Haikuchukua muda dada mtu aliamuka hata
kabla hajafanyiwa huduma ya kwanza, akasema alihisi kizunguzungu tu, na sasa
yuopo salama, akasema anataka kuondoka kwani mume wake atakasirika kama
akichelewa zaidi.
‘Dada lakini unaonekana haupo sawa,
kwanini tusikupime kwanza, ..?’ nesi akamuuliza
‘Hapana wewe mwenyewe unamfahamu shemeji
yako, mimi sina tatizo, mtoto…’akajisahau kuwa hatakiw kuondoka na mtoto.
‘Kalala…’akaambiwa
‘Oh mungu wangu unajua nilihisi ninaota
kumbe ni kweli…mungu wangu, ..haya mimi nitafanyaje..’akasema akianza kuondoka
‘Dada lakini nakuona haupo sawa…’akasema
nesi
‘Nipo sawa, ….usijali, nimekuachia huyo
mtoto lakini moyoni sijarizika,….’akasema sasa akitembea kwa mwendo wa haraka
kuondoka…
Tuendelee na kisa chetu.
‘Yaani mdogo wangu, ndio umeamua hivyo, yaani wewe na shemeji yako
mumeamua kuninyang’anya mtoto wangu, kipenzi changu…’ akaanza kulia kwa sauti,
huku akimpa mdogo wake mkoba waliokuwa wamebebea juice ya mtoto na maziwa.
Nesi huku naye machozi yakimlenga lenga akachukua ule mkoba na
akageuka kuondoka hakutaka kuangaliana na ndugu yake tena, kwani nay eye
angeendelea kulia,
Nesi aliondoka moja kwa moja hadi ofisi ya mkuu wa madakitari kwa
bosi wake, alipofika akakuta huyo bosi wake katoka. Akageuka na kwenda ofisi ya
dakitari bingwa, akamkuta naye hayupo, ikabidi asubirie hapo..aliona labda ,
aende moja kwa moja wodini akaongee na huyo mama anayedai mtoto wake, kuwa
mtoto huyo keshamleta. Akaona sio vyema,
lazima kwanza akutane na wakubwa zake ili ajue utaratibu upoje.
Ni wakati huo akiwaza hatua gani ifuate ndipo simu yake ya mkononi
ikaita, na alipoitizama akaona ni simu kutoka nje,akaihisi atakuwa ni dakitari
kijana, japokuwa namba ilikuwa tofauti na ile anayoifahamu yeye.
‘Vipi sister, mambo yanaendaje huko, ulipata kumbukumbu zozote za
yule mama…?’ akauliza, ilikuwa sauti ya docta kijana. Na nesi alipoikisikia
hiyo sauti akashukuru mungu, akijua sasa angalau kapata mtu wa kubeba naye hilo
jukumu. Akatafuta sehemu ya kukaa, ili aweze kuongea vyema.
‘Docta, yaani hapa nilipo nimechanganyikiwa maana mambo yamekwenda
haraka na hata sijui nifanyeje…’akasema
‘Kwani kumetokea nini..?’ akaulizwa, na mara akamuona nesi akija
kwake akiwa na yule mtoto, akamuashiria huyo nesi kuwa anaongea na simu.
‘Hutaamini kuwa hapa nilipo nipo na yule mtoto, …’akasema
‘Oh, kwanini, utafanyaje kazi na huyo mtoto , si mtoto huyo
alikuwa kwenye mamlaka ya ndugu zako kwani imetokea nini,….?’ Akauliza
‘Kumetokea mambo makubwa..ikabidi huyo mtoto aletwe hapa
hospitalini, kwani yule mama anadai kuwa ni mtoto wake,…’akasema
‘Kwa ushahidi gani mna uhakika huyo mama ndiye mwenyewe, muwe
makini na hilo…’akasema
‘Utawala na watu wa usalama wamesema wamethibitisha kuwa ni kweli
huyo mama ndiye mwenye mtoto..’akasema
‘Watu wa usalama ina maana polisi wameingilia kati?’ akauliza
‘Ndio na nilishikiliwa kituoni kwa kosa la kumchukua mtoto bila
maandishi, kilichoniokoa ni ukweli tu…..’akasema.
‘Mhh na ndugu zake wamesemaje maana nijuavyo watakuwa walishamzoea
huyo mtoto kama mtoto wao?’ akauliza
‘Hutaamini hapa nilikuwa nalia na dada yangu…, dada yangu
hakupenda kabisa, kuachana naye…lakinii hakukuwa na lakufanya kwani huyo mama amedai kuwa hataki ushauri na
yoyote yule anachotaka ni mtoto wake. Yaani hapa nilipo bado nina wasiwasi kwani
huyo mama ananitafuta kila wodi, na ameapa kuwa akininipa atafanyia kitu
ambacho sitakisahau…yaani hapa hospitalini, hakukaliki, ….’akasema
‘Sister, naomba muwe makini na maamuzi yenu, maana mtu yoyote
mwenye nia mbaya anaweza kutunga uwongo wa namna hiyo, mimi sijawa na uhakika,
maana kama mama huyo alikufa..umesema wamathibitisha kwa vipimo…mmh, lakini je
kama ndiye huyo mama yake, kweli anaweza uishi na huyo mtoto…je akili za huyo mama zipo sawasawa…maana kama
ulivyosema analeta fujo, huenda bado akili yake haijakaa sawa….?’ akauliza huyu
docta.
‘Sina uhakika na hilo bado maana mambo yote sasa hivi
yanashughulikiwa na dakitari bingwa wa mambo ya akili..na ulisema bado na wewe
unatafuta zile kumbukumbu umeshazipata…?’ akauliza nesi.
‘Yah….ila bado sijapata muda wa kuzipitia unajua tulikuwa na
mitihani na mambo mengi ya kufanya, nitazipitia na nitaona jinsi gani ya
kusaidia…’akasema
‘Lakini kwa hivi sasa sioni kwamba itasaidia kitu..’akasema nesi
‘Kwanini….?’ Akauliza
‘Mtoto ni lazima akabidhiwe kwa huyo mama, na mtoto ninaye, …huoni
kama itachelewa, sijui ufanyeje..’akasema
‘Nitaongea na huyo docta, ili tujue nini cha kufanya kitaalamu,
naomba umwambia nitampigia simu baada ya nusu saa hivi, kwani nipo kazini kwa
vitendo, unajua masomo yetu yalivyo, kuna vitendo na darasani….’akasema
‘Kwahiyo unataka kusema nini kuhusu huyu mtoto?’ akauliza nesi.
‘Hakikisha kuwa huyo mtoto hafiki mikononi kwa huyo mama kwanza,
mpaak nionge na huyo docta…’ simu ikakatika!
‘Mhh, mbona huyu naye ananichanganya kwani kagundua nini….mbona
hawa wamesema kuwa wamehakikisha kuwa huyu mtoto ni halali ya huyo mama,
….mmh,..’akawa anaongea peke yake na nesi aliyekuwa na huyo mtoto akamsogelea
na kumwambia
‘Mtoto anamtaka mama yake….’akasema, na nesi akamchukua huyo mtoto
na kuanza kumuongelesha
‘Mama kaenda sokoni, atakuja na zawadi…’akasema
‘Nataka-mama angu….’akasema
‘Atakuja sasa hivi, …’akasema na kuchukua ule mkoba alioachiwa na
dada yake, akatoa ile chupa yenye maziwa akampa mtoto na mtoto kwanza alikataa
akisema anamtaka mama yake.
‘Nataka mama..angu….’akawa anaanza kulia, nesi akahisi machungu
moyoni akatamani amchukue na kuwakimbilia ndugu zake kama hawajaondoka, lakini
hilo haliwezekani tena, ikabidi afanye kazi ya ziada ya kumbembeleza yule mtoto
hadi mtoto akakubali kunywa yale maziwa na alipomaliza akashikwa na usingizi
ikawa ndio nafuu yake.
Huyo mtoto alikuwa ana afya njema, miaka miwili, ila alionekana
hajaweza kuunganisha maneno vyema, akawa kakaa naye akiwa kamlaza mapajani, na
kwa mbali fikira zikamjia kuwa huyo angekuwa ni mtoto wake, na na docta kijana, mbona angejisikia raha.
Akachukua mkono wa yule mtoto kumwangalia vidole vyake, halafu
akawa anamshika kichwani huku akiwaza, mengi, hasa jinsi gani angepata nafasi
ya kumwambia docta kijana anampenda na hatamani mwanaume mwingine yoyote, kwani
muda mwingi amekuwa akimuwaza yeye.
‘Umegeuza ofisi yangu, chumba cha kulelea watoto…huyu mtoto ana
matatizo ya akili..?’ akagutuka kusikia sauti ya bosi wake..alikuwa dakitari bingwa
wa mambo ya akili, na kwa haraka akainuka pale kwenye kiti huku akiwa kambeba
huyo mtoto mkononi
‘Kwani huyo mtoto ana matatizo gani, kwanini usimpeleke kwa
dakitari wa watoto unanileta huko ofisini kwangu, na leo nina mambo mengi ya
kufanya…’akasema akionyesha kuchoka.
‘Docta, huyu ndiye yule mtoto anayetafutwa na yule mama…’ akasema
nesi na yule dakitari aliposikia hivyo akainua kichwa na kumtizama huyo mtoto,
halafu akasema.
‘Oh, lakini haya maswala unatakiwa kwenda kwa dakitari mkuu,
hayapo mikononi mwangu si unajua tena utaratibu au nenda kwa msaidizi wake..’akasema
huyo mkuu wake.
‘Sawa najua wewe ndiye unyeshughulika na huyo mama, nikaona na
wewe ni mhusika mkuu, au nimekosea….’akasema.
‘Ok ni hivi…sasa hivi tumetoka kujadili hili swala na
ilishaamuliwa kuwa huyo mama apewe mtoto wake, akishapewa tutaangalia
maabdiliko ..ni lazima kutakuwa na mabdiliko kwa huyo mama, na inaweza
kumsaidia akapona kwa haraka, na kukumbuka kila kitu…’akasema
‘Sasa mimi nauliza huyo mtoto si ndio anatakiwa kukabidhiwa kwa
huyo mama, sasa si wewe docta wake, ndiye unatakiwa kumpeleka huyu mtoto na
kumkabidhi au…’akasema
‘Mhh, hapana kwanza mtoto huyo tunatakiwa tumkabidhi kwa
utawala,…kulikuwa na ajenda nyingi sana leo,…na nyingie zimeshatekelezwa,a
ilibakia hili la huyo mtoto tumetoka mapumziko kidogo, …nimetoka nikajikuta
Napata kazi nyingine, wagnjwa ni wengi…..sasa mimi naona uende kwa msaidizi wa
docta mkuu atakuambia kila kitu,..natumai umenielewa…niache nifanye kazi moja
kwanza’akasema
‘Sawa bosi..’akasema
‘Na kuna swala jingine, …tunataka kujua zaidi kuhusu huyo mama, na
hili tunataka ushirikiano na ndugu zako, nahisi yule mwanaume, ni nani
kwako..?’ akauliza
‘Shemeji yangu..’akasema
‘Kuna kitu anakificha kwa huyo mama..atakuwa anamfahamu huyo mama
unajua lolote kuhusu hilo? ,…hatutaki kulichukulia uzito wake, lakini tunaomba huyo
shemeji yako, ajaribu kutoa ushirikiano tu…ni kwa manufaaa ya huyo
mama,…..’akasema
‘Mimi kwakweli sijui….nitajaribu kuongea naye nisikie
atasemaje…’akasema na kabla hajasema zaidi, simu ya huyo nesi ikaita akagundua
ni simu ya docta kijana, akamgeukia bosi wake na kusema;
‘Kuna docta aliyekuwepo kipindi hicho cha huyo mama, yeye ndiye
aliyemfanyia huyo mama upasuaji anataka kuongea na wewe..’akasema nesi
‘Kwanini siku zote hukusema hilo, kumbe ulikuwa na mawasiliano
naye…oh’akasema huyo docta na kuipokea hiyo simu
Akageukia upande mwingine na kuanza kujitambusha, na wakaanza
kuongea na huyo docta kijana….alisikiliza kwa muda halafu akasema
‘No..no…mimi sina maamuzi, …mwenye maamuzi ni docta mkuu,…unasema una uhakika...?'’akasema
na kuendelea kusikiliza.
Alisikiliza maelezo, na akawa anaandika andika kitu kwenye karatasi,
na hadi mwenzake alipomaliza kuongea, akainua uso na kumuangalia huyo nesi, na
bado akawa anasikiliza, akageuza kichwa na kumuangalia huyo mtoto, alikuwa bado
amelala. Halafu tena akamwangalia yule nesi kwa makini,…akatabasamu.
‘Ok nimekuelewa…nitalifanyia kazi,..’akasema na kumaliza maongezi
halafu akamwangalia nesi na kusema;
‘Samahani sana nesi, mimi nilishakuweka kwenye kundi la watu
wasiotimiza wajibu wao, sipendi kabisa watu wanaochezea kazi, hasa ikimuhusu
mgonjwa…unajua nesi watu wengi wanatulalamikia kuwa hospitali zetu zina utendai
mbaya, na kiukweli wanaosababisha ni watu wa ngazi zenu.
'Unajua nesi, sisi madakitari kazi
yetu ni kutoa maagizo kwenu, sasa utekelezaji unakuwa mgumu sana katika ngazi
zenu…’akasema huku akionyesha kutabsamu ile sura ya kukasirika ikawa haipo tena
hadi esi akashikwa na mshangao, hakujua wameongea nini na dakitari kijana.
‘Mimi nikiwa kazini nataka uwajibikaji, na msipotoa ushirikiano, unafikiri
sisi tutafanya nini …kwakweli kama nisingeyasikia haya maelezo,nisingeliweza
kukutetea maana swaal lako lilishafikishwa mbele ya utawala, na sijui maamuzi
yao yangelikuwaje…ok, sasa hebu twende huko kwa huyo mkuu naona kuna mambo
muhimu tunahitajika kuyafanya kabla hatujamkabidhi huyo mama mtoto wake…’
akasema akiwa na hamasa ya jambo hilo.
Wakaondoka hapo ofisini ya docta mkuu, ilikuwa ofisi ya pili yake,
wakaingia na docta mkuu alikuwa akiongea na simu, alipowaona, akawaashiria wamsubiria kwani
anaongea na simu muhimu, na alipomaliza akawakaribisha.
‘Vipi naona mna mtoto…kuna nini tena..?’ akauliza
‘Yule mtoto wa yule mama, ndiye huyo hapo, ….’akasema
‘Aah, si muda wa kuliongelea bado au kuna haraka sana..?’ akauliza
‘Nimepokea simu kwa mmoja wa madocta waliowahi kumuhudimia huyo
mama..’akasema
‘Oh , ni nani huyo..?’ akauliza huyo mkuu kwa hamasa
‘Ni docta mmoja sasa hivi yupo nje anasoma….kanielezea hilo tukio
kwa kirefu na nimemuelewa…unajua sasa hivi tunahitajika kuchukua vipimo kwa huyo
mama na mtoto tuthibitishe, kuna kuwalakini, na huenda kuna mchzo mchafu unachezwa.…kaniambia na mimi nimeona ni muhumu kuchukua vipimo, na maelezo yake yana uhakika, na
huko alipo ana vipimo kwahiyo tukishavipata hivi vipimo, tutajirizisha na yeye
pia yupo tayari kututumia vipimo vyake…na hata picha ya huyo mama…’akasema
‘Ina maana mlikuwa hamjalifanya hilo..la vipimo!, mbona mliniambia
kuwa mumeshamfanyia huyo mama vipimo na mtoto..?’ akauliza nesi.
‘Tulifanya hivyo ili huyo mtoto apatikane,….na kwasababu kaptikana
sasa cha muhimu ni kufanya hivyo vipimo vyote, na kama huyo mama sio mama wa
huyo mtoto tutajua nini cha kufanya…kwani kama tusingelifanya hivi kunamengi yangelitokea,...kuna ushahidi wa wizi wa watoto....hayo ni mambo ya kiusalama zaidi....’akasema huyo docta na kumuacha nesi akiwa
kaduwaa, kumbe yote ilikuwa ni mbinu za kuhakikisha kuwa huyo mtoto
anapatikana.
‘Sasa nesi wakati utaratibu wote huo ukifanyika, vipimo na kila
kitu huyo mtoto atakuwa kwenye mamlaka yako, utakwenda kukaa naye huko
kwako..’akaambiwa
‘Oh,…jamani mbona mnipa majukumu makubwa namna hii, mtoto mwenyewe
anamtaka mama yake..’akasema
‘Mama yake yupi ..?’ akauliza
‘Mama yake aliyemlea…’akasema.
‘Ni lazima hili lifanyike,…na wao walielewe hivyo, vinginevyo tungelijikuta
kwenye matatizo,…kwani kuna shida yoyote, hivi vipimo vitachukuliwa leo, na
kesho kila kitu kitakuwa tayari….hatuna haja na vipimo vya huyo docta
anayesoma huko nje, tutachukua vipimo vyetu kwa kujirizisha tu…..na kama unaogopa usalama, useme tu, ...’akasema huyo docta
bosi
‘Mhh..kazi kweli..’akasema nesi akimtizama yule mtoto ambaye
alishafungua macho, na yule docta akamsogelea, akamwangalia huyo mtoto akasema;
‘Baby…’akasema na kumchunguza yule mtoto machoni, akageuka
kumuangalia mwenzake, akasema;
‘Haina shaka…ndio yeye, ni swala la uhakiki tu…’akasema
WAZO LA LEO: Kila jambo lina uhakiki wake, hatuwezi
kuthibitisha jambo mpaka tuwe na uhakiki wa kitaalamu, kama ni ugonjwa kuna
vipimo, kama ni kosa kuna ushahidi wa kitaalamu wa kuthibisha kosa, na ni
muhimu kukawepo na vidhibiti ili kuhakiki huo uthibitisho au kosa lenyewe.
Kuongea tu hakusaidii, maana kuna watu wanajua kuongea na hata kugeuza ukweli
ukawa vinginevyo. Tuwe makini katika kuhukumu mambo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment