Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, March 3, 2015

NANI KAMA MAMA -39


‘Unajua kuna tetesi kuwa huyu mama hakutaka sura yake ionekane na mtu baki, na nijuavyo mimi, watu hawa wapo tayari kuonekana..sana sana ni ndugu zake au jamaa zake wa karibu kama nyie mliokuwa mkiishi karibu naye au sio...

‘Na wenzangu wakati nafika pale nimewasikia wakikuhoji kama uliwahi kumuona huyo mama sura yake, na ukawa unawaelezea alivyo, au..sio, kwahiyo kwako wewe ni rahisi, maana unamfahamu sio sura ngeni kwako..au sio’akasema

‘Rahisi kufanya nini, ..afande sijakuelewa, …maana swali kama hilo limekuwa ni kero, wenzako wameniuliza nikajaribu kuwaelezea ukweli, lakini hawaniamini,..sasa sijui mnataka nini…?’ akauliza

‘Sio tatizo kubwa…kama nilivyokuambia sisi japo ni askari, lakini, tunahitajika kuona haki na utashi wa mtu unaheshimiwa…sio vyema kumfunua mtu , hata kama keshakufa, ..si ndio..sasa nikaona wewe utusaidia,….kwa hilo’akasema

‘Afande mimi , naona nyie mnakwepa majukumu yenu, mimi, sioni tatizo lipo wapi,…’ akasema na akacheka kicheko cha kebehi,

‘Hahaha afande, nimeshawashitukia…’akasema

‘Sikiliza kwanza…’akasema afande

‘Mhh, afande, naona umeshaingiwa na uwoga…, kama huyo mwenzenu kajaribu kumfunua yaka mkuta yaliyomkuta, mnataka na mimi yanikute hayohayo au sio…afande mimi siwezi kufanya hilo unalotaka wewe…’akasema huku akirudi kinyume nyume

‘Unajua , unielewe, mimi ni kiongozi wa hiki kikoso kilichofika hapa, kama kiongozi natakiwa kuwa muadlifu, hata mimi nimeliona hilo, kuwa sio vyema, kumfunua…ndio maana kwa busara zangu, nikaona wewe utusaidia kwa hilo…’akasema

‘Eti nini..afande kwani kuna taizo gani..huyu mtu keshakufa, hata ukimunnua kwasasa..hana..hawezi….oh, hata sijui nisema nini, ila kiufupi mimi siwezi kuifanya hiyo kazi, maana hata mimi hakuwahi kunionyesha sura yake..’akasema

‘Basi nikawa na wazo pia,, mke wako…yeye ni mwanamke mwenzake, au sio..lakini pia nikaona je atakuwa na ujasiri wa kufanya hivyo..kwahiyo kura ikaangukia kwako,…wewe si ulikuwa unaishi naye , umebahatika kumuona, unamfahamu …kwahiyo sio kazi sana kwako..eeh?’ akasema huyo afande kwa sauti ya chini kwa chini.

‘Afande, kwanza kiukweli hata mimi  kichwa kinaniuma sana…naomba nikatafute dawa, …unajua nikuambie kitu kama huyu mama angelikuwa yupo hai angeshanitibu hiki kichwa, huwa inatokea hivi,…nina tatizo ya maumivu ya kichwa, ..sasa yeye alipofika hapa nyumbani , kila kikianza basi namwambia, akikishika tu kinapona…, ‘akasema

‘Basi kumbe utatusadia sana, maana wewe ukimshika ni sawa nay eye kakushika, au sio.,…kwako haitakuwa ni shida….wewe fanya hivi..’akageuka kuangalia huku na kule, akajikuta wenzake wapo mbali kidogo, akasema

‘Mpiga picha yupo wapi tena…hajarudi kutoka huko nje, ..muiteni, haraka, maana hili zoezi linachelewa…’akasema

‘Sasa ndugu.., tusaidie kwa hili..maana hili ni muhimu sana, wewe, nenda kamfunua halafu mpiga picha atafanya kazi yake na tumemaliza kazi, unasemaje?’ akawa akama anauliza

‘Afande hunanielewa, hapa kichwa kinaniuma kweli kweli…..sitanii, mara nyingi kichwa changu kikiuma hivi, akinishika kichwa huyo mama kinapona, sasa ndio huyo..’akasema na kugeka kumuangalia huyo mama pale alipolazwa.

Aligeuza kichwa kuanglia pale alipolazwa huyo mama, …ile kugeuza kichwa kuangalia,..akashituka,..unajua kushituka, ..binadamu anapoona kitu cha kutisha huwa anashituka kisai kwamba mwili unajirusha bila hata kutarajia,…ni kama vile mtu kahisi kakanyaga nyoka, basi ndivyo jamaa alivyoshituka.

Wakati huo afande alikuwa karibu yake, alishamsogelea kumshika mkono ili asogee pale kwa huyo mama aweze kuifanya hiyo kazi, sasa ule mshituka wa baba mwenye nyuma, ukamfanya afande ambaye alishaingiwa na kitu mwilini, kutokana na yalitokea kwa mwenzake, …

Afande huyu naye alijikuta akiruka hatua mbili nyuma kama kukwepa kitu, huku akimuangalai baba mawenye nyumba na jicho la kujiiba likitizima kule alipokuwa huyo mama, huku akauliza;

‘Kuna nini…?’ akauliza

Tuendelee na kisa chetu

******************

Baba mweney nyumba alibakia kapanua mdomo, na jicho limemtoka akainua mkono na kushika kichwa, kilichofuata hapo hakijua, kwani giza lilitanda usoni, akajikuta akizama kwenye giza….akadondoka chini.
Afande akabakia kaduwaa, akageuka kushoto na kulia, halafu akahesabu hatua moja mbili tatu akajikuta yupo nje, alipofika nje, akasema;

‘Gari la wagonjwa haraka…’akasema na wenzake wakawa wamebeba zile zana za kubebea wagonjwa, wakaekea ndani, walipofika hawakukuongeja nini, wakajua ni hayo maiti yanahitajika kubebwa, lakini cha ajabu wakaona mu mwingine kalala sakafuni.
‘Afande…na huyu naye ?’ akauliza
Yah, ..wote…hatuna muda wa kupoteza…’akasema na baba mwenye nyumba akainuliwa na kuwekwa kwenye machela, huku nyuma yake ukichukuliwa mwili wa huyo mama na wote wawili wakaingizwa kwenye gari la wagonjwa ambalo lilishafika muda mchache uliopita kwa ajili ya kubeba mwili wa huyo mama.
‘Mume wangu kafanya nini?’ ilikuwa ni kelele ya mama mwenye nyumba…
‘Kapata mshituka tu, hana tatizo lakini ni muhimu twende naye huko mele atatusaidia kazi ya kuitambua maiti ya huyo mama..’akasema huyo afande
‘Kama ni mshituka tu kwanini tusimfanyie huduma ya kwanza?’ akauliza mtu wao mwingine
‘We..niachie hii kazi, huyo hana tatizo…namuhitajia sana, atazindukana tu, waambie wenzangu waendeele sisi tunaiwahisha hii maiti muchwari na huyu jamaa anaisaidia polisi..’akasema na kuamrisha gari kuondoka.


                                          **********
‘Naomba unielewe sana kuwa nafanya hili sio kwasababu sikupendi, ila imenibidi nifanye hivyo, kutokana na mambo yaliyo juu ya uwezo wangu…sina zaidi ya kukueleza ila usihangaike kuja nyumbani kwani sasa hivi mimi ni mke wa mtu. Kwaheri ya kuonana!

                                              *****
Haya yalikuwa maneno mafupi katika kibarua kidogo alicholetewa na jamaa asiyemfahamu vyema….alionekana kutisha, na hakuonyesha hata dalili ya tabasamu au urafiki…akanyosha mkono na kumkabidhi hiyo barua…, na jamaa akaipokea,…akaitoa kwenye bahasha, na kukuta hicho kikaratasi, …aliyaona maandishi kama yanapandana, lakini akajitahidi kuyasoma…

Mara ya kwanza alihis anasoma ujumbe wa utani , akarudia mara ya pili nay a tatu, akili ikawa haifanyi kazi! Akainua uso kumuangalia mtu aliyempa hiyo barua, kama kutaka maelezo, na yule mtu alikuwa kama gogo lililosimama, haliongeai halipepezi macho…limekunja ndita usoni,…akainama tena kukiangalia kile kikaratasi, na mara akasikia sauti ya huyo mtu… akisema;

‘Mimi naondoka,..muda unakwenda sana, nahitajika kazini kuja hapa nimejiiba tu kwasababu ya madamu… kama una lolote unaweza kuniambia, au kunipa barua nimfikishie mwenyewe…’saui kutoka kwa huyo mtu ambaye aliongea kwa sauti kavu, ya ukakamavu kama ya askari aliyekariri maneno….

‘Kwani ni nani kakupa hii barua?’ akauliza

‘Kwani hajaandika jina lake…ni madam,..umenielewa?’ akaulizwa na kusema.

‘Madamu…ni nani madamuu…’akasema huku akiiangalai tena ile barua, au ujumbe na kuangalia kwa chini, akaona kifupisho ya majina mawili,…mimi T

Hakuna tena ile lugha ya upendo, aliyoizoea wakati wanaandikiana, …Mimi nikupendaye, mimi barafu wa moyo wako, mimi asali …honey sweetie..’

 Na jaama akaishika tena ile karatasi na kusoma tena kuhakikisha kama kweli ndio yeye, akasoma hadi mwisho wake, na chini ya ile barua akaona  mimi T…na mwandiko ni ule ule,..hakuna ubishi imetoka kwa kwa huyo huyo mpenzi wake....akashika kichwa..

‘Kwanini anifanyie hivi.…hapana..kwanini..una-una..uhakika ni yeye,..una uhakika..ni kweli ?’ akamsogelea huyo mleta barua na kumshika akawa anamsuka suka, lakini ni kama mtu anashika shika jiti nene, kama mbuyu, halitikisiki au hata kuinua mkono kujaribu kujitetea, jamaa baadaye akaona ni uzia akasema;

‘Unafanya nini,  huoni kama unanipotezea muda wangu…wewe vipi..mimi ni mjumbe tu..hayo yenu hayanihusu…unasikia sana…nikuashauri kitu, usijaribu kushindana na matajiri…na ni bahati yako tu...sema kwa vile keshaoa…hana baya na wewe tena…muhimu achana kabisa na madamu, muone kama hakuwepo duniani….’akasema huyo jamaa na kugeuka kuondoka zake.

‘Tajiri wa ng’ombe….kaizima nuru ya moyo wake…sasa iliyobakia kwangu ni aibu, maumivu na mateso...sasa ni mateso, nitauweka wapi wapi uso wangu…’akawa anajiuliza moyoni.

Ilikuwa ni siku ambayo hataweza kuisahau maishani mwake, siku ambayo alihisi maumivu makali moyoni, ilikuwa kama mtu aliyezamishiwa kisu kwenye moyo wake, na akawa sasa anakichomoa kwa taratibu, ili ahisi maumivu yake kidogo kidogo.

Ni siku ambayo alijiona kama mtu aliyevuliwa nguo mbele ya kadamnasi…na akawa hana cha kujifunika, na waliokuwepo hapo ni mkwewe na mabosi wake wa kazi na watu anaowaheshimu, ..hana cha kujifunika…alijiona hivyo kwa vile alishatamba kwa marafiki zake, kuwa hatimaye yule mrembo ambaye kila mtu alikuwa akimtaka sasa yeye keshampata, kudhihirisha pendo lao.

‘Niliwaambia mimi, yule ni wangu…nampenda na yeye ananipenda, hakuna wakutuvurugia pendo letu..utajiri…hata uwe na mapesa vipi huwezi kushindana na nguvu ya pendo…Tausi ni wangu, leo hadi kiama..nikimkosa bora nife….’akawa anatamka hayo mbele ya watu.

 Usiku huo, alikuwa na suti nzuri ya kuazima, maana pamoja na kujipenda, pamoja na kupenda kuvalia suti, lakini siku hiyo alihitajia suti maalumu,suti ambayo, aliitamani sana kuvaa siku hiyo, na alishasema siku akioa atatafuta suti kama hiyo, hata kama hana pesa,ataiazima, na kweli siku hiyo akaipata kwa mmoja wa maraiki zake, na rafiki yake akawa radhi kumuazima…na hapo aliiona suti hiyo ikimeta meta kama ina vita..hakuamini..mbona leo ni zaidi ….

