Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, December 10, 2014

NANI KAMA MAMA-3


Mke wangu alitoka kwenda bafuni, wakati ameshaoga, anatoka mlango wa bafuni, ghafla akateleza na kudondoka chini, Kabla hajainuka alisema kichwa kinamuuma, akaanza kulalamika kichwa, kichwaaa, ghalfa akakurupuka, na kuanza kutingishwa, unajua kutingishwa. Yaani wewe chukua chupa kama hii ya soda uitingishe harakaharaka, ndivyo alivyokuwa akitingishwa. Na huku anaweweseka, na kutoa sauti ambayo siyo yake, kabisaaa…

‘Unaniuliza wewe kuwa nina shida gani wakati unajua wewe ndiye mbaya wangu…’ sauti ya ajabu ikatoka kwa mke wangu.

‘Hebu nieleze ubaya wangu kwako…’ mama akamuuliza

‘Sikutaki humu ndani, uondoke haraka, la sivyo nitaifanya kitu mbaya hii familia, na wewe sio mtu mwema kabisa kwenye hii familia, wewe ni mchawi, unataka kuiangamiza hii familia, kwahiyo u toka,nakumabia hivi utoke kwenye hii nyumba haraka….’ Akawa anayarudia haya maneno huku anamsukuma mama kwa kidole chake.
‘Lakini mimi sio mchawi na wala sijui uchawi unatafutwaje, hilo sio kweli….’akajitetea mama

‘Habu jiuleze kabla hujafika hapa, hii familia ilikuwaje, ilikuwa na raha, mke na mume na mtoto wao, wewe umefika tu, hali imebadilika, …wewe ndiye chanzo cha haya yote, indoka rudi huko ulipotoka….’sauti ikaendelea kusema.

‘ Nikuambie mke wangu, sasa hivi likija hili shetani liambie hilo haliwezekani, siwezi kumrejesha mama yangu na mama yangu sio mchawi..’Nikasema nakuondoka zangu kuelekea kazini

Tuendelee na kisa chetu……

*************

Rafiki yangu huo ulikuwa mwanzo tu wa mitihani katika maisha yangu, ...’akatulia mjumbe akinywa kinywaji chake.

Ndani ya familia ya mke na mume, mtoto au watoto ni faraja, na mimi na mke wangu tulijaliwa kuwa na mtoto huyo mmoja, tulikuwa tunampenda kweli, unajua tena mtoto wa kwanza anavyopendwa na wazazi wake, na akawa anakuwa haraka, na mwili wenye afya hata wenzake wakawa wanamtania kumuita bonge

Mtoto wetu alikuwa akikua vyema tu na afya yake, lakini kipindi alichofika mama ndico kipindi ambacho hali ya mtoto ilianza kubadilika, uone jinsi mtihani ulivyojipanga,  shetani anajua jinsi gani ya kuwaghilibu watu, kwani siku ile alipoanguka mke wangu akitoka bafuni, mtoto naye alikuwa akiumwa ndani, homa ili kali haishuki.

 Mtoto wangu alikuwa haumwi umwi ovyo, alianza kuumwa siku ile mama alipofika , ilikuwa ni ghafla,  mara tukaona mtoto ananyong’onyea, tahamaki  homa, akawa hataki kula, ikawa sasa ndio tabia, tukajua labda ndio makuzi, lakini hali ikaanza kuwa tete, usiku anachemka homa kweli, mchana mara nyingi anakuwa mzima, hata ukimfikisha hospitalini wanashangaa, anakuwa mzima, homa hakuna, ...yaani inakuwa ni ajabu, siku akizidiwa, mkasema sasa tumpeleke hospitalini anaanza kuwa na hali nzuri, na tukifika hospitalini, hajambo kabisa.

Kwa hali hiyo mwili ukaanza kuisha akawa anaconda kwasababu chakula hataki kabisa, yaani aliumwa kiasi kwamba hata makuzi yake yakaanza kupungua, tukahangaika huku na kule kwa madakitari bingwa, lakini hali yake ilikuwa ya kukatisha tamaa. Mwili ukawa unaisha akarudi akawa kama katoto, wakati alikuwa bonge..

Ilifikia muda hata kazini nikawa situlii, maana upo unawajibika, mara napigiwa simu mke wangu kazidiwa kadondoka, kakimbia, siku nyingine mtoto kazidiwa, hajiwezi, kazi yenyewe ilikuwa ya kampuni za watu binafsi,.... meneja utawala, ndio wale wanajua kujipendekeza kwa bosi, mwenye mali, mwanzoni alijifanya kunionea huruma, ananiruhusu, lakini akaona hali inazidi,akaanza kuniandama utafikiri ndio mimi mfanyakazi peke yangu.

Menaja utawala akawa sasa haniamini, akaona hiyo hali ya kuomba ruhusa mara kwa mara huenda sio kweli huenda natafuta visingizio..ikafikia hatua akanipa onyo, kuwa utendaji wangu wa kazi sio mnzuri, akasema huko kuomba ruhusa kwangu kumezidi, inakuwa kama visingizio vya ugonjwa wa familia,..

‘Bosi kama unataka uhakika twende nyumbani kwangu ukajionee mwenyewe...’nikamwambia.

‘Hilo sio jibu la kunipa mimi, acha ‘uswahili’ wako wewe,...kila mtu ana matatizo ndani ya familia yake, lakini tunajaribu kufuata sheria, unafikiri sisi hatuna matatizo ndani ya familia zetu, matatizo yapo, lakini ni lazima tujue kazi ina utartibu wake, ....’akaniambia

‘Ndio bosi nitajitahidi , lakini kiukweli hata mimi sipendi hali hii, sifanyi makusudi bosi nina mtihani mkubwa nyumbani....’nikasema

‘Sasa mimi nakupa onyo la mwisho, maana hata mimi ni muajiriwa, naipenda kazi yangu, siwezi kuharibu kazi yangu kwa uzembe wa mtu mmoja,...sasa sikiliza, itafika hatua  tutakuambia uamue kufanya kazi au uende huko kwa familia yako, usije ukanilaumu, kama wewe unataka muda wa kukaa na familia yako, utaupata sana, ukamalizie hiyo mitihani yako...’akasema na hapo nikawa sina raha.

Kabla ya hapo kuna siku nilikwenda kwake kulalamika kuhusu maswala ya mshahara, kuwa mimi mashahara ninao lipwa sio sahihi, ukilinganisha na wenzangu ambao tuna elimu sawa, na kazi tunazofanya ni hizo hizo, na ni kweli sijui kwanini mimi ilitokea kuwa na mshahara mdogo kuliko wenzangu, hata wenzangu wakawa wanashangaa, nikaona ni bora nilifuatilie hilo jambo, lakini jibu nililopata lilizidi kunikatisha tamaa, meneja utawala akasema;

‘Hii ni kampuni binafsi, hapa kila mtu kaja kivyake, na kila mtu kaingia na mkataba wake binafsi, na mshahara wake umetokana na jinsi alivyomshawishi mwenye mali, hapa,usiangalie wenzako, kinachotakiwa ni kuangalia upande wako, na utendaji wako ndio utakupandisha mshahara, hapa sio serikalini bwana.....’akasema akinikazia macho.

‘Lakini ukizungumzia maswala ya utendaji wa kazi bosi, tangu mwanzo mimi ni mtendaji mnzuri wa kazi, mwenyewe unaona....., hebu angalia hao mnaowapa mshahara mkubwa, ulinganishe na mimi,  ni nani mtendaji mnzuri, mimi naona mnaangalia mambo mengine kabisa, labda mseme, kwa vile wao ni watoto wa wakubwa, wazazi wao ni waheshimiwa, wana majina, au sio....’nikasema

‘Huo ni uzushi wako na chunga kauli yako hiyo,…’akasema kwa ukali

‘Lakini mambo yapo wazi, hata nisiposema wafanyaakzi wanalalamika, kuna ubaguzi wa chini kwa chini, ….watu wanalipwa mishahata kiupendeleo, mnaangalia rangi, majina makubwa, hilo sio jambo jema....’nikalalamika

‘Wewe fanyakazi na kama unaona hapa kuna ubaguzi nafasi ya kuondoka ipo wazi, hujalazimishwa kufanya kazi hapa, katafute sehemu nyingine, na ukiendelea kulalamika, utakuja kujuta...’akaniambia na ikawa jibu ndio hilo kama sitaki kazi nikatafute sehemu nyingine

Kupata kazi sio mchezo,  ningelienda wapi nipate kazi kirahisi, mtoto wa mkulima hebu angalia, wapo waliohitimi chuo kikuu wanahangaika na kazi hawapati,...kisa ni nini sio kwamba hawana uwezo huo au ujuzi, wanao sana, lakini ni kwa vile wanatoka kwenye familia zisizo na jina....nilipowaza hilo, ikabidi nitulie tu na mshahara huo huo.

Basi yalipoanza matatizo hayo ya kifamilia, meneja utawala akapata kisingizo cha kunabana akasema;

‘Unakumbuka wewe ulikuwa unadai kuomba nyongeza ya mshahara, ni nani atakupa mshahara kama utendaji wako ndio huo, unakuja kazini unalala...kila siku unaomba ruhusa, wewe na kisingizio cha matatizo yako ya kifamilia, mimi nakuona wewe hutaki kazi,.....’aliniambia siku hiyo aliponipa onyo.

Basi kila niliyemuhadithia kuhusu hali ya matatizo yangu ya kifamilia , na hali halisi ya kazini, wengi walinisikitikia sana, kwani wananifahamu uchapaakzi wangu ulivyo,na wengine wakafikia kuniambia;

 `Hapo ndugu kuna mkono wa mtu sio bure, chunguza, na huenda tatizo lipo huko huko nyumbani kwako...’akaniambia jamaa mmoja

‘Tatizo litoke nyumbani lihamie kazini, ni kweli nina matatizo ya kifamilia, mtoto anaumwa, mke kashikwa na ugonjwa usioleweka, ndio maana nakuwa hivyo, lakini sio kwamba napenda, inafika muda sijielewi.....’nikamwambia

‘Wewe hujui tu, kunaweza kukawa na mtu hakupendi, hataki maendeleo yako, au hamtaki mke wako,…hapendi hali uliyo nayo hata kama ni kidogo unapata, yeye kwake kinamuuma, mtu huyo akakufanyia ubaya, ukaanza kuhangaika, akatengeneza mambo mpaka kazi ikawa mbaya,kwasababu ya husuda, chuki...’akasema na mimi sikumuelewa.

‘Hakuna kitu kama hicho,…ili iweje, mimi nina kitu gani cha kuonewa husuda,…hapana, ni mtihani tu, najua ipo siku yatakwisha, tatizo ni kwamba sipati haki yangu, mshahara wangu ni mdogo, ningelikwenda hospitali za juu, haya yangelikwisha…’nikasema.

Kuna wengine walinipa ushauri wakisema niende nikaombewe,  kwa watu wa dini, kuna pepo kanipitia, ndio ananisumbua, wakanipa mifano ya watu walioombewa, sasa mambo yao ni manzuri, wengine wanasema nimrejeshe mama nyumbani ,eti kuna mkosi, huenda mama yangu atakuwa haelewani na mke wangu, kwahiyo mkosi unajijenga bila ya sisi kujielewa…,

‘Hapana, mama yangu hawezi kuleta mkosi kama ingelikuwa hivyo asingelinilea kwa shida….imetokea tu kwa vile upo, hata kaam asingelikuwepo, hali hiyo ingeliweza kutokea tu….’nikasema lakini moyoni nilikuwa hata sina uhakika na ninachokiongea.

‘Wewe nenda kwa waganga wa kienyeji, wasafishe nyota yako, una mkosi fulani, kwanini mwanzoni ulikuwa ukienda vyema, mkeo anakusaidia, mnafanikiwa, kwanini sasa iwe hivyo, huoni kuna mtu anakuchezea, huoni kuwa kuna jambp ambalo sio la kawaida, kama hospitali mumekwenda, hakuna ugonjwa kwa mtoto, au mkeo, mnategemea nini sasa…usipoangalia hata kazi utaikosa….’akaniambia rafiki yangu mmoja.

 Yote hayo niliyasikilia, lakini hakuna kilichoniingia, nilichotaka ni namna ya kulitatua bila kuweka shiriki au kumshuku mtu, nikajipa moyo nikisema hiyo ni mitihani tu, imani ilinikaa hivyo, sikupenda kabisa mawazo hayo ya kwenda kwa mganga wa kienyeji...na pia siwezi kumrejesha mama yangu nyumbani.

Kutokana na matatizo ya mke wangu  ikawa usiku silali, na mara nyingi mambo hayo yanasubiri sana, nikiwepo, hasa usiku, lakini siku zilivyokwenda hali hiyo ikawa aiantokea hata mchana, na ikitokea mpaka niitwe, hali ya mke haitulii mpaka nifike ili nipewe ujumbe, nikashasikia huo ujumbe nikasema kwa kutamka tu, nitafanya, au nisameheni, basi hali hiyo hutulia,...

Kwa ujumla usingizi ukawa ni wa shida kwangu, na hili likaniathiri sana kiafya, mwili ukaanza kuisha, nikawa ankonda, na kazi yangu ikawa ni rehani, ikafika mahali unashindwa uamua lipi familia au kazi, …na failia ina uzito wake, upewe taarifa kuwa mke kazidiw, hajiwezi au mtoto anaumwa hajiwezi kweli unaweza kukaa kzini ukatuliza kichwa, usiende….hilo nikashindwa .

 Nikiwa kazini  nikajitahidi kadri ya uwezo wangu kujituma, lakini ilifikia mahali najikuta napatwa na usingizi...sikupenda hii hali ijulikane kwa wakubwa zangu, ambao walishanionya mara nyingi, lakini kumbe walikuwa wameweka watu kunichunguza, watu wakawa wanapeleka taarifa kuwa mimi sasa nalala-lala kazini...

*******

Mtoto hali yake ikaendelea kuwa mbaya, homa za usiku zikawa haziishi, usiku hakuna kulala, mtoto anachemka sana ....mpaka nikaona maisha sasa yamenilemea, ipo siku moja mtoto alizidiwa sana, akawa kama anataka kukara roho, akaanza kuniita

‘Baba, mbona naumwa sana, ina maana nataka kufa, baba mimi sitaki kufa, sitaki nimuache mama, baba usiache nife...’akaniambia

‘Hapana mwanangu utapona usiwe na wasiwasi....’nikamwambia huku machozi yakinilenga lenga.

‘Baba kwanini siponi, kwanini na mama naye anaumwa, kwanini mama anasema bibi ndiye mbaya...kwanini baba hunisaidii nipone...’akasema na mimi hapo nikajikuta naumie, ina maana mtoto keshaona kuwa mimi simsaidii, iliniuma sana.
‘Mwanangu utapona tu usiwe na wasiwasi, dawa tumeshapata wewe huoni nakusaidia nakupeleka hospitalini....’nikasema.

‘Baba mimi nateseka, nionee huruma baba, fanya anavyotaka mama, nipone, nionee huruma baba....’akawa analia na siki hiyo alipoteza fahamu, tulitoka usiku hadi hopitalini cha ajabu anafika hospitalini, homa imeshuka na amezindukana…habu ona huo mtihani.

 Siki hiyo alipozidiwa mchana wake ndio siku nilipata tetesi kuwa kuna taratibu zinapangwa za kupunguzwa wafanyakazi, kutokana na hali ngumu ya kampuni, gharama hazibebeki. Tulipewa kama fununu, tukaambiwa tujiandae, lolote linaweza kutokea.

Tetesi hizo zilikuja na kiujumla ilikuwa mshituko kwetu, kwani kulikuwa hakuna maandalizi yoyote, kutokana na kipato tunachokipata, ni hela ya kudangaya njaa,  muajiri anakupa mshahara wa kukufanya uishi tu, uonekane upo kazini, mshahara hata kula hautoshi, huwezi kuweka akiba ya baadaye au kufanya lolote la maendeleo.

Maisha tuliyokuwa tukiishi hapo kazini ni lazima uwe na mkopo, na safari hii  kutokana na matatizo nilikuwa nayo nikawa nimekpa hadi kupitiliza,  mke aliyekuwa akinisaidia ndiye huyo anaumwa. Nikamuomba mungu anisaidi nibakie kazini japokuwa ninachopata ni  kidogolakini angalau siku zinakwenda, naweza kuishi mjini.

Basi siku hiyo ndio mtoto akazidiwa nikawa naomba, lakini  hata huo muda wa kuomba utaupata wapi, mtoto anaumwa, mke anapandisha, mama akawa ndiye anachukua sasa majukumu yote ya ndani, kuwahudumia wagonjwa, kufanya kazi za ndani , mpaka nikawa namuonea huruma, na mke akipandisha mashetani anamuandama mama kuwa yeye ndiye anataka kumuua yeye na mtoto wake. Mama naye akawa hana raha, lakini asingeliweza kuondoka kutokana na hali ilivyo.

Siku hyo kazini wafanyakazi wakawa wanaitwa mmoja mmoja kuhojiwa, eti kutathiminiwa, niliona ajabu maana wafanyakazi waliokuwepo ni wa siku nyingi, wanajulikana utendaji kazi wao,leo hii wanatathiminiwa na ni kwa maneno sio kwenye shughuli zake, kwahiyo wale wanajua kijieleza, hata kama walikuwa kivitendo sio wazuri, ndio walioonekana wazuri, nashukuru mimi sikuitwa, sijui ni kwasababu gani.

 Siku hiyo ikaisha na japokuwa nilipewa taarifa kuwa mke kapandisha, lakini nikaamua kutokwenda, nikazima simu, kwa mara ya kwanza, niliporejea nyumbani ilikuwa usiku, mke hayupo kapotea..mtoto ndani kama kawaida yake homa imepanda, mama anahangaika huku na kule,ikawa kazi ya kumtafuta mke, mama anahangaika na mtoto tulitafuta hadi maporini mpaka tunampata na kumrudisha nyumbani ilikuwa saa sita za usiku...nipo hoi sijala toka ninywe chain a kipande cha muhohogo asubuhi,

 Tunarudi nyumbani, mtoto anachemka homa, ni homa ya aina yake, ilikuwa sasa kama degedege, mtoto anaweweseka, ikafikia sehemu ananiambia

‘Baba kwaheri mimi nakufa....’kauli hiyo ilinivunja nguvu kabisa nikajikuta nalia, mama akajitahidi kunisaidia,alipoona nalia, akawa kamchukua mtoto anakaa naye nje ili apate upepo homa ishuke na kujaribu kumpooza na maji ili homa ishuke, mimi huku nahangaika na mke wangu, hatulia, tukamfunga kamba, lakini kamba zinakatika,..majirani wamesaidia wamechoka wameondoka kujilalia.

. Niliomba mungu kupambazuke haraka niwahi kazini nikakope hela ili nikamtibie mwanagu kwa dakitari mmoja bingwa niliyesikia kuwa ataweza kujua kiini cha hali ya mtoto, na mke nitakwenda kwa docta bingwa wa magonjwa ya akili huenda kuna athari kwenye akili, hayo diyo yalikuwa mawazo yangu.

Hata hivyo kila nilipowaza hivyo, naishia kukumbuka kuwa deni nililokopa mwanzoni halijaisha hawatakubali, Nikasema potelea mabali nitawaomba hivyo hivyo, sasa nikimbilie wapi, kazini ndiye mkombozi wangu wa mwisho, nikajipanga jinsi gani ya kumuingia meneja utawala, ambaye ndiye anayesikiliza matatizo ya wafanyakazi, na huyo huyo ndiye keshaniona sifanyi kazi na keshanipa onyo la mwisho….

Hauchi hauchi kukapambazuka, nimechoka , sina nguvu...kichwa kinaniuma kweli, njaa, macho yamejaa usingizi....yaani ungeniona siku hiyo ungelijua huyu mtu anaumwa sana mwili umeisha, utafikiri naumwa ugonjwa gani sijui..., lakini nifanyeje. Nikamwambia mama anisaidie, tupitie hospitali ya serikali pamoja, kwani mke alikuwa hajiwezi, kutokana na kujibamiza na kule kukimbia usiku kucha, kwahiyo tukamuacha akiwa amelala, tukamuomba jirani atusaidie kusikilizia .

Tuliamua tumpeleke mtoto hospitalini maana alikuwa kalegea, hana nguvu sijui ni kutokana na hiyo homa,…

Mimi na mama tukatoka kuelekea hospitali, ile tunatoka nje, tunakutana na baba mwenye nyumba, nilijua nini kafuata,anataka kodi ya nyumba, mwezi wa tatu namzungusha, alipotuona tumembeba mtoto huruma ikamshika, akasema tutaonana jioni, nikashukuru mungu, moyoni nikisema jioni naweza kupata chchote, nitakachopata nitagawa hivyo hivyo..

Tulipofika hospitalini, tulikuta kuna watu wengi, foleni kubwa, nikamwambia mama aisubirie, mimi nikimbie kazini, nikipata angalau mkopo, nitamchukua mtoto kwenye hospitali ya kulipia. Mama akanielewa akabakia akisubiria foleni, na hali ya mtoto joto lilikuwa limepoa kidogo kama kawaida yake akifika hospitalini joto hupotea, lakini bado hali yake ilikuwa sio nzuri, kalegea kabisa …nikamwangalia huku machozi yananilengalenga, nikijiona baba nisiye na thamani …lakini nifanyeje…nikainuka haraka kukimbilia kazini.

Nilipofika kazini nikakuta wafanyakazi wamesimama kwenye ubao wa matangazo, nikasogea na kwa maandishi makubwa nikaona kumeandikwa, `ORODHA YA WALIOPUNGUZWA KAZI. Wafuatao wafike ofisi ya utawala, waonane na meneja utawala.

Hapo nikaishiwa nguvu, nikaanza kusoma majina moja baada ya jingine, na kila niliposogea mbele, nikawa napumua nikijipa tumaini kuwa jina langu halipo, nikafika karatasi ya mwisho, kulikuwa na majina nusu ukurasa, nikaanza kusoma la kwanza, nikawa nashuka chini, la pili, la tatu….......

NB: Kidole kinauma, tuishie hapa kwa leo


WAZO LA LEO:Tunapoumwa, tujenge tabia ya kwenda hospitalini kuchunguzwa afya zetu, vipimo ndivyo vitakavyotusaidia kujua tatizo ni nini, tusikimbilie kwenye imani za kufikirika kuwa labda , labda…. Au kukimbilia kunywa dawa tu bila kujua tatizo ni nini kwani dawa zinaweza kukuza tatizo likawa sugu…na dawa hutolewa kutokana na vipimo maalumu. Tuchukue tahadhari kwa afya zetu. 
Ni mimi: emu-three


Ni mimi: emu-three

No comments :