Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, April 27, 2015

NANI KAMA MAMA-66


‘Huyo mwanamke ni nani..?’ swali likaulizwa

‘Ni yule mama mliyekuwa mkiishi naye, aliyekuwa akiitwa mama wa mitaani, akaja kuitwa mama wa mkono wa baraka, ambaye aliletwa hapa kutibiwa kutoka huko kwenu akiwa kaungua…ndiye huyo anayedai kuwa mimi nimemchukua mtoto wake…sasa mtoto huyo ni nani, kama sio huyo mtoto wenu….’ akasema nesi


Shemeji mtu ambaye alikuwa kakaa sasa akasimama, na kuanza kukuna kichwa mfufululizo, akainama akiwaza jambo, halafu akainua kichwa na kumuangalia mkewe, akatembea hatua moja mbele, halafu akasimama…

Nesi alipofika ofisini kwake akawakuta mabosi zake wanamsubiria, wakiwemo wale watu wa usalama wawili. ambao alishawahi kuonana nao, na safari hii wakaongozana na mwanamke mmoja akiwa kavalia sare za kipolisi....

Tuendelee na kisa chetu.

**********

Wanandoa hawa waili walifika nyumbani wakiwa kimia, utafikiri wametoka  mahakama ya usuluhishi wa ndoa na kutokuafikiana, na walipofika nyumbani mtoto walikuwa amelala na aliyewakaribisha alikuwa mfanyakazi wao ndani, akasalamia akaitikiwa na aliona ajbu furaha ya watu hawa walipoondoka sio kama walivyorudi,

Yule mfanyakazi kwa vile aliwazoea hakusita kuuliza,;

‘Mama kuna nini , mbona naona mumebadilika?’ akauliza

‘Hamna shida na kuchoka , unajua safari yenyewe na usafiri ulikuwa ni shida…’akasema

‘Oooh poleni, namuana baba kama anaumwa, …’akasema na wakati huo baba mwenye nyumba alifufuliliza moja kwa moja hadi pale alipolala mtoto, akainama kumtizama alimtizama kwa muda, halafu akageuka kuondoka akakutana na mkewe naye akija kumtizama mtoto.

‘Twende  huku…’akamshika mkewe mkono, na mkewe akamfuata wakatoka ndani ya nyumba hadi kwenye mti, ambao hupenda kukaa wakiwa na mazungumzo yao, hakutaka kuliongelea ndani, asije akasikia mfanyakazi au kumuamusha mtoto.

‘Nimeamini..?’ akaanza kusema

‘Umeamini nini…?’ akauliza

‘Japokuwa hajaamuka, lakini naiona sura kama yake..’akasema

‘Una maana mtoto wetu?’ akauliza mkewe

‘Unasikia usitake kunichefua,..tunachozungumiza hapa ni nini….ni hivi huyu mtoto kweli na wa huyo mama..’akasema

‘Haiwezekani umejuaje,..?’ akauliza

‘Sura yake na huyo mama havidanganyi..’akasema

‘Mhh mume wangu umejuaje maana nijuavyo yula mama muda wote hujifunika, sasa wewe ulimuona wapi…?’ akauliza mkewe,

 ‘Mbona sikumjua mapema huyu mwanamke,… au ndio kwasababu kapata adhabu yake, muda wote kajifunika uso, ili kuficha adhabu ya uovu wake…. Poteleambali, amepata alichokitaka, mimi ninachoweza kusema sasa hivi ni kuwa sitaki hata kumsikia…si-wamesema mtoto huyu ni wa kwake,…eeh, sasa waje wamchukue haraka iwezekanavyo..’akasema

‘Mume wangu vibaya hivyo, huyo ni mtoto wetu, ….’akasema

‘Natumai umenisikia,…kesho mguu kwa mguu tunamrudisha huyu mtoto hospitalini..sitaki blaa hapa, na usitake kujua zaidi,…., vinginevyo, hutaamini kitakachotokea…..labda mimi sio  mwanaume wa hii nyumba..’akasema na alipomaliza hapo akasimama na kuondoka zake

Mama mwenye nyumba akabakia kauduwaa, akainamisha kichwa hadi aliposikia mtoto akimuita

‘Mama….mama…’

**********
‘Nesi tumekuja hapa ofisini rasmi…baada ya kufikiwa na hawa watu, hawa ni watu wa usalama wamekuja kufanya kazi yao baada ya kufanya uchunguzi wa kina wamegundua mengi tu, na moja wapo ni kuhusu huyo mtoto anayetafutwa na mama yake..’akatulia.

Nesi akageuka kuwaangalia akaona kuna mwanamke akiwa akshika pingu, akajua leo kuna mambo, leo ndio siku yake ya mwisho na huenda aakapoteza kazi.

‘Wao baada ya kujirizisha, wamegundua kuwa huyo mama ana haki na anayoongea yana ukweli, nay a kuwa yeye ni mama halali wa huyo mtoto uliye mchukua wewe, na ni kweli kuwa wewe ulimchukua huyo mtoto kutoka hapa hospitalini kama alivyodai huyo mama..’akaendelea kuongea huyo mkuu wa hiyo hospitalini na nesi akabakia kimia.

‘Hatujui kwasababu gani ulimchukua, huenda mlikuwa na nia njema,  …lakini hiyo nia njema ni wewe wa kutuambia, …vinginevyo sisi tutafuata taratibu zote za kisheria za utawala na watu wa usalama watafuta sheria zao za kiusalama….’akasema

‘Tulikupa muda wa kutosha, ukawa unavuta muda natumai sasa una jambo la kutuambia,…’akaendelea kusema, alikuwa akiongea hatua kwa hatua, huku akisubiri kama nesi atasema nini, lakini nesi akawa kimia tu.

Nesi likuwa kazama kwenye mawazo akiwafikiria ndugu zake, ambao wameondoka bila kumpa jibu lenye muafaka, na hakujua afanye nini kwa muda kama huo, asemeje…, na hapo anatakiwa kutao jibu lenye kuwarizisha hao wakubwa zake, akatulia huku akimuomba mungu ampe kauli yenye muafaka.

‘Sasa nesi tuambie ilikuwaje ukamchukua mtoto wa huyo mama, najua utakuwa ana sababu,..maana hilo ni kosa kubwa sana, ina maana gani kisheria kama sio kuiba mtoto au utatuambiaje kama huna maelezo yenye kujitosheleza, unawea kutuambai ilikuwaje, ..?’ akaulizwa

‘Mimi sikumchukua mtoto huyo kwa matakwa yangu,…sikuiba mtoto, naomba mbadilishe hiyo kauli yenu,  naomba mnielewe hilo, ndio maana nilitaka kuwasiliana na waliohusika, kunibebesha hiyo dhamana,…hivi kwanini hamjiulizi hilo kwanini mimi nimchukue mtoto wa mtu ....ili nipate nini….’akasema nesi akionyesha uso wa kukasirika.

‘Ndio maana tulisita kuchukua hatua stahiki, tukawa tunakupa muda, tulijua ni lazima kuna sababu ya msingi, sasa ili kujikosha kwa hilo tunaomba utuelezee kisa na mkasa..au sio? ’akaambiwa na huyo mkuu akiwageukia watu wa usalama.

‘Kisa na mkasa zaidi sina, zaidi ya kuwaambia kuwa mtoto huyo nilikuja kupewa, baada ya mama yake kuondoka, mama yake huyo ninemjua mimi ,alitoroka hospitalini, na kwa vile ilionekana mimi ndiye mwenye makosa nikaambiwa nimchukue huyo mtoto nimlee mimi,….ndivyo ilivyokuwa…’akasema

‘Wewe ndiye mwenye makosa, makosa gani?’ akaulizwa na watu wa usalama.

‘Mimi nilikuwa nesi kwenye hiyo wodi kipindi hicho, nikapewa jukumu la kuwa na huyo mama akiwa chumba cha mahututi, wakati hana fahamu,..ikafikia muda maji na dawa vikawa vimekwisha ikabidi nitoke kwenda kuchukua hizo dawa na maji ya kumtundikia…., niliporudi nikakuta huyo mama katoroka, nikatoa taarifa…msako ulifanyika huyo mama hakupatikana, ndio  nikabebeshwa hiyo dhamana ya mtoto…’akasema

‘Kwahiyo ulibebeshwa hiyo dhamana kama nini, kama adhabu au…ilikuwaje?’ akaulizwa

‘Ni kama adhabu..ndio…’akasema

‘Kwahiyo huyo mtoto ukampeleka wapi?’ akaulizwa

‘Huyo mtoto …’hapo akatulia akiwaza

‘Tunajua wapi alipo huyo mtoto, ndio maana ndugu zako walifika hapa, tunajua yote kuwa huyo mama alikuwa akiishi kwa ndugu zako kipindi kulipotoeka janga hilo la moto,….hayo tumeshayafanyia uchunguzi, na tulitaka kuongea na ndugu zako ili tulimalize kwa amani, lakini nadugu zako wakawa wakaidi..’akasema mkuu

‘Hawakukaidi, ila taratibu za kuwataka muongee nao hazikuwa za kiungwana,….’akasema nesi akimuangalai mkuu wake.

‘Sasa kwanini hukutaka kuwa mkweli muda wote huo, maana kwa maelezo yako inaonyesha kuwa wewe hukuwa na makosa ulibebeshwa dhamana na kilichotokea ni bahati mbaya….’akauliza na watu wa usalama.

‘Baadaye ilikuja habari kuwa huyo mama kafariki, ina maana kutokana na huo uzembe mimi ningelichukuliwa kama msababishi wa kifo cha huyo mama, ndio maana jambo hili likafanywa liwe siri..’akasema

‘Lilifanywa liwe siri ya nani na nani..?’ akaulizwa

‘Watawala na mimi…’akasema

‘Ok…hata hivyo ungetuambia sisi tungelijua la kufanya, …kuna mambo mengi yalitokea hapa,kwa hao waliokuwa watawala wako, kuna ..wizi, ubadhirifu,..na hujuma mbali mbali…na wewe ulikuwepo kipindi hicho, ..tulishindwa kukuingiza moja kwa moja kwenye hilo kosa maana wewe kipindi hicho ulikuwa nesi mdogo tu…’akasema mkuu.

‘Ni kweli mimi sikuwa na mamlaka yoyote zaidi ya kufuata amri….’akasema

‘Kosa lako kubwa na kutokutoa ushirikiano…’akaambiwa

‘Mimi nilitakiwa kufanya walivyotaka wakubwa zangu, hebu chukulieni nafasi yangu..hivi kweli mngelifanya hivyo mnavyotaka nyie…?’ akawa kama anauliza

‘Sasa nesi, sisis tunataka kulimaliza hili kiutaratibu na kisheria ili kesho na kesho kutwa kusitokee kitu kama hiki tena..sisi ni watendaji na tumepewa majukumu, na tunatakiwa tuonyeshe mfano mwema,…sasa,sijui wewe utafanyaje, ..’aaksema mkuu

‘Kufanya nini..?’ akauliza nesi sasa akionyesha wasiwasi.

‘Wewe unasema ulipewa dhamana ya mtoto,..innawezekaan ilikuwa ni adhabu au kushindwa kuwa na maamuzi yenye hekima…wao wakaona wakwepe jukumu kwa kukukabidhi huyo mtoto,…sasa kama ulivyokabidhiwa hiyo dhamana, tunakutaka wewe , uirejeshe hiyo dhamana kwa wenyewe..’akaambiwa

‘Kwa wenyewe akina nani?’ akauliza nesi

‘Ulikabidhiwa hiyo dhamana kibinfsi au kisheria…?’ akaulizwa

‘Mimi sijui..na sikutaka kulifuatilia hilo.., maana nishachanganyikiwa, ..nilikuwa nesi mdogo tu, ….nakumbuaka kuna muda nilishauriwa na mmoja wa madakitari waliokuwepo hapa kuwa niandikishe kisheria, lakini tuliposikia kuwa huyo mama kafariki, tukajua huyo mtoto sasa ni wetu..’akasema

‘Sawa nauliza hivi , wakati unapewa huyo mtoto ulipewa kibinafsi au na utawala wa hospitali?’ akaulziwa

‘Na utawala wa hospitali..’akasema

‘Sasa ni hivi, kwa vile utawala ndio ulikukabidhi hilo jukumu, basi dhamana hiyo irejeshe kwa utawala ..’akaambiwa

‘Utawala huo haupo…’akasema

‘Utawala muda wote upo, kutokuwepo kwa hao watawala wa muda huo, hakusababishi utawala usifanye kazi yake, sisi tupo, ..sisi kwa hivi sasa ndio watawala wa hii hospitalini, tunahitajia huyo mtoto arejeshwe na tutaandikishana kisheria kumpokea huyo mtoto, na kama ….’akakatisha na kuwaangalia watu wa usalama.

‘Na kama mama huyo halali wa mtoto, atakubali muendelee kuwa naye, sasa hapo itakuwa ni jambo jingine..’akasema

‘Lakini mtoto huyo nilishawakabidhi ndugu zangu, na nikawaambia kuwa huyo sasa ni mtoto wao kwa vile mama yake hayupo tena..inaniwia vigumu kuwashawishi vinginevyo…’akasema

‘Ndio maana tukatangulia kukuambia kuwa hilo sasa ni jukumu lako, kama ulivyokabidhiwa na kwenda kuwashawishi kuwa wamkubali huyo mtoto kama mtoto wao, ..basi fanya hivyo hivyo, tumia busara zako kuwashawishi kuwa mama wa huyo mtoto sasa kapatikana..’akaambiwa.

‘Lakini mna uhakika gani kuwa huyo ni mama yake?’ akaulizwa

‘Sisi tulishafanya uchunguzi, hatuna shaka na hilo..na kuna siku tulituma wataalamu kule kijijini, kutoa chanjo kwa watoto, wataalamu hao hao wa chanjo, ndio waliotuwezesha kupata damu ya huyo mtoto, na tulipolinganisha na damu ya huyu mama, tukaona ni sawa…siku hizi kuna vipimo vya DNA, si unajua hilo …’akasema

‘Oh….’nesi akaguna.

‘Sasa baada ya hapo, tutaangalia utaratibu mwingine kisheria, kama itaonekana wewe hujavunja sheria, na huhusiki kweli basi tutaona la kufanya, ila ni lazima taratibu zifuatwe, hawa ni watu wa usalama, utaongozana nao, hadi kituoni, huko mtaandikishana kiutaratibu wao …mengine yatafuata baadaye…’akaambiwa

‘Sasa mnataka kunifunga…?’ akauliza na kabla hawajamjibu akasema

‘Mkinifunga ni nani atakwenda kuwashawishi ndugu zangu…?’ akauliza

‘Hakuna aliyesema unakwenda kufungwa,…hizi ni taratibu tu za kiusalama,wewe utakwenda kuandikisha na ..wao wanajua ni nini kifanyike, kitakachofuata hapo ni taratibu tu, sisi tupo na wewe, ukumbuke kuwa wewe ni mfanyakazi wetu, tutaona ni nini kitakachofuata kiutaratbu, lakini lazima taratbu zifuatwe..’akasema mkuu

‘Mhh..yaani nyie ndio mnanifanyia hivyo..’akalalamika nesi.

‘Kwani wewe una wasiwasi gani..?’ akauliza mtu wa usalama.

‘Najua mnakwenda kunishikilia, …kuniweka rumande, hamuoni kuwa mnanizalilisha kwa kosa mbalo sikulifanya mimi..’akalalamika nesi

‘Wewe usijali,…sisi tunajua ni kitu gani tunachokifanya, muhimu..tuhakikishe kuwa taratbu zote za kisheria zimefuatwa, na waliokuwepo hapa wote waliohusika kwenye makosa mbali mbali ni lazima wanafikishwa mahakamani..’akaambiwa

‘Lakini ndugu zangu hawahusiki..’akajitetea nesi

‘Tunajua hilo..na hilo …la wewe kufikishwa huko, …. huenda likakusaidia, …’akaambiwa

‘Kwa vipi?’ akauliza nesi akionyesha wasiwasi wa dhahiri.

‘Sisi tunachotaka ni mtoto au sio….sasa acha tufanye kazi yetu…na pili kuna mambp mengi bado tunahitajia kufahamu kutoka kwako…kwa ajili ya huyo mama, na yaliyowhi kutokea hapa…’akaambiwa na mkuu wake, na kuwapa ishara watu wa usalama,  na watu wa usalama wakasimama.

‘Lakini mimi sijui zaidi…simjui huyo mama..’akalalamika nsei

‘Twende zetu tusipoteze muda,..utawapigia ndugu zako simu tukishafika huko kituoni…wao wanajua zaidi unavyojua wewe…’akaambiwa na watu wa usalama wakiwa wameshikila pingu.

‘Sitaki kufungwa pingu ninakwenda kwa hiari yangu mwenyewe.’akasema na yule mwanamke wa usalama akatabasamu.

NB: Hii sehemu ina umuhimu wake kwa wenye kujua


WAZO LA LEO: Kunapotokea kosa, sheria hufuatwa, na kusiwe na ubaguzi wa kuangalia sura au kabila,urafiki au umwenzetu, …ni muhimu kusiwe na upendeleo wa aina yoyote ili kweli hiyo sheria ifanye kazi yake ipasavyo, kwani sheria ni msumeno kukata mbele na nyuma.
Ni mimi: emu-three

No comments :