Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, December 8, 2014

NANI KAMA MAMA -2


 Siku zikapita nikawa nimemsahau, na siku moja nikakutana na jamaa yangu mmoja anayemfahamu huyo mjumbe, akaniambia, jamaa alikwisha fariki..

‘Keshafariki, una uhakika?’ nikamuuliza.

‘Hivi kwa hali ile unaliza una uhakika uliwahi kumuona siku za karibu, akiwa kazidiwa, ameisha, anatembea utafikiri mzee aliyechoka, mwili umekuwa kama skeletoni …..’akasita kuongea kwani aliona mdada akipita, na jamaa yangu huyu ni mwngi wa mambo hayo.

‘Nilimuona Lugalo hospitalini…’nikasema nami nikigeuza uso kuangalia huko anapoangalia

‘Pale walimdanganya kuwa hana tatizo,…alishaathirika yule wakamficha kiaina…’akasema

‘Aaah, …wasingelimficha, wangelimuambia wakampa nasaha na jinsi gani ya kuishi maisha ya matumaini, ..sizani kama alikuwa na tatizo hilo...mimi mwenyewe niliona cheti chake na majibu ya vipimo labda kama alikuwa na tatizo jingine..’nikasema.

‘Wewe niulize mimi,…keshaaga dunia yule…tusubiri zamu zetu maana tatizo hilo sio la mmoja, tutakwenda wengi…’akasema akizidi kumuangalia huyo mdada, na vazi alilovaa huyo mdada lilizidi kumchanganya mwenzetu, kwani lilimkaa vyema mwilini, akawa anatembea kwa madawa, na jamaa akawa anajilamba lamba mdomo.

‘Acha tamaa, hebu niambie ukweli…’nikasema.

‘Ukweli upi tena..nisubiri  hapa nitarudi, yule hawezi kupita hivi hivi, lazima nimpe neno, huwezi jua….’akasema na akamfuatilia huyo binti, mimi nikaendelea na mambo yangu, nikijua kweli huyo jamaa ameshafariki, leo hii nakuatana naye akiwa hai na afya tele, na gari alilo nalo linashiria kuwa hali ni nzuri kweli sikuweza kuamini...!  

Tuendelee na kisa chetu....

                                         *******************

`Je rafiki yangu amepata bingo gani…’ nikamuuliza

Yeye akasema;

‘Hebu twende kwenye gari, maana hapo gari lilipo sipaamini sana umeona muda kulitaka kutokea ajali, ukiwa ndani ya gari unajishau, hasa madereva wasiojua nini maana ya kuwa dereva, ..’akasema na kunishika mkono, tukaenda, na kuingia ndani ya gari lake, hali ya hewa, baridiii, nikajihisi nimeingia dunia nyingine,….wenzetu wana raha jamani acheni wazidi kuwa mafisadi…..,

`Ni siri gani ya maisha uliyoigundua, nami niitafute huenda nikapata mafanikio kama yako…’ Nikaendelea kumuuliza yeye akaendelea kuwa kimia huku akiendesha gari lake hadi sehemu nzuri, akalisimamisha

Akageuka na kuniangalia akatabasamu na akainua mkono na kunigonga gonga mgongoni kwa nguvu alizo nazo, nilihsi maumivu, lakini sikusema kitu. Sio ule mkono tena ambao niliogopa kuupokea siku ile, sasa ni mkono ambao una kilo nyingi!

Akauondoa mkono mgongoni kwangu,  halafu akacheka, akaniangalia kwa muda kama vile anatafakari jambo…mara nikamuona akama anataka kutoa machozi, …nikashikwa na mshangao, ikabidi nimuulize

‘Vipi tena, maana kwa hali uliyo nayo sihisi kama unastahili kutoa machozi...'nikasema na yeye akachukau leso yake na kuipitisha machoni, halafu akasema;

 `Unanikumbusha siku ile, tulipokutana pale Lugalo hospitali, unakumbuka, ulipoondoka na kuniacha, unajua nilizidiwa sana hadi kuchukuliwa kulazwa, hakuna hata ndugu aliyekuja kuniona, baadaye nikatoka, nikiambiwa sina tatizo,ikabidi nihame mji, ndipo watu wakajua nimeshakufa…!’

‘Ooh, hata mimi niliskia hivyo ndio maana nakuwa na hamu sana ya kutaka kujua historia ya yaliyokukuta, …ni maombezi, au ni miujiza gani uliyokutana nayo, au ulipata tiba mbadala, maana nasikia kuna wataalamu wa kutibu kila magonjwa siku hizi…’nikasema

`Ndugu yangu hebu tufike hapo hotelini tupate chochote ili nikupe hadithi yangu , kiukweli ni hadithi ndefu, nikianza kuielezea hapa siku itaisha..’akasema huku akifungua mlango wa gari, nami nikafanya hivyo tukatoka na kuelekea kwenye hoteli iliyokuwa hapo karibu. Baada ya kuagiza vilivyoagizwa, akasema;

‘Kisa changu ni kirefu,  nadhani kama nikutunga kitabu basi kitakuwa kitabu kikubwa sana, na labda viwe zaidi ya vitabu viwili..ila nitajaribu kukupa kwa muhtasari tu, kwani dunia hii ina mambo, lakini yote tisa, tuwaheshimu sana wazazi wetu, na kila mara nikimukumbuka mama yangu, natamani kulia, lakini ndio maisha na nikumbie kitu, ndugu yangu, ‘ hakuna kama mama..’ akatulia.

‘Mama!!, kwani mama yako yupo wapi?’ nikamuuliza nikiogopa kumuuliza kuwa mama yake yupo hai au..

‘Rafiki yangu hivi kweli niambie ..Ni ' Ni nani kama mama '…katika hii dunia?’ akaniuliza huku akianiangalia, na machoni nilimuona akijenga ukungu wa machozi.

Nilimwangalia bila kumpa jibu ili aendelee na kisa chake, akatulia kwa muda halafu akaniangalia tena, sasa akiwa na tabasamu usoni.

`Mimi katika maisha yangu kilichonisaidia na kufikia mafanikio niliyo nayo hivi sasa, ni SU-BI-RA, na UCHA MUNGU... Alilitamka neno hili kwa sauti kubwa, `subira’.na 'Ucha mungu'

`Hutaamini kuwa nilishaliona kaburi hilo...na watu walikuwa wanahesabu masaa, wakisikilizia…lakini cha ajabu nilikuwa siumwi na ugonjwa wowote, na siku ile nilipokutana na wewe pale lUGALO, sikujua naumwa nini....mwili tu ulikuwa unaisha, udhaifu, sisikii kula….nikawa nakonda kwa mawazo.

Siku ile nilifika kupima tu, ili niwathibitishie walimwengu kuwa siumwi ugonjwa huo wanoufikiria wao...., ila naumwa ugonjwa usioelezeka, ugonjwa wa  mawazo na matatizo. hakuna ugonjwa mbaya kama mawazo,..., shida ziliniandama, na umasikini  ukanijaa mwilini, laana ikawa imenifika….

Rafiki yangu, matatizo yaliniandama kama mvua, lakini nikakumbuka kile kisa cha nabii Ayubu,jinsi alivyoteseka,.. na matatizo yaliyomkuta, akakimbiwa na jamaa zake wote, lakini hakukata tama, kwasababu ya subira.

`Nadhani hata wewe uliyeniona kipindi kile usingeamini kuwa siumwi, na wengi hata wewe walidhania kuwa nimeukwaa, nimeathirika,  lakini kwa uhakika nilikuwa siumwi, watu walinikimbia wakizani nina ukimwi, lakini yote nilimuachia mungu.

 Matatizo niliyokuwa nayo hakuna aliyejua kiini chake….Ni nani umgemwambia kipindi kile akuelewe..hakuna, kila mmoja alikuwa akisema lake…unajua nilipozidiwa watu walifikia kusem;

‘Mwache afe si-amejitakia mwenyewe, mzinzi mkubwa huyo, …na mengine mengi…’akatulia

'Jamani hivi kweli mimi nimekuwa mnzinzi zaidi ya wazinzi waliojaa humu duniani…ni kweli ujana una mambo yake, lakini hayo waliyokuja kunipakazia jamii, hayakuwa na ukweli, ukweli wa hayo yaliyonkuta ni tofauti kabisa, na hicho walichokuwa wakikifikiria wao…’akasema

‘ Lakini ya mungu mengi, yote hayo yalikuwa maneno ya wanadamu wasiokuwa na simile, na raha yao kuona wengine wakitaabika...mimi nilikuwa na yangu makubwa ambayo kwa wenye kufikiri wataelewa na kujifunza...’ Akasema huku anamimina kinywaji chake.

`Unajua kwa matatizo niliyokuwa nayo ilifikia hatua mke wangu mwenyewe akanikimbia…jamaa na ndugu zangu wakawa hawaonekani tena….’akasema

‘Na kiukweli, matatizo haya yalianzia kwa mke wangu mwenyewe,  na huyo huyo akanikimbia, …na matatizo hayo yalianza pindi nilipoamua kumchukua mama yangu ili aje tuishi naye. ....hapo sasa nianze kukuhadithi vyema....'akasema akijiegemeza vyema kwenye kiti....


            ************* kisa kinaanzia hapa*************


Kama nilivyosema mimi niliamua kuoa mapema, ili kuhimili tamaa zangu kama mlivyoniona kule shuleni nilikuwa situlii, nahisi ndio maana nilipoanza kukonda watu wengi walikimbilia kusema nimathirika, ...lakini kiukweli baada ya kuoa, mimi niliamua kutulia kabisa mimi na mke wangu, na uzuri, mke alikuwa keshanijulia, kwahiyo sikuwa napata taabu.

Nilioa nikiwa bado kwenye nyumba ya kupanga yenye vyumba viwili baadaye nilipopata mtoto nikachukua chumba cha tatu… kipato changu kilikuwa sio kikubwa sana, kama ujuavyo mishahara yetu, lakini maisha nilikuwa nayamudu.

Tulipopata mtoto gharama zikaogezeka, ikabidi kujipanga vyema, mke wangu naye akawa anabangaiza huku na kule, alikuwa muhangaikaji kweli, anajituma,  ili tuweze kuyamudu maisha, maisha yakawa yanakwenda, japokuwa kiukweli kipato hakikuwa kinakidhi haja saana, maana licha ya sisi weyewe, bado mwanzoni tulijitahidi kuwakumbuka wazazi ....

Mama yangu alikuwa kijijini na maisha yake yalikuwa ni ya kimasikini kweli, sikupenda kuoa mapema, ili niweze kumuhudumia mama yangu, lakini mama ni mmoja wa watu walionishinikiza kuwa nioe mapema,....alisema, hataki kuja kuathiriwa na tabia yangu, aliyoiita chafu, na pia anahitajia wajukuu, kwahiyo niliamua kuoa kwa ridhaa yake.

Unajua ukishaoa, umeshakuwa na mwenza wa ushauri, kwahiyo huwi na uhuru wa maamumuzi ya peke yako tena, pili kutegemeana na kipato changu kidogo ilibidi nianze kuangalia maisha yangu na familia yangu kwanza, kwa hali hiyo nikajikuta naanza kumsahau mama, kiukweli ikafika muda sikumbuki kumtumia mama pesa za matumizi kama ilivyokuwa awali,...

Ni mke wangu ndiye aliyekuwa kwa asilimi kubwa akisaidia sana familia, mshahara wangu wa mwezi ulikuwa ni mdogo, ukipata unalipa madeni, umekwisha, ninabakia kutegema kile kidogo anachopata mke wangu kwenye biashara zake, kwahiyo mke wangu akawa ni mtu muhimu sana.

Lakini kipato cha mke wangu ni cha mke wangu, na sio kwamba alikuwa akipata pesa nyingi, hapana ni hela za kusaidia kula kwa siku hiyo, kesho yake anajituma kupata nyingine, kwahiyo  sikuweza kumwambia lolote mke wangu kuhusu hali ya mama ….

Ikafikia muda watu wanaotoka kijijini wakawa wananiletea malalamiko kuwa mama yangu anaishi kwa shida, na mimi nimemtelekeza mama, nimesahau nilikotoka, na lawama nyingi tu na ni kweli kutokana na hali ya kimaisha na kipato, nilikuwa nimeshamshau mama yangu, ningefanyeje.....

Kwa kuona hivyo, ikabidi niongee na mwenzangu kuwa tufanye nini maana mama anateseka huko kijijini, yeye akanishauri tumchukue mama, aje tuishi naye...wazo hilo sikukubaliana nalo, nikijua hali halisi tuliyo nayo,...na mama yangu nimjuavyo hataweza kuivana na mke wangu.

Sio kwamba mama ni mkali, hapana mama ni mtu mpole sana, lakini mke wangu ana tabia ya utegemezi, maamuzi ya kibinafsi, kujiona na msafi sana....sasa akikutana na mama ambaye ni mpole , huruma....nahisi kuna hali itafika nitakuwa upande wa mama, nikitaka hiki kifanyike kwa mama na mke wangu anaweza akapinga, ni mawazo yalinijia tu, japokuwa sikuwa na uhakika nayo.

Lakini cha muhimu sana, ni hali ya kimaisha na kipato tunachokipata je kitaweza kutuwezesha sote hata hivyo  nikaona pia ni wazo jema ili kwa hicho kidogo tunachokipata tunaweza tugawana hivyo hivyo,;

‘Kwanini tusiwe tunamtumia kidogo kidogo ....maisha tunayoishi ni ya shida, akiongezeaka mtu mwingine tutazidi kuumia.....’nikamwambia mwenzangu kuzidi kumpima, kama kweli ana nia hasa ya kuishi na mama yangu, nay eye akasema

‘Unajidnganya, mbona inapita miezi mitatu, hujamtumia mama yako pesa, mimi naona ni bora aje tuishi naye hapa,  hicho kidogo tunachopata  akione, na aone maisha tunayoishi, sio wanasema tunaishi kwa raha, sijui nini na nini, aje ajionee mwenyewe, tunavyohangaika usiku na mchana....’akanishauri mwanzoni nikapuuza, nikatuma vijisenti kidogo, ....

Haikupita muda watu walitoka huko kijijini wakaja na taaarifa kuwa mama pamoja na hali ngumu, anaumwa, anateseka , kwahiyo nikapanga kwenda kumchukua, nikaomba ruhusa ya siku kadhaa, na kukopa kiasi kidogo kazini kinisaidie kwa nauli, nikasafiri kwenda kumchukua mama...

**********

Nikiwa njiani nilikumbuka jinsi gani mama yangu alivyonilea kwa shida, unajua maisha ya kwetu kijijini na ukiwa na baba ambaye hajui umuhimu wa familia, yeye anachopata ni kunywa, na kwenda kutangaza utajiri wa kufikirika kwa marafiki zake, akirudi kalewa, ukali...basi mama akawa anabeba majukumu yote.

Niliwaza mengi kuhusu Mama, mama yangu, nikajuta kwanini sikuweza kumkumbuka, na hadi kufikia kiasi hicho. Hivi ni nani anastahili kufaidi matunda na jash la mwanae, nilijiuliza

‘Kwanza ni mzazi wako, maana ndiye aliyekulea kwa shida,, na hasa mama yako, na bahati nzuri mama yangu yupo hai kwanini nimtese, na ndio nikakumbuka ule usemi, aliokuja kuniambia mmoja wa watu waliokuja kunipa taarifa, aliniuliza swali

‘Ni nani kama mama yako...?’

‘Hakuna ‘ nikamwambia.

‘Sasa kwanini unamuacha mama yako ateseke mwenyewe huko kijijini..?’ akaniuliza

‘Ni kwasababu ya maisha magumu, kipato kidogo, sasa ninashindwa kukigawa,...’nikajitete hivyo.

‘Hivi wewe unajiona ni bora zaidi ya mzazi wako, wewe ule ushibe na mke wako wakati mama yako anateseka kijijini?’ akasema kama ananiuliza.

‘Sio hivyo, na sio lengo kufanya hivyo, ni hali halisi..’nikasema.

‘Fikiria sana...katika dunia hii wazazi ndio baada ya mungu,..wakiteseka ujue na hali yako itakuwa ngumu,...mkumbuke mama yako, kumbuka ulipotoka, hakuna kama wazazi wako, hakuna mama yako....’akaniambia.

‘Ni kweli hakuna mama.....’nikasema wakati nashikwa na usingizi na nilipoamuka nikajiukuta nimeshafika kijijini.

 Kwakweli hali niliyomkuta nayo mama ilikuwa ya kusikitisha kweli, ...analalia mkeka, chakula cha shida, ...siku hiyo niliyokaa hapo nilitamani kupambazuke haraka tuondoke, nilishasahau kuwa ndiyo maisha niliyokulia, ndipo nilipotoka.

Kweli kesho yake tukaondoka naye na kuelekea mjini, japokuwa mama alinisihi kuwa nisichukulie haraka kuondoka naye, kwani hamjui huyo mke wangu yupoje.

Kiukweli  tangu nimuoe mke wangu,  hatukuwahi kuja kukaa hapo  nyumbani, hata siku ya harusi, tuliifanya kinamna yake, kwani tulifika mchana tukaenda kuoa, kufika kwa mke, kukawa na shughuli iliyochukau muda mrefu, tukarudi hapo nyumbani usiku,  kesho yake tukaondoka,.

‘Unajau mke wako hata sura yake siifahamu vyema, maana siku ile ya ndoa yenu mlikuja usiku na mkaondok kesho yake alfajiri,, na hamjapata muda wa kuja kunitembelea, mpaka mumepata mjukuu, hutaki hata kumleta mkeo, si vizuri hivyo....’akalalamika mama.

‘Mama ni hali za maisha, yeye ananisaidia kutafuta maisha, nikisema tuje wote huku, nani atahangaika huko, ndio maana nilikuwa nakuja mwenyewe, ili yeye apate muda wa kutafuta kidogo kwa ajili ya kesho na kumuhudumia mtoto..’nikajitetea

‘Haya twende huko mjini, sijui mkeo atanikubali na hali yenyewe hii...’akasema mama akijiangalia nguo alizovaa, na moyoni nikawa nasononeka, kuwa hata nguo ya maana sikuwahi kumnunulia mama.

‘Mama usijali yeye mwenyewe ndio katoa pendekezo hilo, muhimu ni kusikilizana naye tu, kwani anajitahidi sana kunisaidia katika maisha, na sizani kama atakufanyia ubaya wowote..’nikamwambia

Basi tukaondoka na kufika mjini, na tulifika usiku, baada ya mama kuoga na kuandaliwa sehemu yake ya kulala, tukaongea kidogo, ...joto lilimsumbua mama, kwahiyo kuna muda akawa kajifunua,...mama hapendi kabisa kujifunua sehemu ya uso wake, muda wote kajitanda,na kuacha sehemu ndogo tu ya usoni.

Mke wangu akawa kamuona mama vyema sasa,  nikaona mke wangu akikunja sura yake,  akawa kama kaona kitu cha kumtisha, sikujali nikajua ni ile hali ya adabu kati ya mke na mama mkwe wake,..

Hata kesho yake, sikuona ule uchangamfu wa mke wangu kwa mama, ...tangu siku hiyo, mke wangu akawa kabadilika, akawa mara kwa mara akimtizama mama kama anamuogopa....sikutaka kumuuliza, nikawa najua kuwa watakuja kuzoeana tu.

Hata hivyo nikiwepo karibu, mke wangu alijitahidi kumnyenyekea mama yangu kama ilivyo kuwa ada kwa wake kwa mama zao wakwe, maisha yakaenda hivyo, japokuwa kiukweli sikuona ile hali niliyoitarajia kwa mke wangu kwa mama yangu, kwani mke wangu ni mcheshi, tukiwa naye najisahau kwa ucheshi wake,..lakini alipokuja mama, ikawa kama kuna kitu kimemuingia mke wangu akawa na ukimiya wa ajabu.

Kwa mfani kama nipo  naongea naye , akitokea mama tu, yeye hubadilika, akawa kimiya, akawa kama anaogopa kitu anakuwa hana raha kabisa,  nikaanza kuhisi vibaya, kuwa mke wangu hampendi mama, …nikjajifanya kama sijali, tukaendelea kuishi hivyo hivyo, na masiku yakaendelea mbele na siku moja ambapo ndipo mambo yalipoanzia likatokea la kutokea.

******

Siku hiyo ambayo sitaweza kuisahau, mke wangu alitoka kwenda bafuni, wakati ameshaoga, anatoka mlango wa bafuni, ghafla akateleza na kudondoka chini, Kabla hajainuka alisema kichwa kinamuuma, akaanza kulalamika kichwa, kichwaaa,…

Ghalfa akakurupuka, na kuanza kutingishwa, unajua kutingishwa. Yaani wewe chukua chupa kama hii ya soda uitingishe harakaharaka, ndivyo alivyokuwa akitingishwa mke wangu. Na huku anaweweseka, na kutoa sauti ambayo siyo yakwake…ilikuwa sio sauti yake, kabisaaa…

‘Kwa mtu yoyote atajua kuwa hayo ni matatizo ya mashetani yamempanda, lakini kwa mke wangu tangu nimuoe hajawahi kutokewa na kitu kama hicho, kwahiyo, nilivyotoka nje na kumuona katika hiyo hali, sikukimbilia moja kwa moja kuamini hivyo, nilijua ana malaria au shinikizo la damu…nikamshikilia kwa nguvu, hadi nikachemsha, na kwa muda huo mama alikuwa ndani akisaidia kupika.

Mama aliposikia hiyo hali ikabidi aache shughuli, aje kuona kuna tatizo gani,akanikuta napambana na mke wangu nikijaribu kusmhika, ili asijiumize, maana alikuwa akijigonga gonga, sakafuni, mama akasogea na kumuangalia mke wangu.

Mama ni mama, wanajua mengi zaidi yetu, akaanza kumuongelesha kwa kumuuliza mke wangu,

‘Niambie wewe ni nani na una shida gani kwa mtoto wangu..?’ mama akauliza

‘Unaniuliza mimi ni nani, mimi ndiye mwenye nyumba hii, na kuwepo kwangu ni kwasababu yako wewe, unataka kuiharibu nyumba yangu…wewe ndiye mbaya wangu…’ sauti ya ajabu ikatoka kwa mke wangu.

‘Hebu nieleze ubaya wangu kwako ni nini…’ mama akamuuliza

‘Sikutaki humu ndani, uondoke haraka, la sivyo nitakufanya kitu mbaya, na wewe sio mtu mwema kabisa kwenye hii familia, toka,nakumabia toka…toka, wewe ni mchawi, mwanga, toka humu ndani haraka, unataka kunai na kumuua mtoto wangu….’ Akawa anayarudia haya maneno huku anamsukuma mama kwa kidole chake.

Mama alikaa kimiya, ilikuwa kama kitu kimeshika , akawa hana nguvu, akatulia kwa muda, na wakati huo mke wangu naye akalegea na kulala chini, na hapo tukawa tunampepea mama akawa ananiangalia kwa makini, akiwa kama anataka kujua nitasema nini, lakini mimi akilini sikuwa na mawazo yoyote mabaya kwa mama yangu, nilijua hayo ni malaria kwa mke wangu, kapawa tu.



Baadaye akatulia , mke wangu akarejea katika hali yake, akasimama na kuelekea ndani, na mimi nikamuuliza mama yale maneno ya maana gani, mama akaniangalia machoni , akasema,

`Hayo ni mambo ya kiulimwengu,  ukichukiwa na walimwengu, kila mtu atakunyoshea kidole, sina zaidi ya kukueleza mwanagu, subiri umuulize vyema mkeo yeye atakufafanulia zaidi…’ akasema mama na kusimama kwends kuendelea na shughuli zake

Mimi nikamfuata mke wangu ndani, nilimkuta kajilaza kitandani, nikamuuliza hali yake, akasema kichwa ndicho kinamsumbua, halafu yeye akaniuliza;

‘Kwani kulitokea nini?’ akaniuliza

‘Ulishikwa na kitu kama mashetani, ukaanza kuongea ovyo, sikukuelewa kabisa..’nikasema

‘Nilingea nini?’ akaniuliza

‘Aaahm hayo yaache tu, mimi naona ni heri ukapime malaria …’nikasema

‘Niambie niliongea kitu gani, nataka kujua….’akanisisitizia

‘Uliongea kwa sauti ya ajabu ukasema mbaya wako ni mama eti mama ni mchawi….’nikasema

‘Oh, kumbe…nilijua tu, sasa mambo yametoka waziwazi,  natumai mwenyewe umesikia hayo, mama yako ni nani…umeyasikia mwenyewe, usija kusema ooh , mimi nimzua, sasa elewa kuwa tunaishi na nyoka humu ndani…’akasema

‘Unasema nini?’ nikasema kwa hamaki.

‘Lakini si umesikia mwenyewe…sio mimi , kama ingelikuwa ni mimi ungeliskiai mapema nikiongea, je sauti ilikuwa ya kwangu au ilikuwa sauti ya mtu mwingine?’ akaniuliza

‘Kwahi hata ikiwa sauti ya mtu mwingine, huoni labda ni malaria umechanganyikiwa tu…’nikasema

‘Sikilize mume wangu, hizo ni ishara zinakutkea ili umjue mama yako vyema, siku ila tu nilipomona sura yake, nilihisi moyo ukinienda mbio,….nimekuwa nikimuota ndoto mbaya, mara anataka kuniua,….mara anataak kumuua mtoto, sasa hali imetokea dhahiri, ujue huo ukweli…..’akasema

‘Ujue huyo ni mama yangu, ndiye aliyenizaa…’nikasema
‘Sasa uamuzi ni wako, usubiri mabaya yatokee kwanza, au uanze kuchukua uamuzi wa haraka,…kiufupi ni kuwa mama yako sio mtu mnzuri, na hali ilivyo, mama yako hafai kuishi nasi hapa ndani…’akasema mke wangu.

Kwakweli sikuweza kusema kitu, kuna hali ikaanza kuniingia akilini, nikiwazia hiyo hali liyomtokea mke wangu, nikakumbuka maneno ya watu kuhusu hayo mashetani, kuwa yanaweza kukuelezea mambo usiyoyafahamu.

Lakini huyu ni mama yangu, hawezi kunifanyia hivi…’nikajikuta nikijisema mwenyewe. Siku hiyo nzima ilikuwa kama kumingiwa na jambo kubwa sana ndani ya familia yangu sote tulikuwa kimiya, hakuna kusemeshana, mke wangu akawa haongeai na mimi, na mama halikadhalika.


Ilikuwa jambo la ajabu kwani tangu mama afike hapo sikuona dalili ya mke wangu kumnyanyasa mama, ni ile hali ya kuwa kama anamuogopa tu, lakini hakuwahi kumfanyia mama ubaya wowote, labda kama alikuwa akifanya hayo kisiri, na hata mama sikumsikia akilalamika kuwa mke-mwana wake anamnyanyasa, kwahiyo hiyo hali kutokea ikawa ni mshituko kwangu.

Mama alikuwa kipenzi change, nikikumbuka alivyonilea kwa shida, sikutaka kabisa kutokea kitu cha kumuumiza zaidi ya hali mbaya iliyotokea nikamuacha huko kijijini, nilipanga kuwa kwa vile tupo naye sasa, nitajitahidi awe na maisha ya kawaida na sisi kutokana na kipato tunachokipata, mimi nilikuwa mwana pekee kwake, leo hii mke wangu anadai kuwa mama ni mchawi na hamtaki, kwanini, nilishindwa kupata jibu!

Hali ile ikamtokea tena, siki hiyo hiyo, ya kuweweseka, sasa hivi nikakumbuka kuwa kama ni mashitani kweli kinachotakiwa ni kusoma vitabu vitakatifu, nikawa namsomea mara kwa mara, nilimsomea na kumwagia maji , na baadaye akatulia. Na ghafla akazindikuana, …

Alipozindukana, akanikodolea macho na kuniuliza kumetokea nini, mimi nikamwambia kuwa kapandisha tena mambo hayo kama mashetani, akaniuliza kwa kushangaa, mashetani?

‘Ndio kama yale ya mwanzoni, ulipodondoka ukitoka kuoga…’nikasema

‘Na hayo mshetani  yanataka nini?’ akaniuliza

‘Achana nayo bwana, eti yanadai hayamtaki mama, eti mama yangu ni mchawi,kitu ambacho hakipo na hakiwezekani..hayo ni mashetani na mashetani haya nia njema kwa wanadamu, ni bora yaangamie kabisa..’ nikasema huku naiunuka kuondoka, kwani muda ulishaenda sana na nilitakuwa kwenda kubangaiza.

‘Sasa unakwenda wapi hili unaliona dogo sio, inabidi utafute kwanini hili limetokea, wewe unaondoka, je likija tena nitafanyaje..’ akaniuliza mke wangu huku kanitolea macho.

‘ Nikuambie mke wangu, sasa hivi likija hili shetani liambie hilo haliwezekani likafie mbali, hakuna kitu kama hicho mama yangu namafahamu sana, mama yangu nimtu mwema sana..’Nikasema nakuondoka zangu


‘Huo ulikuwa ni mwanzo tu….’rafiki yangu…

WAZO LA LEO: Jamani tuacheni uzushi, kuna watu wengine wakisikia jambo tu, hata kama hawajalifanyia utafiti kuwa  ni la kweli, wanaanza kulitangaza kila kona, bila kujali kuwa linaweza kuathiri au kuleta sintofahamu. Uzushi ni haufai, ulimi unaweza kuangamiza, tuwe makini kabla ya kutoa kauli zetu na kuwazushia watu wengine ubaya.
Ni mimi: emu-three

No comments :