Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, February 16, 2015

NANI KAMA MAMA -33
Kukasikika kilio!....kilio cha nani, kilio kimetokea wapi....?

 Kila mtu akawa anajiuliza hicho kilio ni cha nani na kimetokea wapi, hata kwenye nyumba ambapo kunasadikiwa ndipo hicho kilio kimetokea, na wakati kilio hicho kinatokea, wakazi wake walikuwa ndani ya usingizi mnzito,...

Japokuwa walishituka, lakini hawakuwa na uhakika kuwa kilio hicho kimetokea hapo kwao, au kimetokea kwenye  nyumba nyingine ya jirani.

 Wakazi wa nyumba hiyo ambao ndio wamiliki wa nyumba hiyo, walipozindukana kutokana kwenye usingizi, na kuanza kuulizana...

‘Umesikia..?’ mmoja akauliza

‘Nahisi kuna kilio..tena kama kilio cha hatari vile,.....’akasema mwingine

‘Hata mimi nimesikia...lakini nilihisi kama naota, kiukweli hata sijui kimetokea wapi?’ akauliza mwenzake

‘Hata sina uhakika, leo nilikuwa na usingizi mnzito kweli haijawahi kuto;kea hivi...’akasema mwenzake.

‘Oh, mtoto, ..hebu muangalia mtoto, ...’akasema mwenzake

‘Mtoto kalala..jana, mama wa baraka alimpa baraka zake, basi mtoto kalala utafikiri hataki kuamuka...sio yeye aliyelia, kilio kimetokea huko nje...’akasema

 ‘Mimi, sioni kama kuna tatizo....kama ingeuwa ni tatizo, kilio kingesikika tena...’akasema baba mwenye nyumba. Basi wakaona waendelee kulala lakini kabla hawajaanza kuuita usingizi ulipotea, mara mama mwenye nyumba akasema;


‘Nahisi kama hewa ni nzito....’akasema

‘Hewa nzito..na harufu isiyo ya kawaida, kama ya moto...’akasema mwenzake.

‘Mimi nasikia kama harufu ya moshi…husikii, ...?’akasema mama mwenye nyumba akiuliza.

‘Sijui nani kachoma mataka taka usiku huu…’akasema baba mwenye nyumba.

‘Hiyo sio haraufu ya mataka taka….nahisi kuna moto..mume wangu, kuna moto nje..amka haraka...’akasema mke mtu, na mume mtu aliposikia moto, akakurupuka na kukaa kitandani, akajaribu kuchunguza kwa hisia za pua  na yeye akahisi hivyo.

Wote wakaamuka na kuanza kutoka nje, hapo hakuna aliyejali kavaa nini, mbio, hadi nje, kuona kuna nini, walipotoka nje tu, kutaka kuelekea sehemu ya uwani ambapo kuna chumba hicho, wakarudishwa na moto,!

‘Moto…’mfanyakazi wa ndani aliekuwa wa kwanza, akarudi mbio, alikuwa keshatangulia nje akikimbilia kumuamusha mama wa mkono wa baraka, kumbe huko anapokwenda ndipo moto ulipotokea.

‘Nyie tokeni nje haraka, mchukue mtoto, kaeni mbali kabisa na mtoto..na mke wangu ita majirani…..’ilikuwa amri ya baba mwenye nyumba, mtoto alishaanza kulia yeye hakujali tena kulia kwa mtoto akaelekea sehemu huko kwenye chumba cha uwani kupambana na moto.

Alipofika na kuona jinsi moto ulivyo akajua ni hasara na huenda mama aliyekuwa akiishi humo kama hakuwahi kutoka basi atakuwa kateketea na huo moto, akageuka huku na kule kutafuta njia ya kufanya, na akaliona pipa la maji, lilikuwa limejaa maji, na lilikuwa juu ya chetezo kilichotengenezwa kwa mbao,..

Akalisogelea, na kuanza kulisukuma, huku akiweka mawe kwa chini ili liiname kuelekea kwenye huo moto, akajitutumua kw nguvu zote, na kweli likadondoka na maji ya ruka kupamana na huo moto,..sehemu ya chini ikazimwa na hayo maji..juu mto ulikuwa ukiruka na kuwaka kwa kazi..paa la nyumba lilikuwa limeshadondoka.

‘Mama wa baraka, yupo wapi...?’ akauliza mfanyakazi, na hakuna aliyempa jibu, kila mtu alikuwa akiharakisha kutoka nje. Na mama wa nyumba akaanza kupiga ukelele wa kuomba msaada,na majirani amboa walishahisi hiyo hali walishaa kujitokeza, na kusikia kelee hizo wakaja kwa iwngi utafikiri walikuwa sehemu wakisubiria.

‘Kwa hivi sasa cha muhimu ni kuuzima huo moto, sizani kama kuna uhai kwenye hilo eneo tena, yule mama alikuwa analala humo?’ akauliza mjumbe, wakati huo watu wanaendelea kuuzima moto.

‘Ndio…’akasema baba mwenye nyumba.

‘Mhh, kama yupo huko ndani,...na huo moto sijui kama atakuwa hai...’wakasema majirani waliokwisha kufika.

‘Moto..moto….saidia kuzima moto..moto…’.ikawa sasa ni ujirani mwema kila mmoja anakimbilia ndoo na maji, kila mbinu za kuuzima huo moto zikafanyika…..’

Tuendelee na kisa chetu..

***********

Moto huo ulikuwa ukiwaka sehemu ile aliyokuwa akiishi huyo mama ambaye watu sasa walikuwa wakimuita mama wa mkono wa baraka na ulikuwa moto mkubwa uliozunguka eneo lote la chumba, utashangaa jinsi ilivyo, maana haukuwa unakwenda kwingine zaidi ya kuzunguka eneo hilo la chumba...watu wakahangaika kuuzima kila mmoja kwa mbinu zake, kila aliyetoka kwake akawa kafika na ndoo ya maji, michanga, matawi ya miti...ulikuwa moto mkali kweli..

‘Jamani kimetokea nini, na huyu mama anayelala hapa yupo wapi..’ ikawa watu wanaulizana huku wakiendelea kuzima moto.

‘Naona hilo jibu kwasasa ni gumu kulipata muhimu ni moto uzimike, na huku hakuna cha gari la zima moto, ndio maisha yetu ya kijijini, kukitokea moto mjue mumeangamia…..’akasema mwenzake akimwagia maji kwenye moto

‘Mimi nahisi ni  madawa ya huo mama yamelipuka…’ wabaya wa huyu mama wakaanza visa.

‘Kwani huyu mama alikuwa na madawa, mimi sikuwahi kumuona akitumia madawa, alikuwa anaombea tu, n asana sana alikuwa akitumia maji ....huo ni moto, na inaonekana moto huu umezunguka sehemu yote ya chumba, huu sio moto wa kutoka ndani...ni moto wa kupangwa huu...’watu wengine wakasema.

‘Hayo ni ya kwako bwana kama ni wa kupangwa basi ni wewe umauwasha, umaejuaje kuwa ni moto wa kupangwa...’akasema mwingine ambaye hakuonekana akihangaika sana.

Baadaye moto ukafanikiwa kuzimwa, lakini kwa asilimia kubwa sehemu kubwa ya chumba hicho iliteketea kabisa, na kama ni kujenga hichoo chumba inabidi kujenga upya, na hakukuonekana kusalimika kwa vitu, vitu vyote vlivyokuwepo humo ndani viliungua vyote na huo moto.

‘Mhh, hapa hakuna uhai wa mtu...’akasema mmojawapo.

‘Lakini yeye si mama wa kutoka mbinguni, huenda amepaa, na kuucha moto ukiwaka..’akasema mwingine kwa mzaha.

‘Mbele ya moto, hata uwe nani kama umo kati yake unageuka kuwa mafuta ya kuuwasha zaidi….mmh, masikini mama wa watu, hata sura hatumfahamu…’wakawa wengine wakiongea kwa mzaha, wakijidai kumsikitikia

‘Kama alikuwa mwanga hio ndio adhabu yake..’kijana mmoja alisema, na watu wakamuangalia kwa mashaka, alipooa hivyo akajibaragua, na kusema;

‘Nilisikia watu wakisema hivyo kuwa mkono wake ni mkono wa mtoto mchanga anautumua kuwangia watu…ndio maana nasema kama ni hivyo, naona zambi zake zimemuandama..’akasema

‘Ni nani alithibitisha hilo kuwa mkono wake ni mkono wa mtoto mchanga, huo ni ushirikina wa dhana, na kama kun awatu wamefanya hivyo wakidhania hivyo, basi wao ndio wachawi,…maana wameua mtu asiye na hatia…’akasema mzee mmoja.

‘Na wewe mzee ndio nyie,…’akasema kijana mwingine akageuka kumnong’onezea mwenzake;

‘Ndio hao hao, unamuona macho yake,…bado zamu yake, hawa lazima tuwamalize…’

 Wakati kundi hilo likiongea, kundi kubwa lililokuwa mbele likihangaika kuuzim huo moto, likawa sasa linamalizia malizia, na mmoja wao akasema;

‘Hebu angalia pale kwenye mlango, naona kama mlango ulidondokea kwa ndani, na pale moto haujazimika vyema...mwagia maji pale…’akasema mmojawapo.

‘Pale hapaingiliki kwa sasa..inabidi tusubiri mpaka kupoe kwanza...maana lile paa lililodondokea pale ni la moto…ukishika bati lake ngozi inabakia kwenye bati…’akasema.

Kwa wakati huo baba mwenye nyumba alikuwa keshasogea sehemu ya eneo hilo, akihangaika huku na kule, kwani hasara ilishamchanganya kichwa hakujali maonyo ya watu kuwa moo bado haujazimika ukiingia hpo unaweza ukaungua viabaya sana,…yeye hakutaka kusubiria kupoe, yeye akasogea sehemu ile ya mlango, uliokuwa bado unafuka moshi.

 Alipoufikia huo mlango akausukuma kwa mguu, ule mlango ukadondoka kwa ndani, …na paa lililokuwa limedondokea pale likazidi kuporomoka chini, ukuta ulishadndoak sehemu  ya hapo mlangoni..ulionekana hauna nguvu..akazama ndani.

‘Wewe unataka kueleta balaa, utaungua huko, hapo moto bado upo chini kwa chini..usijadanganye ndugu….’watu walisema, walikuwa hawajui kuwa mwenye nyumba alipomwaga yale maji ya kwenye pipa, moto wa chini ulikuwa umezimika, na hiyo ilimsaidia baba mwenye nyumba kukanyaga bila kuungua.

Baba mwenye nyumba akasogea hadi sehemu ambayo ana uhakika ndipo kitanda kilikuwepo, alitaka kuhakikisha mwenyewe kama huyo mama kateketea na huo moto au bado yupo salama. Akawa anainua sehemu ya mabati ya paa la nyumba, na kuondoa mabaki mabaki ili kupata upenyo, akaweza sasa kuingia ndani. Joto la moto na moto wenyewe bado ulikuwepo, hakujali..

Alishangaa sana, kwani yeye katika hali ya kawaida, anaogopa sana moto lakini alishangaa kupata uajsiri huo, na kuweza kuuingilia, kuna kitu kilikuwa kikimvuta kufanya hivyo..ulikuwa sio utashi wake,..na akili ilikuwa kama inagongana, kuna hali inamkanya, na kuna hali inamvuta kufanya hivyo, na kujikuta kama anatetemeka vile.

  Alipoingia ndani, akatizama eneo la kitanda, ...kwenye eneo la kitanada, kulikuwa na sehemu kubwa ya paa na mabaki ya paa yalikuwa yamedondokea hapo, sehemu hiyo kwa juu waliweka wa mbati ya akiba, na yale mabati yalikuwa yamedondokea kitandani, na kikawa kama kimevunjika…akawa anayainua yale mabati mengine yalikuwa yameungua kabisa, utafikiri karatasi, mengine yalibakia bakia, kuna ya chini kabisa yalikuwa mazima.

Akayainua yale mazima na kuanza kuyapenga sehemu nyingine nia ni ili afikie kitanda..na hatimaye akafikia kitanda, hutaamini, akakuta kitanda na godoro, havijaungua sana,..inonekana lile paa lilisaidia kuzuia moto usifike, hapo kitandani...lakini hakumuona huyo mamapale  kitandani!.

‘Khaaa. Huyu mama yupo wapi…!?’ akawa anajiuliza kwa mshangao

**********
‘Huyu mama atakuwa hayupo nini..?’ akawa anajiuliza na hapo akajipa moyo kuwa huenda huyo mama aliwahi kukimbia kabla moto haujapamba moto

Akawa sasa anahangaika kuinua bati moja moja, yale yalikuwa mazima, na akiyatupia mbele, na baadhi ya watu wakawa wanajisogeza kwa mbali, na kusema;

‘Tupi huku mzee, tuyapange kwa nje, moto usije ukazuka tena na kuyaunguza, angalau umebahatika kupata kidogo kilichobakia, watu wengine wakawa wanafika kwa mashaka kuyapokea na kuyasogeza kwa mbali.

‘Angalia mzee hapo bado kuna moto…’akasikia watu wakimuambia, watu wengi walishachoka na wengi walikuwa wakusubiria kupoe kabisa, na walishaona kama kulikuwa na mtu humo watamkuta maiti tu.

‘Sasa mbona mnapumzika vijana, hakikisheni kama moto umezimika wote, unaweza kulipuka tena ukaunguza nyumba iliyobakia,..nyie ndio vina tunawategemea,..na kama kuna…mtu au  maiti basi mhakikishe anatolewa, huo ndio ubin-adamu..’akasema mjumbe.

‘Kama kuna mtu hapo ni maiti..na tunaona tuvute subira, maana maiti ya mtu aliyeungua inatisha kidogo..’wakasema hao vijana.

‘Inawezekana bado yupo hai, ni muhimu kwenda kusaidia..’akasema mzee mwingine.

‘Labda awe ni shetani maana mashetani yametengenezwa kwa moto, kwahiyo hayaungui…’akasema kijana mwingine.

‘Nyie vijana mna laana, kama kweli mnafikiria hivyo, kweli maisha yenu yatakuwa mabaya…’akasema

‘Nyie ndio mnafanya maisha yetu yawe mabaya, mlishatumia ujana wenu, sasa mnataka kutufanya sisi tusufaidi ujane wetu…moto tumeshazima inatosha, ngoja tupumzike kidogo….’akasema mmojawapo.

‘Kwa vipi..nani kawafanya hivyo, ina maana sisi kuwakanya msifanya machafu, ndio mantuona wabaya, tuaache tu mvute mabangi yetu, tusiwakemee mkibiwa madawa ya kulevya..hamuoni kama mnajiangamiza wenyewe, na kutusingizia sisi wazee wenu…’akasema mzee mmoja ambaye mara kwa mara anatanaia na hao vijana.

‘Mzee wewe tunakufahamu huna ubaya na sisi, lakini kuna wazee wengine, vigagula..wanatuwangia usiku ili tusiwe na maendeleo, hao ndio tumetangaza vita dhidi yao…’akasema kijana mwingine.

‘Huwezi kutangaza vita na mtu ambaye hajiwezi, kama mna minguvu hiyo nendeni mkaitumie shambani, limeni, fanyani kazi za kuwaingizia kipato,…mkitumia minguvu yenu kupambana na wazee waliojichokea, mnajitafutia laana,…’akasema huyo mzee.

‘Laana haitupai..mwanga atamlani nani…atajilaani mwenyewe..’akasema mwingine.

‘Nyie vijana kila siku nawaasa, acheni kukaa vijiweni na kujidanganya, kuwa kuna wazee wachawi,..uchawi mnajitafutia wenyewe kwa hayo madawa, mipombe…na bangi…mjichawia wenyewe na kukosa maendeleo, kama ngejituma mashuleni, mkafaulu mitihani mngelikuwa mbali..angalieni wenzenu huko Ulaya,…wanajituma ndio maana wana maendeleo…nmkibakia hivyo, kulalamika, mwisho wenu utakuwa mbaya zaidi..’akasema huy mzee.

‘Hutuambi kitu mzee, hiyo ni onyo kwa vigagula,..mmoja mmoja ataondoka, na hata wewe tukithibitisha kuwa una mikoba mzee hatutakuacha…, ..dawa yake ndio hiyo…habari ndio hiyo..’akasema mmoja akionyesha kashalewa na madawa ya kulevya.

‘Mwenyewe hapo ulipo unasubiri kujifia..hayo madawa yatakumaliza siku si zako..’akaamiwa na wenzake wakawa wanamcheka.

‘Mimi sifi, mtaniona hivi hivi….’akasema akiondoka huku akipepesuka.

Baba mwenye nyumba akawa  sasa keshakifikia kitanda, na akawa anajaribu kukinua, kwanza akaondoa godoro, lilikua limeungua upande akaweza sasa kukiona kitanda, chini ya godoro kulikuwa na mkeka, mkeka ulikuwa bado mzima.

Wakati anahangaika akajikwaa, akainama chini kutizama,  akaona mguu wa mtu, akainua kile kitanda, na kukiangushia upande, akauvuta ule mguu., ni mtu..ni yeye,…

‘Oh, ni yeye…’akawa anasema kwa sauti japokuwa hakuwa na uhakika kama huyo mtu ni mzima.

‘Ni mama wa mkono wa baraka…’akasema akihis watu huenda wamemsikia, lakini sauti haikutoka, koo lilikuwa kavu, alikuwa kama anakoroma.

Akawa sasa anaondoa, mabaki yaliyokuwa yamemtanda yule mama, …kweli alikuwa yule mama wa mkono wa baraka....na kwa juhudu sana akaweza kumtoa sehemu ile na kumsogeza pembeni.

Yaonekana huyo mama, alikuwa kajitumbukiza chini ya kitanda..sijui alikuwa anajificha au ilikuwaje, kwa wakai huo huyo mama likuwa kalala kitumbo tumbo, akamgeuza na kuangalia juu, alikuwa katapaa damu, ...

‘Mbona katapaa damu….miguuni, mikononi...mwili mzima ulikuwa na majeraha, kama ya kukatwa katwa na mapanga , akashangaa, alichojua yeye ni moto, sasa iweje huyu mama awe kama kakatwa katwa na mapanga. Alimsogelea karibu yule mama, na kumkuta akiwa katika hali mbaya sana, akamuinua na kuangalia kuwa bado yupo hai.

Alishika eneo la mikononi hakuweza kupata mapigo ya moyo vyema, akainamisha kichwa na kuweka sehemu ya kifuani,..bado akawa hana uhakika..akataka kushika sehemu ya shingoni, lakini zile nguo zilivyo, hakuweza  kutumbukiza kidole,  ikabidi ajaribu kusogeza zile nguo, akawa sasa kama anavuta kwa juu, na alipona hapati nafasi, akaona ni bora kuondoa ile sehemu yote ya juu, hadi kichwani

‘Oh, sijui nitakosea, lakini lazima nifanye hivi kuona kama yupo hai..atanisamehe tu...’akasema na kuanza kuivuta ile nguo ya sehemu ya kichwani , ilikuwa ni kazi, maana inaonekana mama huyo alikuwa kama kajifunga shongoni ili nguo istoke...

Akapata upenyo, na akagundua kuwa mapigo ya moyo bado yapo. Na hapo hamu ya kumfunua kabisa ile sehemu ya usoni ikamjia, akataka aone sura ya huyo mama ipoje, na kwanini siku zote anakuwa kajifunika,...alijua anafanya kosa, lakini hamasa ikamzidi.

‘Usifanye hivyo utapatwa na madahara kama yliyowapta waliojaribu kufanya hivyo…’ilikuwa sauti ikimuonya kichwani, kwani alishasikia kuwa kuna watu walijaribu kumfunua hiyo nguo ya kichwani ili wamuone sura yake, sasa hivi wapo kitandani waganjwa wamekuwa kama wamechanganyikiwa.

Yeye kwanza alichelea kufanya hivyo, sio kwasabau ya kuogopa hayo aliyosikia, bali kwa kuogopa kuwa anafanya kkitu ambacho mwenyewe hakupenda kifanike, kama mwenyewe hakupenda uso wake uonekane kwanini afanya sasa, lakini hata hivyo hamasa ya kumtambua huyo mama ikamjua, akaanza kuvua ile nguo ya kichwani.

Akatumia nguvu na kuivuta ile nguo iliyokuwa imefunika kichwani...taratibu ikawa inavuka baada ya lile fundo la shingoni kuachia,..., na kila hatua akawa anashangaa, ilikuwa sura ya ajabu..…baadaye akakivua kabisa, uso ukabakia wazi…alishikwa na butwaa, akajikuta anadondoak chini....

Akiwa pale chini, akapangusa macho yake, huku mwili ukimtetemeka, alishangaa kwa nini ..lakini hata kabla wakati alipoamua kuuvaa huo maoto na kuingia hapo, alihis mwili ukimtetemeka..mwanzoni alihis huenda anaumwa malaria,..sasa kule kutetemeka  kulizidi.

Akajitutumua na kusimama, akarudi kumwangalia tena yule mama, lakini ile nguo ambayo alikuwa na uhakika kuwa aliitoa, akaikuta imerudi mahali pake, uso umejifunika tena,....akaona ajabu ina maana huyo mama yupo hai kajifunika mwenyewe tena, ..., huyu ni mtu au…mbona …hapana,… akajaribu kuivuta tena ili kumfunua amuone vyema usoni…huku akisema;

‘Hapana..haiwezekani, ..sio yeye, hapana…hapana…’akawa anarudia hayo maneno huku akijaribu kuvuta ile ngo

Na alipofanya hivyo, yule mama akainua mkono na kushika ile nguo kuzuia...jamaa akarudi nyuma, akabakia kaduwaa...na akaona mtikisiko wa mwili wa yule mama akawa anahangaika akijaribu kuinua mguu, lakini ilionekana mguu una majeraha, akawa anagugumia maumivi huku akisema;

‘Msiniue, mimi sio mwanga, mimi sio mchawi… jamani…nimewakosea nini walimwengu…kwanini mnataka kuniua…..niemkuaj kumtafuta mtoto wangu…nataka mtoto wangu’ akaanza kupiga ukelele mara mbili, halafu akaulia kimia..akatikisa mgu mara mbili, halafu akatulia….

NB: Kumbe yupo hai, je mwenye nyumba aliona nini kwa huyo mama….


WAZO LA LEO: Kulalamika tu hakutoshi,..muhimi ni vitendo vya dhati. Kabla ya kulalamika, kwanza tujiulize tumefanya juhudi gani, je tulijibidisha kwenye kazi, tukatimiza wajibu wetu sawasawa,..kama ndio basi tuna wajibu wa kudai haki zetu, lakini  kama sisi wenyewe tunaongoza kwenye utegaji wa kazi, kutwa nzima tupo vijiweni, wanafunzi hatusomi,  tunashindana kwa usharobaro,…kata k, mbano shepu sijui..nk …kuimba kwa kukariri bila kusomea,..kuota doto za Alinacha,…utamlalamikia nani. Hebu jiulize kama kila mtu atafanya hvyo unafikiri taifa litakuwaje..tusitafute mchawi, uchawi tumeutengeneza sisi wenyewe.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Ni muda mrefu sijapita hapa. Ama kweli kazi zako nazihehimu sana endelea kutuelimisha ..Hakuna kama mama.