Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, February 13, 2015

NANI KAMA MAMA-32



 Siku hiyo mama wa nyumba akatembelewa na mgeni jirani aliyejifungua karibuni, na katika maongezi yake akasema;

‘Jamani mwanangu jana hakulala,…siku nyingine inatokea hivyo, lakini cha jana kilikuwa kilio cha aina yake…kalia karibu maasaa matatu, hadi sauti inakauka,…kulia huko sio kwa kawaida,…. ‘akasema huyo mgeni

‘Mhh polen sana…’na yeye alitaka kumuambia hata mtoto wake imetokea kulia hivyo , lakini akaona asubirie mwenzake amalize maelezo yake.

‘Tulihangaika usiku huo maana siku zote analia, tunatafuta njia za kumtuliza, kutokana na matatizo ya   matiti yangu, huwa tunaamua …nayakamua maziwa kwenye chombo tunampa anakunywa analala, lakini usiku huo hakulala akawa analia kupitiliza….’akasema

‘Kabla uliwahi  kwenda kwa dakitari..kuhus matiti yako…?akaulizwa mgeni

‘Mwanzoni tatizo lilipoanza, tuliwahi kwenda kumuona dakitari,  …Dakitari alinipa dawa, ila akanishauri…, kiusalama nimuanzishie huyu mtoto maziwa ya kopo..akaniapa na jina la maziwa sahihi yam tot kama huyo….’akasema

‘Kama dakitari alisema hivyo mimi sioni ni tatizo na kulia kwa mtoto ni kawaida, muhimu ni kuona kama hana tatizo jingine....vinginevyo mnampeleka kwa dakitari…’

 ‘Siku hiyo alivyolia usiku ilikue andio lengo letu, kukipambazuka tu twende kwa dakitari wa watoto…, unafikiri ilikuwa na haja tena…hatukuenda tena..’akasema na mama mwenye nyumba akasema kwa mshangao

‘Kwanini..…?’ akaulizwa

‘Unajua huyu mama wa mitaani, kumbe wakati analia,huyo mama alikuwa kalala upenuni mwa nyumba huko nje, si unajua huyu mama, hana makazi maalumu, hulala popote wanadai akilala kwako kuna baraka….’alipomtaja huyo mama wa mitaani mwenzake akatega sikio kwa hamsa.

‘Mhhh..hata mimi nasikia hivyo…..’akasema akitega sikio maana hata yeye alikuwa na hamu ya kusikia mambo kuhusu huyo mama…

‘Basi huyo mama kumbe alikuwa kalala huko upenuni mwa nyumba yetu, akasikia kilio cha mtoto, akagonga mlango tumfungulie…..

‘Mkamfungulia…?’ akauliza kwa mshangao.

‘Mume wangu alifanya hivyo…’

‘Huyo mama mlango ulipofunguliwa tu akaingia ndani, na tukashindwa hata kumzuia, akaja moja kwa moja pale nilipokaa na mtoto, wote tumeduwaa. Kumzuia tunashindwa, tukabakia kimya…Akaja pale nilipokaa, akamwangalia mtoto anavyolia, akasema `mtoto wangu nyamaza eeh..’

Akainua mkono wake, sijui alikuwa akisema maneno gani, akamshika mtoto kichwani….mara mtoto kimya, na baada ya muda mfupi mtoto akalala. Halafu yule mama bila kusema kitu huyo akatoka nje na kwenda kulala pale alipokuwa kalala mwanzoni…’

Kisa kinaendelea

**************

Habari hizi za huyu mama na muujiza yake , zikaenea haraka sana, na watu wakaanza kumuita mama wa mkono wa baraka, na jina la mama  wa mitaani likaachwa…sasa akawa ni `mama wa mkono wa baraka’ kile aliyemuongelea akawa akitaja miujiza yake

Kile mwenye mtoto akiona mtoto wake analia tu, haraka anatafutwa huyo mama, kufanya vitu vyake, na si zaidi yeye akifika humshika mto kichwani, na kuna maneno anayasema, wengine husema anaomba dua, wengine husema anasema tu…’mtoto mnzuri nyamaza eeh, na mtoto hunyamaza kweli.

Tofauti na ilivyokuwa awali, watu wakimuogopa, watu wakimzarau kama mama wa mitaani sasa ikabadilika, kila mtu akataka mama huyo afike kwake. Sasa ikawa anakaribishwa kila nyumba, ili angalau awashike watoto wao, wapate hizo baraka.

Laki ni cha ajabu sasa alikuwa na makao mahali pamoja, hakupenda kwenda mbali na hapo, karibu siku ningie akawa anaonekana kulala upenuni mwa nyumba ya  huyu mama aliyepata mtoto wa kufikia, akapafanya kama ndio kwake.

Na huyu mama wa kufikia kama wengine akaona ni baraka kwake, akaona afenye zaidi ya hayo kuliko kumuacha huyo mama alale upenuni mwa numba yake, akaaamua kumkaribisha kwenye chumba cha uwani, akamwekea godoro la akiba na shuka.

 Chumba hicho kilikuwa na makorokoro mengi, lakini baada ya siku mbili, kiligeuka kuwa kisafi ajabu, huyo mama wa baraka alikitenengeneza vizuri na akakipanga vizuri, na baadhi ya makorokoro yasiyofaa akayakusanya kwa nje, akisubiri wenyewe kama wayahaitaji akayatupe, na chumba kikawa sio stoo, bali ni chumba kinachoishi mtu.
‘Mhh, utafikiri sio kile chumba tena…’alisema mama mwenye nyumba alipoingia siku hiyo na kuona mabadiliko.

Basi siku hiyo mama mwenye nyumba na baba mwenye nyumba wakawa wanaongea, na baba mwenye nyumba akasema;


‘Huyu mama uliyemkaribisha hapa niliskia mwanzoni mkisema kachanganyikiwa, na wewe umemkaribisha hapa, ..huoni ni hatari..’akasema

‘Ni hatari, hivi wewe unaishi wapi, tatizo lako unarudi usiku na ukirudi hutaki kujua kinachoendelea hapa mitaani, mama huyo kila mtu anataka akaishie kwake,…’akasema

‘Kwanini..?’ aakuliza

‘Mwanzoni niliogopa hata kumkaribia,..na acha ajabu hataki mtu kuwa karibu naye sana…mimi siamini kama ana tatizo lolote la kiakili…ila ninachoona ajabu ni kuwa, l hapendi kuongea, na hata siku moja hajawahi kuacha kichwa na sehemu za uso wake wazi, kwanini…’ akasema mke mtu.

‘Kwani inakuhusu nini, kama umeona hana tatizo,  mwache alale, na kitu cha kuangalia ni huu ugeni wa mara kwa mara watu kuja ku…sijui kutibiwa au nini. Wengine hawana heri na sisi, uangalia sana hilo, mimi nimeona ajabu… ina maana wanamfuata huyo mama…?’akauliza mume mtu.

‘Sawa, lakini mbona imekuwa ni baraka…wewe huulizi vitu humu ndani mbona havipungui, maharage, unga, mchele..unafikiri vinatoka wapi….?’ Akauliza mke mtu.

‘Mhh, najua ni kutoka kwenye biashara zako, kwani vinatoka wapi zaidi ya biashara zako?’ akauliza

‘Hutaamini, ni watu wanaleta…wanamletea  huyo mama wa baraka, na yeye akipewa, analeta kuwa tutumie maana kula tunakula pamoja…’akasema

‘Mhh, ina maana kumbe…unajua kuna siku nilitaka kukuulizia, maana siulizi tena pesa ya matumizi, ninayoacaha anona inatosha, nikawa anjiuliza, labda ni lile tatizo la nyuma umeamua kuishi upendavyo,..’akasema

‘Tatizo gani la nyuma?’ akauliza mke mtu.

‘Tuyaache hayo nisije nikakkumbusha yaliyopita, niambie kuhusu huyo mama wa mitaani..’akasema mume mtu.

‘Sio mama wa mitaani mume wangu, ni mama wa mkono wa baraka…’akasema mke mtu kwa furaha.

‘Ohhh..haya mama wa mkono wa baraka…’akasema

‘Sasa hivi kila anayekuja na tatizo la mtoto wake lazima aache kitu, hele au unga, au maharage, sasa imekuwa ni neema kwetu…..’ akasema mama wa kufikia wa mtoto.

‘Na nimesikia huyu mfanyakazi wa ndani hakai mchana kutwa, na anayemlea mtoto ni huyu mama, ni kweli au si kweli..’ akauliza baba mwenye nyumba.

‘Ni kweli,…lakini anaomba ruhusa, ..na kwa vile huyo mama wa mkono wa baraka yupo sioni ni tatizo sana, maana huyo mtoto na huyo mama, utafikiri ndiye mama yake wa kuzaa…’ akasema mama mwenye nyumba, kwa sauti ya wivu.

‘Basi kama huyo mama wa mkono wa baraka umeona anafaa,kwanini asiwe ndiye mfanayakazi tumlipe yeye badala yake, siumesema anaweza kulea, na huhisi kuwa ana matatizo , wewe unaonaje hilo, maana hawa wasichana wa kazi wakianza kuomba ruhusa ujue wana lao jambo …’akasema.

‘Hapana sio vyema, huyu msichana anasaidia sana hapa nyumbani, ndio huyo mama upo, lakini simwamini sana…na wakati mwingine anaweza kuondoka unafikiri mtoto atabakia na nani..hapana tusimuondoe huyo mfanyakazi wa ndani..’akasema

 Basi Miezi ikapita , mwaka ukapita, mtoto akawa anatembea. Na mtu aliyekuwa akimlea huyo mtoto kwa muda wote ni mama wa mitaani, au mama mwenye mkono wa baraka.

Siku moja alikuja mama mmoja akiwa na mtoto wa dada yake, alikuja baada ya kuelekezwa kuwa kuna mama mmoja ambaye, mtoto akiwa na tatizo la kulia, au kushituka usiku, basi mama huyo kwa kutumia mikono yake anamuombea, na mtoto anatulia na tatizo hilo huisha.

Basi mama huyo kutoka mbali, akafika kwenye hiyo nyumba na mtoto wa dada yake mgongoni. Alipofika siku hiyo, hakukuta wenyeji wengine, zaidi ya huyo mama, na siku hiyo hakukuwa na watu wengi wenye shida kama siku nyingine, kwahiyo akapata nafasi ya kumuona huyo mama kwa haraka tu,  alioingia kwenye chumba anachokaa huyo mama, aakamkuta akiwa anafanya usafi wake hapo ndani kwake;

‘Oh..una shida…?’ akauliza huyo mama, huwa haongei sana

‘Ndio mtoto wangu analia ,anshituka…nataka tiba…’akasema

‘Mimi sina tiba, tiba ni majaliwa ..ya kutoka mbinguni…haya mlete….’akasema huyo mama hakutaka maelezo zaidi.

Mama huyo akamtoa mtoto wake, na yule mama akamchukua yuke mtoto na kumpakata kama anavyofanya kwa wengine na kumshika kichwani, na akamwambia mtoto wake hatashituka shituaka tena usiku au kulia lia, na huyo mama akataka kuondoka.

Waliokuwepo wanasema ghafla, walimuona huyo mama akitoa mbio, huku anapiga ukulele…akiwa hana mtoto na watu pale wakaanza kuulizana kulikoni, na mmojawapo akaingia ndani akamkuta huyo mama akiwa na mtoto kampakata, huyo mama hkuongea kitu .

Baadaye huyo mama aliyekuja na mtoto akarudi kwa huyo mama, lakini hakuingia ndani, akaagiza kwa watu kuwa wamchukulie mtoto wake kwa huyo mama, na mtu mmoja akajitolea akaingia na kumchukua mtoto, na kumkabiddhi huyo mama.

‘Mumemkutaje huyo mama..?’ akauliza

‘Kama kawaida kwani kumetokea nini?’ akaulizwa

‘Hata siwezi kusema hapa ilimradi nimetimiza shida yangu, hapa sikai tena, naondoka..’akasema na kuondoka na mtoto wake.

Mara kukazuka minong’ono ya chini kwa chini,  kuwa mama aliyefika, alitoka mbali, akiwa kaelekezwa na mganga wa kienyeji kuwa tatizo la mtoto wake ni huyo mama. Na alivyoambiwa ni kuwa huyo mama sio kweli kuwa ana mkono wa baraka, kama watu wanavyohisi…mama huyo sio kutoka mbinguni kama watu wanavyodai…

‘Sasa kama sio hivyo mbona anatenda miujiza..’watu wakahoji

‘Hata shetani anatenda miujiza,….’wapambe wakasema

‘Kwahiyo huyo mama ni shetani…?’ wakauliza

‘Huyo mama ni mwanga, …katokea makaburini…’watu wakasema

‘Heeeh..mungu wangu…’waliosikia hivyo wakashituka, na wapambe hawakuishia hapo wakaendelea kuelezea wanayoyajua, japokuwa wengine walisikia tu.

‘Huyo mama mnavyomuona huo mkono wake mnaosema ni wa baraka,  ni mkono wenye mazingara ya kichwawi..’wakasema

‘Mhh, hayo makubwa, mbona upo kawaida tu…nani kauona kuwa ni mkono wa kichawi…’watu wakaendelea kuhoji.

‘Ule mkono mnauona wa kawaida lakini kwa wataalamu wameshauona sio mkono kama mikono yetu mkono ule ni wa mtoto mchanga..’wakasema

‘Tobaa, ..’wakasema waliosema, na wengine wakamaka hivi ‘yesuuuh’….wengine, ‘mamamamama, tumekufa..’ikawa kia mmoja anamaka kwa jinsi anavyoona yeye.

Ulikuwa uvumi, ulioenezwa kwa namna yake…na ulienea kwa kasi kutoka sikio moja hadi jingine. Uvumi wa kusikia huvuta hisia, na kila mwenye kuusikia hujiwa na hamasa ya kujua zaidi.

Wakasema kuwa mama huyo ana mkono wa mtoto mchanga ambao ndio zindiko lake la uchawi, analoga watu usiku, anawawangia wakiwa wamelala, anapita kila nyumba na akichoka hulala kwenye upenuni mwa nyumba.

‘Ni kweli huwa anafanya hivyo..leo yupo hapa, kesho kalala hapa kesho nyingine kule..mama huyo kiukweli hana makazi maalumu, sasa hivi ndio kaamua kwenda kwa yule mama mwerevu, si wanajuana, au ndio zao wote hao…’wakasema watu.

‘Kumbe ndio maana watoto wanalia sana usiku , nahsi watoto hao wanamuona..siunajua watoto wadogo wanaona vitu ambavyo sisi hatuwei kuviona, …, sasa iweje watoto hao hao wakienda kwake hupona..?’ watu wakahoji.

‘Mama huyo ni mjanja, anawaloga watu, hasa watoto usiku, na mchana anakuja kuwaondoa uchawi wake… ndio maana wanalia…, halafu yeye huyo huyo anajifanya kuja kuwaagua, kwa kutumia mkono wake, ngoja atakuja mtoa uchawi mtauona huo mkono wake ulivyo..’wapambe wakazidi kuliongelea hilo, utafikiri walikuwepo kwa huyo mtaalamu.

 Mazungumzo haya yalizuka chini kwa chini, yaakaenezwa, lakini chanzo chake ilikuwa kutoka kwa mama huyu aliyekuja kutoka kijiji cha jirani, akiwa na mtoto wa dada yake, ambaye alisambaza maneno haya kama vumbi katika jangwa, hakuna aliyetaka kujua kwanini huyo mama alikuja na mtoto wa dada yake, kwanini dada yake hakuja yeye mwenyewe…

`Hivi ilikuwaje mpaka ukweli huo ukagundulikana kuwa mama huyo ni mwanga..’ wambea wakaanza kudadisi.

‘Hata mimi nilishamshitukia huyo mama…, hebu muone alivyo, kwanini hajifunui uso wake… hawa watu wanaojifunika funika usoni , kichwani, mimi nawachukia kweli…miguo mwili mnzima, wanaficha nini hawa watu….mimi siwaamini hao watu, yaani nawachukia……akilini mwangu nilishamuhisi vibaya huyo mama, nilihisi kuna jambo..huenda ni shetani, kichwanii pale hakuna kitu ni fuvu tu…’wakazidi kusema wenye kusema.

‘Eti nini…hapana haiwezekani…huyu mama nilikwenda kwake juzi mtoto wangu alikuwa analia, akamshika kichwani na mtoto wangu hajalia lia tena,.., sasa hayo mnayozungumza nashinwa kuwaelewa..’akasema mwingine.

‘Ina maana kuwa usiku alikuja akakuwangia, mtoto akawa analia, ..ulipokwenda kwake, akaondoa uchawi wake,..hahaha, watu wajanja, lakini sasa atashindwa, ashindwe na alegeea…anajifanya ni mpenzi wa watoto..kumbe ndipo uchawi wake ulipo…huyu hafai hapa kijijini…’; watu wakawa wanongea, na wema wa mama ukaonekana ni ujahili…chuki ikaanza.

‘Huyo mama mkimuona alivyo hamtaamini, sio binadamu yule …yupo kama aaah naogopa hata kusema, maana huyo mama aliyetuambia kasema usimtaje alivyo, utakufa…yule mama ni mwanga ..’akasema

‘Ina maana aliyewaambia hivyo ni huyo mama aliyekwenda kwake akatoka mbio akipiga ukelele..nasiki alipofika kwa huyo mama, alitoka mbio na kukimbia eti ni kweli…?’ akaulizwa

‘Yule mama alitokea kwa mganga, mganga mmoja mashuhuri tu, mganga huyo huwa anatoa uchawi majumbani kwa watu…na huyo mama anasema kabla ya hapo kutoka na matatizo ya mtoto wake, aliwahi hata kufika kwa hawa wanaoombea ombea watu, watu wa dini, wakamwambia mtoto wake anaona mapepo….

Sasa wakaona kama ni mapepo, kwanini wasimuone huyo mtaalamu,…umeshawahi kumsikia jamaa mmoja huwa anatoa uchwai majumbani…sasa huyo ndiye aliyemuambia huyo mama, kuhusu huyu mama mchawi…, ngoja siku moja atakuja hapa muone vimbwanga vyake, wachawi wote watatolewa..kuna wachawi humu kijijini,…hawa wazee wazee wote ni wachawi tu..,waone macho yao yalivyo…yanatisha, sasa kiama chao kimekuja…’watu wenye yao moyoni, wenye chuki zao na hasira wakaanza kunadi.

‘Sisi tunahangaika usiku na mchana kutafuta riziki zetu, wenzetu wanafaidi, usiku wanatufanyisha kazi mimi ninausongo na hawa watu…we acha tu….’mmoja aliyekuwa na yake moyoni akasema.

;Hebu tuambie kuhusu hayo tunataka kujua ukweli, na kama kuna ushahidi…we ngoja tu….huyo mama alijuaje…hebu tuambie vyema.

‘Huyo mama aliambiwa ili mtoto wake apone, basi aende kwa huyo mama,..kwani ndiye kamloga mtoto wake, na wao ndio maana wanahangaika hawafanikiwi….akaambiwa kuna mama mmoja kijiji cha jirani huwa anawatembelea usiku, mama huyo usiku anapa na ungo anatembea huku na kule, ni malikia wa wachawi…, ‘msemaji akasema.

‘Unaona..malikia wa wachawi,…watoto wanatumiwa kumlinda,..unaona hata mchana, watoto wamemzunguka, watoto hao wameshaharibiwa vichwa vyao…’msikilizaji akanogezea.

‘Sasa huyo mama aliyejitolea kutoka kijiji cha jirani, akifika kwa huyo mama mnayemuita mama wa mkono wa baraka, mama huyo akajitolea kuja kumtoa mwanga huyo uchawi,..huoni alikuja na mtoto wa dada yake, dada yake aliogopa kufanya hivyo…, yeye kapewa dawa, dawa hiyo ilitakiwa kumwagia huyo mama usoni….’akasema

‘Kumwagia usoni, huo si mtihani …! atamumwagiaje usoni wakati huyo mama anajifunika wakati wote…kama ninja?’mpambe akauliza.

‘Aliambiwa afenya kila mbinu, la sivyo mtoto wao, maisha yao, …yataharibika, akifanya hivyo, watafanikiwa,..mtoto atapona, na maisha yao yatajaa baraka..hata yeye ana shida zake, ..hakutaka uzitaja, ..aliambiwa akifanya hivyo atafanikiwa..’

Alichotakiwa ni kufanya hayo, maana uchawi wa huyo mama upo usoni na mikononi..akimwagiwa huo unga usoni, uchawi wote unapotea, ila kwa msharti....’akasema msemaji

‘Oooh, sasa hiyo kazi alifanyaje maana nasikia ukitaka ubaya kwa yule mama ujaribu kuondoa hiyo nguo kichwani mwake….?’ Wakauliza wapambe.

‘Wakina mama wajasiri , hasa unapogusa maswala ya watoto wao, mama huyo alimua kujitolea liwalo na liwe,..nani kama mama …mnaona, mama ana uchungu na mtoto wake, akasema liwalo na liwe, nitafanya hivyo, na kweli akafanya…’akasema mpambe.

‘Akafanya alifanyaje…?’ wakauliza kwa hamasa.

‘Mama alipofika kwa huyo mama mwanga…, akajifanya hajui lolote, akiwa na uchungu wa mwanae, akiwa na uchungu wa maisha, akiwa na uchungu wa matatizo yake…kwanza akasubiria, mtoto aondolewe huo uchawi wa huyo mwanga, anachofanya ni kuondoa uchawi wake, hakuna zaidi…muhimu baada ya hapo, ahakikishe huyo mama anamwagiwa huo unga usoni…’akasema

‘Tunachouliza aliwezaje kumfunua huyo mama …?’ wakauliza wenye kuuliza.

‘Yule mama alikuwa kampakata mtoto, mikono umemshika mtoto, angeliwezaje kujizuia asitolewe hiyo nguo kichwani, akiwa kampakata hivi…...unaona ujanja aliotumia huyo mama aliyejitoela, hakujali kuwa mtoto anaweza kudondoshwa chini,..alijua kabisa huyo mama atabakia kuhangaika tu…alipohakikisha huyo mama keshamtoa mtoto uchawi, kwa haraka akasimama na kwa haraka akamvamia huyo mama na kuvuta ile nguo kichwani mwake..’akasema

‘Oooh, kwahiyo akamuona huyo mama alivyo, yupoje huyo mama, ana kichwa kama sisi..au ni fuvu la mtu..maana kama ni shetani atakuwa na fuvu la kichwa, sisi tunaona ni kichwa tu au sio….’jamaa wakauliza na wao wakitilia chachandu,

‘Yule mama anasema alichoona ni siri yake,..yeye hakupoteza muda, akamwagia yule mama hiyo dawa, na yule mama akawa ananguruma kama simba, maana uchawi ulikuwa unamtoka,..yule mama akaogopa, akaona sasa ataliwa na simba mchawi, maana wachawi wana vitisho wanaweza kujigeuza maumbo tofauti tofauti wakipambana na maadui zao, mama akatimua mbio…’akasema muhadithiaji.

‘Ndio akamuacha mtoto wake au ilikuaje maana nasikia likimbia ila mtoto…mimi sijaona mama akimuacha mtoto wake kwenye shida….?!’akasema mwingine akitaka kujua.

‘Alijua kuwa dawa ikimaliza kufanya kazi, huyo mama hatakuwa na nguvu tena hataweza kumfanya lolote huyo mtoto, sana sana huyo mama atalegea tu, aliambiwa huyo mama unga ukimgusa usoni, hana ujanja tena..hataweza hata kusimama…atabadilika na kuabdilika lakini ujanja kwisha…..’akasema.

‘Sasa ikawaje, mtoto wake alimchukuaje ..na walimkutaje huyo mama ?’ akaulizwa

‘Yule sio binadamu, mganga alimwambia asije kusema alichokiona, akisema tu, hali ile inaweza kujirudia, na huyo mama mwanga atamuandama mpaka amuue, yeye na familia yake maana wameshagundua siri yake, ili awe salama,asiseme kabisa alichokiona….’akasema huyo mpambe

‘Kumbe ndio maana yule mwanaume aliyejaribu kumfunua mpaka sasa hali yake sio nzuri, ilitakiwa asifanye hivyo eti…..na nasikia hajawahi kusema aliona nini, ndio maana mpaka sasa yupo hai…’akasema msikilizaji

‘Mimi mwenyewe , nilimuona huyo mama akitimua mbio kutoka kwa huyo mama mwanga, nikamfuatilia mpaka hapo alipofikia, nikamsikia akimuelezea huyo mwenyeji wake, na mwenyeji wake, akasema sasa anajisiki vema, atatoka nje,maana muda mwingi kila akitaka kutoka anahisi kuona sura ya kutisha.

‘Usiongee kabisa…usije kusema ulichokiona hiyo ni siri yako mpaka kufa kwako, ..hata mimi usiniambie japokuwa nimeshamuona…’nilisikia huyo mama akimwambia huyo jamaa yake....’porojo ikanoga.

‘Kwahiyo huyo mama aliyekuja na mtoto wanafahamiana na huyo mwanaume aliyepatikana na majanga kwa kutaka kumfunua huyo mama?’ wapambe wakataka kutafuta mengine, siunajue tena wambea, wapuliza mafundo walivyo.

‘Wanajuana, walikuwa wapenzi huko walipokuwa kijijini kwako, baadaye wakaachana, bwana kaja kutafuta maisha akamtelekeza mwenzake,..mwanamke huko alikobakia akaona isiwe taabu akatafuta bwana mwingine, lakini ya kale ni dhahabu, wakati anakuja huku akagundua kuwa mtaliki wake yupo hapa kijijini ..basi akamuendea,..akamkuta yupo kitandani kachanganyikiwa, akauliza akaambiwa chanzo cha matatizo yake ni nini, akawaambia walimuelezea , kua yeye kaja kuyamaliza… ndio hapo alipofikia..’umbea ukafika kwake.

‘Sasa ina maana huyo mwanaume keshapona,..?’ akaulizwa

‘Keshapona, …unajua huyo mwanaume alikumbwa na kitu kama mapepo baada ya kumfunua huyo mama mwanga,…huyo mama mwanga akamvaa kimapepo, akawa anamtokea tokea kumuogopesha, sasa..si uchawi umeshaondolewa, …pepo halina nguvu tena, kwahiyo ni lazima huyo jamaa atapona,..keshapona utamuona mitaani…muhimu asiseme alichokiona…’habari ikaenea hivyo.


‘Mimi sasa naanza kuamini kuwa kweli huyo mama ni mwanga, nimemgundua mbaya wangu, ndiye anayewawangia watoto wetu usiku, halafu anakuja kuwashika kichwa akijifanya anawatoa uchawi…kweli wote hapa kijijini tumelogezewa, katupumbaza, usiku anatufanisha kazi, mali zetu tunampelekea yeye, …hapa ni lazima tufanye kitu…vijana mpo…’akasema mwenye kusema akianza kuwahamasisha vijana.

‘Basi kama ni mwanga, lazima aondoke, ahamie huko alikotoka, nani anajua wapi alikotoka, huenda huko wamemfukuza, ndio maana akaja hapa kwa mbinu hizo…wanga wanakimbili hapa kijijini kwetu sisi tunakaa kimiya..hapana lazima hili lifaniwe kazi…’akasema

‘Lazima, tutawafukuza,..tutawaangamiza mmoja mmoja’ vijana wakaingizwa kwenye mkumbo. Wema wa yule mama uliyeyuka kama barafu kwenye maji ya moto, jina baya akapewa,..matusi kejeli..kashifa, ….sasa iliyobakia nini….

********.

Haikupita siku mbili…jambo likazuka.

Siku moja usiku watu wakiwa wamelala, kukasikika kilio, kilio hiki kilitokea kwenye nyumba moja, kilikuwa kilio cha kuonyesha kuna hatari, watu walikuwa wamejichokea na walipoona kilio kimekoma, wakajua ni wahuni tu, au ni migogoro ya familia na imepita.

Lakini kwa majirani, waliosikia vyema, walilala kwa mashaka, kila mmoja akitaka kujua kuna kitu gani kimetokea, hasa wale wa karibu na hiyo nyumba ambapo kilio hicho kilitokea, na kila mmoja akawa anamuuliza mwenzake, amesikia kilio hicho…nimesikia, lakini kinatoka wapi…watu wakawa wanaulizana.

Kumbe kilio hicho kilikuwa kimetokea kwenye chumba cha uwani ambapo mama wa mitaani, au maam wa mkono wa baraka, alikuwa akilala. Chumba hicho sasa kilikuwa kizuri kwa hivi sasa huwezi kusema ni chumba cha uwani. Mwenye nyumba alimua kukitengeneza vyema, kutokana na misaada iliyokuwa ikiletwa, na neema ya kipato.

Mwenyeji aliamua kukitengeneza vyema kwa ajili ya huyu mama, ili hata wageni wakifika wapate sehemu nzuri ya kupumzikia.

Sasa usiku huo, kilio kikasikika kwenye shemu hiyo, na hata mwenyeji mwenye nyumba aliskia kilio hicho, lakini hakuwa na uhakika ni cha nani, kwani kilikuwa ni kilio cha muda mfupi halafu kukawa kimya

Wenye nyumba waliposikia kilio hicho walizinduaka kwenye usingizi, na kuulizana, na kila mmoja akawa hana cha kujielezea zaidi ya kusema ‘hata mimi nimesikia lakini sina uhakika ni kilio kutoka hapa kwetu au huko nje mitaani…’ basi walipona kimia, wakadharau wakizania kuwa huenda kuna mtu, au watu waliokuja kuhudumia wanapandisha mashetani yao…lakini mara nyingi hakuna watu wanaolala hapo zaidy ya huyo mama na hata mfanyakazi wa ndani huwa  halali huko.

‘Nasikia kaam harufu ya moshi…’akasema mama mwenye nyumba.

‘Sijui nania nachoma mataka taka usiku huu…’akasema baba mwenye nyumba.

‘Hiyo sio haraufu ya mataka taka….nahisi kuna moto..mume wangu, kuna moto nje..’akasema mke mtu, na mume akakupuka na yee akahisi hivyo.

Moshi ukawa umetanda kuzunguka nyumba…

‘Moto…’akawa anasema mfanyakazi wa nyumba kutoka chumba cha pili.

‘Tokeni nje,..umetokea wapi huo moto, mchukue mtoto..’akasema baba mwenye nyumba akitangulia kutoka nje..

Walipotoka nje, walikutana na moto mkubwa ukitokea chumba cha uwani, chumba alichokuwa akilala mama wa mkono wa baraka, …chumba chote kilikuwa kimezungukuwa na moto…majiranai wakaanza kumiminika..

‘Moto..moto….saidia kuzima moto..moto…’.ikawa sasa ni ujirani mwema kila mmoja anakimbilia ndoo na maji, kila mbinu za kuuzima huo moto zikafanyika…..’

NB: Tuone ubaya wa biandamu, jinsi wanavyoweza kubadili mambo wema ukawa ubaya, propaganda.


WAZO LA LEO: Fitina ni mbaya sana, fitina inaweza kuwa chanzo cha vita, fitina huwatengenisha marafiki, na kuwa maadui ndugu na ndugu wakakosana. Fitina inaweza kutengenezwa kwa mdomo, kalamu, au propaganda potofu,…majina mabaya huundwa,..maana ukitaka kumuua mbwa kwanza anza kwa kumuita majina mbaya, vyombo vya habari vikatumika, kurudia rudia hizo propaganda, na mawakala wa fitina wakaeneza uvumi, na hata kile kilichokuwa kizuri kikageuka kuwa kibaya..mwisho wake wanaeleekza malengo yao. Jamani tuweni makini na maneno ya kusikia, uvumi, propaganda zisizo na uhakika.

Ni mimi: emu-three

No comments :