‘Nimesema nataka mtoto wangu….kama hutaki
kunipa mtoto wangu nitamchukua mwenyewe, ni mtoto wangu….mimi nataka mtoto wangu, unanisikia…’akasema huyo
mama kwa msisitizo.
‘Mhh…wewe mama una maana gani kusema
hivyo, ..utafungwa, isije ikawa ndio nyie mnaoiba watoto, huyo mtoto wako
ulimpa nani, au ulimpatia wapi..?’akamuuliza na yule mama kwanza akatulia
halafu akasema;
‘Nilimpatia mbinguni,…unasikia nimetoa
mbinguni,..na wewe ukamuiba mtoto wangu….mimi nimesema nataka mtoto wangu, nipe
mtoto wangu haraka…’akasema akinyosha mikono miwili kama anataka kumvamia huyu
mdada, na huyo mdada akawa anarudi nyuma kumkwepa huyo mama,
Mdogo mtu, alipoona hali sio shwari
akageuka kutaka kumkimbia huyo mama, na huyo mama akawa keshamshika sehemu ya
nguo yake kwa nyuma, mdada akawa najivuta ili huyo mama amuachie, lakini yule
mama akawa ameshikilia sehemu hiyo ya nguo vyema, wakawa sasa wanavutana…
‘Wewe mama vipi hebu niachie utachana nguo
yangu….’akawa analalamika
Mdogo mtu huyo kuona vile akawa anarudi kinyume
nyume kufuata jinsi anavyovutwa na huyo mama, kwa nyuma huku akijaribu kuvuta
nguo yake, huku akichelea isije ikachanika…. na watoto waliokuwepo hapo wakawa
wanashangilia kama vile wameona mchezo..yule mama akawa anavuta huko akisema;
‘Nataka mtoto wangu, nipe mtoto wangu,
umeniibia mtoto wangu….’yule mama akawa anasema hayo kwa hasira na watoto nao
wanamuigizia, huku wakiruka ruka…
Mdogo mtu kuona hivyo, akawa keshatahayari
maana sasa anakuwa kama anasutwa,na kuabishwa, …
Alichofanya ni kama kukubalia anvyofanya
huyo mama, akasogea kinyume nyume adi akamkariia huyo mama, na huyo mama
akaachia hiyo nguo na kusema;
‘Haya nipe mtoto wangu…’akasema
‘Yupo wapi huyo mtoto wako..?’ akamuuliza
‘Unaye….umemficha..namtaka haraka…’akasema
‘Nimemficha wapi?’ akamuuliza
Yule mama, akamsogelea na kwa sauti ya
kunong’ona akasema
‘Najua wapi ulipomficha, nitakwenda
kumchukua….’akasema
Mdada akageuka huku na kule, akiogopa watu
wasije kumuelewa vibaya ionekane kuwa kweli yeye kamuibia huyo mama mtoto,…
japokuwa alishasikia kuwa huyo mama anamfanyia hivyo kila mtu.
Kwa haraka akanyosha mkono kwa mtu wa
bajaji, aliyekuwa akipita, na huyo mtu wa bajaji akafika,na kumsaidia
kumuachanisha na huyo mama, na wakati anaondoka yule mama akasema kwa sauti;
‘Umenisikia eeh, nitakwenda kumchukua huko
ulipomficha…’akasema na wakati huo bajaji ilishaanza kuondoka kwa mwendo wa
kasi…
‘Huyo mama balaa, mimi simuamini,
….’akasema dereva wa bajaji
‘Anatokea wapi?’ akauliza mdada.
‘Nani anajua…mimi nahisi kachanganyikiwa
tu, japokuwa watu wanadai kuwa ni mama sijui kutoka mbinguni lakini…..ni mwehu
tu….ila maadui wake wakubwa ni akina mama…hawapendi akina mama..’akasema.
‘Kwanini anasema kuwa anataka mtoto wake?’
akauliza
‘Inavyoonekama alizaa halafu watu
wakamchukau mtoto wake kwa vilekachanganikiwa, maana hali kama hio ataweza
kulea mtoto…’akasema mwenye bajaji
‘Ulishawahi kumuona sura yake?’ akauliza
‘Mhh, ukitaka mkosane, jaribu kumfunua,
kuna mtu alijaribu kufanya hivyo, alichokipata hata kisahau,…anaugulia
macho…yupo kitandani mpaka sasa….’akasema
‘Alifanywa nini…?’ aakulizwa
‘Huyo jamaa hataki hata kusema….kawa kama
kachanganyikiwa, na huyu mama akisema nitafanya, au utapata tatizo ulani , ujue
litatokea, ndio maana wanamuita mama kutoka mbinguni…..’akasema huyo dereva wa
bajaji
‘Oh, sasa naona hii ni hatari, ngoja
niwapigie ndugu zangu simu….’akasema huku akichukua simu yake kwuasiliana na
dada ake na shemejiye.
Tuendelee na kisa chetu…..
***********
Huku kwa mama yaani dada mtu, hali ikaendelea kuwa shwari…japokuwa
mawazo ya hapa na pale ylikuwa yakitokwa hasa akiwa peke yake hana kazi,
anajaribu kuwazia yale yaliyotokea hasa kuhus mtoto na kufanana kwake na mumewe
lakini alifikia hatua akaona ni kudra ya mungu ipo siku atajua ukweli.
Alikumbuka pia kuwa alipokea simu kutoka kwa mdogo wake siku
alipoondoka kuwa wawe makini na huyo mama, ..simu hiyo iliwafanya wawe walinzi,
na kila akitoka alikuwa akicha onyo kwa mfanyakazi, kuwa mama huyo akifika
hapo, ahakikishe mtto yupo ndani salama..
‘Kama atajaribu kufanya fujo piga kelele, na simu hii hapa nipigie
haraka…unasikia…’akaambiwa mfanyakazi.
Kwahiyo kipindi cha siku tatu wakawa wanaishi kwa mashaka, lakini
hakuna lolote liliwahi kutokea, na hata
kule kupita pita mitaani kwa huyo mama akiimba kukawa kumepungua kwa kiasi
kikubwa, mama huyo akawa anaonekana mara chache chache, hadi wiki mbili
zikapita. Watu wakaanza kumzoea, na kumuona ni wa kawaida tu.
Wiki mbili zikapita, familia hii ikawa ni familia yenye mtoto, na
kila aliyekuja alitambulishwa kuwa huyo ni mtoto wa familia hiyo, wamempataje,
ikawa siri yao, kwani hakuna mtu aliyewhi kumuona huyo mama akiwa na mimba.
‘Mimba nyingine hazionekani wazi..huyu mama muda wote huwa anavaa
gauni pana huenda alikuwa mja mzito, mimi niliwahi kumtania kuwa ana mimba
akaniambia aipate wapi…sasa sijui kama alikuwa akinitania au…’watu wakawa
wanaongea.
‘Haiwezekani..mimi hilo sikubaliani nalo, labda kama mtoto huyo
kaletwa,na-nasikia kuna siku mdogo wake aliwahi kufika kwa siri, mimi nahisi mdogo
wake alijifungua akaona amleta huyo mtoto hapo kwa dada yake…’akasema mwingine.
‘Kwanini afanye hivyo, kwani yeye hawezi kulea..au kuna siri gani
kati yao…?’ akauliza mwingine.
‘Tunasema kama huenda mdogo wake alifanya hivyo, lakini sina
uhakika, nimejaribu kumuuliza huyo mama, lakini anadai ni mtoto wake
alijifungua usiku…unakumuka alikuwa anaumwa umwa…’akasema
‘Yawezekana, …halafu kinachofanya tuamini kuwa ni mtoto wao, ..mtoto
huyo anafanana sana na mume wa huyo mama..kabisa kabisa…sasa hapo
utasemaje…’akasema mwenzake.
‘Mhh, mimi sijawahi kwenda kumchunguza..kama ni hivyo basi
yawezekan kuwa ni kweli,hata hivyo iweje mtu ajifungue na kuendelea na shughuli
zake kama kawaida, ndipo hapo tunamtlia mashaka, mzazi akijiungua angalau siku
sana anakaa nyumbani….’akasema
‘Na pia yawezekana ikawa kuna jambo jingine…mimi nahisi kuna jambo
limetokea ndani ya hiyo familia, lakini wameamua kuliicha kifamilia, wewe
unawaonaje hao watu…’akasema mwenzake
‘Umeanza..jambo gani hilo jingine…mimi nawaona kama kawaida
tu..kwani wewe unahisi kuna nini kimetokea, zaidi ya huyo mtoto?’ akauliza
mwenzake.
‘Hawa wapendwa wamekaa siku nyingi bila kuzaa, huenda walipanga
huyo mume aende kujaribu sehemu nyingine mbali, …halafu akizaliwa mtoto
wamchukue..hilo lawezekana pia, au nikuambie kitu huyo mdogo mtu anaweza
akatembea na shemeji yake akapata mtoto kwa siri, akamleta kwa siri, wewe
waonaje hilo….’akasema
‘Mhh, hilo mimi sijui…na achana kabisa na hizo tetesi zisizi na
mshiko,wakikusikia wenyewe, utafungwa..unaifahamu ile familia haitaki majungu
kabisa, na yule mama mimi namuheshimu kweli, ukiwa na lako anakupasha
waziwazii, unabakia kuaibika, mimi nakushauri haya yaache kama yalivyo…’akasema
mwenzake.
‘Mimi nimesema tu, wala…simuambi mtu mwingine nimekuambia wewe tu
na mume wangu…na wewe ukimuambia mume wako shauri lako..mume wako hana dogo….’akasema
‘Acha majungu wewe..mimi sipendi hiyo tabia yako…mume wangu hana
dogo umemjulia wapi kuwa ahan dogo, mama nanihii hiyo tabia yako tutakosana,
kaa na mume wako, achana na waume wa wenzako, achana na familia za wenzako kila
mtu anajua mambo yeka….nimekukanya siku nyingi, tutakuwa hatuongei tena mimi na
wewe…’akasema mwenzeka, na huyo mama akaonyesha ishara ya kufunga mdomo, na
wakaachana na mwenzake.
Kwahiyo siri ya mtoto huyo ikawa ndani ya familia hiyo hata
mfanyakazi wa ndani alijua kuwa mtoto huyo ni wa huyo mama, hakutakiwa kusema
zaidi, hata pale alipomdadisi huyo mama kwanini hamnyonyesi huyo mtoto.
‘Matiti yangu yana matatizo…nimeshauriwa kuwa nisimnyonyeshe
maziwa yangu, atakuwa akitumia maziwa hayo ya unga…’akasema mama mwenye nyumba.
‘Lakini matiti yako hayafanani kama mtu aliyewahi kuzaa..na iweje
ujifungue nab ado uwe na nguvu za kufanyakzi, mimi nasikia mtu akijifungua
anaakaa nyumbani siku…40, au….?’akasema huyo mfanyakazi na akawa kama anuliza.
‘Kwanza wwe uliwahi kuyaonea wapi matiti yangu?’ akauliza mama
mwenye kwa uso wa mshangao.
‘Wakati mwingine wewe huwa unavaa khanga, na nguo ya kuonyesha , matiti
yako yanaonekana bado madogo, tofauti na akina mama waliojiungua karibuni…’akasema
‘Acha kabisa hiyo tabia, mambo ya hapa ndani yaache kam yalivyo,
wewe umekuja kwa kazi sio kuchunguza chunguza ammbo ya humu ndani, mimi
mwenyewe nimeamua kuwa hivyo sio lazima kila mwanamke anayejifungua kupumzika
hizo siku inategemeana na afya na mazoea ya mtu….kumbuka nikuambie, nyumba hii
haitaki majungu ..umenielewa..’akaonywa, na kweli huyo mfanyakazi akawa kimia
hakuwahi kuhoji tena kuhusu huyo mtoto au familia hiyo.
Kwahiyo ikawa ni siri ya familia, na ikajulikana hivyo kuwa
familia hiyo ina mtoto na mtoto huyo huenda kazaliwa kimuijiza, mambo ya
kijijini yakaenea hivyo na kufifia hivyo.
Mama wa kufikia, akawa amejipanga vyema katika shughuli zake,
miradi yake ikawa inaendelea vyema, ikawa na baraka, wateja wengi,…utafikiri
neema hiyo ililetwa na kuja kwa huyo mtoto, kwa kuongezeka kwa biashara na
wateja, mama huyo ikabidi atafute mtu wa kumsaidia katika baishara zake, na
hapo akawa anapata hata nafsai ya kurudi rudi nyumbani kuona kinachoendelea.
Basi mama huyu akiona
kwenye biashara yake kupo shwari, anamuachia huyo msaidizi wake kazi za
kuendelea na biashara yeye anakimbilia nyumba mara moja kuona kinachoendelea
nyumbani kwake, alifanya hivyo
kuhakikisha kuwa huyo mfanyakazi hafanyi makosa…na bahati nzuri mfanyakazi huyo
alijua nini cha kufanya kwa wakati gani…akawa muda wote yupo nyumbani na mtoto.
Na, siku zikapita,…mawiki , yakapita, inakaribia sasa mwezi …
Siku moja wakati anarudi nyumbani, akashangaa, kuwa yule mfanyakazi wa ndani kakaa
nje na yule mama wa ajabu wakiongea! Siku hiyo alipata mshutuko wa aina yake,
akakumbuka onyo kutoka kwa mdogo wake, akajiuliza kulikoni!
Kwanza hakutaka kuwashitua, akaingia ndani na kufanya shughuli
zake, alipotoka hakumuona huyo mama wa ajabu, siku hiyo hakusema lolote, siku
ya pili yake ikawa hivyo hivyo, na ilipotokea hivyo siku ya tatu, mama huyu
akaona amuulize huyo mfanyakazi wake,..kwani siku hiyo ya tatu alimuona huyo
mama wa mitaani akiwa kambeba mtoto wao.
‘Vipi wewe, mbona unampa huyo mama mtoto, hujasikia
nilivyokuambia, unamfahamu huyo mama alivyo huwa anadai kuwa anataka mtoto
wake, na kila mwenye mtoto mdogo anadaiwa kuwa kamuibia huyo mama mtoto, sasa
kwanini hutaki kunisikia ….?’ Akamuuliza huyo mfanyakazi na huyo mfanyakazi
akasema;
‘Mama, huyu mama wa ajabu, anampenda sana huyu mtoto wako, na
hutaamini, kila mara huyu mtoto akilia sana, mama huyu hutokea, na akimshika
huyu mtoto kichwa, basi mtoto hutulia kabisa….’akasema huyo mfanyakazi
akonyesha uso wa furaha kama vile hilo aliloambiwa halina maana kwake.
‘Mimi nimeshakukanya, kama hutaki kazi usema,..huyo mama anadai
kuwa anataka mtoto wake kwahiyo kila mtoto mchanga ni wake…anaweza akaondoka na
huyo mtoto unafikiri utamapata wapi, unafahamu wapi huyo mama katokea,
nakuambia ukweli, siku mtoto akitoweka, ujue unakwenda kuozea jela….’akasema
‘Ni kweli kila mahali kwenye mtoto mchanga, mama huyu hufika na
kumbeba mtoto, nimeulizia kwa majirani wenye watoto, lakini hafanyi lolote
baya, ndio hivyo mtoto akilia tu huyu mama akifika akamshika huyo mtoto
kichwani, mtoto anatulia…mimi sioni ubaya wake….’akasema.
‘Kwahiyo sio hapa tu, anafika popote kwenye mtoto mchanga?’
akauliza mama mwenye nyumba.
‘Ndio mama, sio hapa tu, ..anafika sehemu yoyoye yenye mtoto
mchanga,..ni kipenzi cha watoto, sio wachanga tu….na sikutaka kukuambia mapema
karibu siku nyingi huyu mama anafika hapa…’akasema
‘Sasa kwanini hukuniambia….’akasema mama mwenye nyumba kwa hasira.
‘Mama sikukuambia tu, mtoto wako anakuwa analia sana ukiondoka, kila nikimpa maziwa hataki, lakini akifika
huyu mama…mtoto ananyamaza, ….hutaamini, mama huyu anamchukua anamnyonyeshwa
maziwa anamshika kichwa, mtoto ananyamaza kabisa utafikiri ….’akasema
‘Anamnyonyesha maziwa! Maziwa gani hayo?’ akauliza kwa mshangao
‘Hayo tunayomtengenezeaga kila siku…’akasema kwa wasiwasi akionyesha
kuogopa.
‘Yaani umeamua kumpa yeye hata maziwa, ina maana wewe umeshindwa
kumnyonyeshaa mtoto wangu, si ndio kazi niliokuchukua nayo, kwanini unafanya
hivyo…?’ akauliza mama akiwa kakasirika kweli.
‘Mama wewe hujui tu, ..sio kwamba nimeshindwa kufanya hivyo, mbona
nafanya siku zote, ila inatokea tu,…mtoto akianza kulia, hata ufanye nini
hanyamzi, ni mpaka huyo mama afike,….’akatulia
‘Eti nini….?’ Akuliza mama mwenye nyumba kwa mshangao.
‘Yani akianza kulia, hanyamazi,…mpaka huyo mama aje…na inabidi
akifika nimpe yeye ndio anamfanya ananvyomfanya, basi ananyamaza,…’
Anamfana nini mtoto wangu, mbona unanitisha….?’ Akauliza
‘Mama mtoto akianza kulia mwenyewe utamuonea huruma,…na anayeweza
kumtuliza ni huyo mama…’akasema
‘Mbona hujaniambia …kuwa mtoto ana tatizo hilo?’ akaulizwa
‘Kulia kwa mtoto ni kawaida, na kama huyo mama kambembeleza
akanyamaza, mimi sikuona haja ya kukuambia…kwahiyo nikaona akianza kulia
namtafuta huyu mama anakuja, anampakata, na hapo ndio naweza kufanya kazi zingine vinginevyo, hata sijui ningefanyaje..’akasema
‘Mmi hata sikuelewi..kwanini hjaniambia hapo ndio naona umekosea
maana nilishakuambia kama kuna tatizo lolote, kama kuna mabdiliko yoyote kwa
mtoto uniambie….haya kaam mtoto ana tatizo, mimi ningelijuaje hayo…’akasema
‘Mama mimi sikuona kama ni tatizo, kwani kama ingelikuwa ni
attizo, angeliendeela kulia, huyo mama nahisi ana karama…anajua kwanini analia,
akimpakata anajua jinsi gani ya kumfanya, na mtoto hutulia,..ipo siku mwenyewe
utaona,..kiukweli, mama huyo hana tatizo,watu wanamuelewa vibaya bure, ukikaa
naye ndio utamgundua, anaongea vizuri tu, anapenda kuimba nyimbo za kubembeleza
watoto,….’ akasema yula mfanyakazi wa ndani.
Huyu mama kusikia hivyo akaona afanye uchunguzi mwenyewe wa kina,….siku
moja akarudi mapema, wakati huyo mfanyakazi yupo nje na mtoto, alianya hivyo
akihakikisha huyo mfanyakazi hajui kuwa yupo ndani, …akiwa ndani akijaribu
kujipumzisha kitandani, mara akisikia mtoto akianza kulia, yule mfanyakazi
akawa anambembeleza, lakini mtoto hakutulia kulia, kile kilio kikampa mashaka
mama mwenye nyumba, akataka kutoka nje aone mtoto kwanini analia.
Wakati keshajiandaa kutoka, mara akasikia sauti
‘Na-nataka mtoto wangu..’ akajua ni huyo mama wa mitaani,
akachungulia dirishani, na yule mfanyakazi kwa vile hakujua mama mwenye nyumba
yupo, akawa anaongea na huyo mama, kama vile wamezoeana,…lakini hakusikia
wanaongea nini.
Mara yule mama akamsogelea yule mfanyakazi akiwa anamchukua mtoto
kutoka kwa yule mfanyakazi…kuna hali ilitokea kama vile huyo mfanyakazi anasita
kumpa huyo mama mtoto, akawa anaangalia huku na kule, kama kuhakikisha kuwa
hakuna mtu halafu akampa yule mama wa ajabu huyo mtoto.
Yule mama wa ajabu akamshika yule mtoto akawa kama anambembeleza,
akatafuta sehemu akakaa na huyo mtoto, akaonekana akimshika kichwa huyo
mtoto,na yule mtoto akanyamaza!
Baadaye yule mfanyakazi akampa yule mama wa ajabu chupa ya maziwa,
na yule mama akaipokea, na kuanza kumnyonyesha yule mtoto, huku akionekana kama
kuimba kwa sauti ya chini, au kumbembeleza mtoto, badaye yule mama wa ajabu
akamuashiria yule manyakazi amchukue mtoto, mtoto alikuwa amelala.
Yule mfanyakazi akamchukua mtoto na kwenda kumlaza kwenye kitanda
chake cha kutembea kilichokuwepo hapo nje…ikatokea wakati huyo mfanyakazi
akataka kuingia ndani, akaonekana kuongea na yule mama…hili likampa mashaka
huyu mama mwenye nyumba, kuwa kama huyu mfanyakazi anaweza kumuachia huyu mama
mtoto ni hatari.
Huyu mfanyakazi akaingia ndani, na wakati anaingia ndani ndio huyu mfanyakazi
akagundua kuwa mama mwenye nyumba yupo, akataka kugeuka kutoka nje, kwenda
kumchukua mtoto, na huyu mama mwenye nyumba akawa kasimama pale pale dirishani akiangalia
nje, hakumumini kabisa yule mama wa mitaani, alitaka kuhakikisha huyo
mfanyakazi anatoka nje kumchukua mtoto;
‘Oh, kumbe umefika..sikukuona ukiingia ndani…’akasema huyo
mfanyakazi, baada ya kutoka nje na kumchukua mtoto na kuingia naye ndani
‘Hamna shida, huyo mama wa ajabu keshaondoka?’ akauliza huyo mama
akijaribu kuficha hasira zake, na huyo mfanyakazi akawa kama kashituka na
kusema;
‘Eeeeh, kaondoka….’akasema na huyo mama mwenye nyumba hakusema
neno kwa muda ule, ila akilini alijawa na mawimbi ya hasira akitamani amfukuze
tu huyo mfanyakazi,…, alijiuliza kwanini mfanyakazi wa ndani hatekelezi hilo,
mengine akiambiwa anatekeleza , na anajituma kweli , kila kitu anakianya vyema,
lakini hilo la mtoto na huyo mama wa mitani linakuwa gumu.
Mama huyu akataka kufanya utafiti zaidi, kabla hajachukua maamuzi
mengine au kumuambia mume wake, siku nyingine akafika tena, bila mfanyakazi
kujua, akiwa ndani akasikia mtoto akilia sana…kilia cha sasa kilikuwa kikali
kweli, kilio kama mtoto kaumwa na kitu…,
mama mwenye nyuma akakurupuka kwa haraak kutaka kutoka nje kwa haraka, ili akamchukue
mtoto, amuangalia kama kuna tatizo, kwa muda huo mfanyakazi wa ndani alikuwa
kambeba anambembeleza…..
Mama huyu alipofika mlangoni kutaka kutoka nje, huyo mama wa
mitaani akatokea, akiwa kajifunga uso wake kama kawaida, huku akiimba nyimbo
yake akiwa na watoto wachache ambao walipofika hapo kwenye aneo la hiyo nyumba,
wao wakasimama, na kuafuta sehemu ya kukaa mbali mbali kidogo na hapo,
wakimsubiria huyo mama, na huyo mama alipoona huyo mtoto analia, akamkimbilia
yule mfanyakazi na kunyosha mikono kama kutaka kumpokea huyo mtoto.
Yule mfanyakazi, akawa anaendelea kumbembeleza huyo mtoto, lakini
hatulii kulia, mwisho wake huyo mfanyakzi akageuka na kutaka kumpa huyo mama
huyo mtoto, mama mwenye nyumba , pale aliposimama akatamani amkemee yule
mfanyakazi , kuwa anafanya nini ..mbona anarudia yale…lakini mdomo ukawa mzito
kusema kitu.
Cha ajabu kabisa, yule mtoto alipokuwa mikononi mwa huyo mama,
mtoto akapunguza sauti ya kulia, ni kama vile mtoto anapojua yupo kwa mama yake
na sasa kinachofuatia ni kupewa nyono….yule mama akampkata vyema, akamweka
karibu na sehemu ya matiti, kama wafanyavyo wazazi wakitaka kutoa titi , ili
kumnyonyesha mtoto.
Akainua mkono wake na kumshikwa yule mtoto kichwani na huyu mtoto
akanyamaza ghafla, kama vile kaamiwa nyamaza, akatulia kimiya. Na yule mama wa
mitaani alimbeba kwa muda yule mtoto na yule mfanakazi alikuwa kashikilia chupa
ya maziwa, alitaka kumchukua mtotoa mnyonyeshe mwenyewe, lakini yule mama wa
mitani akaonekana kutaka kumnyonyesha yeye mwenyewe.
Yule mfanyakazi kuona vile, akaona isiwe shida, akampa ile chupa na
yeye akakaa karibu yake, akiangalia huyo mama anavyonyonyesha huyo mtoto, akawa anamnyonyesha yule mtoto, na yale maziwa
yalipoisha yule mama akamuinua ule mtoto na kumweka begani kwa muda, akawa
anamkanda kanda mtoto mgongoni, halafu akamweka kama alivyokuwa kwanza wakati
aanmnyonesha, hadi mtoto akalala.., halafu yule mama akamrudishia yule
mfanyakazi wa ndani mtoto, na akataka kuondoka.
Yule mfanyakazi wa ndani akampa yule mama kipande cha mkate, kwani
kwa muda ule alikuwa akinywa chai, yule mama akakataa na kusema yeye kashiba,
ila labda awape wale watoto aliokuja nao, akapokea kile kipande cha mkate
nakuanza kuwagawiwa wale watoto waliokuwa nao, na baadaye yule mama wa ajabu akaanza kuondoka
zake na wale watoto aliokuja nao,..lakini baada ya kuhakikisha kuwa yule mtoto
kalala!.
Baada ya yule mama wa ajabu kuondoka mama, mwenye nyumba
akajitokea pale mlangoni, akaenda pale aliposimama yule mfanyakazi wa ndani, na
yule mfanyakazi wa ndani alipomuona mama mwenye nyumba,akawa katoa macho ya uwoga,
akijua sasa kazi hana…
‘Nipe huyo mtoto…’akasema mama mwenye nyumba
‘Aalikuwa analia sana nikashindwa kuvumilia nikaona bora nimpe tu
huyo mama, kama ungeliona…ungejua kuwa kweli huyo mama sio mtu mbaya….’akasema
na mama mwenye nyumba hakusema neno.
Mama mwenye akamchukua mtoto akiwa amelala, akaingia naye ndani
akamkagua vyema kuhakikisha hakuna tatizo kwa mtoto akaona yupe salama kabisa,
akamlaza kitandani, na yeye akalala
pembeni yake, huku akiomba mungu kusije kukatokea jambo baya kwa huyo mtoto,
kwani moyoni keshampokea kama mtoto wake.
Toka pale mama wa kufikia wa huyu mtoto akawa na mawazo sana na
huyu mama wa mitaani, akajiuliza kuna nini kuhusiana na huyu mama, mbona
hafanani kabisa kuwa kachanganyikiwa ki hivyo. Na kwanini muda wote huwa kajifunika
uso wake na hataki kujifunua na huwa haachani na wimbo wake huo wa kusema
anataka mtoto wake, na mara nyingi huwa ana kundi la watoto kama walinzi wake.
‘Hili jambo lazima niongee na mume wangu, maana lolote laweza
kutokea, na isje ikatokea jambo baya nikaja kulaumiwa mimi kuwa kwanini niliona hivyo na sikusema…na pia,
lakini ngoja kwanza niongee na mume wangu..’akawa anaongea mwenyewe kimoyo moyo
Siku huyo mume wake
aliporudi, akiwa na nia ya kumuambia lakini kukatokea mambo mengine akasahau
kabisa kumuambia mume wake, na alipokumbuka ikawa ni siku ya pili yake,..akasema
nitamuoambia tu akirudi… na siku hiyo akatembelewa na mgeni, alikuwa mama mmoja
ambaye alijifungua karibuni.
‘Oh, mzazi umeamua kuja mwenyewe, umeona kimia sijaja kukupa
pongezi ya uzazi….’akasema
‘Oh, hapana jirani, …najua utafika tu,..nasikia hata wewe
ummejifungua lakaini mengi yanasemwa kuwa mimba yako ni ya ajabu hata
kujifungua ni kwa ajabu..hawakuwahi kuona mimba yako…hapa kijijinikuna
mambo….’akasema
‘Achana na hayo mambo ya hapa kijijini , kila mtu anajua maisha
yake,..nimehsjaifungua na mtoto wangu yupo salama ndilo la muhimu…..’akasema
‘Ni kweli muhimu ndio hilo, usalama …na afya, sasa mimi nimefika
kwa shida..’akasema
‘Shida gani mpendwa, mpaka unijie mimi, hebu niambie maana ni
bahati hiyo,mzazi kukutembelea na shida…haya hebu nambia una shida gani jirani
yangu..?’akasema na kuuliza.
‘Unajua nina tatizo la maziwa, matiti yangu yana vidonda,nashindwa
kabisa kumnyonyesha mtoto wangu….imekuwa ni taabu, nikaambiwa nimpe maziwa
mbadala, kwanza wengine alinishauri niwe nayakamua amziwa yangu kwenye
chupa…lakini wewe..nauma kweli kweli..
‘Basi nikaambiwa, kuna maziwa maalumu ya watoto
wachanga,..nimeyanunua, lakini matumizi yake yananipa shida, nikaulizia watu
wakaniambia kuwa wewe unamnyonyesha mtoto wako kwa maziwa kama hayo…..’akatulia
‘Ndio tunamnyonyesha mtoto wangu, kwa maziwaya kopo..unafikiri ni
kazi kubwa sana, hapana muhimu ni kuangalia vipimo, maji safi ya
uvuguvugu…basi…unakoroga..hutakiwi kuyachemsha kama haya ya maziwa ya ngombe….’akasema
na kuanza kumuelekeza.
Alipomaliza hayo maelekezo huyo mama akawa anataka kuondoka,
lakini akawa kama kakumbuka jambo, akiwa kasimama, akasema …
‘Jamani mwanangu jana hakulala,…siku nyingine inatokea hivyo,
lakini cha jana kilikuwa kilio cha aina yake…kalia karibu maasaa matatu, hadi
sauti inakauka,…kulia huko sio kwa kawaida,…. siunajua tena, maziwa yana
vidonda, siwezi kabisa kumnyonyesha, huku kwenye chuchu kunauma kweli, na mtoto
akawa anazidi kulia karibu usiku kucha
‘Tulihangaika usiku huo maana siku zote analia, tunatafuta njia
nayakamua maziwa kwenye chombo tunampa aanakunywa analala, lakini usiku huo
hakulala kilio na yeye,…mimi na mume
wangu tukaona sasa hilo ni tatizo, tutafute njia za kwenda hospitalini, sasa
usiku huo utakwenda wapi…tuhangaika huku na kule, ..nilitamani nimnyonyeshe
hivyohivyo, lakini wee…akigusa chuchu..mungu wangu….sikuweza, kwani kunakuwa
kama kidonda..hooo ..’
‘Mhh pole, sana unavyoelezea nasisimuka mwili mnzima, lakini hukuwahi
kwenda kwa dakitari, na kama mlikwenda dakitari alisemaje hakuna dawa a kutibu
hayo matatizo…?’ akaulizwa.
‘ Tulikwenda, kuna siku tulikwenda, mwanzoni tatizo lilipoanza, …Dakitari
alivyoshauri, kiusalama nimuanzishie haya maziwa.
‘Kama dakitari alisema hivyo mimi sioni ni tatiz na kulia kwa
mtoto ni kawaida, muhimu ni kuona kama hajakojoa..au tumbo limembana,
mnamlalisha tumbo chini ili hewa itoke…utumbo wake unakuwa umejaa hewa..au
umabena kma vile unamweka begani, tumbo linalia sehemu hi ya begani,..unakuwa
kama unamkandamiza kidogo mgongoni hivi….’akawa anamuonyeshea kwa vitendo…
‘asi kama sio tatizo kubwa,..atanyamaza tu….akizidi sana ujue kuna
tatizo, kesho yake mpelekeni hospitalini..’akasema
‘Ohh, tulitaka tufanye hivyo, unafikiri ilikuwa na haja
tena…’akasema
‘Kwanini..?’ akaulizwa
‘Unajua huyu mama wa mitaani, kumbe wakati analia,huyo mama
alikuwa kalala upenuni mwa nyumba huko nje, si unajua huyu mama, hana makazi
maalumu, hulala popote wanadai akilala kwako kuna baraka.
‘Mhhh..hata mimi nasikia hivyo.
‘Ndio baraka ilitushukia, maana alivyokuwa analia mtoto
ningelienda wapi, huko nyuma ya nyumba alilala huyu mama wa mitaani. Mara mtoto alipokuwa kilia, tukasikia hodi,
tukawa tunashangaa, kumbe huyo mama alikuwa kalala nyuma ya nyumba yetu, sijui
kelele za mtoto zilimkwaza,…
Akabisha hodi na kusema, `namataka mtoto wangu..’ tukashangaa,
toka lini mtoto huyu akawa wake. Tukamdharau kwasababu huu ndio wimbo wake.
Wakti huo mtoto akawa analia ile ya kutisha, na huyu mama akawa
anagonga mlango kwa nguvu, tufungue. Nilitamani nitoke nimfukuzilie mbali…maana
sisi tunahangaika angalaua mtoto alale, …sasa huyu mama anakuja na usumbufu
wake.., lakini baba watoto kwasababu ya joto akaamua kufungua mlango, atoke nje
na mtoto huenda, analia kwasababu ya joto..mimi nikamkataza, nikasema nitabakia
na mtoto ndani.
Muda huo kila mtu keshajichokea tumekata tamaa, kabisa….baba
watoto bika kujali akafungua mlango, alipoona huyo mama anaendelea kubisha hodi.
Huyo mama mlango
ulipofunguliwa tu akaingia ndani, na tukashindwa hata kumzuia, akaja moja kwa
moja pale nilipokaa na mtoto, wote tumeduwaa. Kumzuia tunashindwa, tukabakia
kimya…Akaja pale nilipokaa, akamwangalia mtoto anavyolia, akasema `mtoto wangu
nyamaza eeh..’
Akainua mkono wake, sijui alikuwa akisema maneno gani, akamshika
mtoto kichwani….mara mtoto kimya, na baada ya muda mfupi mtoto akalala. Halafu
yule mama bila kusema kitu huyo akatoka nje na kwenda kulala pale alipokuwa
kalala mwanzoni…’Akahadithia huyo mama na kuwaacha wenzake wakiwa wameduwaa, na
kabla hawajamuuliza kitu zaidi, huyo mama akaaga kuwa anamuwahi mtoto wake.
‘Mhh..sasa naanza kuhisi ..yawezekana kweli huyu mama sio mama wa
kawaida…’akasema na mfanyakazi wake akasema;
‘Mimi nimekuambia mama..huyo mama hana matatizo ni mama pekee
mwenye karama…ukikaa naye utalijua hili…’akasema
‘Mliwahi kuongea naye, akakuambia alitokea wapi, na uliwahi kuuona
uso wake anafananaje..?’ akamuuliza..
NB habari ndio hiyo, mama wa ajabu, mara mama wa mitaani, je ni mama gani huyu..yapo
maswali mengi bado anahitajia majibu, kisa kinaendelea, tuzidi kuwepo.
WAZO LA LEO: Dharau ni kiburi cha shetani..usiwe na
tabia ya kudharau wenzako, maana dharau, inamuumiza yule asiye nacho
kisaikolojia, kama una uwezo wako, una utajiri wao, cheo chako, ni majaliwa
yako,…kwanini umdharau yule ambaye hakujaliwa,..
Jiulize, wangapi wangapi walikuwa navyo, cheo, mali…nk, …na
wengine wakafikia sehmu wakawa hawana navyo tena, ama kwa kuharibikiwa,
kupoteza kazi, kufirisiki,a au kufa, hawapo tena duniani, yote hayo yachukulie
kama majaliwa ya mungu kuna kupata na kukosa, yule yule aliyemfanya huyo
unayemdharau asiwe nvyo ndio huyo huyo aliyekupa wewe na anaweza kufanya
vinginevyo. Wewe unachotakiwa kufanya ni kumshukuru mungu kama umejaliwa kupata,
….na usione soo kumsaidia yule ambaye hajajaliwa, huo ndio ubinadamu , na huo
ndio utu mwema.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment