Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, December 16, 2014

NANI KAMA MAMA-7


Ni kweli mama alikuja na mkoba fulani mweusi, hakutaka  upokelewe, na hadi sasa sijui huo mkoba upo wapi,  Ina maana kweli humo ndio kuna vitu alivyotaka mjukuu wake arithi,….?
                   
Waliambiwa na huyo mganga wao: ‘Kuingiwa na uchawi huo kunasumbua sana hasa kwa watoto, ndio maana mnaona mtoto wenu anaumwa, je mliwahi kuabiwa mtoto wenu anaumwa nini huko hospitalini, hakuna ugonjwa, kama hakuna ugonjwa tatizo ni nini….

Mke wangu alikuwa chumbani , sikujua ameshatoka na kwa muda mama anamshika mtoto kichwani, mke wangi aliona, kwa vile shemeji yaani mdogo wa mke wangu alikuwepo wakati wamekwenda huko kwa mganga, na walishaambiwa kuwa mbaya wa familia huwa anamshika shika mtoto kichwani kama anamumbea wakaambiwa kuwa hiyo ni dalili kuwa mtoto anaingiziwa uchawi….

Shemaji yangu aliyekuwa kambeba mtoto alikuwa akimuangalia mama kwa chuki pale alipokuwa kaweka kiganja cha mkono kichwani kwa mtoto, lakini hakuwa na uwezo wa kumzuia..

Mke wangu akawa keshatoka yupo mlangoni akaona lile tendo..kwa hasira na chuki,  akakurupuka kutoka pale mlangoni na kumrukia mama, na kumsukuma mama kwa nguvu zote,  msukumo ambao ulimfanya mama adondoke chini na kwa bahati mbaya kichwa chake kikagonga kwenye meza na mama akapoteza fahamu.



‘Nilipoona hivyo, kwanza nilijua labda mke wangu yupo kwenye hao mashetani yake, lakini nikagundua ni mzima, hapo hapo nikasimama kwa hasira na kumsukuma mke  wangu akapepesuka kutaka kudondoka,..

Kitendo kile kilimfanya mke wangu apandwe na hasira, akawa ananiangalia kama anataka kunimeza, Na kupigana name kwa hasira , lakini mimi sikutaka kuendelea kugombana naye,  mawazo yangu yalikuwa kwa mama, je kaumia, nikamfuata mama pale chini, nikamkagua alikuwa kapoteza fahamu, nikaona nimbebe hadi kwenye sofa,

Mama alikuwa kimiya kama aliyekata roho, nikajua sasa mama ameshakufa nikaanza kulia, na kilio na machozi yale yakamzindua mama,

Mama alipona mtoto wake analia , huruma ikamjaa, ndipo akataka kumuhadithia mtoto wake kuhusu  maisha yake ya  nyuma…

Tuendelee na kisa chetu….

************.

‘Mwanangu huwezi amini kuwa baada ya kujifungua wewe kwa shida, kwa maumivi makali, nilikaa muda mrefu  bila kujijua,..sikuwa na kumbukumbu za nyuma, sikuwa nakumbuka kabisa yaliyotokea huko nyuma, ni kama vie nilizaliwa siku ile nilipojifungua, hali hii iliniandama kwa muda mrefu, nikawa nakumbuka kidogo kidogo baadhi ya matukio, lakini sio yote.

Nahisi nilipodondoka hapa, aliponisukuma mke wako,  na kujigonga kichwa kuna kitu kimetokea kwenye kichwa changu….nahisi kurejewa na kumbukumbu za nyuma, …..’akatulia

‘Wakati ….kwani likuwaje, nililala au nilipoteza fahamu?’ akauliza mama

‘Naona ulipoteza fahamu…’nikamwambia

‘Basi mimi nilijiona kama nimelala, na nikawa naota , ilikuwa ni kama nipo kwenye njozi, na kuonyeshwa matukio yaliyopita…na kiukweli sasa nimeanza kukumbuka mengi yaliyotokea huko nyuma, ooh, ina maana hata, …’ mama akatulia na kushika kichwa.

‘Ni kweli ndivyo ilivyokuwa mwanangu,…mengi nlishayasahau kabisa…sijui hata huyo baba yako yupo wapi, mungu ndiye anayejua kwa hayo aliyonifanyoa..ndio maana naona nikuhadithie yote yaliyotokea,…’akatulia

 Siku nilipotoka hospitalini baada ya kukuzaa wewe sikuwa najua ni kitu gani kilitokea huko nyuma nilichokuwa nakumbuka ni maumivu, ….’akatikisa kichwa kama anajaribu kukumbuka jambo.

‘Wakati nimepotea fahamu mimi nilihisi nimelala, na ndipo Hivi sasa nimeyakumbuka yote yaliyopita. Hali yangu ya zamani ilinijia kama picha, na mwisho wa picha hiyo nikaiona sura yako iking’ara kama nuru, na nilipozindukana na kukuona ukinitizama,  nikasema moyoni, labda nuru ile ni taswira ya matumaini baada ya mateso ya miaka nenda rudi.

Najuta kwanini nimeiota hii ndoto, ni kwasababu nahitajika kukuambia ukweli ambao huujui na dunia na walimwengu wanaweza kuja kukudanganya, kama mlivyodanganywa sasa hivi,… machungu na mateso yaliyopita ni maabaya sana, lakini inabidi nikusimulie yote mwanangu.

Mwanangu ndani ya ndoto, wakati nimezimia ilikuwa ikinielezea jinsi gani nilivyoteseka hadi kukupata wewe..ni ndoto ya haraka haraka sana, lakini imenisaidia kuyakumbuka yote…

                              ********

‘Mwanangu mimi niliolewa na baba yako bila ridhaa yangu, kama ujuavyo maisha ya kijijini!Wazazi wangu walikutana na wazazi wa baba yako,wakakaa na kukubaliana bila mimi kuwepo wala kujua kinachoendelea, nikaja kuambiwa kuwa nimepata mchumba, kwahiyo wiki ijayo ninaolewa Nilikuwa bado mdogo hata maana ya kuolewa sikuwa naifahamu..kwahiyo nilipinga sana.

‘Mama mimi sitaki kuolewa, mimi nataka kuishi na nyinyi..’nikasema

‘Mwanangu maisha ndivyo yalivyo, unaishi na wazazi wako lakini inafika muda unatakiwa uachane nao uende ukaanze maisha yako ili na wewe uwe na familia yako kama sisi..’akaniambia mama

‘Lakini mama mimi bado mdogo, sijui nitaishije huko, naogopa mama, na mume mwenyewe simfahamu, sijawahi kuongea naye…’nikajitetea

‘Kesho atakuja shangazi yako atakufundisha kila kitu usiwe na wasiwasi…’akaniambia mama

Niliwapinga sana wazazi wangu, lakini hawakukubali kwani walishapokea hata mahari. Na muoaji ni mtu anayetokea ukoo unaogopewa sana, ni matajiri , wana mali nyingi, lakini ni wakatili kupindukia. Baba hakutaka kabisa kusikia kauli yangu hiyo ya kukataa kuolewa, alikuja juu na kusema.

‘Hivi na wewe unataka unizalie hapa nyumbani kama dada yako, dada yako alipata mchumba akakataa kuolewa hivi hivi…, na matokea wakamzalisha hapa nyumbani, ana bahati mume aliyempa mimba alikubali kuwa mimba ni yake akamchukua…sikutaka hata mahari yake, ila alilipa faini,…sasa na wewe unataka uwe hivyo hivyo… sikubali, …sikia utaolewa …nataka nikurudi hapa nisikie hiyo kauli imabadilika!

Baba aliondoka, na tulijua kaelekea kulewa, na akirudi hapo nyumbani hakukaliki, hapo mama akanisihi sana nikubali…

‘Mwanangu unamfahamu vyema baba yako akirudi hapa…tutahama hii nyumba tukiwa na majereha, ni bora ukubali ili balaa lisije kutukuta, …’akanisihi mama

Mwisho wa siku nilikubali, kwani wazazi ni wazazi tu. Nikaolewa na baba yako, na kuhamia kwenye ukoo wao. Siku ya kwanza nilianza kuipata joto ya jiwe, kwani bado nilikuwa msichana mdogo bado bikira, na baba yako alikuwa mkatili  mjeuri, hakujali kuwa mimi bado mdogo,nilihitajika kulelewa hatua kwa hatua,

 Baada ya harusi, mimi nikasindikizwa hadi nyumbani kwa huyo mume wangu, tulifika katika makazi mapya, nisiyoyafahamu, na kukaribisha kwenye nyumba niliyoambiwa kuwa ndio nyumba ya mume wangu.

Kiujumla wao walikuwa na uwezo , nyumba nzuri, wana utajiri wa mali,…lakini utajiri wa kijijini unafahamu, …bado nilihitajika kufanya kazi, hakuna cha mfanyakazi huko,…

Basi siku hiyo ya kwanza, tulpofika mume wangu huyo akatoka na kuniacha chumbani, yeye akaenda kusherehekea na marafiki zake, na baadaye sana nikiwa nimepitiwa na usuingiza  akaja chumbani. Alipoingia alikuwa akinuka pombe, kalewa, akanivamia …

‘Mimi kwasababu ya utoto nikawa sijui nini anataka kwangu,…nilivyofundishwa na shangazi sikuwa nimetilia maanani, unajua utoto tena, nilikuwa bado nina akili za kitoto japokuwa mwili wangu ulishapevuka… zaidi nikaishia kusukumana naye nikijitahidi kujikwamua kwenye mikono yake, lakini yeye alikuwa na nguvu sana..kuna muda kwasababu ya ulevi nilimsuka akadondoka chini ya kitanda. Hapo nikawa nimepandidha hasira.

 Alinijia sasa kama mbogo aliyejeruhiwa akanishika na kunikaba shingo karibu kupoteza fahamu,…mimi nikawa, nilijiuliza hii ndio maana ya ndoa, nikaanza hata hivyo sikuacha kujitetea, na kufanya vile nikawa nazidi kumpaandisha hasira, akaniambia;,

‘Wewe mwanamke, mimi nimetoa mahari yangu kibao na umeshakuwa mke wangu, unatakiwa ukubali na ufanye kila nitakalokuambia, na ujue hapa unitimiza haki ya ndoa,…hukuambiwa unatakiwa kufanya nini kwa mume wako,  nashangaa unaleta ukaidi, basi ngoja nikuonyeshe kuwa mimi ni nani,…’

Mwanangu kilichofuata hapo ni vibao, mateke, mangumi, na alipochoka kunipiga, akafanya alilotaka kulifanya. Sitaki kukumbuka kilichotokea siku hiyo, kwani ni mateso ya hali ya juu niliyoyapata..hapo ndipo mateso yangu yalipoanzia, mateso maumivu, kusimangwa….ni taabu isiyoelezeka..

Baada ya siku hiyo, ikawa ndio desturi, na siku zikawa zinaenda mimi nikijua labda ndio maisha ya ndoa, …kupigwa, mateso,  kufanyishwa kazi kama punda, na mwisho wa siku unazalilika, na sikuona raha yoyote ya ndoa. Mwanangu siku za mwanzo nilikuwa naomba usiku usifike, usiku kwangu ilikuwa ni jela, yenye mateso…

Mwanangu nakusimulia haya , na huenda nisingetakiwa kukusimulia hili, lakini nakuhadithia kwa uchungu ili uone jinsi gani mma yako nilivyoteseka, tangu naolewa, na uone uvumilivu gani niliouonyesha mbele ya baba yako, na nini matokeo yake, ambayo ndiyo haya, ndio haya…ndio haya mnayonipa mimi, leo hii mimi naitwa mchawi …

‘Hivi ningeshindwa kuyavumli hayo mateso nikaamua kuukimbia, au nikajiua, ungelizaliwa wewe, leo hii umekua, umekutana na mke, mke hajui umetoka wapi, anakuja kuniita mimi mchawi…anafahamu nini maana ya uchawi, kama anafahau hata yeye ni mchawi….’mama akaongea kwa huzuni,

Mama alipofika hapa alishika kichwa na machozi yakamtoka kwa wingi.

Mama aliendelea kunisimulia kuwa, mateso yalipozidi sana siku za mwanzoni mwa ndoa aliona hilo haliwezekani ana kwao ana wazazi wake kwanini akubali kuteseka!

‘Siku moja nikaamua kutoroka na kurudi kwa wazazi wangu, ili niwasimulie adha na mateso ninayoyapata, lakini sheria za ndoa zilinifanya nirejeshwe kwa mume wangu.

 Sababu za kumrudishwa sio kwasababu ya sheria za ndoa tu, lakini mama yangu aliolewa kwa ngombe nyingi na aliolewa kwenye ukoo wenye utajiri wa ng’ombe, na ukoo huo unaogopewa sana. Je wangeliwezaje kuzirudisha hizo ngombe, wakati baadhi yake waliuza ili wapate hela za sherehe ya harusi. Na nyingine zimeshatumika kwa mahari ya ndugu zake!

‘Mwanangu ndoa ndivyo ilivyo, hata sisi tuliyapitia hayo, lakini baadaye unakuja kuyazoea hayo maisha, wewe vumilia tu,…’akanisihi mama.

‘Hivi mama unajua ni mateso gani ninayoapaat huko, kupigwa kunyanyaswa, kfanyishwa kazi kama punda, ndio mnayotaka kwangu,…mumekula nini chao ambacho mimi natakiwa kukilipa..?’ nikawauliza

‘Mwanangu mara nyingi baba yako akiwa na shida, huwa anakwenda kwa huyo jamaa kukopa kwahiyo ana madeni mengi sana kwake, pia umeolewa kwa mahari ya ng’ombe nyingi ambazo nyingine ndio hizo zimesaidia kaka yako kuoa..na ningine tuliuza ili kupata pesa za sherehe yako, sasa tutapata wapi hizo ngombe tukiambiwa turejeshe….’akasema mama

‘Mama ina maana mimi ndiye nabebeshwa gharama hizo, ina maana mimi kwa vile ni mwanamke, basi sina haki, mimi ni kitu cha kuuzwa kulipiza madeni yenu…’nikasema kwa uchungu, mama alinionea huruma lakini hakuwa na la kufanya. Baba aliporudi akaniona nipo haki akaanza kufoka na kuuliza nimefuata nini

‘Hivi hutaki mtoto wako aje kukutembelea?’ akauliza mama

‘Bila ya taarifa na mume wake yupo wapi?’ akauliza baba

‘Msikilize kwanza mtoto wako ana matatzo gani hebu muone alivyokonda…majereha hayo usoni yametoka wapi?’ akauliza mama

‘Hayo ni mambo ya o ya ndoa, kama kungelikuwa na tatizo tungeliambiwa kwa utaratibu, sio kwa yeye kuja hapa bila hata a taaraifa, umefikuzwa?’ akauliza baba.

‘Baba nateseka sana huko, napigwa kila siku, nafanywa kama mtumwa wa familia,..’nikasema

‘Unaonaeeh, niliwahi kukuambia kuwa mtotow ako huyu ni mvivu, akifika kwa mume wake atatutia aibu sasa unaona matokeo yake…’akasema baba

‘Baba lakini mimi sio mvivu, mbona kipindi nipo hapa mwenyewe ulikuwa ukisifia kwa kufanya kazi,….’nikasema japo kuwa siku aanasema hivi kesho anasema hivi lakini kwa ujumla mimi nilikuwa mchapakazi mnzuri.

‘Sikia wewe binti ndoa ina taratibu zake, huwezi kujiondokea kwa mume wako na kukimbilia kwa wazazi wako, unataka mimi nifungwe, unataka sisi tueleweke vipi kuwa tunakudekeza, nakuambia hivi ..haraka rudi kwenu..’akasema baba

‘Baba ni heri nikajifie tu, mimi huko siwezi kurudi, nikirudi huko wataniua,..’nikasema

‘Unasema nini wewe mtoto, huwezi kufanya nini, ni nani kakufundisha ukaidi huo..’akasema baba akiniangalia kwa hasira.

'Lakini baba, unanona nilivyo, majereha mwili mzima, hivi mnataka nife ndio mjue kuwa nateseka...'nikasema nikimuangalia mama, kama atanitetea

'Sasa mimi naingia ndani nikitoka, nikakukuta bado upo hapa nyumbani kwangu utaniambia vyema…’akasema baba na kuingia ndani, nikajua baba akitoka hapo atakuwa na bakora yake, na huwa akishika bakora yake ujue kuna kipigo, na kipigo chake ni kikali kweli, nikaona hapo hakuna amani tena , nikamuangalia mama nikamuona kainama chini, nikajua hakuna utetezi hapo.

Nikageuka na kuanza kukimbia kueleeka msituni, moyoni nikisema ni bora nikapotelee msituni kuliko kurudi kwa huyo mwanaume…

NB: Tuishie hapa kwa leo

WAZO LA LEO: Ndoa bila hiari ya muolewaji inkuwa haijakamilika, na ni makosa, kwani ndoa ni makubaliano kati ya wawili muoaji na muolewaji na hujengwa kwa mapenzi ya dhati, Tusipende kuwalazimisha mabinti zetu kuolewa kwa nguvu kwa waume wasiowataka, kwasababu ya tamaa ya mali. Madhara ya ndoa hizi ni makubwa kuliko hizo mali zenyewe. Tuwape uhuru waowaji na waolewaji ili waje kuishi kwa upendo na amani.




mimi: emu-three

No comments :