Mlango wa chumbani ulifunguliwa, na
aliyejitokeza pale mlangoni alikuwa mke wa nyumba, na mume wake aliyekuwa
akiongea akakatiza maneno na kugeuka kumuangalia mke wake, kitendo hicho cha
kugeuka kuangalia huko kwenye huo mlango kilitendwa na wote waliokuwemo humo
ndani.
Mke wa mwenye nyumba taratibu akajongea
kuja eneo la mazungumzo, alikuwa
kajifunga khanga mbili, akionyesha kuchoka, tofauti na anavyotoka nje , huwa
akitoka nje huvaa gauni pana ambalo huwezi kujua yupoje….
Nesi ambaye alikuwa kaupa mgongo huo
mlango, naye akageuka kumuangalia huyo aliyetoka huko chumbani alifahamu ni
nani, alijua ni dada yake, lakini alikuwa na hamasa kujua hali ya dada yake,
ambayo ilishamtia mawazo, akiwa akijiandaa kusimama kwa adabu ya kumsalimia
dada yake, akajikuta akishikwa na butwaa,
Kwanza hakuwa na uhakika, lakini
anamfahamu dada yake alivyo, hata akifunga khanga, maumbile yake anayafahamu
vyema, akapepesa macho yakiwa hayabanduki pale yalipokuwa yakiangalia, sasa
akawa kama kagandishwa, nusu kukaa na nusu kusimama. …
‘Hivi ni kweli au ni macho yangu…’akawa
akijuliza…
Tuendelee na kisa chetu
***********
Nesi alipohakiki macho yake na kubaini kuwa hicho alichoona ni kweli,
akasimama kwa haraka, na kuelekea pale
aliposimama dada, japokuwa ni karibu tu, kwa hali ile kwake yeye alipaona ni
mbali,..lakini akajitahidi, hakuweza kuvumilia..
Na wakati huo huo , kiadabu, wote waliokuwemo humo ndani
walisimama hasa walipoona mwenyeji wao, nesi kasimama. Na docta naye alikuwa
kasimama kusalimia, yeye alikuwa karibu na ujio wa huyo mama, kwahiyo akawa wa
kwanza kunyosha mkono wa salamu, lakini mkono huo ulichelewa.
Nesi aliinuka kwa haraka ili awe wa kwanza kumfikia dada yake,akawa
kama anaruka, huku akiendelea kumkagua dada yake kwa macho, na tabasamu tele mdomoni,
…akatikisa kichwa, halafu akainuka mikono juu, akimshukuru mungu na kwa haraka
za ajabu bila kujali kuwa docta alikuwa kanyosha mkono kumsalimia dada yake,…hakujali
yeye akamkumbatia dada yake!
`Dada kwanini mumenificha kiasi hiki, hata mimi mdogo wako,
nimekukosea nini…’ akawa kamshikilia dada yake, lakini huku akiogopa
kumkumbatia zaidi…ni ada yao wawili hawa wakikutana kusalimia kwa hivi,
kuonyesha jinsi gani walivyozoeana kila wakikutana husalimiana kwa kukumbatiana,
ila hili la leo lilizidi zaidi.
Dada yake akiwa na tabasamu mdomoni, akamshikilia mdogo wake, huku
akimuangalai docta, na kwa haraka akamuachia mdogo wake, na kunyosha mkono
kusalimiana na docta…
‘Samahani sana mgeni, ..huyu mdogo wangu, hajali kuwa wewe bosi
wake unatakiwa kupewa kipaumbele zaidi…wewe hebu niachie nisalimiane na wageni…
docta eeh, hujavaa zile sare zako lakini nimekukumbuka..’akasema mama mwenye
nyumba sasa akisalimiana na huyo docta.
‘Ndio mama docta..usijali ni kawaida, yaonyesha siku nyingi
hamjaonana na ana hamu sana ya kukutana na wewe…ni kutokana na
majukumu,..alikuwa akijaribu kuomba ruhusa tunamkatalia…., natumai haujambo,
tumeambiwa ulikuwa na …..una matatizo ya kiafya.., naweza kujua shida ni nini
hasa japokuwa nikuonavyo, hali kama hiyo hutokea sana…?’ akauliza docta.
‘Nani kasema nina matatizo…ni kawaida tu…..’akasema huyo mama
akionyesha aibu fulani
‘Mueleze huyo ni docta …huoni hiyo ni bahati, kaja hadi nyumbani…’akasema
mume wake..
‘Nimesema sina matatizo,…mimi najijua, kama ningelikuwa na
matatizo ningelikwenda hospitalini kwake..’akasema mama akisalimiana sasa na
mlinzi.
Walipomaliza kusalamiana, akageuka kumuangalia mdogo wake, ambaye
alikuwa nyuma yake akiendelea kumfuatilia, tabasamu tele mdomoni akiwa habandui
macho yake pale alipokuwa akipatizama muda wote na dada yake akawa kama
anamzarau sasa…, akasema;
‘Karibuni wageni,…’akasema akigeuka huku na kule, kuna kitu
alikuwa akikitafuta, lakini hakusema, akatafuta sehemu akakaa, na mdogo wake
akasogea na kuja kukaa karibu naye.
‘Samahani mdogo wangu, kila mara tukitaka kukuambia , kunakuwa na
kipingamizi, ila wewe kama nesi nilidhania umeshanigundua, kwasababu kama
unavyoona hali haijifichi, ..nakumbuka siku ile tulipokuja tulikuwa na lengo
hilo la kukuambia, najua nilikuwa nimevaa nguo pana usingeligundua..lakini kwa
nesi au docta mzoefu unaglinigundua…hukuwa na shaka shaka….? ’akauliza
‘Nilikuwa na shaka hiyo, ….lakini sio mara ya kwanza , nakumbuka
kuna kipindi nyuma ilitokea hivi, …na haikutokea…. lakini hii sasa naona ni
heri…na inaonyesha ni ya muda, ..yani muda wote huo msinishitue..’akalalamika
nesi.
‘Samahani sana mdogo wangu, mimi na mwenzangu hatukutaka watu
watufahamu mpaka ifikie mahali ambapo hakuna jinsi…na..wewe tulitaka tukuambie
kwa wakati muafaka, tulitaka iwe kama sepriziii, ….si unakumbuka ile ya mwanzo,
wasiwai wetu ulikuwa isije ikawa hivyo tena…’akasema na kuwa kama anacheka.
‘Dada furaha niliyo nayo haielezeki…sijui nisemeje ….’
Akamkumbatia tena dada yake huku machozi yakimlengalenga, moyoni akisema , hii
ndio miujiza ya mungu, una furaha machozi yanakutoka, una huzunu huku
unacheka….mmh, hatimae familia ina furaha.
‘Haya naona tukiwaachia nyie mtaongea utafikiri hakuna wageni
wengine, shemeji wewe ni mwenyeji, angalia taratibu za kuwakirimu
wageni…’akasema shemeji mtu na mke wake akamuangalia mumewe kwa jicho la
kumuonya.
‘Kwanini, mbona unaingilia anga zangu, wewe nesi tulia, mimi
sijashindwa kuwakirimu wageni, sijachoka, siumwi…sina tatizo lolote…tulieni
kidogo, tulikuwa tunasalimiana kwanza, mambo sasa hivi….mfanyakazi kaenda kwao,
kwahiyo tupo wenyewe,…lakini hatuna shida, …tafadhali nawatoka kidogo…’akasema
mama mwenye nyumba na kusimama..na nesi kwa haraka naye akasimama na kutembea
na dada yake huku akinyosha mkono wa ushindi
Kwa pamoja mama mwenye nyumba
wakaelekea jikoni.
**********
‘Samahani sana baba mwenye nyumba, lakini sina budi nikuulize
hili, kwani mimi ni docta ambaye pamoja
na fani yangu nahitajia sana msaada wa watu, ..kiufupi mimi ni docta
ninayemuhudumia huyo mama mliye-eeh, …mwenye matatizo…’docta akaanza kuongea.
‘Mhh, sawa niulize tu…’akasema baba mwenye nyumba , huku
akionyesha ana furaha fulani tofauti na ilivyokuwa awali.
‘Huyo mama anahitajia msaada mkubwa, mimi kama docta nimejitahidi
kadri niwezavyo kutokana na utaalamu wangu, ni ni kweli sasa anajitahidi na
sasa kilichobakia ni mambo machache ambayo yanahitaji msaada wa jamii… ‘akatulia
kidogo
‘Yah, serikali ipo itamsaidia,…mimi sio tajiri…’akaanza kusema na
docta akamkatiza.
‘Nisikiliza kidogo hapo….kutokana na matatizo yaliyomtokea huyu
mama, ambayo kakumbana nayo, yalisababisha yeye kupoteza kumbukumbu zote za
nyuma, ninaposema kupoteza kumbukumbu nina maana akili yake ilisahau,
haikumbuki kabisa kile kilichotokea huko nyuma, kamsahau hata huyo mume wake..hata
ndugu zake, hata yeye mwenyewe alikuwa hajijui ni nani…’akatulia
‘Hilo ni tatizo na linajulikana kitaalamu, na linatibika…ni swala
la muda, na pia linahitajia usaidizi wa namna moja au nyingine, linahitajia
ushauri nasaha, kauli nzuri,…’akatulia
‘Kwa jinsi alivyokuja hapa,…hata kama ingelikuwa wewe
ungelikasirika…’akasema
‘Ndio hivyo yeye hapo alipo ni mgonjwa , na hiyo ni moja ya athari
za hilo tatizo, …anahitaji kusaidiwa, wewe hushangai kuwa pamoja na kusahau,
pamoja na kumsahau mume wake, lakini wewe kakumbuka haraka..’akasema kama
anauliza
‘Mhhh, labda ni kutokana na hayo aliyonitendea huko nyuma, na
yamepita…’akasema huku akikunja sura tena kutoka kwenye furaha na kuingia
kwenye huzuni.
‘Yawezekana ndio…lakini pia yawezekana yeye bado anakupenda na
yaliyotokea huko nyuma hayakuwa kusudio lake, ..kama unavyoona, mtoto wake
alikuwa kichwani mwake muda wote, kwasababu gani …ni kwasababu ya upendo wa
mama kwa mtoto, upendo huo hauna …angalia hata wanyama , ndege huwezi kufanya
kitu kwa watoto wake, ni lazima atakurukia…ni upendo wa asili…’akatulia
‘Ahaaa, una maana kanikumbuka kwa kuwa ananipenda, hahaha..leo hii
ndio akumbuke hilo, hapana…hilo la kupenda halipo..na kiukweli ni kujidanganya,
hilo..asinidanganye, …pendo langu mimi nay eye limeshapitwa na wakati..’akasema
baba mwenye nyumba
‘Ndio, …kakumbuka kwasababu ya pendo la asili… , kupenda huko sio
lazima kuwa anataka mje mrudiane,..hiyo sio lazima,… mnaweza mkapendana hata
kama kila mmoja kaoa na kuolewa, lakini zile hisia za kweli haziishi moyoni…,
hayo ni maumbile ndugu yangu, hata wewe hili lipo moyoni mwako,…’akasema docta.
‘Sijui…’akasema baba mwenye nyumba huku akitikisa kichwa.
‘Huo ndio ukweli ndugu yangu…, ndio maana hata wewe mpaka sasa
huwezi kulisahau hilo tukio, …ndio maana mpaka sasa unajiona kama una kovu lisiloponyeka…unafikiri
kwanini…’akawa kama anaulizwa
‘Mhh, ni kwasababu alinijeruhi moyo mwangu…’akasema
‘Kwanini akakujeruhi moyoni mwako,…ina maana kulikuwa hakuna
wanawake wengine, wazuri..ambao wangeliweza kuzina nafasi yake…?’ akaulizwa
‘Wapo..mmojawapo si mke wangu, kazina hiyo nafasi na nimesha
msahau yeye..’akasema
‘Hata kama atapatikana huyo,…lakini kama kulikuwa na yule
mliyewahi kupendana naye kwa dhati , pendo la asili, lisilo na masharti, moyoni
hatanduka,…sasa huyu mama kakumbuka, kuonyesha jinsi gani alivyokupenda..’akasema
‘Sijui…’akasema baba mwenye nyumba.
‘Ndugu Yangu, huo ndio ukweli, .. nyie mlikuwa na pendo la asili
pendo lisilo na mipaka, lakini ikatokea ilivyotokea mkatenganishwa….nikuambie
kitu ,yale wanayoonyesha kwenye filamu za mapenzi kusalitiana, kutengana…, sio
maigizo tu , kuwa watu walipendana, wakatenganishwa na sababu mbali mbali,
wakaja kukutana baadaye…zile ni nadharia zinazotokana na uhalisia..yapo,
yanatokea…’akasema docta
‘Kwahiyo unataka kusema nini…?’ akauliza mwenye nyumba
akimuangalai docta.
‘Kwanza umsamehe, pili uangalia jinsi ya kuwa naye karibu, ili
naye ajisikie kama binadamu…au sio docta, samahani nachangia kidogo, nisiwe tu
msikilizaji…’akasema mlinzi, na docta akatikisa kichwa kukubali. Baba mwenye
nyumba akamuangalia yule mlinzi akonyesha uso wa kutahayari, halafu akatikisa
kichwa, akasema;
‘Simuombee mtu vibaya,… lakini ili mjue jinsi gani nilivyoumizwa
hiyo siku, sio hiyo siku tu ..ni miezi , hadi, mwaka, miaka ikapita..nateseka
moyoni, najiuliza, kwanini…kwanini…nyie acheni,…ili mjue nilivyoteseka,
ingelifaa na nyie muipitie hiyo hali..inatesa…lakini nashukuru mungu…’akasema
akiangalia juu.
‘Ni kweli inatesa, ni kweli inaumiza sana..lakini mwenyewe umekiri
kuwa kutokana na hilo ukampata mwenzako mwingine ambaye alikuja kukupa mapenzi
ambayo umeona huenda usingeliyapata kutoka kwa huyo mwenzako mliyetenganishwa
naye, huoni kuwa ni mipango ya mungu…’akasema mlinzi.
‘Ni kweli…hilo nimeliona..na nashukuru kwa …japokuwa siwezi
kusahau, na swala la kumsamehe, mbona mimi nilishamsamehe zamani tu..na sina
kinyongo naye saana..japokuwa ukikumbuka bado unaumia..na kiukweli sikupenda
kuja kukutana naye tena…maana nilijua hili litatokea, nilijua tukikutana anye
hakutakuwa na amani…’akasema huku akitikisa kichwa.
‘Mungu kapanga mkutane ili yeye akuelezee ilivyokuwa kwa kinywa
chake, ili akuombe msamaha, japokuwa alichofanya …hata kama angelikuwa ni mtoto
wako, usingelipenda aende kinyume na matakwa yako au sio..chukulia angelikuwa
ni binti yako, unafikiri ungelifurahia akuhini, akatae ombi lako, akijua nyie
mpo hataraini ya kufanywa watumwa, kunyanyasikia, na ukumbuke wazazi hao
waliyayafanya hayo kwa ajili yenu watoto, mpate kula, nk…hebu angalia hilo kwa
mfano huo..’akasema docta.
‘Unajua …nyie hamunielewi, nyie hamfahamu ilivyotokea,..tulishakaa
naye kabla, tukaliongelea hilo kwa marefu na mapana yake…, na tukaliona
hilo…tulijua ubabe wa huyo mtu, lakini kwanini tumuone kama mungu, kuwa kila
akitakacho yeye hupata, kwasababu yeye ni tajiri basi tumpigie magoti,…hapana
hicho ni kiburi, na kama ni kiburi,ilitakiwa mtu afanye kitu ili ajione yeye ni
sawa tu na wengine, sasa ni nani wa kulifanya hilo….tukasema sisi tuonyeshe
mfano, tujitoe mhanga…’katulia
‘Mliongea hivyo mkakubaliana hivyo..?’ akauliza mlinzi
‘Ndio…ndio maana inaniuma,..tuliliongelea hadi .. mpaka tukala
kiapo, japo ni kiapo cha ujana…si unajua tena..tuliahidiana kuwa hakuna atakaye
msaliti mwenzake, tukaagana, tukitakiana kila laheri, kumbe ilikuwa kuagana kwa
ukweli…mwenzangu akafika huko, sijui waliongea nini, akanigeuka…unajua nyie
kwasababu mnalisikia hilo tukio kijuujuu, hamuwezi kulielewa…’akasema
‘Nakuelewa sana…na nafahamu sana jinsi gani ulivyoumia, hilo ni
moja ya mambo ambayo yakimkuta mtu yanaumiza sana….lakini cha kushukuru mungu
ni kuwa mwenzako , na wewe mwenyewe mpo hai, na mungu kawapa nafasi ya kutubu,
kuombana msamaha,..kuongea tena, na mnaweza kuongea kwa wema tu mkayasahau hayo
kwa wema tu, maanayaliyopita, yamepita muyaone kama majaliwa tu…’akasema docta
‘Docta..mimi nimekuelewa saana tu.., na mimi moyoni eeh, nimeshamsamehe
saana tu, lakini sina muda wa kuongea naye tena..hilo mnielewe…, maana yeye ana
mume wake, na mimi nina mke wangu, tutaongea ili yasaidie nini..hebu angalia
haya yaliyotokea, kaja hapa simjui, kajifunika kabisa huenda ili
nisimfahamu,..kapatwa na nini…nyie hamlioni hilo….hapana mimi na yeye basi….arudi
huko kwa mume wake…hivi kweli mnanishauri kitu kama hicho….’akawa kama anauliza
‘Aaah, lakini kujifunika huko bado ni utashi wake, hakuna
anayefahamu ni kwanini anafanya hivyo, yawezekana ni kutokana na hayo majereha,
huko kuharibika sura..lakini pia yawezekana kuwa imani yake inamtaka kufanya
hivyo…na sio kwamba mrudiane,….’akasema docta.
‘Hahaha, imani yake..hahha, hilo halipo,…mimi namfahamu bwana… labda
hilo la kuficha huko kuharibika sura, lakini pia yawezekana hakutaka
nimfahamu..’akasema
‘Hapana hilo la kutaka usimfahamu sio kweli, ….maana kitaalamu
imethibitisha kuwa mama huyo alipotewa na kumbukumbu, na sasa hivi ndio anaanza
kukumbuka, nab ado hajawa sawa, bado yupo kwenye mapambano , ndio maana nataka
unisaidie kwa hilo..’akasema docta na baba mwenye nyumba akamtolea jicho na
kusema;
‘Ni kusaidie nini…?’
akauliza
‘Nataka mimi na wewe tushirikiane, tuweze kumsaidia huyo mama
aweze kurejea katika hali yake ya kawaida, aweze kukumbuka kila kitu, aweze
kusimama kwa miguu yake mwenyewe, na ikiwezekana tuweze kumpata huyo mwanaume
wake aliyemfanyia hivyo…hilo ndio ombi langu kwako..tafadhali mkuu…’akasema
‘Eti nini…?’ akauliza baba mwenye nyumba.
‘Ni ubinadamu tu…, hebu jaribu kukumbuka enzi zile wewe na yeye
mlipokuwa wapenzi, kumbuka yale mema mliyotendeana, kumbuka …upendo wake
kwako,..usikumbuke hilo tukio lililokuumiza, ili tumsaidie huyo mama, unatakiwa
uondoe hasira, uondoe chuki, umueweke mungu wako mbele, kuwa hayo ni majaribu
na yeye keshajifunza, na kuumia kupita maelezo…hivi wewe humuonei huruma kwa
hali aliyokuwa nayo…’akasema docta.
‘Sikiliza docta, nimeshakuambai huyo ni mke wa mtu, na mimi ni
mume wa mtu, tumeshaweka mipaka,…hivi nikuulize kama inatokea mume wake anafika
halafu anikute mimi nipo na huyo mke wake tunaongea, unafikiri atafanya nini…?’
akauliza
‘Ni mpaka huyo mume wake awepo, kwa hali ilivyo, na kwa hali huyo
mama alivyotendewa, sizani kama huyo mume wake ana haja tena na huyu mama…muhimu
amkumbuke na ikibidi sisi tukutane na huyo mume wake…’akasema docta
‘Wewe hujui tu, ..wewe hujui hili kabila letu lilivyo..haya
tuachie sisi wenyewe, ….huyo mume wake kwa jinsi ninavyomfahamu, hata kama kitu
ni cha kutupa, hawezi kumpa mtu..hata kama kakitupa akaona adui yake kakiokota,
anaweza kupata sababu ya kukuumiza…mimi namfahamu sana yule mwanaume ….’akasema
‘Sisi nia na lengo letu ni kusaidia, na ingelikuwa ni bora sana
tukampata huyo mtu,hiyo ni moja ya kazi zetu kuwanasihi hao watu, kuwaelimisha,
ili waweze kukumbuka ubinadamu, tumeshakutana na watu kama hao saana, na wengi
wamejirudi, …huwezi ukamtesa binadamu mwenzako kiasi hicho,….hilo halikubaliki…yule
mama kateseka sana, kumbuka mateso hayo yatakuwa yamempata kipindi akiwa mja
mzito…’akasema docta.
‘Ni kweli hata mimi nimesikitika sana…lakini ..mmh, mimi siwezi
kukaa na huyo mama tukaongea naye tena, naomba mnielewe hivyo …’akasema
‘Mnaweza….tu..’akasema docta
‘Ili iweje,..eti tumtafute mume wake, kwa kipi ninachokitafuta kwa
huyo mwanaume,…natafuta vita..au nipate faida gani,…mimi siwezi kulifanya hilo,
na nimesema huyo mtoto wake mumrejeshe kwa mama yake, mimi siwezi kumlea huyo
mtoto tena,..nichofanya kinatosha, kwanza shukurani yake ipo wapi…hapana, mimi sipo tayari kukaa na huyo mtoto….’akasema
na kukatizwa na sauti ikisema.
‘Baba….’ilikuwa sauti ya mtoto iliyokatisha mazungumzo na wote
wakageukia kuangalia huko sauti ilipotokea,
ilikuwa ni mlangoni, na kabla hawajasema neno sauti nyingine ikasema;
‘Mimi nipo tayari kukaaa naye, hadi hapo mama yake atakupokuwa na
uwezo wa kuishi naye..’ilikuwa kauli iliyotokea mlangoni.
NB: HAYA ndugu zanguni wapendwa, niambieni hapo…najitahidi
kuwaletea haya, lakini nipo kwenye mitihani, mitihani ya kimaisha,…natafuta
jinsi gani nitaweza kuwekeza kwa hii kazi, ili niweze kutoa vitu bora zaidi ya
hivi, ...mwenye wazo, njia asisite kunitumia maoni.
WAZO LA LEO: Tunapokuwa kwenye mazungumzo ya watu
wawili au zaidi , tupende kupeana nafasi ya maongezi, ni kweli kuna wataalamu
wa kuongea na wakiongea ni rahisi sana kueleweka na kufikisha ujumbe kwa
wengine, na pia kuna ambao hawana utaalamu wa kuongea sana, lakini wanaweza
wakawa wanafahamu hilo jamb mnaloliongelea huenda zaidi ya huyo muongeaji.
Cha muhimu kwenye hadhira, au kwenye maongezi, kupeana nafasi hata
ikibidi kumuongoza huyu ambaye sio muongeaji, maana anaweza akawa anafahamu
jambo lenye faida kubwa kuliko mnavyofahamu. Tusidharau kauli za wengine kwenye
maongezi, tisidharau watu kutokana na jinsi walivyo, tusipende kukatiza watu
wanapoongea tunaweza kukosa faida kubwa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment