Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, February 10, 2015

NANI KAMA MAMA-30


‘Ilikuwa ndoto ya ajabu kweli…’akamalizia kuongea dada mtu  na mdogo mtu akasema;

‘Hayo ni Mawazo dada, hayo ni mawazo yako kuhusu mtoto, inabidi dada sasa uyapunguze na ikibid uyaondoe kabisa, kwasababu sasa mna mtoto, japokuwa hamkumzaa nyie, lakini kuanzia sasa ni mtoto wenu kisheria….’akasema.

‘Ni kweli kisheria inawezekana akawa ni mtoto wetu, lakini je mwenyewe akiwa mkubwa, akijua kuwa sisi sio wazazi wake wa kumzaa, unafikiri mapenzi yatakuwa ni yale yale….’akasema dada mtu.

‘Hivi ni waulize, ni nani mwenye thamani, mzazi wa kukuzaa, ambaye hakukulea, kwasabbu hizi na zile, au mzazi wa kukulea, ambaye alijitolea kwa nguvu zake zote kukulea, hadi kufanikiwa katika maisha yako..?’ akauliza.

‘Mhhh, inategemea, …ukumbuke kuna hatari za mimba, hujui huyo aliyekuzaa kateseka vipi, ..lakini yote ni sawa tu, inategemea mtizamo wa mtoto mwenyewe , cha muimu ni kutimiza wajibu wako, maana unaweza ukamzaa, ukamlea vyema, nab ado asikuthamini..’akasema dada mtu.

‘Umeliona hilo, eeh, sasa dada usiwaze sana, kumbe yote yawezekana unaweza ukazaa, ulea ukatimiza wajibu wako, nab ado usithaminiwe, na unaweza ukalea, ukahangaika weee, mtoto akakutahamini zaiei ya yule aliyemzaa,..muhimuu ni kutimiza wajibu wako, sasa sisi tutimize wajibu wetu…’akasema mdogo mtu.

‘Kwahilo usiwe na shaka nalo, hata kama kuna sintofahamu ya huyu mtoto, maana mpaka sasa hujatuelezea ukweli wake,..kama wazazi wake walikuwaje, ..sisi tutamlea sawa na mtoto tuliyemzaa wenyewe, ..nakuahidi hilo mdogo wangu, na hata ukifika huko kazini kwako ujue kuwa mtoto kafika sehemu sahihi….’akasema dada mtu.

‘Ndio maana nilipokabidhiwa hilo jukumu, mungu akanilekeza kwenu…muhimu sasa dada usiwe na mawazo ya mtoto tena,, mtoto huyo unaye huyo ni mtoto wanu, au sio shemeji…?’’akasema mdogo mtu,  akimchukua mtoto kuondoka naye kuelekea chumbani

Shamji mtu hakujibu kitu alitikisa kichwa tu, akilini hakuwepo hapo kabisa, akili likuwa imekwenda mbali, na hata shemji yako alipondoka na kubakia yeye na mkewe, bado alikuwa akiwaza yake.

Sasa wakabaki mke na mume,…, kimiya kikatanda, kila mmoja akiwa na mawazo yake kichwani, mume akiwa anawaza tukio zima na historia ya maisha yake ya nyuma, ambayo hakutaka mtu aijue,  na mkewe akawa kila mara anamtupia jicho mumewe kwa jicho la kujiiba. Mke alikuwa na yake kichwani, alikuwa na maswali mengi ya kumuulizz mumewe, yaliyohitaji majibu, alitaka kujua ukweli…lakini hakuweza kutamka neno, akawa kimiya, huku akiendelea kumtupia mumewe jicho la kujiiba, kimia kikatanda, utafikiri hawajuani.

Mara mume akawa ni kwanza kufungua mdomo, na kuanza kuongea…

Tuendelee na kisa chetu.

******
Baada ya ukimia wa muda, mume ndiye akawa wa kwanza kufungua mdomo, akasema;

‘Mke wangu …’akaita huku akitabasamu, mke wake akainua uso na kumuangalia, yeye hakustabasamu, kinyume na kawaida yake.

‘Mke wangu, unajua nimeliwaza sana hili tukio, ni moja ya tukio kubwa katika historia ya ndoa yetu..’akasema na kutulia akitafuta maneno mazuri ya kumfanya mkewe angalau atabasamu.

‘Unajua mke wangu, mimi nakupenda sana…sijui nikuambieje..kila mara namshukuru sana mungu kwa hilo kwa kunipataia mke mwema…’akamtupia mkewe jicho kuona kama kuna mabadiliko, lakini hali ilikuwa ile ile.

‘Kwa hili tukio nimejifunza mengi,..kuwa nafsi ya mwanadamu inaweza kubadilika kwa kitu kidogo tu..kitu kidogo kinaweza kumfana mtu akabadilika, na akawa hana amani tena, kumbe..wakai mwingine ni shetani tu…’sasa hakujali kama mke wake atatabasamu au la,..akaendelea kuongea.

‘Mimi kiukweli,  sikutarajia kuwa itafikia muda mimi na wewe tusiaminiane tena….nimeogopa sana ..namshukuru mungu kaliona hilo na kutusaidia,…hivi kweli ningeuweka wapi uso wangu, kama ..mtu angesikia hizi shutuma…mke wangu, nakuomba uniamini, mimi nakupenda na siwezi kukufania hayo unayohisi wewe….’akamuangalia mke wake, ambaye alikuwa kakaa kimia tu.

‘Lakini sawa, kwa yoyote angelizania hivyo, siwezi kukulaumu,  mimi namshukuru mungu,  kuwa mambo yameenda salama ukweli umejiweka wazi wenyewe.…..’akasema mume mtu na mke akawa kimia hakujibu kitu kwanza.

‘Mke wangu,…’akaita na kumuangalai mke wake ambae aliinua uso na kumuangalia, alihisi kama mke wake anataka kulia, akaona abadili muelekeo akaona leo sio siku ya kuongea hilo alilolitaka kuliongea, akasema;

‘Ni kweli kwa muda mrefu tumekuwa tukitamani kuwa na mtoto, ..tulifikia hatua ya kutaka hata mtoto wa kulea…’akasimama alitamani aende pale alipokaa mke wake, lakini akaona sio wakati muafaka akawa kasimama vile vile akaendelea kuongea.

‘Mimi nakumbuka kuna siku ulilitamka hilo wewe mwenyewe, …kuna unahitaji hata mtoto wa kurithi, kama wanavyofanya wazungu….nikakuambia nani kakuambia hutozaa…unakumbuka hilo…’akamuangalia mke wake, mke wake akatikisa kichwa kukubali, akaona eehee, anaanza kuelekea.

‘Tena ulitamka hilo mbele ya mdogo wako, mimi nikakuambia, tuvute subira maana hujui mungu kapanga nini, kila jambo huja kwa wakati wake,…nielewe hapo, kila jambo hufanya nini…huja kwa mapenzi ya mungu… hatutakiwi kulazimisha…unakumbuka siku ile?’akasema na akawa kama anauliza, mkewe bado akawa kimiya alikuwa kinama chini.

Mke wake alikuwa akiwaza yake, alikuwa akiomba mumewe afunguke, azungumze ukweli wote, alihisi bado kuna ukweli umefichwa…lakini aliogopa kusema hisia zake isje ikawa kama alivyomuhisi mdogo wake vibaya, japokuw akiundani, aliona kuna jambo, haiwezekani mtoto afanane na mume wake…labda…na sijui iwe vipi, maana ndugu za mume wake anawafahamu, hawafanani kabisa na mume wake..iweje hii..au kuna ndugu mwingine hamfahamu..hapana kuna jambo hapa.

 Akili ya mkewe ilikuwa na shauku kuwa mtoto huyo anaweza akawa ni damu ya mumewe, huenda mungu kamleta hapo ili kujua ukweli, kuwa mume wake yupoje, …lakini huo ukweli hautakuwa na maana kama mume wake hakukiri,..na kwanini hakuwahi kumuambia hilo, … kama ataendelea kukaa kimia hivyo itamtesa sana moyo wake.

‘Moyo wangu unataka ukweli….aniambie tu…’akawa anaongea kimoyo moyo

‘Kwanza nisikie ukweli wote, kuwa  kweli mume wangu alifanya hilo akakiuka miiko ya ndoa katika kutafuta mtoto, ..halafu ndio atajua la kufanya…lakini  baada ya kuusikia huo ukweli…sijui kama  anaweza kumsamehe,..sijui, lakini kwanza asikie huo ukweli.

‘Kwani nitakosa nini nikichukua maamuzi magumu,..kwanza hatuna familia, sina mtoto wa kuniumiza kichwa kama nitaamua kuondoka, sina cha kupoteza hapa…angeniambia ukweli tu, ili nisiendelee kuumia, nai kama ataendelea kuni ficha hivi nikaja kugundua mwenywe, sijui kama nitaweza kumsamehe tena… siku akigundua tu  itakuwa siku ya kuagana mimi nay eye..lakini mmh, mume wangu nampenda sana, kwanini haya yatokee, ooh, mungu wa ngu nisaidia, …..’akainua kichwa kumuangalia mume wake ambaye alikuwa bado anaongea.

‘Unajua mke wangu kila nikiliwaza hili nahisi kweli, kuwa mungu kasikia kilio chetu na sasa katupatia mtoto..bila hata kuhangaika, na ilivyo na bahati mtoto anafanana na sisi kabisa, unajua kufanana, hii ni miujiza kweli…’akawa kama kamshika mtoto akimuangalai usoni.

‘Yaani, …sura utafikiri…..ooh,  mtu hawezi kuuliza. Hivi mke wangu umemchunguza vyema huyo mtoto, sio tu anafanana  na mimi, lakini pia anafanana na wewe..’akasema na mkewe akacheka, na kicheko kile kilimfanya mume mtu akatize kuongea na kumuangalia mke wake, alitaka iwe hivo, mke wake acheke….lakini kicheko kile ni kma sio chake, sio kicheko halisia.

‘Sasa mke wangu tujipange jinsi ya kumlea huyu mtoto,…mtoto wetu,  maana hili ni kama limetushitukizia, japokuwa tulikuwa tunaliombea litokee hivyo,  lakini kihali a maisha yetu, a kuganga njaa…hili limekuja hatujajipanga.

‘Mimi hapa naona jambo muhimu ni kujua jinsi gani ya kumlea kwanza….unaona hapo, ulezi,..najua wewe upo utamlea,..lakini..mmmh, hapana hapa ni lazima tutafute mfanyakazi,, tunahitaji mfanyakazi wa kutusaidia, …’akasema na kugeuka kumuangalia mke wangu, na mkewe akawa bado yupo kimia, kajiinamia vile vile.

‘Nasema hivi kwasababu, kuna hizo shughuli zako ambazo zinatusaidia hapa na pale, siwezi kusema uziache, uje ukae hapa nyumbani tutegemee hicho kipato kidogo ninachopata, cha mkono twende mdomoni..hapana hilo halitakuwa jambo la busara…’akamuangalia mkewe akitaraji maelezo au kauli kutoka kwa mke wake, lakini mke wake alikuwa vile vile.

‘Nimekuwa nikiwazia hilo kwa muda huu mfupi,…mimi naona tutafute mfanyakazi, haraka iwezekanavyo,..maana ukikaa nyumbani, shughuli zako za vibiashara vyako zitasimama…si unaliona hilo mke wangu…sasa hapo tufanyeje, …,’akamuangalia mke wake akisubiri mchango kutoka kwa mke wake, alipoona kimia akasema.

‘Vinginevyooooh, oh, labda utafute mtu wa kutufanyia hizo biashara, awe anakuuzia biashara zako, lakini mmmmh,… hapo ina maana kumlipa huyo mtu, ni yale yale sawa na kutafuta mfanyakazi wa ndani …unasemaje mke wangu…hebu changia kidogo mke wangu…acha mawazo mengine hili ni muhimu sana, unasemaje kwa hilo?’ akauliza mume mtu na mke akaendelea kuwa kimia.

‘Mke wangu naongea na wewe…’akasema na mke akakumbuka ile kauili ya nyuma ambayo kwa mara ya kwanza mume wake alimuita `wewe mwanamke..’hasira za ndani kwa ndani zikawa zinajisokota tena, akatamani akae kimia au…... Kauli hiyo ilimuuma sana, sijui ataisahau vipi, yeye kwake ilikuwa kama zarau. Mke alipoona mume wake katulia anamkodolea jicho yeye, akasema;

‘Yote sawa…ilimradi tumeafikiana kumchukua huyo mtoto,..vyovyote itakavyokuwa ni sawa tu…kwani hata mtoto kupatikana kwake, yalikuwa maamuzi yako asu sio…sasa mimi niseme nini …’akasema.

‘Maamuzi yangu….hapana, …ni maamuzi ya mdogo wako, kaona sisi tunahitaji mtoto, ndio akamleta hapa….au  ulikuwa una maana gani?’ akauliza

‘Mhh,…kwahiyo vyovyote iwavyo kwangu sawa tu, … ‘akasema na moyoni akawa anasema  ngoja nisubiri ipo mume wake atamuambia ukweli, muhimu kwa sasani zubira japokuwa inauma sana..ila akichelewa kumuambia akaja kugundua mwenyewe, sijui kama kutaeleweka.

‘Mawazo yako ni sawa…tupo pamoja..’akasema akinyosha, hakuona sababu ya kukaa kimia akiumia moyo wake, akaamua kuliacha hilo kwa muda, na mumewe akasema:

‘Kama ni hivyo basi, tutafute mfanyakazi wa ndani…hilo la kumtafuta najua utalifanyia kazi wewe mwenyewe, mimi nijipange jinsi gani ya kuongeza kipato ili kupatikane cha kumlipa huyo mfanyakazi, je unaweza kumpata lini huyo mfanyakazi wa ndani?’ akauliza

‘Hata leo anaweza kupatikana..’akasema mkewe kwa lugha ya mkato, akijaribu kundoa mawingu yaliyokuwa yametanda kichwani.

‘Kweli mke wangu! Ina maana kumbe ulishajipanga kwa hili…mmmh mke wangu…nashukuru sana!’akasema mumewe kwa kuonyesha mshangao.

‘Mhh! …ni kweli, nilishajipanga…sisi wanawake unafikiri tuna shida,..tunawasikiliza nyie waume wa nyumba, nyini ndio waamuzi, …sisi tumeolewa tu…’akasema mkewe kwa sauti ya unyonge. Na kauli hii ilimfanya mume wake aone kuwa mke wake bado ana dukuduku linalohitajika kusawizishwa, lakini kwake yeye aliona muda utakuja kulisawazisha, hana haja ya kuhangaika nalo kwa sasa.

‘Sasa mke wangu  tufanyeje,..mimi naona wewe uwasiliane na huyo mtu, maana unaweza kusema yupo kumbe keshapata sehemu nyingine, mpigie simu…au…. au utakwenda kwao, kwani ni mbali sana,…maana nionavyo mimi muda ni huu huu, ili mdogo wako akiamuka tu tunamfahamisha, ili aondoke akijua hilo, au sio mke wangu..?’ akauliza.

‘Mhh, ni sawa, hata mimi naona iwe hivyo, ….mfanyakazi wa kutusaidia nimuhimu sana,sitaweza kuiacha ile biashara ya sokoni maana nimeshaijengea jina na inasaidia sana hapa nyumbani…mimi nilionelea kama tungelipata mfanyakazi wa muda tu ingelifaa zaidi, akinishikia kwa muda, lakini kuna mfanyakazi ninayemfahamu mimi anahitajia kazi,…yeye anataka sehemu ya kukaa wakati wote, sijui kama tutaweza kumlipa…’akasema sasa akiwa katuliza kichwa.

‘Mambo si hayo mke wangu…mimi naona hilo limekuja na heri zake, ….mimi naona tutaweza tu, tutahangaika tutapata mshahara wake, mimi sioni ubaya wake….’akawa anatafakari jambo mke akainua kichwa kumuangalia mume wake, na mume waka akasema;

‘Sawa tu…unafikiri kutakuwa na tofauti ya malipo,….yaani wa muda na wa kukaa muda wote….,  sizani kama itakuwa kubwa saana tutaoana huko mbele, …mimi naona kama yupo ufanye mpango wa kuongea naye,  maana huyo wa wakati wote hutakuwa na wasiwasi ukiwa kwenye biashara zako. Unaweza ukawa kwenye biashara zako ukatingwa, lakini unajua kuna mtu nyumbani. Sasa muhimu tu ajue jinsi gani ya kulea mtoto kama huyu- mtoto mchanga, je unaweza kuwasiliana naye sasa hivi….?’ Akauliza mume mtu.

‘Usijali hiyo ni kazi ndogo sana kwangu, kuna binti mmoja alikuwa anatafuta hiyo kazi, aliwahi kufika hapa mara mbili, alikuwa akitafuta kazi za nyumbani kama hizi, na niliwahi kumhoji kuwa anataka kazi za namna gani akasema kazi zozote za ndani..’akatulia kidogo.

‘Sawa kabisa anafaa…ukimuona anweza kulea mtoo mchanga maana hapo tuwe makini.’akasema mume mtu.

‘Nilimuuliza hilo, aah,, … akasema kuwa anaweza kulea mtoto hata kama ni mtoto mchanga kwani yeye ana upendo sana na watoto…., nikamwambia kama nitasikia sehemu wanahitaji mfanyakazi wa ndani nitamfahamisha, ….jana alikuja tena kuulizia ..’akasema.

‘Alikuja tena..ooh, hiyo ni bahati, ni mungu alipanga iwe hivyo, unaona mke wangu…mungu ana njia zake zakuelekeza…sasa…’akataka kuongea zaidi na mkewe akamkatiza na kusema;

‘Ni mara kwa mara anakuja kuulizia, maana nilimuahidi kuwa nitamsaidia kutafuta mtu anayetafuta wafanyakazi wa ndani…’akasema.

‘Unaona mke wangu jinsi ilivyo…, kila kitu huja na bahati yake, haya yote kayapanga mungu…ni muhimu tumshukuru mungu na tusiwe na kinyongo chochote, kila jambo litakuja kujieleza lenyewe,…nakuhakikishia hilo mke wangu…hutaumia moyo wako….’akasema na mke akamtupia jicho mumewe, na mumewe akakwepa hakutaka waangaliane moja kwa moja usoni, mkewe akasema.

‘Hamna shida, ….ni kweli kila alipangalo mungu huwezi kuliepuka, na yeye anafahamu ya siri na dhahiri,…na sisi kama wanadamu subira ni muhimu sana, mimi kama mke wako, nitasubiri tu….mume wangu….’akasema mkewe akawa anasimama na mumewe akasema;

‘Nimefurahi kusikia hivyo mke wangu,…. sasa ndio unataka kwenda huko kwanini usimpigie simu kwanza, kuhakikisha kuwa yupo, maana naona tusipoteze muda..’akasema mume we akiwa kashika simu mkononi.

‘Hilo siumesema unaniachia mimi…, ni jukumu langu hilo, wewe tulia tu, kila kitu kitapatikana kwa wakati wake..mtoto kapatikana kwa wakati wake, na hata mfanyakazi atapatikana tu, kwa wakati wake, au sio…’akasema mke wake na mume akasema;

‘Haya nenda kamuambie aje aanze kazi mara moja,…maana ni kweli akija akamkuta na mdogo wako yupo…aah, kila kitu kitakuwa shwari….maana mdogo wako ataweza kumuelekeza yeye mwenyewe kila kitu ambacho ni muhimu kwa mtoto huyo, wewe utakuwa msimaizi tu…sasa itabakia kujua kiasi gani cha mashahara wake…’akasema mume wake.

‘Swala la malipo yake,..tutaona huko mbele….mara nyingi wafanyakzi hawa wa ndani hawahitaji malipo makubwa, maana anaishi kama mwanafamilia, kula kulala na huduma za kawaida ni hapa hapa na atapata bure, muhimu ni posho yake, maana kaja kwa kazi, sio kama mwanafamilia,inabidi alipwe, kwa makubaliano, tusimsononeshe,…

‘Na nijuavyo mimi, wafanyakazi hawa wa ndani, wengi wanalipwa kutegemeana na hali zetu, kama kipato ni kikubwa ni wajibu alipwe vizuri, kama ni kidogo, basi atalipwa hivyo hivo, na kwa vile mwenyewe hali anaiona atarizika tu, ila tusimuonee, akaona kama yupo utumwani…kazi nyingi nitazifanya mimi mwenyewe…’akasema mke mtu, huku akianza kuondoka.

‘Haya kila la heri nataraji utamkuta hajaondoka, ukimkosa inabidi kuulizia sehemu nyingine…’ akasema mume mtu.

‘Siwezi kumkosa, yupo ananisubiria..hilo nina uhakika nalo, ….muhimu ….’akasimama kwanza.

‘Mimi kichwa hapa kinaniuma…nawaza sana,….’akasema

‘Kuhusu nini tena mke wangu….?’ Akauliza

‘Sawa…nitasubiri tu…ila sitaweza kusubiri sana,…nataka nikirudi tuongee hili kwa mapana…au tusubiri mdogo wangu aondoke tukiwa na nafasi naomba hili tuliongee kwa uawazi, mimi ninachohitajia ni ukweli tu….’akasema

‘Mke wangu hebu tuachane na hizo hisia zako kwanza, hili lina umhimu kuliko hizo hisia zako…’akasema mume wake.

‘Lina uhumhimu, ina maana hujali hisia zangu..?’ akauliza mke wake.

‘Sio hivyo mke wangu,..mimi nimeshakuambia ukweli utakuja kujielezea wenyewe, si umeona mwenyewe, ooh, mdogo wangu una mtoto, ooh, mdogo wangu umenisaliti..ooh  wapi…si umeona mwenyewe, na hilo litakuja kujionyesha lenyewe, usiwe na shaka kabisa, utakuja kufurahi , hakuna ubaya wowote kama unavyofikiria wewe…’akasema mume mtu, mke mtu hakusema neno hapo.

‘Unajua mke wangu…usipende kutunga hadithi…….utaumiz akichwa chako bure, mwishowe utakufa kwa kihoro uniache nikiteseka kukuwaza, na mimi sipenzi uniache mke wangu ni heri nife mimi kabla yako….unasikia mke wangu mimi….sipendi wewe…..’akawa anaongea akijua mke wake bado yup ndani.

Mke mtu alikuwa keshaondoka akimuacha mumewe akiendelea kuongea, hakutaka kumsikiliza zaidi, na mume ambaye kwa muda huo alikuwa anaongea akiwa kageukia upande mwingine hakujua kuwa mkewe ameshaondoka.

Mke mtu akiwa na mawazo akawa anatembea kuelekea kwenye hiyo nyumba ambapo huyo msichana anaishi kwa muda, … lakini mawazo yake yakakatishwa na kundi la watoto, na yule, mama, safari hii akaonana na huyo mama ana kwa ana, japokuwa yule mama alikuwa kajifunika usoni kama kawaida yake. Yule mama alipomuona huyu mke mtu yeye mwenyewe akamsogelea na kuanza kusema;

‘Na-na-nataka mtoto wangu….’akasema kwa sauti ya  kukasirika, na huyu mke mtu akatulia na sijui ni kitu gani alijikuta na yeye akisema;

‘Nataka mtoto wangu….’akasema na watoto nao kwa wakati huo wakawa wameitikia hivyo hivyo, huyu mama akarudi nyuma hatua moja, kama vile anaogopa, alirudi  kinyume nyume,…na kumfanya mke mtu kubakia na mshangao, ni kama vile hiyo sauti ilimshitua ule mama, lakini baadaye yule mama akasimama akamsogelea tena huyo mke mtu,na kusimama karibu naye.

‘Nimekuambia…nataka mtoto wangu…’akasema na safari hii mke mtu akajua huyu mama anaongea kionyesha dhamira hana utani, ndipo akamjibu;

‘Kwani mimi nina mtoto wako?’ akamuuliza

‘Ndio una mtoto wangu, wewe huoni,….mimi namtaka mtoto wangu….nitakuja kumchukua mtoto wangu….’akasema

‘Mimi sina mtoto wako, ulinipa lini mtoto wako…, kwanza wewe ni nani mbona unajifunika, kwanini hutoi hiyo nguo usoni tukuone ulivyo….?’
‘Unataka kuiniona eeh..hahaha…’akacheka halafu akasema;

‘Nataka mtoto wangu, wewe unaye mtoto wako, na mimi nataka mtoto wangu…’akasema

‘Ninaye mtoto yupi…?’ akauliza

‘Mtota wako unye tumboni kwako,..huyo uliyemchukua ni mtoto wangu….nitakuja kumchukua mtoto wangu…’akasema na kugeuka kuondoka, akamuacha mke mtu akiwa kaduwaa..

‘Mhh, ….mimi nina mtoto wangu tumboni,…! ‘akainama kujiangalia huku akiwazia ile ndoto.

‘Mhh mbona hii kauli yake inafanana na ile ya kwenye ndoto…’akasema akiwa anaangalia huko mama huyo anapokwenda lakini hakumuona tena, keshatoweka.

‘Mhh,..mbona makubwa…’akasema kwa sauti, akawa sasa anaanza kuingiwa na mawazo kuwa huenda kweli huyo mama ni mama kutoka mbinguni, anafahamu siri za watu, na jinsi alivyotoweka haiwezekani akageuka huku na kule kumtafuta lakini hakuwepo kwenye upeo wake wa macho…akawa kasimama pale akiwaza, hakujua kasimama pale kwa muda gani, lakini baadaye akakumbuka kuwa alikuwa na kazi ya kufanya, akaanza kutembea kuelekea huko alipokuwa akienda.

 Alipofika nyumba ya jirani, akamkuta huyo binti yupo,akiwa anafua nguo…na huyo binti alipomuona huyo mke wa mtu, akaonyesha uso wa furaha na swali likawa;

‘Je umesikia kuna mtu anatafuta mfanyakazi wa ndani, maana mimi najiandaa kuondoka, kesho naondoka zangu, narudi huko kwetu kijijini, nitakuja tena siku nyingine..’akasema

‘Usiwe na shaka, kazi imeshapatikana..’akambiwa na kumfanya yule binti kuacha akzi aliyokuwa akiifanya na kumsogelea huyo mama

‘Wapi huko…ooh, ndio maana jana niliota nafanyakazi nalea mtoto mchanga…nikajua huenda kweli nitapata kazi, napenda sana watoto wachanga, siku nikipata wangu, sijui itakuwaje…umesema kazi imepatikana wapi, kwa nani?’ akauliza

‘Nyumbani kwangu….’akasema na huyo binti akawa kama kakata tamaa, akasema

‘Lakini uliniambia kuwa wewe huhitaji mfanyakazi, na huna mtoto mchanga na pia ulisema kutokana na shughuli zako hutaweza kunilipa..’akasema

‘Usijali, nitakulipa tu….kama upo tayari twende…’akasema na huyo binti akasema

‘Mimi kwasasa nipo tayari kwa kazi oyote maana nilishakaa na kukata tamaa..hapa nilikuwa najiandaa kesho kuondoka, mwenyeji wangu nilishamuaga maana nikaa tu sema katoka kidogo..oh, bahati …., yule pale unamuona ..anarudi, ngoja nijiandae tuondoke, …’akasema.

‘Sawa wewe chukua kila kitu hutarudi tena hapa…’akaambiwa na mwenyeji wa huyo msichana akafika akaelezewa , yeye akawa hana kipingamizi, akatoa baraka zake.

Basi wakaondoka na huyo binti hadi nyumbani kwake alipofika, mdogo mtu alishaamuka, na mdogo mtu aliposikia kuwa huyo ni mfanyakazi wa mtoto kwanza alisita lakini baadaye akakubaliana na hilo, ikawa ni kazi ya kuelekezwa jinsi gani ya kumlea huyo mtu, kumtengenezea maziwa.

‘Hii kazi ya mtoto, utaifanya tu pale nikiwa sipo, na nitajitahidi sana kabla ya kuondoka kila kitu kipo tayari, usiwe na wasiwasi tutasadiana na kama sipo ukiona kuna jambo hulielewi au mtoto analia sana, nipie taarifa haraka, tafadhali….’akasema dada mtu akimuelezea huyo mfanyakazi na mdogo wake akawa anatikisa kichwa kukubaliana na hilo.

Dada mtu akamwambia mdogo wake asiwe na wasiwasi na hilo, imebidi kumtafuta huyo mfayakazi kwa vile ana biashara zake na wakati mwingi huwa anakuwa hayupo hapo nyumbani…lakini kwa sababu ya huyo mtoto atajipanga jinsi gani ya kufanya.

Pamoja na sintofahamu uliyojitokeza, lakini tukio hili likaoneka kuwa litaleta faraja ndani ya familia, na ilikuwa kama vile, dada mtu kajifungua mtoto, japokuwa bado kulikuwa na kitu nafsini mwa mke mtu kwa mumewe…lakini kila hatua hali hiyo ilikuwa ikipungua.

Kesho yake mdogo mtu akarudi kazini kwake, na wakati anaondoka akakutana na umati wa watoto, wakimfuatilia yule mwanamama, akaona ajaribu kumwangalia huyo mama ni nani. Akawa anamuendea pale aliposimama na watoto, na yule mama alipoona mtu anamjia, akageuka kuondoka…akatembea hatua kama tatu halafu  akasimama, akasubiri…

Mdogo mtu, alipoona huyo mama kasimama,…akatembea kumsoegelea…alipomkaribia akasita, lakini alishafika karibu yake, sasa akawa anafikiria amuambieje huyo mama, yule mama akaanza kutembea kuelekea sehemu nyingine alipoona aliyekuwa akimfuata hasemi neno, huyo mdogo mtu akasema;

‘Samani mpendwa, nataka kuongea na wewe…’akasema huyo mdogo mtu.

‘Na-na-nataka mtoto wangu…’akasema huyo mama na watoto wakaitikia

‘Unataka mtoto wako,…yupo wapi huyo mtoto wako?’ akauliza

‘Wewe unafahamu wapi alipo, tena ndio wewe, unayeiba watoto wa watu …nataka mtoto wangu,…mimi nitakwenda kumchukua mtoto wangu….’akasema.

‘Utamchukua wapi huyo mtoto wako, kwani mimi nilikuwa na mtoto wako, umeniona wapi nikiiba watoto?’ akauliza huyo mdogo mtu.

‘Nimesema nataka mtoto wangu….nitamchukua mwenyewe mtoto wangu….nitamchukua mtoto wangu, nataka mtoto wangu, unanisikia…’akasema

‘Mhh…wewe mama una maana gani kusema hivyo, ..utafungwa, isije ikawa ndio nyie mnaoiba watoto, huyo mtoto wako ulimpa nani, au ulimpatia wapi..?’akasema.

‘Wewe ndiye umeiba mtoto wangu nataka mtoto wangu, nipe mtoto wangu…nimesema nataka mtoto wangu, …nipe mtoto wangu haraka…’akasema akitaka kumvamia huyu mdada, na huyo mdada akawa anarudi nyuma kumkwepa huyo mama,

Na alipoona hali sio shwari akageuka kutaka kumkimbia huyo mama, na huyo mama akawa keshamshika sehemu ya nguo yake wakawa wanavutana…mdogo mtu huyo kuona vile akawa anarudi kwa nyuma huku akijaribu kuvuta nguo yake, isije ikachanika…. na watoto waliokuwepo hapo wakawa wanashangilia kama mchezo vile.

‘Ntaka mtoto wangu, nipe mtoto wangu, umeniibia mtoto wangu….’yule mama akawa anasima 

Mdogo mtu kuona hivyo, akatahayari maana sasa anakuwa kama anasutwa,…kuwa yeye kamchukua mtoto wa huyo mama, japokuwa alishasikia kuwa huyo mama anamfanyia hivyo kila mtu,  akaona hapo hapakaliki akaita bajaji na mwenye bajaji alipofika akamsaidia kumuachanisha na huyo mama, na hapo akapata upenyo, akaingia kwenye hiyo bajaji, wakaondoka kwa haraka.

Alipofika njia akachukua simu na kumpigia dada yake……

NB: Je huyu mama kwanini anadai kuwa anataka mtoto wake…je huko kazini kwa huyu mdogo mtu kuna nini kinachoendelea, tuwepo sehemu ijayo.


WAZO LA LEO: Kuna vitu ambavyo kama vingelikuwa ndani a nafsi ya kila mtu, utu na ubinadamu ungelikuwepo , na dunia hii ingekuwa ni kisiwa cha amani, lakini vitu hivyo ni nadra sana kuwepo ndani ya nafsi ya mtu, kwani kila mtu amejawa na ubinfasi, vitu hivyo adimu  ni upendo na huruma. Ikimuuliza mtu anaweza kujinadi kuwa anvyo vitu hivyo, lakini je ni kweli, Mtu kujipima kuwa kweli ana upendo na huruma , ajaribu kujiona jinsi gani anavyoweza kutoa kile alicho nacho kusaidia wenzake bila kinyongo.
Ni mimi: emu-three

No comments :