Nesi akiwa na jukumu la kutafuta ukweli kuhusu huyo mama, kama alivyokuwa ameleekezwa na docta
bingwa,..kuwa ajitahidi kupata ukweli kuhusu historia ya huyo mama…ikiwa na
pamoja na kuongea na ndugu zake ili kama wanafahamu lolote kuhusu huyo mama, …lakini
cha ajabu ndugu zake hawakuweza kuja tena hapo hospitalini.
Ikabidi siku ya pili yake alipokuwa mapumziko, kuchukua jukumu la
kwenda huko kijijini, pamoja na kusalimia, lakini pia alitaka kujua kama
atapata lolote kuhusu huyo mama, lakini hakuna jipya alilolipata.
Leo ni siku ambayo nesi huyu alitakiwa kutoa taarifa kwa mkuu wake
wa kazi wakitengo cha watu wenye matatizo ya ufahamu,ubongo ,akili, na kuchanganyikiwa
(Neurologists and General Psychiatrist ).
Akiwa ameshikilia kabrasha la huyo mama mkononi, aliingia ofisi ya huyo
docta, na kumkuta docta huyo akiwa na msaidizi wake, wakiwa na karatasi za x-ray, ambayo walimpiga huyo mama,…na
walikuwa wakionyeshana kitu kwenye hiyo xray, na ilikuwa dhahiri wanamuongelea huyo mama, na walipomuona huyo nesi, wote wakageuka
kumuangalia;
Docta bingwa ambaye alionekana siku hiyo kama hayupo ofisi kwani alikuwa hajavalia mavazi ake ya kazi akasema;
‘Karibu nesi…utuambie uliyoyaata huko kijijini, kwani nataak kutoka kidogo …ni hili ni muhimu sana..., maana
imefikia hatua huyu mama anakuonyoshea kidole wewe…’akasema docta
‘Ananinyoshea kidole mimi, kwa lipi?’ akauliza nesi akionyesha wasiwasi.
‘Kaa kwenye kiti kwanza tusikie uliyoyapata huko kijijini….maana huyo mama
anaongea mengi…ni kuonyesha kuwa huyo mama alipatwa na jambo likaziba ufahamu
wake wa kumbukumbu za nyuma…sasa anaanza kukumbuka kidogo kidogo....kwahiyo mengi yatasemwa, na huenda yakawa
na ukweli…hatutakiwi kuyapuuzia...’akasema docta bingwa.
‘Anadai wewe umechukua mtoto wake..’akasema docta msaidizi..na nesi
akakaa kwenye kiti huku akili ikianza kuchemka.
Nesi akiwa hata hajui atasema nini kwani pamoja na juhudi zote za hata
kufika huko kijijini alipokuwa huyo mama, lakini hakuweza kupata msaada wowote,
zaidi ya kuchanganywa akili..na vitisho zaidi,…kwani imefikia hatua watu wengine
wanaogopa hata kumuongelea huyo mama.
Akasalimiana na mabosi wake,, huku akili yake ikikumbuka yaliyotokea pale
alivyokwenda huko kijijini…, ilivyokuwa;
********
‘Mhh, mimi hata sitaki kumongelea huyo mama,…huyo mama hata… kuna
watu wameshaanza kupata mabalaa kwa kujifanya wanamuongelea huyo mama, ….mhh,
hapa mimi sijui lolote..’aliambiwa na mtu ambaye inasadikiwa kuwa ndiye aliyekuwa
mtu wa kwanza kumuona huyo mama alipooneana hapo kijijini.
‘Lakini nasikia wewe ni ndiye uliyemuona huyo mama kwa mara ya
kwanza,lipoonekana hapa kijijini au sio…je ulimuona akitokea wapi?’ akaulizwa
‘Nimekuambiaje mimi sijui lolote kuhusu huyo mama…unasikia jirani,
wewe ni ni binti tumekulea wenyewe kwanini nikufiche ukweli…hayo yaache kama
yalivyo,….’akasema huyo mama ambaye ni muongeaje sana, lakini kwa swala la huyo
mama akakataa kata kata kuliongea.
‘Unasikia nikuambie kitu jirani, …hili ninalolifanya ni kwa nia
njema, mimi nahisi kama nilivyosikia, waliopata madhara ni wale wanaomuongelea
huyo mama kwa ubaya, mimi ni nesi, na nipo kwenye hospitali aliyolazwa huyo
mama, lengo langu ni kumsaidia huyo mama atokane na tatizo alilo nalo..huyo mama inaonekana
kapotea, huenda huko alipotokea ndugu zake wanamtafuta hawajui wapi alipo..’akasema
nesi.
‘Nani kakuambia huyo mama kapotea..huyo mama hajapotea,huyo mama
anajua ni nini anachokifanya…kaja kulipiza kisasi, ni wale akina mama waliokufa
kwa kuonewa, kudhulumiwa…’akatulia.
‘Mhh, hizo ni imani tu..huyo mama hakuwahi kufa, kama angelikuwa
ni mfu tungelimuona huko hospitalini, anacho kila kitu kama binadamu..lakini
kama unavyosema huenda alitendewa ubaya, huenda…alipatwa na ajali, huenda…na
atahari hizo ndizo zikafikia kuharibikiwa….’akasema nesi huku akionyeshea kwa
mkono, na jirani akawa katulia huku kaangalia chini.
‘Mhhh….’akaguna huyo jirani kuonyesha kutokukubaliana na hayo
maneno ya nesi
‘Kuna matatizo mengi yanayoweza kumuathiri mtu akawa kama
kachanganyikiwa, ..sasa sisi kwa huruma zetu, maana hiyo sio kazi yetu
kuhangaika hivi, lakini tumeona tumsaidie huyo mama kwa vile alikuwa mwema
kwenu..na pia kwa namna nyingine ni wajibu wetu inapobidi kama hivi…, na ili
tufanikiwe hilo tunahitajia msaada wenu..’akasema nesi.
‘Jirani,… mdogo wangu…Wewe unajitakia matatizo, hebu nikuulize
kitu; Kwanini polisi walishindwa..?’ akauliza
‘Polisi hawajashindwa,… wao wametimiza wajibu wao,..na kama kuna
tatizo wangelipelekewa ili walifanyia uchunguzi…unajua polisi wana mipka
yao..hawawezi kujitungia kesi…. na huenda badoo wapo kwenye uchunguzi, siwezi
kuwasemea…’akasema nesi.
‘Mdogo wangu hata kama umesoma..eeh, lakini kuna mambo mengine
huyajui…nakutolea mfano tu kwa hao polisi,..hii kazi unayoifanya ilitakiwa
ifanywe na polisi ni kweli si kweli..?’ akauliza
‘Mhh…sio kweli inategemea unaongelea upande gani, mimi nafanya
haya ili kuwezesha mgonjwa kutibiwa…’akasema nesi.
‘Nisikilize,…nyie na polis ni ni nani mwenye mamlaka ya kuchunguza
ukweli kuhusu huyo mama,..kama kapotea, kama anatafutwa..kwanini alitaka
kuuwawa.. ina maana polisi wamepatwa na jambo ambalo limewaogopesha…kuna askari
wawili , tumesikia kuwa wamechanganyikiwa…sasa wengine wameogopa…unasikia mdogo wangu..’akasema huyoo
jirani.
‘Inawezekana wamechanganyikiwa na jambo jingine, lakini kwa vile
limetokea muda huo wa tukio ni lazima watu wataliunganisha hapo….’akasema nesi.
‘Mdogo wangu…nikuambie ukweli, mimi ninaona mengi ambayo huwezi
kuyaona licha ya kuwa wewe umesoma…. sasa naona na wewe huko unapokwenda
yanaweza kukuta hayo ya polisi..japokuwa naona nyota yako ni kali…lakini
nakuonya kama mdogo wangu, achana na hayo, achana na huyo mama, huyo mama ni
adui yako…atakusumbua sana, utakuja kuniambia..’akasema huyo mama.
‘Adui yangu kwa vipi…kwani mimi nimemfanya nini?’ akauliza
‘Inaonyesha hivyo…kazi kwako utapata shida, huyo mama atawasumbua
sana….usipoangalia…mmmh, sitakiwi kukuambia hayo, …’akatikisa kichwa na kupiga
chafya.
‘Kama ni kupata shida kwa ajili ya waginjwa kama hao, tumeshapata
sana..lakini hatuwezi kuvunjika moyo..maana ni moja ya jukumu letu jirani
yangu…..’akasema
‘Mengine mnajitakia ..hasa hilo la huyo mama,…utakuja kuniambia..’akasema.
‘Jirani, sisi tupo na huyo mama wakati wote tunamuuguza na sasa
angalau anaanza kuongea na watu..lakini tatizo hana kumbukumbu za nyuma…hayo
mengine na mambo ya kukuza tu, hayana ukweli…’akasema nesi.
‘Nani kakuambia hana akili..akili anazo sana, ..lakini hatakiwa kuongelea
yaliyopita maana ni machungu na shubiri kwake, yamefichwa, anachotakiwa
kukifanya kwasasa ni kutimiza lengo la ujio wake….unasikia, hataongea ya nyuma
mpaka lengo lake litimie…’akasema
‘Jirani hebu niambie, wewe unasema hivyo kwa ushahidi gani?’
akaulizwa nesi akimuangalia huyo mama ambaye wamezoea kumuita jirani maana
zamani waliwahi kuishi nyumba ya kupanga pamoja, na hata walipohamia kwenye
nyumba zao bado wakaendeleza kuitana hivyo.
‘Kutokana na wataalamu,….na mimi huwa ninapatwa na njozi ,
zinanielekeza, si unakumbuka wakati tunaishi pamoja kwenye ile nyumba…sasa kuna
watu wananijia, na wananiambai mengi…sasa hao, siwajui ni akina nani, wameniambia
hivyo...huyo mama sio mwanadamu wa kawaida, ….’akatulia na kuangalia hewani
kama vile anaona kitu.
‘Hao wanakuambia hivyo ni watu, unakutana nao..au ndio hayo majini…?’
akauliza nesi akionyesha tabasamu mdomono la kudharau.
‘Unajua nikufunulie kitu…majini ,mashetani, vibwengo wanaweza kujigeuza na kuwa maumbile
ya wanadamu wakiwa na malengo yao…sasa huyo mama…muone hivi hivi…mhhh, najua hutanielewa,
wewe si msomo bwana…’akatulia akageuka kuangalia huku na kule. Na nesi akaiona
hiyo hali akauliza
‘Nakuona kama unaogopa kitu…, huyo mama yupo huko mjini
hospitalini, kama ndio yeye unayemuogopa…nakuona kama unawasiwasiwasiiih…’akasema
nesi akitabasamu.
‘Ahahaha….mdogo wangu…mmmmh, sio kweli, huyu mama yupo hapo nje…’akaema
huyo mama, huku akiwa kakodoa macho kuangalia mlangoni, na nesi akashangaa..kwanza
kwa jinsi huyo mama alivyotoa macho, na pili kusikia hiyo kauli yake, kuwa huyo
mama yupo nje, lakini hakutilia maanani maana anamahamu sana huyo mama akazarau
na kusema;
‘Jirani, sikiliza nikuambie..hivi hujaacha yale mambo yako..mara
unaona wachawi, mara umeona hiki au kile..sisi wala hatuvioni..hayo
yatakuharibu akili…., ‘akasema
‘Mhhh…acha..acha..namuona huyoooo’akasema na kutikisa kichwa.
‘Jirani vipi tena…nakuambia ukweli, mimi ndiye ninayeshughulika na
huyo mama kwa sasa, sijawahi kuona dalili yoyote ya hayo unayofikiria wewe na
hizo ni hisia zenu tu huku kijijini,…mumezijenga akilini, na zitawaathiri sana,
hayo sio mambo ya kuyajenga kwenye ubongo….huyo mam a nimemuacha hospitalini,
hawezi kuja huku…’akasema nesi, lakini alimuona huyo jirani yake akitikisa
kichwa na akawa kama anaweweseka mdomoni.
‘Mhh, jirani huyo mama yupo hapo nje….kama unabisha hebu toka hapo
nje umuone..’akasema, na nesi akageuka kuangalia nyuma akafikiri na baaadaye akasimama,…
Hakutaka kubishana na huyo mama, akatembea taratibu kama kunyata, hadi
mlangoni kabla hajashika mlango kufungua, akasikia mlio wa nyago, kama mtu anakimbia.
Nesi akafungua mlango kwa haraka na kutoka nje, akatizama huku na kule hakuona
mtu, na kwa mbali akaona kama mtu…ni mwanamama, kajifunika kama vile alivyokuwa
kajifunika yule mama,..na kwa umbali ule hakuweza kuona zaidi na huyo mtu
akapotea…
Nesi akapikicha macho…akatizama tena, hakuona kitu, akatulia na akajaribu
kutizama tena na tena hakuna dalili tena ya mtu, akatulia kuwaza, akageuka
kutaka kurudi kuongea na huyo wanayemuita jirani, lakini akaona haina haja,
taratibu akaondoka zake hata bila kuaga….
*********
‘Unajua..huko nilipokwenda kwa yule mama mliyeniambia kuwa ndiye
aliyemuona huyo mama wa mkono wa baraka kwa mara ya kwanza mhh, nimeondoka bila
kuaga..…’nesi akawa anaongea na ndugu zake, muda huo alishajiandaa kuondoka,
kurudi mjini.
‘Mhh kakuambia nini…maana yule mama naye sijui ana mshetani,
anaweza kuona vitu msivyo viona.. naye ana makarama yake…’akasema jirani wa
dada yake ambaye alikuwepo hapo akimuaga nesi , na kwa vile wamezoeana sana
alitaka pia kufahamu maendeleo ya mgonjwa.
Nesi huyo alipofika hapo
kijijini, akasalimiana na ndugu zake, halafu akataka kujua kwanini hawakurudi
tena kumuona mgonjwa, wakasema mwenye nyumba hataki, kwahiyo wametii amri ya
mume wa nyumba, japokuwa walikuwa na hamu ya kurudi kumuona mgonjwa.
‘Sasa kwanini shemeji kakataa, kama yeye hataki, basi angewaruhusu
nyie mje mumuone mgonjwa....maana yule mama alikuwa mwenzenu, mkaishi naye hapa
kwa wema au sio, na mumesema alikuwa akiwasaidia watoto wenu wenye matatizo...na
pia docta alitaka kuongea na nyie…kwani shemeji kwanini hataki muende kumuona
mgonjwa…’akasema nesi.
‘Hataki, na hataki kutoa sababu…, na unasema docta anataka
kutuona, kwanini docta anataka kuonana na sisi heri basi hatukufika maana tungelisema
nini kuhusu huyo mama, na shemeji yako angesikia kuwa tumeongea na docta…
lolote kuhusu huyo mama mmh, kungechimbika….’akasema dada mtu.
‘Mimi ningekuja mwenyewe, lakini yanayoendelea hapa kijijini yanatisha..nikaona
kwanini nijitakie matatizo, mume wangu hajanikataza….’akasema huyo jirani, na
nesi akaona ndipo pa kuanzia.
‘Kwani kuna nini kinachoendelea hapa kijijini maana sasa mnatia
aibu, kila siku visa vya kuua, kuchomeana moto.., kuumizana ….ukiuliza ni imani
za kishirikina, wivu…unyanyasaji kwa akinamama, imekuwaje jamani…hivi niwaulize,
dini mumepeleka wapi..?’ akauliza
‘Mhh, ya hapa kijijini yaache kama yalivyo, ..usije kuingia
matatizoni,..’akaambiwa
‘Hapana kama ni kuhusu huyo mama ,…hilo ni moja ya ajenda zangu za
kuja hapa, …naaah, ni nani anaweza kuniambia yote kuhusu huyo mama,…nataka
kujua ..au kuonana na ambaye alimuona huyo mama kwa mara ya kwanza…ili tujue
katokea wapi?’ akauliza
‘Mimi nakushauri …japokuwa sina uhakika sana,..nenda kwa yule mama
mnayemuita jirani yenu…yule yupo mpakani mwa kijiji, na ndiye aliyemuona huyo
mama kwa mara ya kwanza….na anajua mengi..japokuwa sijui ufahamu wake kuhusu
huyo mama wa mkono wa baraka…maana kila mtu sasa anaogopa kuyaongea hayo ya
huyo mama..’akaambiwa na mama mmoja ambaye ni jirani yao hapo.
‘Basi ngoja, mimi nawaacha kidogo…sitaki kusubiri…muda
unakwenda..dada mimi nakwenda kwa huyo mama…’akasema nesi na bila kusubiria
zaidi akaelekea kwa huyo mama wanayemuita jirani…ni nje kidogo ya eneo hilo… na
yaliyomkuta ndio hayo……
*****
‘Haya tuambie umepata nini huko, maana nakuona uso
umesawajika….’akamuuliza alipomuona mdogo wake akirudi wangu wangu, muda huo jirani yao pia alikuwepo , na jirani
huyo akawa katega sikio, na kutikisa kichwa kukubalina na hilo.
‘Mhhh…huko eeh, kweli, yule jirani hajaacha yale mambo
yake….unajua baada ya kunikatalia kuniambia ukweli kuhusu huyo mama nikatumia
ujanja kumuhoji,… na katika kuongea akajikuta anamuongelea huyo mama, akadai
kuwa huyo mama nimekuja naye toka mjini…’akasema nesi.
‘Kwa vipi?’ akauliza dada mtu akiacha kile alichokuwa akikifanya
na kumuangalia mdogo wake.
‘Hata mimi sijui…anadai kila ninapokwenda huyo mama yupo nyuma
yangu na pale hakuweza kuingia, alikuwa nje akinisubiria.’akasema
‘Mumeonaee..huyo mama ana machale..anaweza kumuona mwanga,
…mchawi…anaona vitu msivyoviona..ana sijui tuite nini…ana hulka ya uganga wa
kienyeji..sijui kwanini hataki kuwa mganga….’akasema huyo jirani.
‘Mhh, usiende tena kwake, ..asije kutuletea mabalaa…mimi sitaki
kuongea nay eye, hasa akianza mambo yake….mara akaona hiki, mara yule yupo
hivi…hapana , hata mume wangu hataki kabisa yule mama kufika hapa..anaweza
kukukosanisha na watu….’akasema dada mtu.
‘Sasa sikilizeni niwaambie ilivyokuwa..’akasema huyo nesi.
‘Mhuuu, tuambie ikawaje?’ akauliza huyo jirani lakini dada mtu
hakutaka kusikiliza zaidi..akawa kaangalia mlango wa chumbani, akijua mume wake
yupo ndani kalala.
‘Akaniambia kama nabisha kuwa huyo mama hakuja name, nitoke nje, nitamuona huyo mama
akinisubiria..’akaasema nesi.
‘Unaonaeeh..haya ikawaje, ni lazima utamuona huyo mtu kwa vile
kasema umuone, vinginevyo usingeliweza kumuona…’akasema huyo mama jirani.
‘Acheni hayo mazungumzo, ukiongea sana hayo mambo yanakuathiri
kiakili, utajikuta unaamini mambo ambayao hayafai sio sehemu yetu kuyaamini,..mimi
naona tuongee mengine…’akasema dada mtu lakini moyoni alikuwa na hamu kusikia
yaliyomkuta mdogo wake alipokwenda huko.
‘Unajua nataka kuwaambia ilivyokuwa sio kwamba nimeamini,…
hapana..ila imetokea hivyo,..maana nilipotaka kutoka kwanza nilisikia kama
kishindo cha nyayo cha mtu anayekimbia,..nikajua ni mtu tu, labda alikuwa hapo
mlangoni akisikiliza mazungumzo yetu, basi kwa haraka nikafungua mlango n kutizama nje…’akasema
‘Eheee, ikawaje..ukamuona eeh…atakuwa kapotea usingeliharakisha
hivyo…, watu kama hao wanajua na kuhisi nyayo zetu, ..wewe uko ndani unatembea
yeye yupo nje, anajua kabisa unatembea kuja kufungua mlango, na akiondoka hapo
ni kama anapaa huwezi kumuone tena..’akasema huyo jirani.
‘Wewe umejuaje hayo?’ akauliza dada mtu.
‘Niliwahi kuongea na huyo mama,…na mara kwa mara naongea naye,
..ana visa vingi..anawajua watu wote hapa kijijini, ninani mwanga, ni
nani….yaani ukikaa naye utaogopa kuishi hapa kijijini…’akasema huyo jirani.
‘Kwahiyo huyo jirani anasema huyu mama aliyekuwa akiishi hapa ni
mwanga, ni mchawi…au sio?’ akaulizwa huyo jirani, akageuza kicha huku akiwa
kama anafumba macho.
‘Aaah, huko tusiende…mimi sijui, …..nazungumzia huyo mama alivyo ,
sio huyo mama wa mkono wa miujiza, mimi huko sijui…’akasema an kuonekena
kuogopa kumuongelea huyo mama.
‘Au nyie ndio washirika , mlikuza mambo, mkajenga chuki hadi huyo
mama wa watu akafanyiwa hayo mabaya..roho mbaya tu…’akasema dada mtu.
‘Jirani…chunga mdomo wako…mimi na huyo mama tulikuwa marafiki..na
ingelikuwa kidogo tu, ..mimi ningeliweza kuona sura yake..kidogo sana..lakini
siku ile akaja mtu, tukakatisha mazungumzo yetu, yule mama aliniamni kweli,
alitaka kunionyesha uso wake..’akasema huyo jirani.
‘Jirani na porojo zake…sikilizeni mume wangu kalala, akiyasikia
haya …mmh’akasema dada mtu.
‘Ina maana shemeji yupo ndani, unajua nilishamuaga kuwa
naondoka…’akasema nesi.
‘Ndio maana nasema huyu jirani anapenda sana kuongea na
kujionyesha kuwa kila kitu anajua,..ukimsikiliza huyu , unaweza ukapotea, wewe
wahi usafiri, labda kama unataka kulala..’akasema dada mtu.
‘Aaah, ..jirani ngoja amalizie…hebu tuambie ulimuona huyo mama,
akiwa hapo mlangoni?’ akauliza huy jirani.
‘Hapana sikumuona huyo mama…ila niliona mtu kwa mbali sana,
..’akasema nesi
‘Yupoje ni kama huyo mama au?’ akauliza huyo jirani
‘Wanafanana…lakini szani kama ndio yeye maana nilipiga simu
hospitalini, wakaniambia huyo mama yupo….ila huyo niliyemuona kwa uvaaji …na
sio kweli…maana alikuwa mbali, …na..na alikuwa kanipa mgongoo kwa hiyo
nisingeliweza kumuona, siwezi kusema ni huyo mama sio kweli, …’akasema
‘Ulirudi kumuuliza huyo mama ?’ akaulzia huyo jirani
‘Wala sikuwa na haja naye tena, …’akasema nesi
‘Ungerudi angekufunulia mengi….maana angekuwa na uhakika kuwa huyo
mama hayupo hapo nje, na anaongea akiwa na uhakika, wewe umeamua kuondoka kwa
haraka bure na umekosa uhondo..’akasema huyo jirani.
‘Siku nyingine nitaongea naye..ila sasa naondoka, na hata sijui
nitamuambia nini bosi wangu, maana sijapata alichoniagiza..’akasema
‘Haya mtaniagia mtoto…na shemeji tena, japokuwa nilishamuaga….vipi
siku hizi mtoto analia lia tena kumtaka mama wa baraka…naona sasa kawa mkubwa,
..’akasema
‘Wala halii tena, huyo mama wa mkono wa baraka kafanya makubwa,
wale wote waliobahatika kukutana na huyo mama wanasema watoto wao hawana
matatizo kabisa,..sijui kwanini watu wengine waliamua kumfanyia hayo
waliyomfanyia, unajua huyo mama angesaidia sana hapa kijijini…natamani arudi
tena’akasema dada mtu.
‘Yah, lakini huenda na yeye alikuwa na lengo lake,…hatujui
zaidi,..yule mama anasema huyo mama alikuwa na malengo yake, pamoja na huo
uzuri wake..’akasema huyo jirani
‘Malengo gani?’ akaulizwa
‘Mmmh, mimi sijui…utakuja kumuuliza huyo mama atakufunulia yote,
lakini kwa hivi sasa sijui..maana watu wanaogopa kabisa kumuongelea huyo mama…labda
akirudi tena hapa, kama atafikia hapa mtajua zaidi…’akasema huyo jirani.
Mara mlango ukafunguliwa, akatokea shemeji mtu akiwa kashika fimbo
yake mkononi, ..kakunja uso kwahasira…akawaangalia waliokuwepo mmoja baada ya
mwingine, japokuwa alikuwa akiwaangalia
lakini usoni alikuwa kama hayupo hapo, akainua fimbo juu, na kusema;
‘Hivi niliwaambiaje?’ akauliza sasa akimtizama mke wake , na mkewe
akawa kaangalia chini, na kusema;
‘Kwani kuna nini mume wangu?’ akauliza mke mtu sasa akimuangalia
usoni, alikuwa anajua ni kitu gani mume wake anauliza lakini hakutaka kukubali
mara moja.
‘Nawauliza niliwaambiaje?’ akauliza tena huku akitikisa kichwa
‘Tulikuwa tunaongea tu…’akasema mke mtu, na jirani akiwa
kajikunyata kwa uwoga
‘Narudia tena, nauliza niliwaambiaje?’ akauliza sasa kwa sauti ya
hasira.
‘Tusimuongelee huyo mama hapa ndani…’akasema jirani mtu.
‘Sasa wewe jirani, ujirani utakushinda..sitajali kuwa wewe ni
jirani, na wewe mke wangu ….ina maana mimi nilichoongea unaona ni cha
upuuzi,…’akasema kwa hasira.
‘Mume wangu samahani,..hatutarudia tena,..ni mdogo wangu katumwa,
anataka kujua jinsi gani huyo mama alikuwa akiihis nasi, katokea
wapi…inahitajika huko kazini kwao..’akasema na shemeji mtu akageuka kumuangalia
shemeji yake.
‘Mimi nilijua umeshaondoka….’akasema na kugeuka kutaka kuondoka.
‘Sasa shemeji mimi nataka kukuuliza jambo..’akasema nesi.
‘Jambo gani, kama ni kuhus huyo mama, ..sitaki kusikia…unasikia
kama unataka tukosane, uniulize kuhus huyo mama…simtaki na sitaki kusikia
habari zake…’akasema shemeji mtu.
Nesi akamsogelea shemeji yake na kumshika mkono,….shemeji yake
akawa anatembea hakugeuka kumuangalia shemeji yake huyo na nesi, akawa
anatembea naye sambamba…sasa akautoa mkono wake mkononi mwa shemeji yake, na
kuuweka begani,… wakatoka naye huku akionyeshea ishara kwa nyuma kuwa yeye
anaondoka.
‘Haya safari njema…’akasema dada mtu, na jirani akawa anataka
kutoka, nia kuwafuatilia hao waliondoka, akionyesha kutaka kusikia wanayoongea…,
lakini dada mtu akamshika mkono na kumtuliza kwanza. Na huyo jirani akasema;
‘Mhh mtu na shemeji yake bhana, hivi huoni wivu…?’ akauliza
NB: Tupo pamoja
WAZO LA LEO: Kamwe usikate tamaa na kupambana na
majaribu, mitihani na shida zinazokuzunguka, kwani shida hizo au majaribu hayo
yasingeliitwa hivyo, shida au matatizo kama yengelikuwa ni rahisi kuyatatua.
Kila hatua ya vita hiyo, utajifunza mbinu mpya na njia nyepesi ya kuyashinda
hayo majaribu. Jua kuwa Mungu yupo pamoja nawe na kakupa hiyo mitihani kujaribu imani yako,
pambana na mwisho wa siku utafaulu tu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment