Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, January 16, 2015

NANI KAMA MAMA-18


 Kisa chetu kinajaribu kutukumbusha wajibu wetu, kama familia  na jamii kwa ujumla, mapungufu yaliyopo na athari zake. Kuna baadhi ya wanaume wanachukulia vibaya tafsiri ya mwanamume kuwa kichwa au kiongozi wa familia. Tafsiri hiyo hupotoshwa na kutumiwa sivyo ndivyo.

Kama wewe ni kiongozi wa familia je unajua wajibu wako kama kiongozi, usitumie mabavu na nadharia za imla, kuwa wewe ni kila kitu, hapana, uongozi unahitajia hekima, sasa wewe mwanafamilia kama unalijua hilo kuwa wewe ni kiongozi, hebu jaribu kutafakari kwa kila jambo unalolifanya, faida na hasara zake.

Katika jamii zetu, wapo baadhi ya watu wamediriki kuvuka mipaka na kufanya mambo ya aibu, kupiga, unyanyasaji, na imani za kishirikina, haya yapo na yanahitajika kuelimishana.

Katika kisa hiki tunaendelea kuona hali hiyo, inayowakumba akina mama, kama wahanga wakubwa wa madhila ya imani zisizofaa, ubabe uliokithiri, na unyanyasaji usiojali utu wa binadamu.

Ndoa ambao asili yake ni kuunganisha udugu, na kuleta chimbuko jingine kwa ajili ya kuendeleza vizazi, wengine wanaichukulia kama sehemu ya uatawala wa kiimla. Ndoa ikijengwa vyema, ikawa na mahusiano mazuri, ndiyo inakuwa chanzo kizuri cha jamii, na kinyume chake ni kuwa na jamii iliyojaa chuki, uhasama, na mwisho wake ni ukosefu wa amani.

Kama ni hivyo basi, kumbe tunawajibu wa kuwaelimisha wana ndoa wajue wajibu wao, mume na mke, kila mmoja kwa nafasi yake, ili wakijaliwa kupata watoto, wawe walimu wazuri wa kwanza kwani mzazi ndiye mwalimu wa kwanza wa kiumbe kinachozaliwa.

Lakini pia tukubali kuwa, ndoa inaweza ikawa na mitihani yake, inapotokea hivyo, wanandoa kama wanadamu wenye utu, wajaribu kuikubali hali, lakini baada ya kushauriana, kufanya utafiti wenye tija, kuona tatizo lipo wapi.

Kwenye kisa hiki tumeona tatizo la kukosa kizazi, wanandoa wengi wanapofikiwa na mtihani huu, mtu wa kwanza kunyoshewa kidole ni mwanamke, hivi kweli mwanamke anapenda, au alipenda iwe hivyo….tuwe makini. Lakini pia kuna hawa watu wenye elimu nyingine elimu ya kiasili, ambao wanatumia vipaji vyao kujaribukutatua matatizo ya kijamii, hawa wanaoitwa waganga wa asili.

Katika kila hali kuna watu wengine huitumia hiyo hali kwa ubinafsi wao, waongo, wahadaaji, ambao huingilia Nyanja fulani wakati hawazifahamu vyema, nia na malengo yao ni kuharibu au kunufaika kusipo halali.

Tanzania sasa hivi inasfika kwa imani hizo za kishirikina, na chanzo ni kutoka kwa hawa waganga wa kienyeji, ambao wamejivika nguvu ya kutoa riziki, nguvu ambayo hawana. Wanawahadaa watu kuwa wakitumia viungo vya wanadamu wanaweza kutajirika, hili haliiingii akilini kwa mwenye utu na hekima.

Sasa kama jamii tufanyeje, hili ni swai la kila mmoja wetu, kwani, haya yote yanatokea ndani mwetu, sisi ndio tunaokwenda kwa waganga kwa siri kutaka kujua, au kuelekezwa namna ya kupata jambo. Kama ni hivyo basi kumbe sisi wenyewe ndio asili ya tatizo, na kama sisi ndio asili ya tatizo, kumbe pia tunaweza kulimalizia hili tatizo.

Cha muhimu ni kujua kuwa riziki, utajiri, hauji kwa kufikirika, hauji kwa kutumia migongo ya wengine, utajiri wa namna hiyo ni batili na una madhara. Huwezi kupata utajiri kwa kutumia viungo vya watu, hebu niambia hivyo viungo utaviuza kama nyama,….kwanini hatuna hekima ya kulitafakari hili.

Huyo anayekuhdaa, je ni tajiri, …aliwahi kufanya hivyo akatajirika, mbona hali yake ni dhalili zaidi hata na ya kwako. Huyo ni wakala wa shetani mkwepe, na tafuta njia halali za kupata utajiri.

Kisa chetu kinaendelea , sasa hivi tukielekea moja kwa moja kwenye hospitali ya mkoa, hospitali ya rufaa, ambapo mama wa rafiki yangu, ambaye ndiye anatusimulia hiki kisa, alipopelekwa.

Tuendelee na kisa chetu…

************

 Walipoika hospitali ya rufaa, wengi walishakata tamaa, wakijua sasa mama hatapona na huenda wakapoteza mama na kiumba chake kilichopo tumboni, na hata dakitari bingwa alipoona ile hali ya huyo mama, alifikia kutikisa kichwa na kusema;

‘Mhh, hapa kuna mawili, …kumuokoa mama, na kumpoteza mtoto, au kumpoteza mama na kumuokoa mtoto…’ kauli hii iliwaanya waliokuwepo hasa madakitai wasaidizi kujua kuwa kazi iliyopo mbele yao ni kubwa, na kila mmoja lihitajika kutumia ujuzi wake wote.

Dakitari bingwa, aliwaita madakitari wenzake, na kuwaelekza nini cha kufanya. Hili lilikuwa zoezi lakumuokoa mtoto au mama wa hicho kiumbe kilichokuwa tumboni. Kila mmoja kwa nafasi yake akaanza kuhangaika, na mama akaingizwa chumba cha upasuaji.

Tukumbuke mama huyu alifikishwa hapo hajitambui, hata kauli hana. Damu nyingi zilishapotea, kwani alishaanza kuvuja damu, achia mbali ile damu iliyopotea kwa kuchanwa na miiba na seng’enge. Ukumbuke pia kuwa mama huyu bado alikuwa na vidonda vya miba iliyomchoma usoni na sehemu nyingine za mwili.

 Majeraha mengine yalikuwa makubwa, kiasi kwamba, uso ulihumuka na kupoteza taswira yake ya kibinadamu. Na kwasababu alikaa kwenye maji bila ya matibabu vidonda vilishaingiwa na virusi na vingine kuonyesha dalili ya kuoza.

‘Hapa tuna mitihani, kwani mama anahitaji matibabu ya vidonda, lakini hilo sio muhimu kwasasa inabidi tulitulize kwa dawa maalumu, ila cha muhimu kwasasa ni huyo mtoto aliyepo tumboni, inaonyesha dhahiri kuwa tusipofanya juhudi za haraka, tutawakosa wote wakiwa hai, kwahiyo tukimbilie hili kubwa la kumuokoa mtoto. Akasema yule dakitari kuwaelekeza wenzake.

Kipa umbele kikapelekwa katika kuokoa kiumbe kilichopo tumboni,…


Ndani ya lile jopo kulikuwepo na dakiatri kijana, huyu alikuwa kaja pale kupata uzoefu baada ya kupata masomo yake huko nje. Aliporudii na ujuzi wake,hakutaka kusubiri likizo imuishie nyumbani tu, aliamua kujitolea kwenye hospitali hiiyo iliyokuwepo mkoani mwake.

 Kazi hii ya udakitari ilikuwa ndoto yake toka akiwa mdogo, na lengo lake ni kufikia ngazi ya dakitari bingwa wa uzazi. Yeye alishuhudia wakina mama wakipoteza maisha katika eneo lao, kwa kukosa huduma na wataalamu, akaweka nadhiri moyoni kuwa atajitahidi asome hadi kiwango cha juu, ili aje kusaidia katika tatizo hilo na mungu akaikubali nadhiri yake hiyo.

Kwahiyo, pamoja na kupata ujuzi wa kazi yake, lakini moyoni alikuwa na dhima, na utashi wa kuitenda hiyo kazi, hakuifanya kwasababu ya ajira, aliifanya kwa wito, na hata kuja hapo kujitolea hakuhitaji malipo.

Na katika changamoto mojawapo aliyoiwekea kipaumbele, ni kuwa kama itafikia hatua ya kuchagua nani bakie hai. Yeye aliahidi kuwa katika kazi yake hiyo, inapofikia hatua ya kuchagua nani apone, yeye, atachagua wote wapone. Sitaweka kipaumbele kwa mmoja wapo, nitajitahidi wote wapone

‘Dakitari kijana , jana tulikuwa tukiongelea swala kama hili, ukasema una hamu sana ya kuokoa mama na mtoto , pale inapofikia hatua ya kuchagua nani apone, je katika hali kama hii unaweza ukasemaje, …najua wewe sio mzungumzaji ni mtendaji, naombe ushike usukani wa kuokoa maisha ya huyu mama au mtoto….hili iwe ni moja ya mtihani wako wa kutimiza ndoto yako….’akaambiwa.

Katika hospitali hii ya rufaa, kila muda fulani, kunakuja wataalamu wa kujiunza waliohitmi vyuoni , nia ni kujenga uzoefu na kuendeleza fani zao, na kipindi hicho, kulikuwepo hao wataalamu na mmoja wao alikuwepo dakitari kutoka nchi za nje, aliyefika kwa mualiko maalumu, kwahiyo mama akawa na  Bahati ya kupata wataalamu wa aina zote.

Kutoka na hili hospitali hii ikawa na umaarufu fulani, japokuwa wataalamu hao wengi wakimaliza masomo yao hukimbilia nje, kutafuta kipato zaidi, tofauti na walivyo madakitari hao, dakitari huyu kijana alikataa kwenda kufanya kazi nje, kwani akiwa masomono huko nje, alipewa na nafasi hiyo.

‘Kwanini hupendi kufanyakazi huku nje, wakati ukirdi kwenu utakuwa unalipwa mashhara mdogo na hutapata marupurupu ya maana…?’ akaulizwa na wenzake.

‘Hivi wewe unapoona mzazi wako anaumwa utafanyaje?’ akawauliza

‘Nitamtautia dawa?’ akamjibu mwenzake.

‘Basi ndicho ninachokifanya, mimi nimetoka nyumbani nikiwa nimewaacha wagonjwa, wazazi wangu, nikasema nakuja kuwatafutia dawa, nina uhakiak dawa nimeshaipata, je nifaneje?’ akawa kama anawauliza.

‘Nikuambie ukweli, watu kama wewe husihia kufa masikini, na kuja kujijutia baadaye…’wakasema wenzake.

‘Sizani kama kwa kufanya hivyo nitakua masikini, mimi nitakuwa tajiri kuliko matajiri hao wa mali, …..’akasema na wenzake wakamcheka na yeye akaendelea kusema;

‘Mjue kuwa kuna utajiri wa namna mbili, kuna utajiri wa mali na utajiri wa roho, na nadra sana mtu kupata vyote hivi viwili, ni mtihani …..mimi napendelea zaidi utajiri wa roho, maana hata nikifa nitakwenda na utajiri wangu, na utanisaidia, sio hapa duniani tu, lakini pia na maisha ya huko baadaye….’akasema

‘Huko baadaye unakujua wewe, ni nani alikwenda akarudi akasema kuna maisha ..ukia umekufa tu….’wakasema wenzake.

