Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, December 17, 2014

NANI KAMA MAMA-8 Mama aliendelea kunisimulia kuhusu maisha yake, akasema;

‘Mwanangu , mateso yalipozidi sana siku za mwanzoni mwa ndoa niliona hilo halitawezekani kwa vile nina kwetu, wapo wangu, kwanini niendelee kuteseka, nikaamua kuondoka bila kuaga kurudi kwetu!
‘Kurudi kwetu nikaongea na mama, kumuelezea mateso ninayoyapata, mama alinionea huruma, lakini akasema nivumilie tu, kwani hata wao walipitia misha hayo hayo, na wakati tunaongea na mama baba akaja kutoka huko alipokuwa akanikuta naongea na mama

‘Huyu mtu kafuata nini hapa?’ akaulia hata bila salamu kwa ukali, mama mwanzoni alimwambia kuwa nimekuja kutembea, baba akauliza kwa taratibu gani, kwani kurudi kwangu kulihitaji kuwe na taarifa , yeye hajaata hiyo taarifa, ikabidi mama amuelezea kuwa nimekuja kwa shida

‘Shida gani?’ akauliza baba
‘Baba maisha ya ndoa yangu ni ya matatizo nateswa,….’nikalezea baadaye baba akasema;

‘Sikia wewe binti ndoa ina taratibu zake, huwezi kujiondokea kwa mume wako na kukimbilia kwa wazazi wako, kwa madai kama hayo, je uliwahi kuwaambia wazazi wako, …ujue pale wazazi wako ni wakwe zako?’ akaniuliza

‘Sasa hata nikiwaambia watamtetea mtoto wao, hata hivyo mtoto wako ni mkali sana, hakuna anayeweza kuongea naye kumshauri,.hata wazazi wake wanamuogopa…’akasema

‘Nikueleze kitu hicho ulichofanya sio sahihi, simama na urudi nyumbani kwako, hayo ndiyo maisha ya ndoa, usione mama yako yupo miaka mingi, maisha ni hayo hayo, ukiona umeonewa, waambia wazazi ulio nao hapo, watamkalisha chini ataonywa, ikizidi, sisi tutaitwa.. wewe unakuja hivi hivi tu unataka mimi nifungwe, ..haraka rudi kwenu..’akasema baba

‘Baba nyie ndio wazazi wangu nimeshawaambia mateso ninayoyapata , bado hamtaki kunisaidia, mimi naona sina pa kukimbilia,  ni heri nikajifie tu, mimi huko siwezi kurudi tena..’nikasema huku nikilia

‘Unasema nini wewe mtoto….unaona jinsi unavyodeka, hayo ni maisha yako na mume wako, ..unasika, ’akasema baba kwa hasira

‘Baba mimi huko sirudi,….’nikasema huku nikimuangalia mama, mama alikuwa kimia kainamia chini

‘Kwahio unaleta kiburi sio,  sasa mimi naingia ndani nikitoka hapa utaniambia vyema…’akasema baba na kuingia ndani, nikajua baba akitoka hapo aatakuwa na bakaora yake, na huwa akishika bakora yake, ujue kuna kipigo, na kipigo chake ni kikali kweli, nikaona hapo hakuna amani tena , nikaanza kukimbia kuelekea msituni,, moyoni nikisema ni bora nikapotelee msituni kuliko kurudi kwa huyo mwanaume…

Tuendelee na kisa chetu

***********

Nikawa nakimbia huku nikigeuka kuangalia nyuma, nikamuona baba akitoka na bakora yake, akawa anaongea na mama, na mama akamuonyeshea kidole muelekeo wangu, nikaona baba ananifuata kwa nyuma.

Nilikimbia hadi nguvu zikaniishia lakini sikutaka kusimama, baadaye nikajikwaa, nikadondoka chini, baba mguu ukawa umeteguka, kila nikijaribu kusimama siwezi, nilihangaika hadi baba akafika pale nilipokuwepo, akaniangalia kwa macho ya hasira akaniuliza

‘Kwahiyo unataka kwenda kujiua au..?’ akaniuliza.

‘Baba nimeumia mguu siwezi kusimama..’nikasema  baba akaanza kunichapa na bakora yake, nilipoona maumivu yanazidi nikajizoa zoa, na kuanza kutembea, baba akaona kweli nimeumia, akanishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea huko kwa mume wangu.

Ilichukua muda hadi kufika nyumbani kwa mume wangu wakati nafika, kulikuwa hakuna watu hapo uwani, nikaingia ndani na kujilaza, sikujali kufanya akzi yoyote, baadaye nikasikia mama mkwe akiuliza

‘Huyu mwanamke mvivu hajarudi, kaenda wapi, …tangu muda wote huu, keshaanza umalaya huyu akirudi mume wake lazima aambiwe, hatutaki tabia mbaya kwenye hii familia…’akasema mama mkwe

‘Nimemuona akiingia chumbani kwake, akichechemea, na kwa mbali nilimuona mwanaume, lakini mtu mzima, …’akasema wifi yangu mmoja

‘Unaona eeh, kafumaniwa, kapigwa,…mwanamke Malaya huyu.. uneniita nipate ushahidi, lakini subiri ipo siku tutamfamania…’akasema huyo mama mkwe.

Baadaye mume wangu alirudi akanikuta nimelala, akaniuliza kwanini nimelala wakati wenzangu wanafanya kazi

‘Naumwa, nimeteguka mguu..’nikasema

‘Umetegeuka mguu ! ulikuwa wapi hadi ukateguka mguu?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka

‘Nilikuwa nimeenda shambani, nikiwa njiani ndio nikategeuka mguu nikiwa njiani natembea..’nikadanganya

‘Shamba lipi hilo wakati mimi nimetoka huko shambani , nimesikia kuwa muda mwingi ulikuwa haupo hapa nyumbani, nimabie ulikwenda wapi….’akasema, na wakati anaongea nikasikia hodi huko nje, na mara mume wangu akaitwa, ikawa ni ahueni, kwani jamaa alishaanza kutaka kunipiga.

Kumbe wazazi wangu waliamua kuja, sijui ni kwa nia ya kuliongelea hilo au kuna mashauri mengine,…nahisi baba alikuwa na wasiwasi kuhuus hali yangu kwa vile yeye mwenyewe alinisaidia hadi karibu na nyumbani akarudi alipohakikisha nimeingia ndani.

Nilijua hicho kikao kitakuwa cha kunikandamiza mimi, sikutaka kutoka kabisa,nikatulia kitandani kimia baadaye nikaitwa, nilipofika mbele ya kikao, ambapo walikuwepo mama na baba yangu mzazi, mume wangu na wazazi wake.

‘Wewe umeniambia ulikwenda shambani, mbona wazazi wako wanasema ulikwenda nyumbani kwao, ulimuaga nani kuwa unakwenda huko…?’ akauliza baba wa mume wangu

 ‘Nilipitia tu kuwasalimia….’nikasema

‘Ulipitia tu, bila ruhusa ya mume wako, na ulipowasilimia ndio ukaanza kuwalalamikia kuwa unateswa …’akasema baba mkwe.

‘Ni kweli baba mume wangu kila siku unanipiga, nimeshindwa kuvumilia vipigo vyake, …’nikasema

‘Kwanini hukutuambia sisi, kwani sisi sio wazazi wako?’ akauliza baba mkwe

‘Niliogopa kuwa nikiwaambia mtaongea na mume wangu naye atazidi kunipiga zaidi…’nikasema

‘Kwahiyo wazazi wako ndio watakuja kukutetea, haya wakutetee basi…’akasema baba mkwe, na baba yangua kaingilia kati na kusema;

‘Hawa ni watoto wetu, inabidi kuwafundisha, mimi naona tujue upande wa mume wake kuwa kuna taizo gani gani, kwani kupiga kupo, lakini hadi kuumiza, ni lazima kuna sababu…’akasema mama yangu.

‘Kaumizwa wapi huyo…anajitetea bure sisi muda wote tupo naye hapa. Tuulizeni sisi..’akasema mama mkwe, na baba mkwe akasema;

‘Haya wewe mume mtu hebu tuambie kuna tatizo gani kwenye ndoa yako?’ akauliza baba mkwe akimuangalia mtoto wake, ambaye alikuwa katulia,akijizuia kuongea kuonyesha kuwa kalewa.

‘Huyu mwanamke  nampiga kwasabau husikii, mvivu , hujui majukumu yake kama mke, inabidi nimfundishe adabu, ili awe mke anayestahiki kwenye hii familia, hilo ni kosa, hebu niambieni hilo ni kosa…?’akasema mume wangu.

‘Kwanza nashangaa kusikia kuwa alikwenda kwao, hii ni ajabu kabisa, yaani uliondoka bila kuaga ukaenda kwenu kunishitakia mimi....?’ akasema mume kwa sauti ya kilevi.

‘Niliogopa, na nimechoka kupiggwa kila siku, …’nikajitetea.

‘Hili ni doa kubwa kwenye familia hii, haijawahi kutokea,…unajua umefanya kosa kubwa sana, …’akasema baba mkwe

‘Nimekosa baba, lakini kiukweli mume wangu ananipiga sana, hakuna nitakachokifanya kionekane kwema kwake, kila akirudi amelewa, na akifika huanza kunitukana, na nikiongea neno naishia kupigwa, mwili wote huu una majeraha ya kupigwa,..’nikasema huku nikilia.

‘Kwanza ukubali kuwa umekiuka miiko ya ndoa na desturi za mila zetu, na kwa vile ulikwenda kwenu na wazazi wako wakakupokea,  wao wanastahiki kulipa faini, hilo lipo wazi, mlitakiwa msimpokee mpaka mpate taarifa kutoka kwa mume wake, au sisi wazazi wake....’akasema baba mkwe

‘Hatujampokea, tulimwambia arudi huko haraka,….’akasema baba

‘Sasa mumekuja kufuata nini hapa, kama hamkumpokea, inaonekana mumemsikiliza mkaona kuwa kuna tatizo…’akasema baba mkwe

‘Tumemua kuja baada ya kuona kuwa kaumia, kama wazazi tukaona tuje tujaribu kuliongea na kuona jinsi gani ya kuwafanya hawa wanandoa waishi vyema…’akasema mama, na baba akamuangalia kwa macho ya ukali, kwani mama hakuruhusiwa kuongea mpaka apewe nafasi.

‘Huyu binti yenu ni mvivu, na hataki kufundishika, sisi tunayeishi naye tunamfahamu, lakini tukajua atajirekebisha, sasa kama imefikia hatua ya kukimbilia nyumbani kwao bila ruhusa hamuona kuwa anaweza kufanya mabaya zaidi ya hayo…’akasema mama mkwe.

‘Mabaya gani zaidi ya hayo, mimi naona tumuelekeze tu atabadilika, na tusitumie kipigo kama sehemu ya kumfundisha, …’akasema mama, na baba mkwe akawa kama kampuuza mama, akamgeukia mtoto wake, na kusema;

‘Hebu tuambie mume mtu, imekuwaje mpaka mke anakukimbia, anaondoka kwenda kwao, ina maana umeshindwa kuishi na mke?’ akaulizwa baba yake

‘Mimi sijui kama aliondoka, nimerudi nikamkuta yupo kitandani akadai anaumwa, akasema alikuwa anakwenda shambani na kiwa njiani akateguka mguu, hayo ya kulalamika, ni yake tu, …’akasema mume wangu.

‘Mnaona binti yenu alivyo muongo, kwanza mvivu, hana adabu, na pia ni muongo, hzi sio sifa njema kwa mke …’akasema baba mkwe

‘Lakini ni kweli baba…’nikajaribu kujitetea baba akaniangalia kwa jicho baya kuniashiria kuwa nimeingilia maongezi kabla sijaruhusiwa, nikanyamaza na kuinama chini.

Wazazi wangu wakaomba msamaha na kama wazee wakajaribu kutafuta njia bora ya kuwafanya watoto wao waishi kwa amani. Mume wangu akasema;

‘Kwanza ni ajabu wazazi wangu kuja hapa hata bila taarifa…sijui mumekuja kuleta kesi dhidi yangu kuwa nampiga mwenzangu au namtesa kaama anavyodai,..?’ akauliza mume wangu.

‘Kama tulivyosema binti alipitia nyumbani na katuoa hayo malalamiko, na kwa vile kaumia tukaona tuje kumsalimia, na tukaona tuliongelee na hili….’akasema baba kwa upole.

‘Wazazi wangu samahani kuwaambili hili kuwa kiukweli mimi naona mnamdekeza sana mtoto wenu, mimi najaribu kumuweka sawa, ili aishi sawa kama nyie mnavyoishi, lakini naona sasa kama mnaniingilia ndani ya ndoa yangu..’akasema mue wangu kwa sauti ya kilevi, japokuwa alikuwa akijaribu kuongea kwa kuicha asionekana kuwa kalewa.

‘Hapana sio swala la  kumdekeza,…kama wazazi tunatakiwa tuwasikilze wote, ili tuone kama kuna tatizo…’akasema baba

‘Kama mnaona namtesa mtoto wenu, ..samahanini sana kutuia kauli hii, ila kiukweli, hilo ni kosa lenu haya yasingelitokea kama mngelikuwa mumemlea vyema mtoto wenu…sahaman kwa kutumia lugha hiyo ila huo ndio ukweli…, nahisi anahitajia mafunzo, na mimi nitamfundisha, ikishindikana, basi nitamtafutia mwenzake, maana mimi sitaki shida….’akasema mume wangu.

‘Usifanye hivyo, ujue mke wako bado ni mdogo sana kwako, unahitajika umuendee taratibu, umulekeze, sio kutumia nguvu sana….’akasema mama yake.

‘Ana udogo gani huyu, …kadekezwa huyu mama, musitake kumuharibu, sasa mimi nasema hivi, sitaki kuingiliwa kwenye ndoa yangu, kwani kila mtu ana ndoa yake, huyu mimi niachieni, atanyooka tu, na sijashindwa, nikishindwa, wenyewe mtaona, kwani mwanamke nip eke yake. ..’ akasema mume wangu.  

‘Sisi tunakuomba upunguze ukali, wewe umezidsha ukali, mimi kama baba yako nakupa onyo, nimeishi na mama yako hadi leo, sio kwamba hatukosani,  tunakosana sana, lakin hajawahi kwenda kwao kulalamika, …’ akasema baba mkwe huku wakiangaliana na mkewe.

‘Na sio kwamba sijawapi kumpiga,..inatokea mpaka tunapigana, lakini mwisho wa siku tumevumiliana hadi ikafikia hii leo…sasa na nyie mjifunze, wewe mume, ujifunze kuishi na mke na mke ajifunze kuishi na mume…..’ akasema baba wakiangalia na mkewe.

Basi kikao kikaisha hivyo, cha ajabu siku mbili tatu mue wangu akawa mpole, lakini ilikuwa kwa muda tu , baadaye adhabu, vipigo, manyanyaso yakarejea vilevile.

Siku zikaenda , mwaka ukapita, nikaanza kama kuzoea hiyo hali, lakini likazuka tatizo jingine , mimi sikubahatika kupata mtoto mapema..hili likawa ni tatizo, mwanzoni sikumsikia mume wangu akilalamika, nilianza kusikia kwa mawifi zangu..

‘Huyu wifi vipi mwaka  huo unaingia wa pili hakuna dalili, …’akasema wifi akiongea na mama yake.

‘Kama mtu mwenyewe yupo hivyo mvivu haelekei unafikiri kuna kitu hapo…’akasema mama mkwe, hawakujua kuwa nipo karibu, waliponiona wakabadili maongezi

 Hili la mimi kuchelewa kuzaa lilianza kama chokochoko toka kwa wifi zangu, na baadaye likafika kwa wakwe zangu rasimi. Ikawa nasumbuliwa kiaina kwa dharau na kukejeliwa kuwa mimi nimekuja ndani ya familia hiyo kula tu, lakini sina faida yoyote.

Na baadaye mume wangu naye akaingia kwenye mkumbo, akirudii akiwa kalewa, maneno yake na vipigo vikawa vinaenda huko huko kuuliza eti mimi nina faida gani ndani ya familia hiyo.  Kazi yangu ni kula tu….

‘Wewe unakula tu, unanenepeana kama nguruwe, huna faida yoyote humu ndani, angalia wanawake wa rika lako wana watoto wangapi, wewe hata wakutuma chumvi hayupo…una faida gani humu ndani, lazima nikutafutie mwenzako, atakayeleta matunda ndani  ya hii familia…’ akawa anasema baba yako huku anitoa kipigo, mkono wake ulikuwa mwepezi sana kupiga.

Nililia, nikijaribu kuwaza kosa langu hapo lipo wapi, kwani mimi nimependa iwe hivyo, hata mimi nataka mtoto, nikamwambia mume wangu kwa upole;

‘Tuvute subira haya yote sikuyataka mimi, kuzaa ni majaliwa ya mungu….’nikasema

‘Wewe una tatizo, sibure…’akasema na kulala, na akilala hukoroma kama simba mimi nikabakia kuwaza, nikawa sipatu usingizi , nikijiona mimi ni mtu wa shida tu, hadi kufikia kujuta kuzaliwa mwanamke.

‘Mwanangu mateso haya, kashifa na kejeli nikayavumilia hadi ikatimia miaka mitatu ndani ya ndoa, na sikuwa na dalili yoyote ya mimba, na wanafamilia wakakubali kuwa mimi kweli ni mgumba, sizai kwahiyo nina mawili, aolewa mke mwenza, au niondoke kwetu….

‘Kwa ujumla kama ingelikuwa ni uwezo wangu mimi nilikuwa tayari kuondoka kwenda kwetu…hata siku moja nikamwambia kuwa kama ananiona simfai basi anirudishe kwa wazazi wangu…’nikasema

‘Nikurudishe kwenu, unajua nimekulipia ngombe ngapi, unajua baba yako namdai kiasi gani, hapa hutoki, utakaa hapa ili nifidie ngombe zangu na mali yangu,kama huzai basi utakuwa mfanyakazi wa hapa…’akasema bila hata aibu.

Kauli yake ilikuwa kweli, kwani nilianza kutumikishwa sasa kama mtumwa, zaidi ya mwanzoni, nikilalamika, kauli za kejeli ni hizo hizo, kuwa mimi nimekuja hapo sina maana, sizai, kazi yangu kula, kwahiyo ni lazima nifanye kazi ili niweze kupata chakula… nilikaa humo kama mtumwa, kufanya kazi za kila aina, shamba, mifugo , na mwisho wa siku kuzalilishwa.

Haikupita muda akaolewa mke mwenza....

NB: Haya mambo yameanza, mke mwenza atapata mtoto...


WAZO LA LEO: Ndoa ni kusikilizana, mnapoona mjue kuwa mke na mume ni kitu kimoja, kukitokea tatizo nyote wawili mnahitajia kukaa pamoja na kuliongelea hilo tatizo kila mmoja awe na naasi na kujielezea, ili kijulikane chanzo cha tatizo ni nini….kutumia nguvu, kauli chafu, dharau, kunyanyapaana sio misingi ya ndoa, tukumbuke kuwa asili ya ndoa ni raha, na sio karaha.

Ni mimi: emu-three

No comments :