‘Na wewe bwana, zile suti zako mbona nzuri tu..hii ina nini cha zaidi..?’ rafiki yake akamuuliza

‘Hii ina kitu muhimu sana, moyoni mwangu, usijali, sitaiharibu, si  unanifahamu utanashati wangu..’akasema

‘Aaah, mimi hilo sina wasiwasi nalo…nakuaminia hata ukitaka kukaa nayo mwezi sina shida..au hata ukitaka tubadilishanae na moja ya suti zako nipo tayari unasemaje…’rafiki yake akamwambia

‘Hapana itatumika tu kwenye ndoa, baada ya hapo nitabadili na kuvaa suti zangu..nitakurudishia suti yako….’akasema

Basi siku ile akaawaambia marafiki zake maalumu wa karibu na jamaa zake wa karibu, akitamba kuwa, yeye atamuoa  yule aliyempenda, usiku huo kwa vyovyote iwavyo, na kuwa wazazi wa huy binti na huyo tajiri hawawezi kuwazuia kwani walishapendana toka utoto.

Mashabiki walimwambia tena kuwa jamaa ambaye wamesikia anataka kumuoa huyo binti ni yule tajiri wa ng’ombe, na kijijini hapo anaogopwa kwa fujo zake, na asipoangalia anaweza akapata kipigo ambacho hatakisahau, au akauwawa, kabla hajatimiza azima yake.

‘Bwana hakuna ndoa ya kulazimishana hapa, mimi na Tausi tumependana toka tukiwa matumboni mwa wazazi wetu….huyo na utajiri wake, akatafute mke mwingine, na hawezi kunifanya lolote..’akatamba.

Aliwaambia kuwa ndoa ni kati ya mke na mume wanaopendana, yeye na huyo binti wanapendana, hadhani kuwa binti huyu atamsaliti kwasababu ya utajiri wa huyo jamaa…

Basi siku kabla ya siku hiyo alishakutana na huyo mchumba wake wakapanga, vikapangaika na binti akakubaliana na kila kitu,  kwani alishamdokezea kuwa kuna tajiri ameshaongea na wazazi wake, anataka kumuoa, lakini hajajua ni lini.

‘Sasa sikiliza, huyo mtu hatuwezi, cha muhimu, usiku wa leo…tufunge ndoa ya haraka,…mimi nimeshajipanga, kila kitu kipo tayari,  ongea na yule mjomba wako mnayelewana naye, mje kule kwa yule kiongzi wa dini, tutafunga ndoa halafu tunapotea kwa muda…’akasema

‘Mhh hiyo itakuwa ngumu, viongozi wote wa dini wanamfahamu baba yangu, na wanamuogopa sana huyo tajiri, si unajua ndiye mfadhili wao…,..mimi hilo naona haliwezekani..’akasema

‘Kwahiyo sasa unataka tufanye nini?’ akamuuliza mwenzake

‘Labda tufunge ndoa ya bomani, maana kila siku wanatangaza kuwa hakuna kulazimishana kwenye ndoa..na wanajua huku kijijini kuna tabia ya wasichana kuolewa na watu wasiowataka, tutawaambia ukweli..najau wao hawatakataa, na tutakuwa na kinga kisheria…’akasema

‘Basi hilo niachie mimi, maana kiongozi wa serikali za mitaa ni rafiki yangu hilo litafanikiwa, kazi itakuwa kwako…na yule mjomba si umesema hapendi wewe kuolewa na huyo jamaa kaongee naye umuweke sawa awe mwakilishi wako, au       sio..’akasema

‘Hilo halina shida, .., mjona atanisaidia japokuwa karibu watu wote wanamuogopa sana huyo tajiri, ila mjomba alishasema yeye hamuogopi….’akasema binti akiwa naye na hamasa,kwani kiukweli walikuwa wanapendana sana.

Basi jamaa akaenda serikali za mitaa, akaongea na jamaa yake, na jamaa yake akamwambia hilo halina tatizo, kwasababu hata yeye alishasiki tetesi hiz na hapendi binti mrembo kama huyo kuolewa na huyo jamaa kwani tabia za huyo jama ni chafu, ni mkorofi, mlevi, na anaringia sana utajiri wake wa ng’ombe.

Basi hilo hapo likaanikiwa na wakapewa kibali cha kwenda bomani kufunga hiyo ndoa usiku...

Usiku kucha jamaa hakulala , akikumbuka mipangilio yake ambayo alishaipanga, ni wapi wataenda baada ya kufunga ndoa yao, na kazi gani ataifanya ili waweze kuishi. Kwahiyo hakuwa na wasiwasi wa maisha ya baadaye. Alikuwa na akiba ya kutosha aliyochangiwa na wafanyakazi wenzake, alipotoka huko mjini, alichukua likizo ndeu kidogo…akaamua pia kuuza ngombe zake alizopewa katika familia yao.

Aliamua kuziuza zote kwani hakutarajia kurudi nyumbani hapo karibuni, kwasababu aliwajua mzazi wa Tausi wanavyomuogopa huyo mtu. Wao kuna muda walitaka kweli binti yao aolewe na naye lakini alipojitokeza huyo jamaa, wakageuza msimamo kwa vile walimuogopa sana huyo jamaa na alikuwa akiidai hiyo familia pesa ningi tu…

Na huyo jamaa tajiri alishatamba hapo kijijini kuwa Tausi ni wake, na yoyote atakayejitokeza kumchumbia Tausi, atapambana naye, basi wanaume wote waliokuwa wakimnyemlea huyo binti wakafyta mkia,akabakia jamaa yetu huyu…..

*************

Yeye na Tausi, walianza kupendana wakiwa wadogo sana,wakiwa shuleni, walikuwa wakipitiana kwenda shuleni, na hakuweza kuondoka kurudi nyumbani mpaka Tausi awe ametoka darasani kwao kwani hawakuwa wakisoma darasa moja, yeye alimtangulia Tausi kwa madarasa mawili.

Alipomaliza shule, akawa akimsindikiza Tausi shule na muda wa kutoka ukifika anakwenda hadi hapo shuleni kuhakikisha ametoka salama na kuhakikisha kuwa kamfikisha nyumbani kwao salama. Hali hii wazai waliiona na walijua ni utoto, kwahiyo hakuna aliyeitilia mashaka.

Maisha yalivyo hayatabiriki, wazazi wa Tausi wakakumbwa na balaa la njaa, wakajikuta wakiuza mifugo na kuandamwa na madeni mengi. Wakawa wanakopa kwa jamaa mmoja mwenye ngombe wengi, na waliposhindwa kulipa wakapewa masharti kuwa, wamuoze binti yao kwa huyo jamaa, na jamaa akawa tayari kuongeza ngombe wa ziada. Na wazazi wakawa hawana jinsi, ila kumuoza binti yao kwa huyo jamaa.

Tausi alipofahamishwa, aligoma kabisa, lakini alivyoelezwa hali halisi, ikabidi anywee, kwani wazazi ndio hao, wanadaiwa na usalama wao upo mashakani. Alipoenda kumueleza mwenzake hakumuelewa, na ndipo mpango wa ndoa ya harakaharaka ikapangwa, hili lilifanyika kwa siri sana ila kwa wapambe wachache sana waliojua,hata Tausi mwenyewe alijikuta akiletewa gauni la harusi na kuambiwa avae.

‘Kwani mama nilishawaambia…halafu nimesema nahitajia muda wa kulifikiria hilo..’akalalamika

‘Sikiliza mwanangu hapa tulipo tumewaza sana, tukaona kwanini…ngoja tu uolewe na mpenzi wako… anakusubiria..’akaambiwa

‘Mpenzi wangu ananisubiria..mama unatania, au unazungumzia huyo …..mtu ninayemchukia…, kweli mama..ooh, mama, lakini huyo jamaa si atawafanyia ubaya hata kuwawaua……?’ akauliza

‘Ndio hivyo….lakini usijali mwanangu, wewe vyaa hilo gauni la harusi twende , wanakusubiria..’akaambiwa, na pale alipo hakuamini…, hakuwa na uhakika, akauliza tena.

‘Mama ni kweli ni yule mchumba wangu ninayempenda…kaninunulia gauni hili la harusi….mmmh,…?’ akauliza akiwa na raha huku akivalia gauni hilo la harusi

‘Ndio huyo huyo..sisi tumeona tukuozeshe  tu kwa huyo, hatuna la kufanya…’akaaambiwa, basi akatoka nje na kukuta gari likimsubiria,..moyo bado ulikuwa hauna uhakika, akaingia kwenye gari, na kuondoka hadi huko ambapo hakujua ni wapi.

Akajikuta anafika kwenye eneo la mkuu wa dini, akaingia ndani, na mbele yake akamuona huyo tajiri wa ng’ome akimsubiria…akasita akitaka kugeuka  na kukimbia, lakini alipogeuka akakutana na walinzi wa huyo jamaa wakiwa nyuma yake...kipindi hicho huyo jamaa alikuwa tajiri kweli,  japokuwa baadaye mifugo yake ilikuja kuingiliwa na magonjwa, ikafa karibu yote, akawa hana kiu tena, lakini ilitokea baadaye sana.

Mwanadada huyu akageuka upande mwingine akawaona wazazi wake wakiwa wameinamisha vichwa, hawakutaka kumuangalia, …akajikuta machozi yanamtoka, akakumbuka ahadi yake na mtu anayempenda,…akakumbuka kuwa mwenzake yupo anamsubiria, akageuka kutaka kukimbia lakini sura zilizokuwepo nyuma yake,zikawa zinatisha..akawa kasimama.

Pale alipo,alishindwa afanye nini, na wazazi wake walikuwa wamezungukwa na askari wa huyo jamaa, kwani huyo jamaa alikuwa na askari wanaogopewa sana hapo kijijini, kutoka na utajiri wake wa ng’ombe.

Mama akajitosa akamsogelea binti yake na kumnong’oneza,…

‘Binti yangu hapa tulipo tuna mawili, ukubali uolewe, au tuuwawe..na mali yetu kidogo iliyopo inafirisiwa,…hata kile kibanda tunachoishi kitachukuliwa… kwahiyo tunakuomba utuokoe, kwa kukubali kuolewa na huyo jamaa, …’akaambiwa na mama yake akitoa machozi, akageuka kumuangalia baba yake baba yake alikwua akinamisha kichwa chini, hataki hata kumuanglia..ikawa hana jinsi kakubali kuolewa.

Ndoa ikafungwa…na akajikuta akipelekwa kwenye makazi ya huyo tajiri, na asubuhi ndio jamaa akapata hiyo barua….

***********

Jamaa alisubiri toka usiku kucha,…hadi asubuhi akiwa hajakata tamaa…na alipopokea hicho kikaratasi ndio akaamini kuwa sasa ile ndoto yake imeyeyuka mchumba hanaye tena, keshasalitiwa.

Akawa hatoki ndani, hataki hata konana na watu subuhi mpaka jioni na jioni ilipofika akatafuta klevi alikunywa mpaka akawa hawezi kunywa tena,..na kila akikumbuka ile barua ..barua ambayo kwake aliiona kama kisu kikali kilichopenyezwa kwenye moyo wake…alijikuta anaumia moyoni, ...akitamani apate sumu anywe…

 Basi iku ya pili yake akaona hata…ngoja akaamini kwa mcho yake,…akaona labda ni uwongo,akajizoa zoa, na ulevi wake akatembea hadi nyumani kwa huyo binti…, alipofika alikuta wazazi wa huyo binti hawapo, akaambiwa bado wanasherehekea, kwani ilibidi wafunge ndoa kwanza ya harakaharaka, kwani wamesikia kuwa kuna mpango wa kumtorosha huyo binti, halafu sherehe ikafuata kesho yake!.

Jamaa alilia mbele ya watu aliowakuta hapo kama mtoto…., akalaani na kulaani kuwa wamemfanyia unyama ambao hataweza kuusahau maishani, Na akaapa kuwa siku akimuona huyo mwanamke atamfanyia kitu kibaya sana kwa kumsaliti. Akaondoka hapo na kurudi nyumbani kwake.

Jamaa alikaa wiki mbili akiwa hataki kula, akawa kama mgonjwa, na hali ilipomzidi jamaa zake wakaona watafute njia ya kumuhamisha eneo hilo..na halia liyo nayo waliogopa kuwa hataweza hata kurudi huuko kazini anapofanyia maana kwa kipindi hicho alikuwa akifanya kazi ya kuajiriwa huko mjini…mpango ukafanya akahamia kijiji cha jirani, karibu na mjini.

Akiwa katika mateso haya ndipo akakutana na mwandada aliyekuja kumbadili, akamliwaza na kidogo kidogo akaanza kuyasahau maisha..na kujaribu kumsahau Tausi.Mwanadada huyu kumbe naye alishakutwa na mkasa kama huo uliompata jamaa yetu.

Siku alipohadithiwa yaliyompata huyo dada, ndio siku akagundua kuwa ubaya sio kwa wanawake tu hata wanaume wamo…kwani mdada huyo yeye aliachwa akiwa anasubiria harusi ilishapangwa na mdada akawa yupo na watu wakimsubiri bwana harusi aje wafungea ndoa,  jamaa hakuonekana kabisa.

 Mwanadada huyu na wazazi wake wakasubiria mbele ya mkuu wa dini, na mume wa kumuoa, hakuonekana…mdada akaletewa taarifa kuwa huyo mchumba wake kaondoka usiku na aliyekuwa rafiki yake, na wameshafunga ndoa tayari , mdada aliposikia hivyo akadondoka na kuzimia.

Mdada alipopata fahamu akajipa moyo, kidogo yeye alikuwa jasiri akayafanya kama yakupita tu, japokuw amoyoni alikuwa akisononeka, na muna muda aliapa kuwa hataki kuolewa tena, ..siku , masiku yakapita ndio akakutana na huyu jamaa yetu.

Ikatokea kuzoeana, na siku moja kila mmoja akawa anaongelea maisha yake, jamaa akakisikia kisa cha huyu mdada, …akaona kumbee, basi wakaanza kupendana, na wakajikuta kweli wameivana…basi kila mmoja akajaribu kuyasahau yaliyopita na hatimaye wakakubaliana kuowana.. kuna siku alipata taarifa kuwa Tausi amefariki dunia..hakutaka hata kwenda huko kijijini kuhudhuria mazishi yake….sasa

Mara akaona maiti ikibebwa na kuweka pembeni yake, na akawa anajiuliza ni ya nani, akasikia watu wakisema, na akilini mwake, akahisi, ..

‘Ndo Tausi kaletwa hapa, kwanini waniletee mimi, ..mimi sio mume wake…’akasema lakini hakuna aliyemjali….

Mara akasikia;

‘Hajafunua macho lakini anaonekana yupo sawa..’alisikia sauti na harufu kali ya dawa akafungua macho…akahisi mwanga mkali machoni, akageuka kushoto, akaona kama watu wamelala…akataka kujiinua kichwa kikawa kinamuuma..lakini sio sana, akakumbuka ….kumbe alikuwa anaota, ooh, ina maana hiyo ilikuwa ni ndoto, mbona inafanana fana na ukweli!

Oh, ina maana kweli ni ndoto…mmh, ina maana kumbe Tausi…alifanyiwa hivyo lakini hapana asingelikubali, hata, yeye ni msaliti tu, kwangu yeye ni msaliti tu akajikuta akisema,a kageuka huku na kule, akaona …kumbe kweli kaletewa maiti ya Tausi..hapana..ina maana ni kweli

‘Tausi wewe ni msaliti tu…wewe sio mke wangu…kwanini mnaniletea mke wa watu..?.’akauliza

‘Tausi ndio nani..?’ akasikia swali likiulizwa akageuza macho kushoto na kulia, halafu akauliza

‘Kwani nipo wapi?’ akaulizwa

‘Hospitali..’akaambiwa

‘Kwani mimi naumwa?’ akauliza, na mtu ambye alimtambua kama docta kwa mavazi aliyovaa akasema

‘Hapana ila uliletwa hapa ukiwa…hujitambui…’akaambiwa

‘Kwanini…hapana, ..mmh, ila kichwa kweli kinauma …saa naona kimepoa…kwani kumetokea nini, mpaka nipoteze fahamu au una maana gani kujitambua..?’ akauliza, na akawa katulia akiwaza, na kidogo kidogo akaanza kukumbuka

Akageuza kichwa na kuangalia kulia…akamuona yule askari…mkuu wa kundi lililofika , akaanza kukumbuka…kumbe alikuwa kaletwa hospitali lakini kwasababu gani…

Akakumbuka, …moto, ..akakumbuka  yule  mwanamama aliyekuwa akiishi naye,..kwanza akashituka, akakunja uso, akakumbuka kitu, akataka kusema kitu lakini akasita, akajiuliza ina maana kile alichokiona…huko,… ni kweli au ilikuwa taswira tu..

‘Tunakusubiri uitembue hiyo maiti…’akaambiwa, akainua kichwa, akageuka upande wa kushoto..akasema;

‘Maiti ya nani?’ akaulizwa

‘Yule mama aliyetaka kuungua na moto nyumbani kwako…sasa hivi anasubiri kuchukuliwa na madakitari kwa uchunguzi,…’akaambiwa akashituka, akageuza uso kwa mashaka na mara akaona kwenye kile kitanda, mtu kalazwa, na akahis huenda ni huyo mama, halafu akauliza;

‘Ina maana mimi nimelezwa na maiti…lakini mna uhakika…..?’ akauliza

‘Uhakika gani?’ akauliza,moyoni akasema, nilazima nijirizishe, nitajitahidi kujizuia, nitajitahidi kuwa imara ni lazima niione sura ya huyo mtu..ni lazima nihakikishe kuwa..kweli..ni maiti au ni taswira tu zinanijia kichwani,
Akajitutumua akakaa kitako, akasema;

‘Nipo tayari kuitambua lakini kwa masharti..’akasema

 Na yule askari akacheka na kusema;

‘Safi kabisa sema lolote..tupo tayari.., ilimradi umtambe na umpige picha, tunahitajia sura ya huyo mama, …..’akasema.

‘Sharti langu ni hili..nataka nikitambua…huyo…eeh, hiyo maiti..nataka niwe peke yangu, sitaki mtu mwingine humu ndani, pili siwezi ..sitampiga picha kwasasa mpaka nijirizishe..’kaema

‘ujirizishe….?! Ok, lakini sisi tunachohitajia ni picha yake….ni muhimu sana…kabla madakitari hawajamchukua, maana bado hajachunguza …na madakitari’akasema afande

‘Kwanini wanasubiria nini, na wao wana,uogopa..? akauliza na kabla hajajibiwa akaongezea kusema;

‘Masharti yangu ndio hayo,…lakini ni muhimu madakitari wangemuona kwanza, …hata hivyo kama ni yeye..ooh sijui,…ni bora tu ….iwe hivyo…sitaki na simtaki…ila kama ni muhimu  mpaka mimi nihakikishe, basi naomba mtoke nje, ..’akasema

‘Kama kweli ndio yeye!?…una maana gani, sisi tuna uhakika ndio yeye, tuna uhakika…wewe fanya ufanyalo lakini sisi tunataka picha yake kabla madakitari hawajamchukua tumewazua kwanza, hawajamkagua…walikuwa na kazi ningi ndio wamefika, na tukawazuia, …kamera hii hapa si unajua kuitumia…’akaambiwa

Akageuka kuangalia pale alipolazwa huyo mama…akatulia kwa muda akiangalia, akijitahidi kutokuogopa,  alikaa vile kwa muda, hadi aliposkia mlango ukifungwa nyuma yake, akabakia peke yake..


WAZO LA LEO: Hakuna anayeweza kujua shida, au maumivu, au uzuri au ubaya wa jambo mpaka limkute, ..mara nyingi tunaona kitu ni rahisi tu, au jambo au tukio au maumivu , shida..kwa mwenzako ni jambo rahisi tu na tunapeana moyo tu, kuwa jitahidi, ni kawaida tu, ni majaliwa ya mungu..jikaze, lakini ngoja yakukute wewe mwenyewe. Upendo wa kweli ni pale mwenzako yanapomkuta masahibu, mitihani, kuumwa, kuuguliwa, kufiwa, unakuwa msitari wa mbele kumsaidia mwenza wako, rafiki ako jamaa yako, kwa hali na mali kama vile limekukuta wewe, maana mwenzako akinyolewa na wewe tia maji, hujui lini litakukuta jambo kama hilo.

Ni mimi: emu-three

No comments :