‘Tulifanya hivyo ili huyo mtoto
apatikane,….na kwasababu mtoto keshapatikana bila madhara, maana watekaji wa
watoto wanakuwa na ajenda ya siri, kuna hao wa ushirikina wanawakata watoto
viungo, wengine wanawafanyia mambo machafu, …sisi tuliyaona hayo tukaona
tutumia njia hii ya busara…’akatulia
‘Sasa kilichobakia, ambacho kilikuwa
katika mpangilio wetu, ni kufanya vipimo vyote muhimu..kuangalia afya yake, na
jingine kuhakiki kitaalamu kuwa huyu mtoto ni mtoto kweli wa huyo mama, …, na
kama huyo mama sio mama wa huyo mtoto tutajua nini cha kufanya…’akasema.
Na wakati taratibu hizo zikifanyika, nesi
wewe utabeba dhamana ya huyo mtoto, utakaa na huyo mtoto, utakwenda kukaa naye
huko nyumbani kwako..’akaambiwa
‘Docta…’ akaanza kulalamika
Tuendelee na kisa chetu
*************
Amri ikatolewa kuwa vipimo muhimu kwa mtotop vifabyike ili kujua hali ya mtoto
na pia vipimo vingine vifanyika kwa huyo mama, ili kuweza kumtambua kama kweli mama
huyo ndiye mama mwenye mtoto kihalali na hili lifanyike kwa haraka.
Kazi hiyo ikapewa kipaumbele,
huku dakitari wa akili akipewa jukumu la kumhudumia huyo mama na kuhakikisha
anagundua nini kinachomsumbua. Na kuwa muda huo huyo mama alikuwa katulia, na
alikuwa hajaambiwa kuwa mtoto anayemtaak yupo tayari kwenye mamlaka ya
hospitalini.
Nesi naye akaendelea na jukumu la malezi ya huyo mtoto, kwani kama
itaonekana kuwa siyoo huyo mama mhusika, inabidi mtoto huyo arudishwe kwa
wazazi walezi, ambao walishakubali kubebe hiyo dhamana.
Ilikuwa asubuhi, kazi zimeanza kila mtu akiwajibika kwenye kazi
yake, docta bingwa wa magonjwa ya akili akafika chumba maalumu ambapo
wamemuweka huyo mama, alitakiwa kupelekwa wodini, lakini kiusalama akawa kwenye
chumba hicho.
Docta aliingia pale kwenye chumba, hakumkuta nesi, moja kwa
moja akelekea kwenye kitanda anapolala yule mama, alijua kuna mtu kalala,
akafika na kuinua shuka taratibu, huku kichwani akiwaza, nini kimemsibu huyu
mama, au kazidiwa na kupoteza fahamu, au…
‘Huu ulalaji sio wa kawaida…’akawa anaongea kimoyo moyo,
‘Na huyu mama hana kawaida kujifunika kiasi kile, lakini hata
hivyo, aliona ajabu mtu gani angekuwa kalala vile kitandani, ajifunike kutoka
vidolenihadi kichwa chote na joto lote hili, akahisi kuna kitu kimefanyika na
kama ndivyo anavyohisi basi huyo mama ana ajenda ya siri.
Akalifunua lile shuka, sehemu ndogo ya eneo analojua ni la kichwani,
docta akaliachia huku akiguna, halafu akageuka na kumuona nesi anaingia
mlangoni, akalirudishia lile shuka kama lilivyokuwa, na kugeuka kuondoka pale
kitandani
Nesi akaja hadi pale kitandani na kuiona ile hali, akasema
‘Mungu wangu, huyu mama ananini tena…’ akasema nesi huku akilifunua
lile shuka lote kitandani , na alipohakikisha kuwa anachokiona ni sawa,
akamgeukia docta, ambaye alikuwa kaduwaa kwa muda…Docta akatizama huku na kule
halafu akamtizama nesi kutaka kupata maelezo, na nesi kwa muda huo alikuwa akilirudishia
lile shuka na kusogea kitanda cha pili yake! Akamtizama mgonjwa aliyelala
kwenye kile itanda, yule mgonjwa alikuwa kalala fofofo.
Aliogopa kumwamsha, lakini akaona kwa dharura kama ile hana jinsi,
akamtikisa kidogo yule mgonjwa , na yule mgonjwa akafunua macho kwa shida,
kwani usingizi bado umemjaa, lakini alipomuona kuwa aliyesimama mbele yake ni nesi,
akainuka haraka na kuanza kulalamika.
‘Mwambie Docta mbavu zinanibana sana, halafu,. …’ akawa
anaonyeshea sehemu za mbavu, na dakitari aliyekuwa aksimama karibu akasogea
pale kumuona huyo mgonjwa, akajifanya anamchunguza, lakini mawazo yake yalikuwa
yakiwaza mbali.
‘Usijali utapata dawa …’akasema na kurudi kwenye kile kitanda cha
kwanza alichokuwa kalala yule mama, na
kabla hajamwambia kitu yule mgonjwa anayelalamika, akamgeukia nesi, nesi
alikuwa bado kuduwaa hakujua aseme nini nesi mawazoni anahisi huenda huyo
dakitari anajua wapi alipoelekea huyo mama
Baadaye akamsogelea yule mgonjwa na kumuuliza;
‘Mto wako wa kulalia upo wapi?’
Dakitari akawa anaendelea kukagua kile kitanda alichokuwa kalala
huyo mgonjwa, na yule mgonjwa akashangaa alipoona kalala bila mto wake,
akajitetea kuwa yeye haoni tofauti ya kulalia na mto au kutokuulalia, kwani
hana mazoea ya kutumia mto. Docta akasogea kitanda kingine, ambacho kilikuwa
hakina mtu akaona kuwa na mto wake haupo pia.
‘Nesi huyu mgonjwa atakuwa kaenda mbali sana, na sidhanii hata
kama tukimtafuta tutamkuta maeneo ya humu hospitalini, lakini kwa usalama ngoja
tuwaarifu walinzi wamtafute,,’ akasema docta huku akikagua sehemu za vyoo na
bafuni.
Alitaka kumwambia nesi afanye hiyo kazi lakini kwa haraka aliyo
nayo akaamua kufanya ukaguzi huo mwenyewe, na alipohakikisha kuwa huyupo popote
humo ndani,akachukua simu yake na kumwita mlinzi.
Yule mlinzi alipokuja akatizama moja kwa moja kitanda cha yule
mgonjwa akijua kuwa kaitiwa kuhusiana na vurugu za yule mama na alitakiwa
kumdhibiti au kuchukua hatua fulani , lakini hakuona dalili ya yule mama, na
akamwangalia Docta asikie nini anachoambiwa.
‘Nakumbuka tuliwaambia muwe makini na yule mama aliyekuwa analeta
fujo, …na muhakikishe akitoka nje, kuna mtu yupo naye, ….sasa huyu mama
yaonekana katoka, na dalili za humu ndani zaonyesha kuwa alidhamiria kufanya
hivyo…je mlimuona huyo mama akitoka…?’ akauliza docta
‘Sawa kabisa, lakini tangu muda ule hajaleta vurugu yoyote, na
kuna muda tuliamua kuja kumchunguza, na tulimkuta kalala, tena kalala fofofo, tukaona tupumzike tu hapo
nje…’ akasema yule mlinzi
‘Sasa yupo wapi huyo mama?’ akauliza docta
‘Si huyo hapo kalala, na anaonekana amelala kama gogo…’ akasema
yule mlinzi akisogelea kile kitanda, lakini alipokikaribia akashikwa na butwaa,
akamwangalia Docta, halafu akainua shuka kwa mashaka, kwani alijua kama huyo
mama yupo, itakuwa kosa…lakini kwa jinsi ilivyo, ilionekana hakuna mtu au kama
yupo mtu ni mfu… kabla halijafunuka lote akalirudisha lile shuka haraka.
Akamwangalia Docta tena
‘Ina maana gani Docta…?’ akauliza yule mlinzi
‘Nikuulize wewe, kuwa hii ndio kazi mliyopewa kuifanya,, hamuoni
sasa mtawajibika mbele ya sheria, na kama kuna lolote baya itabidi …nyie
muwajibike…’ akasema Docta, na kabla hajamaliza yule mlinzi akaanza kukagua
vyema , akamtizama nesi na kabla hajapata alichotaka kusema akaelekea sehemu ya
vyoo na huko alikaa kwa muda liporudi akasema kwa wasiwasi.
‘Huku hayupo, ina maana aliweka hiyo mito hivyo hapo kitandani
kuonyesha kuwa kalala, halafu akatoroka…lakini akili ya kufanya hivyo imetokea
wapi…..haiwezekani, na katorokea wapi…alipitia wapi….?’ akasema yule mlinzi
kama anauliza
‘Wewe wasema hivyo, na unajua wewe kuwa kafanya hivyo na
kutoroka…sisi hatujui, tunataka mkaandikishe hayo maelezo yenu haraka kwa
Dakitari mkuu..’ akasema Docta huku akitoka mle wodini, na nesi akamfuata docta
wake nyuma, huku wote wakiwaza kuhusiana na tukio hilo la aina yake.
Walipofika kwa Dakitari mkuu na kuelezea nini kimetokea, ikabidi
walinzi waitwe kujieleza, na wao hawakuwa na jipya la kuelezea, zaidi ya kusema
wao walijua kuwa yule mgonjwa kalala, na waliogopa kwenda kumwamsha. Na kama
katoroka, hawana uhakika katorokaje, kwani yeye ni rahisi kugundulika kwa
uvaaji wake wa kujifunika usoni, …
‘Tumejaribu kutafuta sehemu zote za hospitalini na kuulizia kama
kuna mtu yoyote kamuona huyo mama,lakini hakuna mtu yoyote aliyemuona mwanamke
kama yeye, kwahiyo ina maana kuwa alipotoka, labda alijifunua uso au
alijifunika kinamna nyingine ambayo mtu mwingine asingeweza kumtilia mashaka..’akasema
mlinzi.
‘Sasa atakuwa kaenda wapi na kwanini aamue kutoroka
hospitalini..?’ akauliza Dakitari mkuu
‘Au kagundua kuwa alichokuwa akidai ni uongo na kwa vile kaona
atagundulika uongo wake akaona atoroke..jana tulipotaka kumtoa damu aligoma,
hadi tukambembeleza ndio akakubali….sasa hiyo inaonyesha kuwa huyu mama, ana
ajenda ya siri…au?’ akasema nesi kwa mashaka, huku akimtizama docta.
‘Mimi sidhani kuwa ametoroka kwasababu hiyo ya kuogopa kuwa kasema
uongo, mimi nadhani kuwa , kwa vile kumbukumbu zimeanza kumrejea, huenda ana
kitu anakifuatilia na anataka kuhakikisha kuwa jambo fulani alilolifanya
kipindi fulani ni kweli…’ akasema docta bingwa. Alipomuona nesi wake
hajamuelewa vyema, akafafanua nini alichokuwa akimaanisha;
‘Kwa uzoefu wangu wa hawa wagonjwa, pindi fahamu na kumbukumbu
zinapoanza kuwarejea, huwa wadadisi sana, na kujaribu kufuatilia mambo ambayo
waliyayafanya au kuhakikisha kuwa kweli walifanya hivyo…’akatulia
‘Sasa anafuatilia nini..?’ akauliza nesi.
‘Kwasasa huwezi kusema anafuatilia nini…na wakati mwingine inaweza
kuwa hatari, kwani katika kufuatilai hivyo wanaweza wakagundua kuwa walifanya
jambo baya na wanataka kuficha siri, kwahiyo wanaweza hata kudhuru au kuua, ili
kuficha siri…au wakaona wamefanya jambo la aibu, na wengine huishia kujiua,
sasa cha muhimu ni kujaribu kufikiria nyendo zake siku mbili tatu…’ akasema
docta
‘Na huko kijijini alipokuwa akiishi,…alikuwa na tabia za ajabu
ajabu kutoroka…au …?’ aakuliza docta
‘Mimi nijuavyo huyu mama kwa mara ya mwisho alikuwa akiishi na
ndugu zangu, na sikuwahi kusikia kufanya jambo baya. Watu kwa imani zao haba
wao ndio walimzushia kuwa eti ni mchawi, na hata kufikia kumuunguza na moto..’
akasema nesi
‘Isije kawakumbuka hawo wabaya wake na labda kaamua kwenda
kuliipiza kisasi, maana mama mwenyewe anaonekana kaka kishari shari, na alivyo,
anaweza kupambana na midume, na hata kuitoa jasho..’ akasema mlinzi.
‘Cha muhimu watu wajaribu kufuatilia wapi alipopitia hasa huko kwa
ndugu zako …na naona ni vyema uwasiliane na ndugu zako haraka iwezekanavyo,
kama hajafika huko, wajiandae na kama kafika huko tujue kuwa kuna usalama….
hebu wapigie simu nesi sasa hivi tusikie watasema nini, na kuwatahadharisha…,’akasema
Nesi akachukua simu na kuanza kupiga namba ya shekemji yake, ikawa
inaita bila kupokelewa, akapiga simu ya dada yake. Na wakati nesi anajaribu
kupiga simu. Docta bingwa na mkuu wao, wakawa wanaulizana hili na liel kuhusu
huyo mama, kama kuna lolote wanaloweza kulifanya kwa muda huo.
‘Ina haja ya kuwajulisha watu wa usalama…polisi’akauliza mlinzi
‘Bado..sio muda muafaka, yawezekana huyo mama yupo maeneo ya hapa
karibu tu…’akasema docta mkuu, na docta bingwa akatikisa kichwa kukubali.
‘Hawezi akawa kaenda mbali, lakini kwa tahadhari ni bora kufanya
kila liwezekanavyo ili kuona hakuna madhara yanayoweza kutokea kwake na kwa
watu wengine.
********
Docta bingwa alikuwa akimuwazia sana huyo mama, tangu amuone huyu
mama amekuwa akihisi kuna jambo zaidi linalimsumbua huyu mama, na mwanzo alihisi
huenda ni sababu ya kumtaka mtoto wake. Lakini kadri siku zilivyokwenda akahisi
kuna zaidi ya hilo.
Yeye alishahisi kuwa huyu mama hana ugonjwa wa akili kama watu
wengi wanavyomfikiria, kwasababu zile dalili za ugonjwa wa kili hazipo kwenye
matendo yakea. Alichogundua ni kuwa mama huyu alipoteza kumbukumbu, na hii
kitaalamu inaitwa `amnesia’ na lazima
ipo sababu kubwa iliyofikia hadi mama huyu akapoteza kumbukumbu.
Kitu ambacho kinamshangaza ni kuwa kila anapojaribu kupata habari
moja, anajikuta anakabiliwa na tatizo jingine ambalo anashindwa kuliunganisha
moja kwa moja na tatizo lilopita. Alikuwa na hamu sana ya kupata kumbukumbu za
mama huyu, lakini wamejaribu kuzitafuta bila mafanikio, inaonekana kumbukumbu
zote zilishaharibika kabisa, na huyu mama hajaweza kukumbuka kabisa asili
yake,..alichoweza kukumbuka zaidi ni mtoto na jinsi alivyompata…
Na alipojaribu kumuulizia huyo dakitari aliyemfanyia upasuaji , na
yeye alisema hana taarifa zazote za wapi huyo mama anatokea, na hakupata nafasi
ya kujua ni kitu gani kilimsibu huyo mama kama ni kweli huyo mama ndiye huyo
aliyewahi kumfanyia upasuaji.
Kwa uhakika alishindwa
kukubali moja kwa moja kuwa huyo mama aliyefanyiwa upasuaji na huyo docta ndio
huyo mama waliye naye hapo mpaka vipimo vitoke, na hata kama docta huyu ataweza
kumtumia picha, ni jinsi gani ya kumshawishi huyo mama ajifunue, maana kagoma
kabisa kufanya hivyo.
