Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, April 8, 2015

NANI KAMA MAMA-54


‘Ipo kwenye kumbukumbu za madai ya watu, na ushahid ni kama huo kutoka kwa huyu mama, kama atathibitisha hilo ..nesi utakuwa hatarini, ni bora ukaniambia ukweli nikajua jinsi gani ya kukutetea, kama itawezekana kufanya hivyo..’

‘Ina maana umeshanishitakia?’ akauliza nesi.

 Nesi alikumbuka mazungumzo yake na mkuu wake wa kazi akiwa nyumbani kwake, akitaka kujipumzisha kidogo, kabla ya kurudi kazini kwake, na alishapanaga akirudi ni lazima aongee na huyo mama….huwa anapata masaa mawili ya kupumzika na akiwa kwenye mapumziko haruhusu mtu yoyote kuja kumsumbua….

Akiwa kajilaza kitandani, akilini mwake akawa anapanga mikakati ili amuwahi mkuu wake kabla hajafanya lolote

‘Ni lazima nimuoyesha ushahidi wote kuwa huyu mama sio yule aliyekuwepo kipindi kile, yule mama alishafariki,..lakini bado natakiwa kuwa na tahadhari….’akawa anaongea wa sauti ya chini kwa chini..
.
Nesi alijua kuwa mtu ambaye anaweza kumtegemea kwa hivi sasa ni dakitari kijana, kama atakuwa na hizo kumbukumbu kwenye komputa yake basi ataweza kumuokoa, tatizo ni kuwa dakitari huyo hapatikani mpaka yeye apige simu kuwa kuna muda alimsikia huyo docta akiongea na mtu, na akawa anataja neno afande,…na kusema

‘Inavyoonyesha mkuu wangu wa kazi atakuwa keshawasiliana na watu wa usalama, sijui kwa vipi japokuwa ananificha….sijui lengo lake hasa ni nini…..’akajiongelesha.

‘Hata hivyo siwezi kukubali kushindwa kirahisi, siwezi kufichua siri ya mtoto,…yule ni mtoto wa dada yangu, maana mama yake mzazi ni marehemu..haitwezekana mtu ajae kutoka huko alipotoka na kudai mtoto, je ana lengo gani na huyo mtoto, hapana..yule ni mtoto wa dada yangu,…’akasema kwa sauti na mara mlnago ukagongwa…

Tuendelee na kisa chetu…..

*************

Askari idara ya upelelezi, alifika hospitalini, na kwenda moja kwa moja ofisi ya mkuu wa hiyo hospitalini, ....na manesi wanaomfahamu walimuona, na wakajua kuna jambo, maana kama mtu wa usalama huyo angekuwa ni mgonjwa asingeelekea moja kwa moja kwa mkuu wa hiyo hospitali, angepitia sehemu ya maelezo na kuchukua kadi.

‘Mhh hapa kuna jambo...’akasema nesi ambaye alikuwa msaidizi wa nesi mkuu, yeye hakusubiria kujua ni nini kinachoendelea, huwa hapendi kuongea na polisi, kwahiyo moja kwa moja alikimbilia kwa nesi mkuu , hakujali kuwa muda huo esi mkuu hataki usumbufu….


Huku nyuma ofisa huyu wa upelelezi alifika mlangoni kwa mkuu wa hospitalini hiyo bila kupiga hodi akafungua mlango, na kumkuta mkuu huyo akiwa katika heka heka zake za kikazi, na bila kusema neno akaelekea kwenye kiti na kukaa, akachukua gazeti na kulipitia kama vile hajalisoma, huku akimtupia macho mkuu huyo wa hospitali.

Hakutaka kumsumbua, alisubiria mkuu huyo amalize kile anachokifanya na mkuu wa hospitali hiyo alipomazliza kile alichokuwa akikifanya, akainua kichwa na kumuangalia Inspecta na kutoa atabsamu la kujilazimisha, na aliyeanza kuongea ni Inspecta mwenyewe;

‘Unapokuwa kwenye ofisi ya mwenzako bwana, unakuwa huna nguvu, hata kama kwako ulikuwa na nguvu fulani ya ubosi ....’akasema huku akikunja miguu na kuweka nne, akatizama saa yake halafu akatulia.

‘Ni kawaida afande, japokuwa wengine huwa hawajali kupiga hodi maana wanajiona wao ndio watawala wa nchi...., samahani kidogo, kuna kumbukumbu za mgonjwa mmoja nilikuwa naziweka sawa, ...najua tukianza mazungumzo yetu hapa naweza hata kusahau..haya nambie umefikia wapi mwenzangu...?’ akamuuliza akikaa vyema kwenye kiti

‘Hahahaa..watawala wa nchi, sio kweli, ….sisi ni vibarua wenu bwana….Ndio nimerudi toka kule kijijini kama nilivyokuambia nitakwenda huko, sikutaka kuelekea ofisini kwanza, nikaona nikupitia, maana kazi hii nimeamua kuifanya mwenyewe hata bosi wangu sijamfafanulia ni kazi gani ninayoifanya..’akasema

‘Nakujua uwajibikaji wako, ehe, nipe habari..’akasema

‘Kwanza nilikwenda kule kwa huyo mama marehemu, nikafuatilia hadi kwenye kaburi lake, ni kweli kuwa kulikuwa na mati ya mama mmoja alipatikana karibu na bonde la mpunga, njia ya kuelekea kijiji cha mpunga…kijiji hicho kimepewa jina hilo kwa vile wanalima sana mpunga.

Maiti ya mama huyo ilikuwa na sare za hospitali hii, kuashiria kuwa alikuwa mgonjwa hapa, na akaja kutambulikana na ndugu, basi wao na viongozi wa kijiji wakakutana na hawakutaka zaidi, wakaona wazike tu.....nikalitembelea hilo kaburi basi…’akasema akionyesha kuchoka.

‘Umekwenda haraka hapo...najua una haraka ya kutaka kuondoa, lakini nataka niyaelewe haya mambo kiundani zaidi, ....hebu niambie vyema hapo...maana sizani kama ulifika ukaambiwa hivyo, ukaenda kaburi ukalitizama ukaamini ukarudi...’akasema docta

‘Hapo nimekupa kama dondoo, ila kiukweli nimehangaika sana, utafikiri kuna kesi kubwa ipo mbele yetu….’akatulia

‘Lakini hii ni kesi kubwa, kama zoezi la kufanya utafiti wa haya mauaji hautakamilika unafikiri utakuja kusema nini..mimi ni kama msaada tu kwako ,lakini kazi kubwa ipo mikononi mwako..’akasema docta

‘Najua…kwanza tuanzie kwenye kijiji cha huyu mama aliyefariki, ...inavyoonyesha ni kuwa huyo mama aliwahi kutibiwa hapa, na kulazwa hapa ndio maana ana sare za hapa zenye namba kabisa,...’akasema.

‘Wewe hayo uliambiwa hivyo na nani?’ akauliza docta

‘Na ndugu zake, upande wa mume, ..ina maana mama huyo aliolewa hapo alipozikiwa, walichukua jukumu la kumzika ni upande wa kliumeni kutokana na taratibu zao, na walifanya hivyo baada ya kukutana familia za huyo mama na upande wa mume mtu…na nilikuja kuthibitishiwa huo ukweli nilipokwenda upande wa mke anapotokea.....’akasema.

‘Kwahiyo, nesi kasema ukweli…sasa huyu mama anadai mtoto yupi?’ docta akawa anajikuna kichwa, baadaye akauliza swali

‘Sasa hebu kwanza wanasemaje je kuhusu ujauzito hawakuongelea lolote kuhusu mama huyo kuwa alikuwa na mtoto kitu kama hicho…? akauliza


‘Walikubali kuwa kweli huyo mama alikuwa mja mzito, ghafla akatoweka, ...upande wa kiume ukidai, wao walijua mama huyo karudi kwao, na upande wa kikeni wanasema wao walijua mtoto wao yupo kwa mume wake....kuna mashirikiano hafifu kati ya familia hizi mbili, lakini kulipotokea huo msiba wote wakakubaliana kuwa mama huyo alikufa kifo cha kawaida tu....hawakutaka kuanzisha malumbano au kesi….’akasema

‘Je kuhusu mtoto?’ akauliza docta

‘Kiukweli ni ajabu kabisa, wao walijua kwua mama huyo aliondoka akiwa na mja mnzito, lakini swala la kuwa huenda mama huyo aliwahi kujifungua hapa hospitalini na huenda mtoto yupo hai, hawakulitilia maanani …nilivyowaona na kuwahoji, hawa kulizingattia sana hilo, wao walichosema ni kuwa kwa vile mama huyo alikuwa na sare za huko hospitalini basi kama kuna lolote wangesikia kutoka hospitalini,…kwa kutokusikia lolote wao wakajua kuwa mtoto atakuwa amekufa.....’akasema

‘Haiwezekani hata upande wa kikeni, ….hakuna aliyeamua kuja hospitalini kuuliza?’ akauliza

‘Wanasema siku hiyo ya mazishi, alikuwepo nesi mmoja aliyethibitisha hilo kuwa mtoto wa huyo mama alifariki...’akasema

‘Alikuwepo nesi, walisema nesi gani, Ina maana kweli hawakutaka hata kumtuma mtu kuja kufuatilia hapa hospitalini?’ akauliza

‘Unajua kuna mfarakano wa kifamilia, mke na mume kwa upande mmoja mfarakano huo ulifikia hadi familia mbili za mume na ile ya mke kutokuelewana..ni mambo marefu nikianza kukuhadithia hapa tutakesha..ikafikia hatua, huyo mama kufukuzwa kwa mume,..kiubabe tu..kwa vile huyu mama alikuwa mja mzito, yeye akaamua kwenda kujifungulia kwao, na alitaka baada ya hapo kurudi kwa mume wake,....sasa kwa ubabe huyu mume akaamua kuoa mke mwingine ili kuhakikisha huyo mama harudi tena kwa mume wake...’akasema

‘Je ndugu wa huyo mwanamke, yaani huko alipozaliwa wao wanasemaje kuhusu mtoto wao?’ akauliza

‘Wao walikuwa hawana la kufanya,…wanasema walishakubali binti yao arudi tu, maana wameamua ugomvi wao hauishi na binti yao amekuwa akipigwa hadi kuumizwa sana….’akasema

‘Oh, aliumizwa wapi, kama ulidadisi hilo?’ akauliza na ofisa huyu akawa kama anatabasamu halafu akasema

‘Unajua hawa jaama wakianza kupiga hawaangalii wanatumia nini, wanasema waliwahi kumharibu kabisa uso mtoto wako…eti kuondoa huo uzuri anaoringia huyo mwanamke..’akasema

‘Ina maana walimkata kara..kama kukwaruza hivi ..na kitu kama miiba au …?’ akauliza docta

‘Hilo siwezi kuwa na uhakika, …..ingelikuwa nimeiona maiti ningelikumbuka kuuliza hivyo, kwanini unauliza hivyo…” akauliza

‘Kuna kitu nataak kuthibitisha, lakini ngoja kwanza nisikia maelezo yako…’akasema

‘Basi upande wa kikeni, wakaona hakuna haja…binti yao ameshafariki basi na walipoulizia kuhusu mtoto wakaambiwa binti yao hakuweza kujifungua mtoto hai, ....mtoto hakuwa ni bahati,.... kwahiyo wangefanya nini zaidi, walimshukuru mungu maana yeye ndiye kapanga iwe hivyo..ndivyo walivyoniambia...’akasema

‘Je nini maisha ya wanandoa hao, kati ya mke na mume wake?’ akauliza

‘Walikuwa kama paka na chui....kila siku kusuluhisha ugomvi, ...na mume akawa na nyumba ndogo...akawa anaishia huko , na mke huyu wa ndoa akawa hakubali, akaanzisha vita na nyumba ndogo hiyo...na kwa vile mama huyu alikuwa mja mnzito, wengi wakamshauri atulia kwanza, na muhimu  arudi kwao ujifungua kwanza....sasa hapo kati, ndio kukawa hakuna mawasiliano..huku wanajua huyo mama kaenda kwao, na huko kwao mwanamke wanajua mke yupo wa mume wake, .....’akasema

‘Haiwezi ikawa kuna hujuma hapo kati kati, kuwa huenda huyo mama aliuwawa..na najiuliza wanini wanafamilia hawakutaka kulifuatilia hilo.....?’ akaulizwa

‘Kitu nilichojifunza, familia nyingi maeneo ya huko, wanaishi kimila zaidi, na waamini sana mambo ya kishirikina...wanadai mume alioa mke ambaye sio chagua la mizimu ya upande wa mume, na mizimu inataka huyo mwanaume amuache huyo mke  aoe mke ambaye mizimu inataka ndio maisha ya mume yatakuwa mazuri, kwani walikuwa na maisha magumu sana...ni mambo ya kizamani sana....na mume akakiri kabisa eti hakuwa anampenda mke..sasa kwanini walioana, anadai, ilikuwa ujana na shinikizo la wazazi,......’akasema

‘Ajabu kabisa...’akasema docta

‘Ndio hivyo....’akasema Inspecta

‘Kwahiyo kwa kifupi huko hakuna cha maana kuhusiana na hili tatizo?’ akauliza docta

‘Cha maana ni kuwa huyo mama alijifungulia hapa,..inavyoonekana hivyo, na mtoto akafariki....sasa kinachotakiwa kama nilivyokuambia ni kuangalia kama kuna kumbukumbu za huyo mama hapa,zinazoonyesha hivyo.... wewe unasema hukukuta kumbukumbu zozote za miaka hiyo...hapa nabakia bila msaada’akasema akitikisa kichwa.

‘Ni kweli kumbukumbu kama hizo hazipo, ..inaonekana kama ilipagwa iwe hivyo, maana hiyo store ukifika sasa hivi haitaamniniki , nilimwambia mtuza store ajaribu kukusanya kumbukumbu zote atakazoziona zinafaa, lakini hata hizo zilizopatikana hazihusiania na mama yoyote aliyewahi kuwa na matatizo kama hayo...’akasema

‘Kwahiyo inatupa picha kuwa huyo mama huenda ndiye huyo mama anayemzungumizia nesi wako..japokuwa nesi hajakuelezea kila kitu…?’ akawa kama anauliza

‘Kwa hali iliyofikia inaonyesha hivyo, ila mimi sijakubaliana na hilo..nahisi bado kuna kitu kimejificha nyuma ya pazia.....hasa kutoka kwa huyu mama anayedai kuwa huyu nesi kamchukua mtoto wake....nina ushahidi fulani nitakuja kukuelezea wakati muafaka, lakini sasa unanichanganya, unasema huyo mama, alipigwa, akaumizwa, na uso uliharibiwa...hebu nambie zaidi kwenye uchunguzi wako...’akasema

‘Kuhusu alipigwaje, aliumizwaje….hapo inakuwa vigumu ..kama nilivyokuambia sikuweza kuyauliza hayo, kama ningekuwa na jambo la kunifanya niulize hayo ningefanya hivyo….unajua,…si jui unanielewa..’akasema

‘Ok, tuache hayo, ina maana ukaishia hapo..?’ akaulizwa

‘Nilikwenda kumtafuta nesi mkuu aliyekuwepo kipindi hicho...nilimkuta anaumwa sana, hana kauli...nilijaribu kuwaulizia kama aliwahi kuongea lolote kuhusu maisha yale alipokuwa akifanya kazi kwenye hospitali hii wakasema hakuna anayefahamu., wanasema nesi huyo hakuwa na ushirikiano na ndugu zake kipindi akiwa na kazi na maisha mazuri alijitenga kabisa na familia yao, akajiona yeye ni yeye, sasa kazidiwa ndio anakumbuka jamaa zake.....’akasema

‘Huyo nesi anaumwa nini  zaidi...?’ akauliza docta akitafakari jambo

‘Shinikizo la damu, kisukari....mmh.....anakuwa kama kachanganyikiwa,….yaani kila ugonjwa anao...inawezekena na upungufu wa kinga mwilini,…..mmmh, hilo nasema tu maana ukimuona kaisha kweli….wanasema bado anafanyiwa uchunguzi.... kijumla hali yake sio nzuri....lolote laweza kutokea, nikaona hapo hakuna kitu....’akasema na kutulia

‘Baada ya hapo?’ akauliza docta

‘Sikukata tamaa, nikaona niwatafuta wale madakitari wengine waliokuwepo kipindi hicho, ambao waliwahi kufanyia kazi hapa kipindi hicho...nilimtafuta sana aliyekuwa dakitari mkuu, nikaambiwa kahamia nchi ya jirani,kaenda kufanyia kazi huko ...’akasema

‘Acha wee...kaamua kukimbia nchi baada ya hiyo kashifa?’ akauliza

‘Nasikia hata uraia kaukana...japokuwa baba yake alikuwa mtanzania, lakini kwa asili babu zake walitokea nchi ya jirani, ..huyo dakitari akaona afuate nyayo za mababu zake, na kwa vile ana utaalamu wa kidaitari, basi huko akapokelewa...ni dakitari anayetambulikana sana huko..kiujumla ni mtaalamu lakini ndio hivyo,wanasema naye kuna muda anakuwa kama kachanganyikiwa hivi.....’akasema

‘Oh, afande, unajua kuna kitu haoa…`kuchanganyikiwa’….kila anayehusikana na hili tukio naona anaishia huko…lakini hebu tuone zaidi kwenye uchunguzi wako,..je hukufuatilia huko nchi ya jirani kujua zaidi, kwa msaada wa ujirani mwema, maana nyie mnasaidiana au sio, hata kwa simu?’ akauliza

‘Unajua swala kama hili huwezi kuomba kitu kama hicho, maana halijafunguliwa mashitaka, ni tume tu kuchunguza haya mauaji...ingekuwa ni kesi ipo mahakamani ..basi tungefuata taratibu zinazohitajika, ....aaah, nikaona huko kwanza niache kama itabidi basi tutafanya hivyo..lakini kwasasa sioni umuhimu wake...’akasema

‘Wengine?’ akauliza

‘Mdakitari wengine hawajui lolote na hawakumbuki kwani wanadai akina mama kama hao walikuwa wengi maeneo ya huku, wakanitolea visa vingi..na havijaendana na kisa kama hiki…., sasa yupi ni yupi, inawawia wao vigumu kukumbuka...kwahiyo kutoka kwa hao madakitari hakuna nilichopata, sizani kama wanaficha , hakuna dalili kama hzi za kuficha ukweli...’akasema

‘Kwahiyo, ukasalimu amri..nilijua tu hutaiweza hii kesi.....’akasema

‘Lakini docta hapa hakuna kesi...ni kwamba tunajaribu kuangalia kama tunaweza kufungua kesi ya namna hiyo, au kugundua lolote kuhusiana na mauaji ya wazee, akina mama na imani za kishirikina...’akasema

‘Ok, ok..mimi niliona hii ingelikuwa ni njia ya kugundua mengi, sasa ina maana hii haitatusaidia kitu…’akasema

‘Kwa hili, ….mimi naona tukubali aliyosema nesi kuwa mama huyo alifariki, na ndio huyo aliyezikwa hapo.... sasa labda huyu mama anayedai kuwa aliibiwa mtoto aweze kutuonyesha njia na akitupatia ushahidi wake huenda utatusaida kitu...au kama wewe unavyodai kuwa kuna dalili za ushahidi, unielezee tuweze kuufanyia kazi…maana kuna utata mwingine..’akasema

‘Utata kwa vipi?’ akauliza docta.

‘Utaona kwenye sehemu ya pili ya maelezo yangu ilivyo, ...’akasema

**************
Docta akajiegemeza kwenye kiti akisubiria sehemu ya pili, huku akiwa na yake kichwani ambayo hakutaka kumuahdithia kwanza huyo ofisa usalama mpaka apate uhakika fulani kutoka kwa nesi.

‘Ehe niambie…’akasema docta

‘Mhh….’akasema mkuu huyo huku akipiga miayo, na docta huyo akasimama na kwenda kumtengenezea kahawa, ….ofisa akapiga mafundo mawili, halafu docta akasema;

‘Twende sehemu ya pili, ulisema ulikwenda kijiji kingine kipi hicho?’ akauliza

‘Kule alipotokea huyu mama anayedai kuwa mtoto wake kachukuliwa..kule  alipopatwa na hilo janga la kukatwa mapanga, na kuchomwa moto, …’akasema

‘Ehe huko uligundua nini au ni yale yale?’ akauliza docta akionyesha kukata tamaa

‘Unajua hata wakati nakwenda huko nilishapata vitisho, ...’akasema Inspecta

‘Vitisho!! vitisho gani?’ akauliza docta akionyesha mshangao usoni

‘Kuna hawa wenzangu ambao waliwahi na wao kutumwa kuchunguza matukio kama haya…na japokuwa hakuna kesi iliyofunguliwa rasmi kuhusu huyu mama, ..kitu ambacho niliona ni ajabu, …..’akasema

‘Labda waliona hakuna kesi ya kujibu, hebu niambia huko Ilikuwaje maana naona muda unakwisha na hapa nina mgonjwa wa kwenda kufanyiwa upasuaji…huko wao waligundua nini?’ akaulizwa

‘Hahaha, hao jamaa wameamua kabisa na kucha kazi, mmoja alikuwa kachanganyikiwa kabisa akapelekwa kwao, huko wakahangaika, na hata sasa hayupo sawa, basi kiafya akaona apumzike...niliongea naye  kipindi fulani, huyu ndiye wa kwanza kunionya, aliposikia nimehamishiwa kituo hiki kufanya yale yale waliotumwa wao....’akasemaa

‘Kwanini afikie kukuonya, ni kuhusu hilo, au kilichomkuta yeye ni kitu gani hasa......?’ akauliza

‘Hakutaka kuniambia undani zaidi na kwa kipindi kile sikuwa na lolote kuhusu hili, na lilipojitokeza ikabidi nijaribu kuwasiliana naye..ndipo akanionya akaniambia..niachane kabisa na jambo hili la huyo mama aliyeunguzwa na moto na kukatwa na mapanga....’akatulia

‘Ina maana kuchanganyikiwa kwake kunaweza kuhusiana na huyu mama?’ akauliza docta

‘Hakutaka kabisa kuniambia zaidi,…mimi  nikaona ngoja mimi nifuate nyayo zao, nikaifuatilia walipopitia, hadi hapo huyo mama alipopatwa na hili janga la moto na kukatwa na mapanga...wao wakanielekeza kwa huyo mama ambaye wanadai yeye anafahamu zaidi kuhusu huyu mama mgonjwa, kwani yeye alikuwa wa kwanza kumuona, zaidi ya hayo hawajui kwani wao walifanya usamaria mwema kumuhifadhi tu, na ndio likatokea hilo janga.....’akasema

‘Mhh, kwahiyo hapo hukudadisi sana, kama huyu mamaalikuwaje, alikuwa na mataizo gani hakuweza kuongea nao lolote?’ akauliza

‘Nilipanga nitarudi tena hapo, lakini niliyoyasikia kwa huyo mama huko, nikajikuta nimesahau hata kurudia hapo…’akasema

‘Haya hebu niambia katika kumbukumbu ofisni kwako, ulikuta nini...waligundua nini, hao waliowahi kufika huko siku hiyo ya tukio...kitu cha kusaidia maana naona kama unanipotezea muda wangu…?’ akauliza

‘Hakuna kitu...hakuna kesi kama hiyo..hakuna walichogundua, yaani walipoteza muda wa serikali bure….’akasema Inspecta

‘Lakini si ilikuwa ni kesi, mama kakatwa na mapanga..kaunguzwa na moto....huoni kuna jambo hapo linafichwa…?’ akauliza.

‘Hakuna kumbukumbu..ni kama halikuwepo hilo tukio, mimi nikalifufua, ..ilikuwa ni kazi kumshawishi mkuu wa kituo cha huku...sijui kwanini hakutaka hiyo kesi ifufuliwe tena, ..nikaichukua kama moja ya majukumu yetu...kuona kama tunaweza kugundua kitu...’akasema

‘Ehe haya nambie huko kwa huyo mama ulipofikwa uliambiwa nini cha kusaidia,… akaulizwa

‘Huyu mama naye ni kama alidondoka kutoka mbinguni, maana alipotokea hasa haijulikani, ....nilitarajia kuwa huyu mama ataniambia la maana, kama anajua wapi huyu mama katokea,….ndio akanipa habari za utata kabisa....nikaona hawa watu wameharibiwa akili na ushirikina...’akasema

‘Kwanini..?’ akauliza

‘Anadai huyu mama sio mwanadamu wa kawaida,...ni mwanadamu ndio lakini kaingiwa na shetani, ambalo limemgeuza huyo mama kuwa huyo mama aliyefariki kipindi cha nyuma kwa dhuluma....’akasema

‘Sijakuelewa...mama yupi aliyefariki huko nyuma…!’ akauliza

‘Huyu mama kwa kauli ya huyo mama aliyenisimulia  ni kuwa  huyu mama sio binadamu wa kawaida ni mzimu,au mfu aliyefufuka...lakini kwa kupitia, ina maana yeye ni mtu, kaingiwa na hilo shetani, ..na hilo shetani likitoka  kwa huyu mama, huyu mama anakuwa maiti,...kwahiyo huyu mama..ni kama mtu- shetani, yeye ni mzuka au tuite mzimu wa mama mdhulumiwa....ni vitu visivyoelezeka, nikaona ni yale yale mambo yako unayofanyia uchunguzi,....’akasema

‘Yaani umenifanya nihamasike kusikiliza …ikibidi nikaonane na huyo mama, ehee….ok naona nina dakika chache, hebu nambia alikuambia nini…hasa kuhusu huyu mama, maisha yake ya huko nyuma yalikuwaje?’akauliza

‘Huyo mama aliyekufa, alikufa kwa mateso makubwa, na alikufa akiwa mja mzito, na mtoto wake akachukuliwa....’akasema

‘Wauuuuh, .akachukuliwa …yule kula wanasema alikufa…unaona vinakuwa vitu viwili tofauti au?’ akauliza

‘Wanaosema ni wanandugu wasiotaka kufuatilia,..huenda kweli mtoto alichukuliwa ndio maana mama huyu akarudi kubainisha ukweli…’akasema ofisa.

‘Ndivyo ulivyoambiwa au ni maelezo yako?’ akauliza

‘Huyo mama alichoniambia ni kuwa huyo mama roho yake haitatulia mpaka kuhakikisha kampata mtoto wake...ina maana alikuwa na mtoto kabla ya kufa, na alijua akiondoka mtoto wake atachukuliwa na watu….na ukweli utapotea, sasa akarejea kuubanisha huo ukweli na haki itendeke….’akasema

‘Mtoto wake yupo wapi, huyo mama alikuambiaje kuhusu hilo....?’ akaulizwa

‘Huyu mama, anasema yeye kwa mujibu wa mambo yake hawezi kulisema hilo, na hajafunguliwa kujua wapi alipo huyo mtoto, ila huyu mama ...yeye anamuita mzimu, anajua wapi mtoto wake yupo...’akasema

‘Ok, tuchukua kampata mtoto wake ...ndio basi kakamilisha ujio wake huo au kuna aho waliomtesa keshawapata au ndio hao wanaochanganyikiwa…?’ akaulizwa

‘Kumpata mtoto wake ni jambo jingine na kulipiza kisasi ni jambo jingine...’akasema ofisa

‘Kulipiza kisasi kwanani sasa....kwa hao waliomuibia mtoto wake, au kwa hao waliomtesa?’ akauliza

‘Wote.....ikibidi’akasema

‘Mhh, ina maana kama ni hivyo nesi yupo matatani...?’ akauliza docta akiwa kainamisha kichwa chini kama anawaza jambo

‘Nao hao walioshirikiana naye...’akasema ofisa usalama

‘Ina maana hao madakitari waliokuwepo kipindi hicho au kuna watu wengine wameshirikiana na huyu nesi...?’ akauliza

‘Ungeuliza swali kwanza …Mtoto yupo wapi..ina mama kama kuna mtoto...atakluwa anaishi mahali na watu waliomchukua,…..na huyo mama kufika eneo hilo la hicho kijiji nia ni kumfuatilia huyo mtoto….. kuhakikisha anampata mtoto wake...’akasema

‘Mhhh....mimi bado sijaipata hiyo yeye alijuaje kuwa mtoto yupo wapi na kwanani...’akauliza docta

‘Unajua kurudi kwa huyo mama, kwa mujibu wa huyo mama aliyenisimulia ni kurudi kulipiza kisasi, kutokana na mateso aliyoyapata...lakini pia kuna mtoto, kama alikuwa na mtoto, basi alitaka pia kuhakikisha kuwa mtoto wake yupo salama...’akasema

‘Kwahiyo kulipiza kisasi hakutawagusa waliochukua mtoto wake...?’ akauliza

‘Kama wanahusika na kuteseka kwa huyo mama, basi na wao wanaadhabu yao,...kisasi kitawapitia...ndivyo alivyoniambia huyo mama..’ akasema

‘Mhhh...hapo kuna walakini....kisasi nikionacho ni kwa hao walimtesa, hawa waliomchukua mtoto huenda wamemchukua kwa nia njema ya kumlea...’akasema.

‘Waliomchukua mtoto wanatakiwa kumrejesha mtoto huyo kwa huyu mama wakifanya hivyo hawana makosa,...na huyu mama atajua la kufanya kwa hao waliomtesa...’akasema

‘Unajua unapozungumzia huyo mama, ni mama huyu ninayemfahamu mimi, au sio...huyu mama hajiwezi, ni masikini..na kwa hali aliyo nayo, naona kama itachukua muda kupona matatizo aliyo nayo ...mimi sioni kama ni jambo la busara yeye kumchukua huyo mtoto kama yupo mahali salama..., ni heri huyo mtoto abakie kwa watu wenye uwezo,wamlee ikibidi wamsomeshe..ni maoni yangu tu...’akasema

‘Ukumbuke hayo ni maelezo ya huyo mama, wanaysema ana kipaji cha kujua mambo, unielewe hapo...hatuna uhakika na hilo  ni maneno yaliyotokana na utabiri au sijui ramli vitu kama hivyo, au njozi maana ukianza kuongea naye nakuwa kama sio yeye, kama vile yupo njozini kwahiyo ni...uoni wake..., kama tukikubaliana nayo ina maana tunaamini ushirikina,..na tukiamini hayo tutakuja kuamini kuwa huyu mama..mgonjwa wako ni shetani, sio mwanadamu...kaja kulipiza kisasi,....je unayaamini hayo...’akasema Inspecta kama anauliza swali

‘Nikuulize wewe kwa jinsi ulivyofuatilia huko, je wewe unayaamini hayo...?’ akauliza docta

‘Tunarudi kule kule..ndio maana nikakuambia hapa hakuna kesi....ni bora tuyaamini maneno ya nesi,..kuwa huyo mama alikufa...maana kaburi lake lipo...ila kuna kitu kingine kilinitia mashaka..ndio maana nikakuambia kuna utata..’akasema

‘Kitu gani...?’ akauliza docta

‘Kaburi la huyo mama..kule kwenye kijiji nilipokwenda awali lilikuwa limefukuliwa....sikukuambia awali ili nije kuoanisha na sehemu hii ya pili..’akasema

‘Limefukuliwa na nani, uligundua siku ile ile, au baadaye…..na je maiti ipo?’ akauliza

‘Haijulikani ni nani kalifukua....na maiti haipo...ni siku ile ile nilipokwenda, hata wao waligundua siku hiyo, wakawa wanashangaa….’akasema

‘Oh, ulijuaje kuwa maiti haipo hapo alipozikwa?’ akaulizwa

‘Nilipoona hiyo hali, nikamuomba mkuu wa kijiji na watu wengine tukafukua tuhakikishe kuwa maiti hiyo ipo au la...wakakubali tukafanya hivyo, hatukukuta maiti...’akasema Inspecta

‘Mhh, sasa ni nani alifanya hivyo...hapo unasemaje?’ akamuuliza

‘Mhh...unajua kama una imani ndogo huwezi kuendelea na hii kesi, lakini mimi kwetu nimeaga, nikasema nitapambana mpaka nione mwisho wake nahisi kuna kitu nyuma ya pazia, haya mambo yanapikwa na watu na wanajua watafanya hivyo ili kuwahadaa watu wasio na utashi wa kuangalia mambo kwa uhalisia wake...’akasema

‘Kwahiyo?’ akauliza docta

‘Nakusikiliza wewe...mimi nimeshafuatilia vya kutosha, sasa nasubiria upande wako, je umegundua nini kwa huyo nesi....?’ akauliza ofisa usalama

‘Kwa huyo nesi naona ama anapotezea muda,au na yeye anahusika kwa namna moja au nyingine...sasa nilikuwa nakusubiria wewe, kama utatoa kibali, ....tumfikishe kituoani, nahisi ana mambo mengi anatuficha, na hili litatutafanya tushindwe kutimiza wajibu wetu...’akasema docta

‘Kwa kosa gani...?’ akauliza

‘Kwa madai ya huyo mama kuwa kaibiwa mtoto na huyo nesi, nahisi tukianzia hapo tunaweza kugundua mengi makubwa yaliyojificha...’akasema docta

‘Mimi naona tufanye hivyo....kama kweli kulitokea wizi wa mtoto , kuna sababu za kufanya hivyo na kuwanasa wahusika, na hao watatusaidia kuweza kuifufua hiyo kesi iliyozimishwa kiaina ..

‘Na hii ni kwamba mkuu wa hospitalini wa kipindi kile atashitakiwa hata kama yupo nchi jirani, pili ...ni najua pia ni lazima kutakuwa na watu wa usalama wanahusika...’aaksema

‘Ndio nilitaka kuukuliziai je ulichunguza kwa upande wako kuhusu mkuu wa kituo kipindi hicho alikuwa nani,  nina hisi naye atakuwa anahusika na hili sakata, maana kesi ilifika kwake kwanini kumbukumbu zote zipotee?.....’akauliza docta

Ofisa usalama akawa kimia na alionekana kama amekazia macho dirishani, na mwenzake alipoona hivyo akageuka nyuma kuangalia hakuona kitu, maana dirisha lilikuwa limefungwa na lina pazia

‘Nahisi kuna mtu anasikiliza hapo dirishani...’akasema ofisa usalama kwa kunong’ona, na docta akafungua pazia..akawa anajaribu kutizama nje akasema

‘Mbona hakuna mtu,....’akasema

‘Nina uhakika nimeona kivuli cha mtu...’akasema ofisa usalama na kufungua mlango kwa haraka na kutoka nje..


WAZO LA LEO: Kuna mambo mengi yanatokea , na wengi tunayachukulia kama yalivyo na hata kujitia kwenye ushabiki kwa kugawana makundi yenye kuhasimiana, kutokana na utofauti fulani fulni,  iwe ni tofauti za ki-itikadi za vyama, imani za dini au hata hali za kiuchumi, ili mradi kuwe na makundi hasi na chanya….Watu bila kutafakari tukio au ajenda, wanakimbilia kwenye ushabiki wa tofauti zao, hakuna uchunguzi, hakuna kutafakari watu wanaanza kunyosheana vidole,.. 

 HILI NI LENGO, la walioandaa mikakati hiyo, na mikakati hiyo haukuanza leo, ni endelevu,…. wameshatusoma, na walijua itakuwa hivyo ili maisha yaendelee…ni wazoi tu, mwenye akili ataona na kulitafakari hili.

Ni mimi: emu-three

No comments :