‘Tumeua……’wakasema kwa pamoja mume mtu na mkewe, huku wakimuangalia mama akiwa kalala kwenye miba, uso hautambulikani, ni damu tupu...
‘Hili
sasa tatizo, ……’akasema mume akionyesha wasiwasi baada ya hasira kumuisha, akawa anapikicha macho kama haamini vile, mkewe alipoona hivyo akamshika mumewe bega na kujigemeza kimtindo.
‘Ni
kuambie kitu mume wangu, huyu keshakufa, cha muhimu tukamtupe huko mabondeni, ataliwa na
fisi ……na hakuna atakayejua kuwa ni sisi tumemuua...’akasema mke wake huyo huku akimtupia jicho mumewe la pembeni.
Mume
bila kufikiri akaona ni wazo zuri,...akaangalia huku na kule, na kwa vile giza lilishaanza kuingia
hakukuwa na watu wakipita, au kushuhudia hilo tukio, na kwanza watu walishachoka kuamua ugomvi kwenye nyumba hiyo, kwahiyo hata wakisikia kelele, hawasumbuki tena.
Watu wawili hawa kwa pamoja
wakambeba mama, kwa kushirikiana, ilikuwa kazi kumtoa kwenye zile kuni zenye miba, na ukizingatia kuwa mama alikuwa mja mzito, basi na uzito wake ulikuwa mkubwa.
Hawakujali, akuhurumia wakati wanamtoa, miba ikazidi kumchana hata nguo zikawa ni kambakamba tu..wakamtoa pale na kuanza kumbeba kuelekea bondeni
Ili kurahisisha hiyo kazi hapo nyumbani kulikuwa na torolo la kubebea mizigo, wakampakia hapo na kuanza kulisukuma hilo torili, wakiwa wamefunika, kwahiyo hata kama mtu angeliwaona angelijua wamebeba gunia la taka, wanakwenda kutupa bondeni.
Walifanya haraka wakafika kwenye hilo bdone na kumtupia mama.....
Je mama keshakufa, au
ilikuwaje, tuendelee na kisa chetu
****************
`Wewe ndio umemuua mke
mwenzako, …’akasema mume mtu wakati wakirudi nyumbani.
‘Nyamaza bhana watu
watatusikia,….’akasema mke mdogo akionyesha wasiwasi kwa kuangalia huku na huku.
‘Mungu wangu, ina maana
mke wangu kweli ameshamekufa…’ akawa analalamika baba bila kujali onyo la
mwenzake.
‘Sikiliza mimi nipo
nitakuzalia watoto, cha muhimu ni sisi kuhangaika, tutakwenda kwa mganga atairejesha nyota yangu,
maana mchawi wetu ameshaondoka una shaka gani tena…’akasema mke mtu.
‘Mhh, tatizoo lako
huelewi, ….’akasema na huku akikuna kichwa kwa kasi
Bwana alikuwa kama
kachanganyikiwa, akawa anashika kichwa, mara anaruka ruka, na mke mdogo
akimsogelea yeye anamsukuma, na hali hiyo iliendelea hadi wakaenda kulala.
Usiku ulikuwa wa maruerue
kwa bwana mtu, hakuweza kulala, kila akijaribu kupata usingizi, anajikuta
akiota ndoto za kutisha, mara anatokewa na mke wake, kwa maumbo toauti ya
kutisha, akiwa kalowana damu au kicha kimekatika, ….na wakati mwingine anamuona
mke wake mdogo akimjia na kisu kuwa anataka kumuua na yeye….akashituka na kukaa
kitandani
Aalikaa kwa muda, huku
akitafakari, akaona hakulaliki, akaretemka kutoka kitandani na kutembea hadi
eneo la dirisha la pili, akasmama hapo kwa muda baadaye akageuka kumuangalia
mke wake mdogo ambaye alikuwa kalala fofo alikuwa anakoroma usingizini bila
wasiwasi.
Mke wake mdogo alimuoa
akijua atatatua tatizo la kupata mtoto, na hilo alilifanya baada ya kupata
ushauri kwa watu na pia baada ya kumuendea mganga wake anayemuamini….lakini
matokeo yake ndio hayo.
Akazidi kumuangalia mke
wake mdogo ambaye bado alikuwa usingizini, na hakuonekana kuwa na wasiwasi,
akamlinganisha na mke wake mkubwa, akakumbuka siku alipomoa mke wake kubwa,
baada ya kutoa ng’ombe wengi, na ilikuwa kazi kumpata….sasa ndio huyo
ameshakufa, akashindwa kujizuia, machozi yakamtoka.
Alisimama pale kwa muda,
akishindwa kujua afanye nini, na mara akakumbuka jambo, akageuka, na kutoka
chumbani na kuelekea sebuleni, huko akaangalia pembeni ya kabati anapoweka
kinywaji chake, akaikuta chupa ina chochote kitu, akapiga mafundo matatu ya
harakaharaka, alikunywa kwa harakaharaka, na kujikuta akikohoa mfululizo.
Kikohozi kilipokwisha
akakaa kwenye kiti na kutuliza kichwa, na huku gongo likifanya kazi yake.
Akajipa moyo, kuwa kama kaua nani atajua, kama ikibidi ataoa mke mwingine…
‘Lakini mimi sikutaka afe,
mbona kila siku ninampiga, tena sana, zaidi ya kipigo hiki, lakini hakuwahi
kufa….aaaah,hili eeeh, lazima kuna sababu….’akasema na kuinua chupa, akagundua
haina kitu akainua juu nakujaribu kumimina yakadondoka matone mawili.
‘Mhh, …..nani kamaliza
pombe yangu…’akasema na kuitupa hio chupa pembeni. Akakumbuka kitu na kuinuka pale
alipokuwa kachuchumaa,na kwa akaelekea chumbani.
Alipofika chumbani akakuta
mke wake kalala vile vile, ila sasa kaelekeza kichwa juu, akikoroma
‘Wewe mwanamke, nimeshajua
kuwa , ulipanga uje hapa ili umuue mwenzako…’ akasema na mwenzake alikuwa kimia
akiendelea kukoroma.
‘Hunisikii, unanizarau
eeh, yaani mimi naongea wewe unaendelea kunywa
uji,..koroo-koroo….nitakubamiza…’akasema na kugonga kitanda kwa mguu, na kwa
kufanya hivyo akajigonga ugoko, na kupata mauimvu, akainama kujishika kwa
hasira.
‘Mhh, ….sasa utanitambua…maana
siku zote naishi na mwenzako hapa, tunapigana, hafi , sasa umekuja hapa kwa nia
ya kumsaidia kumbe ulikuwa na lako jambo, na umesababisha mwenzako kufa, sasa
na wewe hulali, dawa ya muuaji na yeye ni kuuliwa…’ aliposema hivyo akasogea
pale alipolala mke wake mdogo na kulivuta shuka kwa nguvu.
Mke akawa analalamika
usingizini, akageuka upande wa pili, na jamaa kuona hivyo akaona kama
kazarauliwa akaanza kumpiga mangumi,….akarusha teke kama kawaida yake na badala
ya kumpiga mtu akawa anajigonga kitandani, na alipopata maumivu, hasira
zikazidi kumpanda.
Mkewe mdogo akawa sasa
kashituka kutoka usingizi, akakaa vyema kitandani.
‘Kwani kuna nini tena….?’
Akauliza bado akiwa anapiga miayo.
‘Kuna nini tena…wewe ni
muuaji, …..yaani mimi nashindwa kulala, wewe unakoroma,…’akasema
‘Sasa nianyeje , usiku
maana yake ni nini, mbona …..unanipiaga, tulale bwana….’akasema akijaribu
kujilaza, na bwana mtu akamfuata pale na kuanza kumzaba vibao.
‘Mungu wangu,…mbona
unanipiga…’akasema na kuinuka pale kitandani, tayari kwa kupambana alishajua
kuwa kuna shari, na yeye kwa shari hajivungi, kwani na yeye sio mtu wa kukubali
kuonewa akajiweka sawa na kumwangalia mume wake anataka kufanya nini.
‘Hivi wewe una akili
sawasawa, usiku kama huu unataka kuleta fujo, nani kaua, situmekubaliana tukae
kimya, ukianza fujo hapa huoni majirani watajua…’ akasema huku anasogea mbali
na mume wake.
Kabla hajatulia vyema
akaisikia kibao kikipiga nyuma ya shingo, alishangaa jinsi mume wake alivyokuwa
mwepesi kiasi kile, ule umbali aliosimama, hakuzani kuwa mume wake angeweza
kuruka na kumzaba kibao cha haraharaka, akapepesuka, na yeye hakukubali akageuka
na kurusha ngumi ikampiga mumewe puani, akaishia kusikia maumivu yeye mwenyewe
na kuupuliza mkono wake.
‘Unajifanya unajua
kupigana sio, ngoja sasa na wewe uione njia aliyoondokea mwenzako..’ kabla mke
hajajibu kitu, akawa kavamiwa, na kipigo alichokipata ilikuwa kama yeye ni
gunia tu, sio binadamu. Mume alipotulia kupiga, kwasababu aliona mke hajibu
mashambulio, akamuachia, na mke huyo akadondoka kitandani…kimya,
‘Nimeua tena…..’akasema
kimoyo moyo
Hee vipi tena, wewe
ulikuwa unajifanya mwamba, mbona kipigo kidogo umelegea, kumbe hamna lolote,
alizoea mke mkubwa ulikua akipiga , na kupiga, lakini , mtu yupo pale pale,
sasa huyu kagusa kidogo, …oh, akatizama chini pale alipodondoka mkewe kwa woga,
huku akili ikisema ‘nimeua tena..’
. Akamtikisa mkewe,
akamuona kakauka kimiyaaa, akatikisa kichwa kuondoa mawimbi ya pombe, akasimama
huku akishika kichwa….
‘Huu mkosi…..’akasema, na
kugeuka, akarudi sebuleni, akatafuta ile chupa, akaiona,akaweka mdomoni, hakuna
kitu…
Kwa hasira akaibamiza ile
chupa ukutani…., akaanza kukohoa mfululizo, huku akisema akilini , mbona siku
hizi nakohoa namna hii, kuna sababu. Akakaa kwenye kiti chake na kutulia..haikuchukua
muda usingizi ukamchukua ghafla….
Hakujua alilala pale muda
gani, kwani alijikuta shingo inamuuma kwa kuegemea upande mmoja, na bega ,
akajaribu kuinuka kujinyosha, akaona kichwa kinamgonga, maumivu ya kichwa…na
dawa yake ni kuzimua
Akasimama akiyumba
yumba,akasogea pale anapoweka chupa yake, akakuta haipo. Akatuliza kichwa
kufikiria nini kimetokea, na kwanini kalala pale kwenye kiti. Akaanza kukumbuka
kwa mbali , japo kidogo, matukio ya jana, akakumbuka kuwa alikuwa na kazi ya
kumalizia chumbani, akaita jina la mke wake wa kwanza, akaona kimya, akaita
tena kimya.
‘Hivi nipo wapi,….mke
wangu namuita hanitiki…..’akasema akitembea kuelekea chumbani.
Alipofika chumbani ,
akakuta kitanda kipo shaghala baghala na shuka, hata godoro lipo chini, akaangalia
pale alipokuwa kalala mke mdogo, akaona shuka limefunika kitu, akajua ni mke
wake mdogo kalala, na kwanza akasimama.
‘Wewe umeuata nini
huku…..’akakumbuka akatikisa kichwa,
‘Ohoo, wewe jana
ulijifanya bondoa, nikakupiga moja tu, nikakutoa knock-out….sasa sijui na wewe
umekua au, kwanini toka jana hujaweza kuinuka..’akasema.
Akasogea pale kitandani
akainama kumtaka kutoa lile shuka, lakini
Kabla hajafanya hivyo,
akasikia sauti za watu kwa mbali, akaona sasa kama wanakuja humo kwake
atashindwa la kujitetea.
‘Hili sasa ni balaa….huyu
naye atakuwa amekufa…hao watu wanakuja hapa…ohooo….’akasema akageuka na
kuangalia dirisha, akatikisa kichwa
‘Hapa ni kukimbia
tu….’akasema, na akageuka kwa haraka akaliendelea kabati anapoficha salio lake,
akakuta bado lipo,akachukua baadhi ya nguo zake na kuzifutika kwenye mfuko, halafu akaelekea mlangoni.
Akasikia watu wameshafika
eneo la numba yake, wanaongea, na moja ya sauti aliyoiskia ni ya
mjumbe,…akageuka, na kuelekea dirishani, hakupoteza muda, akapanda dirishani na
kwa haraka akarukia nje, na wakati anaruka akasikia jina lake likitwa kwa nje.
Hakusubiri…..taratibu
akachekupa njia inayoelekea vichakani. Mkononi alikuwa na kifurushi kidogo cha
nguo na rungu lake la dharura.
‘Duuh, ina maana nimeua
wake zangu wote wawili nitaenda wapi leo. Akaongoza njia ya porini, akikusudia
kukimbilia kijiji cha karibuni, halafu atatafuta usafiri na kwenda kokote,
mbali kabisa wasipomjua.
Alihakikisha kachukua
akiba yake ya pesa na vitu vya kumsaidia njiani, na wakati anaingia njia ya
uchochoroni, kwenye kimsitu kidogo, akasikia sauti nyuma, akajibanza pembeni ya
mti na kuangalia wapi sauti inatokea asubihi hii. Kwa mbele akaona kikundi cha
watu wanne, akajaribu kuwatizama vyema ajue ni akina nani na nani. Ajabu akaona
wanelekea kwake. …
Aliyetangulia hakumuona
vyema, lakini alionekana ni mtu wa makamo, ila aliyekuwa karibu naye,
alionekana mrefu, na pande la jitu, mkononi kashika rungu. Mungu wangu ni
nanihii…oooh, shemeji yake….
‘Mhh, shemeji
huyo,….’akasema ni kweli alikuwa kaka wa mke mdogo. Mtu kama yule utamjua
popote alipo, kwa umbo na ushari wake. Alianza kutetemeka kwa woga, licha ya
kuwa yupo mbali na wao. Huyu shemji yake ni kiboko wa kijiji, anaogopewa kama
simba, akakumbuka kauli yake siku anamuoa dada yake.
‘Oya, umekubali kumuoa
dada yangu kwa hiari yako mwenyewe, ole wako nisikie umemtoa damu, najua kupiga
kidogo sio mbaya, lakini umtoe damu…umvimbishe mahala, … utakumbukwa hapa
kijijini..’hiy ilikuwa suti ya njemba hilo.
‘Usijali shemeji siwezi
kumtoa damu, nampenda sana dada yako….’akamwambia.
‘ Dada yangu nampenda
sana, na kama wewe unampenda kama ninavyompenda mimi, ukae naye kwa salama na
amani, la sivyo, watakuhadithia jinsi maiti yako itakavyoharibika sura…’
akampiga na kiwiko cha mkono ubavuni, maumivu aliyoyapata siku ile bado
anayakumbuka hadi leo. Anakumbuka alikaa wiki nzima kila akihema anasikia hayo
maumivu…
Akawa anawaangalia wale
watu hadi walipofika nyumbani kwake, na wakakutana na kundi lile la mwanzo,
ambapo alikuwepo mjumbe. Walikuwa wanagonga mlangoni, na kwa vile mlang
ulifungwa kwa ndani hawakuweza kufungua, na sauti ya shemeji yake ikasema;
‘Vunja mlango huo, haina
haja ya kupiga hodi…’ akasikia sauti ya shemeji yake akitoa amri.
Alinekana mjumbe kama
hakubaliani na hilo wazo lakini yule shemeji mtu hakusubiri, akajirusha na
alichosikia ni kishindo cha mlango wake ukivunjwa.
‘Wameshanitia hasara ya
mlango….lakini sio muhimu kwa sasa….’akasema pale alipojificha.
Pale kwenye lile kundi alimuona
mwanamke. Akajaribu kutizama vyema, na kugundua kuwa mwanamke yule anafanana
sana na mke wake mdogo. Akajiuliza ni mke wake mdogo au ni mdogo wa mke wake,
kwani mke wake na mdogo wake wanafanana sana.
Lakini akakumbuka kuwa, mke wake alikuwa kitandani
hadi wakati anaruka dirisha kukimbia, mke wale alikuwa kafa usiku, haiwezekani
awe ndiye yeye, …akajaribu kutizama kwa uangalifu, lakini ule umbali na majani
ya miti hayakuweza kumsaidia kuona vizuri. Inawezekanaje ndugu zake wajue
kilichotokea, inawezekana kuwa mke wake huyo mdogo hakufa, na alikimbia kwao
kutoa taarifa kuwa kapigwa…
‘Haiwezekani…’akasema
akijaribu kutafakari, akajaribu kukumbuka matukio ya jana baada ya kumpiga mke
mdogo, akajua keshaua, akaenda varandani akitafuta kinywaji, akakuta hakipo,
akavunja chupa…akakumbuka kuna muda aliamuka kwenye kiti…akitaka kujisaidia,
….akatoka nje na kujisaidia mlangoni, hakuenda mbali….
‘Mimi nilifungua mlango
kweli au ulikuwa upo wazi…?” akajiuliza
‘Nakumbuka ….kweli nilifunga
mlango vyema nilipoingia, ila wakati natoka, mlango …..mmmh, wakati natoka
sikumbuki mlango nilifunguaje….’akawa anawaza lakini hakupata jibu.
‘Sikumbuki kabisa kumuona
mke akitoka, kwanza mfu, angetokaje…..aaah,kichwa kinauma’akawa anawaza.
‘Aaah hilo sio muhimu kwa
sasa,…..yule mwanamke atakuwa ni dada yake maana dada yake ni mshari kama
alivyo ndugu yake, kaja kushabikia tu, akijua kaka yake yupo…’akasema
Mara akasikia sauti, wale
jamaa walioingia ndani kwake, walikuwa wametoka nje….hawakuwa na kitu chochote,
alitarajia angeliona wamebaba mwili,au wanasubiri polis wafike….akata kusikia
lolote kuhusu mke wake, lakini hakusikia kitu kama hicho, alichoskikia ni…;
‘Huyu mfu mtarajiwa hayupo
humu ndani, katoroka, tumtafuteni , hajaondoka mbali huyu…’, akasikia sauti ya
shemeji yake ikitoa amri. Na aliposikia hivyo kuwa yeye sasa ni ‘mfu mtarajiwa’
hapo akaona asipoteze muda akaingia msituni na kuanza kukimbia….
**************
Hebu sasa turudi kwa mama
yangu, unakumbuka alitupwa kwenye bonde, je yupo hai…ukumbuke bonde alipotupwa
mama sio bonde dogo, limekuwa likichimbika kwa mvua za mara kwa mara, kwahiyo
limeenda ndani sana. , lilikuwa kubwa.
Hilo bonde mara kwa mara
kipindi cha mvua wanakijiji wamekuwa wakilitumia kulima mpunga. Baba na mke
mdogo wao walipomfikisha hapo, walijua kuwa wameshaua. Kwa muda ule wao
walikuwa wanajua kuwa wamebeba mzoga, kwahiyo walimtupa tu kama gunia, na mama
aliserereka kuelekea chini kwa kubingilika kama gunia hadi chini ya bonde, na
kutua kwenye lundo la majani ya mpunga.
NB:
Tutaendelea sehemu ijayo
WAZO LA LEO: Kuna watu huwa wanapenda kuchukua sheria mikononi mwao, …kupiga,
kuua, kwao ni jambo la kawaida bila kujali sheria.
Kuna
matuko kadhaa watu wameuwawa, wakidhaniwa kuwa ni wezi, baadaye inakuja
kugundulikana kuwa hao waliouwawa hawakuwa wezi, hawakuwa wachawi nk…waliokuwa
wezi waliwahi kukimbia, au hao waliodhaniwa kuwa ni wachawi ni uwongo wa mganga
wa kienyeji.
Hebu jiulize wewe uliyeshabikia, au kutenda
kosa kama hilo la kupiga hadi mtu akafa, utakuja kusema nini mbele ya mungu…,
kuwa eti ni `bahati mbaya’ ya bwanawakubwa ambao wakiua husema ni Bahati mbaya…..tusihukumu
kabla sheria haijasema hivyo…hilo ni kosa kubwa.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment