Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, April 16, 2015

NANI KAMA MAMA-59



Nililala, na nilipoamuka nilijikuta kwenye dunia nyingine…ni ndoto, …lakini kuna kulala na kuamuka, sasa kwenye hiyo dunia nyingine, nikajikuta sikumbuki cha dunia iliyopita, hapa nakumbuka kuwa dunia ya kwanza vitu vilikuwa vinaonekana vikubwa, watu wakubwa, kila kitu kikubwa,…

Lakini huko kwenye ndoto nilipoingia kwenye dunia hiyo mpya vitu vikawa vimebadilika, na hata akili ya kufikiria ikawa kama imefungwa kukumbuka ya nyuma, sikujua nimetokea wapi au ninakwenda wapi….sikumbuki ilikuwaje, au mimi ni nani, yaani unakumbuka hicho unachokiona mbele yako tu.... yaani sijui nielezeje….ohooo kichwa kinauma..’huyo mama akasema

‘Unahitajika kupumzika mama umeongea vya kutosha, …chukua dawa hii kunywa itakusaidia..’.

Tuendelee na kisa chetu…

****************

Baadaye jopo la madakitari hao wawili walifika kwa huyo mama, na nesi alipitia kwa nyuma ili asionekane na huyo mama, walichukua tahadhari kuwa nesi awepo lakini huyo mama asimuone

Madocta wakafika kwenye kitanda cha huyo mama akiwa keshahudumia kila kitu kinachohitajika akawa kalala lakini kaegemea mto wa kulala, akionyesha kuzama kwenye mawazo.

‘Habari yako mpendwa mama…usione tunakuita mama, lakioni ndivyo tumezoea, tulitakiwa tukuite dada au sio..?’ wakaanza hivyo

‘Vyovyote niiteni mpendavyo, wala sioni tofauti, hata mkitaka niiteni bibi,….’akasema na kuonyesha kutokuwa na furaha

‘Mbona unaonekana huna furaha?’wakamuuliza

‘Simuoni nesi …..nesi ambaye namdai….’akasema na madocta wakainamisha vichwa maana wakati huo nesi alikuwa akija kwa nyuma, na kukaa pembeni kabisa ili sionekane, na kwa umabali ule angeliweza kumsikia huyo mama akiongea,

‘Nesi yupo, ila ana majukumu si unajua yeye ni nesi mkuu, kwahiyo ana takiwa kuhakikisha manesi wote wanawajibika, atakuja tu kukuona..’akaambiwa

‘Mbona mwanzoni alikuwa hakosi kuja , na alikuwa anafika hapa kwanza kabla hajaanza shughuli nyingine, au alikuwa anataka kunipima kuwa nakumbuka, au ananiogopa,….?’ Akauliza

‘Usijali kwani wataka kumuona sasa hivi?’ akaulizwa

‘Ndio mimi nataka kusikia kauli yake, je mtoto wangu yupo wapi…akinipatia jibu kuwa yupo mahali fulani, basi kesi imekwisha, la sivyo, mimi nitachukua hatua ninazozijua mwenyewe..’akasema

‘Utamshitakia…au utamfanyaje..?’ akauliza

‘Mnataka kumtetea, jaribuni, ….haki ya mtu haipotei bure, hasa haki ya kudhulumiwa damu yako…nimeshamuomba mungu, najua kila aliyenitenda na atakayenitenda, atalipizwa..ila …ila, wale wenye nia njema kwangu…nina imani hao walio na mtoto wangu wana nia njema kwangu ila kama watashindwa kunipatia mtoto wangu,….’akatulia


‘Sasa mama sisi tuna nia njema kwako, ndio maana tunataka kukusaidia,….na ili tuweze kukusaidia tunahitajia ushahidi, na moja ya ushahidi ni kutuonyesha kwanza kuwa umekumbuka kila kitu….’akatulia maana huyo mama alikuwa kama anataka kukaa vyema

‘Wala usihangaike kama unataak kitanda kiinuke juu zaidi wewe sema..tutakusaidia, akasema docta na mwenzake akafika kwenye kitanda na kukipandisha juu, akawa kama kaka..

‘Kwahiyo mnataka nini, niwaambie nini ili mniamini,…?’ akauliza

‘Jana ulisema kuwa kutokana na ndoto yako ndio ukajua ukweli, na ulituelezea ndoto yako hadi tukafikia sehemu ukasema umefika dunia nyingine, dunia ambayo uliweza kuona vitu kwa jinsi vilivyo sio vikubwa tena…lakini ukawa umesahau wapi ulipotoka, na hukujua wapi unakwenda, ehe..sasa tuendelee na ndoto yako ikawaje…?’ akaambiwa

Yule mama akatulia akawa kama anawaza jambo, halafu akasema;

‘Nikawa sasa natembea tu...sijui nilipotoka, ....sikumbuki kabisa nyuma kulitokea nini, nikatembea weee, na ujue kutembea kwenyewe ni kama roboti lakini napaa, ina maana ukiinua mguu hapa unafika mwisho wa chumba, ajabu kabisa, maana ni ndoto lakini kiukweli haikuwa hivyo...’akasema

‘Una maana gani ukisema kiukweli…?’ akaulizwa

‘Hiyo doto imenifunulia ukweli, nakumbuka kabisa kuwa nilitembea sana, lakini kutembea huko kulikuwa ni kwa kawaida, ila ndoto ilinionyesha kuwa nilitoka hapa nikaenda hapa, kwa mtindo huo…’akasema

‘Mhhh,…ikawaje…?’ akaulizwa

‘Nikafika sehemu nikakutana na watoto...waliponiona nilivyovaa wakanikaribia, wakawa wananishangaa, sijui ni kwa jinsi nilivyovaa, au kwa jinsi ninavyotembea, alianza mmoja, wakawa wawili na baadaye wakawa wengi tu...

Nesi ambaye alikuwa kasimama kwa mbali aliposikia hivyo akashika mdomo, kama vile anaona ajabu au kushangaa, au kutoakuamini hicho anachokisikia..

‘Niliona ajabu, yaani inakuwa kama unaona kitu ambacho hujawahi kukiona, watoto wazuri, moyoni nikatamani na mimi niwe na watoto kama hao,...sikujua kwanini wananishangaa...sijui , ..hata hivyo akilini nilihisi nipo hatarini...’akasema

‘Kwanini?’ akaulizwa

‘Nasema sijui, akili ndio ilikuwa inanituma hivyo, si akili haikumbuki kabisaaa…! Ila kuna onyo, kuwa sipo salama, kwahiyo nikawa na tahadhari, nikawa naangalia huku na kule, ..nikawa natembea na hao watoto wanifuatilia nyuma. Nilihisi kupitia sehemu mbalimbali.

Kuna kitu kingine kilikuwa kinanionyesha au kuniambia kuwa natafuta kitu, na sikujua ni kitu gani, lakini baadaye, ..kutokana na wale watoto kunijia , wengine wakaanza kuniuliza wewe ni nani, mimi sijua niwajibu nini, jibu lilikuja lenyewe tu , nikasema;

‘Mimi ni mama kutoka mbinguni…’nikasema

‘Malaika…au?’ wakaniuliza

‘Hapana mimi sio malaika ila ni mama tu kutoka mbinguni…’nikasema

‘Umakuja kufuata nini..?’ wakanizidi kunihoji, na jibu likaja lenyewe tu, bila hata kufikiria, nikasema;

‘Namtafuta mtoto wangu….’nikasema na jibu hilo lilipotoka tu mdomoni, ikawa kama kitu kimegusa ubongo na kukiwekea msisitizo kuwa kweli namtafuta mtoto, kweli nilikuwa na mtoto, sasa mtoto huyo yupo wapi…’akatulia

Kwahiyo kutokea hapo, kauli yangu kubwa ikawa kuulizia wapi mtoto wangu yupo, na kwa vile nilishawaammbia hao watoto, na wao wakalichukulia hivyo ila kimzaha zaidi, …wale wa mwanzo nilioongea nao, nahisi kama walinielewa, ili hao niliokutana nao baadaye ndio wakafany ani mzaha, wakafanya ni wimbo, na mimi bila kujau, sijui kwanini nikawa nafanya wanavyotaka wao..ili ujumbe ufike..’

‘Ulifanya nini ili ujumbe ufike?’ aakulizwa

‘Kila aliyeniuliza nilikuwa nasema `nataka mtoto wangu…mwanzoni niliongea kwakigugumizi maana sikuwa na uhakika na ninachokiongea, na watoto wakachukulai kile kigugumzi kama mzaha na ukabadilika na kuwa wimbo…’akasema

‘Wimbo gani?’ akaulizwa

‘Na-na-nataka mtoto wangu…’akasema , na nesi aliyekuwa kasimama, aligeuka pembeni, na hakuweza kujizuia machozi yakaanza kumtanda usoni..lakini kwa hali nyingine bado alikuwa hajaamini,…kama kweli ndiye huyo mtu, bado alihitajia ushahidi wa kutosha, na kwa namna nyingine alikuwa akijiuliza jinsi gani ya kumuondoa mtoto yule kwa dada yake, mtoto ambaye keshamtambua dada yake kama mama yake..hilo lilimtia uchungu akajikuta anabubujikwa na machozi.

‘Hata hivyo sijaamini kama ni huyu mama, nahitaji ushahidi zaidi…’akajikuta anaongea, japo kwa sauti ndogo.

‘Mhh ikageuka kuwa wimbo su sio, …?’ akaulizwa na docta  

‘Ndio kila ninaposema hivyo kwa watu naona wananishangaa, na watoto wakawa wananisaiia kuulizia, japo kwa mzaha, maana wao walishaoona kuwa ni wimbo, kwahiyo nikisema hivyo na wanaitikia hivyo, `nataka mtoto wangu....nataka mtoto wangu…’

Lakini watoto ni watoto, wao wakageuza kuwa ni mzaha na ikawa ni karaha mpaka nikafikia kukasirika na kuna muda nilitafuta fimbo kuwachapa ili wawe mbali na mimi, lakini wakiwa mbali na mimi najiona mpweke, wao wakawa ni sehemu ya family yangu, wao wakawa wananitafuta chakula….wakienda majumbani mwao wakirudi wananiletea chochote,..

Mwanzoni nikaona ni msaada kwangu, nikaona labda hii ndio salama yangu, hawa watoto  watakuwa wakifikisha ujumbe wangu kwa watu, wakinisaidia kupata chakula, na hakuna atakayenihisi vibaya..basi ikawa kila nikihisi uwoga, au kutaka kufikisha ujumbe kuwa mimi namtafuta mtoto wangu nikawa naimba hivyo, namtaka mtoto wangu,....’akatulia

‘Kiukweli akili ya nyuma ilikuwa haipo akili iliyobakia ni kuwa natafuta mtoto, kuwa, nilikuwa na mtoto, na mtoto huyo amapotea...kwahiyo namtafuta kila kona kila mahali, nilipita kila uchichoro, kila nyumba, … ndio maana nikawa  natembea huku na kule, na kama mtoto kapotea wewe kama mzazi hasa mama huwezi kutulia, huwezi kuwa na amani, ….mimi ni mama, na sitakuwa na amani mpaka nimpate mtoto wangu...’akatulia .

‘Lakini sasa mama, hebu turudi nyuma kidogo, wewe kutokana na ndoto yako uliota kuwa ulikuwa umezungukwa na wala nyama…ukaona mtoto wako akichukuliwa na hao wala nyama, huoni kuwa mtoto wako atakuwa sio hai….’akaambiwa

‘Kama angekuwa sio hai , hata mimi nisingelikuwa hai…mimi kama mama najua yupo hai, nahisi, na mungu kanifunulia kuwa mtoto wangu yupo hai…’akasema

‘Ehee, hebu endelea ikawaje…?’ akaambiwa

‘Kwahiyo nikawa nahangaika huku na kule..na moyoni, nilijua mtoto wangu atakuwa mahali, ...na mtoto wangu atakuwa anafanana na mimi,...’akasema

‘Huko kufanana na wewe umakujauje na wakati umesema ya nyuma huyakumbuki?’ akaulizwa

‘Katika kuhangaika na kuuliza, na watu nao wakawa wananiuliza mtoto wangu yupoje anafananaje, nikawa nawajibu hivyo, kuwa mtoto wangu anafanana na mimi…’akasema

‘Kwa vipi kwa sura au kwa vipi maana wewe si umejifuniak uso, hao watu watajuaje kuwa mtoto huyo anafanana na wewe…’akaulizwa

‘Hata watu waliniambia hivyo, nikawajibu kuwa kutokana na sheria za mbinguni mimi sitakiwi kujifunau uso..nilikuwa naamini hivyo, kwasababu kubwa nilihis nipo hatarini, nikionekana nitadhurika niliamini hivyo  na akili yangu ikawa imeshika hivyo, na nilihidi kabisa nikiambiwa akilini kuwa salama yangu ni kuhakikisha kuwa sionekani uso wangu…

‘Kwahiyo hujifuniki kwasababu ya imani..?’ akaulizwa

‘Tunazungumzi kuhusu ndoto, tunazungumzia tukio hilo,..naomba mnielewe, mistake niwaambie mnavyotaka nyie, ..’akasema huyo mama

‘Tumekuelewa mama endelea ikawaje…?’ akaulizwa

‘Kuna hatua nikahisi kuwa kuna mtu kamchukua mtoto wangu, kamficha...lakini sijui ni nani...basi ikawa maisha yangu ndio hayo,  nikaja kuishi kwa watu…ni baada ya kuhangaika sana, kuna mtu akaamua kunichukua nikawa naishi naye..

Sasa hapo kwenye hiyo nyumba..ajabu kabisa sijui kwanini, kuna mtoto, sijui kwanini, sina uhakika hadi leo labda nirudi tena,maana akili sasa naiona ipo barabara, japokuwa sijawa na kumbukumbu za nyuma kabisa, huko nilipotokea, sikumbuki jinsi nilivyopata mimba, sikumbuki kama nilikuwa na mume..huko sijakumbuka…’akatulia

‘Hiyo itakuja tu, unajua hata haya mama unayotuelezea bado hayajakaa sawa ndio maana tunajaribu kukuhoji ili kukuongezea ufahamu wa kukumbuka, maana huenda hata huyo mtoto hayupo, huenda ni kumbukumbu za kutamani kuwa na mtoto…’akasema mkuu wa hospitali na mwenzake akasema

‘Mama hebu tuendee na maelezo yako kwanza, tusikupotezee muelekeo…’akasema na mama alikaa kimia kama anatafakari jambo, halafu akasema;

‘Sipendi kabisa hiyo kauli yako….lakini ipo siku utakuja kujua kuwa haya ninayoyaongea ni ya kweli, siitaki kukuona mbaya maana umenisaidia sana, ila kauli yako imeniuma sana…mimi nina uhaika nina mtoto..’akasema

‘Tumekuelewa mama endelea….’akaambiwa

‘Basi..kwenye hiyo nyumba, na sio nyumba moja nikawa napewa watoto, kwa vile niliamini kuwa natokea mbinguni, nikawa nikiwaombea wale watoto wanapona, wanakuwa na furaha, hata wakiwa wanalia wanakuwa huwalii tena…’akasema

‘Oh, ni kweli au ni kwenye ndoto..?’ akaulizwa

‘Kwenye ndoto…sijui kama kweli nina kipaji hicho sikumbuki, maana ya nyuma kabisa siyajui,..ila kwenye ndoto,…na hata nikijaribu kukumbuka uhalisia kama nilifiak sehemu, ndio nakumbuka nilifiak sehemu, nikawa naishi,…lakini sikumbuki kuwa hivyo, kuwa nina kipaji hicho ila kwenye njozi nimeota hivyo…’akasema

‘Unaonaeeh, bado hujakumbuka kila kitu..’akasema mkuu wa hospitali

‘Lakini la mtoto ni kweli..hilo huwezi kubisha..’akasema

‘Ndio tunatafuta ushahidi..’akasema huyo docta

‘Ohooo…ushahidi, unataka nikuonyeshe ushahidi..wewe hukuona mshono..wewe..wwe sitake niaksirike, utapaat shida..’akasema

‘Ina maana ukimkasirikai mtu anapaat shida?’ akaulizwa

‘Nahisi hivyo, maana katika kuota, nakumbuka kama kuna sauti iliniambia kuwa duwa yako , maombi yake yamekubaliwa na omba chochote kuhusu wabaya wako , na utakachoomba kitatimia…kitu kama hicho ila sikumbuki vyema,..’akasema

‘Mhh, hapo unatuweka njia panda,..kwani wewe unahisije, umetoka mbinguni kweli au ni mtu kweli, au ulikufa ukafufuka…?’ akaulizwa

‘Kwanini unaniuliza hivyo…?’ akaulizwa

‘Yaani kutokana na ndoto yako, kutokana na mtizamo wako, wewe unahisije…?’ akaulizwa

‘Sijui niwajibu nini..kwani nyie mnanionaje, mimi sio binadamu, mimi sio mtu…?’ akauliza

‘Aaah, sisi tunajaribu kupekenyua kumbukumbu zako, sisi tunajua wewe ni nani, lakini tunapima akili yako kama inakumbuka vyema kama ina uafahmu au bado ipo kwenye njozi…?’ akaulizwa.

‘Mhh, hata sielewi, maana naona kama umesoma kichwa change, kama vile umeona ninachokiwaza, na ukaniuliza hivyo hivyo..bado sijajielewa, ..bado akili ina mawingu, nahisi kama sipo duniani, nahisi kama tofauti…sijielewi kwakweli, na nyie ni madakitari nahitajia msaada wenu..’akasema

‘Ndio maana tunakuhoji , ndio maana tunahitajia kila kitu ulichokiota…unachokumbuka… , maana kutokana na ndoto hiyo unakukumbuka yote yaliyotokea huko nyuma,au sio…, na sisi kwa kuhakikisha na kukusaidia tutajaribu kuyafuatilia hayo matukio kama yalikuwa ni kweli..huko ulipokwenda ukakutana na watoto, tutakwenda huko…., na ikibidi tutaongozana, mpaka tufike huko ulipozaliwa….’wakasema

‘Nilipozaliwa…hahaha..sijui, nahisi kama zikuzaliwa,..hebu niambie kama nilizaliwa wazazi wangu wapo wapi…ndugu zangu, na kama nilikuwa na mume , huyo mume yupo wapi…mimi ninachojua ni kuwa nilikuwa na mtoto, na mimi ni mama yake…ndio maana namtafuta mtoto wangu, huyo ndiye  ndugu yangu, …’akasema

‘Oh nani kama mama…’ilikuwa sauti kutoka kitanda cha pili cha mgonjwa, na wote wakageuka kumuangalia na huyu mama akasema;

‘Unasikia,…mimi ni mama nina uchungu na mwanangu, ningelikufa, nahisi mateso niliyopata sijui ni mateso gani, nahsi hivyo tu, ningelikata tamaa nikasema bora nife, nahisi kuna muda niliulizwa, nahisi hivyo tu kuwa upo tayari kufa usahau haya mateso au upo tayari kuishi, nikasema kwa ajili ya huyu mtoto nipo tayari kuteseka, ..’akasema

‘Hapo ilikuwa wapi…mbinguni au ulipokufa au ndotoni..?’ akaulizwa na mkuu wa hospitali

‘Sikumbuki, na wala sikumbuki kufa..ila mbinguni, hilo nililiota kuwa natokea mbinguni, maana sijui nilitokea wapi, sikumbuki kabisa..ila la kufa hapana sijafa, ila nilimuona mtu amekufa nikachukua nguo zake..’akasema

‘Sawa mama, unaweza kuendelea ilikuwaje baadaye…?’ akaulizwa, nesi alikuwa kainama, alikuwa hataki hata kuinua uso, lakini wenzake walikuwa hawana habarai naye, walikuwa na mama..wakitaka kujua zaidi…

Siku moja, nikachukuliwa na watu waliokuwa na nyumba yao wakataka niishi nao, walikuwa na mtoto..na nakumbuka niliwahi kufika hapo mara kwa mara, nikampenda huyo mtoto, sijui kwanini..’akasema

‘Unahisi huyo mtoto anafanana na mtoto wako…?’ akaulizwa

‘Wengi…watoto wengi niliowaona  nilihisi wanafanana na mtoto wangu ila huyo ….mmh, kama kusingelikuwa na mama yake,..ningelisema huyo ni mtoto wangu…’akasema

‘Kitu ambacho nilishindwa kuhakiki, kule ..huko nyuma, kuna muda ilinijia hali nikakumbuka kidogo, kuwa mtoto wangu ana umbo kubwa, huyo mtoto kwa hao watu anaumbo dogo...’akasema

‘Haya endelea….’

‘Basi siku zikaenda, nikaona watu sasa wanajia na watoto, wanadai watoto wao wanaumwa, wanalia ovyo usiku, …nikawa nawaombea wanapona….’akasema

‘Wanapona kwa vile wewe unatokea mbinguni au una kipaji cha kuponya watu..?’ akaulizwa

‘Unakumbuka nilikuambieni, kuwa kuna hali, sikumbuki kwenye njozi, huenda niliota siku nyingine kuwa nilifika mahali nikasikia sauti, ikasema kilio change kimepokelewa na maombi yangu, yamekubaliwa, na kila nikiombacho kitatimizwa, kwa muda maalumu na apendavyo muumba….’akatulia

‘Kwahiyo kumbe ni kutokana na kilio chako, huenda hayo ndio hayo ambayo hujaweza kuyakumbuka…, na sio kwamba umetokea mbinguni,…?’ akaulizwa

‘Hapo sijui…sielewi , sikumbuki…ila kutokana na ndoto, ilikuwa nikiwaombea, wanapona…ikawa watu wanakuja na watoto wao nawafanyia hivyo, na wanapona,…na hapo nikapata nafasi ya kuwaona watoto wengi, na kujaribu kuwakagua kama ni miongoni mwa watoto wangu…, lakini hawakuwa wakifanana na mtoto wangu, nikawa nawashukuru na kuwabariki.....’akatulia

‘Hayo yote uliyaona kwenye ndoto au kumbukumbu zako baada ya hiyo ndoto zimekuelekeza kuwa kweli ulifanya hivyo…?’ akaulizwa

‘Mimi nina imani kuwa nilifanya hivyo, japokuwa mengine siyakumbuki sina uhakika nayo, lakini ndoto hiyo imenionyesha njia.....’akasema.

‘Kwa hapo huna uhakika..unakumbuka tu kutokana na ndoto kuwa uliwaombea watoto wakapona, unakumbuka tu kuwa ulipata ufadhili kwa mtu…je nikuulize hapo ulipopatiwa ufadhili unapakumbuka ambapo uliona mtoto anafanana, unahisi anafanana na mtoto wako?’ akaulizwa

Nikienda, nitapakumbuka,…na sina uhakika na huyo mtoto….ila nahisi, anafanana ..lakini ukiangalia kimaumbile, …hili la kimaumbile nalisema sasa hivi kwa vile nimekumbuka kuwa sehemy ya kwanza ya dunia ilikuwa maumbo makubwa na sehemu ya pili maumbo ya kawaida…kwahiyo huyo mtoto nilimuona kwenye dunia ya kwanza, mtoto alikuwa an umbo kubwa..kitu ambacho kihalisia sio hivyo…..’akasema

‘Hata nesi ulimuona kwa umbo kubwa lakini ukamkumbuka , kwahiyo huyo mtoto ukimuona unaweza kumkumbuka kama ndio yeye..?’akaulizwa

‘Mhh..’akaguna na kuwa kama anawaza na docta akauliza swali jingine..

‘Ok,… hayo unayotuelezea hadi kufikia hapo kukutana na watoto ukafadhiliwa, umeyaona kwenye ndoto, kwa kiasi kikubwa hujawa na uhakika nayo au unasemaje….?’ Akaulizwa

‘Kama nimemuona huyu nesi na kweli alikuwepo kwenye njozi,…mimi nin uhakika yote ni ya ukweli na nina uhakika nayo…ni swala la kufuatilia kama mnahitajia, ila nataka niongee na nesi aniambie ukweli, ….’akasema

‘Lakini sis bado tuna wasi wasi, tunashauri usichukulia haraka, maana mengine yanaweza kuwa sio ya ukweli….’akasema docta yule mwingine

‘Ni ya kweli docta,…akili yangu inaniambia ndivyo ilivyotokea,…’akasema

‘Kama kweli umeshaanza kukumbuka, ni nani mume wako aliyekupa hiyo mimba unaweza kumkumbuka hiyo...? ‘akauliza na mama akakaa kimia

‘Si unaona hapo, kisheria unaweza kukataliwa …maana mimba haiwezi kuja hivi hivi, mtoto hawezi kuja hivi hivi, ulikuwa na mume? Hujui, hukumbuki, …au ulimpataje huyo mtoto hukumbuki au unasemaje…?’ akaulizwa na mkuu wa hospitali na huyo mama akakaa kimia kama anajaribu kukumbuka halafu akasema;

‘Hayo ya huko nyuma kiukweli sikumbuki kabisa, sijui nilipataje hiyo mimba, sijui kama nilikuwa na mume, sijui tulikuwa tunaishije,… ila eeeh, kuna ndoto ilinijia nyuma, nikaona kama napigwa,  nateswa…lakini sikumbuki vyema, sina uhakika kwa kweli..’akasema

‘Usijali hayo yatakuja taratibu..hebu nikuulize hapo ulipofadhiliwa, ukamuona huyo mtoto, na unasema anafanana na mtoto wako, ni kitu gani unaweza kukumbuka ambacho huenda kinaweza kusaidia…?’ akaulizwa

‘Kitu ambacho nakumbuka, kinafanana na huyo mtoto, hata nikimuona..ninaweza kukumbuka, eeh …japokuwa…unajua yule alikuwa bado mchanga,…ila nilimuona kwa muda mfupi, lakini kwa vile alikuwa mkubwa, …unaona kila kitu kwa uwazi…’akatulia

‘Hahaha hiyo ni miujiza ya mungu alitaka kila kitu kiwe kikubwa ili niweze kuona vyema..unaona hapo..na hicho kinanionyesha kuwa ni mtoto wangu,..nimekumbuka … macho yake yanafanana na macho yangu....’akasema.

‘Macho…!!’ kauli hii ilitamkwa na watu watatu wakishangaa, docta mkuu, docta bingwa, na sauti nyingine ilitoka kwa mbali, na sauti hiyo iliyotka mbali, iliongezea neno la kushangaa…

‘Khaaa…’ilikuwa ni sauti ya nesi aliyeshindwa kuvumilia, na mama akaisikia hiyo sauti, na akawa kama kapigwa ganzi, akatulia na akawa taratibu anageuza kichwa kuangalia huko sauti ilipotokea…



WAZO LA LEO: Sio rahisi kudanganya na kuwahadaa wenzako siku zote, hadaa na uwongo unafikia mwisho, na ukweli hata kama ni chembe ndogo tu, inag’ara kuliko uwongo uliojaa dunia. Dunia sasa imegubikwa na hadaa, uzushi na propaganda, kitu cha uwongo kitapambwa na kuonekana ni kweli, lakini athari zake huja baadaye, na kuleta maangamizi. Migongano ya kijamii, uhasama, vurugu, migomo, hadi vita chanzo chake ni tabia hii ya udanganyifu, iwe kwenye utawala, biashara…na maisha ya kila siku hadaa ni mbaya na inaleta athari kwa jamii.
Ni mimi: emu-three

No comments :