Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, March 6, 2015

NANI KAMA MAMA-41


‘Tayari umeshampiga picha?’ akaulizwa na askari ambao walipomuona akitoka tu walimfuata hata kabla hajawafikia.

‘Picha!?....?’ akauliza akionyesha mshangao , kama vile hajui ni kitu gan anauliziwa, halafu akawa kama kukumbuka akiangalia ile kamera na kusema;
‘Picha ya nini, ..sizani kama picha hiyo mnayotaka nyie  ina umuhimu huo kwasasa..’akasema akitembea kuwakaribia pale waliposimama hao maaskari akiwemo kiongozi wao.

‘Kwanini..?’ akauliza yule mkuu wao kwa sauti ya kukasirika, halafuu akajirekebisha na kuongea sauti ya kawaida, akasema;

‘Au umeshindwa tena, ..sasa umefanya nini…oh, …mbona kazi hii imekuwa nzito sana…tatizo ni kuwa, docta akimpiga hayo masindano yao, hatutaweza kupata picha tunayoihitajia..picha hiyo ni muhimu sana kwetu…’akasema huyo askari.

Yule jamaa akawa anawaangalia huku akionyesha uso wenye fikra, ni kama vile hakuwepo hapo, na aliona kama wanampotezea muda, akasema;

‘Mnaitaka hiy picha,…Ili iweje?’ akauliza huku akiwa kainua mkono juu kumkabidhi huyo askari kamera yake, na yule askari akawa anasita kuipokea, na yule mkuu wao akasema;

‘Tunaihitajia hiyo picha ili tukamtangaze huyo mamae kwenye nyombo vya habari, ili wenyewe kama wapo,waione hiyo picha, wewe hulioni hilo… unajua vyombo vya habari vinasaida sana… wanaweza kupatikana ndugu zake, na hasa wakisikia kuwa amekufa…habari kama hizo za msiba husambaa haraka sana,..ni lazima wakisikia watakuja hapa, na wataelekezwa kuwa maiti yao ipo hapa..’akasema huyo askari.

‘Hakuna maiti humo ndani….’akasema huyo jamaa huku akiinua mkono kumkabidhi huyo askari kamera yake…;

**********

‘Mpelekeni chumba cha uchunguzi nakuja..’aliyeema ahoy alikuwa docta ambaye alikuwa aktokea chumba alichokuwa kaweka huyo mama,..sasa alikuwa akitoka kwa haraka huku anaongea na simu,

Baadaye huyo mama, au mwili wa huyo mama ukatolewa pale ulipokuwa ukiwa umelazwa kwenye machela, sasa kuashiria mwili, kupelekwa chumba cha maiti au chumba cha uchunguzi zaidi.

Asakari alipoona huyo mama anapelekwa chumba cha uchunguzi akashangaa, akawauatilia hao waliombeba huo mwili wa huyo mama , akitaka kupata maelezo zaidi, na alipowakaribia akawauliza.

‘Ina maana huyo mama hajafa?’ akauliza wale waliombeba wakashitka na kugeuka kumuangalia huyo askari, wakasema;

‘Kwani alikuwa amekufa?’ wakauliza hao manesi, kwa mshangao.

‘Oh ni miujiza, sisi tulileta maiti…sasa tunaona ajabu..’akasema huyo askari

‘Labda maiti bado ipo huko ndani sisi tumeambiwa na docta tumchukue huyo, hatujaona amity huko ndani..’akasema mmoja wa nesi



***********

‘Katokea wapi huyumama naona kama …eeh, kaungua mkono….’akasema nesi mkuu akijaribu kumkagua…?’ akauliza

‘Katokea kijijini..’akaambiwa

‘Kijijini ..kijiji cha wapi…. ?’ akauliza huku akijaribu kumchunguza, sasa akitaka kumshika lakini kutokana na yale majeraha na ahkuwa amevaa kinga akwa ana mchunguza tu kwa macho

‘Unamfahamu?’ mara akauliza askari ambaye kwa muda huo alikuwa nyuma yako, akiwa kimiya..na yule nesi mkuu akageuka kumuangalai huyo askari akasema;.

‘Sina uhakika kama ndio yeye…’akasema huyo nesi

Yule nesi mkuu, akamtizama yule mama kwa makini halafu alapata wazo , akainama karibu na kichwa cha yule mama ambacho kilikuwa kimefunikwa, akasema kwa sauti ndogo karibu na sikio la huyo mama;

‘Nataka mtoto wangu….’n akukawa na mtikisiko kuonyesha huyo huyo mama anajitkisa, na askari aliyekuwa nyuma akaona ile hali, akawa kama kashikwa na mshituko, kwani alikuwa bado hajaamini, akabakia kushangaa, halafu akasikia sauti kutoka kwa huyo mama…

‘Nataka mtoto wangu…’wote wakabakia wameduwaa, hasa askari, ambaye alikuwa akiangalia hilo tukio kwa aina yake….;

‘Mhh, sijawahi kukutana na tukio kama hili katika misha yangu ya kazi,..na anhitaji kulifuatilia hili tukio kwa karibu,…nataka nionane na huyo docta..’akasema

Tuendelee na kisa chetu

*************
 Siku ya pili yake wakaja ndugu waliokuwa wakiishi na huyo mama, yaani mama mlezi wa mtoto na jirani yao wa karibu…, baba mwenye nyumba hakufika, wakapitia wodini ambapo walijua wanaweza kumpata huyo mgonjwa ..au huyo mama aliyeletwa hapo usiku lakini hawakumuona, ikabidi waulizie, …na kwa muda ule hakuna aliyeweza kuwapa jibu la haraka;

‘Ni kama vile huyu mama hakufika hapa, au hayupo hai nini.?’ Akauliza jirani yake.

‘Atakuwa hai..mtu akifa bwana, haicheleweshi kujulikana,  nahisi kwa vile aliletwa usiku bado atakuwa chumba kingine..labda cha uchunguzi zaidi..sasa ngoja tufanye hivi, …tumuone mdogo wangu, sikutaka kumsumbua sana, lakini kwa vile tumekwama, hatuna jinsi…’akasema mama mwenye nyumba

Wakarudi mapokezi na kuomba kuonana na huyo ndugu yao, na simu zikapigwa, baadaye wakalekezwa waende wapi, ….wakaenda huko walipoelekezwa….

Walimkuta akiwa katika hekaheka za kuwahudumia wagonjwa wa chumba cha akina mama wajawazito, ni chumba maalumu kwa akina ama wenye matatizo makubwa yanayohitajia upasuaji..,..na kwa vile alishapigiwa simu alipowaona wageni wake wapo wamesimama mlangoni akawaonyesha ishara kuwa wamsubiri anakuja,…akaonekana kuongea na docta aliyekuwepo hapo, …..

‘Oh, docta nina wageni muhimu sana, naomba nikawaone sijui kuna nini nyumbani…’akasema na docta wake kwa vile alishawaona hao watu wakiwa wamesimama mlangoni…. Akasema;

‘Hamna shaka..mwambie mwenzako afanye hicho ulichokuwa unakifanya...’akasema docta na huyo nesi akamuendea mwenzake na kumkabidhi majukumu yake kwa muda.

‘Usikawie….maana mimi nataka kutoka, muda wangu umekwisha..’akasema mwenzake, na huyo nesi kwa haraka akawafuata wageni wake.

‘Vipi kuna tatizo jamani, mbona sina taarifa…’ akawauliza wageni wake na wageni wake wakonyesha uso wa furaha wakisema;

‘Waooh, mdogo wake huyoo…’ilikuwa sauti ya jirani, ikawa ni kusalimiana kwanza kwa muda, halafu dada mtu akasema;

‘Ndio kuna tatizo…samahani kwa usmbufu,…yupo mama mmoja tulikuwa tukiishi naye, unakumbuka kipindi kile ulipofika kumleta mtoto ulimuona mama mmoja aliyekuwa kama kachanganyikiwa….’akasema na mdogo mtu akawa kama anatafakari kukumbuka, na dada mtu akaendelea kuongea;

‘Nakumbuka ni muda, na wewe umekuwa mtu wa kuja mara mojamoja, na kila mara ukifika humkuti huyo mama...lakini alikuwa akiishi na sisi…huyo mama,..uliwahi kumuona siku ile ulipomleta mtoto…’akasema

‘Mhh…sikumbuki..hasa ni nani huyo mama, unajua ….muda eeeh, alikuwaje huyo mama?’ akauliza

‘Alikuwa akiimba imba hivi..nataka mtoto wangu, nataka mtoto wangu..unakumbuka?’ akasema huyo jirani.

‘Ohoooo, nimekumbuka,…ina maana ni yule mama wa mitaani, nakumbuka mlisema ni mama asiyejulikana wapi alipotokea, na alikuwa kama kachanganyikiwa..ndio yule mama,  ooh, nimekumbuka kweli alikuwa  akiimba, namtaka mtoto wangu..oh….nimekumbuka,..kwahiyo?’ akauliza

‘Huyo huyo….unajua tulikuja kuishi na huyo mama, tuliamua kumchukua na tukawa tunaishi naye pale nyumbani, nakumbuka kama niliwahi kukuambia, …au hukuwa makini sana…. ‘akasema

‘Mhh…nakumbuka kitu kama hicho, ulisema kuna mama mmoja mwenye  karama mnaishi naye…lakini sikuwahi kumuona….. mlisema huyo mama anahudumia watu..sasa sikujua ni huyo mama wa mitaani, aliyekuwa akiiimba, mmmha mbona haiji..ok, ndio kuna mama aliletwa jana…nakumbuka kumuona..’akasema.

‘Ndio huyo mama alikuwa akiimba mitaani, ndio huyo mama wa mkono wa baraka..’akasema jirani

‘Mhh,lakini jamani!..nyie watu mbona mna hatari  mlimchukuaje huyo mtu ambaye hajulikani wapi alipotoka, na zaidi anadai kila mtoto ni wake…oh, ..na mtoto,…. kwanza mtoto yupo wapi?’ akauliza nesi akiwaangalia kwa uso wenye wasiwasi

‘Tumemuacha na baba yake..’akasema dada mtu, na nesi akawa ana shauku ya kujua mengi, akaangalia saa halafu akasema;

‘Ehe, sasa ilikuwaje, ….?’ Akauliza

‘Unajua huyo mama, walikuja watu wakataka kumchoma moto huyo mama….wakamkata na mapanga…’akasema

‘Unajua jana nilimuona mama mmoja kama yeye, kaletwa hapa, sikuwa na uhakika sana kama ndio yeye, ila nikasema ngoja nijaribu kitu, nikaimba huo wimbo wake…heee, ajabu akaitikia vile vile, nikahisi ndio yeye..lakini pia akilini sikuamini sana, maana yoyote anayefahamu tukio hilo, aua nayetoka huko kijijini  anaweza kuitikia hivyo…’akasema

‘Sasa yupo wapi?’ akauliza mama mwenye nyumba kwa hamasa

‘Bado yupo kwenye wodi ya uchunguzi, kwa hivi sasa sipo huko, kuna msaidizi wangu anahusika na wodi hiyo, mimi sasa hivi ni mkuu wa manesi wote, kwahiyo napitia kazi za manesi wote au kukiwa na jambo muhimu ndio nalifuatilia kuhakikisha kazi zinakwenda vyema, ..’akasema.

‘Mhh, mungu mkubwa sisi tulijua huyo mama ni maiti, kaletwa huku akiwa maiti, mara taarifa zinafika huko nyumbani kuwa kafufuka…’akasema jirani

‘Oh, kafufuka…hapana, aliyemchunguza hakumchunguza vyema,..unajua kuna watu wanaweza kuzimia kabisa ukashika sehemu husika ukahisi kafariki, kumbe hajafariki, siku hizi kuna vipimo maaalumu vya kuthibitisha hilo…hakuwa ameferiki bwana..’akasema nesi akitabasamu

‘Wewe unasema tu kwa vile humfahamu mama huyo na vituko vyake….’akasema dada mtu

‘Kwani alikuwaje,..maana nahitajika kazini,..’akasema akiangalia kule kazini kwake na kuangalia saa yake ya mkononi.

‘Basi huyo mama alikuja kuwa mtu muhimu sana kwetu..na sio kwetu tu….nilikuambia mfanyakazi wetu kuna muda alikuwa anamuachia huyo mama kazi za kulea…ni kwa vile mtoto alikuwa analia hamtaki mtu mwingine zaidi ya huyo mama, na sio mtutu wetu tu…’akasema

‘Mhh hiyo ni mpya..’akasema nesi.

‘Huyu mama ana makarama ya ajabu, kila mtoto aliekuwa na matatizo hasa ya kulia, kushituka shituka…kuumwa umwa mahoma yasiyo na maelezo, huyo mama akawa anawatibia kwa kutumia mkono wake…,’akasema na nesi akatabasamu.

‘Ni kweli wengi walikuwa wakizania hivyo kuwa huyo mama huenda kweli ana tatizo la akili lakini pia ana uwezo huo…sasa kwanini alale nje, na alipendelea sana kulala upenuni mwa nyumba yetu..nikuambie ukweli mama huyo aliweza kuishi vyema kabisa na mtoto wetu, na mtoto mwenyewe akawa anampenda sana huyo mama kama mama yake vile…’akaendelea kuongea dada mtu

‘Sasa ikawaje…maana simnaona nipo juu, kwa juu…’ akauliza nesi

‘Basi siku mbili zilizopita, wakaja wahuni, nawaita ni wahuni kwasababu eti wanadai huyu mama ni mwanga…walichofanya ni kumkata kata na mapanga, halafu wakachoma nyumba moto, ili wamteketeze, bahati nzuri huyo mama hakuungua ila,….ndio akakutwa kapoteza fahamu..na walipomchunguza vyema wakaona ameshakata roho…’

‘Mungu wangu , ina maana nyumba yetu imeteketea na moto…, na mtoto wakati huo alikuwa analala na nani…? Akauliza nesi

‘Sehemu iliyoungua ni kile kibanda cha uwani, ambapo ndipo alikuwa akiishi huyo mama na kufanyia shughuli zake na…mtoto hana matatizo, tunalala na yeye..atalalaje na huyo mama wakati mama yake nipo…sasa yaliyotokea baada ya hapo hutaamini,..polisi wenyewe walichemsha wakashindwa kuigusa maiti yake….’akasema.

‘We mbona mnanipa habari ya aina yake,….ngoja, naona nahitajika kuyasikia haya yote, ngoja nimtumie ujumbe wa maneno mwenzangu naona nimuambi hivi… kuwa kuna ndugu zangu wamekuja wana shida kubwa, nahitaji muda kuwahudumia..anivumilia kidogo..’akawa anaandika,…na haikupita muda ujumbe ukaingia kwa simu ya huyo nesi, naye akasema;

‘Sasa tunaweza kuongea haya nipeni kisa chote,….mnasema polisi wakachemsha wakakimbia maiti, …hahaha, hakuwa amekufa…nahisi kuna kosa lilifanyika…lakini hata polisi..hebu niambie  ilikuwaje..na ni nani aliyeongozana na polisi kumleta huyo mama huku, maana wakati analetwa huyo mama mimi sikuwepo..?’ akauliza.

‘Polisi walitaka kumfunua uso yule mama, ili waione sura yake,..hakuna aliyeweza, yule aliyejaribu wa kwanza, alikula muereka..yaani wakati anamfunua, sijui ilitokeaje, kilichoonekena ni yule polisi kudondoka chini, na mawnzake akataka kutimua mbio…na huyo aliyedondoka chini,  akawa kama kachanganyikiwa, nasikia hadi sasa hayupo vyema…’akasema

‘Huyo polisi aliyedondoka chini, ndio kachanganyikiwa,..mbona mambo ya ajabu hayo…?’ akauliza nesi.

‘Ndio sisi wenyewe tulimuona wakati anaondoka, alionyesha kuwa na wasiwasi, anaangalia huku na kule kama mtu aliyechanganyikiwa, na sio huyo tu, kila aliyejaribu kumfunua huyo msms kabla ya hilo tukio la moto, alipatwa na masahibu kama hayo …ya kuchanganyikiwa..’akasema jirani

‘Mhh, ina maana huyo mama ni mtu gani, na kwanini watu wachanganyikiwe…nakumbuka iku ile, …eeh, nakumbuka hata mimi kipindi kile nilijaribu kutaka kumfunua… kumuona sura yake, alitaka kunipiga,akawa anadai mimi nina mtoto wake..kumbe kama ningetaka kumfunua kwa nguvu, na mimi ningekuwa matatani…’akasema

‘Kwa wanawake hana matatizo sana na wao, ..ila hakuna aliyebahatika kumuona sura yake..hadi sasa….’akasema

‘Mhh, mnanipa mtihani…maana kiukweli, ..alipoletwa hapa alionekana ana majeraha, na ilitakiwa kuitibiwa hayo majeraha, ..hakukubali kufunuliwa usoni,.., tulihangaika, baadaye docta akasema tumuache kwanza, baadaye docta akaenda peke yake sijui alimfanya nini, akakubali…

‘Docta mwanaume..?’ akaulizwa

‘Ndio..maana ndiye docta bingwa wa kitengo hicho…akamsafisha yeye mwenyewe na kumtiibia, na tangia hapo hakuna anyekubaliwa kumuona zaidi ya huyo docta…sasa sijui..hata docta mwenyewe hataki kusema huyo yupoje , anafananaje..ila kasema tu huyo mama hana kumbukumbu, hajitambui… na tusimlazimishe kumfunua atamuhudmia yeye mwenyewe…’akasema.

‘Mhh..kweli kaamua,..hata mimi niliekuwa nikiishi naye, hakutaka kabisa nimuone sura yake, hata mfanyakazi wetu aliyekuwa karibu naye, anasema hajawah kuiona sura yake..sasa mnamtibiaje kama nyie manesi, maaana si anahitajia huduma kama docta hayupo…poleni sana, yaani tangia tugfike hapa tumeona watu karibu wanne wanavuja madamu…utafikiri kuna vita ya kukatana na mapanga, …kuna nini jamani?’ akaulizwa dada mtu

‘Mhh..sisi tunafuata alivyosema docta…tumezoea  hayo,  maana kwenye hii hospitali tunapokea watu wenye matatizo kama hayo wengi tu hasa kina mama, na akina baba pia…unajua huku watu wanavuta bangi ovyo..basi kupigana ..na kupigana kwao huku ni kwa mapanga..wanakatana utafikiri nini..Kwakweli wagonjwa kama hawo siku hizi ni wengi, wa majeraha, kuungua..basi naona kama ule ubinadamu huku, mmmh, hakuna..sisi tumezoea kucheza na damu za watu…na unachojali ni kusaidia…ndio kazi tutafanyaje’akasema nesi.

‘Kwahiyo sasa tutamuonaje,..maana sisi ndio kama ndugu zake tumeleta chai..na matunda….na tunataka kujua mchana itakuwaje..?’ akauliza dada mtu.

‘Sasaaaah, oh,....sijui kama nitakubaliwa mkamuone, maana hakuna mtu anayeruhusiwa kumuona zaidi ya huyo docta wake, na docta wake, keshatoka…ngoja nikafuatilie nione tutafanyaje, mnasema anaitwa nani vile?’

‘Jina lake?...hutaamini hakuma mtu anayejua jina lake, ukumbuke yeye ukimuuliza anaitwa nani hajijui sana, hajui kabisa wapi alipotokea, ina lake nani…na nini kilimkuta huko alipotokea, hasemi, hajui…., sisi tunamuita mama wa mitaani, wengine mama mwenye mkono wa Baraka na sasa wanamuita mama mwanga…na zaidi yeye anaweza kukuambia nataka mtoto wangu hilo ndilo hitimisho lake baada ya hapo hataongea tena…’ akasema dada mtu

‘Haya ngoja nikaulizie halafu nitawajulisha nini kinaendelea..’. Huyo nesi akaondoka kwa muda na baada ya nusu saa akarudi, na kuwajulisha kuwa huyo mgonjwa anahamishwa kwenda wodini, lakini kwa hivi sasa hatakiwi kusumbuliwa na ile hali mbaya imeshaondolewa kilichobakia ni matibabu ya kawaida tu , kwa siku hiyo hawataweza kumuona labda waje siku nyingine kumwangalia na kama kuna lolote jipya atawajulisha.

 Basi mama na mwenzake wakawa hawana la kufanya, wakaacha vile walivyokuja navyo kwa huyo nesi,  sasa wakawa wanaaga kuondoka, na ndipo nesi akakumbuka kuulizia

‘Mnasema shemeji kabakia na mtoto, yeye hakutaka kuja huku…?

‘Hahaha hivi sikukuambia,..unajua siku walipomleta huyo mama huku, shemeji yako alichukuliwa na huyo mama, akiwa hajitambui…’akasema

‘Makubwa ….kwanini, au yeye alitaka kumfunua huyo mama yakamkuta yaliyomkuta huyoo polisi?’ akauliza huyo nesi.

‘..hutaamini, unajua shemeji yako haamini sana hayo mambo…polisi wakataka kumtumia yeye, nasikia ..maana mpaka sasa hataki kuhadithia, ilikuwa hivyo hivyo..akataka kumfunua, kilichomkuta ndio hicho…akapoteza fahamu, sasa tangia arudi, kabadilika ghfla, na wala hataki kusema ni kwanini…’akasema

‘Mungu wangu..ina maana na yeye atakuwa kachnganyikiwa kama  huyo polisi, sasa mtafanyaje…mleteni huku hospitali tumchunguze…’akasema nesi.

‘Tulimshauri hivyo hakukubali na hataki kabisa kuja huku,..unajua alichosema..’akasema

‘Ehe…kasemaje?’

‘Sitaki kumsikia huyo mama, na sitaki nimuone huyo mama hapa nyumbani kwangu tena…kama ni mwanga akawangie huko huko…mimi simtaki, sitaki hata mtu kuongelea kumhusu yeye, kama nyie mnakwenda kumuona nendeni…’akasema dada mtu.

‘Mhhh, lakini yeye alikuja na huyo mama huku, akiwa hajitambua au akiwa na akili zake…maana mnasema alikuja na huyo mama usiku au sio..sasa alikuwaje?’ akauliza

‘Alichukuliwa akiwa hajitambui, tuliambiwa na askari aliyekuja naye huku, kuwa alizindukana huku huku hospitalini, kwahiyo dakitari alimchunguza akasema yeye hana tatizo lolote....sasa tukimuuliza mwenyewe hataki kuongea lolote lililotokea huku..’akasema

‘Jamani shemeji yangu….mpeni pole, nitakuja kumona..’akasema nesi.

‘Yaani hata ukija usije kuliongeela hilo, mtakosana.. hataki kabisa kusikia habari za huyu mama, na amesema hangependa huyo mama akipona arudi tena kwake, sijui ni kwasababu ya hilo tukio kuwa linaweza likaleta balaa jingine, kuwa hawa watu wanaweza wakaunguza nyumba nzima…lakini nadhani kuna kitu kingine ambacho hataki kutuambia kwa sasa….’akasema dada mtu.

‘Sasa itakuwa ni kitu gani?’ akauliza nesi.

‘ Unamjua shemeji yako, hapendi kuongea kitu kwa kubahatisha, anaweza akasikia jambo aua kahisi jambo…akakaa kimiya… hawaambii, eti mpaka apate uthibitisho…ngoja tusubiri hadi hapo atakapotaka kutuambia, lakini nina uhakika kuna jambo ambalo linamkera na huenda linahusiana na huyu mama…maana kuna muda nilimuona kiongea pake yake..na akaonekana ana jaziba kweli kwelii…mmh mpaka niliogopa…lakini ngoja tusubiri tuone…’akasema

‘Kama ni hivyo kuna tatizo..haya jamani kama ukiona vipi niambie nije nione naye mwenyewe..’akasema mdogo mtu.

‘Usijali yatakwisha hayo..wewe wajibika tu…, kwaheri nenda wasije wakakufukuza kaza..’ wakaagana na nesi akarudi wodini sasa akiwa na jambo kichwani;

 ‘Huyo mama ni nani..,na kwanini hataki kuonekana sura yake…na mbona docta kamuona na hajapatwa na lolote, na kwanini docta naye hataki kusema huyo mama yupoje usoni..na kwanini…na kwanini…’ Basi nesi akawa na maswali mengi kichwani hadi anafika ofisini kwake.

‘Nesi mkuu, docta alikuwa anakuita…’akashituka kutoka kwenye mawazo

‘Kuhusu nini?’ akauliza.

‘Kuhusu huyo mama..’akaambiwa na msaidizi wake, na nesi kusikia hivyo mbio mbio akakimbilia huko alipo huyo mama, huku mwili ukimsisimuka….


WAZO LA LEO: Mtoto kama alivyo hajui lipi jema na lipo ovu, mwalimu wake ni wewe mzazi, na jamii inayomzunguka.  Mtoto huyu akiumwa, anahitajia huduma,..na huduma nyingine ni za haraka, wewe kama mzazi ukikosea ina maana umeharibu afya,..au hata mstakabali mzima wa mtoto huyo,..kulea watoto ni jukumu la kila mtu,na taifa kwa ujumla, sasa najiuliza inakuwaje mtoto aumwe, au ahitajie matibabu ya haraka, bado kuwe na kuzungashana. Waheshimiwa wakiumwa haraka wanakwenda kutibiwa ulaya au nchi za nje, basi hawa watoto ambao ni wakubwa watarajiwa kwanini tusiwape kipaumbele….kiafya, na kielemu…kusiwe na ubaguzi wowote.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hi there! Quick qսestion that's entirely off topic.
Do yοu know how to make youг site mοbilе frіendly?
My site looks weird when browsing from my iphone 4. I'm trying to find a template or plugin that
might be ablе to fiх this isѕue. If you have any recommendations, please share.

Thаnk уou!

Ѕtop by my ԝeb site; temp