Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, January 21, 2015

NANI KAMA MAMA-21


   Nesi ambaye aikuwa kaduwaa akiendelea kukumbuka jinsi ilivyokuwa, wakati huo madocta walikuwa wakitaka awape taarifa, lakini mdomo wa nesi ulikuwa mgumu, kwani akili yake ilikuwa mbali, ilikuwa ikijaribu kukumbuka ilivyokuwa, ili aweze kujitetea. 

Na zaidi kilichomvunja nguvu ni pale alipoanza kuelezea, na kabla hajamaliza docta bingwa akamkatiza, alipoona kuwa yeye anapoteza muda, na kumkatiza kule kulimfanya ashindwe kuongea, akawa kama kagandishwa, na akilini akawa anakumbuka pale alipofika chumba cha mgonjwa akitokea kuchukua chupa ya kumuongzea huyo mgonjwa maji….

Nesi alikumbuka kuwa, alipofika chumba alichokuwa kalazwa yule mama, alifungua mlango, na mcho yake yakawa yametua kitanda alichokuwa amelala yule mgonjwa. Alichokiona kilimfanya adondoshe hata kile kisinia kidogo, ambacho aliwekea maji ya kumuwekea mgonjwa na dawa zake.

 Macho yalimtoka pima, kwa uwoga, alijikuta akitetemeka na kutamani akimbie, lakini angekimbilia wapi,…akatamani apige yowe, lakini ingesaidia nini…akashikwa na bumbuazi kwa dakika moja, huku akishindwa afanyeje…

Alijikuta amaichukua ile chupa ya maji na kuweka kwenye kile kisinia na kutoka mbio kuelekea kule walipokuwa madocta,....akijua huenda, wao ndio wamchuekua hata hatua hiyo..lakini haikuwa hivyo....


 Tuendelee na kisa chetu

************

Madakitari walipoona nesi kaduwaa, hasemi kitu, hasa alipokatizwa na docta bingwa, wakati anaanza kujieleza, akimuuliza mkuu, kuwa kumetokea nini, ilikuwa kama kapigwa sindani ya gazi, akawa kimiya, huku mdomo ukimtetemeka kutaka kusema jambo….

‘Wewe vipi….’ilikuwa kauli ya docta bingwa, ambaye alishahisi kuwa huko alipotoka nesi kuna tatizo kubwa sana,  docta bingwa akavuta hatua moja, mbili, akamkaribia nesi, huku akisubiri kuwa labda nesi atasema lolote, lakini hakuna kauli iliyotoka kwa nesi, zaidi ya kutetemesha mdomo

Docta bingwa  naye kama ilivyokuwa docta kijana hakusubiria tena, akampita nesi na kwa haraka akatoka nje kukimbilia huko wodi aliyolazwa huyo mama, na akilini alijua tayari huyo mama huenda keshakata roho, au vinginevyo kuna jambo jingine kubwa limetokea.

Madocta wengine na wao wakawa wanamfuatilia nyuma bosi wao, huku kila mmoja akimpita nesi, anakuwa na shauku kuwa huenda nesi ataongea lolote ili liwape fununu, lakini nesi hakuweza, mdomo ukawa mzito, basi wote wakawa wanaelekea huko chumba cha mgonjwa wao.

Ikawa ni mbio mbio, kuelekea chumba hicho cha wagonjwa maalumu, na chumba hicho kilikuwa chumba cha pili yake kutoka hapo, lakini wenyewe waliona kama chumba hicho kipo mbali ajabu, walipofika mlangoni walishangaa, kwani chumba hicho muda wote kinakuwa kimefungwa kwasababu ya kipoza hali ya hewa, lakini muda huo chumba kilikuwa wazi, wakahisi huenda docta kijana ndiye kakiacha wazi kwa dharura hiyo, au  nesi kasahau kuufunga ule mlango kwa kuchanganyikiwa.

Mbio, mbio wakisukumana kuingia mlangoni, kila mmoja akitaka atangulie yeye kuingia. Na wa kwanza alikuwa docta bingwa, akiwa na lake kichwani, kuwa sasa yule mama hauyupo tena duniani, anahitajika kuandika taarifa, na sijui kama nesi alikumbuka muda huyo mama alipotulia kuonyesha kuwa keshakata roho.

Weengine halikadhalika walikuwa na yao, kuwa huenda,…huenda…...

Waliyemkuta mle ndani alikuwa docta kijana, alikuwa kasimama pembeni ya kitanda huku akiangalia mashine ya mapigo ya moyo, akiwa kashika kidevu hakugeuka, alikuwa katulia kimiya…

*******

‘Vipi kuna nini kimetokea,…..?’ akauliza docta bingwa akiangalia kitandani, lakini hakupata jibu. Docta bingwa akainua kichwa kumuangalai docta kijana, na docta kijana, alikuwa kimia kaduwa, mtindo ule ule wa nesi, hakuwa na jibu.

Docta bingwa akamsogelea docta Kijana, na kuwa naye sambamba, na yeye akawa anatizama ile mashine ya mapigo ya moyo, kama vile atapata jibu sahihi, …na waliokuja nyuma yao walikuwa madocta wengine, wakiwa na swali lile lile

‘Kwani kuna nini , kumetokea nini….?’ Wakauliza, na wao hawakupta jibu, wakasogea pale waliposimama wenzao, na wao wakawa wanaangalia kule kule walipokuwa wakiangalai wenzao. Mshine ilikuwa kimiya kama haianyi kazi!

Huku nyuma nesi alikuwa kaachwa  peke yake, akiwa anatafakari jinsi gani ya kujitetea, alikuwa kabakia mwenyewe kwenye chumba cha mapumziko cha hao hawo madakitari, akiwaza, nini afanye, kwani mdocta wote walikuwa wameshakimbilia huko kwenye tukio.

Nesi alikuwa kama ndio katoka usingizini, akashituka, na akili ikaanza kufana kazi, mdomo uliokuwa mkavu, sasa ukawa na umajiumaji, tayari kwa kuongea, lakini kwa muda huo angeliongea na nani, madocta, wakubwa wake wa kazi walikuwa wameshaondoka, na kwa kukaa kwake kimia itakuwa imetafsriwa vingine, kuwa hayupo makini, hawezi kutoa taarifa kukitokea tatizo, mzembe…hayo yote yanaweza kumkosesha kazi,

‘Mungu wangu nimefanya nini, kwanini nilishindwa kujieleza…..’akawa anajilaumu, lakini alikuwa ameshachelewa.

 Nesi taratibu akageuka, akavuta hatua kutoka nje, akawa anaelekea mlangoni, huku, moyoni akiwaza mengi,  na mwishowe akasema;

‘Ngoja na wao wenyewe wafike wajionee kama nilivyojionea mimi…, najua baada hapo nitatakiwa kujibu maswali mengi, ambayo kiukweli sina majibu sahihi, na labda nitaonekana mzembe, lakini watakuwa wamenionea, mmmh, najua sasa nakosa kazi, sijui nitakuwa mgeni wa nani,  …’akasema  huku akishika kichwa.

Nesi alipofika nje, akasimama, akijaribu kuwaza aende wapi, alifahamu fika anatakiwa kwenda kujieleza, maana yeye ndiye aliyekabidhiwa majukumu yote, kwahiyo anabeba lawama, anatakiwa kwenda kujieleza,…’
‘Nitawaeleza nini mimi…?’ akajiuliza, kwanza akasubiri kidogo , halafu kwa mwendo wa taratibu akaanza kutembea kuelekea huko walipokwenda hao madocta akijua sasa anakwenda kujibu kesi, kesi ambao hana cha kujitetea, na hata hajui  kabisa atasema nini, akawa najilaumu kwanini alipoteza muda kuongea na shiga yake.

‘Lakini sikukaa sana, niliongea kidogo tu, nikatoka,…sasa sijui kuna nini kilitokea…’akawa anajiongelesha mwenyewe huku anatembea mwendo wa kusua sua.

‘Ngoja niende huko huko…. Mungu atanipa njia….mungu naomba unipe kauli maana hili sio fungu langu…’akawa ansema huku anatembea kulekea kile chumba alichokuwa kalazwa huyo mama, kwenda kukutana na madocta…..


************

 Katika kitongoji kimoja nje ya mji, kulizuka sintofahamu, watu walisikia ghasia, na ghasia kitogo ikigusa masikio ya watu, huvuta hisa za kutaka kujua kuna nini, basi watu wakatega masikio, na pale masikio yaliposikia, lakini hayakutosheka, akili ikamtuma macho aone ni nini kinaendelea.

Watu wakajikuta wakitoka majumbani mwao na kuangalia hicho kinachoendelea huko barabarani, na mara sauti moja ikasikika, sauti nyembamba ya kike, na sauti nyingine ya watoto wakimuegelezea huyo msemaji ikasikika ikiitia.

Wanasemaje vile….akili ikajiuliza na kusikiliza zaidi, na sauti ikarudia;

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu ….’ Ilikuwa sauti ya kike.

Waliobaatika kutoka haraka kabla kundi la watoto halijaongezeka, wanasema aliyekuwa akighani hiyo saui alikuwa mwanamama aliyekuwa akipita njiani, na watoto wakaanza kumfuata nyuma, wakimuigizia hiyo sauti, wakisema; ` Nata-nata, nataka, mtoto wangu’

Ilianza kama mchezo, watoto wawili, watatu, wanne, na mara kundi kubwa la watoto, likawa linamfuatilia nyuma huyo mama. Watu wakawa wanashangaa, ni nani huyo, na kwanini anaimba hivyo, na kwanini watoto wanamfuatilia nyuma wakimuegelezea anavyoimba, au kutoa kauli hiyo.

Kuna muda sauti ya mwanamama huyo ilikuwa kama inakaripia, na kuona ni kero, na kwa kufanya hivyo, watoto nao wakaona ni kama mdhaha, akisema na wao wanamgeza, na huyo mama anatembea huku na kule, akigeuka kuwaangalia watoto, watoto wanasimama, na yule mama anageuka kuendelea na safari yake,  na watoto nao wanamfuata nyuma.

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu ….’ Anasema na watoto nao waniga, ` Nata-nata, nataka, mtoto wangu , …’ ikawa ni wimbo, hata akina mama majumbani na wao wakawa wanageza, ` Nata-nata, nataka, mtoto wangu , ….’


Watu wakawa wanashangaa na kila mmoja akawa na hamu ya kumsikia huyo anayeimbisha huo wimbo wa aina yake ni nani, na kitu gani kimewafanya watoto wavutike naye…huku wazazi wengine hasa wenye watoto wakiingiwa na wasiwasi na watoto wao wakiogopa asije ikawa ni mbinu ya kuwadhuru watoto wao.

‘Hivi mnamfahamu huyo mama?’ ilikuwa sauti ya mama mmoja aliyejitokea kwa jirani yake akiwaangalia watoto waliokuwa wakizidi kuongezeaka kumfuatilia huyo mama

‘Hata hafahamiki, sijawahi kumuona kabla,  …kwanini anafanya hivyo, au kapungukiwa nini….’akasema mwingine.

‘Jamani visa vya kupotea watoo vimezidi , mumesikia juzi kijiji cha jirani watoto wawili wamepotea hivi hivi mpaka leo hawajulikani walipo,….’akasema mama mmojawapo.

‘Pia kijiji kingine kuna mtoto alipotea na wkagundua mwili wake ukiwa umenyofolewa sehemu za siri,  sasa isije ikawa ni mbinu ya huyu mama kuwateka watoto wetu…’mama mwingine akasema.

‘Ikishindikina inabidi tumuambie mjumbe, mama huyo akamatwe…’akasema mwingine

 Na kwa minajili hiyo kile mwenye mtoto akawa anakimbilia barabarani kumtafuta mtoto wake, kwahiyo badala ya watoto, sasa wakawa watu wazima na wao wapo kwenye kundi, na wengi wao wakiwa ni akina mama, wakawa wanamfuatilia huyo mama, na wengine wakawa wanawaita watoto wao majina.

Kwa jnsi ilivyo, ilikuwa vigumu kumuona huyo mama yupoje, kwani watoto walimzunguka, na ilikuwa kama vurumai sasa, na kila mmoja alikuwa na hamu ya kumuona huyo mama anayeimbisha watoto ni nani

Kundi la watu wakawa nawo wanamsogelea huyo mama, lakini kwa tahadhari, na kila wakimkaribia, anakuwa kama anakimbia, watoto wanamkimbilia,  na yeye huanza kuimba, ‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu..’ watoto kwa furaha na kwa mdhaha na wao huimba, ` Nata-nata, nataka, mtoto wangu’

Basi  watoto wakawa wanaongezeka kuwafuta  watoto wenzao, na wazazi wakawa wanawakimbilia watoto wao kuwarudisha nyumbani, na wazazi hawa wakikutana na wenzao wanabakia kuulizana

‘Huyu ni nani, nasikia ni mama…?’ wakauliza.

‘Hata mimi sijamuona vyema,…’akasema mwingine

‘Nasikia ni mama tu, lakini hajulikani wapi alipotokea….’mwingine akaongezea kusema.

‘Anafananaje?’ akauliza mwingine.

‘Hatujui, maana kazungukwa na watoto, kuna mtoto mmoja kasema mama huyo kajifunika sehemu kubwa ya kichwa chake, na amevaa gauni kubwa, ambalo sio la kawaida. Ni mwanamke mgeni sana hapa kijijini kwetu…

‘  Nata-nata, nataka, mtoto wangu…’ sauti ikawa inaongezeka kila muda.


*************
Kwenye nyumba moja ya jirani na hapo barabarani, kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa kajipumzisha ndani ya nyumba yake, alikuwa kajilaza kitandani baada ya shughuli za ndani, na pilika za hapa na pale, aliona ajipumzishe huku akimsubiri mume wake, ambaye huja kula chakula mchana nyumbani, akawa kajisikia kuchoka, na kausingizi kakawa kamempitia.

 Akiwa katika usingizi wa mang’amu ng’amu, mara akawa kama anaota, watu wanatafuta watoto, na watu hao wakawa wanapita kila nyumba kuulizia mtoto aliyepotea. Na cha ajabu muulizaji akawa anauliza kama vile anajua kuwa mtoto huyo yupo hapo anasema kwa sauti kali ya kigugumizi…

`Na-na-na taka mtoto wangu..’ huyu mama akiwa ndotoni, akamjibu

‘Mbona mimi sina mtoto wako…’akajitetea

‘Na-nataka mtoto wangu..?’ akaulizwa tena, kwa hasira, na anayeuliza akawa na panga akitaka kumcharanga nalo, na huyo mama akasema;

‘Mimi mwenyewe nataka mtoto …’akasema.

Mara akakurupuka toka usingizini, na kusikia kelele nje, akainuka na kuangalia dirishani baada ya kusikia kelele zikizidi.

Alipofunua pazia la dirisha na kutizama nje, aliwaona wale watoto wakiwa wanaimba kwa sauti, na sauti ya kike ilikuwa kama ndio inaimbisha, ikisema; ‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu , ..’ na watoo nyuma hata baadhi ya akina mama wengine wakawa na wao wanaigilizia, …` Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..!

Yule mama akashangaa, hii ndoto ina maana gani, na kwanini iwe sawa na tukio hilo linaloendelea huko nje,…! Ndoto za mchana mbaya, inakuwa kama kweli.

Mama yule akapangusa pangusa uso na kuwaangalia wale watoto, wanavyoimba kwa furaha, na kwa jinsi wanavyoruka ruka na kuimba kwa furaha, na mama zao wakijaribu kuwashika mikono kuwarudisha nyuma, mama huyu akaingiwa na mawazo ya huzuni.

Mawazo yalimrudisha nyuma, akawa anawaza kuwa kama naye angejaliwa watoto, au hata mtoto mmoja tu,  na yeye angelikuwa miongoni mwa hao akina mama akimrudisha mtoto wake nyumbani,lakini yeye hajajaliwa mtoto.

Yule mama alipokuwa akiwaza hivyo akajikuta machozi yanamlengalenga, akawaza na kutikisa kichwa huku anasema moyoni;

‘Hivi mimi nina kasoro gani, mbona sipati mtoto, mwaka wa kumi sasa, tangu tuoane na mume wangu, lakini hakuna cha mimba au mtoto, angalau ningepata mimba, itoke, nione nina tatizo lakini  la, hakuna hata dalili, au kweli nimelogwa…’akasema

‘Mmmmh mungu wangu, nisije nikawa…mmmh, hapana, kizazi ninacho hii nina uhakaika, sasa tatizo ni nini…mume naye haeleweki, hanisikilizi…’akawa anongea peke yake huku akiwaangalia watoto wanavyoruka ruka.

Akawaangalia wale watoto, huku machoni kukiwa na ukungu wa machozi, yaliyoanza kububujika, …akainua kichwa juu kumuomba mungu kuwa amjuze tatizo lake ni nini, kuwa yeye hatazaa tena, au kuna tatizo gani zaidi.

Alikumbuka jinsi gani akimwambia mume wake asivyotaka kusikiliza kilio chake kuwa waende hospitli wakapime , ili wajue tatizo nini, lakini yeye hakubali. Huishia kwa maneno mengi, utafikiri yeye ni mtaalamu wa vizazi…na jana tu alisema;

‘Kwani wewe una tatizo gani, unaumwa, unajisikia vibaya, mtoto ni kudura ya mungu, kama tutapata tutashukuru mungu, kama hatukupata, basi ndivyo tulivyopangiwa, mimi sioni tatizo lipo wapi…’akasema

‘Mume wangu lakini tumesubiri sana….’akasema

‘Hivi kwanini, nakuona siku hizi unawaza saaana kuhusu mtoto, mbona mwanzoni nilipokuambia swala hili ukalipuuza, sasa unajifanya kujisikia uchungu…achilia mbali mawazo hayo…mtoto, mtoto, mtoto tutapata tu…’ hayo maneno aliyasema mume wake jana, kabla hawajalala.

Ni kweli maneno hayo, kama ingelikuwa yeye na mume wake tu asingelijali, kwani kupata mtoto ni kudura ya mungu, lakini kila wanapokuja mawifi zake inakuwa ndio gumzo, kwanini wifi hupimi, kwanini wifi hampati watoto…kwanini, kwanini…’mazungumzo kama hayo, yanakuwa hayampi raha.

Japokuwa mawifi zangu wananipenda, lakini itafika muda watanichukia tu ..kwa jina la kukosa mtoto…’akajisemea moyoni.

Ni kweli, mawifi zake wanawmpenda kama anavyowapenda wao, hajaona chuki yoyote kwao, lakini kibinadamu ,lazima watakuwa wanamjadili huko majumbani kwao vinginevyo. Kwani, eti, nani asiyependa kuona ndugu yao, au mtoto wao ana watoto…raha ya mzazi ni kupata mtoto, mtoto ni tunda na faraja ndani ya familia…oh!

‘Mhh, namuonea sana huruma mama yake mume wangu, najihisi kama mimi ndiyo yeye, nina mtoto wa kiume, kaoa, natamani mjukuu toka kwa mtoto wangu lakini hapatikani…’akafuta machozi.

‘Mmmh, pia namkumbuka mama yangu, huenda huko alipo na yeye hana raha, anajiuliza kuna tatizo gani kwa mtoto wake, sijui niende kwetu kwa mama, nani kama mama, kila jambo ni yeye tu,  sijui huko ulipo  ananikumbukaje…’ alishika tama huku anazidi kuwaangalia wale watoto wanaoendelea kuimba!

‘Nata-nata, namtaka, mtoto wangu..’ sauti hiyo ilikuwa inazidi kusikia kwa nguvu na sasa walikuwa wakija eneo hilo alipo huyo mama, na kelele ile sasa akaiona ni kama kero, na yeye akajikuta akiimba, `na mimi nataka mtoto wangu..’

Akatokeza kichwa nje, na kusubiri huyo mama aimbe, na yeye akawa anaitikia, ..na  karibu na dirishs hilo, akawasikia akina mama wakiteta, na mwanaume mmoja, na huyo mwanaume  akasema;

‘Huyo ni mtu katumwa kutoka mbinguni, kuwakomboa akina mama wasio na watoto, ndio maana anaimba hivyo, kuwa mwenye kutaka mtoto naye aimbe, ‘nataka mtoto wangu..’akasema huy o mwanaume.

‘Nani kakuambia anhitaji mtoto, tulio nao wanatushinda, fujo kelele, gharama za kuwasomesha, …wewe unataka watoto tena…’akasema

‘Wewe hutaki, lakini kuna wanaowataka, angalau mmoja tu hawampati….’akasema mama mwingine.

‘Ndio hao wameletewa huyo mjumbe, akisema `nataka mtoto wangu…’ na wewe unayetaka mtoto, unatakiwa uutikie, uombe, shida zako, ndio maana watu wanamfuatilia huyo mama wakimuigizia…’akasema huyo mwanaume.

Ulikuwa umbea uliotungwa na mmbea mmoja, na umbea humea haraka na kusambaa, umbea ukazaa matunda, watu wengine wakachukulia ni kweli, na baadhi yaakina mama wenye shida zao, wengine za watoto, au wanajiona hawaelewani na waume zai, wakatoka majumbani wakajua ni kweli, wakaanza kuitikia  ili waipate hiyo baraka.

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu…’akisema huyo mama, na watoto na wale waliosikia huko umbea, na wao huitikia,  ‘nata-nata, nataka mtoto wangu

Huyu mama kusikia huo umbe akajiuliza nay eye atoke nini, lakini aliogopa mume wake anaweza kurudi, akakuta hayupo, na ikawa ni kesi, lakini akasema;

‘Ngoja nitoke mara moja, nikaitikea mara mbili mbili tatu, huenda nikaipata hiyo Baraka,…’akasema na kutoka kulifuatilia hilo kundi, na yeye akawa miongoni mwa wanaoitikia,

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu’

 Huyu mama alipofika barabarani, akajikuta anavutika sana kumuona huyo mama anayeimbisha huo wimbo wa maneno ya aina yake, kwahiyo naye akasogea mbele, na kusukukumana na watoto ili apite amuone huyo mama, na akina mama wengine wakawa wanasukumana ili kuwaikia watoto wao wawarudishe nyumbani,  huyu mama akawa nay eye anaitikia  kiitikio ;

‘Nata-nata, nataka, mtoto wangu …..’aliitikia sijui kwa ajili ya hiyo kauli ili apate hiyo Baraka au ni kuvutika tu kuimba nay eye huo wimbo, akawa anaimba huku anasukumana na hao watoto ili amakaribie huyo mama amuone ni nani huyo mama, akawa sasa anamkaribi..

NB: Ngoja nisiwachanganye, soma kwa makini sehemu hiyo


WAZO LA LEO: Kuna baadhi ya ndoa huvunjika kwa tatizo la kukosa mtoto, na mara nyingi kunapokuwepo na  tatizo hili, anayetupiwa lawama ni mwanamke. Au ikatokea kupatikana watoto wa kike tu, au wa kiume tu,  halikadhalika, lawama anatupiwa mwanamke.  Tunashau kuwa ndoa ni mke na mume. Tukumbuke kuwa kwenye ndoa kuna mitihani yake, na hilo mlipokee kama moja ya mtihani, ya kuwa ikitokea hivyo,  kaeni chini muongee, kwanza mkubali kuwa yote ni mapenzi ya mungu, pili kujitahidi katika njia sahihi za kitaalamu, kama vile kwenda hospitalini kupimwa kama kuna tatizo la kiafya. Na jithidini sana kuiweka imani yenu ya dini mbele , kuwa mungu ndiye anayejua zaidi.
Ni mimi: emu-three

No comments :