Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, January 13, 2015

NANI KAMA MAMA-16



Hebu sasa turudi kwa mama ,kama unakumbuka vyema mama alitupwa kwenye bonde, na waliomtupa walikuwa na uhakika kuwa mama huyo ameshakufa, kutokana na hali aliyokuwa nayo.

Bonde alilotupwa mama huyo ni bonde la mpunga, asili ya bonde hilo ilitokana na mvua nyingi iliyonyesha kipindi cha nyuma, ikatengeneza kitu kama korongo, korongo likazidi kuchimbika na kutengeneza bwawa ambalo likawa linaongezeka kila kukinyesha mvua...kwahiyo maji yote yalitoka sehemu ya miinuka hufikia hapo.

Likawa ni bonde lenye rutuba, na kipindi cha mvua hujaa sana, kipindi cha jua hukauka-kauka.

 Watu wakaanza kulima mpunga , hasa kipindi cha mvua, na mpunga unakubali kweli,unastawi sana, kutokana mbolea asili kutoka sehemu za juu, na taka taka zinazotupwa humo.

Baadaye kukatokea muwekezaji mmoja kutoka uchina, akalihodhi hilo eneo, japokuwa wananchi walilalamika na kuja juu kuwa eneo hilo ni lao, lakini kutokana na uzito wa muwekezaji ambaye alifuatilia ngazi za juu na kupata hati miliki, ikafikia hatua wananchi wakashindwa, na muwekezaji huyo akawa analima kilimo cha kisasa cha mpunga.

Ikabidi wananchi wafike hapo kuomba kazi na wachache waliobahatika, wakawa wanalipwa mshahara, na mshahara wenyewe ndio huo wa mkononi hadi tumboni. Ila kwa ujumla muwekezaji huyo kwa vile alikuwa na zana za kisasa, akachimba kisima kikubwa ambacho kilikuwa kinatoa maji ya umwagiliaji, basi eneo hilo likawa linatoa mpungwa kwa wingi.

‘Wazungu bwana, sijui wanatumia uchawi gani?’ wananchi wakawa wanaongea.

‘Sio uchawi bwana nizana na uwezo wa kiuchumi, kama hata sisi tungelikuwa na matrekta, mbolea na utaalamu kwani tungeshindwa, lakini wapi tutapata hizo nyenzo, ukimba mkopo masharti yake ni makubwa, kumiliki ardhi kwenyewe ni jambo adimu kwetu...’akasema.

‘Hivi kwanini hati miliki inakuwa ngumu kupatikana wakatii ardhi ni yetu wenyewe?’ akauliza mwingine.

‘Ni ukiritimba tu, lakini kama serikali ingelijali watu wake, kila mwenye eneo angemilikishwa, na kupewa hati miliki, akapewa namba za usajili ili kila mwaka alipie kodi ya maeneo, ...kukawa na wataalamu, wanatembelea, wananchi hao wanawalipa kutegemeana na uwezo, tungelikuwa mbali...lakini tatizo, ubinafsi....’akasema

‘Ubinafsi..nani mbinafsi?’ akauliza

‘Watendaji wetu...kwanza ukifika ofisi zenyewe, mpaka uje uandikiwe hayo maelezo, ni kazi, haya umeshaandikiwa, unatakiwa kumpata mtu wa kuja kupima maeneo, huyo mtu utampata wapi..labda umpe pesa ya usafiri....kuna kazi kweli, kwa mwanachi wa kawaida inamuwia ngumu...lakini kama una pesa, pesa inangea....’akasema

‘Mhh, lakini mbona hapo kama unaongelea mambo ya rushwa ina maana hawa wawekezaji wanatoa rushwa?’ akaulizwa

‘Mhh, hili siwezi kusema, ila akifika, akapenda eneo, yeye anachofanya ni kutuma maombi kwa wanahusika, anatajiwa kiwangao cha pesa, yeye anata hana longolongo...pesa anazo, ...tatizo lipo wapi?’ akasema

‘Lakini kama ni eneo la kijiji, kiutaratibu si inatakiwa wananchi wahusishwe, wakubali, walipwe fidia au?’ akaulizwa

‘Hahahaha....unanichekesha kweli, labda huko mjini kwa watu wenye upeo, wanaweza kudai hadi kulipwa fidia, huku ...watendaji wetu wataitwa watapewa kitu kidogo, watawashirikisha watu wawili watatu, itaonekanana watu waliitwa wakakubali,....eneo hilo, linachukuliwa

‘Ujue wenzetu hawa wakija wanajaribu kuchunguza sheria na watendaji wetu wapoje, sisi tunaongea porojo tu..mwisho wa siku tusipoangalia maeneo yote yenye manufaa kwetu, kama yenye madini, rutuba, mali asili kama gesi vyote vitachukuliwa, ...ukoloni unarudi kwa njia nyingine...’akasema.

‘Mhh, unajua ndio maana nchi za wenzetu kunazuga fujo, maandamano, kuuwana hatimaye vita, ni mambo kama haya, ...na ukichunguza sana, tatizo limeanzia kwetu, elimu ya kujua haki zetu haipo...tunachagua viongozi wenye uroho na ubinafsi...’akasema mwenzake

‘Umeonaeeh, ndio hayo...’wakaachana

Basi bonde hilo likazungushiwa uzio, hakuna mtu kupita tena, hata wale wenye mifugo yao waliokuwa wakichunga eneo hilo, ikabidi watafute maeneo mengine, eneo hilo likawa sio la wananchi tena.

*******

Usiku huo, mume mtu na mkewe walipomfikisha mwili wa mama eneo la bondeni, wakamtupa, wakijua wanatupa mfu, kwahiyo hawakujali walimtoa kwenye toroli, kabla hawajamtupa, mume mtu alikumbuka kitu.

‘Hiki kimkoba chake cheusi, sijui tukifanyeje?’ akauliza mume mtu.

‘Huo ndio uchawi wake, mungie kiunoni, maana hatujui una nini, akiliwa na fisi na wenyewe utaliwa, ….’akasema mke .

‘Mhhh, lakini…..’mume akasita akiuangalia ule mwili.

‘Tunapoteza muda, …..’akasema mke huku akijaribu kuusukuma, lakini kwake ilikuwa kazi nzito, mume mtu akasogea pale kwa pamoja wakauskuma ule mwili kuelekea bondeni. Pembeni ya hilo bonde kuna nyaya zimepita, kwahiyo mwili wa huyo mama ulipita kati kati ya nyaya za seng’eng’enge zikazidii kumchana mama, na bahati mbaya zililenga sana usoni,

Bonde hilo refu, kwahiyo kutoka pale walipomsukumia hadi chini kuna umbali , hata kama mtu ungekuwa mzima, unaweza kuumia sana....na mama aliserereka, na akapitiliza kwenye hizo seng’enge, na kudondoea bondeni.

Eneo la chini ya hilo bonde ndipo kuna sehemu wamelundika mabaki ya majani ya mpunga uliokwisha vunwa ili yaje kutengenenezee mbolea, kwahiyo kulikuwa na malundo makubwa makubwa karibu na bonde hilo, na hicho ndicho kilimsaidia mama, kwani mwili wake ulitua juu ya lundo mojawapo, vinginevyo angelivunjika viungo.


Usiku huo ikazuka mvua kubwa, na bonde hilo lina kawaida ya kujaa maji, basi maji yakaanza kujaa kidogo, kidogo, kutoka milimani kutiririka kuelekea chini ya hilo bonde. Jinsi mvua ilivyoongezeka ndivyo maji yalivyokuwa yakija kwa kasi, na yakaanza kusomba yale malundo ya makapi ya mpunga na takataka zingine na mama akiwemo humo.

Mama alikokotwa na maji kutoka sehemu moja ya bondoe hadi karibu na sehemu nyingine ya bonde, ambapo alinasa kwenye matakataka yaliyokwama kwasababu ya mizizi ya miti na uzio wa seng’enge.

***********

Siku alichelewa kurudi nyumbani, na kilichomchelewesha ni ugomvi kati yake na mwanamke mwingine, mwanamke huyo alimfahamu kama mwizi wa mume wake, walianza kuzozana, na mzozo wao, ukazusha vita, na vita ikafikia kukatana na visu.

Na wakati huo mvua inanyesha lakini hakuna aliyekubali, kila mmoja alikuwa na hasira na mwenzake, mwenzake alionekana kuwa na nguvu, na kisu chake kilikuwa na makali, kwenye makali kuna ncha kama meno ya msumemo kwahiyo kila kikitua usoni mwake, kinamchana chana uso wake…

Hakuna mtu aliyewaamulia, wakawa wanaendelea kupigana na visu, na huyo mwanamke mwizi wa mume wake, akawa kila mara anapitisha kisu na kumkata usoni, alihisi uso wake ukikatika vipande vipande…na kujaa damu ningi hadi akahisi kupoteza damu nyingi alitamani watu waamulie, alkini hakuna aliyewajali

Cha ajabu jinsi alivyokuwa akikatwa usoni alikuwa anaona, ni kama vile mtu anayejiangalia kwenye kiyoo, na kila akijaribu kuzuia asikatwe, mkono nao unakatwa, akawa anashindwa ajizuie vipi, na yeye akijaribu kumkata mwenzake na hicho kisu chake, mkono wake haumfikii huyo mbaya wake.

‘Sasa na kuchinja kabisa, maana sura yako haifai kutazamamika kwenye jamii, wewe ni kama shetani , mchawi…’huyo mke mwenzake akawa anasema na akiongea sura yake inakuwa pana ya kutisha zaidi.

Mama akajua anapambana na shetani mtu asiyejali kuua, akatamani kukimmbia, lakini miguu ikawa haina nguvu, akajaribu kujitetea kwa kuomba msaada, lakini sauti ikawa haitoki, kisu kilicholenga kukata shingo yake kikawa kinakuja kwa kasi, kila akijaribu kusogeza kichwa kukikwepa ikawa inashindikana, akajua sasa nauwawa…

‘Oh mungu wangu nisaidie ili nisife ni hiki kiumbe tumboni..’akawa anasema kimoyo moyo, huku akili yake nyingine ikisema;

‘Wewe si mgumba tu utakuwa na kiumbe gani….’ Akataka kuinama chini ili atizame kama kweli ana kiumbe, ….oh, aliona tumbo lipo wazi, kubwaa, na dani hakuna kitu…

‘Oh….mtoto wangu yupo wapi…’akawa analia lakini sauti haitoki, na kumbe kule kuinama kwake kuangalia tumboni, ndio ikawa salama yake kisu kilicholengwa kukata shingo, kikapita kichwani na kukata nywele zake,

Akainua uso, na safari hii akiwa na hasira kuwa huyo mpinzani wake ndiye kamuibia mtoto wake tumboni, na alipoinua uso, akakiona kisu kingine, na kisu hicho kilikuwa kikubwa kama jamvia, kinakuja kwa kasi kummaliza, …akajua safari hakuna kusalimika.

Akawa , akajitutmia kujikunjwa,…ili kukwepa kisu hicho, oooh, kisu kikawa kimefika shingoni..tahamaki….ohooo.

Kumbe ilikuwa ni ndoto….mama akazindukana, na kujikuta akihema huku akitafuta pumzi, pumzi ilikuwa nzito, haawezi kuhema…

**********

Kutokana na maji ya mvua, na ubaridi, na ndoto mbaya ya kutaka kukutwa kichwa mama akazindukana, na giza nene lilikuwa limetanda, sauti zilizosikika na milio ya chura, kuashiria kuwa yupo maeneo ya maji,..na kweli ilikuwa usiku wa manane.

Mama alihisi maumivu ya mwili, japokuwa shemu nyingine za mwili zilikuwa kama sio zake, ni kama mwili ulikatwa vipande, na kila upande unajihisi kivyake. Akajaribu kujisogeza, akahisi maji,…ina maana yupo ndani ya maji.

Akatembeza mboni za macho yake huku na kule, japokuwa ilikuwa usiku, lakini alihisi macho yake kama hayaoni vyema, yanaona sura mbili mbili,..akatikisa mguu, akahisi maji,….mmh, kumbe nipo kwenye maji,…mvua imengia ndani, na huenda gododro limelowana.

