Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, December 11, 2014

NANI KAMA MAMA-4


Nilipofika kazini nikakuta wafanyakazi wamesimama kwenye ubao wa matangazo,wengine wanaondoka wakicheka wengine wakisikitika, na mimi  nikasogea  kuangalia, hapo nikaona maandishi makubwa yameandikwa; `ORODHA YA WALIOPUNGUZWA KAZI NA WATAKAOENDELEA NA KAZI. Wafuatao wafike ofisi ya utawala, waonane na meneja utawala, kwa ajili ya kupata mkataba mpya au kupata barua za kupunguzwa kazi.

Niliposoma maandishi hayo mwili ukalegea, miguu ikaisha nguvu, nikageuka kuwaangalia wenzangu ambao nao kila mmoja alikuwa akipepesa macho kusoma majina yaliyopo, hapo ni kila mtu  lake…

Nikaanza kusoma majina moja baada ya jingine, na kila niliposogea mbele, nikawa napumua nikijipa moyo kwa matumaini kuwa jina langu halipo, kwani nilikuwa mchapa kazi hodairi kilichoharibu ni haya matatizo ya kifamilia na yametokea karibuni tu, hawawezi kuchukua matatizo ya miezi kadhaa, wakasahau juhudi zangu za miaka mingi nyuma, nikawa najipa matumaini hayo huku nikiendelea kusoma majina

Nikafika karatasi ya mwisho, katatasi hiyo ilikuwa na majina nusu ukurasa, nikaanza kusoma la kwanza, nikawa nashuka chini, la pili, la tatu….......

Tuendelee na kisa chetu

***************

Nikafika jina la mwisho, macho yakashikwa na ukungu, nikawa sioni vyema, japokuwa herufi za mwanzo zilikuwa za jina langu,…nnikafuta macho na kuinama chini nikainua kichwa, nikasoma kwa sauti…

Kweli lilikuwa jina langu, nikakuna kichwa nikainama nikauka kuangalia wenzangu, wengi walishaondoka, waliobakia ni kaam mimi, kila mmoja akilalamika ndani ya nafsi yake, na baadaye wote wakaondoka nikabaki mwenyewe, sijui ilitokea je, nikahisi kizungu zungu, na kudondoka chini.

Nilibaki pale chini kwa muda, nikajizoa zoa, na kujipa nguvu, nikijua kuwa hayo yameshatokea na mimi ndiye muhusika mkuu, hakuna wakunionea huruma hapo nisipowajibika picha itakwisha, …., nguvu ziliponirudia nikainuka na kuelekea masijala ambapo kulikuwa na ofs ya meneja utawala,  ili kupewa barua yangu.

‘Yah, mjumbe, umefika, au familia bado inasumbua, natumai umeangalia orodha je jina lako lipo?’ akaniuliza kama vile hajui

‘Lipo bosi…’nikasema

‘Pole sana, ndio maisha, usikate tamaa, mlango mmoja ukifungwa mwingine unafunguliwa, huwezi jua, albda kuna sehemu nyingine bora inakusubiria sehemu nyingine, cha muhimu ni kujipa moyo na kupambana…’akasema huku akinikabidhi barua yangu.

Kwa mkono unaotetemeka nikapokea hiyo barua nikafungua na kuanza kuisoma, maelezo yaoo ya kisiasam kuwa kutokana na gharama za utendaji kuwa kubwa kampuni imeona ni bora ipunguze wafanyakazi, na kama hali itakuwa nje baadhi wataitwa tena, na maelezo kuwa malipo ni mwezi mmoja , na mshahara wa mwezi huo, hakuna pesa ya usafiri maana wote wamechukuliwa kama wakazi wa Dar-esalamu.

Nikafungua ukurasa unaonyesha mahesabu, kama nilivyotegemea, deni nililokopa lilikatwa kwenye mafao yangu, kwahiyo sikuwa na cha kuchukua zaidi ya kusubiri kile kinachoitwa ‘akiba ya penshion ya kustaafu au kuacha kazi. Nayo sio nyingi kutokana na mshahara wenyewe ulivyokuwa mdogo. Nayo natakiwa kusubiri miezi kadhaa, ili uanze kuomba, na ukiomba unaweza ukazungushwa wee, kwahiyo pesa hiyo sio ya kutegemea kwa sasa, sasa nitaishije...

‘Vipi umeshasoma, kama tayari weka sahihi yako, na chukua karatasi ya malipo nenda kwa mhasibu….’akasema

‘Ipo wapi hiyo karatasi ya malipo?’ nikauliza na meneja utawala akawa anapekua pekua, siku kama alifahamu kuwa sina cha kulipwa au alijifanya kupoteza muda

‘Mhh, naona hakuna, hebu hiyo barua yako, nione…’akasema na akachuka ile barua akasoema, halafu akasema;

‘Haiwezekani ina maana ulichukua deni kubwa kiasi hiki, …ilikuwaje, madeni mawili kwa wakati mmoja, …mmh, ndio matokea yake haya mkiambiwa msikope kupita kiasi mnaona watu wabaya, sasa unaona, hakuna cha kulipwa hapa…mafao yako ukitoa madeni unbakia bado unadaiwa na kampuni…’akasema

‘Kwahiyo mnataka kusema nini…?’ nikauliza


‘Mimi kazi yangu ni kufuata taratibu za kampuni, na kuhakikisha zinatekelezwa,  kuanzia sasa wewe huhesabiki tena kama mfanyakazi wa kampuni hii, unachotakiwa ni kukabidhi vitu vyote vya kampuni, na tunakutakia maisha mema....’akasema

‘Nyie watu mbona hamna huruma, ina maana nyie kukaa kwenye madaraka mnajiona mumefika, ....sawa tu,, lakini mkumbuke  mwenzako akinyolewa na wewe utie maji, mateso haya ninayoyapata kama niliomba yanipate, basi na nyie hamtakuja kuyapata...nashukuruni sana....’nikasema

Meneja utawala akaniangalia kwa macho ya huruma, lakini akibenua mdomo kwa dharau na kusema;

‘Sasa wewe ulitaka mimi nifanye nini...haya sio maamuzi yangu binafsi, ni maamuzi kutoka kwa idara yako, na ukapita mjadala wa kina, mwenyewe umeona utendaji wako ulivyokuwa, mwanzoni ulijituma baadaye ukaona familia yako ni bora zaidi,....’akasema

‘Lakini mika yote nilikuwa mtendaji mnzuri nimechaguliwa mfanakazi bora mara tatu..ina maana hiyo haonyeshi kuwa nilikuwa mtendaji bora…hii miezi mingapi ya matatizo imefanya nionekane sio mtendaji bora?’ nikauliza

‘Hayo yote yalionekana, lakini imeonekana .huna jipya,..hata kaam ungeliachwa hali ingeliendelea kuwa hivyo, maana kama ni matatizo yangeishaje..sana sana utazidi kuipa kapuni hasara….’akasema

‘Kwakweli tenda wema mara mia kosa moja wema wote unasahaulika ndio hivyo….’nikalalamika.

‘Ndugu cha  muhimu ni kuhakikisha unamalizana na mambo yako ya kifamilia, ili ukipata kazi sehemu nyingine usije ukafanya kosa kaam hili, jifunze jinsi gani ya kutataua matatizo huku sheria za kampuni unazifuta…ni kweli wewe ni mtedaji bora, lakini umeonyesha udhaifu mwishoni, kama umeshindwa kutatua matatizo yako ya kifamilia je ukipewa uongozi utawezaje kuongoza, kuwajibika ili kampuni iendelee kuwepo…’akasema

‘Mimi naomba nionane na mwenye kampuni, maana kunifanyia hivi ni kama kutaka nikafe, mtoto anaumwa sasa hivi yupo hospialini, hajiwezi, , mke anaumwa, sina pesa,nadaiwa kodi ya nyumba, hapa sina hata akiba ya kuanzia maisha, nyinyo leo hi mnanifanyia hivi, mumeshahau jasho langu lililomwagika kwenye kampuni hii,.....’nikasema.

‘Nielewe ndugu haya sio maamuzi yangu binafsi , ama kwa mwenye kampuni, yeye haya hayamuhusu, yeye katupa sisi majukumu yote, …yeye ni mtu wa miwsho wa kuhalalisha tu, hakujui wewe, hajui utendaji wako wa kazi, anatujua sisi washauri wake..’akasema

‘Kwahiyo nyie ndio mlimshauri kuwa mimi sifai…?’ nikauliza

‘’Utendaji wako unajieleza…nimekuonya mara ngapi, au umesahau…’akasema

‘Lakini umenionya miezi hii ya karibuni baadaya kuaptwa na mataizo ya kifamilia, huku nyuma uliwahi kunionya, au ilikuwa ukinipa pongezi za utendaji bora, hayo ya nyua mumeyasahau…?’ nikauliza
‘Ulimi wako, ndio umekuponza, unakumbuak..nilikuambia chunga ulimi wako, …sasa ndio hayo,..nakupa tu kama dokezo, ukiwa sehemu ya kazi usijifanye wewe unajua kuongea sana, kumbuka kila mtu kaja na mikono yake nyuma baraua ya maombi mbele…hapa ndio unajua kuwa , kila mtu kaja na hamsini zake…’akasema

‘Mimi naomba nikaonane na mwenye kampuni..’nikasisitiza na yeye akasimama na kuondoka.

Nilikaa pale kwa muda, nilipoona harudi nikatoka nikitaka kwenda kumuona mwenye kampuni, na wakati natoka nikaona mwenye kampuni akitoka na huyo meneja utawala, kuonyesha kuwa walikuwa wakiongea , nikaona sio vyema kwenda oja kwa moja kwa mwenye kampuni, nikamsubiria meneja utawala, ambaye alikuja ofisini kwake nikamuuliza;

‘Je umemueleza mwenye kampuni tatizo langu?’ nikamuuliza.

‘Amesema sheria ni msimeno , hakuna atakayependelewa kwa vile tu ana matatizo yake ya kifamilia, tukifanya hivyo wengine watalalamika, kwahiyo,...kasema kampuni itakusaidia nusu ya deni lako la kawaida, sio deni kubwa,...deni kubwa kampuni imesema haitawajibika nalo, kwani haina pesa ndio maana imefikia hatua ya kupunguza wafanyakazi, deni kubwa utalipa wewe mwenyewe...’akasema meneja utawala

‘Lakini hata hiyo nusu ya hilo deni dogo  ni shilingi ngapi, ni pesa ndogo tu ya kunifiksiha siku mbili tatu.....’nikasema

‘Kwahiyo tukate deni lote ndivyo unavyotaka, shukuru hicho kidogo ulichopata, nenda kanisubirie nje, nikamilisha barua yako mpya....’akasema akienda kutayarisha barua nyingine, nikatoka hadi sehemu ya kusubiria hadi pale nilipoitwa kuchuku barua yangu nyingine.

Haya nenda kwa mhasibu ukachukue pesa yako…’akaniambia

Mambo yameanza hapo, mke ana-mashetani, mtoto anaumwa magonjwa yasiyojulikana , kazi sina, pesa sina…pale nilipopewa hizo pesa an kuona si pesa kitu.nililia kama mtoto, nikarudi tena kwa  meneja utawala nikampigia magoti, ili angalau wanisamehe hilo deni, kwani nyumbani mtoto anaumwa, sina hela ya matibabu, mke anaumwa anahitaji uangalizi, kodi ya nyumba inanisubiri…lakini meneja utawala hakuwa yule ninayemfahamu tena, hapo kawa kama askari

‘Ondoka, nimekuvumilia vya kutosha, niwaite walinzi wakutokea kwa nguvu….’akasema kwa hasira. Hapo nikaona sina la kufanya nikaondoka zanu huku nikiangalia ajengo ya kampuni, nikikumbuka kuwa sisi ndio waanzilishi, tulipigana usiku na mchana na mwenye kampuni hadi hapo ilipofikia, lakini leo nafukuzwa bila hata thamani, nimeshasahaulika…

 Nilijikuta natembea huku naongea mwenyewe kama mtu aliyepagawa, nikielekea nyumbani, na kwasababu ya kuchanganyikiwa, nikajikuta nipo kati kati ya bara bara bila kujijua...

Wakati natembea sikujua kuwa nimeshafika barabara kuu,  nikawa natembea kati kati ya barabara, sisikii sioni, akili yangu ilikuwa moja, …dunia sasa sio yangu….nilikuwa mbali nikiwaza dunia nyingine isiyokuwepo, akili hafanyi kazi, sasa nikawa nakatisha ile barabara kulekea upande wa pili.

Nilisikia honi zikipigwa,  tahamaki, nikajikuta nikipigwa na kikumbo kikubwa, na mara nikwa napaa hewani, nikatua chini, sio chini ni kwenye kitu, kumbe nilikuwa nimegongwa na gari, na hapo nilipotua, ilikuwa sehemu ya mbele ya gari, .....giza likatanda, sikujua kilichoendelea baadaye.

******


Nilipozindukana nilikuwa hospitalini nikiwa nimefungwa mabandeji , na mwili ulikuwa unauma kila sehemu nikasikia mtu akisema;

‘Ana bahati sana huyu mtu, kwenye vipimo vya mwanzo, inaonyesha hajavunjia mfupa labda huku kwenye mbavu, ambapo tunahitajika kusubiria vipimo vya x-rays, na pia inahitajika kupimwa utra-sound, ili tuone kama ndani kuna madhara ...’akasema huyo mtu nahisi ndiye docta.

Na mtu mmoja ambaye nahisi ndiye dereva aliyenigonga akasema;

‘Gharama nyingine inabidi azibebe yeye mwenyewe, kwasababu kosa ni lake yeye mwenyewe, hata trafiki wameliona hilo....anaonekana alikuwa na mawazo mengi wakati anavuka bara bara...’sauti ikasema nilijaribu kugeuza kichwa kuangalia huo upande walipo hao watu lakini sikuweza shingo ilikuwa imevalishwa dude zito.

‘Mume wangu kwa hali ilivyo, ni vyema tukamsaidia tu huyu mtu,..angali hali aliyo nayo kakonda,a anonekana hata kula hajala,  mume wangu tumsaidie tu...’ilikuwa sauti ya kike naona alikuwa mke wa huyo mtu.

‘Hiki tulichosaidia kinatosha, angalia gari lilivyoharibika kwa sababu ya uzembe wake, unafikiri atatusaidia matengenezo yake, gari la nyuma limetugonga tulipofunga break ya haraka, sehemu kubwa inahitajia matengenezo….mimi naona tumuache dakitari aendelee naye, tunamlipa gharama za leo, kama kuna zaidi, tutawasiliana….’huyo mtu akasema

‘Inatakiwa muache kitangulizi cha nusu ya gharama, hiki mlicholipa ni kidogo sana…’akasema docta

‘Tutawasiliana docta, sasa hivi hapa sina kitu utanipigia ngoja nikaone taratibu za kulitengeneza gari,, …’sauti ikasema na hao watu wakaondoka. Nikajua huenda kesho yake watakuja, lakini hawakuonekana tena, hata docta alipojaribu kuwapigia simu wakawa hawapatikani, hapo docta akaaja kwangu na kuniambia;

‘Watu wako waliokuleta, wameshakimbia mawsiliano hayapatikani, na pesa waliotoa ni ndogo sana,..wewe huna pesa..?’ akaniuliza

‘Nilikuwa na pesa kidogo kwenye nguo zangu…’nikasema na docta akasogea pembeni kuna nguo zangu zilikuwa zimewekwa akaniletea nikasema;

‘Angalia hapo mfukoni kuna bahasha ina pesa ndani…’nikasema, yeye akajaribu kutafuta kwenye mfuko wa suruali akasema;

‘Mbona hakuna kitu….’akasema

‘Kulikuwa na bahasha kuna barua yangu kutoka kazini na pesa…kwani ni nani alinivua nguo zangu?’ nikauliza

‘Mimi mwenyewe na nesi wangu, hakuna mwingine aliyegusa nguo zako…’akasema

‘Kulikuwa na bahasha na pesa zangu za mafao…’nikasema nikijaribu kujiinua lakini nikashindwa, maumivu, nikatulia, akili sasa ikaanza kufanya kazi, ina maana hata hicho kiodgo nilichopata nacho kimeibiwa

‘Hamna bahasha humu ndani, huenda ulipopatwa na hiyo ajali wali walikupekua wakakuibia…ulipoletwa hapa sis hatukuwa na muda wa kukagua nguo zako, na humu hakuna tabia ya kuibia wagonjwa, haijawahi kutokea, nawaamini wafanyakazi wangu….’akasema docta.

‘Huu sasa mkosi,…’nikasema


’Je una ndugu na jamaa zako ambao unaweza kuwasiliana nao, ili waje kukusaidia, maana siwezi kuendelea na matibabu wakati sijui hatima ya malipo yako, unajua hii ni hospitali ya kulipia, ilitakiwa upelekwe hospitali ya serikali, lakini waliona sehemu ya karibu ni hii hapa…’akasema

‘Ndugu na jamaa zangu hawapo hapa Dar, na waliopo hapa hata ukiwapigia simu hawataweza kunisaidia lolote, mimi naona nitoke tu, nitajua mwenyewe mbele kwa mbele…’nikasema

‘Kwa hali hii siwezi kukuruhusu utoke hivi hivi, hali yako bado sio nzuri unahitajika vipimo, hatujui hukondani kupoje,…inaonekana kuna athari ndani, tunahitaji tuchukua vipimo vya vya utra –sound, lakini havitapimwa mpaka tuwe na uhakika wa malipo, jamaa zako hawajafika, na hali uliyo nayo haihitajii kusubiria sijui tufanyeje…’akasema

‘Naomba msaada wako docta, nimekwama, mimi nilijua kuna pesa kwenye mfuko wangu kama wameniibia tena, sijui hata nifanye nini, nidhamini nikipona nitajua jinsi gani ya kukulipa…’nikasema kwa uchungu.

‘Mimi ni docta tu, sio mwenye hospitalini natimiza wajibu wangu tu, …labda nikushauri jambo, sasa hivi kuna gari linapeleka mgonjwa muhimbili, nitakachofanya nitakuandikia kuwa uende muhimbili, kwa matibabu zaidi, watakuchukua …’akasema

Na kweli ikafanyika hivyo nikachukuliwa hadi Muhimbili, kipindi hicho Muhimbili kama humjui mtu umeumia, nimefikishwa pale nikapokelewa nikapewa kitanda, nikaandikiwa kupimwa hivyo vipimo…siku ya kwanza ya pili, ya tatu, hakuna cha vipimo wala nini, kila docta akipita anasema nisubirie vipimo.

Ndani kwa ndani kunauma,…lakini kila siku nikawa nahisi kupungu kwa maumuvu, na siku moja alipofika docta nikamwambia kuwa mimi najisikia nafuu nitoke tu;

‘Unatakiwa usubirie vipimo …’akaniambia.

‘Mpaka lini, leo ni siku ya nne, sipimwi, mimi naona nitoke tu….’nikasema na sijui ikawaje, docta akaondoka na baadaye nikachukuliwa kwenda kupata hivyo vipimo, na majibu yakaja kuwa hakuna matatizo, ikabidi siku iliyofata nitoke.

Unajau mwili ni wa ajabu sana, siku hizo tano, mwili ulikuwa umekwisha, nimekonda, natisha, …mpaka macho yamezama ndani, siku ile Lugalo uliponiona macho yametoka nje, sasa hapo ilikuwa kinyume chake, ndipo utashangaa mwili wa bindamu ulivyo. Mungu ni mkubwa

Basi nikaruhusiwa na ukumbuke siu zote hizo hakuna anyejua nipo wapi, ajali ile ilitokea hakuna mfanyakazi aliyewahi kuniona, kwani kama wangeliniona taaarifa ingefika nyumbani.

Nikiwa nimechoka sina nguvu, nikapanda dala dala kwa nauli na kuomba kwa mmoja wa wagonjwa ambaye nilimuelezea matatizo yangu akanionea huruma akanipa pesa kidogo ya nauli

Nikafika nyumbani, nilipokaribua nyumbani nikashangaa kuona watu wamejaa , kwanza nikasimama na mawazo ya haraka yakakumbuka mtoto aliyekuwa kiumwa, ..hapo nikavuta hatua ili nijue kumetokea nini....

NB: Jamani leo matatizo, lakini hicho kidogo kinatosha


WAZO LA LEO: Kuna watu wanakufa njaa lakini hapo hapo kuna watu wanamwaga chakula. Kuna matajiri wa kukufuru na hapo hapo kuna masikini waliovuka mpaka, hawajui leo watakula nini, kuna mayatima, kuna wasiojiweza wagonjwa…wanahitaji misaada, hapo hapo kuna watu wanachukua dhaana ya hao wenye shida na kushibisha matumbo yao na utajiri wao. Kwa hali hii,  baraza katika ardhi inapungua. Kumbuka ukishiba, ukamwanga umedhulumu halali ya watu wengine, kwanini umwage, kwanini usimwangali jirani yako mwenye njaa, maana tunajuana.. 

Ni mimi: emu-three

No comments :