Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, March 27, 2015

NANI KAMA MAMA-50


‘Lakini mimi bado najiuliza kwani wewe shida yako ni nini hasa kwani huyo mama kashitaki, kwani kumetokea nini zaidi, ni huko kwa mgonjwa kuwa ana mtoto, huyo  kachanganyikiwa, ni kawaida tu,  akipona itakwisha wasiwasi wako ni nini…?’ akasema dakitari yule wa zamani.

‘Docta, siwezi kukuelezea kila kitu kwa hivi sasa, ila ni muhimu sana, …’ akasema nesi maana alijua hiyo ilikuwa ni siri, na jinsi anavyoongea na watu ndivyo maswali yanavyokuwa mengi..akaona hatapata kitu kwa huyo dakitari akaelelea kwa mtunza store na huko hakuambulia kitu, kumbukumbu za huyo mama zimapotea…

Sasa atafanyaje..sasa atajiteteaje kwa wakubwa zake

Tuendelee na kisa chetu


Nesi alipotoka kwenye store ya zamani akiwa kakata tamaa ya kupata kumbukumbu za huyo mama wa zamani alifululiza moja kwa moja hadi kile chumba alicholazwa huyo mama, ulikuwa sio muda wake wa kumtembelea huyo mama maana kulikuwa na nesi anashughulikia,… lakini kama nesi mkuu anawajibu wa kuhakikisha kuwa wagonjwa wanahudmiwa vyema, akaona atumie mwanya huo kumuona huyo mama.

Kitu cha ajabu cha huyo mama, ipo siku moja yeye mwenye alitaka kumpima huyo mama, kwani huko kijijini walikuwa wakidai kuwa huyo mama kila akiona mwenye mtoto anadai huyo mtoto ni wakwake, basi akamuita nesi mmoja, akamwambia amchukua mtoto mdogo, apite karibu ya huyo mama ili waone itakuwaje..

Yule nesi akafanya hivyo,na huyo mama alichofanya siku ni kuwaangalia tu, huyo nesi na mtoto wake, utafikiri alijua kuwa wanampima akili yake,…lakini huyo mama alionekana kama anawaza jambo, lakini hakudai kuwa huyo ni mtoto wake kama ilivyokuwa huko kijijini, ikaonekana kuwa huyo mama sasa anaanza kupona…na nesi akamuendea na kumuuliza

‘Yule mtoto sio wa kwako..?’ akamuuliza na huyo mama akamuangalia tu bila kusema neno, na baadaye nesi akaondoka,..maana ilionekana huyo mama hataki kabisa kuongea., toka siku ile akawa anapita kwa huyo mama anamsalimia, na huyo mama kuna mda anaitikia na kuna muda mwingina akakuwa kimia kabisa..

Leo nesi akaona aende kuonana naye tu….akilini alishaona anahitajia kuongea na huyo mama na takachomuuliza hata hakijui, lakini ni lazima aongee naye…

Kuna kitu kilimsukuma kwenda kumuona huyo mama tu, lakini hakuwa na sababu ya msingi..alihisi anataka kumuona…, akili na mwili vikamtuma kufanya hivyo  huku akijiona kama anaulizwa, na bosi wake wamefikia wapi, nay eye hana la kusema…sasa nitasema nini, akawa anajiuliza .

‘Huyu mama mbona anipa shida…’akasema

‘Hata siwezi kuvumilia tena,  leo ni lazima niongee naye nijue kwanini ananishuku mimi kuwa nimechukua mtoto wake, …wakati sio kweli, kwanini ananifanya niwe na wakati mgumu..kwanini, kwanini…ni lazima nikaonane naye leo..’akasema kwa sauti sasa

‘Kwanza yeye …hafanani na yule mama kabisa, yule mama alishakufa… iweje tena huyu mama, sijui ni nani, anakuja an madai ya ajabu ajabu ya kutaka mtoto..’akasema na akilini akawaza, huenda inawezekana huyu mama anadai mtoto wake ambaye hayupo hapa..ambaye labda yupo kwa ndugu zake….labda, lakini kwanini wakubwa zake wanamshinikiza na mambo yaliyopita,….mmh, lakini hili nimejitakia mwenyewe kwanini niliwaambia kuna tukio kama hilo…’akawa anajisema mwenyewe,

Nesi hakujua kuwa anaongea peke yake tena akionyesha vitendo vya mikono, akawa anakaribia mlango, na huku anasema;

‘Mtu alishakufa, na ikathibitishwa na yule nesi…hapana..hawa wanataka kunipotezea muda wangu bure,…..eti mzuka uje kulipiza kisasi haiwezekani, huyu ni mama mwingine tu…mimi siamini mambo hayo…hapana…’akawa anaongea kwa sauti na kuonyesha msisitizo wa mikono.

Akawa ameshafika mlangoni, akafungua mlango, na hakwenda moja kwa moja kwenye kitanda, ..humo ndani kulikuwa na vitanda viwili na vyote sasa vina wagonjwa….alichofanya yeye,…., kwanza akaenda sehemu ya kuhifadhia vifaa vya kusafishia vidonda kama geresha, ili tu aonekane alikuwa na dhamira ya kumkagua huyo mama vidonda na ikibidi kumsafisha.

Akatoka na sinia akiwa kaweka mkasi, pamba, na dawa za kusafishia, ….

Alipofika kwenye kitanda cha huyo mama anayemtaka yeye,….alimkuta huyo mama kalala, inaonekana alishapewa dawa ambazo akizinywa mgonjwa, hupatwa na usingizi.

‘Mhh, sasa naweza kulifanya zoezi langu bila wasiwasi….’akasema moyoni.

Taratibu akamsogelea yule mama pale alipolala kitandani, wakati anamsogelea akawa anamtizama kwa makini, kama kuna lolote analoweza kuliona la kumkumbusha siku za nyuma kuwa ndio yule mama wa wakati ule au anamfananisha tu, lakini haikuwa rahisi, kwasababu huyo mama kalala, na kajifunika shuka, toka miguuni hadi shingoni, na kuacha sehemu ya kichwa tu. Na kichwa kavaa kile kitambaa cheusi…kama vijana wa mitaani wapendavyo kuita `ki-ninja’ kavaa kininja

Kuna mtu alimletea huyo mama kitambaa kizuri tu cha kujifunika kichwani, ambacho kinamuwezesha kupata hewa bila shida,…nesi alipokumbuka hilo neno la `ninja’ akacheka, kweli huyu mama anaonekana kava kama ninja-mwafrika….na hafanani kuwa kavaa hivyo kwasababu ya imani ya kidini, anakumbuka aliwahi kumuuliza na huyo mama, alisema anavaa tu maana ndivyo wanawake wanatakiwa kuvaa hivyo.

‘Ni kutokana na imani yako ya dini au?’ akamuuliza

‘Kila mwanamke anatakiwa kuvaa hivi, na kuvaa hizi  sio swala la imani peke yake…kwanza kwanini unapenda kuniuliza uliza maswali kuhusu mavazi yangu..’akasema kwa ukali na toka siku hiyo nesi hakupenda kumuuliza uliza tena maswali ya namna hiyo..

‘Lakini kama ni kwa ajili ya imani yake ya dini, mbona sijawahi kumuona akiswali,…au kwa vile ni mgonjwa..sijui,..labda ni imani yake,..lakini nahisi kuna kitu anaficha huko usoni, lazima nikione hicho anachokificha……mmh naogoapa kumuuliza tena maswali maana siku ile alinijibu kwa hasira…ngoja leo nijione mwenyewe….’akawa anajisema akimsogelea karibu.

Alipofika pale kitandani, akasita kidogo, nia yake ilikuwa amfunue kile kitambaa alichojifunika usoni…lakini kuna mawazo yakawa yamsuta, akikumbuka wale waliowahi kufanya hivyo, walivyokuja kupata taabu,…hata hivyo akaona ajaribu tu…yeye haamini hayo mambo , kwanza yeye ni nesi mkuu, anatakiwa kuhakikisha mgonjwa yupo salama…

Taratibu akausogeza mkono wake….taratibu hadi ukafikia ncha ya kila kitambaa, kilikuwa cheusi cha kama hariri, sehemu ya macho pua..ni nyepesi zaidi..na sehemu nyingine kichwani kipo kama kofia, na mahususi kwa wale wanawake wenye imani yao ya dini…lakin nesi hakuwa na uhakika kama kweli huyo mama anavaa hivyo kwa ajili ya imani ya dini. Akakumbuka yule aliyemletea hilo vazi, alivyosema;

‘Nimemuona yule mama anapenda kuvaa ‘nikabu’ naona ana imani thabiti na dini yake..’akasema mama mmoja,

‘Mhh, hata hatujui, na hapendi kuondoa ile nguo yake aliyojifunika …’akasema huyo nesi

‘Basi mimi nitamletea vazi sahihi, linaitwa ‘nikabu…’ asijifunge ile nguo..naona imeshachakaa, imeungua ungua..…na haipo sahihi….’akasema huyo mama na kweli siku ya pili akamleta huyo mama hilo vazi, na yule mama akalipokea, na hakubadili hapo hapo, alikuja kubadili kwa wakati wake.

Basi nesi mkono wake uliposhika sehemu ya lile vazi,ili alivute kwa juu, akashangaa kuona mkono wake unatetemeka,…sijui kwa woga…au, na hakujua kwanini mkono unamtetemeka vile wakati hiyo ndio moja ya kazi zake. Na pia moyo ulikuwa mzito kufanya alichotaka kukifanya,k wani moyoni alikuwa akijisuta kuwa anachotaka kukifanya pale sio taratibu zake za kikazi,…

Taratibu zake za kikazi, ilitakiwa kumwamsha mgonjwa kwanza…amueelzee ni nini anachotaka kukifanya…, akakumbuka jinsi wagonjwa wanavyolalamika kuwa hawatendewi haki, ..na yeye ni kiongozi anatakiwa kuhakikisha haki za wagonjwa zinatimilizwa,..na akionekana na yeye anakiuka hizo haki na ikafika kwa wakubwa si ndio atazidi kujiaharibia kazi na kuonekana kumbe kweli yeye alifanya hicho anachodai huyo mama,kitu ambacho sio kweli…

‘Aaah, nitajua la kujitetea, kwanza mimi ni nesi mkuu, nina wajibu wa kuhakikisha utendaji wa manesi upo sahihi….ngoja nimtizame kidogo..’akasema huku, akakivuta ile sehemu ya vazi kwa juu, akaona inavutika, taratibu, halafu….

Alishituka ghafla mkono wake umedakwa, na kabla hajasema neno, ukaachiwa mara moja…!

Alishangaa sana, jinsi huyu mama alivyokuwa mwepesi kuulinda uso wake, utafikiri hilo vazi la kitambaa, ni shemu ya mwili wake. Nesi alishituka karibu adondoshe vile vyombo alivyokuwa amebeba vya kusafishia vidonda.Na akajikuta anayatizama macho ya yule mama, ambaye naye alikuwa kamkodolea macho.

Kwa ukaribu ule aliweza kuona yale macho, maana sehemu ya mcho kuna uwazi ..na akayaona macho ya yule mama yakipepesa…macho….

‘Mhh huyu mama kumbe ana macho mazuri hivi…sijui sura yake ipoje…’akajikuta akisema kimoyo moyo…

‘Mcho yake kama ya wazungu, yana rangi ya kibuluuu, makubwa, na nyusi nyingi…..mmh, ningekuwa na macho yenye mvuto kama haya, …’ akajikuta akijisemea moyoni, huku akitamani kuyatizama yale macho.

‘Kwani unataka kufanya nini..?’ mgonjwa akauliza

‘Oooh, samahani, upo macho, mimi nilidhania umelala…dawa hazijafanya akzi yake nini…?’ akasema nesi.

‘Nilipitwa na usingizi, mmmmh, mimi naona nimepona huku usoni, hakuna haja ya kunisafisha tena, sipendi watu kuniangalia uso wangu…’ akasema yule mama.

‘Hebu nikuulize tena mpendwa wangu…., kwanini unaficha huu uso wako, …ni imani au,…kama ni kwa ajili ya imani yako, sawa, …nijuavyo mimi, sijui kama nakosea, hapa upo ndani ya hospitali na hii ni wodi ya wanawake watupu, unaogopa nini…ndivyo imani yakoo inavyokuagiza hivyo kweli..?’ nesi akaona aanze kutafuta ugomvi tena.

‘Mhhh, naona mara ya  pili unanidadisi kama sikosei au sio wewe…aah, kumbukumbu haziji, sijui kwanini.., na…na..sio imani kufanya hivi, jana mwenzako karibu anikimbie nilipofunua uso wangu…sipendi kuwatisha watu kwa uso wangu ulivyoharibika kwa kuungua na moto, na wamenichana na mapanga…’ akasema huku akijifunika vizuri.

`Ina maana unafanya hivyo kwasababu ya kuogopa hayo majeraha au…kwani moto uliunguza uso pia…, au kuna jingine lilitokea…?’ nesi akamsogelea ili asikie vyema.

‘Mhh, …sikumbuki vyema, ..lakini nahisi…nilipokuwa nakimbia nguo ilinitoka nikadondokewa na kitu chenya moto, kikaniungza usoni…kwenye majeraha waliyonikata na mapanga…sikumbuki vyema…sijui ndio hivyo…’akasema

Nesi alishangaa kumsikia huyu mama akiongea kwa utaratibu mnzuri sio kama siku zilivyopita…, kwani alivyofika hapa mara ya kwanza huyu mama alikuwa haongei sana, na madakitari walishauri asisimbuliwe na maswali mengi, kwani anaweza akaathirika kisaikolojia…kuna muda akiona watu wanamshangaa kuhusu uso wake alivyojifunga, basi anatafuta jinsi ya kujificha hata kujifunika gubi gubi na shuka…!

`Inaonyesha sasa unaanza kupona, maana mara ya kwanza ulikuwa huongei sana ukiulizwa wakati mwingine unakuwa mklai sana…’ akasema nesi

‘Kweli kabisa, na nahisi kama vile nimefufuka kutoka kwa wafu..’akasema na nkauli hiyo ikamfanya nesi ashituka

‘Kafufuka kutoka kwa wafu…’ akawa anayarudia yale maneno akilini

‘Yaani hapa najiona kama, akili ilizibwa, kama mtu alikuwa ndani ya maji, maji yakaingia msikioni.. unasikia ndiiiii, akilii inakuwa kama ina giza, na kila mara kunakuja kitu kama kinataka kuzibua ganda lililoganda ndani..sijui nikuelezeje…’akasema

‘Usijali hayo ni maendeleo mazuri, naona sasa unapona..’akasema nesi.

‘Na…na, na sijui kuwa nilikuwa wapi, na nipo wapi…mmh, umesema, aah, hapa ni hospitali eeh, …hivi hapa ndio hospitali ehe, wapi, hapa panaitwaje?’ akauliza yule mama. Nesi hapo akamuangalai tena yule mama, sasa akianza kuingiwa na wasiwasi, maana mwanzoni alikuwa akienda vyema, lakini hii kauli ya sasa inatia mashaka…akasema;

`Hii ni hospitali ya mkoa, na uliletwa hapa ukiwa umeungua na moto…na majeraha ya kukatwa katwa na mapanga’ akasema nesi.

Kwenye hicho chumba kulikuwa na mgonjwa mwingine, mgonjwa huyo naye alikuwa kaunguza sana..sasa alishaanza kupona. Na yule mngonjwa mwingine akawa anawaangalia wanavyoongea nesi na huyo mama.

Yule mama mwingine,akahisi yule mama kama anafuatilia yale anayoongea na huyo mama,…mpaka nesi akashuku jambo, ikabidi amtizame vyema yule mama, na yule akashituka na kugeuza kichwa chake kuangalia juu, sasa akawa kachukua simu yake akionekana kama anabonyeza bonyeza

Nesi akawa kashuku kitu, kwa huyo mama mwingine, akawa haongei tena na huyu mama aliyekuwa na matatizo naye, akawa anamchunguza yule mama mwingine na kila akimchunguza yule mama mwingine, moyo akamuona kama anafanana-fanana na yule mama aliyeletwa kipindi kile, umbo, na sura…na yeya alinguza karibu mwili mzima..uso umebadilika,…yeye hajifuniki, anaachia uso wake kama ulivyo….

‘Yule mama kama angedai kuwa ndiye yule mama aliyekuja kipindi kile ningehisi vinginevyo maana ninavyokumbuka yule mama alifanana vile vile…’akawa anasema kimoyo moyo moyo.

Nikimalizana na huyu nitakwenda kumuulizia, maana anafanana sawa kwa sawa…huenda akawa ni ndugu yake yule mama ….ngoja nimalize na huyu hapa! Akagutuka toka kumtizama yule mgonjwa mwingine, aliposikia huyu mama akimuuliza swali, kama vile anatoka usingizini…!

‘Unasema niliungua na moto, niliungua na moto, wapi nilipoungulia, sikumbuki…sikumbuki…kichwa kinaniuma,…kwanini kinauma hivi…, ilikuwaje mpaka nikaungua…?’ akauliza huku anashika kichwani, kuonyesha kuwa ana maumivu makali. Na nesi akachukua dawa za kutuliza maumivu na kumpa.

‘Kunywa hizi hapa dawa, ulikuwa hujapewa dawa zako za maumivu ….’akasema alipona kumbe kweli dawa za maumivi hajapewa.

 Na yule mgonjwa alipomaliza kumeza zile dawa , akawa kama anataka kujifunua kile kitambaa, lakini akasita…baadaya akawa kimia.

‘Umelala..?’ nesi akamuuliza, na hakupata jibu nesi akajua huyo mgonjwa ameshalala, akaona ajiondokee zake

Nesi…akapanga atakuja kumuhoji huyo mama mwingine wakati mwingine, aliona muda huo sio wakati muafaka wa kumhoji zaidi, lakini alihisi kuwa huyu mama hafanani kabisa na yule mama aliyekuwa na mtoto akafariki, aheri angelisema yule mama mwingine

Akageuka kumtizama huyo mama vyema alivyojilaza pale kitandani, na moyo wa huruma ukamwingia akifikiria unyama wa wanadamu, kama kweli alivyosikia ni kweli basi wanadamu sio wema, wanadiriki kumteketeza mama wa watu kwa imani za kishirikina! Wanamkata kata na mapanga halafu bado hawakutosheka, wakamuunguza na moto…hata huyo mama mwingine aliyeletwahapo alikuwa na masahibu hayo hayo….kweli dunia …kweli wanadamu hawana huruma tena..imani tu, hisia tu…mmh ni hatari.

Wakati anageuka kuondoka, mara akasikia huyu mama akisema maneno yaliyomshitua kidogo …

‘Jana niliota ndoto ya ajabu sana… , na sijui inamaanisha nini, …nahisi kuna mtoto, nina mtoto…nahisi  niliwahi kuwa na mtoto, nahisi yupo mtoto… hata nikigusa tumboni langu upande huu… naona kama..nilifanyiwa upasuaji..eeeh,…sasa mtoto wangu yupo wapi…’akawa kama anauliza

‘Hiyo ni ndoto tu mpendwa…wewe lala dawa ifanye kazi…’akasema nesi baada ya kitambo kidogo.

‘Mhh, natamani sana niiote tena hiyo ndoto, maana naona kama inanionyesha njia, na kunifunulia jambo lililojificha…kama nina mtoto yupo wapi, mimi ni lazima nimpate..’akasema

‘Oh, nesi, naomba uniache nilale…., kwani kichwa hakinipi raha, kinakuwa kama kina mawingu, kinazibuka na kuziba, nakuwa kama nakumbuka mambo emngi kwa wakati mmoja, hata sijui nipo wapi…, au sijui…aaah..ngoja…ni-la-le…’ akalalamika halafu akatulia. Na yule nesi akachukua vifaa vyake na kuanza kuondoka huku akiwaza alichosikia kwa huyo mama.

‘Amesema , nahisi `kuna mtoto’ sio `anahisi kuwa ana mtoto’ au sikusikia vizuri…akaongezea maneno kuwa `nahisi yupo..’Huyu mama kachanganyikiwa, lakini kama kweli ana alama ya upasuaji huenda aliwahi kuwa na mtoto, sasa sijui huyo mtoto wake yupo wapi…mimi nahisi huyo mtoto atakuwa kwa ndugu zake, au…alishakufa…sijui…kwa hali kama hiyo sizani kama ndugu watakubalia abakia na mtoto…’nesi akawa anawaza.

‘Mhh, naona …akili zake zinamrudia na kumvuruga kabisa, inabidi nimuambia docta kuhus haya ambadiliko…na mimi nataka akili yake ikiwa sawa, nikae naye nimdadisi vyema, ataweza kunisaidia kuondokana na hizi shutuma za hawa mabosi ambao wanataak niongee yale nisiyotakiwa kuyaongea

‘Mhh, mungu wangu nisaidia, maana hayo yalishapita….’akasema huku akikunja uso kwa huzuni.
‘Mungu wangu…usiniache nikaabika…sio kuaibiak tu, naweza kuishia jela..aheri wahusika wangelikuwepo…sasa hawa mabosi wangu wananishuku vibaya…wanataak niongee iliyokuwa siri…hapana, hata iweje siwezi kuiongea hayo yaliyopita..siwezi kamwe….’akasema akiondoka kwenye hiyo wodi maalumu.

Akiwa anatembea kuelekea kwa docta, akasimama akashiak kichwa

‘Nahisi kichwa kinauma ghafala…labda ni uchomvu…aah, nahis ni kuchoka, ngoja nikapumzike nyumbani…!’ akasema na kugeuka hakutaka kwenda tena kwa huyo dakitari.

‘Mhh, hata hivyo nilitakiwa kufuatilia yale maswala ya kumbukumbu za yule mama aliyekuwa na mtoto…’akasema

‘Mhh, na huyu mama mgonjwa naona mabadilio yake yananipa mashaka mengine..sasa hanidai mimi mtoto, anadai alikuwa na mtoto…. kutoka kudai mtoto na kusema mtoto wake atakuwa mahali fulani, sasa hivi hamnyoshei yeye kidole…anaongea ongea yasiyoyoeleweka….naona sasa haitakuwa na haja sana ya kuumiza kichwa kuhusu kumbukumbu za yule mama, za nini kwanza, huyu mama atakuja kujielezea mwenyewe mtoto wake kamuacha wapia…!’akawa anaongea peke yake. Na mara akasikia akiitwa

‘Sister, simu yako inaita huku njoo haraka…’ akasikia mwenzake akimuita na akakumbuka kuwa aliiacha simu yake kwenye chaji na hakuizima, akakurupuka mbio akijua simu hiyo inaweza ikawa ya muhimu sana. Huenda inatoka kijijini na hajaongea na ndugu zake wa huko kijijini kwa muda mrefu..na alitaka kujua maendelea ya mtoto na wazazi wake.

 Alipofika sehemu ilipo simu yake, akaikuta imeshakatika, akatizama ile namba akaona ni namba ya nchi za nje..

‘Daaaah...nani huyu kanipigia toka nchi za nje…nani ,jamani, naomba apige tena, …’ akatizama salio lililopo kwenye simu lilikuwa halitoshi kabisa kupiga simu ya nje, akaangalia pochi yake na kukumbuka kuwa hana pesa za kutosha kununulia vocha ya kuongea nchi za nje.

‘Mhh tarehe mbaya hizi..pesa hakuna..’akalalamika

‘Maisha haya, mshahara hautoshi ….hata sijui nitawatumia nini huko kijijini, sasa ningelikuwa naishi na huyo mtoto sijui ningefanyaje, aheri ndugu zangu wamemchukua…’akawa anaongea peke yake huku akichukua simu yake kwenye chaji.

‘Na hii namba ni ya nani…mhh, hata sijui….’akasema huku akiiangalia kwa makini.

‘Basi tena kama ni mtu muhimu atanipigia…sina jinsi nifanyeje…’ akairudisha simu yake tena kwenye chaji..maana aliona haijajaa..lakini akakumbuka kuwa anataka akajipumzishe nyumbani kidogo, nyumbani kwake sio mbali sana na hapo hospitalini,  

Akainama kiuchukua ile simu na mara akakumbuka jambo…akaitizama ile namba tena, akatabasamu, ….

‘Mhh atakuwa ni yeye nini….hapana, hii namba ni ya nchi gani..’akawa anajiuliza

‘Ni lazima nitafute pesa hata kukopa nipige hii namba hata nisikie tu ni nani, halafu hata ikikatika najua huyo mtu atanipigia…’akasema na kuichukua simu yake na kutoka nayo nje…


WAZO LA LEO: shida zinapotushika, matatizo ya kiuchumi, maisha kutuelemea, tusikate tamaa, tuzidi kujibidisha katika shughuli zetu za kutuapatia riziki iwe ni sehemu zetu za kazi, au biashara au shambani…na kamwe tusiingiwe na tamaa ya kufanya yasiyostahili kama kuiba ,kugushi  na mambo mabaya ysiyostahiki, …tukumbuke kuwa shida na matatizo ndio ngazi ya kutupeleka juu, ndio chachizo la kutufanya tufanye bidii au kutafuta njia mbadala au nama nyingine ya kupata maendeleo, lakini hala hala njia hizo ziwe za halali..pambana kihalali, na utapata faida yenye manufaa. Wito, Tusikate tamaa, tutafanikiwa tu…
Ni mimi: emu-three

No comments :