Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, January 22, 2015

NANI KAMA MAMA-22


‘Huyo mama ni nani…?’ wakauliza

‘Huyo ni mtu katumwa kutoka mbinguni, kuwakomboa akina mama wasio na watoto, ndio maana anaimba hivyo, kuwa mwenye kutaka mtoto naye aimbe, ‘nataka mtoto wangu..’akasema huyo mwanaume.

‘Nani kakuambia anhitaji mtoto, tulio nao wanatushinda, fujo kelele, gharama za kuwasomesha, …wewe unataka watoto tena…’akasema mama mwingine,

‘Wewe hutaki watoto, lakini ukumbuke kuwa kuna wanaowataka, angalau hata mmoja lakini hawajajaliwa kupata….’akasema mama mwingine.

‘Sasa ndio hao wameletewa huyo mjumbe, akisema `nataka mtoto wangu…’ na wewe unayetaka mtoto, unatakiwa uutikie, uombe, shida zako, ndio maana watu wanamfuatilia huyo mama wakimuigizia…’akasema huyo mwanaume.

Umbea ukaanzia hapo…

Je ni kweli, mama huyo ni mjumbe kutoka mbinguni…

Tuendelee na kisa chetu

********
‘Ngoja nitoke mara moja, nikaitikea mara mbili mbili tatu, huenda nikaipata hiyo Baraka,…’akasema mama huyu, na kutoka kulifuatilia hilo kundi, na yeye akawa miongoni mwa wanaoitikia,

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu’

 Mama yule akawa aanalifuatilia hilo kundi, halikuwa mbali sana, lakini kwa vile lilikuwa likitembea, na watoto wamejaa, ikawa ni kazi kufika karibu sana, hasa pale alipokuwa huyo mama.

Na mama huyu akawa na hamasa, ya kumuona huyo mama muimbishaji, ili apate cha kuongea, kama akiulizwa, sasa akawa anamkaribia huyo mama anayekuwa kama anaimbisha, lakini kila akimkaribia , huyo mama anakuwa kama kahisi kuna mtu nyuma anamfuatilia, akawa anaongeza mwendo, au anapinda kushoto au kulia kumkwepa, na watoto wanamzonga kiasi kwamba anashindwa kumfikia.

Alijaribu tena na tena lakini baadaye akakumbuka kuwa anahitajika nyumbani, mume wake anaweza akawa karudi,…kwahiyo akakata tamaa kumfuatlia huyo mama, na kugeuka kurudi huku akisema;

‘Mbona huyo mama anaonekana kama sio wa kawaida,  na kwa jinsi anavyoonekana mimi nahisi ana walakini….’akasema kimoo moyo huku akigongana na watoto wanaomkimbilia huyo mama.

‘Mhh, na kwanini haonyeshi uso wake,….ningemuona angalau sura yake, nikajua yupoje, na kwanini watu wanasema ni mama kutoka mbinguni…kwa kigezo gani, au ni tetesi za uvumi, maana watu hawaachi kuvumisha uwongo….mmmh mimi, sijui lakini, nitasikia ukweli baadaye….’akatulia kwanza alipoona watoto wanazidisha ghasia na yeye hawezi kushindana nao.

 Mama yetu huyu aliyeota ndoto, akawa anarudi kwake, huku bado akiendelea kuusikia huo wimbo ukiimbwa, maana umeshakuwa wimbo tena, ‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’na watoto nao huitikia hivyo hivyo …..’ ‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’ hata mama huyu naye akawa anaitikia hivyo hivyo akipiga piga miguu yake chini kufuatilia jinsi wanavyoimba, haraka haraka kurudi nyumbani.

 Mama alipofika nyumbani kwake, alikuta mlango upo wazi, alikumbuka aliurudishia japokuwa hakuwa ameufunga na uungua kwani hakutarajia kukaa sana, na kuuona upo wazi akaanza kuhisi wasiwasi.

‘Mhh, nisije nikawa nimeingiliwa na wezi….’akasema

Akawa anausogelea mlango wake, na kuchungulia ndani, akahisi harufu ya mume wake, kila mtu anajua harufu ya mwenzake, mafuta gani anapendelea kupaka, manukato, na mama huyu anajua kabisa harufu ya mume wake ipoje, akajua kuwa ni mume wakeyupo ndani.

Akaingia kwa aibu akijua yeye ni mkosaji, kwa kuondoka nyumbani na tena hakuwa amefunga mlango vyema,  hata hivyo haijatokea kabla , mara nyingi mume wake akirudi anakuwepo ndani, akajipa moyo kuwa mume wake hatakasirika sana, ni kweli mara nyingi mume wake akirudi kazini yeye ndiye anayempokea.

Alipoingia ndani akamkuta mume wake amekaa kwenye sofa yao ya kuanzia maisha, akiwa kajiegemeza, alionekana kuchoka na akawa kama kasinzia, alimtupia jicho mume wake akamuonea huruma, ….kachoka, ana njaa, …

Mume wake akahis mtu kuingia, akafumbua macho, na macho yake yakakutana na macho ya mke wake, mke wake alisogea na kusimama mbele yake. Mume huyu akajiinua na kujinyosha na kumuangalia mke wake, mke wake akatangulia kumsalimia

‘Za kazini mume wangu….?’ Akamsalimia

‘Nzuri tu, za hapa…’akasema kwa sauti kavu kuashiria kutokuwa na furaha , mke alijua ni kwasababu ya kuondoka hapo nyumbani, na akataka kugeuka kwenda kumtayrishia mumewe chakula na mume wake akauliza

‘Niambie kuna nini kimetokea?’ mume wake akauliza sasa akiwa kasimama akijinyosha, na yeye akaanza kumsimulia mume wake habari za huyo mama, na mume wake akasema;

‘Wewe nipe chakula niondoke zangu, maana nyie watu msio na kazi kitu kidogo tu hamtaki kiwapite…..’mume wake akasema.

‘Samahani mume wangu, unajua niliposikia kuwa mama huyo ni mtu kutoka mbinguni kaja kuleta baraka za uzazi, na kuondoa mikosi kwenye ndoa, nikaona na mimi nikajionee, tuipate hiyo baraka….’akasema

‘Sasa umeshaipata hiyo baraka?’ mume akamuuliza kwa dharau.

‘Mhh, mume wangu naye…baraka utazipataje na kuziona kwa sikumoja, onaje si mpaka ipite siku kadhaa, sisi tuombe mungu, ila huyo mama ni mtu wa ajabu sana, sikuwahi kuona uso wake, hata sijui anafaanaje, bado nina mashaka naye…’akasema

‘Ohooo, wewe mwenyewe umeshatilia walakini,…imani yenye mashaka sio kamilifu, hebu niambie  kwani yupoje huyo mama?’ mumewe sasa akawa na hamasa kusikia zaidi.

‘Ni….sijui nimuelezeje, anisamehe nikisema hivyo, ni kama vile hana akili nzuri , maana anavyokimbizana na watoto, anavyoimba ni kama mtu hajitambui vile kawa kama mtoto mtoto kivitendo…’akasema

‘Ndio huyo unasema analeta baraka, si nimekuambia kwa vile huna kazi, basi umeona hilo ni la muhimu, umeacha nyumba bila hata kufunga mlango na funguo, hivi ungeibiwa ungekuja kulalamika…’akasema mume wake .

‘Mume wangu samahani, nilijua nafika mara moja na kurudi tu, kwanza nani angetuibia wataiba nini humu, …ila kwakweli mume wangu, mimi nikisikia jambo linalohusu kupata mtoto, sitaacha kuliendea ilimuradi tu liwe la halali…’akasema

‘Haya bibiye, maana na wewe na mtoto….hujasikia watu wanatupa watoto majalalani au chooni, unafikiri wanapenda kufanya hivyo, ni shidaa tu mke wangu…., watoto wana heri zao, nakubali kweli, mkioana mnatarajia hilo,  lakini pia kutokana na nakama za maisha watoto wanaweza kuwa mzigo….’akasema.

‘Ukiwa nacho ni lazima utasema hivyo, na wanaosema hivyo wanasahau kuwa kuna watu wanatafuta, hawana kabisa….’akasema

‘Ni kweli mke wangu, kuna wanaotafuta kama sisi, lakini wenye nao, wana matatizo yao wewe waulize watakuambia, ndio ni kweli watoto ni furaha ya ndoa, ….hata sisi tunatamani tuwapate, lakini kwanza tumshukuru mungu, kwani, hujui kwanini mungu ameamua kutucheleweshea kupata mtoto, wewe hujui hekima ya mungu,….’akasema mume wake.

‘Ni kweli lakini subira hii imezidi, miaka kumi, hatuna hata , angalau hata mima ingelitunga na kutoka, hakuna hata dalili,….mmmh, inataka moyo,….’akasema mke wake na hapo akamuona mume wake kama na yeye kazama kwenye mawazo, akajua hilo na yeye limempa jakamoyo. Halafu mume wake akainua kichwa na kumuangalia mkewe, akasema;

‘Kwahiyo unataka kusema nini?’ akauliza

‘Tujaribu upande wa pili….’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo, sijakuelewa…?’ akauliza mume wake akimkazia macho

‘Twende kwa wataaalamu wa tiba mbadala…’akasema mke wake kwa sauti isiyo ya kujiamini.

‘Mbona tulishaenda huko mara nyingi, au una maana gani ,…kuna watalaamu wengine zaidi ya hao,…mke wangu mara ngapi tumeenda huko na kupata dawa, hebu achana na hayo mawazo..’akasema.

‘Ndio tatizo lako mume wangu, tuliowaendea sio wale wataalamu wenyewe , kuna wale wataalamu wa kuangalizia,…wanagundua tatizo lipo wapi…’akasema

‘Eti nini, umeanza kuwazia hayo, hebu nipe maji ninywe niondoe zangu, maana nyie wanawake mkiwa hamuna kazi mnadandaganya tu, ….’akasema mume mtu.

‘Nani hana kazi mume wangu, wewe unafanya kazi huko nje, na mimi nafanya kazi humu ndani, ni mpangilio tu, hiyo kauli yako ya kusema hatuna kazi sio sahihi, na sijakaa kuongea na watu ovyo, …’akasema .

‘Sasa sikiliza sitaki hayo mawazo , na nisije kusikia umeenda huko, unakumbuka mdogo wako alivyokuasa kuhusu watu hao, mdogo wako shule imemkomboa, ana mawazo mapana, na vizuri kasomea maswala ya afya, mimi nimemuelewa sana, ..tusubiri mke wangu, achana kabisa na imani hizo, umenisikia…’akasema.

‘Nimekusikia mume wangu….’akasema mke mtu alipoona mume kapandisha sauti kuashiria kukasirika, na haraka haraka akaondoa vyombo.

Baadaye mume wake aliondoka.

Yeye akawa kakaa pale alipokuwa kakaa mume waks na kushika shabu, akiwaza, na akashituka pale aliposikia zile kelele zikirudi tena, ilikuwa kama zile kelele nje zimetoweka, kama vile hao watu walimuogopa mume wake, kwani mume wake alipoondoka tu,  haikupita muda, mara akasikia kutoka barabarani;

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’, aliposikia hivyo, mama huyu akasimama na kusogea dirishani, kuchungulia dirishani, sasa watoto walishapungua, walibakia watoto wachache, akaweza kumuona yule mama, lakini alikuwa kampa mgongo.

 Pale aliposimama yule mama, kulikuwa na kundi la watoto wamesimama wakimchokoza, na yule mama aliokota fimbo akawa anawatishia kuwachapa wale watoto , na watoto wakakimbia na baadaye wanamrudia tena , na wakimfikia yule mama yule mama anawaimbia;

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’ ananyosha mikono kama anaomba halafau anashika kichwa kama kukata tamaa, basi na watoto nao wanakuwa kama wameamrisha waimbe na kuigiza vile vitendo, na baadaye wanaruka juu hewani;

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’

Kwa hali ile watoto wengi wakawa hawaondoki karibu na yule mama, na kila muda ilionekana wakisogea karibu na nyumba ya huu mama, kiasi kwamba na yeye aliona ni kero. Akashindwa hata kujipumzisha, kwani muda kama huo, wakati mume wake hayupo hujilaza kidogo, akiamuka huanza kazi za usafi na mapishi kwa ajili ya chakula cha usiku, lakini kutokana na hizo kelele karibu na nyumba yao akajikuta hawezi kulala, akasema;

 ‘Watoto wazuri, lakini fujo zao…aah, mimi nitatoka hapo nje niwafukuze…’ Akasema na kufungua mlango kutaka kutoka nje, akiwa na dhamira ya kuwakemea waondoke eneo la nyumba yake, na wakati anafungua mlango simu yake ya kiganjani  ikaita, akatulia kusikilizia iliita ikakatika.

Baadaye tena ikaanza kuita, akajua mpigaji kweli anahitajio na yeye,  Ikabidi arudi ndani pale alipoiweka simu yake.

Akaichukua, na hakutaka kuangalia aliyepiga ni nani, akaiweka hewani na kusema …

‘Halloh, nani mwenzangu…’ aliuliza kabla hajaangalia nani aliyepiga, aliposikia sauti akajua ni sauti ya mdogo wake.

‘Shikamoo dada…’, akasalimiwa

‘Marahaba, hamjambo huko kazini..?’ akauliza

‘Mhh, dada, ….’akaguna na sauti anayotoa sio sauto yake ya kawaida, na mara mdogo wake akaanza kulia, na aliposikia hivyo kilio, mwili ukamuisha nguvu, akakaa vyema kwenye kiti, maana kilia kina maana nyingi, na mara nyingi ni ishara ya msiba.

Kiujumla ndugu hawa wanapendana sana, na kusikia kilio kwa mdogo wake, ilikuwa ni kama kapigwa sindani ya ghafla, na akilini akaanza kumuwaza mdogo….

Mdogo wake anafanya kazi hospitali ya mkoa, amehamishiwa huko hivi karibuni tu, na mara nyingi walikuwa wakimtegemea sana yeye walipokuwa kwenye hali mbaya, japokuwa na wao ndio waliomsaidia kupata mafunzo hayo ya unesi, na alipopata kazi, hakuwatupa, akawa ni tegemeo lao kubwa na kwa wazazi pia, hasa kipindi walipokuwa kwenye mkwamo wa kimaisha.

Sasa hivi angali mume wake ana kibarua wanajiweza wenyewe, japokuwa kipato sio kizuri sana, lakini siku zinakwenda. Mwanzoni kabisa mume wake alikuwa na kazi nzuri, kabla hajapunguzwa kazini, na kipindi hicho ndipo walimchukua huyo mdogo wake alipomaliza kidato cha nne, wakawa wanamsomesha unesi.

Alipomaliza hayo mfunzo, na kufaulu vizuri akaomba kazi hospitali ya wilaya, na bahai nzuri akapata kazi, na akawa na juhudi kubwa , akiwa humo kazini, akawa anajitahidi kujiendeleza na kufikia kiwango kizuri, ikatokea uhamisho.
‘Dada na shemeji nimepewa uhamisho kwenda kufanya kazi hospitali ya mkoani, hospitali ya rufaa…’akawaambia
‘Oh, hongera, ina maana cheo kimepanda…’wakamwambia.
‘Ndio hivyo, nashukuru kuipata hiyo nafasi maana huko nitajitahidi nisome zaidi, nataka niwe dakitari kabisa…’akasema
‘Ni wazo zuri, na juhudi yako itakueletea matunda muhimu ni kuzingatia kazi, na usifanye mzaha, kama unavyoona hali zetu, …wazazi wetu , kwahiyo uije kuharibu kazi, …’akaaswa.

‘Kwakweli kazi kwangu ni muhimu sana, sitafanya makosa, …nitajitahidi sana, sitawaangusha…’akasema.

Na baadaye kweli akaondoka kwenda kufanyia kazi hospitali ya mkoa ya rufaa, alipopata uhamisho huo ikabidi atafute chumba huko huko mjini, karibu na maeneo anapofanyia kazi, na kuondoka kwake mwanzoni ilikuwa kama pigo, kwani asilimia kubwa walikuwa wakimtegemea yeye pale walipokuwa wamekwama kabisa, hakuwa na hiana ya kutoa msaada.

Ikawa wanawasaliana kwa simu, na siku akiwa mapumziko anakuja kuwatembelea mara moja moja, na kuna kipindi anakuwa adimu kabisa kutokana na kazi zake.

Katika familia yao wamezaliwa wao wawili tu yeye na mdogo wake huyo, kwahiyo wanapendana sana, na kipindi wanaishihapo  pamoja, watu walidiriki kuwaita mapacha, japo kiumri walikuwa hawaendani, waliwatania hivyo kwa vile kisura wanafanana,  ingawaje yeye alishaanza kuonekana mtu mzima zaidi, na ukichanganya na mawazo, sasa hivi anaonakana mama …

 Basi aliposikia sauti ya mdogo wake akilia..kwanza alivuta pumzi, lakini aliposikia nalia, hata yeye akajikuta machozi yanamlenga lenga, akavuta pumzi , akisubiria kusikia tatizo, na hasa inavyoelekea ni msiba….ni nani kafa…’akawa anajiuliza


‘Vipi habari za huko..?’ akaulizi akijaribu kujipa moyo , alihisi sauti ya mdogo wake, japo anajitahidi lakini yupo katika wakati mgumu, kuna jambo baya limetokea huko anakofanyia kazi, au kuna taaarifa ya msiba.

‘Habari sio nzuri dada….kuna matatizo…..’akasema na kilichofuata hapo ni kilio.

‘Unasema kuna matatizo, tatizo gani , kwani  imekuwaje, sema basi mbona unaanza kulia, mimi unanitisha, kuna msiba au kumetokea nini…’ kabla hajasikia vizuri simu ikakatika.

Alipoangalia akakuta simu yake haina chaji, akakumbuka kuwa alisahau kuichaji usiku, kwasababu umeme ulikatika, Akakimbilia kuichaji, lakini akakuta umeme hakuna.

‘Mungu, hili sasa balaa,…huu umeme jamani, kila siku kukatika, sasa sijui nifanye, maana nahisi mdogo wangu yupo kwenye matatizo makubwa, mume wangu angelikuwepo tukashauriana, hata ikibid mtu apande basi aende huko, …’ akajikuta anaongea peke yake, mara ningi akasikia kelele sasa zikiwa zinatokea mlangoni mwake.

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’ mama huyu subira ikamshinda, akasogea pale mlangoni na kufungua mlango, kwa hasira akasema;

‘Hata mimi nataka mtoto wangu..ondokeni hapo nje, mnanipigia kelele, nataka mtoto wangu, nataka mtoto wangu, nani kawaambia mtoto wenu yupo hapa, ….’huyu mama akaongea kwa hasira na watoto wakakimbia, lakini yule mama akawa kasimama pale pale, akiwa kageukia barabarani.

Mama huyu akamuangalia yule mama akiwa kabakia peke yake…alikuwa kavaa gauni refu linampwaya, la mistari mistari, kulikuwa na mikanda ya kufunga kati kati, lakini hakuiunga, kaiacha inaning’inia tu….miguuni hajavaa kitu…, akataka kumuambia yule mama ageuke amuone sura yake.

Alipoona huyo mama kasimama tu hageuki, akaona asipoteze muda, kwanza wa nini, wakati ana linalomsumbua kichwani,  akageuka kurudi ndani akiombea umeme urudi, lakini hakukuwa na umeme,  akachukua simu yake na kujaribu kuiwasha tena,  bila mafanikio. Akairudisha sehemu ya chaji na sasa akawa anawaza la kufanya.

‘Mhh, hapa inabidi nikaombe msaada….’akasema

Akatoka nje ilia aone kama atampata mtu wa kumuomba simu, lakini alichoona ni wale watoto wakiwa wanazidi kujaa eneo karibu na nyumba yake. Akatoka hadi kwa jirani, jirani yake hakuwepo, akarudi nyumbani akiwa hajui afanye nini.

‘Hapa inabid niende kupiga simu za vibandani, lakini pesa niliyo nayo hapa ni ya matumizi ya usiku, haitoshi, …na hata sijui nifanyeje…’akasema akijaribu kuhesabu pesa aliyo nayo, akagundua kuwa haitawezekana, akabakia kushika shavu, na mara akasikia mlango ni kukigongwa.

‘Hodi hodi hapa…’ akasikia sauti ya mume wake ikiita kwa nje

Kwanini mume wake akapiga hodi hivyo kwa mbali, sio kawaida yake, na sauti hiyo inamtisha akikumbuka na simu ya mdogo wake, basi nguvu zikamuishia, ….’taratibu akawa anatembea kuelekea mlangoni, akashika kitasa na kufungua mlango, moyoni akiwa kidogo na amani kuwa mwenzake kaja wataongea la kufanya,  lakini bado moyoni hakuwa na amani, kuna nini kimetokea ….

NB: Tusihie hapa kwa leo


WAZO LA LEO: Mawasiliano ni kitu muhimu sana, japokuwa wengi siku hizi hawatilii sana umuhimu wa mawasiliano…wengine hutumia mawasiliano hayo kudanganyana tu, nipo ‘nipo mahali fulani kumbe sio kweli, au mtu akipokea simu au kupiga simu haweki kipaumbele cha jambo, anaweza kuanza kuongelea mambo mengine yasiyo na umuhimu, au salamu ndefu, na kuliweka lile jambo la muhimu baadaye. Tukumbuke kuwa wakati ni ukuta, na umuhimu wa jambo ni kipaumbele chake. Lipe jambo umuhimu wake, hasa unapoongea kwenye simu, na mengine yasiyo na umuhimu yaje baadaye, na pia tujali gharama zake.

Ni mimi: emu-three

No comments :