Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, April 22, 2015

NANI KAMA MAMA-63‘…na kama mlivyomuona bosi wangu, alikuwa anakuja kutaka kuongea na mimi kuhusu hilo tatizo na nisingeliweza kuongea naye kabla sijakutana na nyie..kwahiyo namshukuru mungu mumefika tena kwa wakati muafaka…’akasema akawaangalia ndugu zake na kwa haraka akaangalia pembeni.

‘Mhh ni kuhusu nini maana unaanza kututisha hebu ongea moja kwa moja kuhusu hilo tatizo acha kulolonga maneno, hili tatizo linahusu nini….?’ Wakamuuliza sasa wakiwa wote wamenuangalia nesi, ambaye ni mdogo mtu na shemeji mtu.


Nesi kabla hajawajibi taswira ya dada yake akiwa na mtoto ilimjia kichwani aliona ile furaha, akamuona mtoto naye akicheka kwa furaha akijua yupo kwa wazazi wake, sasa furaha hiyo itageuka kuwa huzuni ….na mtoto sijui atakuja kuishije…lakini atafanyeje, muda umeshafika kusema ukweli, na ukweli ndio utaamua la kufanya.

Akawageukia ndugu zake na kuwaangalia halafu aaksema;

‘Ni kuhusu huyo  mtoto wenu…’aliyatamka maneno haya kwa suati ya chini, kama vile hakutaka mtu mwingine ayasikie,… halafu kwa haraka  akasimama na kugeukia dirishani machozi yakaanza kumtoka.

‘Mtoto wetu ana nini….?’ Wakauliza ndugu zake hao kwa pamoja utafikiri walipanga kuuliza hivyo….

Nesi kwanza akatulia hakuwajibu kwa haraka…

Tuendelee na kisa chetu

************

‘Ni kuhusu mtoto wenu,…yeye kama yeye hana tatizo, tatizo ni kuwa kuna mama kaja hapa anadai kuwa huyo mtoto ni wake…mpaka sasa kiukweli mimi mwenyewe sijamkubali, ila wakuu wangu wa kazi wamemuamini …’akasema

‘Mhh, unataka kusema nini, mbona mimi sielewi,…’akasema dada mtu


‘Kiufupi ni kuwa mama wa mzazi wa huyo mtoto kapatikana, ingawaje hatujakuwa na uhakika wa moja kwa moja,..’ akasema nesi

‘Lakini kama sikosei wakati unamleta huyo mtoto, ulisema kuwa mama yake kamtelekeza, kakimbia, na baadaye ukasema mama wa huyo mtoto keshafariki na kwahiyo mtoto huyo ni wetu, na kama tunahitajia, taratibu za kumrithisha kisheria, basi wewe utazifuatilia…’akasema shemeji mtu.

‘Ndivyo hata mimi nilikuwa najua na sikuwa na shaka na hilo,…’akasema nesi

‘Hapana hili hatutakubaliana nalo, ukukmbuke tumeshamlea huyo mtoto na anatutambua sisi ni wazazi wake, iweje leo …hivi hebu jiulize…hapana…haiwezekani,…’akainua mikono kuonyesha kukataa.

‘Hivi na hao wakubwa zako kweli , kweli…hawana ubinadamu wa kufikiria hilo, au ni kwa vile sio mtoto wao, ..hebu jamani fikirieni, eeh, mtoto wetu keshaishi nasi, tumemlea na tumeshajenga ukribu wa mzazi na mtoto wake, mtoto keshatukaa moyoni, leo hii eti,  twende tumuambie sisi sio wazazi wake..?’ akasema dada yake kwa hamaki.

‘Sikilizeni ndugu zangu, ilivyokuwa ndivyo tulivyofikiria kuwa mama wa mtoto kakimbia na kumtelekeza mwanae na baadaye taarifa zikaja kuwa amefariki, lakini kwa muonekano, kwa jinsi ilivyotokea, haikuwa hivyo…sijapenda mimi, na sikujua hili litakuja kutokea..hata mimi naumia kweli, hamjui kwa kiasi gani nimeteseka..‘ akasema

‘Sasa ni nani alisema kafariki na sasa kafufuka..?’akauliza shemeji mtu

‘Yaani ndugu zanguni mkitaka nielezee yote ilivyokuwa tutakesha….ni mambo ya ajabu ajabu tu..na yamenifanya nisiwe na raha kabisa,..nashindwa hata kutimiza wajibu wangu kikazi,..naogopa kusema kama likiendelea hivyo ninaweza …..kupoteza kazi, kama sio kupoteza uhai….ndio hivyo’akasema, alipomuona dada yake akimuangalia kwa mshituko

‘Sasaaa..wewe unataka tukubali tu, eti kwa vile wewe ndiye ulituletea mtoto na ya kuwa una maamuzi ya kufanya utakavyo,au sio..?’akasema shemeji mtu akimuangalia mkewe halafu mdogo mtu.

‘Shemeji, dada..niwaambie hivi, mimi sijafikia hivyo….kuwa nifanye nipendavyo, eti kwa vile mimi ndiye niliyewaletea mtoto..hapana sio hivyo, mjue mpaka muda huu nilikuwa sijakubaliana na hilo, najua hali ilivyo, najua jinsi gani mtu atajisikia kwa yoyote yule ambaye keshajenga hizo hisia kuwa huyu ni mtoto wangu, hawezi, hatakubaliana na hilo kirahisi, lakini sasa tufenyeje….’akatulia

‘Nesi..naona hata nikuite kwa cheo chako  cha kazi yako labda ndio utanielewa maana huu udugu sasa naona unaleta kipingamizi…., sikiliza nesi, sisi hatukubali, kamwe, kawaambi hao wakubwa zako, sisi hatuna mtoto wa mtu tuna mtoto wetu, wakitaka waende mahakamani, wapi walipotukabidhi mtoto wao, waache wafanye wakalo,..’akasema dada mtu.

‘Kwani huyo mama alikuwa wapi siku zote hizo na leo ndio anajitokeza?’ akauliza shemeji mtu na mke mtu akamuangalia mumewe kwa jicho la ukali, kama anataka kumsema kuwa yeye anakubali kirahisi rahisi.

‘Huyu mama aliyeibuka sasa hivi anadai kuwa ndiye mama mzazi na anadai kuwa alikuwa hajui nini alichokifanya, alikuwa hana kumbukumbu yoyote ya nyuma..na ni kweli kitaalamu hilo limethibitishwa kuwa huyo mama kweli hakuwa na kumbukumbu za nyuma..’akasema nesi kwa utaratibu.

‘Hilo tu ndilo mfikie hatua tya kukubali…hivi nyie, hamjui sasa hivi kuna matapeli wa watoto..mwenyewe uliwahi kutuambia kuwa tuwe makini na hilo, leo hii mumebadilika, ..mbona siwaelewi, sikiliza, hili swala litaamuliwa na mahakama, kama wao wataamua kufanya hivyo na sio kirahisi kihiivyo ..’akasema dada mtu

‘Sasa dada, ukienda kisheria tutajikuta sisi tuna makosa, je tulimchukua huyu mtoto kwa misingi gani, kosa tulilolifanya ni kuwa hatukufuatilia kisheria …hatukuwahi kumilikisha huyo mtoto kisheria…., tulifikia mahali tukadharau tukaona kwa vile mama yake kashafariki basi hakuna shida..’akasema nesi

‘Na wapi tuliandikishana kuwa tumemchukua mtoto kwao..wapi hakuna maandishi, kisheria pia tutawashinda…’akasema

‘Tukienda huko watapima damu, siku hizi kuna vipimo vinaitwa DNA, kama kweli mama huyo ndiye mwenye mtoto itajulikana..’akasema nesi

‘Sasa..kwanini sisi tulikuja hapa kuomba mtoto, watuambie kama sis tulikanyaga hapa tukasema tupeni huyo mtoto , walituletea wenyewe, walipoona hawana mlezi…mimi hapo sijakubali, hata kaam kuna kipimo kama hicho…’akasema dada mtu

‘Huyu mama yupoje, na kwanini madakitari wamuamini kwa haraka hivyo, ametokea wapi huyo mama..?’ akauliza shemeji mtu.

‘Huyo mama ni mama wa maajabu tu mambo zake hadi sasa hakuna namyemuelewa…, yeye kaja hapa kutibiwa, na wakati anatibiwa ndio akaanza kuninyoshea kidole mimi kuwa mimi ndiye nimechukua mtoto wake….’akasema

‘Hivyo tu kakuona na kuanza kudai, au..?’ akaulizwa

‘Huyo mama kalazwa hapa , pamoja na matatizo aliyo nayo pia alikuwa na tatizo la kumbukumbu, hakuwa anajua ni nini kilimtokea huko nyuma. Yeye anadai kuwa alivyoondoka hapa hospitalini, baada ya kujifungua, hakuwa amejielewa, na akatoweka asipokujua,..’akasema

‘Huyo ni tapeli, kwa hayo maelezo tu , mimi siwezi kumkubalia, ana akili sawa huyo mama?’ akauliza dada mtu.

‘Tatizo lake kubwa ndio hilo, hakuwa na kumbukumbu,…. na sasa kumbukuimbu zimemrejea na anakumbuka kabisa kuwa alijifungua hapa kwa upasuaji, na mtoto wake niliyemchukua ni mimi,, …na baya zaidi madakitari waliopo humu hivi sasa ni wageni kabisaa, sio wale waliokuwepo siku hizo wakati mtoto huyo anazaliwa..’akasema

‘Hao madakitari waliokuwepo hawawezi kupatikana, maana hao ni mashahidi wazuri, kwani lolote likitokea kwa huyo mtoto, kwa hivi sasa ni sisi, hasa wewe uliyebeba dhamana utakuja kuulizwa…’akasema shemeji mtu.

‘Ni kweli ndio maana mpaka,… hadi mnafika hapa nilikuwa sijakubaliana na hilo..lakini sasa nitafanya nini, maana dakitari bingwa wa mambo ya akili anataka kujua nini kilimtokea huyo mama…mkuu wa haspitali ndio usiseme, yupo tayari hata kunifukuza kazi kwasababu ya hilo…wanataak kujue maelezo ya huyo mama…’akasema

‘Maelezo ya mama yupi sasa….?’ akauliza shemeji mtu, dada mtu alikuwa kainama, na ilionekana alikuwa akilia, hakutaka kuinua uso.

‘Huyo mama ambaye namtambua mimi, huyo mama aliyejifungua huyo mtoto, na tukaambiwa kuwa keshafariki…sio huyu mama wa sasa, nia ni kutaka kuhakikisha kuwa huyu mama ndiye huyo mama wa kipindi hicho….’akasema

‘Yeye anataka umuelezee ilivyokuwa, na kwanini usimuelezee, huoni hiyo itawasaidia kujua ukweli…?’ akaulizwa

‘Ndugu zanguni, ..tukio hilo lina mitego mingi..kama nitawaambia hawa watu kila kitu kunaweza kukazuka kesi,…japokuwa kesi ya maujai itakuwa haipo tena, maana aliyejulikana kuwa kafariki kutokana na uzembe wangu atakuwa yupo..’akasema nesi

‘Kwahiyo hapo hakuna tatizo, huwezi kuhukumiwa kwa kesi kama hiyo kama marehemu yupo hai au sio waambie ukweli ulivyokuwa mimi hapo sioni tatizo….’akasema shemeji mtu

‘Kuna mambo mengi yamejificha hapo, mambo mengi ambayo sitaki yajulikane, pia niliambiwa na wahusika waliokuwepo kipindi hicho nisije kusema lolote, hata kama atakuwa ni nani, ni ahadi niliyoiweka mbele yao,…sasa nitaivunjaje hiyo ahadi…pia kaam huyu maam sio yule mama, na yule mama alishafariki , hamuoni kuwa mimi nitafungwa kwa kesi ya mauji…’akasema

‘Mhh….unajua hadi hapo sisi unatuchanganya tu, sikiliza mdogo wangu, hili halitawezekana, mtoto ni wetu fully stop..baba nanihii twende zetu…’dada mtu akasimama kutaka kuondoka, lakini shemeji mtu akabakia kakaa akasema;

‘Sikiliza kwanza, kaa,…usichukulie jaziba,  hatuwezi kuondoka kwa hali kama hii, tunatakiwa tujue cha kufanya kabla hatujaondoka, tukiondoka sasa hivi huoni tutabakia katika hali ya mashaka…’akasema shemeji mtu na dada mtu akiwa bado kasimama akamuangalia mdogo wake kwa macho yaliyojaa hasira.

‘Unajua  mimi natakiwa kuelezea nini kilitokea kipindi hicho, kwanza kwasababu nilikuwepo, na pili huyu mama kanikumbuka, na kuninyoshea kidole mimi, kuwa ndiye niliyemchukua mwanae..kutokana na utaalamu  mtu kama huyo hawezi kusema uwongo…. Hili swala limeshafikishwa kwenye jobo la madakitari, kamati ya nidhamu, wote sasa wanadai niseme ukweli wote….’akasema akaona ndugu zake wametulia na hapo akaendelea kuongea;

‘Kama nilivyoaambia hili swala lilichukuliwa kisiri, ili nisije kufungwa kwa uzembe wa kusababisha kifo, lakini pia walienda mbali zaidi wakasema wanachotaka wao ni kuhakikisha kuwa huyo mtoto asije kuambiwa kuwa nyie sio wazazi wake wa kumzaa…’ akasema nesi kwa harakaharaka.

‘Sasa unatushauri nini..maana hadi hapo hatujaelewa ni nini sisi tufanye, unataka tukubali tu kirahisi kihivyo….au?’ akauliza shemeji mtu

‘Na huyo mama ni nani hasa ambaye anakuja tu bila nidhamu na kuanza kudai kuwa wewe ulimchukua mtoto wake, anajua kilichotokea nyuma, je angeachwa, je …mimi jamani sitakubaliana na hilo hata kama nyie mtakubali, mimi hapa, sitaki mtoto wangu achukuliwe, mtaniua.., ‘akasema.

‘Huyo mama ni nani, anatokea wapi….?’ Akauliza shemeji mtu.

‘Huyu mama mnamfahamu sana…’akasema mdogo mtu na kuwafanya hao wanandoa wawili kuangaliana.

‘Tunamfahamu kwa vipi, ..?’ wakauliza

‘Hamtaamini nikiwaambia kuwa huyu mama mliishi naye kwenye nyumba moja, na huyo huyo ndiye kaja hapa kudai kuwa mtoto wake nimemchukua mimi..’akasema

‘Mama gani huyo..?’ akaulizwa

‘Yule mama wa mitaani,..’akasema mdogo mtu, na wote wakamtolea macho kila mmoja akionyesha uso uliojaa maulizo..

NB: Naishia hapa maana afya sio nzuri kidogo,

WAZO LA LEO: Tuweni makini sana tunapochukua majukumu ya kuwalea watoto ambao hatujawazaa sisi wenyewe kutokana na sababu mbali mbali.  Watoto hawa ni rahisi kuumia kisaikolojia , …wao kuwaza kwanini imekuwa hivyo wasiwe na wazazi wa kuwazaa..na kitu kidogo kwao, itakuwa kama wanateswa kwa vile wao sio watoto wa kuzaliwa na hao wazazi wanaoishi nao.

Wewe kama mlezi umeamua kuchukua jukumu hilo la kuwalewa watoto wa kufikia, hakikisha unafanya kila linalowezekana kuondoa hali ya ubaguzi,..kuhakikisha wote wanapata haki sawa, kwani mzazi wa watoto hao kwa muda huo ni wewe, na wewe utabeba dhamana zote za uchungi, ikiwemo madhambi yanayotokana na ulezi, kama kutokuwajibika ipasavyo, au kuwalea watoto hao vibaya wasiwe na nidhamu adbu njema na hata kukosa elimu nk.


Kiujumla jukumu la malezi kwa watoto ni jukumu la kila mtu bila kujali kuwa ni mtoto wako au sio,…tukilitambua hilo, hakutakuwepo tena na watoto waitwao watoto wa mitaani, mayatima nk….
Ni mimi: emu-three

No comments :