‘Sasa nesi nilichokuitia hapa ndio hicho,
ila kwanza wewe mwenyewe uonyesha upo tayari kwa hilo…na hatua ya pili, ambayo
sio shida sana, ni kubadili kila kitu, hilo sio tatizo kwangu…’alisema dakitari
mkuu.
‘Unaona, nia ni kuonyesha kuwa huyo mtoto
hakuzaliwa hai kwa huyo mama, maana mama mwenyewe hayupo..keshafariki…
,’akasema na kumuangalia nesi, nesi ambaye alikuwa katoa macho ya kutoamini
hicho anachosikia.
‘Na nesi kama ulivyosema, dada yako alikuwa
akihitajia sana mtoto au sio, mungu kampa mtoto kwa njia rahisi tu, lakini
urahisi huo unategemea na wewe mwenyewe,kwahiyo ukikubali basi, dada yako ndiye
mama halali wa huyo mtoto, je wewe unasemaje,…kwanza upo tayari kwa hilo?’
akaulizwa, nesi ambaye alikuwa akimuangalia huyo mkuu bila kummaliza akajikuta
akisema;
‘Nipo tayari kwa vipi?’ akauliza nesi
akiwa katahayari, haamini,…mkuu ambaye anafahamika kuwa ni mtu asiyetaka
uzembe, mkali kwa mambo yasiyofuata sheria, japokuwa ana mapungufu yake ambayo
nesi mara nyingi alikuwa anaona kama wanamsingizia tu,.. leo hii anatakamka
hayo mbele yake…, hakuamini, akawa hata haelewi…kumbe ni kweli…mhh!.
Lakini hata hivyo kwa hali ilivyo hakuwa
na la kufanya, kwanza alijiuliza hayo yote yanafanywa kwa ajili yake, na
familia yake kwa malipo gani, ina maana kuna kitu atatakiwa kukifanya kufidia
hayo, au….akasubiria jibu la mkuu wake…
Jibu ambalo lilimuweka njia panda,…lakini
alipotajiwa kwendqa kusoma, ooh, akawa kaswajika, na ndio ukawa mtego wake… na
kilichotokea ni kujitoa mhanga..kwa ajili ya mtoto, kwa ajili ya ndugu zake,
ambao walishajua kuwa huyo mtoto ni wao…,
Sasa leo siri ya miaka hiyo siri iliyojificha
na yenye mambo mengi, siri ambayo akiikumbuka inamtonesha moyoni, na kumpa
wakati mgumu…siri ambayo ilitakiwa iwe siri…inahitajika kujulikana….itakuwaje?
Tuendelee na kisa chetu
***************
Nesi akiwa kazama kwenye mawazo, na maneno yenye kumchomo moyo
yakawa yanasikika masikiono mwake kwa sauti ya kuwewesa…..
‘Nesi …umesikia, wewe sasa kula maisha, ukiwa na mimi usipate
shida….unaonaeeh, sasa unakwenda kusoma, ila kumbuka; …..’ hiyo ila kumbuka
ikamfanya ajaribu kukatisha hayo mawazo, lakini sauti ile bado ikawa na nguvu
kichwani
‘Nesi…hakikisha siri hii inakaa moyoni mwako, maana ikijulikana tu,
mmmh, umeniharibia kazi..na ama kwa mwengu anaweza kukufanyia visa ukafungwa na
kupotelea jela..ujue nesi mimi nimeyafanya haya kwa vile nakupenda,…eeh, umeona
mpenzieeh… ‘ sauti ikazidi kupenya masikioni mwake, huku machozi yakianza kumtoka.
Akasimama na kushika kichwa na kuziba masikio, lakini wapi…sauti ile ikawa
inajirudia, …..
‘Siamini..kwanini mimi…’akawa analia, baadaye akatulia, akajiuliza
analia nini, maana hayo yalishapita, hata akilia machozi ya damu hayo yalikuwa
yameshafanyika, ni kama kutamani maziwa yaliyomwagika ardhini na kunywea
mchangani…
Sasa akatuliza kichwa na
kuanza kuingia kwenye hali halisi akajiuliza;
‘Je nilifanya makosa,..ndio ni makosa, lakini kulikuwa na njia
gani nyingine ya kuepuka na lile tatizo…sikuwa nalo, sasa…..’
Kiukweli siku ile alijiona kama msaliti, pamoja na kuwa hakufanya
hivyo kwa ridhaa yake, maana ilikuwa ni kuona huyu kanifanyia hivi nitamlipa
nini, na pia, na kwa ajili ya mtoto, ni kwa ajili ya dada yake…akajuta , lakini
majuto yakawa na mjukuu
‘Nimeshamsaliti niliyempenda..’akasema, hata hivyo akajiuliza huyo
aliyempenda kweli na yeye anampenda hivyo hivyo…`aaah, hata sijui, …imebakia
kuwazia hivyo, tu maana yupo moyoni mwangu namuwaza yeye kila siku, japokuwa
kaondoka hata bila kuniaga….sasa huyu mtu kanitega, nimekusaliti mpenzi ,
usiyependeka…nisamehe…’
Mara ile sauti ya kukera ikasikia masikioni mwake tena,
..ikiwewesa, ikawa na harufu ya ulevi, ikasema;
‘Unasikia nesi, …kama ningeliachia hili liende inavyotakiwa
kisheria, basi ujue wewe ungeishia jela, ungefungwa, unaonaeeh, lakini
sikukubali, kwa vile mapenzi yangu kwako ni makubwa, …huyu aliyekudanganya yupo
wapi, fimbo ya mbali hata siku moja haiwezi kuua nyoka…’kauli yenye kukera
ikapenya ubongo wake
Na alikumbuka kuwa alitaka kumuambia kuwa yeye atapenda wangapi
maana kauli kama hiyo kaeshaitamka kwa manesi wengi waliowahi kutembea naye.
‘Na ujue nesi hapa hospitalini, wewe peke yako ndiye ninayekupenda
sana…wengine wanajipitisha tu kwangu, siwataki kabisa….unaona kama
ingeliwezekana kuoa mke mwingine ningekuoa wewe, lakini imani yangu haitaki
hivyo…’akasema
‘Lakini unazini je imani yako inataka uzini..?’ akamuuliza, lakini
hakupata jibu, alisikia maneno mengine tofauti
‘Na ninachokupendea zaidi ni kuwa wewe ni mtu mwenye huruma
sana..na kwahiyo usingelipenda mtoto kama yule aje kuteseka….’akasema sijui hakusikia
swali lake au alifanya hivyo kupotezea.
‘Na pia, umesikia mwenyewe alivyosema yule mkuu wa kituo, yule
namuamini sana tuna mambo mengi mimi na yeye..unakumbuka alivyosema…, kasema
familia ile anapotoka huyo mtoto, alipokuawa kaolewa huyo mama, ni familia
yenye maisha magumu…sasa utafurahi huyo mtoto aende kuteseka…unaona kwahiyo
umefanya maamuzi sahihi…usihuzunike kwa hili, naomba ubadili muelekeo na
kunipenda mimi tu…’akasikia sauti hiyo ikiendelea kupenya kichwani.
‘Nitakupendaje na wewe una mke wako, na imani yako haitakia kuoa
wake wawili..?’ akauliza na hata hilo swali halikupatiwa jibu, ni kama anaongea
na kitu kilichorekodiwa kazi yake na kuongea yale yaliyomo tu….
‘Sasa mimi na wewe ni kitu kimoja na sitakuangusha…kesho utaondoka
kwenda chuoni, ..ukirudi hapa aaah, wewe ni bosi, na tutakuwa karibu
karibu,..unaonaeeh, haya ndio maisha…mke wangu hana shida, hatufuatani yeye ana
maisha yake na mimi yangu…’sauti ikizidi kumkera akilini
Alipokumbuka hilo tukio, na maneno hayo yakipenya kichwani kwake,
akahisi kichwa kinamuuma, akahisi kichefu chefu, anakumbuka siku ile alipotoka
pale, alikimbilia maliwatoni akatapika sana…alitapika mpaka nguvu
zikamuishia..na toka siku ile kila akikumbuka lile tukioa, akawa anahisi
kutapika,..kichefu chefu… ingelikuwa ni mtu ambaye sio mtaalamu angelihisi ana
uja uzito.
************
Nesi akijaribu kuziondoa hizo kumbukumbu kichwani, alitoka mle
ofisini na kupita chumba cha huyo dakitari bingwa ambaye kwa kipindi hicho pia,
alishikilia nafasi kuu kama kiongozi wa hospitali, akajua hatima ya maisha yake
imeingia kwenye mtihani mwingine, kwa matu kama yule yule…
Ni kweli ulikuwa ni mtihani, mtihani ambao unaweza kuwa kama ule, japokuwa
sasa anajiamini, hawezi kuingia kwenye mtego mwingine, mwenye akili hafanyi
makosa mara mbili, …
‘Sasa nitafanyaje, na nianzie wapi…’nesi akajiuliza swali,
akakumbuka moja ya mafunzo yake kuwa unapojikuta kwenye wakati mgumu wa kufanya
jambo, kitu cha kwanza ni kukaa chini na kulitafakari hilo jambo,kama kuna muda
wa kufanya hivyo, weka mipango, na mikakati..ikibidi andika utaratibu hatua kwa
hatua…kama hakuna muda, chukua hatua na matokea yatakupa muelekeo ulio sahihi…
Kwanza akahakikisha majukumu ya watu yamekamilika akapitia kwa
wagonjwa na kuhakikisha kazi zinakwenda sawa, akatizama saa yake akaona ni muda
wa kuanza uchunguzi wake, …kwanza akachukua karatasi, na kabla hajaanza
kuandika kitu, akakumbuka jambo, ..
‘Oh, kweli,..anaweza akanisaidia, anaweza akakumbuka ngoja niende
kwake..’akasema na haraka akaacha kila kitu , akatoka pale ofisini na kwa
haraka akakimbilia ofisi ya madakitari wa kawaida,..ambappo wagonjwa wengi
hutibiwa hapo, hakujali wingi wa wagonjwa, yeye moja kwa moja akaingia kwenye
chumba cha dakitari huyo aliyemkumbuka kichwani.
‘Vipi nesi mbona waingia bila hodi..’akaulizwa na dakitari huyo ambaye
kwa muda huo alikuwa akihudumia mgonjwa.
‘Samahani sana docta, kwa hili, limenifanya niwe kama
mwendawazimu, hata sijijui nafanya nini, ..’akasema nesi akiwa kasimama
mlangoni na yule dakitari mtu mnzima, kutokana na hekima za utu uzima wake
akamuelewa huyo nesi, akasema;
‘Basi ngoja nimtoe huyu mgonjwa,…’akasema huyo dakitari ambaye ishara
za uzee zilishatanda kichwani mvi, na uonekanaji, kijumla alionekana kuwa ni
mtu mzima, na huenda pale kazini ndiye dakitari mwenye umri mkubwa kuliko wote,
na wagonjwa wengi wanapenda kuingi kwake kwa vile pamoja na utaaalmu wake,
lakini pia ni mzoefu wa magonjwa mbali mbali,na anajua jinsi gani ya kuongea na
mgonjwa …
Alipomaliza kumuhudumia yule mgonjwa, nesi akasogea na kukaa kile
kiti cha wagonjwa na kumuangalia huyo dakitari,..mawazoni akakumbuka siku
dakitari kijana ndio kwanza amefika hapo hospitalini na kutambulishwa kwake
kuwa yeye atashirikiana naye katika utendaji , akambiwa yeye ndio atakuwa nesi
wake wa karibu…na kuna siku walikuwa wakipata chakula pamoja, akiwemo huyo
dakitari na dakitari kijana akiwa pembeni…, na huyo dakitari alisema kiutani;
‘Nyie mnafaa muwe mke na mume….’ Na kauli hiyo iliwafanya wacheke,
maana ilikuwa ni mwanzoni tu, na hakuna aliyekuwa akifahamu undani wa mwingine,
ndio kipindi dakitari kijana amefika hapo hospitalini na hana mazoea kabisa na
huyo nesi zaidi ya kuambiwa kuwa ndiye atakayekuwa nesi wake kwa kazi mbali
mbali za hapo.
Nesi alipokumbuka hivyo akasema kimoyo moyo;
‘Oh… kama dakitari kijana angelikuwepo hapa leo ningeliweza kupata
msaada mkubwa, sijui nitampataje huyu dakitari…maana hata sina mawasiliano naye
tangu aondoke. Huenda keshanisahau, huenda keshaoa mzungu..’akajikuta akiwaza
hivyo
‘Mhh natamani sana niisikie angalau sauti yake, kwenye simu,
mmmh…., lakini..hio sasa ni kama ndoto na hili tukio mmmh, naliona ni langu
peke yangu..aheri na mimi ningelipata uhamisho a kwenda sehemu nyingine….,
lakini hata hivyo hapa nimepazoea sana…!’ Akawa anawaza akimuacha yule dakitari
amalizie kuandika kile alichokuwa akiandika baada ya kumaliza kumhudumia yule
mgonjwa aliyetoka.
‘Docta mimi nina shida kubwa sana, na wewe pekee ndio naona utanisaidia….’akasema nesi, na huyo dakitari
akawa katulia akimuangalia huyo binti usoni, na huyo binti akaendelea kusema;
‘Docta, nakumbuka sana wewe
ndiye uliyenipokea hapa nikiwa bado kabinti…’akasema nesi akitabasamu, na huyo
dakitari akacheka na kusema;,
‘Hahaha unanikumbusha mbali kweli, …Ni kweli, nakumbuka kipindi
chenu waliingia manesi wengi wadogo wadogo, unajua kipindi chenu, mnaajiriwa
mabinti wadogo sana..nakumbuka wewe ulikuwa bado unadeka, unakumbuka kudekezwa
na wazazi wako, jambo dogo tu unalia, umeacha kule kulia lia kwako..’akasema
dakitari akiendelea kucheka.
‘Hapana docta,… acha utani wako, nilikuwa siliilii ovyo, siunajua
tena ujana, utoto…na ilikuwa mara ya kwanza kuajiriwa…hahaha, eti nilikuwa
nalia lia..hapana bwana unavumisha sasa…tuache huo utani docta…, nisikupotezee
muda wako pia, mimi nauliza, hapa zamani kulikuwa na makabati makubwa ya
kuhifadhia kumbukumbu,..hivi wewe unaweza kukumbuka yalipelekwa wapi, na
kumbukumbu zake?’ akauliza.
Ni kweli hiyo ofisi
anayotumia dakitari huyu huyu kwasasa haikuwa hivyo kabla…kipindi hicho ilikuwa
ni sehemu kubwa, na kulikuwa na makabati makubwa…, lakini sasa imeshafanyiwa
ukaratabati, na kugawanywa kuwa ofisi ndogo ndogo za madakitari…
‘Mhh, kwanza ya nini,…. pili unanikumbusha kitu, maana hata mimi
kuna muda nilikuwa nahitajia nyaraka zangu, unajua ilitokea kama mshitukizo,
mara ofisi zinafanyiwa ukaratabari, tukahamishwa huku na huku…hapa sasa
kulikuwa kukubwa eneo lote hili, ..kulikuwa ni kama sehemu ya kuhifadhia
kumbukumbu, kulipangwa makabati makubwa tu….mara makabati yakatolewa, sisi wala
hatuna habari…unajua sisi tulikuwa tunatumia ofisi zile kule za jengo hilo la
sasa ambalo limefanywa kuwa jengo la wagonjwa maalumu…’akasema
‘Nani alifanya hivyo..yaani nani alisimamia hilo zoezi la
kuhamishwa hizo kumbukumbu, maana
nijuavyo hizo kumbukumbu ni muhimu sana, na ilitakiwa kuwepo dakitari wa
kusimamia…unajua mimi hayo yakifanyika nilikuwa sipo, nilikwenda kusoma?’
akauliza nesi
‘Mhh, sijui kama kulikuwa na mtu wa kusimamia..wenyewe utawala
wanajua walichokifanya…basi, yalitokea
mambo ya ajabu kweli, maana sisi ndio tunaoweka kumbukumbu zetu muhimu, tunajua
umuhimu wake…sasa wanakuja watu wengine wanajifanya wamesoma wanataratibu mpya
za mitandao, komputa sijui..basi wewe..ikawa ni karaha..muda gani utaweza kujua
kipi ni kipi ukihifadhi kwenye komputa..walioweza wakafanya hivyo, na wengine
wakaacha kama ilivyo…
‘Basi yale makabati yakebebwa, ..ujanja ujana tu, wenyewe
waliyataka yale makabati kwenye hospitali zao, wakayachukua kwa kisingizio cha
kuchakaa, wakajifanya kupiga manada… hata bila sisi tunayoyatumia kupewa
taarifa…’akashika kichwa
‘Sasa inafika muda unakumbuka kitu unakwenda kuangalia …oh,
unakuta ofisi inavunjwa kuna ukarabati ukiuliza, unaambiwa kamuone mtunza
store,..na mtunza store naye atahangaika weee, kama kakipta sawa, kama
hajakipata ndio basi tena…kumbukumbu zikapotea…’akasema.
‘Sasa kuna kitu nataka kukifahamu, ni muhimu, unakumbuka katika
kazi za upasuaji wagonjwa, kuna kipindi kile alikuwepo yule dakitari
kijana,..’akasema
‘Hahaha..unasema oohm, nimekumbuka yule handsome boy,….yule si alikuwa mchumba wako bhana…, hivi hamkuwahi
kuvishana pete, maana aliondoka ghafla, ilikuwaje?’ akauliza huyo dakitari
akitabasamu.
‘Aaa, docta achana na huyo mtu,…mimi nataka urudishe kumbukumbu
zako kipindi kile….. , unakumbuka kuna mama mmoja alifikishwa hapa hospitalini,
wewe ulikuwa kule kwenye kitengo cha upasuji…huyo mama alifishwa akiwa na hali
mbaya, akafanyiwa upasuaji, na aliyeshiriki alikuwa huyo dakitari kijana…na
ikawa ni ama mtoto au yeye, lakini kwa bahati wakapona wote, unakumbuka hilo tukio?’
akaulizwa
‘Mhh, mbona hayo matukio yalikuwao mengi..sasa sijui ni lipi kati
ya hilo,…?’ akauliza.
‘Yupo mama mmoja, ambaye baadaye alitoroka…hukumbuki tukio kama
hilo?’ akaulizwa
‘Nakumbuka kuna matukio kama hayo wagonjwa wanakuja kutibiwa na baadaye
wanatoroka, unajua mimi nilikuwa kama dakitari msaidizi tu, na kawaida yangu
hata ya kimaisha, huwa sitilii maanani sana mambo yasiyonihusu…na kawaida yangu,
nikimaliza kusaidia kazi fulani narudi huku kutibia wagonjwa mambo ya huko
nayaacha kama yalivyo…maana huku ndio ofisi kwangu mimi ni dakitari wa amgonjwa
yote,…siunajua hilo…, japokuwa tulikuwa hatutumii ofisi hii, maana haikuwepo ,
tulikua kulee….’akasema akionyeshea kidolee
‘Doctaaa…hebu jaribu, kukumbuka bwana…kuna mama mmoja bwana…
alikuja kuleta taabu kweli,..alitoroka… mpaka polisi wakaitwa wakafanya
uchunguzi ….maana tulijua kuwa kapoteza fahamu na hauenda asizindukane..kwa
hali aliyokuwa nayo..lakini cha ajabu akazindukana na kutoroka, na hakupatikana
na baadaye wakasema kafariki..’akasema
‘Aaah, nimekumbuka..lakini hata hivyo kwa kumbukumbu zangu
kichwani mimi kipindi kila sikuwa na nafasi kubwa ya kufuatilia hayo mambo…nilikuwa
nashiriki kwenye upasuaji kama msaidizi tu…na wakati mwingine nasaidiana na
nyie kwenye kutumwa lete hiki, naleta…’akasema
‘Lakini siunakumbuka tukiolenyewe lilivyokuwa..?’ akauliza
‘Mhhh, ..sasa kwa yule mama..mmh, namkumbuka…. maana yule mama baada
ya kumaliza ule upasuaji, tukawa tunasikilizia tu, tulishamkatia tamaa ya
kuishi....na mimi baada ya ile kazi nikaondoka, nilikuwa na dharura fulani,
kama sikosei, kwahiyo sikujua kilichokuja kuendelea baadaye, nilikuja kusikia
tu…’akatulia
‘Nilikuja kuambiwa kuwa huyo mama alikuja kupona,..lakini akapotea
kiajabu-ajabu wengine wakavumisha mengi kuwa ni …mama wa ajabu ….unajua,,
lakini mengine zaidi ya hayo sijui ilikuwaje baadaye...ilikuwa sio kazi yangu…na
unajua ilikuwa ni kazi kubwa uende kusaidia huko, huku wagonjwa wa kawaida
wanakusubiria..oh, sikuwa na muda wa kufuatilia kwa kweli… ‘akasema
‘Oh, mbona shidaah..’akasema nesi.
‘Sasa kuna nini kinahitajika, maana kama ni yule mama keshaoza ni
muda eeh…na sikuwa na uhakika kuhusu yule mtoto wake,…sijui ilikuwaje, unajua
mimi sina muda na mambo mengine yasiyohusu kazi zangu, nikimaliza kazi zangu
haraka nakwenda zangu kwenye shughuli zangu nyingine..sina muda kabisa na mambo
ya hapa kazini….ambayo hayanihusu..huo ndio utaratibu wangu, kwahiyo sahamani
sana kwa hilo sizani kama nitaweza kusaidia zaidi!’akasema huyo dakitari
‘Unajua docta huyo mama tunavyojua sisi alifariki, lakini cha
ajabu kuna mama mmoja kaletwa hapa, huyo mama kaungua vibaya, akatibiwa, na
katika kutibiwa akaonekana ana kitu kama kuchanganyikiwa, mara akaanza kudai
kuwa tumechukua mtoto wake..mara eeh…’akasema
‘Lakini hiyo ni kawaida wagonjwa kama hao kuchanganyikiwa au..?’
akauliza dakitari akionyesha mshangao, na kuonekana kutokujua ni nini nesi
anakihitajia.
‘Sasa wakubwa wanadai kuwa huyo mama huenda, alitibiwa hapa
kipindi cha nyuma,..ndio maaana anadai mtoto wake kuchukuliwa hapa hospitalini,..wanadai
huyu mama anaweza akawa yule mama wa kipindi kileeeh, nikawaambia huyo mama wa
kipindi hicho keshafariki…’akasema
‘Kwani huyo mama na yule mama wa kipindi kile wanafanana, na
kwanini waseme ni huyo mama wa kipindi hicho, mimi haliniingi akilini, waambie
huyo mama sasa hivi ni mifupa ukifukua kaburi lake sana sana utakuta mifupa,
…hao watu wamechanganyikiwa nini , sasa wanataka nini, kuna nini kikubwa
kimetokea..’akasema
‘Cha ajabu huyo mama aliyefika sasa anadai kuwa mimi ndiye niliyemechukua
mtoto wake..’akasema
‘Kachanganyikiwa huyo achane naye, wewe endelea na kazi yako
bwana..aaha, mimi kwanza nimejichokea, naona nistaafu nikaendeleze hospitali
yangu, hapa napoteza muda wangu bure…sikiliza nikushauri kitu, achana na huyo
mama wewe pambana na kazi, hayo yapo na yanakuwepo…unasikia,..na kama hao
wakubwa wako wanadai kuwa eeh, ni kweli…waambie wathibitishe, na kwanini
wasikuamini, kwanini wanakuja kumuamini mgonjwa aliyechanganyikiwa, kama vipi
waniulize mimi maana nilikuwepo, au sio…’akasema
‘Mhh, hapa nimekwama…’akasema nesi
‘Sasa wewe ulihitajia nini kwenye kumbukumbu za zamani naona
kwanza ulivyofika hapa ukaniuliza kuhusu makabati na kumaanisha unahitajia kumbukumbu
za zamani , za kumuhusu huyo mama au sio,
ili uweze kuthibitisha kuwa huyu mama wa sasa sio yeye, au sio?’ akauliza
‘Ni kitu kama hicho..’akasema nesi akisimama kutaka kuondoka
‘ Sasa wewe ulitakaje kuwa
zipatikane hizo kumbukumbu za zamani, na tuchukua kumbukumbu za huyu wa sasa
ikibidi tuchukue DNA, ..ndio unataka hivyo, lakini kwanini yote hayo, kuna kesi
mahakamani ya madai, au ni kauli tu ya huyo mgonjwa, mimi sielewi hapo…!
Dakitari yule akamuuliza
‘Mhh docta sio kesi, ni kauli ya mgonjwa tu, na dakitari bingwa,
anataka kuhakikisha kuwa ni kweli au si kweli kuhusu madai ya huyo mgonjwa kuwa
mimi nimemchukua mtoto wake
‘Kwani wewe ulimchukua mtoto wake?!..., na kwanini umchukue mtoto
wake wa nini,…kujipa mzigo wa bure… mbona hao wakubwa zako naona hawana kazi ya
kufanya, waambia kama kazi zimewaishia waje huku tusaidiane, maana wagonjwa
siku hizi ni wengii…’akasema
‘Docta mimi nilikuwa nahitajia hizo kumbukumbu na kama unakumbuka
lolote zaidi kuhusu huyo mgonjwa zamani, na sura yake kama unakimbuka
vyema…’akasema nesi.
‘Sura yake…hapaan siwezi kumkumbuka kabisa…Lakini yote hayo ya
nini, unahitajia yote hayo, ili iweje?’akamuuliza
‘Mhh, hata sijui..’akasema nesi
‘Sawa kama unahitajia hizo kumbukumbu za zamani, mimi nakushauri
ukamuone mkuu wa bohari, mtunza nyaraka, huenda akawa na hizo kumbukumbu.. kitu
ambacho sizani kama utafanikiwa, ..maana hizo kumbukumbu zilichukuliwa kama
zimepitwa na wakati …zitakuwa zimeliwa na panya…’akasema
‘Na mtandao..sijui hiyo, komputa waliokuja kuhifadhia baadhi ya
kumbukumbu nayo iliharibika, ikawa ni hasara..pesa zimetumika, na kazi
iliyofanyika haionekani..yaani watu wanakuja na mambo yao wakiwa na malengo
binafsi,..ten parcent hiyo.. aah acha
tu, hata sitaki kuongea hayo mambo maana hayatanisaidia kitu.’akasema.
‘Sawa dakitari nimekuelewa..kama nitaona kuna umuhimu , nitafanya
hivyo…naona nikuache tu uhudumie wagonjwa…’akasema nesi
‘Lakini mimi bado najiuliza kwani wewe shida yako ni nini hasa
kwani huyo mama kashitaki, kwani kumetokea nini zaidi, huko kudai kwa mgonjwa,
kachanganyikiwa akipona itakwisha wasiwasi wako ni nini…?’ akadadisi yule
dakitari tena.
‘Docta, siwezi kukuelezea kila kitu kwa hivi sasa, ila ni muhimu
sana, …’ akasema nesi huku anatoka kuelekea ofisi za mtunza nyaraka na
kumbukumbu za hospitalini. Hata yeye hakujua hizo kumbukumbu zitamsaidia nini,
ila kila mara alikuwa akikimbuka kauli ya dakitari mtoto ikisema;
‘Nimekuambia tu wewe, kama itatokea
kuhitajika taarifa za huyo mama, basi jaribu kukumbuka hivyo kuwa kumbukumbu
hizo unaweza kuzipata kwenye kabati
namba 5, hili ni maalumu kwa kumbukumbu nyeti za kwetu kama madakitari,
sitarajii kuwa hapo zitaharibiwa....’
**********
Nesi aliachana na dakitari yule wa zamani baada ya kuona hana
msaada kwake akaelekea kwa mtunza store na nyaraka wa hospitalini,….
Mtunza store na nyaraka alimkatisha tamaa kabisa, kwani
alimwambia, kutokana na kulundikana kwa nyaraka nyingi za zamani, wao waliona
kuzipunguza zile za zamani, na nyingi zilikuwa zimeharibika vibaya,..lakini
waliogopa kuzichoma, wao wakaona nyaraka zote za zamani zihifadhiwe kwenye stoo
ya zamani, na humo hapatamaniki…!
‘Stoo ipi hiyo?’ akaulize nesi
‘Mhh, nesi huko hapaingiliki, kwani wewe unahitaji kitu gani hasa…kuna
mtu anatafuta asili au kuna tatizo,..kuna kesi ..au… mbona huna hata barua ya
madai au chochote cha kuweza kunisaidia…., kwasababu hiyo ingetusaidia kutafuta
visaidizi, hiyo stoo nesi …haiingiliki kwa hivi sasa , tumeomba kibali
tuyachome tu hayo mabaki….sasa sijui nitakusaidiaje…’ akasema yule mkuu wa
kumbukumbu!
‘Lazima nikalitafute hilo faili…na makabati yaliyotokea ofisi za
madakitari yapo wapi?’ akauliza
‘Makabati?!, wewe hukumbuki au hukuwepo, mengi ya makabati ya
zamani yalipigwa mnada, na kumbukumbu
zake ndio zikachanganywa na hizo za zamani…lakini kuna baadhi bado yapo,….’akasema
‘Oh,…nimekwama, lakini lazima niende nijionee mwenyewe ..’ akasema
yule nesi huku anatoka kwenye ile ofisi, akijua hana msaidizi wa jambo hilo,
inabidi alijizatiti mwenyewe.
Alijisema moyoni kuwa ,ili
moyoni ajirizishe na kuweza kujikwamua kutoka kwa bosi wake, basi akiwa na
nyaraka za huyo mama marehemu ataweza kuwa salama, akawa anajijutia kwanini alikumbuka
tukio hilo, maana mkuu wake kalishikilia bango, utafiri lina umuhimu .Sijui
kwanini kalikazania…akawa anajiwazia mwenyewe.
‘Lakini ni muhimu, kwa vile imetokea hivi, basi na mimi nahitajika
kujua vyema kumbkumbu za yule mama, maana sisi ndio tunaoishi na huyo mtoto
huenda ikaja kutokea huyo mtoto akataka kujua zaidi…sasa inanipa hamasa la
kuzitafuta hizo kumbukumbu….’akawa anajipa moyo kihivyo…
‘Kitu ninachojiuliza kichwani ni kwanini miminilikumbuka tukio
hilo na kuliongeleaa kwa hao madakitari wakati ilikuwa ni siri….oh sasa
nitaumbuka, nimeshindwa kuficha siri….’akawa anajilaumu.
‘Hata hivyo..ni ukweli usiofichika kuwa yule mama alikuja
akafanyiwaupasuaji, na baadaye akatoroka na ikaja kuokotwa maiti yake, na
akazikwa, sasa……kwanini huyu mama mpya aje kuleta shida, na madai kuwa mimi
nimemchukulia mtoto wake..hapa ndio inakuja shida ..hapo ndio maana nikakumbuka
kisa cha huyo mama maana kama ni mtoto , niliyemchukua ni mtoto wa yule mama
marehemu, sasa huyu mama katokea wapi….mmh hapa kuna kitu , sio bure..’akawa
anajiuliza na muda huo akawa anatembea kuelekea ofisi hiyo ya zamani.
Alipofika kwenye stoo iliyowekwa mafaili ya zamani, alikata tama
kabisa, kwani lilikuwa kama dampo la
uchafu, makaratasi mengi yalishaharibika na mengine panya walishayatafuna
kabisa. Akajaribu kupekua pekua na aliambulia kuwatibua panya waliokwisha jenga
makao yao, akakimbilia nje huku akipiga ukulele..baadaye akakumbuka siku ile
dakiatri kijana alivyomwambia,
‘Kumbukumbu hizi nitaziweka kwenye kabati
no 5. ..’ Kabati namba
tano, ndio kabati gani hilo, mbona humu ndani hakuna makabati, zaidi ya
marobota ya mafaili yaliyofungwafungwa na mengine yamefumuka, na hata hivyo
ilikuwa namba tano au mia tano…akawa anajaribu kujiuliza.
‘Na huyu mtunza store anadai makabati yalipigwa mnada..naona hapa
kuna baadhi lakini yamechakaa..sizani kama ndio hayo yaliyochukuliwa kule
….haya sio yenyewe mmh, hapaingiliki kabisa…’akasema
‘Kabati namba tano au mia tano…au….mmh hata sikumbuki
vyema…’akasema
Alikuwa hakumbuki vyema, maana siku ile wakati wanaongea na dakitari
kijana, akili yake haikuwa kwenye
kusikiliza hayo aliyokuwa akiagizwa, akili yake ilitekwa na hamasa za mapenzi,
…yeye alitaka angalau asikie neno moja la kimapenzi kutoka kwa huyo dakitari
kijana, angalau ajue kama kweli huyo dakitari anampenda, …
‘Sasa nitafanyaje….maana juhudi zangu mwenyewe zimegonga ukuta,
siwezi kuingia tena humo ndani, ..hawa wadudu walivyo, macho yao
yanatisha,mmmh, panya hapana, namuogopa sana huyu mdudu…na siwezi kuomba
msaada, nikiomba msaada zaidi kwa huyu mtunza store, nitakuwa naanza kuitoa
siri isiyotakiwa kujulikana…..’akasema nesi akijikagua, na mara akasikia kitu
kikiruka akajua ndio hao panya acha atimue mbio kuondoka eneo hilo…
Je itakuwaje, huyu nesi atafanya nini, au atakaa kimya,
...tuzidi kuwepo!
WAZO LA LEO: Tujengeni tabia ya kuhifadhi kumbukumbu
za vizazi vyetu…hili ni jambo ambalo wengi hatulitilii maanani, na vizazi
vinatawanyika, na wengine hata hawajui asili yao, lugha yao ya asili na hata
utamaduni wao. Ni kweli sababu kubwa ni kutokana na mishughuliko ya kimaisha,
lakini kama familia mnaweza kujenga taratibu za kuhifadhi kumbukumbu za asili
za vizazi toka kwa mababu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment