea, …sitalisahau,
na ndilo lililonitenganisha mimi na mama yangu, sikuonana na mama tena, hadi nimekuwa
mkubwa..….’hapo akatulia na machozi yakawa sasa yanamtoka
‘Naombeni sana niishie hapa kwa leo….nitajitahidi nije niwasimulie
sehemu iliyobakia..’akasema na sikuweza kumzuia
WAZO LA LEO: Masikini, wasiojiweza, mayatima…wanastahiki
kusaidiwa , sio kwamba wamependa hiyo hali, bali ni kutokana na nakama za
kimaisha na huenda kwa kiasi kikubwa nakama hizo zimetokana na udhalili, wizi, na
ubadhirifu, wa matajiri, ambao kwa namna moja au nyingine wamafisidi haki za
hawa watu. Hata kwenye maandiko matakatifu tumeamuriwa kuwasaidia hawa watu,
..kwahiyo tusiwanyanyapae, tujitahidi kadri tuwezavyo kuwasaidia, hasa watoto…wapo
mayatima, wapo waliotelekezwa na wazazi au kwasaabbu ile na ile …hawa watoto wanahitaji
huduma yako,…kama una uwezo usione ubahili, kwani utakachotoa kwao, ndilo fungu
lako baada ya maisha ya hapa duniani.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment