Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, December 18, 2014

NANI KAMA MAMA-9‘Wewe unakula tu, unanenepeana hapa kama nguruwe, huna faida yoyote humu ndani, tangu nikuoe, huna hata mimba ya kusingizia, angalia wanawake wa rika lako wana watoto wangapi, wewe hata wakutuma chumvi dukani hayupo…’akasema akionyesha uso uliojaa hasira.

‘Mume wangu lakini mimi sijapenda iwe hivyo…’nikajaribu kujitetea lakini hakunipa naasi akaendelea kuongea

‘Hebu niambieuna faida gani humu ndani, nilikuoa ili uje kula tu hapa, ni lazima nikutafutie mwenzako, atakayeleta matunda ndani  ya hii familia…’ akawa anasema baba yako huku akitaka kunipiga, mkono wake ulikuwa mwepezi sana kupiga.

Mimi nikawa nalia tu, nikijaribu kuwaza kosa langu hapo lipo wapi, kwani mimi nimependa iwe hivyo, hata mimi natamani sana niwe na mtoto, nikamwambia mume wangu kwa upole;

‘Mume wangu hata mimi natakani tuwe na mtoto, lakini mungu hajapenda, kwanini tusivute subira haya yote sikuyataka mimi, kuzaa ni majaliwa ya mungu, na kama ikiwezekana twende hospitalini tukaone tatizo lipo wapi….’nikasema na yeye akaniangalia kwa macho yaliyoja hasira na kusema;

‘Wewe una tatizo, unasema twende wapi hospitalini, unataka kunipotezea muda wangu kwa kwenda kwa hao wadanganyifu, …huna kwa ujumla juma kizazi, nimeshaangalia kwa wataalamu wanasema huna kizazi, …’akasema na kupanda kitandani kulala.

‘Ina maana kumbe alikwenda kwa hao waganga wao, akaambiwa hivyo, kwanini hakunishirikisha’ nikawa najiuliza

‘Ni muhimu nikaongee na mama yangu mzazni huenda akanisaidia, lakini nitafikaje huko, wazazi wangu walishanipiga maruuku kwenda nyumbani mpaka mume wangu anipe ruhusa, na taarifa ipelekwe kwanza…mmh, sasa ni nani atanisaidia,’nilikesha nikiwaza huku nikisikiliza mikoromo ya mume wangu maana yeye akilala hukoroma kama simba, nikawa usiku sipati usingizi , nikajiona mimi ni mtu wa shida tu, hadi kufikia kujuta kuzaliwa mwanamke.

‘Pamoja na hayo yote mateso, kashifa na kejeli, sikukaidi wala kukiuka sheria za ndoa,  nikavumilia hadi ikatimia miaka mitatu ndani ya ndoa, fikiria miaka yote hiyo hakuna siku unaweza kusema leo nina raha na mume wangu, kila siku kuna kosa linabuniwa, kila siku kuna kupigwa au kutukanwa, kusimangwa,  na miaka ikaenda sikuwa na dalili yoyote ya mimba..’akasema mama

‘Miaka mitatu , utajitetea nini tena, nilitumia dawa za miti shamba nilizopata kwa marafiki zangu lakini hakukuwa na dalili ya mimba, hata mume wangu kuna siku anakuja na dawa anasema kunywa hizi huenda ugumba utaondoka, lakini hakukuwa na dalili hiyo hadi wanafamilia wakakubali kuwa mimi kweli ni mgumba, sizai kwahiyo nina mawili, aolewa mke mwenza, au niondoke kwenda kwetu….

Mimi nilitamani sana kurudi kwetu, na niliposikia kauli hiyo kutoka kwa mawifi kuwa ni lazima kaak yao atafute mke mwingine au niondoke hapo,  mimi nikamwambia mume wangu kuwa nipo tayari kuachika nirudi kwetu kuliko kuendelea kuwatia hasara, yeye akasema kwa dharau;

‘‘Nikurudishe kwenu, unajua nimekulipia ngombe ngapi, unajua baba yako namdai kiasi gani, hapa hutoki, utakaa hapa ili nifidie ngombe zangu na mali yangu,kama huzai basi utakuwa mfanyakazi wa hapa…na hivi karibuni tu nitakuolewa mke mwenzako…’akasema bila hata aibu.

Haikupita muda akaolewa mke mwenza....

 Tuendelee na kisa chetu

             ************

Kweli akaolewa mke mwenzangu, na jinsi ilivypapangwa hadi kuolewa huyo mke sikushirikishwa, ilikuwa joni naona msafara wa watu unakuja na ngoma, kuuliza kuna nini, mawifi wakacheka kwa kejeli;

‘Hehehe sasa huna lako, mwenzako anakuja kuwa malikia na wewe utakuwa kijakazi wake…’wakasema

‘Mna maana gani ina maana mume wangu kaamua kuoa bila kunishirikisha..?’ nikauliza

‘Akushirikishe wwewe kama nani, hayo ni maswala ya kifamila na yeye ni mume wako ana maamuzi yote, hujui tatizo ni nini, tatizo ni wewe, ….’wakasema

Basi mimi moyoni japokuwa nasononeka, nikasema ni aheri maana adha na mteso ya kupigwa na kunyanyapaliwa zitapungua maana atakuwepo mwenzangu …lakini haikuwa hivyo.

Haikuwa hivyo kwani alipoletwa huyo mkwe mwenza nikawa mimi ndiye mhudumiaji wake mkuu. Kazi zote nafanya mimi , mwenzangu kujipamba na kumtumikia mume wake, na siku ya zamu yangu mume akija ilikuwa ni karaha tupu, na nilitamani hiyo zamu yangu isiwepo kabisa, lakini utaratibu wa zamu haukuweza kupingwa, ni lazima jae kwangu, siku za zamu yangu.

Mungu ana miujiza yake kwani hata huyu mke mwenza aliyeolewa ndani nyumba kwa mbwembwe na vifijo naye akawa kama mimi , mwaka ukapita hakuna cha mimba wala mtoto, ikawa ngoma sawa.

‘Ina maana na huyu hajapata mimba, nahisi kuna  tatizo, sio bure, maana mtoto wetu kaangaliwa ahna tatizo sasa kwanini hata huyu hashikimimba..’wakawa wanalalamika wanafamilia

‘Hili linahitajika kuangaliwa zaidi, tusije tukawa tunafuga tatizo,..huenda kuna jambo hapa, ni lazima tuhangaike..’akasema mzee mmoja wa familia, basi mke mwenza yeye akaomba kwenda kwao kwa muda, akitaka akaonge na wazazi wake akakubaliwa tofauti na mimi.

Alikwenda kwao kwa muda baadaye akarudi, na akarudi na mapya, nikazushiwa maneno kuwa mimi ndiye niliyemfunga mke mwenzangu kizazi, ili asizae. Haya yaliletwa na wazazi wa mke mwenzangu. Walisema walipoenda kwa mganga imegundulikana kuwa mimi ndiye ninayezuia mwenzangu asizae kwasababu mimi ni mgumba.

‘Hayo yametoka wapi tena,…’nikauliza

‘Ndio hivyo, sasa utatuambia ukweli kwanini unafanya hivyo, hatutaki uchafu kwenye hii familia, kama una mambo yako ya kiuchawi ni bora uyaondoe haraka….’akasema wifi yangu

‘Huo uchawi nitautoa wapi, na ina maana kama mnadai mimi ni mchawi hata wazazi wangu ni wachawi mnaweza kuyaongea hayo mbele ya wazazi wangu?’ nikauliza

‘Ataongea huyo mtaalamu akija kuutoa huo uchawi wako..tutamuita, na hapo ndipo utaumbuka, yawezekana umenunua, wazazi wako hawajui…’wakasema

‘Hilo sasa sitaweza kuvumilia kama hamnitaki kwanini mume wangu hataki kuniacha nikaondoka zangu kwetu…’nikasema

‘Huwezi kuondoka mpaka gharama za mahari yako zilipwe, na pia mpaka uhakikisha umetoa uchawi wako…’nikaambiwa

Ikawa mumewe naye akirudi ulevini kama na ni zamu yangu huja na matusi, vurugu na hata kusema kuwa ugumba wangu unasababisha hata mwenzangu asizae, nikamuuliza kwa vipi. Akasema ipo siku nitajua tu, kwani dawa bado ipo jikoni.

Kutokana na hali hiyo yeye nasikia aliamua kutoka nje ya ndoa ili kuona kuwa ni yeye mwenye matatizo au kuna jambo jingine, siku moja nikamuuliza kuwa mzaha, mbona nimesikia kuwa anatembea na wake wengine wa pembeni.

‘Kuliko kufanya hivyo  , kwanini asiongeze mke mwingine ujaribu Bahati yako kwingine kuliko kutembea nje ya ndoa…’nikamwambia kwangu mimi sikuona tatizo, hata wakiwa kumi ndio vizuri nipate muda wa kujipumzikia.

‘Usiniingilie katika maisha yangu, ninaanya nipendavyo, na huwezi kunizuia, ..na nitaamua jinsi gani ya kufanya mimi mwenyewe...'akasema kwa hasira

'Aaah mimi nilikuwa nakushauri tu,...wewe si kidume, basi oa mwingine, ...'nikawambia na akaniangalia kwa hasira nikajua kipigo kinakuja na nimejitakia mwenyewe, lakini akaguka na kuangalia pembeni , nahisi hata yeye ilikuwa inamkwaza, halau akasema;

'Unajua , nimeshaahamu kuwa wewe ndiye mbaya kwenye hii familia, kwa vile wewe umejiona ni mgumba unataka kila mtu awe hivyo,...nimeambiwa kamwe sitaweza kuzaa na wewe, kwasababu wewe ni mgumba, huna kizazi, ...na kwahiyo wewe unachofanya ni kuwaharibia wenzako, sasa sikia dawa yako inachemka…’akasema

‘Unasema nini, ina maana hata wewe unakubaliana na hilo kuwa mimi ni mchawi, je hayo unaweza kuyaongea mbele ya wazazi wangu?’ nikamuuliza

‘Wazazi wako watanifanya nini mimi,  kwanza nawadai ngombe zangu nyingi tu, nawadai mali nyingi na pesa nyingi tu, …’akasema kwa nyodo.

‘Kwahiyo mimi ninakuwa malipizo kwa mambo yenu, na mnadiriki kunisingizia mamboya uchawi,…’nikasema kwa uchungu

‘Hilo utajua wewe mwenyewe, na kama unataa nioe mke mwingine nitaoa tu, si ndivyo mnavyotaka, nitaoa hata kumi, kwasababu nina mali ya kulipa mahari, lakini sio kwa shinikizo la mtu, nitafanya hivyo kwa muda wangu…’akasema

Dua la mja mwema hukubaliwa lakini kwa wakati mwingine sio anavyotaka yeye mwanadamu, mungu anajua mwenyewe wapi na wakati gani wa kukutimizia maombi yako,huwezi ukaomba na kupata hapo hapo...unaweza ukaomba wee mpaka ukakata tamaa, na ukaja kupta muda usiotarajia kabisa.

‘Nikawa nahisi kuumwa, na kawaida mimi sio mtu wa kuumwa umwa ovyo, kama nikumwa labda niwe nimeumia shambani au kuteguka, lakini magonjwa ya homa tumbo kwangu ni nadara sana…nikashangaa kuhisi hali hiyo, mara tumbo mara najisikia vibaya hili ikanipa mashaka sana.,

Mwanzoni nilihisi labda ni kutokana na vipigo, huenda vimeniletea madhara mwilini, nikawa najitibia kwa dawa za kienyeji, lakini hakukuwa na dalili za kupona, nikamwambia mume wangu , mume wangu akasema;

‘Ndio hayo, tabia ya uvivu wako,…kwanini usitinywe dawa za miti shamba, unajua dawa za tumbo ni zipi, unataka kutega kazi tu hapa,sitaki kusikia tena hiyo kauli ya kuumwa…’akaniambia

Mimi nilishayazoea maneno yake, mwishowe nikaamua kwenda hospitalini.

Siku hiyo niliondoka kwa kujiiba na kufika kituo cha matibabu….maana baba yako hakutaka kusikia naumwa, anasema ni uvivu wangu , nasingizia tu ili kutega kazi,..nikaondoka kwa kisiri hadi kituo cha matibabu…’akasema mama.

‘Nilifika kituoni, nilipitia shambani kama kisingizio, na nikavuga vuga  hadi mume wangu akawa kaondoka, kawaida yeye huondoka mapema kupitia kwa marafiki zake,hapo nikaondoka, hadi kituo cha hospitalini, nikamuelezea dakitari, na vipimo vikachukuliwa, kwa vile nilichelewa kufika, nikaambiwa nirudi kesho kuja kuchukua vipimo.

‘Kesho tena,kwani haiwezekani leo..’nikalamika

‘Hatuwezi kutoa majibu leo mpaka kesho,na taratibu za hapa umezisoma vyema …’akasema huyo docta , ni mzungu alifungua dispensary yake, na watu wanaipenda sana, na yeye anafahamu sana Kiswahili na hata lugha yetu ya kienyeji, kwahiyo watu wanakimbilia kwake kuliko kwenye hospitaliz za kawaida na gharama yake sio kubwa sana.

Basi , mimi nikamuitikia tu kuwa nimezisoma wakati sijazisoma, kailini nikasema `mimi hapa nimefika kutibiwa sio kuangalia taratibu zao..wazungu bwana, kila kitu taratibu, sheria..hawajui watanzania hatujali hayo..’

Na kesho yake nikarudi, nilifika mapema kidogo maana ilikuwa sio zamu yangu na niliskia mume wangu kasafiri, kwahiyo niliondoka mapema na kumkuta dakitari. Dakitari akaniuliza

‘Mume wako yupo wapi,….?’ akaniuliza

‘Mume wangu, …unanichekesha kweli, hata kuja hapa kutibiwa nimefanya kama kutoroka, hataki hata kusikia ninatibiwa hospitali, yeye anaamini dawa ni za kienyeji tu…’ nikamwambia dakitari, na dakitari akaniangalia usoni, akionyesha kitu kama mashaka, na nikahisi majibu sio mazuri na sijui nina tatizo gani

 Dakitari akasema;
‘Haya majibu yako ni vyemaa angelikuwepo mume wako ili nyote myasikie na ikibidi na yeye pia apate kupimwa, hiyo ndio inatakikana, na ndio taratibu zetu,…’akasema

‘Lakini yeye haumwi na kama nilivyokuambia yeye haamini matibabu ya hospitalini, hatakubali kuja…’nikasema

‘Ni vyema urudi uje naye, mwambie ni muhimu sana, na ni muhimu pia na yeye asikie majibu ya vipimo hivyo..yanataka nyote wawili muwepo…unasikia haya nenda kamuite..tafadhali’ akasema. Mama kusikia hivyo wasiwasi ukamwingia, akamuuliza dakitari;

‘Kwani nina ugonjwa gani mbaya kiasi hicho mpaka na mume wangu awepo…?’ nikauliza.

‘Sijasema una ugonjwa mbaya, hakuna ugonjwa mbaya,…ni muhimu sana hasa katika taratibu zetu za hapa haospitalini mje wewe na mume wako…’akatulia

‘Nia yangu ni kuhakikisha wote mnatibiwa, mnajua tatizo ni nini, au kuna matokeoa gani,  kuna mambo tunataka kuyapiga vita, hasa hili la kuja kutibiwa mke peke yake au mume peke yake…’akaangalia ile karatasi kama anataka kusoma majibu ila akasita na kusema

‘Unajua piaa kuna magonjwa yanahitajia muwepo wote wawili ili iwe rahisi kwetu kutoa maelekezo, na matibabu pia…ndio maana nataka na mume wako awepo ili mpate majibu yenu kwa pamoja, na matibabu pia, na pia ndio utaratibu wetu wa hapa hospitali…’akasema dakitari.

‘Mungu wangu…’nikasema huku nikiwa nimeshika kichwa kwa mikono yangu miwili..

‘Dakitari nimeshakuambia kuja hapa nimefanya kujiiba…wewe hunielewi, mume wangu akisikia nimekuja huku kutibiwa ataniua, na hata hivyo kwani kuna tatizo gani kubwa mpaka yeye awepo…..ina maana nina ugaonjwa mbaya sana, au….oh, au nimeathirika, na hilo gonjwa la…ooh, docta niambie kama ninao nijue moja….?’nikasema kwa wasiwasi maana nilishasikia mengi kuhusu ugonjwa wa ukimwi, nikajua ndio maana dakitari anaogopa kunipa majibu yangu.

Docta akaniangalia kwa mashaka, akainua karatasi ….Naona kwa leo tuishie hapa, tuwepo kesho kusikia nini majibu ya vipimo hivyo na kwanini dakitari akashauri kuwa ni muhimu mumewe awepo!.


WAZO LA LEO: Ni vyema mke au mume anapoumwa, mkawa mnahurumiana, mnasaidiana, na mkienda hospitalini muwepo pamoja, kwani mume na mke ni kitu kimoja, na mmoja akiumwa ni sawa kama wote mnaumwa, lakini pia kuna magonjwa ya kuambukizana, mkiwa pamoja ni rahisi sana tatizo hilo likatatuliwa kwa haraka. Kumbukeni kiapo chenu cha ndoa kuwa mnaoana na kuwa kitu kimoja na mtakuwa wote wakati wa shida  na raha, kwahiyo kujaliana wakati wa matatizo hasa ya ugonjwa ni moja ya masharti ya ndoa, na pia hujenga mapenzi ya dhati.

Ni mimi: emu-three

No comments :