Mwanangu,
Baba yako hakuwa na kufanya, akakubali kwa shingo upande kwani wazee wa kimila
wanaheshimiwa sana huko kijijini, na hata hivyo akasema anasubiri mtoto
akizaliwa kama ana sura ya huyo jamaa atahakikisha anamletea huyo raiki yake
kiwiliwili kisicho na kichwa na mke atakuwa kiwete. Na rafiki yake akamjibu
naye kwa maneno ya kejeli;
`Na
hata akizaliwa sura kama yako, namchukua huyo mtoto kwangu, kwani hustahili
kuwa na baba kama wewe anayepinga uhalali wake, hivi utapata wapi mke kama huyo
anayejiheshimu, mke ambaye amejitahidi kulinda heshima yak oleo hii umadhania
ubaya….wewe ni mtu wa ajabu sana…’akasema rafiki yake
‘Najua
wewe utamtetea sana, si mpenzi wako, sioni ajabu….’akasema baba yako
‘Hivi
kweli, mimi nitembee na mkeo, shemeji yangu, mtu na muheshimu kiasi hicho, na
kwanini mimi nitembee na mke wako, wakati mke wangu unamtambua kwa uzuri wake,
na wao wawili ni kama ndugu, kamuulize mke wangu kama anaweza kuamini maneno
yako...’akasema
‘Kama
mke wako angekuwa ni mzuri kama unavyodai wewe, kwanini uekuja kuzini na mke
wangu, na unaweza kumdanganya mke wako lakini sio mimi, mimi nina akli ya
kutambua, sio kama mkeo, mdanganye yeye, na ipo siku nitakunasa tu, na, subiri
mtoto azaliwe ushahidi utabainika…’akasema
‘Kwahiyo
unaamini kuwa wewe huzai ni tasa….?’ Akasema rafiki yake.
‘Umeanza,
unafikiri mimi nitajali hao wazee, nitaliwasha hapa na wakija kuamua utakuwa
hautamaniki..’akasema.
‘Thubutu,
wewe kai yako kukimbilia rungu, pigana na mikono mitupu uone kazi yangu…sema
mimi sipendi ugomvi, kupigana sio ani yangu…’akasema rafiki yake.
‘Ndio
ujue sasa, kuwa kama wewe ni mtaalamu wa kuiba wake za wenzako kuna wataalamu
wa mengine, nab ado, hii kesi wamenionea, ila nikikupatia hawatakuwa na kesi a kujibu,
utakuwa maiti…wewe utaona….’akasema
‘Kwa
kauli yako sitaki urafiki na mtu kama wewe, na ole wako, ukanyage kwangu, na
huyo mtoto akizaliwa sio halali yako hata kama mnafanana naye, na kama
atakusaidia, hatafanikiwa, maana hustahili msaada wake, kwani umeshamkana…’
akaambiwa na rafiki yake.
‘Utajua
mwenyewe, ….ngoja azaliwe, utaona maajabu yangu…’akasema
‘Huyo
umeshamkana, sio mtoto wako tena huyo ni mtoto wa mama,maana hakuna mama
anayeweza kumkana mtoto wake, hakuna mzazi anayekana mtoto wake, wewe ni mtu wa
ajbu sana, unamkana hata mtoto, hata kabla hajazaliwa..…’ rafiki yake akasema.
`Tatizo
lako unafikiri mimi ninatania, we subiri uone, labda kama sio mimi…wewe
unanionaje mimi, mimi siwezi kulea mimba za watu, azaliwe mwanaharamu mimi
nilee tu, utakuja kuchukua kinyago chako, kikusaidie wewe…’ baba yako akasema
na kuondoka hapo kwenye kikao.
Mabiashan
hayo yaliendelea hata bada ya kikao, ikaonekana kuwa marafiki hao sio marafiki
tena, wameshakuwa maadui..
Tuendelee na kisa chetu….
*************
Kikao kiliamua kuwa mama
bado ni mke halali wa baba yako, na baba yako anastahiki kuhudumia mimba hiyo,
kama mke wake, mwanzoni baba yako alipinga,lakini baada ya wazee kuja juu,
akakubali kwa shingo upande na wanafamilia hao wakarudi majumbani kwao.
Mama aliendelea kuishi
kimashaka na mume wake, hawakuwa na maongezi ya mke na mume,mume akija,
kunakuwa kama hakuna mtu, kila mtu kanuna, mume bado ana hasira zake, mke naye
keshajenga chuki kwa mumewe ikichanganya na matatizo ya mimba.
‘Nilimchukia mume wangu
wangu kupita kiasi, sikutamani hata kumuona, na kila nikimuona mume wangu,
nasikia kutapika, na wakati mwingine natapika kabisa…’akasema mama.
Moyoni nilihuzunika sana,
kwani siku ile nilipotoka kwa dakitari nilitarajia iwe mwanzo wa furaha katika
familia, kwani sote tulikuwa tunahitajia mtoto, sasa mungu kasikia maombi yetu,
lakini cha ajabu ikageuka kinyume chake, taarifa hiyo ikazua mambo mengi,
kiujunla kila nikitathimini nakuja kuona kuwa mchonganishi mkuu ni mke
mwenzangu, yeye ndiye alijenga hiyo fitina japokuwa alikana kwenye kikao cha
wazee.
Nilipoongea na watu, wengi
waliniambia wao walisikia kabisa kutoka kwa mke mwenzangu, wakasema;
‘Mke mwenzako ndiye
aliyekuwa akipita mitaani na kutangaza kuwa wewe unatembea na rafiki wa mume wako….na
alisema, alishamuelezea mume wako kuwa rafiki
yake hufika hapo nyumbani, kila akitoka kwenda kwenye shughuli zake, na wakati
mwingine rafiki yake huyo hushinda..’akaambiwa.
‘Mume wako nasikia kwanza
alisema hana shaka na rafiki yake huyo lakini mkewe huyo akamwambia, kwanini
rafiki huyo ashinde humo ndani, na akitoka anashindikizwa kwa kicheko cha
kimapenzi….’
‘Jamani toka lini huyo
rafiki yake akashinda nyumbani kwangu, sikumbuki kitu kama hicho maana yeye
husalimia tu na kuondoka,ina maana mwenzangu aliamua kunisingizia mimi kwa kisa
gani …’akajitetea mama
‘Basi ndio hivyo fitina haichanganui
ukweli, na uwongo, kama vyote vinaharibu, vitasemwa tu, na ujue fitina
ikijengwa husambaa kama ugonjwa wa kuambukiza,kwahiyo uwe makini na mke
mwenzako huyo…’akaambiwa.
‘Mimi sikujali sana,
nikamuachia mungu, na hata nikikutana na mke mwenzangu namsalimia, yeye
huitikia kama hataki, sikujali.....’akasema mama
Basi toka siku hiyo ya tukio rafiki wa mume
wangu, akawa anapita bila kusalimia, kwasababu ndio njia yake, akilekea
nyumbani kwake, akawa amekata urafiki na baba yako kabisa, na hata hivyo bado chuki
za chini kwa chini , chuki hizi zikazidi kuendelea hadi kufikia familia,
familia kwa familia zikaanza kuchukiana.
‘Lakini nyie watu wawili
mlikuwa marafiki kwanini mfikie hatua hiyo?’ rafiki huyo akaulizwa siku moja na
mzee mmoja
‘Hata mimi sipendi, lakini
kama mwenzangu kalikoroga atalinywa yeye mwenyewe, mimi sijali tena,….’akasema
‘Mimi sikuwepo kwenye
kikao, na nilisafiri, niliporudi nimesikia juu juu hivi ilikuwaje mpaka
mkakosana na mwenzako, maana katika kijiji hiki mlikuwa mfano wa marafiki ,
watu mlioshibana mpaka mkasaidia kwenye ndoa zenu, leo hii nasikia mumekosana,
kuna kitu gani kikubwa kimetokea?’ akauliza huyo mzee.
‘Mzee hata mimi mpaka
siamini, lakini imebidi iwe hivyo, ni ajabu siku hiyo, maana mimi nilikuwa
sokoni, nikamuona shemeji yangu…, alikuwa akinunua bidhaa zake, nikamsalimia
akasema anaumwa, katokea hospitalini, basi kwasababu njia ni moja nikaone
nimchukue na baiskeli, sasa kumbe hilo ni kosa….’akasema
‘Kwanini ni kosa mbona
wengi wanafanya hivyo,...hilo sizani kama ndio tatizo lazima kuna jambo
jingine, lakini hata hivyo kwa vile unamfahamu rafiki yako, kwanini ubebe wake
za watu kwenye baiskeli yako si unamfahamu huyo jamaa alivyo…’akasema huyo mzee
kwa mzaha.
‘Lakini mbona sio mara ya
kwanza, …maana huyo ni rafiki yangu, …na kijijini hapa ni jambo la kawaida, na
kama ulivyosema hilo sio chanzo, nasikia aliambiwa kuwa mimi natembea na
shemeji yangu huyo...’akasema
‘Mhh, wewe utembee na mke
wa rafiki yangu,labda umebadilika,..sijui au na wewe umeshikwa na ibilisi
ukajikuta umefanya hivyo, maana binadamu unaweza ukatekwa na shetani bila
kujijua....?’ akauliza huyo mzee.
‘Hapana mzee, mimi
sikufikia huko...namuheshimu sana shemeji, na rafiki yangu huyo, hizo ni fitina
zilijengwa na watu, na mwenzangu bila kufahamu akatekwa na hizo fitina,
hakutaka kuchunguza vyema...’akasema
‘Kwahiyo alipokuona
umemchukua mke wake kwenye baiskeli akakuvamia mkaanza kupigana?’ akaulizwa
‘Ilikuwa kama mzaha vile,
mimi nilimpa lifti shemeji yangu huyo, nikamfikisha nyumbani kwao,...muda kama
huo mara nyingi rafiki yangu anakuwa hayupo, lakini siku hiyo nilimkuta
nyumbani, akatuona, sikuwa na shaka, mimi nikamsalimia kama kawaida, nikashangaa
haniitikii, mimi nikajua mwenzangu kwa vile ana matatizo yake, nimuache tu,
nikaondoka zangu…’akasema
‘Nikiwa nyumbani kwangu, mke
wangu akaniambia kuwa, kuna jamaa mmoja ana ng’ombe mweusi kama alivyomtaka
rafiki yangu, niliposikia hivyo, nikapanda basikeli yangu na kukimbilia kwa
rafiki yangu,....’akasema
‘Ukajirudisha, ...huoni
kwamba ulijitakia mwenyewe...’akasema mzee.
‘Unajua yule ni rafiki
yangu, matatizo yake ni yangu pia, kwahiyo niliposikia kitu kama hicho nikaona
matatizo ya rafiki yangu yatakwisha. Nilikwenda kwake, nikijua hiyo itakuwa
taarifa nzuri kwake. Mke wangu alipoona naondoka akalalamika, maana tulikuwa na
safari muhimu na yeye, nikamwambia;
‘Mke wangu huyu ni rafki
yetu, ni muhimu tuwahi huyo ng’ome asije akachukuliwa na mtu mwingine,
nikamuacha mke wangu ambaye alitaka twende sehemu muhimu kwenye shughuli zetu
za kibiashara..unaona mzee, nilifanya hivyo kwa kujali urafiki wetu, kumbe
najipaleka kweney matatizo…’akasema.
‘Unajipeleka ndio,
ungetumia akili kidogo, siku hiyo ikaisha, ulivyomsaliamia akakataa kuitikia
ina maana ana hasira,je hukuwahi kusikia tetesi kama hizo kabla kuwa watu
wanasema unatembea na mke wake....!?’ akauliza mzee kwa mshangao
‘Mzee sikuwahi kusikia,
ningelisikia ningelishaangea naye, kumuweka sawa, kuwa hizo tetesi sio kweli,
....na ningelijua kuwa imefikia hapo, hadi yeye kuamini, nisingelikwenda, maana
mimi namfahamu sana huyo rafiki yangu, akiamini kitu, kumrudisha nyuma ni kazi
ya ziada...’akasema
‘Sasa si unaona,
....lakini ilipangwa itokee ....Ehee ulipofika ikawaje?’ akauliza mzee
‘Nilipofika, nikapiga
hodi,....kwanza sijui kwanini, maana nilipokaribia eneo lao, nikahisi mwilini ukinisisimuka,
nikahisi hakuna amani, moyoni nikasema labda shemeji kazidiwa, maana nilipomla
lifti, alisema katokea hospitali anaumwa, ....’akasema
‘Anaumwa! Alikuambia
anaumwa nini?’ akauliza mzee.
‘Alisema hajisikii vyema,
mwili mzima unama, tumbo,..alisema ni karibu kila kitu, mimi nikamtania au ndio
dalili zenyewe nini, akacheka tu, hakuniambia kuwa ana ujazito....’akasema
rafiki
‘Ujauzito....?’ akauliza
mzee kwa mashangao.
‘Nilimtania tu, sikuwa
najua loloye mzee, na niliona ajabu yeye kusema katokea hospitalini, wakati
mume wake, niliongea naye alisema kwanza hapendi kutibiwa hospitalini yeye na
mkewe, lakini pia kutoka na masharti ya dakitari, mkewe au yeye hatakiwi kwenda
hospitalini ...’akasema
‘Mhh, mbona hiyo mpya,
hata akizidiwa, hata akiiumwa?’ akauliza mzee
‘Sasa kumbe nilipokutana
na mke wake alikuwa katoka hospitalini kwa kujiiba kupimwa,...uone jinsi gani
hali ilivyojikoroga, mume akisikia hivyo, anaweza kuhisi kuwa na mimi
nimeshiriki kumshawishi mkewe akatibiwe, na hata nilipomsalimia akakataa
kuitikia, nikajua huenda...huenda, sikuwa na uhakika na hilo...’akasema
‘Ina maana mume wake
alijua kuwa mkewe ana uja uzito?’ akaulizwa
‘Hakuwa anafahamu, hata
mkewe mwenyewe alifahamu baada ya kwenda hospitali kupimwa, hata mimi sikuwa
nafahamu, maana mkewe ahakuniambia kuwa ana uja uzito, ...’akasema
‘Ohooo,
kumbe...nimeshaanza kuelewa....’akasema mzee
‘Sasa ikawaje,...maana
habari inaanza kunoga, maneno ya mitaani yanatiliwa chumvi zaidi, nimesikia
kutoka kwako naanza kuelewa..’akasema mzee
‘Mzee nilipofika nikiwa na
furaha, nikapiga hodi, mlango ukafunguliwa uso kwa uso na rafiki yangu, kumuona
sura yake nikajua kuna tatizo,...nakaribishwa moja kwa moja na kauli ya
shutuma, oooh, nimesikia wewe unatembea na mke wangu, oooh, ….sikuelewa,
nilipoona shutuma zinazidi nikaamua kuondoka, ile nageuka tu, rungu
likanikosa,…sijakaa sawa mateke ngumi,….nikaona sasa vita, ikabidi na mimi
nijjihami, tukaanza kuzipiga kweli…..’akasema
‘Mkewe akakutetea, ndio
akapigwa au ilikuwaje mpaka yeye apigwe na kupoteza fahamu..?’ akaulizwa
‘Wakati naingia mkewe
alikuwa kalala sakafuni kapoteza fahamu, kumbe alishapigwa hadi kupoteza
fahamu...kwahiyo hadi tunapiagana mkewe hajui.....’akasema
‘Rafiki yako ana hasira
sana, lakini hasira hizo ni kwa vile hajapata mtoto kwahiyo ni pamoja na wivu, hata
hivyo alitakiwa kuipokea hiyo taarifa ya mkewe kwa furaha, na kama anahisi
vinginevyo angesubiri mkewe ajifungue kwanza….’akasema mzee
‘Anasema hataki kulea
mimba za wenzake, yeye ana uhakika kuwa mtoto sio wa kwake....’akasema
‘Oh, anasema ana uhakika
kuwa mimba sio yake!? Huo uhakika kaupatia wapi,...ujue yeye anajijua mwenyewe
yupoje, kama kafikia kusema ana uhakika, .....huoni kuwa kuna jambo, ...halafu
anasema wewe umetembea na mkewe ukampa mimba, mmmmh, hilo lazima lina sababu,
..kuna kitu kimemfanya aamini hivyo sizani angelishikilia wazo hilo bila sababu...’akasema
mzee.
‘Mganga wa kienyeji ndiye
aliyemfanya aamini hivyo, hakuna sababu nyingine mzee....huyu jamaa yangu
anaamini sana waganga wa kienyeji, na alipofika mitaani, maneno ya mitaani
yakazidi kumchanganya, akaambiwa kuwa mimi natembea na mkewe basi kwa akili
yake fupi, ikamfanya aamini hivyo, hakuna jingine ni fitina na uvumi usio na
ukweli mzee wangu...’akasema
‘Ohooo, nilijua tu...hawa
waganga wa kienyeji wa ramli, usipokuwa makini, unaweza ukaghilibika,...mimi
najiuliza kwanini asingelienda kwanza hospitalini akajihakikishia, kwanini
akakimbilia huko...’akasema mzee
‘Hata mimi nilimshauri
hivyo hakunisikia, mzee, jamaa yangu huyo huwa hapendi kwenda hospitalini
kabisa, yeye anaamini kuwa tiba nzuri ni hiy ya waganga wake.....’akasema
‘Mimi sikatai, kuna tiba
nzuri za miti shamba, lakini kuna waganga matapeli vile vile, na kuna
washirikina, ambao lengo lao ni kujenga fitina kwa watu.Unaona hao wanaoua
maalibino, unajua wamepata wapi hayo, ni kutoka kwa hao waganga wa
kienyeji...’akasema
‘Mzee, hayo kamuambia huyo
jamaa, hamtaelewana...’akasema
‘Huyo ni sawa na ha
wanaodanganywa, wanaambiwa miili ya watu inaleta utajiri, kwanini yeye asikate
mwili wake, akaupta huo utajiri ...mimi sijui kwanini watu hawaelemiki,...na
kwanini hamuuliza huyo sijiu mganga au mtaalamu, kuwa, kwanini yeye asifanye
hivyo akawa tajiri..binadamu ana akili ya ajabu sana....’akasema mzee.
‘Mzee pamja na imani zake
hizo, lakini kubwa zaidi ni kuwa yote hayo yamefikia hapo, kwa vile kachelewa kupata mtoto...’akasema
rafiki huyo
‘Mtoto, mtoto, hivi yeye hajui
kuwa kupata watoto ni majaliwa ya mungu hakuna anayependa iwe hivyo,...huwezi
kumlaumu mke, au kutupia lawama kwa wengine,na tatizo jingine mke wake mdogo
naye hajatulia, namfaahmu sana yule binti...lakini tuyaache hayo, muhimu rafiki
yako anatakiwa awe makini hasa na mke wake mdogo, mimi nikikutana naye
nitamshauri hivyo…’akasema huyo mzee
‘Utakosana naye, hataki
ushauri kuhusu maisha yake, mimi ni rafiki yake, lakini inapofikia kumshauri
kuhusu maisha yake na wake zake, tunakosana....’akasema
‘Mhh, kama ni hivyo kuna
tatizo...’akasema mzee
‘Mimi sasa nimeahidi, kama
atanileta vurugu tena, safari hii nitapambana naye kiukweli, haniwezi kwa
kupigana yule, kazi yake kukimbilia rungu, mimi niachieni huyo mtu,
keshanichokoza, nitamtengeneza barabara, mimi sichezewi na watu kama hao, mimi
ni mpole sana,lakini mtu akinichokoza vita yake haiishi, atakuja kukimbia hiki kijiji,
mwenyewe utaisikia…’ hayo yalikuwa maneno ya rafiki mtu.
‘Hapana usifikie hapo,
huyo anahitajia ushauri....sijui tutafanyaje, lakini tukiliachia hivi hivi
linaweza kuzua balaa jingine, namuonea huruma huyo mke wake mkubwa...sijui
wataishije...ana mtihani...’akasema mzee , na kuagana na rafiki huyo.
******
Usuluhisho wa kimila
ulishapitishwa ulitakiwa uheshimiwe,….lakini chokochoko zikawa zinachangia kila
mmoja akawa anatia neno, na neno huwa maneno, na yakiwafikiwa wahusika
huzidisha hasira jamaa wakawa mahasimu kweli. Wazee waliposikia kuwa bado kuna
uadui wa chini kwa chini kwa watu hao, ikabidi wakuu wa koo hizo mbili waitwe,
ili kusije kukavuja damu tena.
`Kama bado hamjatosheka na
hukumu hii, tutaingilia sehemu ambayo mtakuja kujuta wenywe, tunatoa onyo
kali…’ akasema mzee wa kimila, na mzee huyo huheshimiwa sana na wengi
wanamuogopa kwa karama zake.
Wakiambiwa hivyo
wanatulia, lakini choko choko za watu, wafitina, zikawa bado zinapalilia chuki.
Mvutano huo uliendelea
chini kwa chini na baadaye ukafifia, baada ya kuona hakuna ushahidi wa moja kwa
moja. Miezi ikapita na mimba ya mama ikawa inakuwa, japokuwa ni kwa shida kwani
mume mtu alikuwa hajali kuwa mkewe ni mja mzito na anastahili kuhudumiwa , yeye
akikasirika bado anaendeleza vipigo.
Mama aliomba kama baba
hana uhakika na uhalali wa hiyo mimba basi amuache arudi kwao, lakini hoja hiyo
ilipingwa kabisa na mumewe na hata wazee walikataa hilo kwenye vikao
vilivyopita, aliambiwa;
‘Kisheria mke anapokuwa
mjamzito ni wajibu wa mume husika kumlea mkewe hadi ajifungue, haruhusiwi
kumuacha, ….’akaambiwa.
‘Lakini sasa nitaishije
kwa hali hii, mimi namchukia kweli mume wangu, na akija hana subira na mimi,
akiona kuna jambo anakimbilia kunipiga bila hata kujali kuwa mimi ni
mjamzito…’akasema mama
‘Tunahitaji ushahidi
akukupiga waite watu, piga ukelele, watu waje washuhudie, na sisi tutachuku
hatua…’akaambiwa, lakini tatizo la mama alikuwa mvumilivu sana, anapigwa anakaa
kimiya.
Matatizo ya familia hii
yakawa yanaendelea, baadaye wazazi wa pande mbili wakakutana kulijadili
kiundani hili tatizo, maana mume bado anashikilia kuwa hiyo mimba sio yake, na
akiulizwa sababu gani muhimu, anadai kuwa keshachunguza, na anajua kabisa hiyo
mimba ni rafiki yake, sio mimba yake.
Wazazi wa mume walionekana
kuwa upande wa mtoto wao kuwa kwa dalili zilizojionyesha na sababu za mtoto
wao, kwasababu yeye ni mume, na yeye anamfahamu zaidi mke wake kwahiyo huenda
kuna ukweli, kwahiyo wakawa wanamsikiliza mtoto wao jinsi anavyosema, lakini
hawana uhakika wa moja kwa moja…
‘Mkisema hivyo mnakosea, hawa ni watoto, na
tukisikiliza maneno ya mitaani tutayumbisha hiyo ndoa yao, sisi tunamfahau
binti yetu , hana hiyo tabia kabisa, lakini muhimu ni kuwasuluhisha, na sio
kusimamia upande mmoja…’wakasema wazazi wa kikeni.
Mwisho wa kikao hicho wakafikia
muafaka kuwa,waache mpaka mtoto azaliwe halafu watakuwa na ufumbuzi kamili…
‘Na kama ni kweli mtalipa
mahari yangu….’akasema mume wangu.
‘Ukishazaa naye mahari
haipo tena hapo….’akaambiwa baba yako.
‘Haipo wakati sijazaa
naye, hiyo mimba sio yangu….mnataka niwaelezeje…’akasema baba, kuonyesha kabisa
hajakubaliana na hiyo mimba kuwa ni yake.
Kwa vile alishajenga hiyo
hoja kuwa mimba si yake, akawa akifika kwa mkewe huyo mkubwa anaanzisha visa,
na mkewe kwa vile naye keshajenga chuki, basi inakuwa ni uhasama kati ya mke na
mume, na mume hacheleweshi kupiga.
Kwahiyo mama bado akawa
anapigwa, anasimangwa, na hilo la kuonekana kuwa mimba sio ya familia hiyo
likawa limeshika kasi kweli, mawifi wakawa wanamsimanga mama kuwa kazaa nje ya
ndoa.
‘Mwanamke gani Malaya ,
anakwenda kuzaa nje ya ndoa…kalichafua jina la familia, anataka ili kaka yetu
aonekane hazai kumbe kisa ni yeye….’akawa anaambiwa. Mama akavumilia akijua
kuwa akijifungua ukweli wote utabainika, na hayo yatakwisha.
‘Mimi namuachia mungu,
tusubiri nijifungue na mtathibitisha huo umalaya wangu…’akawa anawaambia.
Jinsi mimba ilivyokuwa
inakuwa, na ndivyo mama alivyozidi kuchoka, ikawa kazi nyingi haziwezi, wenzake
bila huruma wakawa wanamsimanga kuwa yeye ni mvivu, kazi yake kutaka kulala na
kula tu.
‘Kama hawezi kazi amtafute
mfanyakazi wake…na kwanini mwenzake asimsaidie kazi…..’wakawa wanasema mawifi.
‘Hayo watajua wenyewe,
yeye kama mke anawajibika sio kulala tu asubiri kupikiwa, ….’akasema mama
‘Kaka katuambia tuwe
tunakwenda kumsaidia kazi, sisi tumechoka, ukifika ndio anajilegeza kabisa, na
sisi tunashughuli zetu….’wakawa wanalalamika mawifi.
Kucha na kuchwa, mateso
yalikuwa yanazidi na hakuna aliyejali ile hali yake hadi ikitimia mimba ya
miezi nane.
Siku moja baba mtu alirudi
nyumbani akawa amefika na mke mdogo, ilikuwa kama ajabu kwa mama, kwani mke
mwenza alikuwa hafiki hapo kwake mara kwa mara hakutaka kuuliza kwanini leo
imekuwa hivyo akawasubiri asikilize nini kimewaleta.
‘Nimemleta mwenzako awe
anakusaidia kazi kwasababu ya hali yako,sitaki iwe sababu, nataka ujifungue ili
nione ukweli, kwahiyo sitaki mkorofishane hapa..’ akasema mume mtu hakuataka
hata kusikia mama atasema nini , yeye akaondoka zake. Mama hakuamini hayo,
kwani yeye alishafikia hatua kuwa kama inawezekana akakae kwao mpaka ajifungue.
Lakini hiyo ikapangwa ili mama asiende kwao, hakujua wenzake wana malengo gani.
Mke mwenzake akawa anafika
hapo asubuhi kwa nia ya kusaidia kazi, lakini cha ajabu akawa akifika hapo
hafani kazi yoyote, hatoi msaada wowote, anaweza akafanya kazi ndogo ndogo
nyingine akaacha na kulala, hata chakula akawa hapiki.
‘Vipi mwenzangu sasa
tutakula nini?’ anauliza mke mkubwa
‘Unaniuliza mimi, hapa ni
kwako, wewe ndiye ujue utakula nini, na wewe ndiye una tabia ya kuchagua
chakula, pika unachoona kinakufaa…’akasema mke mwenza kwa nyodo
‘Lakini si umekuja hapa kunisaidia
kazi , mbona tangu ufike hapa hakuna kazi unayofanya, sana sana unafanya kazi
ndogo, ukachukua mkeka na kulala, si bora ungejikalia nyumbani kwako tu.....?’
akauliza mama.
‘Nilizofanya zinatosha,....maana
hata kwangu kuna kazi za kufanya ni nani atanisaidia kazi zangu, yaani mimi nikufanyie
wewe kazi zao nichoke, niende kwangu kazi zangu za nyumbani zinanisubiri, na
mume anahitajia,...sijaolewa kuja hapa kuwa mfanyakazi wako….’akasema mke mdogo.
‘Lakini mpaka kuja kwako
kwangu, mimi nilijua mumekaa mkakubaliana, ukakubali kuwa unakuja kunisaidia
kazi au sio?, kama huwezi basi kwanini usisema ili mimi niende kwetu, maana
mimi kwa hali hii kiukweli nahitaji mtu wa kunisaidia kazi…’akasema.
‘Kwenda kwenu hilo
mtajuana wewe na mume wako...najua unachokitaka, ili ukajifungulie kwenu,
ufiche ukweli,ndio maana nikakubali, nije kukusaidia, sipendi ila, nataka ukweli ujulikane, ..maana watu wanasema mimi
ni muongo nimekufitinisha, nataka uzalie hapa mtoto aonekane…’akasema mke
mdogo.
‘Mhh kumbe ndio nia yako....basi
ngoja nizae, ukweli utawaumbua,...’mama akasema, na mke mdogo akamuangalia mke
mwenzake kwa mashaka, halafu akawa kama kakumbuka jambo, akatoka nje.
Mama akaamua kujifanyia kazi
zake na hata chakula akawa anajipikia mwenyewe,…na mume akija wakati mwingine
anamuona akifanya kazi, haulizi kisa ni nini, …lakini baadaye mama akaona ni
bora aseme ukweli, akamueleza mume wake kuhusiana na hiyo tabia.
Alipoulizwa mke mdogo kwanini
hafanyi kazi kumsaidia mwenzake, akasema;
‘Huo ni uongo, kila nikifika
asubuhi nafanya kazi zote, yeye hataki nipumzike, na kila ninachofanya anakitoa
kasoro, nikipika chakula hataki kula, anasema ni kibaya, mara haikaiva, mara
kinanuka, anamkaripia kama mfanyakazi wake, anafikia kunisimanga kuwa mimi sizai…’akasema
hivyo mke mdogo
‘Jamani hayo yote yametoka
wapi, mimi niliongea hivyo…?’ akauliza mama
‘Sasa unakataa sio, au
niseme yote uliyoniambia….’akasema huyo mke mwenza, na mama hakujua mwenzake
anataka kusema nini tena.
‘Useme yote yapi hayo,
nimekuambia nini mimi, mbona wewe mwanamke mshari, kwanini humuogopi mungu
wako, unazua uwongo,….’akasema mama
‘Mshari ni wewe, uliyeanza
kunisingizia kuwa mimi sifanyi kazi, hayo yote umeyaanza wewe, sasa nitasema
yote uliyoniambia, wewe siunajifanya unajua kuema wenzako, ….’akasema na mama
akakaa kimia.
‘Amekuambia nini
unachoogoap kusema?’ akauliza mwanaume.
‘Ameniambia mengi sana, na
hata mengine sitaki kuyasema kwani nimeshayazoea, nilishawahi kuyasikia kwa
watu nikayazarau, lakini sasa nimeyasikia moja kwa moja kutoka kwake, kaniambia
mwenyewe, kwa mdomo wake…’akasema
‘Kakuambia nini….?’
Akauliza mume mtu, kwa hasira, na mke mdogo akamuangalia mama, na kumuuliza;
‘Niseme, …au ukiri kuwa
hayo uliyomwambia mume wetu umetungia mwenyewe, ….?’ Akamuuliza
‘Kwani mimi nimekuambia
nini, …wewe mwanamke, muogope mungu wako, unajua kusema uwongo ni
dhambi,…’akasema na mke mdgo akabenua mdomo kwa dharau, na kuinama chini.
‘Nataka kuyasikia hayo
aliyokuambia, vinginevyo nitakuadhibu wewe mwenyewe uliyeanza kuongea, kama nu
uzushi wako ..kakuambia nini …?’ mume akamsogelea mke wake mdogo kwa hasira, na
mke mdogo akaonekana kuogopa, akasema;
‘Kasema kuwa yote hayo ya
wewe kutokuzaa, anayafahamu na….na amefanya hivyo kwa kiherehere chako cha
kutaka kuoa mke mwingine, na alicho kifanya, alishajua kuwa wewe hutazaa tena,
ndio maana akaenda kutembea na mume mwingine…’akasema mke mdogo bila kuogopa,
na mume akawa kama kapigwa na shoti ya umeme, akasema.
‘Na hiyo ni siri ya yeye
na rafiki yako.....kama utambana vizuri rafiki yako atakuambia..kwani yeye
kafanya kama kukusaidia, usiadhirike...’akazidi kusema.
‘Nini amesema nini….!?’ Mume
mtu akajitanua kifua na kupumua kwa nguvu, akamgeukia mke mkubwa na huku
akitetemeka kwa hasira, akasema;
‘Hivi, wewe mwanamke
unanitaka nini mimi, kumbe yote hayo sababu ni wewe, unajua kuwa ni kweli, sasa
unaongea kwa kujiamini kwa vile una uhakika kuwa wewe unazaa, wewe sio mgumba
tena, na mimi umeshaniharibu, ili nisizae, eeh, ...hata nikikuacha huna hasara
au sio…’akasema akimuangalia mke mkubwa kwa hasira.
‘Sio kweli mume wangu, huo
ni uwongo…’akaweza kusema maneno hayo lakini akajikuta hawezi kuendelea,
alihisi vibaya, kutapika, akawa anajizuia, na mke mdogo akadakia na kusema;
‘Ndio hayo aliyoniambia
mume wangu muulize, aliniambai na sio mara moja, muulize si huyo hapo….?’ Akasema
akimuangalia mume wake kwa macho ya namna yake, na mume mtu akaguna, halafu mke
mdogo akamgeukia mke mkubwa na kumuambia;
‘Je, ni kweli si kweli, je
hukuniambia hivyo....?’ akauliza mke mdogo na mama alijikuta hawezi kutamka
neno, ilikuwa kama kapigwa sindano ya ganzi, akabakia kaduwaa, mdomo wazi
haamini hayo aliyoyasikia, anajisikia vibaya, pumzi inakuwa ndogo.
Mume akawa anamwangalia
mama asema neno, lakini mama akawa hawezi hata kutamka neno, akiwa haamini….,
na kukaa kwake kimia, mume mtu akaamini ni kweli…’ na kabla mama hajarejewa na
fahamu na kuanza kujitetea baba akaingia ndani….
Mke mdogo akamuangalia
mwenzake kwa zarau, akasema;
‘Unaona umelitaka mwenyewe
kwa umbea wako...’akasema mke mdogo huku mama akiwa kashikwa na butwaa, hasira,
na akahisi kama mwili unamuishia nguvu, akaanza kujisikia vibaya...akasimama na
kuanza kutoka nje....
NB Haya haya mambo hayo
WAZO LA LEO: Hakuna kitu kinachoumwa kama
kusingiziwa uwongo wa nguoni, kusingiziwa imani za kichawi, wizi ...kusingiziwa
vitu ambavyo vinagusa hisi za binadamu, ...ndugu zanguni tuwe makini katika
kutoa kauli kama hizi,....`wewe mwizi, wewe mchawi, wewe malaya...wewe ni...’
kauli hizi huumiza sana nyoyo za watu ikizingatiwa kuwa kauli hizi nyingine ni
uzushi, sio za kweli, hebu fikiria unamwambia mtu kama huyo kuwa yeye ni mwizi,
yeye ni malaya, yeye ni muongo, na kumbe hana kabisa tabia hizo, utakwenda
kujibu nini mbele ya muumba, tuache kabisa kauli hizo...
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment