Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, November 24, 2014

DUNIA YANGU-67


 Inspecta Moto akatoka pale mahakamani kwa haraka akimfuatilia yule nesi, ....alimuona akiwa kasimama ....akionyesha kuwa na wasiwasi, akionyesha kuwa kuna kitu kinamsumbua, ....akajiuliza ni kwanini kaamua kufika hapo mahakamani, wakati alipoongea naye alisema hatafika, anataka kupumzika kwa ajili ya kazi, kwa hali kuna kitu kimemleta, je ni huo mziko aliogizwa akauchukue kwa fundi.

‘Inawezekana, atakuwa na, inawezekana, kaja nao kwa nia  ya kumpa huyo mtu wake...’akasema Inspecta.

Wakati anawaza hayo, akawa anatafuta mwanya wa kutoka,lakini haikuwa kazi rahisi kuwapita watu waliopata nafasi ya kupenya na kusimama eneo la mahakamani, kwa muda huo watu wengi walikuwa wamejazana mlangoni, ilionekana kama vile polisi waliamua kuwaachia watu waliokuwa wamendelea kubakia waingie tu, maana wengine walishaamua kuondoka,.…

Hata Inspecta alipotoka eneo hilo,alikuwa bado hajamuona nesi alipokuwepo, akageuka huku na kule kumtafuta na baadaye akamuona akiwa  kwenye eneo la barabara kuu, kunaposimama bajaji, alikuwa kasimama karibu na bajaji, kuashiria kuwa anataka  kuondoka, na pembeni yake  alikuwa  kasimama jamaa mmoja wakiongea naye, jamaa huyo alikuwa kavalia vyema kabisa, suti, na mawani meusi machoni, alionekana kama hawo jamaa wanaojiita ‘misheni town’.

Inspecta akawa anajaribu kumpungia nesi mkono, ili amone, lakini nesii hakuwa akiangalia muelekeo wake, alikuwa akiendelea kuongea na huyo jamaa huku bajaji tayari imeshawashwa,..Inspecta akawa anajitahidi kwenda pale waliposimama, ili amuwahi kabla hajaingia kwenye hiyo bajaji ...

Ilionena kuna kitu walikuwa wanakabidhiana,  maana nesi alitoa bahasha kwenye mkoba wake akampa yule jamaa, na yule jamaa akawa anatoa bahasha nyeupe anamkabidhi nesi, lakini nesi hakuiweka ile bahasha moja kwa moja kwenye mkoba wake, ...aliifungua, akatoa karatasi, ni kama  barua, ni karatasi yenye maandiko, na nesi akawa anayasoma.

Nesi  akawa  akawa akatoa peni kwenye mkoba wake, akawa anaandika kitu, zilionekana ni nakala mbili, moja akamrudishia yule mtu na nyingine akabakiwa nayo huyo nesi, nesi akawa kama karizika, bila kurudishia ile barua kwenye bahasha, akaingia kwenye bajaji  akiwa kshikilia ila karatasi mkononi, na yule jamaa akawa kashikilia ya kwake, akaikunja na kuweka kwenye koti lake pamoja na ile bahasha ya mwanzo, wakashikana mkono wa kukubalina.

Inspecta Moto kwa wakati huo alikuwa anawakaribia, tatizo kubwa lilikuwa ni watu, jinsi ya kupata njia ya haraka ya kuwafikia, lakini matendo yote hayo yalionekana wazi. Inspecta  akawa anatembea kwa haraka akisukumana na watu, akijaribu kupunga mkono na hata kuita, lakini ukelele wa magari yaliyokuwa yakipita na mngurumo wa ile bajaji ambayo ilikuwa ipo tayari kuondoka, iliwafanya nesi na mwenzake wasimsikia Inspecta akiita.

Na Inspecta akawa karibu yao,  lakini kabla hajawafikia , nesi akawa ameshaingia  kwenye bajaji na kuanza kuondoka;

‘Nesi subiri....’Inspecta Moto akasema kwa sauti, lakini alikuwa keshachelewa, bajaji ikawa imeshaondoka kwa mwendo wa kasi, na yule jamaa aliyekuwa na huyo nesi akawa anatembea muelekeo wa kwenda mahakamani.

Inspecta Moto akamfuata yule mtu aliyepewa ile bahasha na karatasi,, akamuonyesha kitambulisho na kuamwambia

‘Mimi ni askari-usalama, nimekuona ukikabidhiwa bahasha na yule nesi, nataka kujua ni kitu gani kipo ndani ya hiyo bahasha...’akasema Inspecta na kumfanya yule jamaa kwanza aonyeshe kushangaa, halafu akatoa maneno kama ya ukali;

‘Mimi sijui ni kitu gani, kazi yangu ni kumpelekea muhusika,....’akasema huyo mtu akionyesha kukasirika.

‘Nataka kumjua huyo muhusika unayetaka kumpelekea huo mzigo ni nanii...hicho kitu kimeibiwa ni mali ya mahakama, ni ushahidi, tumekuwa tukiutafuta toka asubuhi, kwahiyo unakamatwa kwa kuhusika katika upotevu wa ushahidi wa kimahakama...’akasema Moto akiwa hana uhakika kama ndio chenyewe au la, alifanya hivyo kama kubahatisha tu.

‘Wewe mwenyewe umeona nikikabidhiwa na huyo mdada,....siumesema hap umeona nikibabidhiwa na huy o mdada, sasa iweje unishuku kwa kuchukua, au kuiba ushahidi wa mahakama, ....mimi sijui lolote, mimi ni wakala tu, wala sijui ni kitu gani. unachozungumzia..’akasema

‘Nimekuuliza unatakiwa kumpelekea nani, usipoteze muda, maana nasubiriwa mahakamani?’ akaulizwa huyo mtu, na alipoona huyo mtu wa usalama hatanii, akasema;

‘Nimeambiwa nimkabidhi askari mmoja aliyewaleta hao washitakiwa, ambaye ataufikisha huo mzigo kwa mlengwa, sijui mlengwa  ni nani...’akasema

‘Twende ndani ya mhakama, unahitajika ukakabidhi hicho kitu mbele ya hakimu, na uelezee ulivyokipata , na tunatakakumfahamu huyo askari ambaye unahitajika kumkabidhi,...’akaambiwa,

‘Mimi  huyo anayetakiwa kukabidhiwa simfahamu....na mimi siwezi kufanya kazi hiyo...unaniingiza kwenye matatizo nisiyyafahamu.....’akalalamika

‘Hapo huna jinsi, ni lazima ukabaliane na hayo niliyokuambia, up chini ya ulinzi....’akasema Moto.

‘Sikiliza afande, kwanza ujue mimi ni wakala , ukitaka nifanye hivyo, unataka kazi yangu iharibike, nitaonekana sio mwaminifu kwa wateja wangu,..tafadhali, elewa umuhimu wa kazi yangu, kama ningelijua ni kitu cha kimahakama nisingelikubali kukipokea....’akasema huyo mtu akionekana sasa kuwa na wasiwasi.

‘Nimeshakuambia huna jinsi yoyote, kwa usalama wako ni muhimu twende ndani  ya mahakama, nitakuonyesha mtu ganii sahihi wa kumkabidhi hicho kitu, na wewe utakuwa salama kuwa umewakilisha nyaraka za kimahakama kwa muhusika, vinginevyo utakamatwa, na hata hiyo kazi yako hutaweza kuifanya tena...unanisikia haya twende ndani usinipotezee muda...’akaambiwa na  yule mtu akawa hana la kufanya wakaongozana na 

Inspecta Moto hadi ndani ya mahakama, na wakati wanaingia ndio pale muendesha mashitaka alikuwa akiulizwa kwa mara ya mwisho kuwa anahitaji muda gani, masaa au siku, ili kuwakilisha ushaidi wake ...

********

‘Muendesha mashitaka, umesema unahitaji muda, ili uweze kuwakilisha ushahidi wako, na maelezo sahihi dhidi ya huyu mtuhumiwa,  je unahitaji muda gani…?’ akaulizwa muendesha mashitaka na kabla hajajibu akamuona Inspecta Moto akiingia na huyo mtu, na muendesha mashitaka akasema

‘Muheshimiwa hakimu, kabla sijajibu hilo swali naomba niongee na mwenzangu, ....’akasema na akamsogelea Inspecta Moto akisema;

‘Ushahidi upo wapi, nashindwa hata kuelezea, maana jamaa katushinda ujanja,…niambie umeleta nini?’ kauliza

Inspecta Moto akasema kumuambia yule mtu;

‘Mkabidhi huo ushahidi muendesha mashitaka na mwambie ilitokeaje kwa haraka na kwa kifupi, ....’akasema Moto na yule jamaa akasema kama alivyomwambia Inspecta Moto, na muendesha mashitaka, akasita kuipokea ile bahasha kwanza, akasema;

‘Kuna nini ndani?’ akauliza

‘Mimi sijui kuna nini, kazi yangu ilikuwa kumpa mzigo niliopewa dada huyo nay eye kunikabidhi huu mzigo ambao natakiwa kuufikisha kwa askari, hayo mengine hayanihusu,  sasa ukiniuliza kuna nini, mimi hiyo sio kazi yangu kutegemeana na makubaliano yetu , lakini kwa kusika mkononi, inaonekena kuwa na kitu kigumu kama simu…’akasema huyu jamaa

‘Hebu kitoe hicho kitu kwa haraka, tunataka kuhakiki kama kama ndio chenyewe…’akasema  muendesha mashitaka na yule mtu jamaa akaifungua ile bahasha, na kutoa kitu kilichokuwemo ndani, na Inspecta Moto akasema;

‘Ndio chenyewe…..’na muendesha mashitaka akapumua kama mtu aliyekuwa akishusha mzigo mnzito , na kwa haraka, akageuka kumuangalia hakimu akasema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu naomba samahani kwa kuchelewesha taratibu za mahakama yako tukufu, lakini tumefanya hivi ili kuhakikisha kuwa haki inatendeja, ndugu muheshimiwa hakimu,  ushahidi tuliokuwa tukuitafuta ambao uliibiwa tumefanikiwa kuupata, na tunaomba tuuwakilishe mbele yako, ...’akasema  muendesha mashitaka, na mshitakiwa akasema;

‘Ushahidi gani huo, na huo ushahidi kwa kesi ya nani…..?’ akauliza mshitakiwa mkuu kwa kujiamini.

‘Kwa kesi yako wewe, wewe ndiye mshitakiwa ...’akasema muendesha mashitaka

‘Mimi kama nani, maana mliyemshitakia, kutokana na jina, mtu mwenyewe, kiukweli hayupo hapa, je mimi ndiye huyo mkuu wenu? Jibu ni hapana, sasa je mimi nashitakiwa kama nani na kama mnanishitakia mimi kama mhalifu, basi mfuate taratibu za kisheria, na hiyo itakuwa kesi nyingine sio hii hapa....’akasema kwa kujiamini, na akaendelea kuongea kwa mbwembwe

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, tuwaulize hawa wanaoshitakii watu bila utatibu, je ushahidi huo walioleta unanihusu mimi au huyo mshitakiwa waliyemtaja, au huyo mliyemtaja hapo kama mshitakiwa ni mimi, maana uthibitishe wa kitaalamu unaojulikana kimataifa umethibitisha kuwa sio mimi, kuna mtu anapinga DNA test?’ akauliza mshitakiwa akionyesha  kujiamini...

Wakati anaongea hivyo , alikuwa hajamuona yule mtu aliyeingia na Inspecta Moto, lakini sasa akamuona, na sauti ile ya kujiamini ikafikia, akasema;

‘Niambieni mimi ndiye huyo mhalifu mliyemtaja hapo, au mnamshitaki nani, akawa sasa anamuangalia yule mtu aliyekuwa karibu na Inspecta Moto kwa macho ya chuki.

‘Tunakushitakia wewe kama muhalifu, uliyehusika na matendo maovu ikiwemo ya kuongoza kundi haramu, mauaji, na udanganyifu...’akasema Inspecta Moto akisogea pale aliposimama muendesha mashitaka. Na muendesha mashitaka akadakia, na kusema;

‘Umeshitakiwa wewe , kwa vile wewe ni mhalifu kutokana na makosa hayo yaliyoainishwa, kutofautiana kwa jina sio sababu, tunachoangalia kwa sasa ni muhusika mwenyewe, ambaye kapatikana na ushaidi utathibitisha hilo, na mhalifu mwenyewe ni wewe uneyeongea?’ akasema  muendesha mashitaka

‘Na wewe unaongea hapa kama nani?’ akauliza mshitakiwa akimuangalia Inspecta Moto

‘Kama msaidizi wa muendesha mashitaka...’akasema Inspecta Moto, na hakimu akaona aingilie kati kwa kusema;

‘Hebu tuwekane sawa hapo, muendesha mashitaka na msaidizi wako mnasema mumeleta ushahidi wa kesi dhidi ya mshitakiwa, lakini mshitakiwa mliyemtaja kwenye hii kesi, ameshakana kuwa  sio yeye, mumeshika yeye kimakosa, na ameweza kuthibitisha  hilo kuwa yeye sio huyo mliyemshitakia,  kwa uthibitisho wa kipimo kinachitambulikana cha DNA,...sasa huo ushahidi mliouleta ni wa nani, na kwa kesi ipi?’ akauliza hakimu.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, kundi hili limeundwa na watu wajanja sana, watu ambao wanatumia sheria, akili za watu, na ujanja ujanja kuhakikisha mambo yao yanakamilika. Ushahidi huu utaonyesha mbinu zilizotumiwa na hawa watu , huyu mshitakiwa akiwa kama kongozi, yeye ndiye mshitakiwa mkuu, tutalithibitisha hili kwenye huu ushahidi, kwa jinsi gani anahusika....’akasema Moto.

‘Lakini  huyo mliyemshitakia kwa ,maandishi, sio huyu kweli si kweli, …?’ akauliza hakimu.

‘Muheshimiwa hakimu ndiye huyu huyu, ….tutaona kwenye huo ushahidi, huyu mtu katumia ujanja tu, nahapa anataka kuruka ili asionekane ndio yeye, ukimuachilia leo akitoka hapa hatutampata tena ushahidi huo utaonyesha kila kitu….’akasema Moto, na mshitakiwa akataka kupinga lakini hakimu akasema;

‘Kwa vile muda umekwisha, na sioni sababu ya malumbano zaidi, kama mna uhakika na huo ushaidi wenu, uonyesheni, lakini nawaonya kama hautakuwa na hayo yanayohitajika, na kuwa na uthibitisho kuwa muhusika huyu ndiye anayehusika, basi sheria itawaandama nyie..i,kwa huvi sasa nabidi kukiuka baadhi ya vipengele ili kuokoa muda....’akasema hakimu.

‘Sawa muheshimiwa hakimu, tupo tayari kwa hilo, tunaomba mtaalamu wa mitandao aje hapa atuwekee chombo kitakachowezesha sote kuona kila kitu kwa uwazi zaidi….’akasema na mshitakiwa akawa kashika mdomo,  huku akitoa kauli za kulalamika kuwa sheria haifuatwi,  lakini hakimu hakumsikiliza na mara ushahidi ukatolewa kwenye bahasha

Mshitakiwa akaonekana akishika mdomo kwa mshangao, hakuamini, na hapo akaanza kusema sema ovyo kwa sauti

‘Haiwezekani, kwanini umewapa hao watu, uliambiwa nini uwape hao watu hicho kitu,….kwanini , haiwezekani…nitakuonyesha kazi yangu wewe mtu, nikitoka hapa ujue wewe umekwisha.....’akawa anapiga kelele,, na kutaka kutoka ile sehemu aliyokuwepo ya mshitakiwa, lakini askari wakamdhibiti……

Na ikafika muda wa kuangalia kile kilichokuwepo kwenye huo ushahidi, watu hawakuamini, ...ukweli wote ukabainika, na ndoto za bwana Diamu, zikafikia ukingoni , na hapo hapo mtu huyu akadondoka na kupoteza fahamu.

Mwisho wa 'dunia yangu' ukafika......
NB: Kisa hapa ni kama kimekwisha, lakini hatuwezi kuachia hapa maana Maswali hapo ni mengi, tutakuwana sehemu mbili zitakazofuata ambazo ni  hitimisho la hiki kisa likifafanua kilichoonekana kwenye huo ushahidi wa kifaa cha komputa, kwa ufafanuzi uliotolewa na Inspecta Moto mbele ya waandishi wa habari baadaye.

Ni mimi: emu-three

No comments :