Kwa uchunguzi wa
harakaharaka na dalili inaonekana akawa ndiye huyo mama, ..na docta mkuu ambaye
aliwahi kumuona huyo mama usoni, anasema mtoto anafanana na huyo mama, lakini
kufanana yaweza ikawa sio sababu, anaweza akazuka ndugu wa huyo mama kwa
malengo yake akaja kumdai huyo mtoto …!
‘Je huyo mama tunawezaje kumpata?’ lilikuwa swali muhimu kwao.
‘Ni kwanini atoroke…?’ akauliza docta mwenzake.
‘Huyu mtu hajatoroka, nina uhakika kuna jambo analifuatilia,…’akasema
docta mwenzake.
‘Lakini umesema kapanga mito kaam vile mtu kalala,..hivi
unalionaje hilo si kuonyesha kuwa huyo mama kadhamiria, ni kama shushu fulani
hivi….’akasema docta mkuu.
‘Unahisi ana akzi anaifanya humu..hahahaha, sio kweli….’akasema
mwenzake
‘Simu za ndugu zangu zote ..mwanzoni nilipiga zikaita lakini sasa
kila nikipiga hazipatikani tena, sijui
kuna tatizo gani, sio kawaida yao kuzima simu zao wote wawili..’ akasema nesi
huku akiwa kachanganyikwa.
‘Labda zimeisha chaji, siunajua tena tatizo hili la umeme na
mgawo..’ akasema docta mkuu. Na wakati wanaongea nini kifanyike zaidi simu ya
nesi ikaita ghafla na namba iliyoita ni namba ngeni kwenye simu yake.
‘Halloh wewe ni nesi .?.’ sauti ikawa inauliza na simu hakiuwa na
mawasiliano mazuri.
‘Ndio wewe ni nani,..?’ akauliza
‘Mimi ni jirani na ndugu zako,….hapa kijijini’ sauti ikasema
‘Kuna tatizo gani huko kijijini….?’nesi akauliza kwa mashaka
‘Nimepewa ujumbe nikupigia, dada yako anasema kaam inawezekana uje
huku kwani ana matatizo makubwa…’ simu ikawa imekatika na hata walivyojaribu
kupiga tena ikawa haipatikani.
‘Kuna tatizo ..ndugu zangu wamepatwa na nini tena, na kwanini simu
zao zisipatikane…’nesi akawa anajiuliza na madocta wakawa kimia wakilitafakari
hilo.
‘Au huyo mama keshafika huko…sasa utamuuliza nani, hakuna jamaa
yoyote wa huko unayeweza kumuulizia kama una namba yake..?’ akauliza docta
‘Mhh, sina nilikuwa nayo ya jirani wa hapo, lakini akabadili
namba, simu yake ilipoibiwa, na sijawahi kupata namba yake hiiyo mpya…’akasema
‘Jaribu kuwapigia tena na tena…’akaambiwa na nesi akafanya hivyo
bila mafanikio…
‘Mhh….sasa tufanyeje, maana wewe huwezi kuondoka kwa vile kuna
hili tatizo, kwanza mtoto yupo wapi..?’ akaulizwa nesi
‘Yupo chumba cha watoto anacheza na wenzake, nesi anamlinda hakuna
tatizo naye…’akasema
‘Una uhakika..?’ akauliza docta mkuu
‘Kwanini unasema hivyo…’akauliza nesi,
‘Nenda kahakikishe….’akasema docta akionyesha wasi wasi fulani...
NB:Je kuna nini ,usicheze mbali!
WAZO LA LEO: Tumshukuru mola kwa kila jambo likiwa jema au baya...japokuwa mengine yanaweza kua magumu kiasi kwamba mtu ukajiona kama wewe umeonewa huo ugumu unaweza kuwa ndio ngazi ya kwenda kwenye mafanikio. Muhimu, kujibidisha kwenye mambo ya heri , na kuwa na subra kwenye matatizo, tutafanikiwa tu
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment