Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, April 10, 2015

NANI KAMA MAMA-56‘Nesi unaitwa wodini,...’ akaambiwa,

‘Sawa…wodi gani?’ akauliza

‘Ya yule mama, mgonjwa wako…’akaambiwa nesi alivyosikia hivyo akajua kuna jambo, kuna kitu kimetokea huko kwa huyo mama...na simu aliyokuwa akiongea na dada yake ikawa imeshakatika, kwahiyo kwa haraka akakimbilia huko wodini huku akiwa na mawazo mengi kichwani..huku akiombea apate nafasi ya kuongea na dakitari kijana, kwani dakitari kijana ndiye tegemeo lake la mwisho....

'Hata iweje, usije kukubali kumtoa huyo mtoto, huyo ni dhamani kwako, kama mama yake ameshafariki basi ujue wewe ndiye mama yake...mmh, ..'akakumbuka kauli ya dakitari kijana.


Haya tuendelee na kisa chetu...

************

‘Namtaka mtoto wangu, nimesema, sitatulia hapa mpaka ijulikane wapi mtoto wangu alipopelekwa…na mumlete huyo nesi wenu, asije akakimbia…najua yupo hapa, ananikwepa siku hizi..yupo wapi.....’ ni maneno aliyoyasikia nesi wakati keshafika mlangoni mwa ile wodi.

Nesi ambaye hakujua kaitiwa nini, aliposikia hivyo tu akasimama….akageuka nyuma kutaka kurudi au ikibidi kukimbia na kujificha hadi awasiliane na dakitari kijana huenda dakitari kijana atakuwa ameshapata hizo kumbukumbu za nyuma za yule mama ambay ndiye mwenye haki na mtoto.

'Huyu mama ni mwizi, mwanga tu anataka kumchukua mtoto ambaye sio wake mimi sikubali...'akawa anajisemea akilini.

Aliposikia hizo kelele, kwanza akatulia na kutafakari anachotaka kukifanya,…arudi, arudi wapi, akimbuie, akimbilie wapi,..na anakimbia nini, wakati yeye hana hatia...hapana, huyu mama ni muongo, najua ni muongo, ….akaendelea kuwaza akiwa kasimama kwenye mlango wa hiyo wodi.

Huko ndani kelele za `nesi yupo wapi, nesi yupo wapi….’ Zikawa zinaongezeka na akiwa hajaamua la kufanya mara gari aina ya landrover, likaonekana nje ya hiyo hospitali na kuingie kwenye geti halafu moja kwa moja  likaja kusimama karibu na eneo wanaposimamisha wafanyakazi wa hiyo hospitali...

Nesi akashangaa ni nani anaweza kuingiza gari hadi eneo hilo la wafanyakazi..., na gari lile ni geni kwake…akiwa anaangaza-angaza macho, nyuma akasikia akiitwa na bosi wake , kumbe walishamuona, akageuka kuingia wodini.

Nesi akiwa kashikilia vile vipimo mkononi alitembea haraka haraka huku akiweka macho yake kuangalia kule walipo wagonjwa, alijua tu watamuona, lakini hakutaka kukutana na huyo mama, kwani anaonekana kuwa na hasira, na huenda akamdhuru.

Yeye moja kwa moja akaingia chumba anachokaa dakitari huyo akiwa kwenye wodi hiyo, akamkuta dakitari huyo kakaa huku kashika mikono kama anaomba....kiujumla alionekana ana mawazo...

Nesi akajifanya hajui kitu, akaingia mle ndani na moja kwa moja, kumbe huku nyuma, yule mama kamuona, akawa anasukumana na wale madkitari waliofikahapo kusaidia, mama huyo alikuwa  mbogo, na kwa muda ule dakitari alisema hatakiw kupewa tena hizo dawa aanzopewa ambazo akizinywa analewa na kupatwa an usingizi.

‘Eeehe, ndio huyo hapo, amerudi, hajakimbia…mwambieni anipe mtoto wangu..’wakasikia huyo mama akipiga ukelele, na nesi akajifanya kushangaa, akasema;

‘Vipi huyo mama vimecharuka tena nini…’akasema na bosi wake akmuangalia kwa macho ya udadisi.

‘Vimecharuka nini…?’ akauliza akiwa kakunja uso. Nesi akaona hapo sasa kuna jambo, akanyosha mkono kumkabidi dakitari vipimo, dakitari akavipokea na hakuviangalia kwa makini,  akasema;

‘Yule dakitari pale unamkumbuka…?’ akaulizwa  nesi, na nesi akageuka kumuangalia huyo dakitari,akamkmbuka kuwa ndiye dakitari aliyekuja mara ya kwanza kumuona huyo mama, ni dakitari bingwa wa magonjwa kama hayo ya akili.

'Ndio kwanini nisimfahamu wakati alikuwa mara kwa mara anakuja hapa...ila kipindi sasa hajafika hapa kwetu....'akasema

‘Imebidi arudi tena kuhangaika na huyo mama, maana mimi nimejitahidi nikaona hapana kwa vile yupo dakitari kabobea kwa kazi hiyo tu, kwanini asije akaendeela na huyu mama ili mimi niweze kufanya kazi zangu nyingine..’akasema

‘Lakini wewe pia ni bingwa wa mambo hayo…na huyo mama ulisema anakaribia kupona au...?’akasema nesi

‘Lakini ukumbuke pia, mimi ni mkuu wa hii hospitali,. Nina majukumu mengine ya utendaji…siwezi kuyacha, au sio, lakini hili la huyu mama limefikia ukingoni, ndio maana nimewaita watu wa usalama pia na wa waje, tulimalize hili tatizo....’akasema na wakati anaongea hayo kwa nje walionekana wanaume wawili wakija kuelekea kwenye huo mlango, na haikupita muda mara mlango ukagongwa.

'Watu wa usalama....wa nini..?' akauliza nesi

Nesi akashikwa na bumbuwazi, akamtizama bosi wake huku akiwa kakunja uso, ...kwani aliona bosi wake kafiki ahatua ya kumshitakia...., halafu akageuka nyuma kuona ni nani wameingia,….wakaingia maofisa upelelezi wawili....na mmojawapo anamfahamu kwani mara wka mara huwa anafika hapo hospitalini kuongea na huyo mkuu wa hospitali

‘Karibu mkuu, karibuni maafande... kutana na nesi mkuu….’akasema mkuu wa hiyo hospitali

‘Nashukuru, …naona kuna vurugu kwa mgonjwa wenu vipi mama kazidiwa nini?’ akauliza mmojawapo

‘Ni kawaida tu, siunajua hapa ni hospitalini....na naona huyo mama leo  kaamua iwe hivyo..’akasema.

‘Sasa…??' akauliza mwingine na mwingine akasema

'Mhh maana tulitaka tuingilie kati,... ila cha ajabu huyo mama alipotuona tu akatulia, utafikiri anatufahamu..’akasema mmojawapo.

‘Huenda yeye anawafahamu yeye ni mama wa kutoka mbinguni….’akasema dakitari kwa mzaha na yule ofisa mmojawapo anyefika hapo mara kwa mara akatabasamu na kugeuka kumtupia jicho nesi, halafu akageuka kumuangalia huyo bosi wake.

‘Haya niambia umetuitiani nini, au ni hilo la huyo mama, mnataka akalale selo..’akasema akigeukia dirishani kuangalia kule alipokuwa kalala huyo mama, kuliilkuwa sasa kumetulia.

‘Nimekuita ili tulimalize hili tatizo, kama tulivyoongea, ….naona umekuja na mwenzako..hujiamini nini.....’akasema

‘Tulimalize kwa vipi?’ akauliza akigeuka kumuangalai nesi, halafu akageuka kumuangalia huyo mkuu wa hiyo hospitali.

‘Nataka tuendeshe kesi ..’akasema na huyo ofisa usalama kwanza akacheka halafu akashika kidevu, na kumuangalia mwenzake na mwenzake akasema;

‘Nakusikiliza wewe maana mimi hapa ni mualikwa tu..., na sijui mimi nimealikwa kama shahdi au kama nani..’akasema huyo ofisa mwingine

‘Wewe utakuwa hakimu..’akasema na yule ofisa akawa kama anajikagua kujiangalia, ilikuwa kama wanaigiza, lakini wao walijua ni nini wanachokifanya, nesi akawa kimia tu.

‘Mhh, sijui kama nafaa kuwa hakimu, maana unaona nilivyovaa,….hapana naona utafute hakimu mwingine, unaonaje mkuu, wewe uwe ni hakimu..’akasema.

'Mhh....'huyo ofisa mzoefu wa hapo akaguna na mkuu wa hiyo hospitali  akasema;

‘Naona tusipoteze muda, wakati umefika…’akasema na kutembea kuelekea mlangoni nesi aliyekuwa bado kasimama, akageuka kuangalia kule alipokuwa huyo mama, akaona kumetulia na yule mama kalala kitandani kwake.

Mkuu wa hiyo hospitali akafungua mlango na kumuita yule dakitari aliyekuwa akimuhudimia huyo mgonjwa, akasema;

‘Huyo mama anaweza kuja hapa..?’ akauliza kukawa na ukimia halafu mkuu huyo akaingia ndani na kusema;

‘Nesi unaweza kukaa pale huyo mama ataletwa na kigari , atakitumia hich hicho kama kiti, japokuwa anaweza kutembea, lakini kwa tahadhari naona tufanye hivyo….’akasema na nesi akawa kimia hakujua hata afanye nini akaona atulie aone ni nini kitakachoendelea lakini akilini alishaamua moja…hatakubali mtoto wao achukuliwe na mtu asiyefahamika…

************

 Docta bingwa wa magonjwa ya akili, alimuangalia yule mama, na akamuuliza

‘Mama si unaweza kutembea..?’ akamuuliza

‘Nani alikuambia siwezi kutembea, mimi nimeshapona..’akasema huyo mama akijitutumua pale kitandani.

‘Lakini mwili wako bado hauna nguvu, naona ukae kwenye hiki kigari twende ofisi ya mkuu, anataka kuongea na wewe kuhusu hayo madai yako…’akasema

‘Sio madai …sijamshitaki mtu, ninayoongea ni ya ukweli…na huyo dakitari wangu mbona kajificha huko ofisini ....anaogopa eeh, au ndio kaamua kumtetea nesi wake...?' akauliza

‘Sio..unajua anataka kukusaidia, lakini kama uonavyo hapa hatuna mtoto wako, na wewe unadai mtoto wako kachukuliwa na nesi,na nesi hakubali kuwa kachukua mtoto wako, sasa hebu niambie tutahibitishaje hayo madai yako…’akasema

‘Mimi yote hayo nimeyaona kwenye ndoto, wiki hii nzima nimekuwa nikiota hayo hayo…na nina uhakika ndoto hiyo inanielezea ukweli ulivyokuwa na ndivyo ilivyokuwa, maana sasa hivi nina akili zangu timamu,nimekumbuka kila kitu. …msifikiri mimi ni kichaa, au malaria imepanda kichwani…hiyo haipo kabisa…, ‘akasema

‘Tunajua, hata mimi nionavyo, wewe umshapona,…lakini….unasema hayo unayodai yanatokana na ndoto, kama ni ndoto tu huwezi kuiweka kiushaidi, si unajua sheria au….hebi nikuulize ina maaana kila ukiota inakuwa ni kweli….?’akamuuliza, na yule mama akatikia kichwa na kusema;

‘Ni ndoto iliyonisaidia kunikumbusha ukweli....hayo ninayosema sio ndoto bali ni ukweli, yalitokea, ndoto hiyo imenisaidia tu...’akasema

‘Basi utaielezea hiyo ndoto huko kwa bwana mkubwa, unasemaje ?’ akauliza

‘Najua nyie mnafikiria kuwa bado kumbukumbu zimepotea, kumbukumbu zangu zimesharejea, na ukweli umeshadhihiri,…nimekumbuka kila kitu nilipotoka na kile kilichotokea siku ile hapa kwenye hii hospitali….mimi sitaki jingine nataka moja tu… namtaka mtoto wangu …’ akasema huku anamwangalia huyo dakitari.

‘Ni sawa ndio maana nataka ukaliongelee hilo kule ofisini, unaona hapa kuna huyo mgonjwa tutakuwa tunamsumbua, …wewe si umepona lakini mwenzako hajapona…unaonaeeh, sasa sio busara kumsmbua mgonjwa, au..?'akasema na yule mama akageuza kichwa kumuangalia yule mgonjwa aliyelazwa pale kitandani, akasema;

‘Samahani mgonjwa, ni hawa watu hawataki kunielewa, sikutaka kukusumbua..eeeh samahani sana..’akasema akiinua mikono juu kama kuomba msamaha..na yule mgonjwa akatikisa kichwa kukubali.

‘Kwahiyo tunaweza kwenda huko kwa mkuu …..au bado hujisikii vyema?’ akauliza huyo dakitari

‘Sawa….tunaweza kwenda, na yule nesi yupo huko huko...au kakimbia?' akauliza

‘Yupo si ndio unayemdai, anatakiwa kusema wapi kampeleka mtoto wako au sio?' akaulizwa

'Ndio...nataak leo kieleweke...sijui kampeleka wapi mtoto wangu, lakini nina uhakika yupo mahali..sikumbuki ni wapi, ..hapo akili haitakia kunifunulia,..ni lazima asema yup[o wapi...'akasema

'Sasa...naomba maana wewe umepona,..usije kuleta vurugu kwa huyo nesi, unasikia,  au sio tukiona...ukileta vurugu tutajua hujapona, itabidi tukupige masindano..’akasema

‘Hahaha..hivi huniamini eeh,…twende…, ila mimi nitatembea mwenyewe sitaki hicho kigari chenu, mimi sio kiwete..’akasema na yule dakitari akatabasamu, na akamuacha huyo mama, akatoka pale kitandani alikuwa tayari kutoa msaada, lakini huyo mama alionekana na nguvu tu, akatoka pale kitandani, akajiweka vyema, akageuka kuelekea hiyo ofisi ya huyo mkuu, na kuanza kutembea kwa hali nzuri na huyo dakitari akawa nyuma yake.

Docta huyo akiwa nyuma yake alikuwa akiwaza kuhusu huyu mama, akijaribu kuyapima maneno yake kama yana ukweli au bado kachanganyikiwa. Kwa uzoefu wake, huyo mama atakuwa alipatwa na matatizo yaliyoyomfanya apoteze kumbukumbu. Na sasa kumbukumbu zimeshamrejea.

Yeye alifika mwanzoni na kujaribu kumhudimia huyo mama, na kipindi hicho alikuwa na safari kikazo, kwahiyo alimuona mara moja, na kuondoka, na safari hii nia ya tatu kuonana na huyo mama…

Katika kumbukumbu za historia yake alisoma kuwa huyu mama, pamoja na meraha ya kuungua, huenda ana matatizo ya akili, kwahiyo akashauri yeye kama mtaalamu wa mambo hayo akutanae na dakitari wa bingwa wa mambo ya akili.

 Siku nyingine aliyofika na kuonana na huyo mama hakupata ushirikiano wowote, kwani akila alipomhoji, huyo mama alibakia kumwangalia tu. Na hata alipojaribu kumuondoa hicho kitambaa anachojifunga usoni, ikawa ni ugomvi, hakukubali kabisa.

Siku hiyo hakupenda kumlazimisha kwa lolote, kutokana na ujuzi wa kazi yake, aliona amuendee kihatua moja baada ya nyingine. Na leo ndio safari ya tatu, kakutana naye keshacharuka, na hapa akagundua kuwa huyo mama kumbukumbu zilishamrejea, lakini alitaka kujua undani wa tatizo, kwani hata kama kumbukumbu ndio hizo zimemrejea, huenda ikawa ni marejeao ya vipindi vipindi, anaweza akarejewa na tatizo hilo tena.

Akivitizama  vipimo mbali mbali vya huyo mgonjwa, hakuna hata kipimo kimoja kilichoonyesha kuwa huyo mama anaumwa malaria `celebra-malaria’ kama alivyokuwa akihisi mwanzoni, kuwa inawezakana ikawa chanzo cha matatizo yake, hayo ni malaria sugu…. Lakini kutokana na vipimo hakuna matatizo kama hayo, akaguna na kukuna kichwa.

Akiwa nyuma yake akiwaza, sasa walishafika mlangoni kuingia kwa mkuu huyop wa hospitali, yeye aliendelea kuwaza jinsi mam huyoa livyokuwa na nguvu kama isingekuwa walinzi kumshikilia basi huenda mama huyo angmtafuta huyo nesi na kuleta vurugu kubwa.

Lakini swali kubwa likawa, huyu mama anadai kuwa alikuwa na mtoto, na anadai kuwa mtoto huyo alichukuliwa na huyo nesi, kwa vipi….aliwahi kuongea na huyo nesi, na huyo nesi akasema mama huyo kachanganyikiwa anamtambua toka huko kijijini….sasa hali ndio hii, mama akili zake zimerejea nab ado anadai kuwa nesi huyo kamchukua mtoto wake, …nesi atasemaje

Yule mama alipofika pale mlangoni akasimama, hakushika mlango, dakitari akasogea na kushika kitasa cha mlango, halafu akasema;

‘Unaweza kuingia,….yule mama akabakia amesimama, …dakitari akamshika mkono, wakaingia wote …na jicho la kwanza ya huyo mama lilitua kwa nesi, na hapo akasimama, akaupachua mkono kutoka kwa yule dakitari akawa kamuelekea nesi…

Mkuu wa hiyo hospitali akasimama, na yule ofisa usalama naye akafanya hivyo, ambaye hakuonekana na wasiwasi alikuwa dakitari aliyekuja naye alikuwa kasimama mlangoni akimuangalia nesi,

Nesi, akawa anaonyesha wasiwasi, macho ya woga yakamtanda …..

NB: Sehemu inayokuja ni muhimu sana, tuwemo pamoja

WAZO LA LEO: Mara nyingi kunapotokea mgomo vurugu, vita wanaokuja kuumia ni wale ambao hata hawajui ni nini kiini cha hiyo vurugu. Mgomo au vita…kwa wenye moyo wa huruma na utawala bora, wanastahiki kuviangalia hivi vitu mapema, katika meza ya majadiliano, ili kukwepesha maumivu, shida na adha zinazowapata wale ambao hawana hatia, hasa wazee, akina mama ambao wengi wanateseka kutafuta riziki za watoto wao kwa shida, wapo watoto wadogo na wazee wasiojiweza…au wananchi wa akwaida tu ambao kipato chao ni cha shida…


 Jamani,… ubabe, ushindani, ni sawa na mafahali wawili, ambao wakipambana vinavyoangamia ni nyasi, na sasa nyasi ni wananchi wasio na hatia,…tuweni waungwana na tutumie hekima na busara katika maamuzi yetu, na sio kuangalia ubinafsi na njia za kujinufaisha kivipato,au hata kisiasa .
Ni mimi: emu-three

No comments :