Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, December 5, 2014

NANI KAMA MAMA-1(KISA KILIPOANZIA)
Kisa kilivyoanzia:

Siku hiyo nilikuwa kituo cha basi nikisubiria usafiri, mara kukatokea tukio la aina yake, pikipiki, ilikuwa inakatisha barakabara kwa kasi, ikakoswakoswa kugongwa na daladala zilizokuwa zikifukuzana, watu wakabakia mdomo wazi , na kila mmoja akawa anaongea lake.

Wakati hayo yakiendelea mimi nikasogea pembeni, nichelea ajali maana madereva wa madala dala walikuwa wanasogeza magari hadi sehemu wanaposimama abiria,  mimi nikawa naingia kwenye dunia ningine ya mawazo,  nikiwazia jinsi ya kupata usafiri mara  gari la kifahari likasimama hatua kidogo mbele na pale niliposimama,  na jamaa akiendeshwa alikuwa akitabasamu na simu yake mkononi, mimi nikaliangalia kwa macho ya hamasa, moyoni nikasema wenye nacho wana raha zao.

Wakati naendelea kuwaza, mlango wa lile gari ukafunguliwa, na jamaa mmoja akatoka nje ya hilo gari, nahisi  kwa muonekano wake atakuwa muheshimiwa, au mkurugenzi fulani, kwani alikuwa, pande la mtu, kitambi, suti ya maana, eeh, mungu kamjalia kama kipato anachopata ni cha halali akafunga gari lake na ugeuka kutuangalia.

Nikawa nataka kuondoka ile sehemu maana watu walikuwa wanasukumana, na kwa muda huo nikamun yule jamaa akiwa anakuja upande ule niliosimama, mimi nikajua kuna mtu anamfuata kumsalimia…nikawa sina habari naye, lakini machoyangu yalikuwa yanamtizama anavokuja pale tuliposimama.

Cha ajabu nikamuona huyu jamaa akinijia mimi, akanisogelea pale niliposimama, na kwa muda ule sikujua ni nani, mpaka aliponikaribia akawa anatabasamu na kuniangalia usoni, hakunysha mkono hapo hapo wa kunisalimia, na mimi sikutaka kujibaragua, eti kwa vile ni tajiri, basi nianze kumsalimia, nikatulia nikiwaza huyu mtu ni nani, mbona sura inakuja na kutoka.

Wakati huo alikuwa kasimama mkabala na mimi, ananikagua usoni, kama nay eye anajiuliza, au kunisanifu,…sikupenda hiyo hali, nikataka nisogee pembeni, lakini nikahis kama hiyo sura naifahamu, hata hivyo sikupenda kuwazia huo, maana nikiwazia huko nahisi moyo ukinienda mbio …nikapepesa macho kama siamini, bado akili haikubali kuwa huyo ndiye huyo huyo ninayemfikiria mimi au ni mtu mwingine.,

‘Mjumbe habari yako….’akasema

 Mjumbe ni neno tulilokuwa tukilitumia tukiwa shuleni, tukimaanisha  mwenza katika msafara, maana kipindi cha likizo tulikuwa tunapangwa mafungu mafungu kwa ajili ya usafiri wa kurudi makwetu, enzi za neema, wanafunzi wanalipiwa usafri na serikali, kutoka shuleni na kurudi shuleni,  sasa sisi tuliokuwa tunasafiri kwenda Dar, tulikuwa tunaitana `mjumbe’

‘Mjumbe….!’nikasema kwa mashaka na sasa nikitafuta usawa wa kumkwepa na ikibid kukimbia, kwani niliona ni mzuka, au kibwengo, lakini kama ni mzuka au shetani sijui, halingelikuwa na hali ile, gari zuri, hali nzuri….nikajilaumu kwanini nimesema hilo neno ‘mjumbe’ …

‘Habari yako, za siku nyingi….’akanyosha mkono sasa kunisalimia, nikasita kuinua mkono wangu, sasa akili haikuwa swa, moyo unanienda mbio naogopa, natafta usawa wakukimbilia, nikaanza kujivuta kinyume nyume, na watu wakawa wanatuangalia, wakinishangaa, maana mwenzangu kanyosha mkono kunisalimia tena mtu wa wadhifa, lakini mimi siupokei…

 Jamaa akatabasamu, akashusha mkono wake, na kunisogelea, akasema;

‘Mhh, mjumbe, unahisi umeona mzuka, mfu kafufuka au…..’akasema

Sikuamini macho yangu vyema, nikayapepesa mara mbili na kumbukumbu zikanijia kuwa ni yule yule jamaa ninaye mfahamu, nikajikuta natikisa kichwa na maneneo haya yakanitoka ;

‘Aisee ndio wewe…haiwezekani, Mungu kweli mkubwa …ume-ume…imekuwaje’ nilishikwa na kigugumizi, na kushindwa kutamka hayo maneno vizuri…..

‘Hahaha, ndio hivyo..hujakosea nimefufuka, na sasa unaongea  na mzuka wa yule uliyemfahamu, mjumbe….lakini ukumbuke kuwa mungu ni mkubwa, na yeye anajua siri za waja wake wote, leo na kesho hadi mwisho wa dunia…najua umeshangaa sana kuniona na hata sasa huwezi kuamini kuwa ni mimi, ni mimi, na wala sio ndugu yake huyo unayehisi alikufa….ndio mimi `mjumbe’…’akasema

‘Ni kweli ni wewe au nafananisha…hapana, lakini mbona….?’ nikamuuliza

‘Ndio mimi bwana..usiumize kichwa kuwaza sana,….’akasema, na sasa akanyosha mkono wake tukashikana mikono na kusaliamia saa nikiwa na uhakika kuwa ndio yeye, na ni binadamu sio mzuka, .. lakini hata hivyo  kichwani nilikuwa na maswali mengi yanayohitaji majibu ya haraka , kwani kwa mara ya mwisho nilipoonana na huyu jamaa alikuwa taabani, na baadaye nikasikia tetesi kuwa huyo jamaa keshafariki…

                                                                  ****

‘Unajua mjumbe, sijui nikuambije,..unaweza ukasema  milima haikutani lakini wanadamu hukutana, hata hivyo, mbona nilipata taarifa za kijabu ajabu ina maana wanadamu wanaweza kukutana na wafu…’nikasema sasa kiutani japokuwa moyoni nilikuwa bado na mashaka.

‘Hahaha, watu bwana, unajua wabongo tunapenda sana uvumi, mzaha, na ushabiki bila tathimini au uchunguzi, na hili ni tatizo,…ni kweli nilikuw anusu mfu, ndio maana watu walisema nimeshakufa au sivyo…?’ akauliza na kucheka

‘Ndio hivyo, …ningekuwa na imani haba ningeogopa hata kukusalimia, hapa nilitaka kukimbia, lakini nikajipa moyo maana kuna watu wengi..’nikasema

‘Yaani imekuwa kama siku ile ulipokutana na mimi pale Lugalo Hospitalini, ulivyoogopa hata kunishika mkono, ukijua nimeshaathirika, au….’akasema  tukacheka.

Ni kweli siku nilipoonana na huyu ‘mjumbe’,  ilikuwa ni hospitali ya Lugalo, alikuja kupata matibabu, mimi nilifika hapo kumuona mgonjwa wetu aliyekuwa kalazwa hapo hospitalini.

Mara nikiwa naingia kwa haraka maana muda ulikuwa umekwisha wa kuona wagonjwa, ghfala nikamuona mtu anatembea mwendo wa shida, kakonda,…ukomo wa kukonda, binadamu akikonda hubadilika kabisa….anazeeka, hata kama alikuwa kijana.

Mtu huyu akawa ananijia na huku akijaribu kuatabsamu, lakini uso ulionyesha huzuni na labda machungu, nikawa naogopa, maana ni kile kipindi ugonjwa wa ukimwi unaogopewa, moyoni nikajua ni muathirika tu.

Jamaa akanisogelea, akanyosha mono kunisalimia kiukweli mkonow angu ulikuw amnzito kuitikia ile salamu, nikawa kama nimeshikwa na ganzi, nikabakia kumuangalia huyo jamaa, kwangu bado sikuwa nimempata vyema, lakini aliponinyoshea mkono kunisalimia, nikaanza kumtambua.

Jamani binadamu akikonda hubadilika,..na hasa kama alikuwa mnene, na akaisha kihivyo….mabega yamepaa, mkono umekuwa mwembaba, binadamu anabadilika, na akibadilika hata sura huwa nyingine kabisa, jamaa yangu alikuwa hivyo, niliogopa hata kuitikia salamu ya kumshika mkono, lakini kiujasiri w kujidanganya nikainua mkono wangu tukashikana,..mkono wangu ukawa unatetemeka.

‘Mjumbe, …..aheri nimekuona, maana hapa sina nguvu,  naomba unipelekee hiki cheti pale mbele, ili niweze kuingia kumuona dakitari,…..kuna majibu yangu ya damu na vipimo vingine….’akaniambia

‘Una matatizo gani mjumbe?’ nikajikuta namuuliza.

‘Sijui ….aheri ningelijua nikajua moja, lakini ngoja tusubiri vipimo, ndivyo msema kweli,  ni aheri ningelijua kuwa naumwa ukimwi, ningelijua kuwa mimi ni muathirika, lakini hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi mwili, ya kwanza niliambiwa sina tatizo,watu hawakuamini…mimi najua ni kweli sina,..lakini kwanini nakonda, kwanini mwili unaisha,..hiyo ni siri yangu, au labda madocta wananificha ..sijui …’akasema.

‘Kiukweli sijakuelewa..unasema unajua kwanini unaisha hivyo na hiyo ni siri yako…na bado umepimwa, huna tatizo, kwanini sasa husemi hiyo siri yako, ili ukatafutiwa dawa, au ufumbuzi…..’nikamwambia

‘Hakuna atakayenielewa….ni adhabu mpaka iishe…….’akasema

Sikuweza kuongea naye zaidi, basi nikachukua kile cheti na kukipeleka kwa dakitari kwa ajili ya kupewa majibu yake, nilitamani nimuombe dakitari nifahamu ukweli, lakini haikuruhusiwa, hata hivyo, sikuwa na muda zaidi, nikageuka, …kumuangalia jamaaa, nilimuona kaka kainama chini…,

Sikuwa na muda wa kurudi kuongea naye tena, maana muda wa kuona wagonjwa ulikuwa umepita, na mimi nilihitajika kumuona mgonjwa wangu, nikatembea uelekeo mwingine nikajua nitarudi  nitakuja kuonana naye nijua vipimo vyake vinasema nini, na wakati nampita akainu uso akatikisa kama kunishukuru, ila niliona ajabu, kwani macho yake yalikuwa yanatoa machozi, alikuwa analia...

Machozi yalikuwa yakitoka kwenye macho ambayo, yamemtoka kwa ajili ya kukonda,.., uso wake ulikuwa umekunjamana, na hata nywele zilionekana kama kunyonyoka, nikajikuta na mimi machozi yananitoka.

Wakati namuangalia  nikakumbuak enzi zetu za shule tukiwa sekondari ya Umbwe (mti safi wa matunda bora). Jamaa huyu alikuwa pandikizi,  japokuwa kipindi hicho hakuwa na kitambi, na kipindi hicho alikuwa na sura ya utoto, ujanaa …lakini siku hiyo nilipokutana naye Lugalo, alikuwa kaisha kikomo cha kuisha, kazeeka,  ….oh.

Machozi yalipomtoka, akachukua leso yake kwa mkono usio na nguvu, na kuyafuta machoz yake kwa haraka, na mimi sijui kwanini,  machozi yakinilenga lenga, nikijaribu kujizuia nisiendelee kumtizama, na akilini moja kwa moja nikajua ni muathirika,  huruma, ikanija, nikijua mwenzangu huyo anahijia huduma, na nasaha ya hali ya juu, na sio kulia. Yeye akasema;.

‘Usijali rafiki yangu haya ndiyo majaribu ya dunia, lakini sijambo, ujue nilipima hospitali moja, nikaambiwa sina tatizo, nikasema haiwezekani, jamaa yangu mmoja akaniambia, hao walionipima,  wamenidanganya, akanishauri nije hapa, ndio nikaona nifika hapa nipime tena…’akasema

‘Usijali, yote ni heri na kuumwa sio kufa , na ukiumwa muhimu nikutambua tatizo ni nini….’nikasema hata mimi kichwani nilijua ni lazima kaathirika.

Nilitaka niwe nay eye hadi kwa dakitari, ili niwe na uhakika lakini muda ulikuwa hautoshi kumsubiria, nikamuacha na kuelekea chumba cha wagonjwa walilazwa, nikamuona jamaa yangu tukasalimiana kidogo, baadaye nikaambiwa nitoke maana muda wa kuona wagonjwa umekwisha. Ikabidi sasa nirudi kumuona huyo rafiki yangu.

Wakati natoka, nikamuona rafiki yangu akiwa ametoka kwa dakitari, akiwa kashikilia kile cheti chake na karatsi nyingine ya majibu, akaniona akatabasamu, halafu machoni nikamuhisi anataka kulia, nikamsogelea na kumshika, nilijua analia kwasababu ya hayo majibu kuwa `kaathirika’ na kwahiyo anahitajia ushawishi na kumpa moyo.

Nilipomshika kama kumkumbatia hivi, akaanza kulia, ile kulia kwa kwikwi kwa kutikisika, hadi baadaye akatulia, na mimi hapo nilipo nguvu zikawa hazipo,nikijua nimemshika muathirika na sijui..unajua siku hizo elimu japokuwa nilikuwa nayo kuwa huwezi kuambuskizwa kwa kumshika mtu, lakini ila hali ya udhaifu wa kibinadamu, ilinifanya niwe na mashaka, woga, na nikijua mwenzngu sasa ndio anaanza safari ….nikawa nimetulia nikisubiria aniambie kaambiwa nini, na moyo sikuwa na shaka, nilijua jibu ni moja, kuwa kasha-athirika.

‘Samahani rafiki yangu usione nalia,…nalia na mawili, kwanza nalia kwa vile huenda kama wanavyosema watu madakitari wanaendelea kunificha, wananiambia sina tatizo..wanasema damu yangu ni safi, na sina tatizo ..labda nipime vipimo vingine vya `utra sound..’ lakini siumwi ndani, mimi siumwi hivyo wanavyofikiria wao, hata sasa…sielewi rafiki yangu…’akasema.

‘Lakini pili ambalo ni baya zaidi, nalia kwa vile jamii na dunia imeshanitenga, nalia kwa vile sina raha, sina ndugu sina….unakumbuka nilishaona, niliamua kuoa mapema tu, nikijua nitajituliza, kama unijuavyo tamaa za ujana ziliteka, na ushauri niliokuwa nimepewa ni kuoa, sasa mke kanikimbia….’akasema na sasa akaanza kulia tena.

Alipotulia akanionyeshea karatasi yake ambayo kweli  ilionyesha hana matatizo yoyote zaidi ya udhaifu wa mwili na hakuwa na tatizo la maradhi mengine, damu , mkojo na kila kitu hakina matatizo, moyoni nikajisemea, mara nyingi madakitari hawasemi moja kwa moja una ukimwi watakuambia unaumwa homa, tumbo , kwahiyo labda walitumia hekima hii kumficha huyu jamaa. Lakini hata hivyo mbona hata magonjwa mengine hana!

‘Pole sana,natumai wamekupa dawa itakayokusaidia…, na vipi maisha mengine, yanakwendaje?’ nikamdadisi, akaniangalia akajitahidi kutabsamu, akainama chini na hakusema jambo hapo, alipoinua uso, jibu nikaliona… machozi…!

Machozi yale yaliashiria mengi, na kwa mwenye akili alijua kwanini alitoa machozi yale. Na kabla hajanihadithia lolote nikaitwa na jamaa zangu kuwa wanataka kuondoka, na mimi nilikwua nimedowea lifti , sasa nikajiona nipo njia panda, nibakia hapo nimliwaze rafiki yangu na nisikia masahibu yake au

Wenzangu wakawa wananiita kwa ishara kuwa tunachelewa na mjumbe akawaona, akasema;

‘Nenda tu rafiki yangu…mungu akipenda tutaonana, na kama labda ndio siku ya mwisho kuoanana na wewe, usiache kuniombea duwa,….’akasema, basi  Ikawa sina jinsi nikamuaga rafiki yangu huyo kwa kumpa chochote mkononi.

Siku zikapita nikawa nimemsahau, na siku moja nikakutana na jamaa yangu mmoja anayemfahamu huyo mjumbe, akaniambia, jamaa alikwisha fariki..

NB: Ndio tumeanza kisa chetu hivyo, kaeni mkao wa kula

WAZO LA LEO: Unapokutwa na matatizo ya dunia, usikate tamaa, japokuwa matatizo yanazidiana, unaweza ukaandamwa na matatizo mfulululizo mpaka ukasema `kwanini mimi’ ukafikia hata kukufuru na hata kuingia kwenye shiriki. Kumbuka matatizo ni yetu wanadamu , na matatizo ni sehemu ya mitihani ya kimaisha, usikate tamaa, zidi kumuomba mungu, huku ukijitahidi kupambana nayo, ipo siku utashinda
Ni mimi: emu-three

No comments :