‘Mimi imani yangu inaniambia hivyo, na ninaamini hivyo kuwa nikifa kuna maisha mengine ambayo mungu katuandalia, lakini yote inategemea maandalizi yako ukiwa hapa duniani…..’akasema

‘Sasa kwanini ukawa dakitari kwanini hukuwa mtangaza dini…’wakamkebehi.

‘Kila kazi unayofanya ina imani ya dini, ….mimi nina imani hiyo, ukiwa umemuweka mungu mbele kwenye kazi zako, basi hutashindwa, kwani yote yanawezekana kutokana na uwezo wake mungu,..ndio maana mimi napenda kuwa tajiro wa moyo,….nyie tafuteni utajiri wa mali, lakini kumbukeni utajiri wa mali ukifa, mali utaicha,huwezi kuzikwa na utajiri wako wa mali…’akasema

‘Hizo ni nadharia za kiimani tu,…muhimu ni maisha mazuri, mengine ukia mbele kwa mbele…..’wakasema wenzake.

‘Hahaha, mbele kwa mbele..niwaambie ukweli, mimi namwamini mungu mmoja, na najua kwake yeye haya yote tunayofanya ndio muweza, usjione una akili sana, unaweza sana,  ukatabakari, na kujiona hakuna zaidi yako, na mungu hayupo, utakuwa umefanya kosa kubwa sana…’akasema.

‘Hatujasema mungu hayupo, lakini mungu kwanini katuumba, ni ili tuishie kila mtu kwa juhudi zake,…ukikaa kumuamini tu, huku hutafuti maisha bora, utachanganyikiwa, na utakufa, na mungu atakuhukumu kuwa alikupa uwezo, na namna ya kuishi ukashindwa kuutumia….sasa ndio maana tunakuambia maisha yapo huku, ukurdi nyumbani utakwenda kusota waya…’wakamwambia.

‘Nimeshawaambia mimi nilitumwa na wazazi nikwatafutie dawa, …wanaumwa, wanasubiri dawa, wanasubiri utaalamu wangu, siwezi kuwatupa, …..’akasema na kuwashangaza wengi.

Leo kijana huyu mwenye dhamira ya kweli ya kazi yake, mwenye wito na uzalendo, yupo chumba cha upasuaji na mbele yake yupo mama, na kiumbe tumboni, na anatakiwa kudhirisha taaaluma yake….

*****

 Tukiwa ndani ya chumba maalumu cha upasuaji, Chumba hiki kilitengwa pembeni kidogo ya jengo kubwa la hospitalini, na kilijengwa kwa utalaamu wa hali ya juu, kilikuwa na vyumba vingine viwili vya upasuaji, ina maana wagonjwa watatu wangeliweza kuhudumiwa kwa dharura za upasuaji. Moja ya chumba hiki cha upasuaji ndipo alipokuwepo mama tunayemzungumzia.

Mama alikuwa katika hali mbaya sana, vile vidonda vilipakwa dawa za kawaida za kutuliza, lakini vilihitajia matibabu zaidi ya hayo, vidonda vingine vilishaanza kuoza, lakini muhimu ikawa sio yeye, sio vidonda vyake, muhimu ikawa ni kumuokoa mtoto…jamani ni nani kama mama!

‘Ni nani kama mama?’….

Alisikika dakitari huyo dakitati mtoto akimonea huruma yule mama, na hapo akamuomba mungu kuwa amjalie huyo mama apone, na mtoto wake, ili baadaye mtoto ajue kiini cha mateso ya mama yake, ambaye alikubali kuteseka kwa ajili yake, na alikuwa tayari yeye kufa ili mwanae apone, hakukata tamaa, hadi hapo alipo…

Kwa muda huo, ndani ya hicho chumba kulikuwa kimya na sauti iliyosikika na ya mashine ya kupozea hali ya hewa. Usingeamini kuwa ndani yake walikuwepo madakitari, wakiongozwa na dakitari bingwa wa uzazi, wakijaribu kukiokoa kiumbe kilichopo tumboni kwa mama asiyejitambua, mama ambaye hali yake ilikuwa mbaya sana.

Dakitari kijana akifanya kazi yake chini ya dakitari bingwa wa akina mama, alikuwa kayaweka mawazo yake kwa kile anachokuwa akikiifanya, na siri kubwa ilikuwa kichwani mwake…kwani pamoja na maelekezo ya dakitari bingwa, pia yeye alikuwa akifanya mengine zaidi.

Akiwa anaongozwa kwa kauli ya msimamizi wake kuwa juhudi zake zote kwasasa ni kumuokoa mtoto, kwani mama hali yake ni mbaya uwezekano way eye kuishi ni mdogo. Lakini kwa dakitari huyu kijana haikuwa hivyo, yeye aliomba wote wapone, lakini angelifanyaje, na wakati wito ulishatolewa kuwa juhudi ziwe kwa mtoto.

‘Oh, sasa hili zoezi likishindiana, nitakuwa nimeongpa,, kuwa nilikwenda nje kuwatautia akina mama, wazazi wangu dawa,…’akawa anajisemea moyo huku akiendelea na kazi hiyo. Akinyosha mkono kuomba hiki na kile, huku dakitari bingwa akiwa pembeni yake kuhakikisha kila jambo linakwenda kama inavyotakiwa.

 Humu ndani kilichokuwa kikongea ni mikono, na jopo la wataalamu wa upasuajil ilikuwa likijitahidi kila mmoja kwa nafasi yake. Dakitari kijana alijitahidi kufanya kazi yake kwa makini, huku akimuomba mungu aweze kufanikiwa, kwani ile ilikuwa moja ya mitihani yake, lakini licha kuwa ni moja ya mitihani yake, nia yake kubwa ni kutimiza ahadi yake ya siku nyingi!.

Baada ya kazi ngumu ya kumuokoa mtoto , kama agizo lilivyokuwa, madakitari walitoka chumba cha upasuaji kwa muda kujadili jambo wakiwa wamekata tamaa,….dkitari mtoto akawa wa mwish kutoka, kwani kulikuwa na kazi akimalizia, baada ya mtoto kuchukuliwa kwenye chumba kingine cha watoto kama hao.

Kwa hali ya mtoto ilikuwa sio nzuri,ilikuwa mbaya sana…, dakitari kijana, akamuangalia yule mtoto na akilini mwake akahisi uhai wa huyo mtoto, kwa mbali akatabasamu, akawaachia wengine wakaendelee na huyo mtoto, yeye mawazo yake yakawa kwa huyo mama, kwani wenzake walishamkatia tamaa.

Wenzake walikuwa wanasubiria muda wa mama huyo kukata roho, kwani walijua yeye ni marehemu tu, kutokana na hali waliyoiona toka awali. Kinyume na madakitari wenzake, dakitari kijana alikuwa na mawazo tofauti alikuwa na yake kichwani ambayo hakupenda kuwaambia wenzake kwa muda huo. Alimuomba mola wake hicho alichokifanya kizae matunda.

Anakumbuka wakati anakifanya dakitari bingwa msimamizi alitaka kumzuia, lakini akawa keshachelewa, na hakukuwa na muda wa kuulizana, ikawa ni siri yake, na huenda siri ya huyo dakitari bingwa kama alikuwa makini kuuatilia kile alichokifanya.

Walipotoka nje yule dakitari kijana akaiinua mikono juu na kumshukuru mungu wake, na tendo hili liliwashangaza madakitari wenzake iweje amshukuru mungu wakati zoezi lakumuokoa mmoja kati ya mtoto au mama yake lilinaonekana kama limeshindikana.

Yeye akawajibu huku akionyesha uso wa furaha, na kusema;
              
`Halijashindikana, na hamtaamini kitakachotokea baadaye, nyie subirini ile kazi tuliyoanya ifanye kazi yake, …' alisema na yeye akaamua kurudi chumba cha upasuaji peke yake. Alitaka kuhakikisha kuwa alichokuwa kakifanya kwa usahihi, alitaka kuhakikisha kuwa anayaona matunda ya kazi yake yeye mwenyewe. Akawa sasa anajaribu kumuhudimia yule mama majeraha yake, hakusubiri muda mwingine.

Baada ya nusu saa miujiza ya mungu akaanza kufanya kazi yake, mtoto akaonyesha dalili ya kuishi, na kilio cha kwanza kikasikika,…na madakitari hao wakasimama na kwenda kuangalia pale walipokilaza kile kichanga, na huduma nyingine zikafuatia.

Wote walikuwa wakisubiria taaria ya muda gani mama huyo atakuwa kaiga dunia, na hakuna aliyekuwa na moyo wa kurudi ndani kwenye chumba cha upasuaji, walimuachia kzi hiyo dakitari kijana.

 Dakitari kijana alikuwa peke yake ndani ya kile chumba , alikuja kuhakikisha kuwa alichofanya kimezaa matunda! Alifikiria moyoni kuwa kama alichofanya hakikufanikiwa basi, ina maana alichojifunza kina walakini, lakini hakukata tama, akajipa moyo kuwa  itawezekana tu, na kama haitawezekana basi ni mapenzi ya mungu!

Akamsogelea yule mama pale alipolala na kutafakari lile alilolifanya kwa yule mama, na alichojifunza masomoni kama dakitari ni kuweka mbele kufanikiwa, na kama itatokea kutokufanikiwa, ni muhimu sana kujua kosa lipo wapi, na ulianyie kazi mara moja….

Muda ukawa unakwenda na hakukuwa na dalili zozote za uhai kwa yule mama akawa anaangalia saa na mashine ya kuonyesha mapigo ya moyo, kuna muda mistari ilikuwa kama inataka kunyoooka,na inafika mahali inaanza kujipinda tena

‘Oh, …mungu wangu nakuomba utoe matunda mema ya kazi hii, sio kwamba ni kwa ujuzi wetu, ila yote yanatokana na wewe…mama anamuhitaji mwanae na mtoto anamuhitajia mama yake….nakuomba mola ..’akawa sasa anaomba hadi machoz yanamtoka, lakini hali ikawa ile ile.

‘Nimefanya kaosa gani mbona nimefuata maelekezo kama ilivyotakiwa…’akawa anasema na kujariu kukakiri kile alichokifanya na kuona kuwa alifanya vyema zaidi.

Basi moyoni akasema iliyobakia sasa nakuachia wewe mungu, kwani hata tungelifanyeje kama mungu hakupenda iwe haitakuwa. Hii ilikuwa moja ya imani zake…Alikumbuka nyaraka zake alizokuwa keshazitayarisha kuhusina na ugunduzi wake ambao alikuwa hajauonyesha wazi kwa wakubwa zake kwani alihitajia tukio kama hilo, kama litafanikiwa basi ataweza kukamilisha ugunduzi wake huo.

Dakitari kijana hakutaka kutoka nje, kuona nini kinachoendelea kwa mtoto, moyoni alishajua kuwa mtoto atapona iliyobakiwa ilikuwa kama huyu mama, sasa alikuwa amemaliza kumganga huyo mama majeraha, akawa anasubiria matokea ya upasuaji, na kile alichokianya, akawa kakaa kwenye kiti karibu na yule mama akimuangalia;

‘Huyu mama alipatwa na nini…..?’ akajiuliza

‘Mhh, labda  alikutana na simba, akawa amemburuza kwenye miba., Vinginevyo, kwanini uso uraruliwe kiasi hicho.

Kila mara dakitari yule alikuwa akikumbuka yale maneno ya yule mama alipokuwa akiweweseka kabla kazi haijaanza ya kumfanyia hiyo operesheni, mama huyu alisema;

 `Muokoeni mwanangu, lakini mimi niachane nife, na nikifa nileleni mwanangu, msimpe mtu, nileleeni mwanangu hospitalini….' alijiuliza sana kwanini yule mama alisisitiza sana kuwa mwanae alelewe na hospitali na wala sio jamaa zake.

‘Kwanza hao jamaa zake ni wakina nani?’ akajiuliza kwani kuna muda alitoka kuwatauta ili kuwaelezea kilichotokea, lakini hakukuta mtu.

Alisema moyoni kuwa huenda ni ile hali aliyokuja nayo yule mama, au huenda kuna ugomvi huko alikotoka, au aligombana na mumewe,lakini haiyamkini kwa binadamu kuwa na unyama kiasi kile, kumpiga mama mjamzito na kumchana chana mama huyo usoni kiasi kwamba sura ilikuwa haitamaniki.

Basi siku ikaisha na hakukuwa na dalili ya kuzindukana kwa mama, lakini pia hakukuonyesha dalili ya kukata roho kama walivyokuwa wametarajia hao madakitari wengine. Siku ya pili ikaingia, hakukuwa na matokeo zaidi, matokea mazuri yalikuwa kwa mtoto

Baada ya siku tatu mtoto akawa amechangamka na kuondokana kabisa na dalili zozote mbaya, lakini mama mtu bado alikuwa hajazindukana, na hali hii iliwatia wasiwasi madakitari wakijua kuwa hawataweza kufanya lolote kumsaidia yule mama kuzindukana. Ilibidi waitane tena kushauriana ili kama imeshindikana wayaondoe yale mashine ya kumsadia mgonjwa kupumua,

Lakini dakitari kijana akakataa, akasema ana imani mgonjwa atazindukana muda mchache ujao.

‘Wewe bado kijana una munkari na kazi bado, na hili ni jambo jema kabisa, endeela na moyo huo, sisi kazi hizi tuna uzoefu nazo, hali kama hii…ni ya kupoteza muda tu,……’akasema yule dakitari bingwa, akiwa na nia ya kumpa yule kijana uzoefu wake wote, kwani kijana huyo alionekana kuipenda kazi yake vyema. Alisema kichwani, huyu yupo kama mimi nilipokuwa makamo yake, nilipenda sana kusaidia watu…kama nchi yetu ingetujali sana,huenda mimi ningekuwa mbali sana, lakini…

Walitoka ndani ya kikao chao kwa haraka kwani aliletwa mgonjwa mwingine mahututi, sana, na kwa haraka wakaingia chumba kingine cha upasuaji, na kuanza kazi hiyo, jopo zima likaelekea kumhudumia huyo mgonjwa mpya.

Wote wakawa katika kazi ya kuhakikisha wanamsaidia huyo mgonjwa mpya apone, na Ilibidi wamsahau mgonjwa wa zamani kwa muda,kwani mgonjwa huyo wa zamani, alikuwa anasubiriwa azindukane, au amalize uhai, na kama atapona kuna kazi nyingine ya ilihitajika dhidi yake ya kuponyesha majeraha yake, na kama itahitajika upasuaji mwingine.  Lakini matumaini ya mgonjwa huyo kupona yalikuwa hayapo.

Walichofanya ni kumuachia nesi majukumu ya kuangalia mambo mengine yanakwenda sawa, huku wakimwambia kama kuna badiliko lolote atoe taarifa haraka iwezekanavyo.

NB: Haya ngoja tuishie hapa kwa leo,

WAZO LA LEO: Kuna fani ambazo zinahitaji kujitolea tu, fani ambazo zinagusa uhai na utu wa mtu, fani kama za udakitari. Wengi wanaujua fani hii, wanaifanya kwa wito, wapo wachache wanaoweka masilahi mbele, lakini hata ulipwe nini, kutokana na ugumu, na unyeti wa kazi yenyewe ilivyo, haitaweza kutosheleza. Muhimu kwa vile umeikubali hiyo kazi, basi jitolee kwa moyo kuwasaidia watu, mengine mungu atakulipa.Ni mimi: emu-three

No comments :