Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeSaturday, April 25, 2015

NANI KAMA MAMA-65


 Dada mtu akiwa kaduwaa, kakaa kwenye kiti , nguvu zimemuishia, aliinua uso na kumuangalia mume wake, ni baada ya kuuondoa mkono uliokuwa umemshika, ni baada ya nesi kuja na kumshika shemeji yake na kumsihi akae kwenye kiti kwanza,

Nesi sasa akaanza kuogopa, akahisi kuwa kafanya makosa kuwaambia tatizo hilo kwa muda huo, lakini alikuwa hana jinsi, akageuka kumuangalia shemeji yake ambaye alikuwa kakaa lakini alionekana kama hayupo hapo.

‘Mume wangu mbona hivi..?’ akauliza mkewe, lakini mume hakutoa jibu, jibu ni kuinuka kwenye kiti na kuanza kuondoka, hakutaka kusikia lolote, mke mtu akabakia akimuangalia mdogo wake…

‘Jamani…mbona imekuwa taabu..’akasema nesi

Tuendelee na kisa chetu….

*************

Mdogo wangu una uhakika huyo mama ndiye huyo mama mwenye mtoto..?’ akauliza dada mtu na mdogo wake akiwa na huzuni akamuangalia dada yake, hakutaka kuficha akamwambia.

‘Kiukweli sina uhakika huo…uhakika ningeupata kama ningemuona huyo mama sura yake,…hata huivyo hata kama ningemuona sura yake..aah sijui kama ningemkumbuka, unajua sijui kwanini imtokea hivyo…yule mama alipoletwa alikuwa kaharibiwa uso, kwahiyo katika matibabu walikuwa wamefungo uso wote, kwahiyo mimi sikupata muda wa kumuangalia usoni…’akasema

‘Na labda ningepata ushahidi kutoka kwa yule dakitari aliyemfanyia upasuaji, maana yeye ndiye alimshugulikia mwanza hadi anamfanyia upasuaji…na aliwahi kuchukua picha zake, na vielelezo vyote muhimu....’akasema

‘Kwani hapa hivyo vielelezo havipo?’ akauliza dada mtu akiongea kwa sauti ya utaratibu.

‘Vimepotea, havipo, yaani hakuna hata kitu kimoja kinachomuhusu huyo mama….’akasema nesi

‘Kwa vipi?’ akaulizwa dada mtu akionyesha uso wa mshangao.

‘Hata sijui,… hayo yalifanyika kipindi nimeenda kusoma, kwahiyo wanaojua ni kwanini kumbukumbu zote za wakati huo zimepotea ni hao hao madakitari , ambao ndio chanzo cha haya yote..’akasema

‘Lakini ulituambia chanzo ni wewe..’akasema dada mtu

‘Ndio kosa lilitokea kwasababu niliondoka nikamuacha mgonjwa,…na mgonjwa akatoroka, ..sikukusudia, …lakini hiyo ya kuficha ukweli, ni wao walifanya sio mimi..’akasema

‘Lakini nahisi walifanya hivyo kwa ajili ya kukulinda wewe, ili usifunge, hebu chukulia kama wangelikuchukulia hatua, ukafungwa, ina maana ungekwua bado upo jela mpaka ukweli ujulikane, na kama huyu ndiye huyo mama, ina maana sasa ndio ungelitoka jela , au sio…?’ akauliza

‘Dada…wakati mwingine najuta kwa kulifanya hili, lakini …ningefanyaje,….kwahiyo dada naombeni mnielewe hivyo,….hicho ni muhimu sana, msiponielewa nyie, basi …’akasema

‘Haya ngoja nikuulize tena mfano huyu mama ndiye huyo mama,..na ulisema huyo mama alifariki, au sio… ina maana basi kalifufuka na wanachozungumza watu ni cha ukweli, ..si ulisema huyu mama alikufa, akazikwa..sasa huyu …huyu mama anatokea wapi,…?’ akauliza dada mtu

‘Hapo ndio mtihani,hata mimi nachanganyikiwa, ila kuna kitu aliongea sina uhakika nacho…huenda alitunga uwongo…ndio maana sikubali, ndio maana nilikataa kabisa kusema ukweli, nikujua kuwa huyu mama ni mtego tu ni tapeli tu, na nimegundua kuwa hawa wakubwa zangu wametumwa kuja kufanya uchunguzi kujua yaliyotokea huko nyuma, wanaweza pia wakamtumia huyu mama kupata mambo yao..’akasema

‘Sasa hata kama wametumwa, wewe linakuhusu nini, wewe una kosa gani, …wakubwa zako ndio wenye makosa au na wewe unahusika kwa namna moja au nyingine…niambie ukweli mdogo wangu….?’ Akauliza

‘Dada mimi kuhusika ni kuhusu huyo mama kuacha..kuwa niliondoka akatoroka, na kuhusika kwingine ni kubeba dhamana ya huyo mtoto, na hilo ni kutokana na shinikizo lao….mengine siyajui..’akasema nesi

‘Ina maana kuna mabaya yalifanyika, ndio maana hawa watu wakatumwa kuja kuchunguza..?’ akaulizwa

‘Nahisi hivyo..sina uhakika..’akasema akijaribu kufikiri, maana mambo mengine hawezi kuyaongea japo huyo ni ndugu yake.

‘Mhh, sasa wewe unatushauri nini….maana mimi kiukweli sijakubaliana na hilo, na sitakubaliana kamwe…, mtoto yule ni wangu..sijui mfanyeje ili nikubaliane na hilo…’akasema.

‘Hata kama huyo ni mama yake mzazi?’ akauliza nesi

‘Nipeni ushahidi..ukipatikana basi tutakaa na huyo mama tukubaliane, kama ni gharama, kama …aah hata sijui ..sio rahisi kihivyo…na hamuoni kuwa tutamfanya mtoto asiwe na raha….?’ Akauliza

‘Unajua dada unaongea hayo ukifikiri kuwa mimi sijafanya juhudi kulikataa hilo…hapa nilipo nasubiriwa kutoa jibu, kutoa maelezo, maelezo ambayo sikutakiwa kuyasema abadani,…hebu kaa upande ujaribu kuona jinsi gani ilivyo ngumu..’akasema

‘Mhh mimi hapo hata sina neno..hata sijui ….sizani kaam nitakubaliana nanyi,..sizani..’akasema

‘Basi mimi nitafungwa…nitapoteza kazi…na sijui hatima yake itakuwaje….’akasema nesi kwa huzuni.

Dada akasimama, akamuangalai mdogo wake, akilini akawa anajiuliza ni nani bora ndugu au huyo mtoto…akatikisha kichwa, akaanza kuondoka.

‘Dada sasa mbona unaondoka tumekubaliana nini..?’akauliza nesi

‘Unaona jinsi shemeji yako alivyoondoka hapa, unajua anakwenda kufanya nini, akigongwa na gari….mimi naondoka, ila msimamo wangu ndio huo huo….’akasema na kuondoka.

Nesi akamfuata nyuma

‘Dada…’

***************

 Getini ilikuwa ni kazi kubwa, baba mwenye nyumba alikuwa akipambana na walinzi, ambao walifuata amri ya mkuu wao kuwa hao wageni wakifika hapo waambiwe waende ofisi ya mkuu wa hiyo hospitali,  kuongea na daktari mkuu, lakini jamaa huyu akakataa, hakutaka kuongea zaidi akawa anataka kutoka nje kwa nguvu.

‘Sikiliza ndugu yetu, hili ni agizo na sisi ni lazima tulifuate, huna haja ya kutumia nguvu, kinachotakiwa ni wewe kwenda kuongea na mkuu, halafu mtaondoka kwani tatizo nini…’akasema huyo mlinzi

‘Nimesema sitaki kuongea na mtu yoyote, kwani nimeiba,kwani nimefanya kosa gani..?’ akauliza huku akiwa katoa macho na yule mlinzi akawa anapiga piga fimbo yake mkononi.

‘Hatujui kwanini amri hiyo metolewa, na sisi kama walinzi ni lazima tuifuate..’akasema

‘Sasa nawaambia hivi sitaki kwenda..niacheni nitoke…’akasema akisukumana nao, na ndipo mke mtu akatokea, na nyuma yake akija nesi, mdogo mtu.

‘Jamani kwani vipi, mbona mnamshika mume wangu kafanya kosa gani..?’ akauliza mke mtu.

‘Wewe nay eye mnahitajika kwenda kwa mkuu wa hii hospitali, ndilo agizo tulilopewa, mengine hatujui..’akasema

‘Kwa kosa gani?’ akauliza mke mtu

‘Hatujui ni agizo tu, kama kuna kosa, au hakuna kosa mtajua huko mbele kwa mbele..’akasema

Nesi akawa amefika, naye akauliza swali hilo hilo,

‘Mbona mumewashikilia wageni wangu kuna tatizo gani..?’ akauliza

‘Ni kutokana na amri ya mkuu, kuwa wageni hawa wanahitajika kuongea na mkuu, wakija hapa tuwaambie waende huko kwanza..’akasema mlinzi

‘Huu ndio utaratibu wa kazi..?’ akauliza

‘Aaah, sister sisi hatujui, kwani sisi tumefanya kosa gani, hebu tuambie, sisi ni walinzi , mkuu kaagiza kuwa hawa watu wakija niwaambie waende ofisini kwake, ana maongezi nao, na wao wanagoma…’akasema
‘Kwani hawa ni wageni wa nani?’ akauliza

‘Wa-wa kwako sister..’akasema

‘Kama ni wageni wangu kwanini huyo mkuu hakuja kuniambia mimi kuwa ana maongezi na hawa wageni wangu..kwanini aje kuwaambia nyie, ni uatartibu gani huu,..’akasema akatoa simu na kumpigia mkuu wake.

‘Nasikia umetoa amri kuwa wageni wangu wasitoke, mpaka waje kuongea na wewe…’akaongea akiwa kashikilia simu, akasikiliza kwa muda, halafu akasema

‘Lakini huo sio ustaraabu, hata kaam nyie ni mkabosi, lakini hamuwezi kuingilia mamlaka yangu, hawa ni wageni wangu mlitakiwa mniambie mimi…hivi wakiondoka hapa mnajua watasema nini huko waendapo..’akasema na akasikiliza halafu akasema;

‘Ili niwaelewe kuwa mumefanya kosa, naomba wageni wangu waondoke, mengine tutaongea mimi na nyie….tafadhali, ..’akasema na akatulia akisikiliza simu, halafu akaitoa masikioni na kumpa mlinzi, na mlinzi akasikiliza halafu akasema

‘Sawa mkuu..’akasema na mara akamrudishia nesi simu yake, halafu akatembea hadi getini akafungua mlango akasema

‘Mnaruhusiwa kuondoka,….’akasema akiwa kainama kama kutoa heshima kwa bwana mkubwa.

Mume mtu akiwa kakasirika akamuangalia yule mlinzi kwa hasira akatulia kwa muda, hadi mkewe alipofika na kumshika mkono, na kumuambia;

‘Mume wangu tuondoke…yamekwisha…’akasema akawa kama anamvuta mume wake lakini mume wake alikuwa kasimama hataki kuondoka, kamkazia macho huyo mlinzi, na huyo mlinzi akaondoka na kwenda seheme yake ya kukaaa.

Hapo Ndipo akaweza kuinua mguu kuondoka na nesi naye akiwa katahayari akageuka kurudi ofisini kwake, hakutaka kabisa kuongea na mabosi wake, hakujua awaambie nini…na alipofika ofisini kwake akawakuta mabosi zake wanamsubiria, wakiwemo wale watu wa usalama wawili..

********

WAZO LA LEO: Mitihani ya maisha ni mingi, unaweza ukakuta unaandamwa na matatizo moja juu ya jingine, na ukajiukuta hata wale uliowategemea kuwa ni mrafiki, wakakugeuka na kuzidi kukukandamiza,  yote hii ni mitihani, na huna budi kupambana nayo, kwani yote ni maisha.


NB:Tuombeane dua na heri, maana emu-three yupo kwenye mitihani migumu ya kimaisha.

Ni mimi: emu-three

No comments :