 Akili yake ilikuwa haijakaa sawa, yeye alijua yupo ndani kwake, kumbe alikuwa pembeni ya maji, ambayo yalikuwa yakienda kwa kasi kuelekea bonde jingine. Akawa sehemu moja ya mwili ipo kwenye maji na sehemu nyingine kwenye mauchafu, makapi ya mpunga, lakini kwa wakati huo hakuwa anafahamu hivyo, alijua yupo kitandani na maji yameingia ndani…

Akili zikawa zinamjia kama ndoto, na kuona sura mbilimbili, alijaribu kufunua macho lakini yalikuwa mazito bila maelezo , lakini akili zilikuwa kama sio zake, alikuwa kama mfu…na alijihisi kama vile hana kiwiliwili kilichokubali kuinuka.

Mwili ulikuwa umekufa ganzi. Kitu ambacho alikuwa akihisi na kukisikia sana ni maumivu tumboni, na wakati anataka kujishika tumboni, alihisi kitu kina mlambalamba miguuni…mwili ukamsisimuka, alikuwa na uhakika huo ni ulimi, wenye mkwaruzo, ….ni kitu gani kinamlamba.

Akajaribu kuinua kichwa, laini kichwa kilikuwa kizito sana, aaliposikia tena kitu kikiendelea kumlamba, akainua kichwa nguvu, na akaona mnyama, nauoni wake ni mnyama, au wanyama wawili,wote wakiwa wameinamia mwili wake.
 ‘Oh, sasa naliwa mzima…sijui ni mzima au nis ehemu ya mwili ndio nzima…’akawa anasema kimoyo moyo.

Akajitahidi kuinua kichwa tena, kutizama ni wanyama gani, alikuwa ni myama mmoja, lakini macho yake yalikuwa yakileta sura mbili mbili, na ni kweli alikuwawepo myama, na mnyama huyo ni fisi.

Yeye alipoinua kichwa chake tena, akili ya harak haraka ikahisi ni mnyama mkubwa, na atakuwa ni simba, au mnyama mbaya, ambaye anakula nyama za watu…Mungu wangu. Alipohisi, hivyo mwili mzima, ukatetemeka, akawa sasa anasita hata kusogeza mwili, maana akianya hivyo huyo myama atamtafuta , au kumararua

Mama japokuwa akili yake haikuwa sawa, lakini hisi za uwoga zikamtawala, akawa anajiuliza ni aina gani ya mnyama kama yule,…ni lazima atakuwa nis simba, akasema sasa nimekwisha, kama ni simba, nahisi atanila mzima mzima, na nahisi keshanila sehemu ya mwili, kwa vile sehemu ya mwili ilikuwa kama sio yake.

Kwa mawazo yale, na hisio hizo, mwili ukaanza kufanya kazi kwa haraka, na zile sehemu zilizokuwa zimekufa ganzi zikaanza kusisimuka akaweza kukiinua kichwa na kumwangalia yule fisi ambaye yeye akili yake ilishamtambua kama simba, yule fisi alikuwa akilambalamba miguu na sijui kwanini alikuwa haumi..huenda alikuwa akilamba mabaki ya damu.

Woga ukamshika mama zaidi, na kujua kweli, nimeshaliwa miguuni, bado kiwiliwili cha juu, hapo akapata nguvu za ajabu za kujiinua, alijua kabisa na yule simba ambaye ni fisi akaonekana kushituka, akasogea hatua mbili nyuma….mama kuona vile, akajitutumua zaidi kuinuka, kila akijaribu aliona anazuiwa na tumbo.

‘Mbona nina tumbo kubwa...?’ akawa anajiuliza, akajiangalia tumboni,lakini hakuweza maana mgongo umekakamaa, hata kuinamisha kichwa inakuwa ni vigumu, lakini alihisi tumbo lake ni kubwa.

‘Oh, mbona tumbo ni kubwa hivyo, imekuwaje, ina maana nimevimba! Wazo la simba likawa limepotea, akawa anawaza kwanini tumbo lake limekuwa kubwa hivyo, na wakati anatafakari akainua uso na kumuona yule simba…oh,

‘Oh simba mungu wangu akakurupuka, na kujaribu kuinuka kwa haraka. Na hapo yule fisi akashituka, akajua kumbe huo aliozania ni mzoga kumbe ni mtu hai. Yule fisi akarudi kinyume nyume huku akitaka kugeuka kukimbia.

Mama naye kwa uwoga akawa anajitutumua huku akirudi kinyume nyume, huku akijaribu kuinuka vyema, lakini tumbo, …..

Kitu kingine alichokihis kuwa kuwa viungo vyake vilikuwa kama vimekufa ganzi.. Akamwangalia yule fisi ambaye alikuwa anageuka kwa woga, akitaka kukimbia, na mama naye uwoga wa kuwa yule ni simba, au dude linalikuwa watu ukawa unamwingia, kwahiyo alitaka kukimbia kujiokoa, angalau kusalimisha sehemu ya mwili anayohisi haijatafunwa na huyo simba.

Mama, akageuka upande mwingine, hutaamini kuwa huyo fisi hakumfanyia kitu chchote muda wote aliokuwa kalala pale chini, na sasa alipogundua kuwa huo sio mzogo, fisi huyo alishageuka na kuanza kukimbia, lakini mama akili na taswira zake zilikuwa sasa inaona simba, simba wa wajabu, yupo, anataka kumla…mama akajikakamua na kuinuka,akasimama na kuanza kujitutumua kikimbia.

Wakati anajitutumia kukimbia na fisi naye alikuwa kakimbia kivyake, lakini mama alihis kuna mnyama nyuma yake anamjia…kwahiyo akawa anavuta hatua akijitutumua kikimbia…alikuwa kama anajiburuza. Akilini alijua keshatafunwa nusu na nusu ya mwili imebakia, ndio maana sehemu nyingine ya mwili haina nguvu ya kujiinua,na tumbo limevima kwasababu ya kutafunwa.

Mama akawa anajikokota kukimbia.ilikuwa sio kazi rahisi, lakini kwasababu ya uwoga, na hisia kuwa nyuma yake yupo simba, akawa anajirusha, kukimbia kwa namna ya peke yake.

 Alijaribu kukimbia kwa shida, na kila alipofikiria ukali wa meno ya simba, akaona lazima ajitahidi kukimbia, na ile hali ya uwoga, kujitahidi, ikamsaidia kuchamgamsha mwili na sasa akaweza kuchechema, na kuondoka sehemu ile, kumbe muda ule alikuwa akitembea kuzunguka uzio, na kwa vile kulinyesha mvua, walinzi hawakupo karibu.

Kila muda ulivyopita ndivyo mama alivyoweza kupata nguvu za ajabu zilizochangiwa na uwoga wa kuliwa na simba ambaye kiukweli hakuwa ni simba alikuwa ni fisi akilini mwake yeye alijua kuwa ni simba ,akaongeza mwendo, lakini hakujua yupo wapi na  anaelekea wapi.

Mama, alichechemea hivyohivyo kwa shida sana, kwani tumbo lilikuwa likimuuma sana…mwili hauna nguvu, mgongo unakuwa kama umekaza hautaki kupinda….akawa anaambaa, ambaa na bonde hadi akatokea sehemu yenye uwazi, sehemu hiyo ilizoelewa na maji na uzio ukakatika.

Akatoka eneo la bonde na nje ya uzio ule wa seng’enge, na kwe mbele akaona nyumba zilizojengwa karibu sana na hilo bonde. Akashukuru mungu kuwa sasa atapata msaada. Akatizama nyuma, akiogopa kuwa yule simba atakuwa anamkaribia. Na kila akijaribu kugeuka shingo haukubali, ila akili yake ilikuwa bado inaona mnyama, na mnyama mwenyewe ni simba anamkaribia,

Kingine alichokuwa akihisi ni maji yalikuwa yakishuka toka milimani kwa kasi sana na sehemu ile ya bonde ilikuwa inazidi kujaa maji, kuashiria kuwa akichelewa kidogo, atamezwa na maji, hayo yote yalimsaidia kujitahidi kukimbia japo, kukimbia kwenyewe ilikuwa kama kuchechemea.


Bahati nzuri nyumba mojawapo iliyopo karibu na hilo bonde ni ya mama mmoja mtaalamu wa ukunga wa jadi, anajulikana sana pale kijijini. Mama huyu hakutambua kuwa nyumba hiyo anayoelekea kwa muda huo ni nyuma ya mtalaamu huyo, alipofika akagonga mlango huku akitaka kugeuka nyuma kuangalia kama huyo simba yupo karibu na ile taswira ya mnyama bado ilikuwa kichwani mwake.

Kwa muda huo mvua ilikuwa imetulia, lakini wananchi wengi walikuwa bado wamelala. Aliyefungua mlango alikuwa mama huyo wa jadi, mama huyo wa ukunga wa jadi alipomuona huyu mtu aliyesimama mlangoni mwake akarudi nyuma kwa hofu huku kashikilia mdomo, akitaka kupiga yowe

Mtu gani huyo alikuwa hana sura, ..uso umevimba, hata macho hayaonekani, ni kama dude lenye kichwa na matundu ya macho, kifuani kumelowana damu, mama huyo akajua ni shetani mla watu…..akataka kupiaga yowe…lakini aliposhusha macho tumbono akashangaa mtu huyo ni mja mnzito, au shetani limeshiba nyama za watu….

 Japokuwa mama huyu mkunga ana ujasiri, kazoea kucheza na damu za watu, lakini sura aliyoiona mbele yake ilimtisha sana akataka kufunga mlango kwa haraka, lakini mama alishaingiza mguu mmoja ndani na alikuwa sasa anayumba yumba akitaka kudondoka.

Yule mama mkunga akataka kupiga yowe la msaada ili kibidi mume wake aje, lakini kabla hajafanya hivyo, huyo mama akayumba na akawa sasa antaka kudondokea ndani kilichokuwa kimemzuia ni huo mlango……mama mkunga akawa bado kashikilia mlango, akili ikawa inashindwa kuamau afanye nini, na hapo akawa kachelewa.........

Nb: Inatisha eeh

WAZO LA LEO: Jukumu la kulea watoto, kutunza vijana wa taifa hili ni kwa wazazi wote, kama jamii, itakuwa inalizarau hili, ikawa ni kila mtu kivyake-vyake, asilimia kubwa ya taifa hili itakuwa kwenye giza. Sasa hivi kunazuka vurumai kila mahali, na ukiangalia wengi wanaofanya hivyo ni vijana, hawana muelekeo, wameshakata tamaa …wanaona taifa kama mzazi wao limewatupa, wasimamizi wanajijali wenyewe, wao wakipata nafasi wanajichotea mapesa tu.

 Tujiulize hili kundi kubwa lisilo na waheshimiwa wakuchota mapesa litakwenda wapi…ndio maana sasa mnaona `panya road’, hatujui baadaye kutazuka nini.

Juhudi za makusudi zinahitajika, kuangalia jins gani ya kuwekeza nguvu rasilimali hii, badala ya kuiacha itanga tange yenyewe.Tunaweza kutumia JKT, kama sehemu mojawapo ya kuwaendeleza hawa vijana,…hili liwekwe kwenye katiba kuwa kila kijana asiye na ajira, ajiunge  JKT…badala ya kuwachukua tu wasomi ambao wameshakuwa na muelekeo fulani.

 JKT, ikishirikiana na VETA, inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwawekeza hawa vijana, kwanza wajengwe kinidhamu na hili linawezekana ndani ya JKT, na baadaye wakiiva, wanapimwa vipaji vyao hili linawezekana ndani ya VETA,maana kila mwanadamualivyo ana kipaji chake, cha muhimu ni kukifufua tu na kukiendeleza kitaalamu, na wakitoka hapo kila mmoja anaweza kujiajiri. Ni wazo tu kwa leo.


Ni mimi: emu-three

No comments :