Katika kupata ukweli wa tukio zima, askari
hawa waliotumwa waligawana katika makundi matatu, nia hasa ni kutafuta ukweli
na chanzo, cha watu kuuwawa ovyo, hasa wazee na akina mama kupigwa hadi
kuumizwa, na kwanini kunakuwa na ajali za moto za mara kwa mara.
Tulishaliona kundi la kwanza , ambalo
liliingia kumchunguza mmoja wa wahanga wa moto ambaye ni mama wa mkono wa
karama, au wengine kama wanavymuita, mama kutoka mbinguni, na wale wasiompenda
wakamuita, mama kutoka kuzimu…na kundi la tatu lilikuwa na kazi ya kuchunguza
chanzo cha moto.
Katika kundi hili la pili, ambalo kazi
yake ilikuwa kuwahoji watu ili kujua kinachoendelea hapo kijijini, …na
kuhusiani na hilo tukio la moto uliotokea karibuni hadi kueleta maafa.
Askari hawa wakiwa wanaendelea kumhoji,
baba mwenye nyumba maswali mbambali na kwa muda huo walikuwa wakitaka kufahamu
huyo mama mhanga wa moto ni nani…..
Akiendelea na maswali, askari kanzu
akamuuliza baba mwenye nyumba swali ambalo kwao lilikuwa na umuhimu wake,
japokuwa alitarajia kupata maelezo kutoka kwa kundi la kwanza lakini kutokana
na utata uliopo, akaona amuulize baba mwenye nyumba ambaye aliweza kuishi na
huyo mama kwenye nyumba moja kwa muda sasa…akamuuliza swali;
‘Je wewe uliwahi kuiona sura ya huyo mama…maana
nasikia muda wote kajifunika usoni?’ akaulizwa baba mwenye nyumba, na baba mwenye nyumba kwanza akatulia akijua
hilo swali sasa linamuingiza kwenye mtihani, na pia inawezekana ni mtego kwake,
akasema;
‘Mwenyewe umesema kuwa mama huyu muda wote
huwa anajiunika,sasa kama muda wote anakuwa amejifunika, mimi nitawezaje
kumuona sura yake..’akajibu akiwa kakereka na maswali ya mwanzoni ambayo
hakuyaenda.
‘Hivi ni kweli mtu mumeishi naye nyumba
moja karibu miaka mingapi,…akawa anakulelea mtoto wako…mkazoeaan akawa kama
mmoja wa familia yako, ina maana haikutokea hata siku moja kuiona sura yake au
ni kwa vile hutaki kutoa siri zake, labda kwa kujali utashi wake…?’ akaulizwa.
‘Nikuambie ukweli, akina mama kama hao
wanakuwa makini sana…inaweza ikatokea bahati mbaya kama unavyosema,..kwa bahati
mbaya,na kwa vile ni kwa bahati mbaya huwezi kuwa makini kumuangalia …’akasema.
‘Tunataka hiyo bahati mbaya,…maana wewe
kama baba wa nyumba,una jukumu la ulinzi na usimamizi wa nyumba na familia yako
, huwezi kumpoeka mtu tu, humjui, hujui sura yake, hujui jina lake..haya
limetokea kama hili janga, tunahitajia ukweli na unatakiwa kusema ukweli wote
li tuweze kuhakikisha kuwa haki inatendekea, na pia tuweze kumaliza hili tatizo
linaloendelea haapa kijijini kwenu..’akasema
‘Lakini hamuwezi kulimaliza kwa kupitia
kwangu tu au…?’ akauliza baba mwenye nyumba.
‘Chanzo kimoja kinaweza kuwa sababu ya
vyanzo vyote, hapa tumeona ndipo pa kuanzia, na kwa jinsi ilivyo, hawa watu
waliofanya hivi hapa ndio hao hao wamekuwa wakifanya kila siku sehemu mbali
mbali za hapa kijijini,…sasa ukituficha inawezekaan tukahisi kuwa unashirikiana
na hao watu….’akasema askari.
‘Ndio tatizo lenu hilo..mtu akijitolea
kusema ukweli anaweza akapata taabu hata kuliko muhusika mwenyewe au muhalifu
mwenyewe mnayemtafuta…sawa mimi sikatai kushirikiana nanyi kuupata ukweli,
maana hata mimi kama raia mwema wa hiki kijiji napenda tuishi kwa amani..lakini
sio kwamba kila kitu nitakifahamu mimi..’akajitetea
‘Ndio maana tunakuuliza maswali ambayo
tunahisi wewe unayafahamu na sio kwamba tunahisi lakini kiukweli haya maswali
tunayokuuliza, tunaamini wewe unayafahamu..hasa kuhusu huyu mama…’wakasema
‘Haya mnataka mimi niseme nini?’ akauliza
‘Utujibu swali letu tulilokuuliza awali ,
au niulize tena, je, wewe uliwahi
kumuona huyo mama sura yake,…usoni,… hata kwa bahati mbaya tu…?’ akaulizwa
‘Mhh..,hata
kwa bahati mbaya tu, mmh….?’ Akauliza huku akisita kusema kitu na kumbukumbu la
tukio la nyuma likamjia akilini na kujaraibu kuwazia sura ya huyo mama, akawa
hakumbuki vyema ….maana mara zote
ilikuwa kwa bahati mbaya na kwa haraka.
Wakati baba mwenye nyumba anatafakari
akilini akahisi kuonywa, kuwa asiseme, akisema atakufa au kupatwa majanga kama
yalivyowapata wengine…lakini kwa upande mwingine akawa anajipa matumaini,
akisema; mmh huenda ndio yeye, kama ndio yeye kwanini niogope kusema ukweli,
lakini hata hivyo, mwenyewe hakutaka sura yake ionekane kwanini mimi niwe
mtoaji wa siri zake,…
Tuendelee na kisa chetu
****************
Baba mwenye nyumba akakumbuka tukio wakati alipoingia kuhakikisha
kama kweli huyo mama kateketea na moto uliounguza chumba hicho alichokuwa
akilala huyo mama…na kwa kumbukumbu zake tukio hilo ndilo lililomuwezesha kumuona
huyo mama, japo, sio kwa uhakika sana,.. ni kwa muda mchache sana, na
kilichotokea pale alipoivua ile nguo iliyokuwa imefunika kichwa, alijikuta
akipata msituko na akili yake kuwa kama imeganda.
Akili ilikuwa kama imeganda kwa kutokuamini kwa yale aliyoyaona
ambayo mengine hataki hata kuyakumbuka, sembuse kuyasema..macho na akili ikawa
kama haiamini kile alichokiona…na mengi yalipita kichwani na hata hakuweza
kukariri vyema kile alichokiona..
Ilivyotokea ni kama vile umepita njiani ghafla ukaona kitu cha
aajabu au kisichochofaa, ukakwepesha macho yako kwa haraka usikiingalie, na kwa
tabia ya macho hutuma taarifa kwenye ubongo, na ubongo hutaka uhakika, kwahiyo
utageuza kichwa kuangalia kile kitu tena….ndivyo inavyokuwa kwenye akili ya
kibinadamu na ndivyo ilivyotokea kwa huyu mjamaa….
Akajaribu kukumbuka…na
kuvuta akili, kuanzia pale alivyomfunua….na nguo ya kichwani ilipotoka, uso
ukaonekana, ..kwa kumbukumbu za uhakika, kilichotanda usoni kilikuwa ni damu na
majeraha yakuonyesha kuwa mama huyo alikatwa na mapanga, na damu bado zilikuwa
zinavuja….
‘Hawa watu jamani ni wanyama..’akajikuta akisema kimoyo moyo
Lakini pia aliona kitu kingine cha ajabu ambacho kilimfanya
ashindwe kuamini, kilimkumbusha jambo, jambo ambalo hakutka alikumbuke
tena,..na kwa mchanganyiko wa yote hayo, akili ikashindwa kuhimili, kilichofuatia
hapo ni yeye kudondoka chini…macho….macho
‘Macho, macho yana nini?’ akawa anajiuliza bila kupata jibu
Akakumbuka kuwa aliposimama ili kuangalia tena, kama akili
ilivyomtuma, akakuta ile nguo iliyomfunika huyo mama usoni, ilikuwa imerudi
kama ilivyokuwa, uso umefunikwa,…hiyo iliashiria kuwa kumbe mama huyo kwa muda
huo alikuwa bado yupo hai,…. akataka kujaribu tena kumfunua, huyo mama
akazuia…na baadaye kukaja dalili za kuonyesha kuwa huyo mama anakata roho…
Sasa hapo atawaaambia nini hao askari kuwa huyo mama yupoje…?
‘Afande,… huyu mama alijitahidi sana kujifunika, alijitahidi sana
kuhakikisha hata mimi, hata mke wangu, hata mfanyakazi wa ndani ambaye
wamezoeana sana, hakuna anayefanikiwa kumuona sura yake…’akasema
‘Unajua unaongea na nani?…sisi sio watoto wadogo….ni lazima kuna
siku ulimuona huyo mama,…sisi tunachotaka ni uhakika tu, je huyo mama yupoje,
na kwanini watu wanafikia kumuona sio mtu wa kawaida,…’akasema askari.
‘Mhh,sijasema huyo mama sio mtu wa kawaida, maana anakula anafanya
kila kitu tunachokifanya, najua wengi wamehadaika na huo uvumi kuwa huyo mama
ni mama wa mbinguni,..mimi sijui, maana kwangu mimi nilimuona kama mwanadamu
tu….ila..tofauti yake ni hiyo kuwa matendo yake yalikuwa na utofauti kidogo na
watu wengine, kwa jinsi walivyozoea..’akasema baba mwenye nyumba
‘Tunakuuliza tena hili swali kwa kumbukumbu zetu, maana kama
itatokea kuwa ulimuona..na unatuficha, sheria itachukua mkondo wake, sikufichi
ndugu, hapa tunaongea kirafiki, lakini ukifika kwenye anga zetu…hutaaamini…utajuta
kuzaliwa..’akasema
‘Ina maana mnanitisha?’ akauliza.
‘Sio kwamba tunakutisha…, ila tunakuambia ukweli, sisi tuna njia
nyingi za kupata ukweli..kuna njia hii ya kirafiki tu, kwa raia wema
wanashirikiana nasi tunapata tunachokitaka basi mambo yanaishia kwa usalama
kabisa lakini kwa wale wanaojifanya vichwa ngumu,..hatuna jinsi….tunakwenda
kama wanavyotaka wao..hujawasikia watu kaam hao, hujawaona…..?’ akauliza
‘Afande, huko unapokwenda sio sahihi, tangu mwanzo nimejaribu
kuwajibu maswali yenu, na nikawajibu kwa jinsi ninavojua, nikasema ukweli wote,
ili kusaidia kama raia mwema…, kwanini sasa msiniamini kwa hili, na surayake itasaidia
nini kwenu..mimi hapo sielewi ina maana na nnyie mnaamini kuwa huyo mama hakuw
amtu wa kawaida….ni..ni …?’ akauliza huku akishindwa kumalizia hicho alichotaka
kusema.
‘Sisi tunajua kwanini tunakuuliza hivyo na wajibu wako kutujibu,…je
kama huyo mama alikuwa mhalifu sehemu fulani, na sasa kaamua kuja kujificha hapa
ili asionekane…’akasema huyo askari
‘Lakini huyo mama yupo hapa,…na kwa urahis kabisa mnaweza kumuona,
kwasababu keshakufa, hawezi kuzuia kumuona, au…. kama mnataka kuthibitisha
kwanini msiende kumuona wenyewe,…mnaogopa nini..’akasema kwa sauti kubwa kidogo.
‘Unajua sisi tunakuuliza maswali mengine kukupima ulivyo, je wewe
ni mkweli, …unaona eeh…tunaweza hata kukuuliza swali wewe ukaliona ni la
kitoto, lakini sisi tuna malengo yetu..nia ni kukupima ukweli wako, ….’akasema
‘Najua….mnataka kunibambikia kesi ..nyie ndio kawaida yenu
mkishindwa kupata ukweli, mnalazimishia mambo…acheni hizo bwana…’akasema
‘Ndugu, sisi tunajua ni nini tunachokifanya..naona tukuambie
ukweli…ili ujue hilo,sio kwamba tunaogopa kwenda kumfunua na kumuona huyo mama,
…marehemu..kwanza kwanini, tuogope, na wenzetu wapo wanaifanya hiyo kazi,
tulichotaka kutoka kwako ni kujua ukweli kutoka kwako,..ukweli wao tutakwenda kuulinganisha na ukweli halisi kutoka kwa
wenzetu..sasa kama umeamua kuficha basi….’akasema
‘Mama huyo kwa shida sana, na sio kwa usahihi, nilimuona nilipokwenda kuona kama kateketea
kwa moto…’akasema.
‘Sasa kwanini ulikuwa unatuficha..ehe tuambie alivyokuwa..yupoje.?’
wakamuuliza kila mmoja akiwa na hamasa ya kusikia atakachosema huyu jamaa.
‘Nyie mliuliza niliwahi kumuona kipindi nipo naye….sio kwenye
tukio la moto, ndio maana nikashindwa kuwajibu, ila…hapo alipokuwa hajitambui
mimi nilimfunua nikitafuta upenyo wa kuweka vidole ili kupima mapigo ya moyo
kwenye mshipa wa shingoni…kuhakikisha kuwa yupo hai, na ili aweze kupata hewa,
maana alivyokuwa kajifunika asingeliweza kupumua vyema..’akasema
‘Eheee, unaona eeeh,ile hamu ya kutaka kumuona, kama ilivyo kwa
wengine ikakujia, ukaona kuwa wakati ndio huo..au ulikuwa na sababu nyingine..hebu
tuambie ndugu…?’ akaulizwa.
‘Sababu gani nyingine mbona siwaelewi?’ akauliza huku akiwa
kakunja uso.
‘Hebu tuambie ukweli, ….wewe na huyu mama hamjawahi kujuana
kabla…?’ akaulizwa swali na akajikuta kama mtu kapigwa na kitu usoni, akahisi
kichwa kikilia nziiiiiiii, akakunja uso kama kukasirika , akatikisa kichwa kama
kuondoa hayo mawingu, halafu akajikuta akisema;
‘Kujuana na huyu mama !?, wapi , mbinguni…au…mbona siwaelewi…?’
akauliza na kabla hajaendelea mara mkuu wa hao askari aliyekuwa kundi la
kumchunguza huyo mama akaingia.
‘Samahani kuwakatiza, lakini hili ni muhimu sana..’akasema.
‘Afande hakuna shida, tulikuwa tunamuhoji ndugu yetu na
tunaendelea vyema sana, na sasa tulitaka kupata ukweli wake maana yeye ndiye
aliyekuwa akiishi na huyo mama, kwa kipindi cha muda,..akawa analea mtoto
wake,…walipata bahati hiyo maana wenzake wanakuja kuipata ile baraka ya mkono
wake, lakini wao baraka ilikuwa ndani…’akasema
‘Sawa sawa, nimekuelewa, lakini kuna jambo muhimu sana..’akasema
mkuu wao huyo.
‘Ndio afande,..’akasema huyo askari aliyekuwa akimuhoji huyo baba
mwenye nyumba, akimuangalia mkuu wake wa kazi.
‘Sisi tunamuhitaji huyu mtu huko …kuna kitu tumeona ni muhimu yeye
awepo,..’aaksema akimuangalia baba mwenye nyumba.
‘Eti….si wewe uliyemuona huyo mama, yaani wewe ulikuwa mtu wa kwanza
kumuona huyo mama baaada ya moto?’ akaulizwa baba mwenye nyumba na akili
ilikuwa haijatulia vyema akasema;
‘Unasema…kwenye moto..ndio mimi ndiye niliyemuona…’akasema
‘Mbona unakuwa kama hujiamini, unaulizwa swali na mkuu…je wewe
ndiye mtu wa kwanza kumuona huyo mama baada ya moto kuisha, ?’ akauliza yule
aliyekuwa akimuhoji kabla
‘Nimesema ndio…kwani nimesema vipi, sijakataa..’akasema baba
mwenye nyumba kwa hasira.
‘Usijali, tunachohitajia ni ukweli wako…maana wewe ndiye
uliyemuona kwanza, na pia wanasema wewe ndiye uliyethibitisha kuwa huyo mama amekufa,
kweli sio kweli?’ akaulizwa na kubakia kimia, akawa anajiuliza akilini ina
maana yeye alipotoa kauli ile kuwa huyo mtu keshakufa, hakuna aliyetaka
kuthibitisha zaidi…,
Lakini ana uhakika yeye alimuona huyo mama akikakata roho, na dalili
zote za kukata roho zilikuwepo, hakumbuki kumchunguza zaidi..lakini hata
hivyo..hana shaka yule mama alishafariki, kama ingelikuwa bado muda wote huu
angekuwa ameshazindukana, sasa wanataka nini zaidi, ..akawa anawaza.
‘Ni kweli afande, mimi nilipofika nilimpima kwa vidole, mkononi na
shingoni,…kwanza alionekana yupo hai, alikuwa hajakata roho, ..lakini baadaye
akapiga zile tatu, tatata… za kukata roho, kujivuta mguu, mara tatu, akawa
kimia..kimia kabisa..
‘Kwahiyo afande…mmh, na …kwa hali aliyokuwa nayo, mimi niliwaambia
mtu huyo mtu keshakufa….mimi niaondoka nikawaachia wao wakiendelea, walitakiwa
na wao kuthibitisha hilo…sasa mimi sijui..’akasema.
‘Je hukuhakikisha tena kwa vidole..maana mwenzetu wewe ni
mtaalamu, ukajua kuwa kweli keshakata roho..?’ akaulizwa.
‘Lakini kwanini mnaniuliza maswali hayo, huyo mtu yupo mikononi
mwenu, mnaye,au si yupo mikononi mwenu…bado tu mnanisakama kwa maswali ni kama
vile mnanishuku kwa jambo fulani…je mumeona nini kwake?’ akauliza.
‘Swali uliloulizwa na mkuu, je uliweza kuhakikisha tena kuona kuwa
amekata roho, au hizo dalili za kutikisha miguu kama mtu anakata roho, kwako
zilitosheleza kuonyesha kuwa ameshafariki?’ akauliza yule askari aliyekuwa
akimhoji awali, na yeye akasema;
‘Hivi…mbona siwaelewi, …ina maana huyo mtu kazindukana,
kafufuka..kiukweli, hata ingelikuwa na nyie mngajua hilo…sikuwa na haja ya
kumchunguza tena kwa vidole, nilijua tu ameshakufa, kwa hali aliyokuwa nayo,…na
zile dalili…hata hivyo mimi niliondoka nikawaachie wengine wenye mamlaka,…je
wao hawakuthibitisha…walitakiwa kuanya hivyo…’akasema.
‘Wewe uliwahi kuwa docta?’ akaulizwa
‘Nilianza kusomea…, lakini nikaishia kati nikaamua kujiunga na
fani nyingine..kwasababu zangu binafsi…’akasema
‘Kwanini ulibadili fani,…hatuhitajiki kuzitambua hizo sababu?’
akaulizwa
‘Niliona hakuna muelekeo,…hasa nilipoona madocta awali walivyokuwa
wanalipwa, ..maisha yao ni kama wanavyofanyiwa walimu, nikaona huko hakunifai,
nikageuza kibao na kusomea mambo mengine..’akasema
‘Kwahiyo una ujuzi wa kidakitari japokuwa sio kamilifu au sio?’
akaulizwa
‘Ndio nilikuwa nimeanza kusomea,..siwezi kujinadi kuwa nilikuwa na
fani hiyo, maana sikuingilia undani wake, ilikuwa ni mwanzoni tu mnafundishwa…aaah
nikaona huko hapana sitakuweza, basi nikaamua kubadili mchepuo na kuijiingiza
kwenye mchepuo wa masoko na manunuzi(sales and marketing) ‘akafafanua kwa
kiingereza.
‘Kwahiyo kwa ujuzi huo mdogo, ukajua kuwa huyo mama amekata roho
au sio..ndio mkuu anakuuliza hivyo…’akasema huyo askari.
‘Sio swala la ujuzi,..hata uzoefu tu kwa mtu mzima, ambaye umewahi
kukutana na watu wakikata roho utajua huyo mama alikuwa anakata roho….maana
alifikia sehemu akazima …watu wakaanza kuja,..muda huo nilishachanganikiwa,
nimechoka,nikaona niondoke niwaachie wenzangu waendelee…pale kulikuwa na joto,
hewa ngumu, sikuweza kukaa zaidi…ndio hivyo’akasema.
‘Unasema wewe una uzoefu wa kuona watu wakikata roho, ulishawahi
kuona watu wangapi wa namna hiyo, yaani wakikata roho?’ akaulizwa.
‘Unajua maswali yenu yananipa mawazo, hiivi mnanishuku nini mimi,
siwaelewi…hebu niambieni ukweli kama wanaume, je mimi mnanishuku nini mimi?’
akauliza kwa jaziba.
‘Aaaah, hebu njoo huku…’yule mkuu wao akamshika mwenye nyumba
mkono, na kutoka naye hapo kwenye chumba na wale askari wawili wakasema;
‘Ei kama wanaume kweli…hahaha,….sawa mkuu, sisi tunaendelea na mtu mwingine naona tuongee
na mama mwenye nyumba, tuitieni huyo mama…sijui nay eye itakuwa mume kama mke…’wakawa
wanaongea wale askari wawili, huku mkuu akiondoka na yule baba mwenye nyumba.
Baba mwenye nyumba aliposikia hivyo, akahisi kama janga sasa
linaikumba familia yake, anavyomjua mkewe ataongea kila kitu, na hata kile
alichokuwa akikificha yeye…lakini hakuwa na la kufanya, na hakuwa anajua nini
mkewe anafahamu zaidi,..na sijui hata mfanyaakazi wao watamuhoji pia,mmh, mungu
aepushie mbali ….
‘Lakin nina wasiwasi gani…’akawa anajiuliza, halafu akasema
‘Mimi sina kosa, ..kosa langu ni kulinda utashi wa mtu, kama
mwenyewe hakupenda kuonekana akiwa anajitambua, kwanini nitoe siri yake akiwa
hajitambui, akiwa keshakufa,..mimi naona nimefanya sahihi, ..sina
kosa..’akajipa moyo hivyo
‘Lakini kwanini huyu askari ananishuku..naona kama hawa watu
wananishuku, ni kama vile wanajua jambo, ambalo linanihusu na mimi,..je ni
jambo gani, kwanini asema; wewe na huyu
mama hamjawahi kujuana kabla…
Kauli ile ilijirudia rudia kichwani mpaka akahisi kichwa
kinamuuma, kichwa, ikawa kichwa akajitahidi kujizuia,lakini ikawa ni shida…na
huku akizidi kusikia sauti nyingine na nyingine,..akajaribu kutiliza kichwa na
sasa ikaja sauti nyingine ikisema;
‘Tulikuambia usiseme lolote
..kama ulimuona huyo mama, hutakiwi kusema yupoje, sasa umeanza kusema,..ole
wako..utakufa..utakufa…’sauti ile ikawa inasema na ile ya awali ya afande ikawa
inafifia,..kwa jinsi ilivyo, akili haipo inawaza mengine, huku kashikwa mkono
na fande, anakuwa kama anakokotwa tu hajitambui.
‘Sasa sikiliza, wewe ndiye uliyemfunua kule….kwenye tukio au sio, ukahakikisha
kuwa amefariki au sio...na wewe kwa bahati nzuri una utaalamu wa dakitari au
sio..’akatulia akimungalia huyo jamaa, na jamaa alikuwa katulia akiwa kwenye
mawazo yake.
‘Sasa,…sisi yupo mtaalamu, ndio..lakini kapatwa na dharura….hajitambui..unemuona
yule kalala pale..’akasema na mwenye nyumba akageuka kumuangalia huyo
anayeonyeshwa,, akamuona ni yule askari aliyekuwa akaimfunua huyo mama, hapoa
akshituka, akili ikaanza kufanya akzi tena, akauliza;
‘Kwani imekuwaje..?’ akauliza sasa akijaribu kupambana na maumivu
ya kichwa
‘Aaah, nahisi hajisiki vyema, toka tulipotoka naye huko ofisini
alikuwa akidai kichwa kinamuuma, sasa na tukio hili linaonekana limemuathiri
sana, unajua huyu mama, haeleweki…kuna mambo tunataka msaada kutoka kwako, wewe
ulikuwa unaishi naye na unamfahamu vyema, kwahiyo kwako haitakuwa ni taabu
sana..’akasema
‘Kwa-kwa-kwahiyo mnataka mimi nifanye nini?’ akauliza huku akianza
kuhisi jambo, akawa anaanza kujihami.
‘Usijali, au kuogopa,..unajau maiti anatakiwa sana sana kukaguliwa
na wanandugu kuhakikisha kuwa ni ndugu yao, au sio..lakini pia sisi kama
askarii eeeh, tunahitajia kumpiga picha ili kama ikibidi tukatangaze , ili
ikiwezekana ndugu zake waje kumuona au kumchukua, au sio..?’ akauliza yule
afande.
‘Sasa tatizo ni nini, kwanini hamfanyi hivyo..haina haja ya
kuniomba mimi kibali..kwanza hata hivyo mimi sio ndugu yake….sio mtu wake wa
karibu..ni watu tulioamua kukaa naye tu…kwani kuna tatizo hapa?’ akauliza.
‘Unamuona yule….yule yupo kitengo cha udakitari ..nilikuwa naye
hapa…sasa hajiwezi, kichwa kinamshumba ndio nikaaona nikuchhukue wewe
unisaidia,..si umesema wewe umesomea udakitari, unajua jua..nakumbuka
uliniambia wakati naingi, si ndio…?’ akauliza
‘Hapana…nitaka..na sikuweza kuusomea..hata hivyo afande, kwani ni
tatizo sana kumfunua na kumpiga picha..?’ akauliza
‘Unajua kuna tetesi kuwa huyu mama hakutaka sura yake ionekane na
mtu baki..sana sana ni ndugu zake na jamaa zake, hasa nyie mliokuwa mkiishi
naye karibu,..nimesikia wenzangu wakisema walikuwa wakikuhoji kama uliwahi
kumuona sura ya huyo mama, na ukawa unawaelezea alivyo, au..sio, kwahiyo kwako
wewe ni rahisi..au sio’akasema
‘Rahisi kufanya nini,..afande, naona nyie mnakwepa majukumu yenu,
mimi, siwezi kufanya mnalotaka …naona kama…hahaha afande, nimeshawashitukia,
kama huyo mwenzenu kajaribu kumfunua yaka mkuta yaliyomkuta, mnataka na mimi
yanikute hayohayo..mumenoa…siwezi…’akasema huku akirudi kinyume nyume
‘Aaah, wewe si ulikuwa unaishi naye bhanaa..eeh?’ akasema huyo
afande kwa sauti ya chini kwa chini.
‘Afande, kwanza kiukweli hata mimi kichwa kinaniuma sana…naomba nikatafute dawa, …unajua
nikuambie kitu kama huyu mama angekuwa hai angekitibu hiki kichwa, hua inatokea
hivi, nikisemakichwa kinauma, akikishika tu kinapona…, ‘akasema
‘Oh, kumbe,…kwako haitakuwa ni shida….wewe fanya hivi, mpiga picha
yupo wapi tena, tusaidia, jambo, nenda kamfunua halafu mpiga picha atafanya
kazi yake na tumemaliza kazi, unasemaje?’ akawa akama anauliza
‘Afande kichwa kinaniuma..sitanii, mara nyingi kichwa changu
kikiuma hivi, akinishika kichwa huyo mama kinapona, sasa ndio huyo..’akasema na
kugeka kumuangalia huyo mama pale alipolazwa…ile kugeuza kichwa
kuangalia,..akashituka, ule mshituka wa kama kuruka,
Na afande aliyekuwa karibu yake, akaruka hatua mbili nyuma kama
kukwepa kitu, huku akauliza
‘Kuna nini tena, umeona nini….’
NB: Kidole kinauma, tuonane kesho
WAZO LA LEO:Kuna watu hupenda kukwepa majukumu yao,
hasa pale wanapoona kuwa jambo hilo au kazi hiyo ina matatizo, au ni ngumu
kwao,…hawataki kusema moja moja kuwa imewashida, au ina jambo ambalo
wanaliogopa,… lakini hapo hapo, wanahitajia masilahi yake au faida yake au sifa
kutokana na jambo hilo au kazi hiyo.
Wanachofanya watu hao ni kusakiziana, au kuwategea wengine waifanye, huku
wakisubiri matunda yake wayafaidi pamoja.
Huu kiukweli sio uungwana, kama kuna jukumu au tatizo liangaliwe
kihekima, au litafutiwe njia yenye muafaka kwa kusaidiana…, na sio kukwepa
wajibu na kuusogeza jukumu hilo kwa mwingine kwasababu mbambali. Wajibu ni
dhima, na kila anayestahiki ana takiwa kuwajibika nao, ndio kujitoa muhanga
huko, kwa nia njema na kwa malengo ya kulitaua hilo tatizo, ukikwepa wajibu
wako, utaulizwa,..
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment