Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, January 6, 2015

NANI KAMA MAMA-14


‘Kakuambia nini....’mume mtu akauliza kwa hasira

‘Kasema kuwa yote hayo ya wewe kutokuzaa, anayafahamu....’akasema mke mdogo

‘Anayafahamu kwa vipi?’ akauliza mume mtu kwa sauti ya juu.

‘Anafahamu kuwa wewe huzai,  na….na amefanya hivyo kwa kiherehere chako cha kutaka kuoa mke mwingine...’akasema mke mdogo.

‘Mimi sizai, ....nani kasema mimi sizai?’ akaulize mume kwa jaziba

‘Alianiambia kakufanya wewe usizae,...kwa vile umetaka kuoa mke mwingine...kwa jinsi alivyofanya ni kuwa wewe hutaweza kuzaa tena, ndio maana akaenda kutembea na mume mwingine…’akasema mke mdogo bila kuogopa, na mume akawa kama kapigwa na shoti ya umeme, akasema.

‘Na hiyo ni siri ya yeye na rafiki yako.....kama utambana vizuri rafiki yako atakuambia..kwani yeye kafanya kama kukusaidia, usiadhirike...’akazidi kusema.

‘Nini amesema nini,....kakumbia hivyo huyu mwanamke...? ‘akauliza sasa akimgeukia mama

‘Hebu niambie wewe mwanamke unanitaka nini mimi, kumbe yote hayo sababu ni wewe,.....na ndio maana ukakimbilia hospitalini ili kubadilisha ukweli, ionekane kuwa tumevunja masharti...nimelewa....’akatikisa kichwa

‘Kwahiyo sasa unaongea kwa kujiamini, unamsimulia mwenzako kwa vile una uhakika kuwa wewe unazaa, wewe sio mgumba tena, na mimi umeshaniharibu, ili nisizae, eeh, ...hata nikikuacha huna hasara au sio…’akasema akimuangalia mke mkubwa kwa hasira.

‘Mume wangu, si-sio...’akawa anashindwa kuongea

‘Ndio hayo aliyoniambia, ni kweli si kweli haya mwambia na mume wako, je hukuniambia hivyo....?’ akauliza mke mdogo na mama alijikuta hawezi kutamka neno, ilikuwa kama kapigwa sindano ya ganzi.

Mume akawa anamwangalia mama asema neno, lakini mama akawa hawezi hata kutamka neno, pumzi ilikuwa haitoki, alikuwa akisikia vibaya..., na kwa kukaa kwake kimia, mume mtu akaamini ni kweli…’ na kabla mama hajarejewa na fahamu na kuanza kujitetea baba akaingia ndani….

Mke mdogo akamuangalia mwenzake kwa zarau, akasema;

‘Unaona umelitaka mwenyewe kwa umbea wako...’akasema mke mdogo huku mama akiwa kashikwa na butwaa, hasira, na akahisi kama mwili unamuishia nguvu, alikuwa akijisikia vibaya...akasimama na kuanza kutoka nje....

Tuendelee na kisa chetu

**********


Mama anamfahamu sana mume wake na alijua ni nini kitafuata baada ya hapo, hata hivyo hakuwa na la kufanya maana kwa jinsi alivyokuwa akijisikia, hakujali kingine tena, akakusanya nguvu, na kuinua mguu taratabu kutoka nje, kwani alihisi kama kutapika, kiuno kinamuuma kweli, hata kuinua mguu ilikuwa shida...

Baadaye kidogo hali ikawa nzuri, maumivu na ile hali mbaya ikampungua, akainua mguu, akaona unakubali , na kwa mwendo wa kunyata akatoka nje, huku mwenzake akimuangalia kwa kumsanifu, aliona kama mke mwenzake anaigiza

‘Hahaha ndio mwendo wa kichawi huo, unaanza kuwanga mchana…’mke mwenzake akasema huku akiendelea kumuangalia kwa makini.

Mama alipofika nje akakaa kwenye kigogo kilichopo hapo nje, huwa wanakitumia kama kiti, akatulia kidogo maana pumzi ilikuwa nzito, alitulia kidogo hadi pumzi ilipomkaa vyema, akawa sasa anaanza kufikiri la kuanya, hasa mume wake akitoka, aliwaza hivyo akiwa kainama….alijua kwa vyovyote kuna kupigwa hapo, naolote kutokea, mara akahisi hayupo peke yake, akainua kichwa kuangalia.
                                                                              
Mke mwenzake alikuwa kasimama mbele yake huku kashika kiuno kwa nyodo, hakujali kuwa mwenzake yupo katika hali gani, akaanza kuongea;

‘Hahaha nguvu zote z kichwawi leo zimegonga mwamba, hahaha, ungejiona ulivyokuwa ukitembea utafikiri roboti, ndivyo wachawi wanavyotembea hivyo ehe….’akasema na kucheka

Mama hakumjibu akawa kimiya akiwaza yake, lakini moyoni alitamani amtapikie huyo mtu,…..

‘Mhh, nambie mbona umekimbia, kwanini hukusubiri upambane na mume wako, wewe si unajifanya unajua kuongea, wewe umeanza  kwa kunichongea kuwa mimi sifanyi kazi,eeh, vikapanda vikashuka, ...ulifikiri mimi nitashindwa kujitetea, sasa umelikoroga mwenyewe....utakiona cha mtema kuni…’akasema huku akichezesha chezesha kiuno kwa mapozi ya nyodo.

Mama aliendelea kukaa kimiya hakumjibu, na mke wenza akaona hafaidi, maana kazoea kujibishana, akamsogelea mama pale alipoinama, na akaongea kwa sauti ya chini.

‘Jamaa anakuja na bakora na rungu, anakutafuta, alivyokasirika, sijawahi kuona,...sasa wewe si ulitaka kuondoka,...huu ndio muda wa kuondoka maana akitoka hapa uchawi wako wote utautoa, na huko ndani kwako alipoingia kagundua mambo yako mengine, kumbe kuna mambo yako unaficha huko ndani ehee....’akasema mke mdogo.

‘Mambo gani,....?’ mama sasa akainua kichwa na kumuangalia mke mwenza, na alishangaakuona mume hatoki, ni muda kaingia huko ndani.

‘Ulifikiri hutagundulikana eehe....’akasema mke mdogo, na mama akawa anamuangalia kwa macho yaliyochoka, hakuwa na hata nguvu ya kujibishana.

‘Hivi wewe mwanamke unanitaka nini mimi, nimekukaribisha kwa mikono yangu miwili kwa wema,  nikijua utampatia mume kile anachokitaka....mtoto, sasa...jamani hebu niacheni mngelijua hali niliyo nayo mungenihurumia…’akasema mama kwa sauti ya kinyonge.

‘Hahaha, mtoto,… mtoto eeh, wakati unafahamu fika kuwa umeshafunga njia ya mimi kupata mtoto na mume wangu, umeichukua nyota yangu ukaimeza, ili wewe uzae, mimi ndiye niliyetakiwa kuzaa, na kutokana na mimi ndio na wewe upate mimba, sasa....sasa unasema eti umenikaribisha, ili nimpatie mume mtoto... acha unafiki wako wewe...’akasema mke mdogo.

Mama akawa anamuangalia huyo mke mwenza kwa macho ya kushangaa, huku mwenzake akiwa kashika kiuno akijichezesha kwa mikogo, mama akasema;

‘Hivi wewe kweli umekwenda shule, nasikia ulisoma sekondari,..hivi kweli wewe una dini kweli wewe, nilisikia mume akisema wewe ni mcha mungu, haaah, siamini...’akasema mama

‘Huamini nini, kusoma kwangu, ucha mungu wangu haukuhusu,….muhimu ni uchawi wako….’akasema

‘Wewe mwanamke….ni nini lengo lako, hebu niambia mara moja, ina maana gani kunifanyia hivi, unanipakazia uwongo kuwa mimi ni mchawi, sijui nimekuloga usizae, sijui nimemloga mume wangu asizae, kwanini unakuwa Mwongo kiasi hicho,...?’ akauliza mama

‘Kwani ni uwongo, kwani wewe sio mchawi,...ngoja mume aje akuonyeshe ndumba zako, wewe ni mchawi hata mganga alisema hivyo, usitake kujishaua hapa, sasa nataka nikuonyeshe kuwa mimi ni nani,….mimi namtambua mchawi hata kama akijificha vipi, siri zako zote nimeshazifahamu, huna ujanja tena, lakini kabla hujaondoka, nataka nikupe vipande vyako .....’akasema

‘Vipande gani, matusi na kashifa zako nimeshazisikia una mengine zaidi ya hayo…?’ akauliza mama.

‘Nataka uijue hii sura, unijue kuwa mimi ni nani na hata ukikutana na mimi ujipange vyema, unasikia, huyu binti sio waleee…..unaona eeeh, hebu iangalie hii shepu, mume kazimia hapa, na hayo mengine usiombe, hahahaha….mwenamke ovyo….’akashika pua

‘Hivi wewe mwanamke nia na lengo lako ni nini…kwakweli wewe sio binadamu, wewe ni shetani mchonganishi tu umeolewa kwenye familia hii kuja kuangamiza ndoa za wenzako, nikuambie ukweli, wewe ni wakala wa shetani.....’akasema mama sasa na yeye akipandisha hasira

‘Ndoa za wenzako!!, kwanini mimi sio mwanandoa,huyo mume kanioa mimi baada ya kuona udhaifu wako, kwanza hujui mapenzi...mke gani hata kujiremba hujui,hebu jiangalie.., pili ulikuwa huzai, mume akaona achukue chomb kipya..mmh, kumbe kanichanganya na mwanga…ukani…loga….’akasema kwa kusita aliposikia mlango ukifungulia.

‘Na jingine ambalo mume alikuwa halijui ni kuwa wewe ni mchawi, halafu unaniita mimi shetani,  wewe ndiye shetani mchawi mkubwa wewe’ akasema kwa sauti.

‘Wewe binti, chunga ulimi wako....’akasema mama akimnyoshea kidole

‘Wewe ndiye umetaka mimi nisizae ili wewe uonekane zaidi, umeona mimi ni mzuri zaidi yako,basi unataka nisiwe na maana, sasa utaikimbia hii ndoa, maana kwetu nimeaga bibi wewe, na naweza kukufanya lolote na mume akanisikiliza mimi...’akasema mke mdogo akipiganisha viganja vya mikono.

‘Yaani lengo lako ndio hilo, kuleta fitina, umekwenda huko kwa mganga kawadanganya, binti mdogo kama wewe unaendekeza ushirikina, badala ya kufikiria maendeleo, ni nani kakuambia wewe huzai, ...angalia mimi walisema sizai, mbona nimezaa, hiyo ni mitihani tu,kwanini usiende hospitalini ukajichunguza kwanza.....’akasema  mama

‘Hospitali,…kumbe …aah, ndio mliongozana na mzazi mwenza, ili kuhakikisha mambo yameiva, na unarudi kumbambikia mume …hahaha, wenzko hayo tulishayaona mapema,…..’akasema

‘Mimi nakushauri kwa nia njema, mume wetu hana matatizo, nenda ukapime uone tatizo liko wapi, achana na ushirikina,….mbona mimi nimepata mimba, huoni kuwa hao waganga wamewadanganya…..’akasema mama kwa shida, kuna hali ilikuwa aikimjia na kuondoka.

‘Wewe si umezaa kwa kuzini, kwa kutembea na rafiki wa mume wako, unafikiri mimi sijui yote mliyokuwa mkifanya na huyo mwanaume nilikuwa nayaona yote, siku ya zamu yangu unamkaribisha hawara wako kwa siri kweli si kweli, yote hayo nilikuwa nayaona,... sikutaka kumuambia mume wetu mapema, sasa yeye mwenyewe kajionea,....mwanamke malaya wewe.....’akasema.na mama kusikia kauli hiyo hasira ikamjaa

‘Yaani wewe binti unazidi kunichefua, siwezi kuvumilia hayo matusi yako tena,  ....sasa kama umefikia hapo, sikubali, umeniita mchawi , bado haitoshi, unaniita malaya, huo umalaya umejulia wapi kama sio tabia yako....kama hujafundishwa adabu kwenu leo mimi nitakufundisha adabu....’mama akasema kwa hasira alipoona hali imetangamaa, akasimama

‘Thubutu, hebu niguse uone, wazazi wangu wenyewe hawajawahi kunipiga wewe ...hebu niachie...nita.....’akawa anausukuma mkono wa mama huku akijifungwa kibwebwe tayari kwa shari, inaonekana shari kwa huyu binti ndio fani yake.

 Mama mtu hakuvumilia, akamshika yule binti bila kujali hali yake wakaanza kupigana, yule binti ni kama alijiandaa, akaanza kumpiga mama, kwa ngumi na mateke, na mateke yake aliyaelekeza tumboni kwa mama, hakujali kuwa mwenzake  ni mja mzito.

Baba akawa anatoka na rungu lake na bakora mkononi, akakuta wanawake wameshikana, akaingilia kati, na kuingilia kwake, hakuwa na nia ya kugombolezea, alikuwa na hasira zake kichwani, akaanza kutembeza bakora

Cha ajabu yeye hakujali anampiga nani akawa anazungusha bakora inampiga huyu au yule, na mwishowe akalizungusha rungu hili bahati mbaya likamgonga mama kichwani, mama akayumba kwa kizunguzungu na kabla hajakaa sawa mke mwenzake akamsukuma kwa nguvu zote, msukumo ambao ulimfanya mama akose balansi na kudondokea kwenye kuni.

Kuni alizodondokea mama alizikusanya mwenyewe kwa ajili ya banda la mifugo. Kuni hizo nyingi zilikuwa za miba mikali kweli, zilikuwa maalumu kwa kujengea banda la mifugo, na miba hiyo ikamuumiza sana mama usoni. Miba ile ilimchanachana sana mama, kama mtu aliyetumuia wembe kurarua raua uso na sehemu nyingine za mwili .

Mke mwenza akaitumia ile miba sasa kuzidi kumchana mama usoni, ilikuwa hali mbaya , mama uso wote ukageuka damu….akawa anaguna tu kwa maumivu

Mume naye bado alikuwa na hasira zake akaanza kumcharaza mama kwa hasira, wakishirikiana na mke mwenza, walipiga bila kujali wapi wanapiga, hadi mama mtu alipopoteza fahamu….

Baba hasira zikapoa, akiwa kashikilia kimfuko cheusi, akasema;

‘Huu ndio uchawi wako sio….sasa utaenda kuwangia kuzimu na hiyo mimba yako utaenda kuizalia kaburini..’akasema na mke mwenza akawa anakiangalia kile kimkoba, ni kimkoba kidogo kama pochi za akina mama, cheusi,

‘Ohoo, kumbe…umeona eeh, nilikuambia huyu mwanamke ni mwanga, unaona hiki kimkoba ndio urithi wa kichawi, sijui kutoka kwa bibi zake…’akasema akiogopa kukishika.

Mume akamtupia mama na kugeuka kutaka kuondoka, mama alikuwa kalala pale chini kapoteza fahamu, huku damu nyingi zikimvuja, na kwa hali ile, walijua wameshaua na huenda kukazuka vita vya kiukoo.

‘Mume wangu tumeua, usiondoke…..’akasema mke mwenza.

‘Hajafa huyu wachawi hawafi kirahisi hivyo….’akasema mume sasa na yeye akionyesha wasiwasi, akasogea na kumuinua mama kichwa, akaona kalegea, uso ulikuwa hautambulikani ni kama nyama nyama zimeraruliwa.

‘Mhh, nani kamchana hivi, wewe..umemfanya nini mwenzako…’akasema mume mtu.

‘Nimemfanya nini,….tulikuwa tunampiga wote, miiba hiyo, ….sasa mume wangu tufanyeje….?’ Akauliza mke mwenza.

‘Hili sasa tatizo, ……’akasema mume akionyesha wasiwasi.

‘Ni kuambie kitu, huyu keshakufa, cha muhimu tukamtupe huko mabondeni, ataliwa na fisi …….’akasema mke .

Mume bila kuikiri akaona ni wazo zuri, na kwa vile giza lilishaanza kuingia hakukuwa na watu wakipita, wakambeba kwa kushirikiana hadi eneo la bondeni,na kumtupa kama gunia.....


WAZO LA LEO: Mwanadamu akizidisha chuki, huwa kama mnyama, na ni bora ukutane na mnyama kuliko huyo mwanadamu,..yote haya husababishwa na kushindwa kujenga uvumilivu na subira kwenye mioyo yetu. Pupa, tamaa husuda hutawala nasi zetu na matokea yake, nafsi hukutuma kufanya hata yale yasiyofaa. Tujaribu kufikiri kabla ya kutenda, tujaribu kuwa na subira pale tunapofikwa na masahibu yenye kuchochea ubaya.

Ni mimi: emu-three

No comments :